ﮘ
surah.translation
.
ﰡ
Alif, Lām, Rā’. Maneno yametangulia juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqrah. Hizi ni aya za Kitabu kilichobainika kilicho wazi katika maana yake, mahalalisho yake, maharamisho yake na uongofu wake.
Sisi tumekuteremshia Qur’ani kwa lugha ya Waarabu, huenda nyinyi, enyi Waarabu mkayatia akilini maana yake, mkayafahamu na mkatenda kulingana na uongofu wake.
Sisi tunakusimulia wewe, ewe Mtume, visa vizuri zaidi kwa wahyi tuliyokuletea wa hii Qur’ani, na ingawa, kabla ya kukuteremshia, ulikuwa ni miongoni mwa walioghafilika nazo, hujui chochote kuhusu habari hizi.
Kumbuka, ewe Mtume, kuwaambia watu wako neno la Yūsuf kumwambia babake, «Mimi nimeota usingizini kuona nyota kumi na moja, jua na mwezi, zote zikinisujudia.» Ndoto hii ilikuwa ni bishara ya cheo kikubwa, cha ulimwenguni na Akhera, alichofikia Yūsuf, amani imshukiye.
Ya’qūb, amani imshukiye, alisema kumwambia mwanawe Yūsuf, «Ewe Mwanangu, usiwatajie ndugu zako ndoto hii, watakuhusudu, watakufanyia uadui na watafanya hila za kukuua, hakika Shetani kwa binadamu ni adui ambaye uadui wake uko waziwazi.
«Na kama kama Alivyokuonesha Mola wako ndoto hii, pia Atakuteua na Atakufundisha uaguzi wa ndoto ambazo watu huziona usingizini, ujue matokeo yake ya uhakika, na atazitimiza neema zake kwako na kwa kizazi cha Ya’qūb, kama alivyozitimiza hapo nyuma kwa wazazi wako wawili, Ibrāhīm na Is’ḥāq, kwa kuwapa unabii na utume. Hakika Mola wako Anamjua yule Anayemteua miongoni mwa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe vyake.
Hakika katika kisa cha Yūsuf na ndugu zake kuna mazingatio na dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu na hekima Yake kwa anyeuliza habari zao na akataka kuzijua.
Waliposema ndugu zake Yūsuf wa kwa baba kuambiana wao kwa wao, «Hakika Yūsuf na ndugu yake wa kwa baba na mama wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi. Anawafanya wao bora juu yetu, na sisi ni kundi lenye idadi kubwa. Hakika baba yetu yuko makosani waziwazi, kwa kuwa amewafanya wao ni bora juu yetu bila ya sababu tunayoiyona yenye kupelekea kufanya hivyo.
«Muueni Yūsuf! Au mtupeni kwenye ardhi isiyojulikana iliyo mbali na mji, hapo yatasafika kwenu mapenzi ya baba yenu na muelekeo wake kwenu, na hatageuka kwa wengine na kuacha kushughulika na nyinyi, na mtakuwa, baada ya kumuua Yūsuf au kumuepusha, ni wenye kutubia kwa Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha baada ya kosa lenu.»
Akasema mwenye kusema, miongoni mwa ndugu za Yūsuf, «Msimuue Yūsuf, na mtupeni ndani ya kisima ataokotwa na wapita njia miongoni mwa wasafiri, na hapo mtapumzika na yeye; na hakuna haja ya nyinyi kumuua, iwapo muna azma ya kulifanya hilo mnalolisema.
wakasema ndugu zake Yūsuf, baada ya kuafikiana kumuepusha, «Ewe baba yetu, unani wewe hutufanyi sisi ni waaminifu juu ya Yūsufu pamoja na kuwa yeye ni ndugu yetu, na sisi tunamtakia wema na kumhurumia, tutamtunza na tutampa ushauri mzuri wa kidhati?
«Tuachie awe na sisi kesho tutakapotoka kwenda kwenye malisho ya wanyama wetu, apate kutembea, apumbae, afurahike na acheze kwa kushindana na mfano wake miongoni mwa machezo yanayofaa. Na sisi ni wenye kumtunza na kila unalomuogopea.»
Ya’qūb alisema, «Hakika nafsi yangu itaniuma akiepukana na mimi na mkaenda na yeye malishoni. Na mimi nachelea asije akaliwa na mbwamwitu, hali mkiwa kwenye shughuli zenu mumeghafilika na yeye.»
Wakasema ndugu zake Yūsuf kumwambia baba yao, «Ikiwa mbwamwitu atamla na hali sisi ni kikundi chenye nguvu, sisi wakati huo tutakuwa ni wenye kupata hasara, hatuna wema wowote, na hakuna manufaa yoyote yanayotarajiwa kutoka kwetu.»
Hapo baba yao akawaachia wawe naye, walipokwenda na yeye na wakaamua kumtupa ndani ya kisima (na wakafanya hivyo) na hapo tukamletea wahyi Yūsuf, «Utawaambia ndugu zako mbeleni kuhusu kitendo chao hiki walichokufanyia na hali wao hawakitambui.»
Na wakaja ndugu zake Yūsuf kwa baba yao mwanzo wa usiku kipindi cha isha, huku wanalia na wanajionesha wana masikitiko na msiba.
Wakasema, «Ewe baba yetu! Sisi tulikwenda tukawa tunashindana kukimbia na kurusha mishale, na tukamuacha Yūsuf kwenye vyombo vyetu na nguo zetu; na hatukufanya kasoro katika kumtunza, kwa kuwa tulimuacha mahali pa amani petu, na hatukumuacha isipokuwa kwa wakati mchache, mbwamwitu akamla. Na wewe hutatuamini, ingawa sisi ni wenye sifa ya ukweli, kwa sababu ya mapenzi yako makubwa kwa Yūsuf.
Wakaja na kanzu yake ikiwa imerowa kwa damu ambayo si ya Yūsuf, ili iwe ni ushahidi juu ya ukweli wao, ikawa ni dalili ya urongo wao, kwa kuwa kanzu haikuchanika. Baba yao Ya’qūb, amani imshukiye, akawaaambia, «Mambo sivyo kama mlivyosema, bali ni nafsi zenu zenye kuamrisha uovu ziliwapambia jambo ovu kumfanyia Yūsuf, mkaliona ni zuri na mkalifanya. Basi nitasubiri subira nzuri isiyokuwa na malalamishi kwa kiumbe chochote, na namuomba Mwenyezi Mungu msaada wa kuweza kuubeba huo urongo mnaoupanga; sitegemei uwezo wangu wala nguvu zangu.
Likaja kundi la wasafiri wakamtuma mwenye kuwatafutia maji, alipoiteremsha ndoo yake kisimani, Yūsuf aliishikilia. Hapo mchota maji alifurahi na akachangamka kwa kumuokota mtoto na akasema, «Ni bishara njema iliyoje! Huyu ni mtoto wa kiume mzuri.» Mchota maji na wenzake walimficha Yūsuf asijulikane na wasafiri wengine wasiwaoneshe, na wakasema, «Hii ni bidhaa tuumeinunua.» Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa wanayomfanyia Yūsuf.
Na ndugu zake wakamuuza kwa wachota maji miongoni mwawasafiri kwa thamani chache ya dirhamu, na wakawa hawana haja na yeye, wanataka kuepukana na yeye. Hivyo ni kwa kuwa hawakijui cheo chake kwa Mwenyezi Mungu.
Na wasafiri walipoondoka na Yūsuf kuelekea Misri, kiongozi wake alimnunua, naye ni waziri, na akamwambia mke wake, «Kaa naye vizuri na uyafanye mema makazi yake kwetu, huenda tukafaidika na utumishi wake, au tukamuweka hapa kwetu kama mtoto.» Na kama tulivyomuokoa Yūsuf na tukamfanaya kiongozi wa Misri kuwa na huruma na yeye, vilevile tulimmakinisha kwenye ardhi ya Misri na tulimfanya asimamie hazina zake, na ili tumfundishe kuagua ndoto na apate kujua kwa uaguze huo matukio ya wakati unaokuja. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi kwa jambo Lake, uamuzi Wake ni wenye kupita, hakuna Mwenye kuutangua, lakini wengi sana kati ya watu hawajui kwamba mambo yote yako kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu.
Yūsuf alipofikia umri wa kukamilika nguvu za ujana wake, tulimpa fahamu na elimu. Na mfano wa malipo haya tuliyomlipa Yūsuf kwa wema wake, tutawalipa walio wema kwa wema wao. Katika haya kauna kumliwaza Mtume, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye.
Na mke wa yule kiongozi, ambaye Yūsuf alikuwa nyumbani kwake, alimtaka Yūsuf kwa upole na kubembeleza, kwa kuwa alimpenda sana na kwa ajili ya uzuri wake, na akamfungia milango na akasema kumwambia Yūsuf, «Njoo kwangu.» Akasema, «Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na najihifadhi Kwake na kujihami kutokana na hayo unayoniitia ya kumfanyia hiana bwanangu aliyeyafanya mazuri mashukio yangu na akanikirimu. Sitamhini kwa watu wake. Hakika hafaulu anayedhulumu na akafanya mambo ambayo hatakiwi kuyafanya.
Na nafsi yake ilivutika kufanya machafu, na Yūsuf nafsi yake ilipitiwa na mawazo ya kukubali, lau si yeye kuona alama miongoni mwa alama za Mola wake zenye kumkemea kufanya yale ambayo nafsi yake ilimzungumzia. Hakika tulimuonesha hilo, ili tumuepushiye baya na chafu katika mambo yake yote. Yeye ni miongoni mwa waja wetu waliosafishwa walioteulia kwa ujumbe na waliotakasa katika kumuabudu kwao Mwenyezi Mungu na kumpwekesha.
Yūsuf alikimbilia mlangoni kutaka kutoka, na yeye (mke wa kiongozi) akafanya haraka kumshika na akamvuta nguo yake kwa nyuma ili kumzuia asitoke na akaipasua. Wakamkuta mumewe kwenye mlango, hapo akasema (mke wa Kiongozi), «Ni yapi malipo ya anayetafuta jambo baya kwa mke wako, isipokuwa ni afungwe au apewe adhabu yenye uchungu?»
Yūsuf akasema, «Yeye ndiye aliyetaka hilo kwangu. Na akatoa ushahidi mtoto wa mlezini katika jamaa zake(mke wa kiongozi) na akasema, «Iwapo kanzu yake imepasuka kwa mbele, basi mwanamke amesema kweli katika tuhma alizomfanyia na yeye (Yūsuf) ni miongoni mwa warongo.
«Na iwapo nguo yake imeraruliwa kwa nyuma , basi mwanamke amesema urongo katika kauli yake, na yeye (Yūsuf) ni miongoni mwa wakweli.»
Yule mume alipoiona nguo ya Yūsuf imeraruliwa kwa nyuma alijua kwamba Yūsuf hana hatia na akasema kumwambia mke wake, «Urongo huu uliomtuhumu nao kijana huyu ni katika jumla ya vitimbi vyenu, enyi wanawake, kwani vitimbi vyenu ni vikubwa.»
Akasema kiongozi wa Misri, «Ewe Yūsuf! acha kutaja mambo yaliykuwa kutoka kwake na usimwambie yoyote. Na uombe msamaha wa dhambi zako kwa Mola wako, ewe mwanamke, iwapo wewe ni miongoni mwa wale waliofanya hatia kwa kumtaka Yūsuf kimapenzi bila ya yeye kutaka na kwa kumzulia urongo.»
Habari ziliwafikia wanawake mjini wakaizungumza kuhusu hizo na wakasema kwa njia ya kumpinga mke wa kiongozi, «Mke wa Bwana anajaribu kumtaka mtumwa wake na amwita amjie. Na mapenzi yake yamefikia kwenye ngozi ya moyo wake. Hakika sisi tunamuona yeye kuwa yuko kwenye upotevu waziwazi.
Aliposikia mke wa Kiongozi kusengenya kwao na hila zao za kumtukana yeye, aliwatumia ujumbe na kuwaita kuja kumtembelea, na akatayarisha mito ya kutegemea na chakula cha kula, na akampa kila mmoja miongoni mwao kisu cha kukatia chakula kisha akasema kumwambia Yūsuf, «Jitokeze kwao.» Walipomshuhudia, walimuona ni kitu kikubwa chenye haiba, na wakashikwa na babaiko la uzuri wake na kuvutia kwake, wakajikata mikono yao katika hali ya kukata chakula kwa babaiko kuu na mshangao, na wakasema kwa kustaajabu, «Twajilinda na Mwenyezi Mungu! Huyu si binadamu!» kwa kuwa uzuri wake sio ule ujulikanao kwa wanadamu, «Huyu si mwingine isipokuwa ni mtukufu miongoni mwa Malaika.»
Mke wa kiongozi alisema kuwaambia wanawake waliojikata mikono yao, «Haya ndiyo yaliyowapata kwa kumuona yeye. Aliyefanya mpatikane na haya ni huyu kijana ambaye nyinyi mumenilaumu kusalitika naye. Kwa kweli nilimtaka na nikajaribu kumvutia ili anikubalie, akajizuia na akakataa. Na asipofanya ninachomuamuru mbeleni, atateswa kwa kutiwa jela na hapo atakuwa ni miongoni mwa wanyonge.
Yūsuf akasema, akijilinda na shari lao na vitimbi vyao, «Ewe Mola wangu! Jela ni bora kwangu kuliko yale wanayoniitia ya kufanya machafu. Na usiponiepulia vitimbi vyao, nitalemea kwao na nitakuwa ni miongoni mwa wachache wa akili wenye kujifanyia madhambi kwa ujinga wao.
Mwenyezi Mungu Akamkubalia Yūsuf maombi yake, akamwepushia kile alichotaka mke wa Kiongozi na marafiki zake kutoka kwake cha kumuasi Mwenyezi Mungu. Mwenyezi mungu Ndiye Mwenye kuyasikia maombi ya Yūsuf na maombi ya kila mwenye kuomba kati ya waja Wake, Ndiye Mwenye kuyajua matakwa yake, haja zake na kile kinachomfaa, na pia haja za viumbe Vyake vyote na yale yanayowafaa.
Kisha ikamdhihirikia waziri na marafiki zake, baada ya kuziona dalili za kuwa Yūsuf hana hatia na amejiepusha na machafu, wamfunge mpaka muda fulani, mrefu au mfupi, ili kuzuia fedheha.
Wakaingia jela pamoja na yeye vijana wawili. Mmoja wao akasema, «Mimi nimeota usingizini kwamba mimi nakamua zabibu ili ziwe pombe.» Na mwingine alisema, «Mimi nimeota kwamba nabeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaula. Wakasema, «Tupe habari, ewe Yūsuf, uaguzi wa ndoto tulizoziota. Sisi tunakuona wewe ni miongoni mwa wale wanaofanya wema katika kuabudu kwao Mwenyezi Mungu na kuingiliana kwao na viumbe Wake.»
Yūsuf aliwaambia, «Hamtajiwa na riziki ya chakula kwa namna yoyote ile, isipokuwa mimi nitawapa tafsiri yake kabla ya kuwajia. Tafsiri hiyo nitakayowapa nyinyi wawili ni miongoni mwa yale niliyofundishwa na Mola wangu. Mimi nimemuamini na nimemtakasia ibada na nimejiepusha na dini ya wasiomuamini Mwenyezi Mungu wala kuamini kufufuliwa na kuhesabiwa.
«Na nimefuata Dini ya baba zangu: Ibrāhīm, Is’ḥāq na Ya’qūb, ndipo nikaamuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake. Haikuwa kwetu sisi kumfanyia Mwenyezi Mungu mshirika katika kumuabudu. Kumpwekesha Mwenyezi Mungu huko, kwa kumhusu Yeye Peke Yake kwa ibada, ni miongoni mwa yale ambayo Mwenyezi Mungu Ametutunukia sisi na watu, lakini wengi zaidi wa watu hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na Imani.»
Yūsuf akaendelea kusema kuwaambia vijana wawili waliokuwa na yeye jela, «Je, kuwaabudu waungu walioumbwa wa aina mbalimbali ni bora au ni kumuabudu Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu?
«Nyinyi hamuabudu chochote kisichokuwa Mwenyezi Mungu isipokuwa ni majina yasiyokuwa na maana yoyote, mumeyafanya ni waola, nyinyi na baba zenu, kwa ujinga wenu na upotevu; Mwenyezi Mungu Hakuteremsha hoja au dalili yoyote juu ya usahihi wake. Hukumu ya haki ni ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika. Yeye Ameamrisha kwamba msimwandame wala msimnyenyekee Asiyekuwa Yeye, na kwamba mumuabudu Yeye Peke Yake. Na hii ndiyo Dini iliyolingana sawa isiyokwenda kombo. Lakini wengi zaidi wa watu hawalielewi hilo, hawaujui uhakika wake.
«Enyi marafiki wangu gerezani, haya uchukueni uaguzi wa ndoto zenu: ama yule aliyeona kwenye ndoto yake kuwa anakamua zabibu, yeye atatoka jela na atakuwa ni mwenye kuishughulikia pombe ya mfalme. Ama mwingine aliyeota kuwa anabeba mkate juu ya kichwa chake, yeye atasulubiwa na aachwe, na ndege waje wamle kichwa chake. Limeshapitishwa jambo ambalo mlikuwa mnaliuliza na limeshamalizwa.»
Hapo Yūsuf akamwambia yule aliyemjua kuwa ataokoka kati ya wale marafiki wake wawili, «Nitaje kwa bwanako mfalme na umwelezee kwamba mimi nimedhulumiwa, nimefungwa bila hatia.» Shetani akamsahaulisha mwanamume yule kumtajia mfalme hali ya Yūsuf, na kwa hivyo akakaa Yūsuf ndani ya jela myaka kadha.
Na mfalme akasema, «Mimi niliona ndotoni, katika kulala kwangu, ngombe saba wanono wanaliwa na ngombe saba walioambata kwa kukonda, na niliona visuke saba vibichi na visuke saba vikavu. Enyi mabwana na wakubwa, nipeni habari ya ndoto hii, iwapo nyinyi ndoto mnaagua.»
Wakasema, «Ndoto yako hii ni mchanganyiko wa ndoto usiokuwa na tafsiri, na sisi hatukuwa ni wenye ujuzi kuagua ndoto namna hii.»
Hapo akasema yule aliyeokoka na kuuawa kati ya marafiki wawili wa Yūsuf ndani ya jela, na akakumbuka habari ya Yūsuf baada ya muda kupita, «Mimi nitawapa habari ya tafsiri ya ndoto hii. Nitumeni kwa Yūsuf nipate kuwaletea uaguzi wake.»
Alipofika yule mtu kwa Yūsuf alimwambia, «Yūsuf! Ewe mkweli sana! Tuagulie ndoto ya aliyeota ng’ombe saba wanono wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda, na akaona masuke saba mabichi na mengine makavu. Natarajia nitarudi kwa mfalme na marafiki zake niwape tafsiri ya hiyo niliyokuuliza na ili wapate kujua cheo chako na utukufu wako.»
Yūsuf akasema kumwambia aliyemuuliza juu ya ndoto ya mfalme. «Uaguzi wa ndoto hii ni kwamba nyinyi mtaendelea kulima kwa bidii kwa myaka saba mfululizo ili mapato yawe mengi, basi kile mtakachokivuna kila mara kiwekeni akiba na mkiache kwenye masuke yake ili kihifadhike na kuingiwa na wadudu na ili kisalie kwa kipindi kirefu zaidi, isipokuwa kiasi kidogo cha nafaka mtakachokila.
«Kisha itakuja, baada ya myaka ya neema, myaka yenye chaka kikali. Watu wa wakati huu watakula chakula mlichowahifadhia hapo nyuma, isipokuwa kichache mtakachokihifadhi na kukiweka akiba kiwe ni mbegu za kupandia mimea.
«Kisha utakuja, baada ya myaka hii ya chaka, mwaka ambapo watu watanyeshezewa mvua, na hivyo basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Awaondolee shida, hapo wakamue matunda kwa wingi wa mavuno na neema.»
Mfalme akasema kuwaambia wasaidizi wake, «Mtoeni jela huyo mtu aliyeagua ndoto, na mleteni kwangu.» Yule aliyetumwa na mfalme alipomjia (Yūsuf) kumwita. Yūsuf alisema kumwambia, «Rudi kwa bwanako mfalme umtake awaulize wanawake walioijaruhi mikono yao juu ya uhakika wa mambo yao na habari zao na mimi, ili ukweli ufunuke kwa wote, na kutokuwa na hatia kwangu kuwe wazi, kwani Mola wangu ni Mjuzi zaidi wa mambo waliyoyapanga na waliyoyafanya, hakuna chochote kinachofichika Kwake katika hayo.»
Mfalme akasema kuwaambia wanawake walioijaruhi mikono yao. «Habari zenu ni zipi, mlipomtaka Yūsuf siku ya makaribisho? Kwani mliona chochote kutoka kwake chenye kutia shaka?» Wakasema, «Mwenyezi Mungu Atulinde! Hatujui chochote hata kidogo cha kumtia ila.» Hapo alisema mke wa Kiongozi, «Sasa umefunuka ukweli baada ya kufichika. Mimi ndiye niliyejaribu kumtia hatiani kwa kumbembeleza, na akakataa. Na yeye ni katika wakweli katika kila alilolisema.
«Neno hilo nililolisema la kumwepushia Yūsuf tuhuma na kuikubalia makosa mimi mwenyewe ni kwa ajili mume wangu ajue kwamba mimi sikumfanyia hiana kwa kumzulia urongo na hayakutukia machafu kutoka kwangu pamoja na kuwa nilimtaka Yūsuf. Nimekubali hilo ili kuonyesha wazi kuwa mimi sina hatia wala yeye hana hatia na kwamba Mwenyezi Mungu Hawaafikii wala Hawaongozi wenye kufanya hiana katika uhaini wao.»
Akasema mke wa kiongozi,»Sijisafishi nafsi yangu, kwani nafsi inamwamrisha mtu sana kufanya maasia, kwa kutaka kupata utamu wa inavyopenda, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemhifadhi. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waliotubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye huruma nao sana.»
Mfalme, mtawala wa Misri, ilipomfikia habari kwamba Yūsuf hana hatia, alisema, «Mleteni kwangu nipate kumfanya ni miongoni mwa marafiki wangu wa kikweli na washauri wangu.» Yūsuf alipokuja, na mfalme akasema na yeye, akajua kwamba yeye hana hatia na kwamba ni muaminifu sana na ni mwenye tabia njema, alimwambia, «Wewe leo hapa kwetu una heshima kubwa na unaaminiwa kwa kila kitu.»
Yūsuf akataka kuwanufaisha waja na kueneza uadilifu baina yao, alimwambia mfalme, «Nifanye mimi kuwa msimamizi wa hazina za Misri, kwani mimi ni mshika hazina mwaminifu mwenye ujuzi na busara juu ya vitu ninavyosimamia.»
Na kama Mwenyezi Mungu Alivyomneemesha Yūsuf kwa kumtoa jela, Alimmakinisha katika nchi ya Misri akawa ashukia popote pale anapotaka. Mwenyezi Mungu Anampa rehema Zake Anayemtaka kati ya waja wake wachamungu, na Hayapotezi malipo ya yoyote aliyefanya matendo mema.
Na kwa hakika malipo mema ya Akhera ni makubwa zaidi kuliko malipo ya duniani kwa wenye Imani na uchamungu ambao wanayaogopa mateso ya Mwenyezi Mungu na wanamtii Yeye katika maamrisho Yake na makatazo Yake.
Nduguze Yūsuf walifika Misri, baada ya kushukiwa na ukame katika nchi yao, ili wachukue chakula kutoka huko. Wakaingia kwake na yeye, kwa nguvu ya akili yake ya kutambua na werevu wake, akawajua na wao wasimjue kwa muda mrefu uliopita na kwa kubadilika umbo lake.
Yūsuf aliamuru wakirimiwe na wakaribishwe vizuri, kisha akawapa chakula walichotaka. Na walikuwa wamemwambia kwamba wana ndugu yao wa kwa baba ambaye hawakumleta pamoja nao, wakimaanisha ndugu yake Binyamin, akasema, «Nileteeni ndugu yenu wa kwa baba, kwani hamuoni kwamba mimi nimewapimia chakula vizuri na nimewakirimu kwa kuwakaribisha, na mimi ni mwema wa kuwakaribisha?
«Na msiponijia na yeye, basi nyinyi hamtakua na chakula ambacho mimi nitawapimia, na msije kwangu.»
Wakasema, «Tutafanya bidii yetu kumkinaisha baba yake atuachie, na hatutaacha kufanya hivyo.»
Yūsuf aliwaambia watumishi wake, «Ichukueni thamani ya vitu vyao muiweke kwenye vyombo vyao kwa siri, kwa matarajio wapate kuiona watakapofika kwao na watambue vile sisi tulivyowakirimu ili wapate kurudi wakiwa na matumaini ya kupata vipewa vyetu.»
Waliporejea kwa baba yao walimsimulia yaliyokuwa ya ukarimu aliowafanyia huyo kiongozi, na wakasema, «Yeye hatatupatia kitu mbeleni isipokuwa iwapo ndugu yetu ambaye tulimuelezea kuhusu yeye atakuwa na sisi. Basi tuachie tuende na yeye tutaleta chakula kingi, na tunakuahidi kwamba tutamtunza.»
Baba yao akawaambia, «Vipi nitawaamini juu ya Binyāmīn, na nilishawaamini juu ya Yūsuf kabla yake, mkaahidi kumhifadhi na msilitekeleze hilo? Mimi siziamini ahadi zenu na utunzi wenu, lakini mimi nauamini utunzi wa Mwenyezi Mungu, Bora wa wenye kutunza na Mwenye huruma zaidi kuliko wenye huruma. Namtarajia Anirehemu, Amtunze na Amrudishe kwangu.»
Na walipofungua vyombo vyao walipata kwamaba thamani ya bidhaa waliyoitoa wamerudishiwa. Wakasema, «Ewe baba yetu! Tuombe nini zaidi ya hii? Hii ni thamani ya bidhaa zetu, Kiongozi ameturudishia, basi kuwa na utulivu kuhusu ndugu yetu na muache aende na sisi ili tupate kuwaletea watu wetu chakula kingi, tumtunze ndugu yetu na tupate kuongeza twesha ya ngamia kwa ajili yake. Kwani Kiongozi anampimia kila mtu twesha ya ngamia mmoja; na hilo ni jambo jepesi kwake.»
Ya’qūb, amani imshukiye, akasema kuwaambia, «Sitamuacha aende na nyinyi mpaka mchukue ahadi na mniapie kwa Mwenyezi Mungu kwamba mtamrudisha kwangu, isipokuwa iwapo mtashindwa nguvu msiweze kumuokoa. Basi walipompa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa lile alilolitaka, Ya’qūb alisema, «Mwenyezi Mungu kwa tunalolinena Ndiye mtegemewa» Yaani, ushahidi Wake kwetu na utunzi Wake zinatutosha.»
Na akasema baba Yao kuwaambia wao,»Enyi wanangu mtakapoingia nchi ya Misri, msiingie kwa mlango mmoja, lakini ingieni kwa milango mbalimbali, ili msipatwe na jicho la husuda. Na mimi nikiwapa wasia huu, siwakingi na chochote Alichokiamua Mwenyezi Mungu kwenu. Hakuna uwamuzi wowote isipokuwa ni ule wa Mwenyezi Mungu Peke Yake, Kwake Yeye nimetegemea na nimeamini, na juu Yake Peke Yake waumini wanategemea.»
Na walipoingia kupitia milango mbalimbali, kama alivyowaamrisha baba yao, hilo halikuwa ni lenye kuwazuilia uamuzi wa Mwenyezi Mungu kwao, isipokuwa ilikuwa ni huruma ndani ya moya wa Ya’qūb juu yao wasipatikane na jicho la husuda. Na Ya’qūb ni mwenye ujuzi mkubwa wa mambo ya Dini yake aliyofundishwa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya wahyi, lakini wengi wa watu hawajui mwisho wa mambo na undani wake, na pia hawayajui anayoyajua Ya’qūb, amani imshukie, katika mambo ya Dini yake..
Na walipoingia ndugu zake Yūsuf kwake, katika nyumba yake ya kukaribisha wageni, wakiwa pamoja na ndugu yake wa kwa baba na mama, Yusuif alimkumbatia nduguye wa kwa baba na mama na akamwambia kwa siri, «Mimi ni ndugu yako. Basi usihuzunike wala usiingiwe na dhiki kwa yale waliyonifanyia kipindi kilichopita.» Na akamuamuru alifiche jambo hilo kwao.
Na alipowatayarishia Yūsuf na akawabebesha chakula ngamia wao, aliwaamuru watumishi wake wakakiweka kile chombo, ambacho alikua akiwapimia nacho watu, kwenye vyombo vya ndugu yake Binyamin kwa namna ambayo asitambue yoyote. Basi walipopanda kwenda zao, aliita mwenye kuita akisema, «Enyi wenye ngamia waliobebeshwa chakula, nyinyi ni wezi!»
Wakasema wana wa Ya’qūb, wakimwelekea yule aliyeita, «Ni kitu gani mnachokikosa?»
Yule aliyeita na waliokuwana yeye walisema, «Tumekikosa kipimio ambacho mfalme anapimia nacho. Na zawadi za mwenye kukileta ni twesha ya ngamia mmoja ya chakula.» Na yule aliyeita akasema, «Na mimi naidhamini na kuitolea ahadi hiyo twesha ya ngamia ya chakula.»
Ndugu zake Yūsuf wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu, nyinyi mna uhakika kwa mliyoyashuhudia kutoka kwetu kwamba sisi hatukuja nchi ya Misri kufanya uharibifu, na si katika sifa zetu kuwa wezi.»
Wale waliopewa jokumu la kukitafuta kipimio walisema kuwaambia ndugu zake Yūsuf, «Ni ipi adhabu ya mwizi kwenu nyinyi, iwapo nyinyi ni warongo katika kauli yenu: ‘sisi si wezi’?»
Ndugu zake Yūsuf wakasema, «Malipo ya mwizi ni kwamba yule ambaye kitapatikana kilichoibiwa kwenye mzigo wa ngamia wake basi yeye ndiye malipo yake.» Yaani atakabidhiwa, kwa sababu ya wizi wake, kwa yule aliyemuibia awe mtumwa kwake.»Malipo mfano huu, nayo ni ya kufanywa mtumwa, tunawalipa wenye kufanya dhuluma kwa kuiba. Hii ndiyo dini yetu na mwendo wetu kuhusu wezi.»
wakarudi na ndugu zake Yūsuf kwake, akasimama mwenyewe kupekua mizigo yao. Akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa ndugu yake, ili kuimarisha mpango wake wa kumfanya ndugu yake abakie pamoja na yeye, kisha akamalizikia kwenye vyombo vya ndugu yake na akakitoa chombo humo. Hivyo ndivyo tulivyomsahilishia Yūsuf mpango huu ambao ulimpelekea kumchukua ndugu yake kwenye mamlaka ya mfalme wa Misri. Kwani si katika dini yake kummiliki mwizi, isipokuwa kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu yamepelekea mipango hii na kutaka uamuzi kwenye sheria ya ndugu zake Yūsuf yenye hukumu ya mwizi kufanywa mtumwa. Tunawainua daraja tunaowataka ulimwenguni juu ya mwingine kama vile tulivyomuinua Yūsuf daraja. Na juu ya kila mwenye ujuzi kuna mjuzi zaidi kuliko yeye, mpaka ujuzi ukome kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Mjuzi wa yaliyofichika na yanayoonekana.
Wakasema ndugu zake Yūsuf, iwapo huyu yuwaiba, ametangulia ndugu yake kuiba (wakimaanisha Yūsuf, amani imshukiye). Yūsuf akalificha hilo alilosikia la uzushi kutoka kwao ndani ya nafsi yake,na akauzungumzia moyo wake kwa kusema, «Nyinyi ni wabaya zaidi wa mahali kuliko huyo mliyomtaja, mliponifanyia njama zile zilizokua kutoka kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa sifa za urongo na uzushi mnazozitoa.»
Wakasema kwa njia ya kubembeleza na kutaka kuhurumiwa ili watekeleze ahadi ya baba yao, «Ewe kiongozi, hakika yeye ana mzazi wa kiume mkubwa wa myaka anayempenda na asiyeweza kuwa mbali na yeye. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala ya Binyamin. Sisi tunakuona ni miongoni mwa watenda wema kwa vile unavotutendea sisi na wasiokuwa sisi.»
Yūsuf akasema, «Tunaomba hifadhi ya Mwenyezi Mungu na himaya Yake, tusiwe ni wenye kumchukua yoyote isipokuwa yule ambaye tulipata kipimio chetu kwake, kama mlivyoamua wenyewe. Kwani sisi tukifanya hayo ambayo mnataka tutakuwa ni miongoni mwa wanaohesabiwa kuwa ni waonevu.»
Walipokata tamaa ya kukubali kwake matakwa yao, walikaa kando na watu wakawa wanashauriana baina yao. Mkubwa wao kimyaka alisema, «Je hamjui kuwa baba yenu alichukuwa kwenu ahadi ya mkazo kuwa mtamrudisha ndugu yenu mpaka mshindwe, Na kabla ya tukio hili mlifanya kasoro kuhusu Yūsuf na mkamzungukia kinyume kwa hiana. Kwa hivyo sitaondoka kwenye ardhi ya Misri mpaka baba yangu aniamuru niondoke au Mola wangu Anihukumie niondoke na niweze kumchukua ndugu yangu. Na Mwenyezi Mungu ni Bora wa wanaohukumu na ni muadilifu zaidi wa wenye kutoa uamuzi baina ya watu.
Rudini nyinyi kwa baba yenu, mpeni habari ya yaliyojiri na mwambieni, «Mwano Binyamin ameiba, na hatukushuhudia isipokuwa kwa lile ambalo tuna uhakika nalo. Kwani tumekiona kipimio kwenye mzigo wake, na hatukuwa na ujuzi wa ghaibu kuwa yeye ataiba tulipokuahidi kumrudisha.»
Waliporejea, wakampa habari baba yao yaliyotokea na wakamtaka ahakikishe yale waliyomwambia wakisema, «Na waulize, ewe baba yetu, watu wa Misri na wale waliokuwa pamoja na sisi kwenye msafara tuliorudi nao. Na sisi ni wakweli kwa yale tuliyokusimulia.»
Akawaambia, «Bali nafsi zenu zinazoamrisha mabaya ndizo zilizowapambia njama mlizozipanga, kama mlivyomfanyia Yūsuf. Basi uvumilivu wangu ni uvumilivu mzuri usio na babaiko wala ulalamishi. Kwani huenda Mwenyezi Mungu Akanirudishia wanangu watatu: Yūsuf, nduguye wa kwa baba na mama na ndugu yao mkubwa aliyebaki nyuma kwa sababu ya ndugu yake. Hakika Yeye Ndiye Mjuzi wa hali yangu , Ndiye Mwenye hekima katika uendeshaji mamboWake.»
Ya’qūb akawapa mgongo na asishughulike nao, ukiwa moyo wake umeingia dhiki kwa maneno waliyoyasema, na akasema, «Ewe hasara yangu juu ya Yūsuf!» Na macho yake yakawa meupe, kwa kuondoka weusi wake kwa masikitiko mengi. Moyo wake umejaa tele huzuni, lakini alikuwa akiificha sana.
Wanawe wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu, utendelea kumkumbuka Yūsuf na kuwa na huzuni nyingi juu yake mpaka ukaribie kuangamia au uangamie kikweli, basi ipumzishe nafsi yako.»
Ya’qūb akasema kuwajibu, «Simuonyeshi hamu yangu na masikitiko yangu isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Yeye Ndiye Mwenye kuondoa shida na matatizo. Na ninayajua, kuhusu rehema ya Mwenyezi Mungu na maliwazo Yake, mambo msiyoyajua.»
Ya’qūb akasema, «Enyi wanangu! Rudini Misri mpeleleze habari za Yūsuf na ndugu yake , wala msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa wenye kuukanusha uwezo Wake, wenye kumkataa Yeye.»
Wakaenda Misri. Na walipoingia kwa Yūsuf walisema, «Ewe kiongozi, tumepatikana na ukame na ukavu, na tumekujia na thamani isiyokuwa nzuri na iliyo chache, basi tupe kwa hii thamani kiasi ulichokuwa ukitupa kabla kwa thamani nzuri. Na utunuku kwa kukubali kupokea thamani hii mbaya iliyo chache, na utulegezee juu ya hiyo thamani, hakika Mwenyezi Mungu Anawalipa wema wale wenye kuwasaidia wahitaji kwa mali zao.»
Aliposika maneno yao alilainika juu yao, akajitambulisha kwao na akasema, «Je, mnayakumbuka mabaya mliyomfanyia Yūsuf na ndugu yake mlipokuwa katika hali ya kutojua vile matendo yenu yataishia?»
Wakasema, «Je, kwa kweli wewe ni Yūsuf?»Akasema, «Ndio. Mimi ni Yūsuf na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu Ametukirimu, akatukusanya pamoja baada ya kupambanukana. Hakika Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na akavumilia shida, Mwenyezi Mungu hamuondolei malipo ya wema wake, Hakika atamlipa malipo mema zaidi.»
Wakasema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba Mwenyezi Mungu amekutukuza juu yetu na Amekufanya bora kwa elimu, upole na utukufu, ingawa sisi ni wakosa kwa yale tuliyokufanyia wewe na ndugu yako kwa kukusudia.»
Yūsuf akawaamia, «Hamlaumiwi leo; Mwenyezi Mungu Atawasamehe. Na Yeye ni Mwenye huruma zaidi ya wenye huruma kwa anayetubia dhambi zake na akarejea kwenye utiifu Kwake.»
Na alipowauliza kuhusu baba yake, walimpa habari ya kupofuka macho yake kwa kumlilia. Akawaambia, «Rudini kwa baba yenu mkiwa na kanzu yangu hii, mtupieni usoni mwake na macho yake yatarudi kuona, kisha waleteni kwangu watu wenu wote.»
Msafara ulipotoka nchi ya Misri wakiwa na ile kanzu, Ya’qūb alisema kuwaambia wale waliokuwa na yeye, «Mimi nasikia harufu ya Yūsuf, ingawa nyinyi mtanifanya ni mchache wa akili, mtanicheza shere na mtadai kwamba maneno haya yametoka kwangu bila ya fahamu.»
Waliohudhuria hapo kwake walisema, «Tunaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wewe bado uko kwenye telezo lako la zamani la kumpenda Yūsuf na kwamba wewe hutamsahau.»
Alipokuja mwenye kumpa bishara Ya’qūb kwamba Yūsuf yuko hai, akaitupa kanzu ya Yūsuf usoni mwake akarudi Ya’qūb kuwa yuaona, akajawa na furaha na akawaambia waliokuwa hapo kwake, «Je, sikuwapa habari kwamba mimi nayajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua ya fadhila Zake, rehema Zake na ukarimu Wake.»
Wanawe wakasema, «Ewe baba yetu, tuombee Mola wako Atusamehe na Atusitirie dhambi zetu, hakika sisi tulikuwa wakosa katika yale tuliyomfanyia Yūsuf na ndugu yake.»
Ya’qūb akasema , «Nitamuomba Mola wangu Awasamehe dhambi zenu, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake wanaotubia, ni Mwingi wa rehema kwao.»
Ya’qūb na watu wa nyumbani kwake wakatoka kuelekea Misri wakimkusudia Yūsuf. Walipofika kwake, Yūsuf aliwakumbatia wazazi wake wawili na akawaambia (wao wote), «Ingieni Misri kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu na hali mkiwa mko kwenye amani na mumeepukana na shida, ukame na kila zito.»
Akawakalisha wazazi wake wawili kwenye kitanda cha ufalme wake kwa njia ya kuwatukuza. Na wazazi wake na ndugu zake kumi na moja wakamsalimia kwa kumuinamia kwa kumwamkia na kumtukuza na sio kumuabudu na kumnyenyekea. Na hilo lilikuwa linaruhusiwa katika Sheria yao, na limeharamishwa katika Sheria yetu, kwa ajili ya kuziba njia inayopelekea kwenye ushirikina. Na Yūsuf akamwambia baba yake, «Kusujudu huku ndio uaguzi wa ndoto yangu niliyokusimulia kabla, katika udogo wangu, Mwenyezi Mungu Ameifanya ni kweli. Na amenifadhili aliponitoa jela na akawaleta nyinyi kutoka jangwani, baada ya Shetani kuharibu uhusiano wa undugu baina yangu mimi na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni Mpole wa kupitisha Analolitaka. Yeye Anayajua sana maslahi ya waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake.»
Kisha Yūsuf alimuomba Mola wake akisema, «Mola wangu! Umenipa ufalume wa Misri, na umnifundisha uaguzi wa ndoto na elimu nyinginezo. Ewe Muumba, na Mtengenezaji, mbingu na ardhi! Wewe Ndiye Msimamizi wa mambo yangu ulimwenguni na Akhera. Nifishe unichukue kwako nikiwa Muislamu na unikutanishe na waja wako wema miongoni mwa Manabii watenda mema na wasafiwa walioteuliwa.»
Hayo yaliyotajwa ya habari za Yūsuf ni miongoni mwa habari za ghaibu, tunakuelezea , ewe Mtume, kwa njia ya wahyi. Na hukuwako pamoja na ndugu zake Yūsuf walipompangia kumtia kisimani na wakamfanyia hila yeye na baba yake. Hii inaonesha dalili ya ukweli wako na kwamba Mwenyezi Mungu Anakuletea wahyi.
Hawakuwa wengi wa washirikina miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, ni wenye kukusadiki wala kukufuata, ingawa una pupa juu ya Imani yao. Basi usisikitike kwa hilo.
Na hutaki kwa watu wako ujira ya kuwaongoa kwenye Imani. Na yale uliyotumwa nayo ya Qur’ani na uongofu ni mawaidha kwa watu wote wanajikumbusha kwayo na wanaongoka.
Na dalili zenye kuonyesha upweke wa Mwenyezi Mungu na uwezo Wake ni nyinygi, zimeenea kwenye mbingu na ardhi, kama jua, mwezi, majabali na miti. Wanaziona lakini wamezipa mgongo, hawazifikirii na wala hawazingatii.
Na hawa wenye kuzipa mgongo dalili za Mwenyezi Mungu hawakubali kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaumba, ni Mwenye kuwapa riziki, ni Muumba wa kila kitu na ni Mstahiki wa kuabudiwa isipokuwa katika hali ya kumshirikisha kwa kuabudu kwao masanamu na mizimu. Mwenyezi Mungu Ametukuka na kuepukana na hilo kabisa.
Je, wana chochote kinachowafanya wameaminika isiwashukie wao adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu yenye kuwaenea au iwajie wao Siku ya Kiyama ghafla na hali wao hawatambui wala hawana hisia na hilo.
Waambie, ewe Mtume, «Hii ni njia yangu, ninaita kwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, nikiwa kwenye hoja inayotoka kwa Mwenyezi Mungu na uhakika, mimi na anayenifuata. Na ninamuepusha Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, na washirika na mimi si katika wale wanaomshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu mtu mwingine.»
Hatukuwatuma kabla yako, ewe Mtume, kwa watu isipokuwa wanaume miongoni mwao ambao tunawateremshia wahyi wetu, na wao ni miongoni mwa watu wa mijini, kwani hao wana uwezo zaidi wa kuuelewa ulinganizi na ujumbe, wawaamini wenye kuongoka kwenye haki na wawakanusha wenye kupotea njia yake. Basi si watembee katika ardhi wajionee ulikuwa vipi mwisho wa wakanushaji waliopita na ni maangamivu gani yaliyowashukia? Na malipo mema ya Nyumba ya Akhera ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani, kwa walioamini na wakamuogopa Mola wao. Basi hamfikirii mkazingatia?
Na usiwe na haraka, ewe Mtume, ya kupata ushindi juu ya wanaokukanusha, kwani Mitume kabla yako hawakuwa wakijiwa na ushindi wa haraka kwa hekima tunayoijua. Ifikapo hadi ya Mitume kukata tamaa na watu wao na kuwa na hakika kwamba watu wao wamewakanusha na hakuna tamaa ya wao kuamini, ushindi utawajia wakati ambapo shida imezidi, basi hapo tuwaokoe tunaowataka kati ya Mitume na wafuasi wao. Na adhabu yetu haitorudishwa kutoka kwa Aliyefanya uhalifu na akmfanyia ujasiri Mwenyezi Mungu. Katika hili kuna kumliwaza Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Kwa hakika kwenye habari za Mitume tulizokuelezea na mambo yaliyowakumba wenye kukanusha kuna mawaidha kwa wenye akili timamu. Hii Qur’ani haikuwa ni habari ya urongo iliyozuliwa, lakini tumeiteremsha ikiwa ni yenye kutolea ushahidi ukweli wa vitabu vilivyoteremshwa vilivyotangulia na kwamba vinatoka kwa Mwenyezi Mungu, na ikiwa ni ufafanuzi wa kila ambalo waja wanalihitaji la kuhalalishiwa na kuharamishiwa, linalopendeza na linalochukiza na mengineyo, na ikiwa ni muelekezo kutoka kwenye upotevu na ni rehema, kwa wenye Imani, ya kuzifanya nyoyo zao ziongoke, wapate kuyafuata kivitendo maamrisho na makatazo yaliyomo.