ﯟ
surah.translation
.
ﰡ
«Qāf» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah. Anaapa Mwenyezi Mungu kwa Qur’ani tukufu, yenye ubora na heshima.
Bali wale wenye kumkanusha Mtume waliona ajabu kuwa walijiwa na muonyaji miongoni mwao anayewaonya mateso ya Mwenyezi Mungu, basi wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume Wake walisema, «Hili ni jambo geni la kuonewa ajabu.
«Je, tunapokufa na tukawa mchanga, itawezekana vipi kurejea baada ya hapo tukawa kama tulivyokuwa? Hayo ni marajeo ambayo kutukia kwake kuko mbali.»
Hakika tunakijua kile ambacho ardhi kinakipunguza na kukimaliza katika miili yao, na tuna Kitabu kilichohifadhiwa kutokana na mageuzo na mabadiliko, kilichosajiliwa kila kitu kitakachowapitia katika maisha yao na baada ya kufa kwao.
Bali hawa washirikina waliikanusha Qur’ani ilipowajia. Wao wako kwenye hali ya babaiko na kuchanganyikiwa, hawasimami imara kwenye jambo lolote, na hawana kituo cha kutulia.
Kwani walighafilika walipokanusha Ufufuzi, wasianagalie mbingu juu yao: vipi tulizijenga zikiwa zimelingana sawa pande zote, limeimarika jengo lake, na tukazipamba kwa nyota, na hazina pasuko na nyufa, zimesalimika na hitilafu na kasoro?
Na ardhi tumeipanua na kuitandika, na tukaweka humo majabali yaliyojikita, ili ardhi isiende mrama na watu wake, na tukaotesha humo kila aina ya mimea yenye mandhari ya kupendeza na yenye kunufaisha, inayomfurahisha mwenye kuiangalia.
Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu, ardhi na vilivyomo baina ya hivyo viwili miongoni mwa alama kubwa, ili viwe ni mazingatio ya kumfanya mtu aone na atoke kwenye giza la ujinga, na ni ukumbusho kwa kila mja mnyenyekevu, mwenye kucha na kuogopa, mwenye kurejea sana kwa Mwenyezi Mungu Aliyeshinda na kutukuka.
Na tumeteremsha kutoka juu mvua yenye manufaa mengi, tukaotesha kwayo mabustani yenye miti mingi na nafaka za mimea ya nafaka zinazovunwa.
Na tukaotesha mitende mirefu yenye makarara yaliyojaza na kupandana.
Tumeviotesha hivyo viwe ni riziki za waja za wao kuzila kulingana na mahitaji yao, na tukahuisha, kwa maji haya tuliyoyateremsha, ardhi iliyokuwa kavu na kame, haina nafaka wala mimea mingine. Na kama tunavyohuisha, kwa maji hayo, ardhi iliyokufa, tutawatoa nyinyi Siku ya Kiyama mkiwa hai baada ya kufa.
Walikanusha, kabla ya hawa washirikina miongoni mwa Makureshi, watu wa Nūḥ, watu wa Kisima na Thamūd.
Na 'Ād na Fir'awn na watu wa Lūṭ.
Na watu waliokuwa kwenye tuka la miti nao ni watu wa Shu'ayb, na watu wa Tubba' wa Himyar. Watu wote hao waliwakanusha Mitume wao, ikapasa juu yao adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaonya nayo kwa ukafiri wao.
Kwani tulishindwa kuanzisha uumbaji wa kwanza tuliyouanzisha na hakukuwa na kitu chochote, mpaka tushindwe kuwarudisha wao wakiwa viumbe wapya baada ya kutoweka kwao? Hilo halitushindi. Bali sisi ni waweza wa hilo, lakini wao wako kwenye mshangao na shaka juu ya jambo la kufufuliwa na kukusanywa.
Hakika tumemuumba binadamu na tunakijua kile ambacho nafsi yake inamhadithia kwacho. Na sisi tuko karibu na yeye zaidi kuliko ukambaa wa roho (nao ni mshipa ulioko shingoni unaoshikana na moyo).
Pindi Malaika wawili wanaotunza, kuliani kwake na kushotoni kwake, wanapoyaandika matendo Yake: aliye kuliani anaandika mema na aliye kushotoni anaandika maovu.
Hatamki neno kulisema isipokuwa mbele yake pana Malaika anayetunza maneno yake na kuyaandika, naye ni Malaika ambaye yupo wakati wote aliyeandaliwa kwa hilo.
Na hapo ikaja shida ya mauti na kizaazaa chake na ukweli usiozuilika wala kukimbilika! Hali hiyo ndiyo ambayo ulikuwa, ewe binadamu, ukiikimbia na kuihepa.
Hapo baragumu likavuviwa mvuvio wa pili wa Ufufuzi. Mvuvio huo utakuwa kwenye Siku ya matekelezo ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaahidi wakanushaji.
Na ije kila nafsi, wakiwa pamoja nayo Malaika wawili: mmoja anaiongoza kwenye Mkusanyiko, na mwingine Anaitolea ushahidi wa ililolifanya duniani, la kheri na shari.
Kwa hakika wewe ulikuwa katika mghafala kuhusu tukio hili unaloliona leo, ewe binadamu, ndipo tukakifunua kifiniko chako kilichoziba moyo wako, kughafilika kukakuondokea, basi leo macho yako, katika kile unachokitolea ushahidi, ni makali.
Na Malaika mwandishi mwenye kumtolea ushahidi atasema, «Haya ndiyo niliyonayo kutoka kwenye rikodi ya matendo yake. Nayo imetayarishwa, imehifadhiwa na ipo hapa kwangu.»
Na Mwenyezi Mungu Aseme kuwaambia Malaika wawili: mwenye kuongoza na yule shahidi, baada ya kutolewa uamuzi baina ya viumbe, «Mtupeni ndani ya Jahanamu kila mwenye kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki, aliye mwingi wa ukafiri na ukanushaji, mwenye kuipinga haki,
mwenye kuzuia kutekeleza haki zilizo juu yake katika mali yake, anaye wadhulumu waja wa Mwenyezi Mungu na kukiuka mipaka Yake, anayelifanyia shaka agizo la Mwenyezi Mungu na onyo Lake,
aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kukiabudu kiabudiwa kingine miongoni mwa viumbe Vyake pamoja na Yeye. Mtupeni ndani ya adhabu ya moto wa Jahanamu ulio mkali.»
Shetani wake aliyekuwa na yeye ulimwenguni atasema, «Mola wetu! Mimi sikumpoteza, lakini alikuwa kwenye njia iliyokuwa mbali na njia ya uongofu.»
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aseme, «Msitete mbele yangu leo kwenye Kisimamo cha Malipo na Hesabu. Kwani hilo halina faida, na mimi niliwaletea duniani onyo la adhabu kwa aliyenikufuru na kuniasi.
«Halibadilishwi neno kwangu, na simuadhibu yoyote kwa dhambi za mtu mwingine, simuadhibu yoyote isipokuwa kwa dhambi zake baada ya kusimamiwa na hoja.»
Watajie watu wako, ewe Mtume, Siku tutakayoiambia Jahanamu, «Je umeshajaa?» Na Jahanamu iseme, «Je kuna nyongeza yoyote ya majini na binadamu?» Hapo Mola, uliotukuka utukufu wake, Aweke unyayo Wake ndani yake, na hapo ijikusanye na ijikunjekunje na iseme, «Basi! Basi!»
Na hapo wachamungu wakaribishiwe Pepo, iwepo mahali ambapo si mbali na wao, wawe waiona, kwa kuwaongezea furaha zao.
Na waambiwe hao Waumini, «Hii ndiyo ile mliokuwa mkiahidiwa, enyi wachamungu, kwa kila mtubiaji dhambi zake, mwenye kukitunza kila kinachomkurubisha kwa Mola Wake miongoni mwa mambo ya lazima na ya utiifu;
mwenye kumcha Mwenyezi Mungu duniani na akakutana na Yeye Siku ya Kiyama kwa moyo wa mwenye kutubia dhambi zake.»
Na hapo waambiwe hao Waumini, «Ingieni Peponi kuingia kunakoshikamana na kusalimika na maafa na shari, hali ya kuhifadhiwa na mambo yote mnayoyachukia. Hiyo ndiyo Siku ya starehe za milele zisizokatika.»
Watapewa hawa Waumini ndani ya Pepo wanavyovitaka. Na tuna nyogeza za neema juu ya zile tulizowapa; kubwa zaidi la neema hizo ni kutazama uso wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Na tuliwaangamiza, kabla ya hao washirikina wa Kikureshi, ummah wengi. Walikuwa wana nguvu na ujebari kuliko wao. Walizunguka mijini wakafuata kila njia kutaka kuyakimbia maangamivu. Basi je, kuna makimbilizi yoyote ya kujiepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu itakapowajia?
Hakika katika kuziangamiza kame zilizopita kuna mazingatio kwa aliyekuwa na moyo wa kufahamia na mashikio ya kusikilizia, na akawa yupo kwa moyo wake, hakusahau wala hakughafilika
Na kwa hakika tuliumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili miongoni mwa viumbe kwa muda wa Siku sita, na hatukupata tabu yoyote wala shida. Katika uweza huu mkubwa kuna dalili ya nguvu zaidi ya kuwa Yeye, Aliyetakasika, Ana uweza wa kuhuisha wafu.
Basi vumilia, ewe Mtume, kwa yale wanayoyasema wakanushaji, kwani Mwenyezi Mungu Yuko chonjo nao. Na swali, kwa ajili ya Mola wako kwa kumshukuru, Swala ya Alfajiri, kabla ya jua kuchomoza, na Swala ya Alasiri kabla ya jua kuchwa,
na uswali kipindi cha usiku na umtakase Mola Wako kwa kumshukuru baada ya Swala.
Na usikilize, ewe Mtume, siku Malaika atakapoita kwa kupuliza kwenye Baragumu kutoka sehemu iliyo karibu.
Siku watakapousikia ukulele wa Ufufuzi wa ukweli usio na shaka, hiyo ndiyo Siku ya waliyo makaburini kutoka makaburini mwao.
Ni sisi tunaohuisha viumbe na kuwafisha duniani, na ni kwetu sisi ndipo mwisho wao wote watakapofikia Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na walipwe.
Siku ambayo ardhi itapasukapasuka itoe wafu waliozikwa humo, watoke mbio kuelekea upande wa yule anayeita. Kuwakusanya watu hivyo kwenye Kisimamo cha Hesabu ni jambo sahali kwetu na rahisi.
Sisi ni wajuzi zaidi kwa wanayoyasema hawa washirikina, ya kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na kukanusha aya Zake. Na hukuwa wewe, ewe Mtume, umepewa nguvu juu yao ya kuwalazimisha waingie katika Uislamu, hakika ni kwamba wewe umetumilizwa uwe mfikishaji. Basi mkumbushe kwa Qur’ani anayeogopa onyo langu, kwa kuwa asiyeogopa onyo (la Mwenyezi Mungu) hafaidiki kwa kukumbushwa.