ﯪ
surah.translation
.
ﰡ
Vimemtakasa Mwenyezi Mungu na kumwepusha na kila kisichonasibiana na Yeye vyote vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na Yeye ni Mshindi Ambaye hakuna mwenye kushindana na Yeye, Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake.
Enyi miliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Kwa nini mnatoa ahadi au mnasema maneno bila kuyatekeleza? Haya ni makaripio kwa ambaye matendo yake yanaenda kinyume na maneno yake.
Ni machukivu makubwa sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi mnaposema kwa ndimi zenu maneno msiyoyafanya.
Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wale wanaopigana katika njia Yake wakiwa wamejipanga kama kwamba wao ni jengo lililopangika na kuimarika kwa namna ya kutoweza adui kupenyeza kupitia jengo hilo. Katika aya hii pana maelezo ya ubora wa jihadi na wenye kupigana jihadi, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila upungufu, Anawapenda waja Wake Waumini wanapojipanga kupambana na maadui wa Mwenyezi Mungu.
Wakumbushe watu wako, ewe Mtume, pindi aliposema Nabii wa Mwenyezi Mungu. Mūsā, amani imshukie, akiwaambia watu wake, «Kwa nini mnaniudhi kwa maneno na vitendo, na hali nyinyi mnajua kuwa mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu?» Basi walipopotoka na kuwa kando na haki pamoja na kuwa wanaijua na wakaendelea juu ya hilo, Mwenyezi Mungu Aliziepusha nyoyo zao wasiukubali uongofu, ikiwa ni mateso kwao kwa sababu ya upotevu wao waliojichagulia wenyewe. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu wenye kutoka nje ya utiifu na njia ya haki.
Wakumbushe ewe Mtume, watu wako pindi Īsā, mwana wa Maryam, alipowaambia watu wake, «Mimi ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwenu, ni mwenye kusadikisha Taurati iliyokuja kabla yangu na ni mwenye kushuhudilia ukweli wa Mtume atakayekuja baada yangu, jina lake ni Ahmad, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ni mwenye kulingania watu wamuamini, basi alipowajia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa aya zilizo wazi walisema, «Huu ni uchawi waziwazi.»
Na hakuna yoyote aliye dhalimu zaidi na adui zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo na akamfanya kuwa ana washirika wa kuabudiwa, na hali yeye anaitwa aingie kwenye Uislamu na kumpwekesha Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa ibada. Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii, wale waliozidhulumu nafsi zao kwa kukufuru na kukanusha, kwenye njia ambayo ndani yake kuna kufaulu kwao
Hawa madhalimu wanataka kuitangua haki aliyotumilizwa kwayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, nayo ni Qur’ani, kwa maneno yao ya urongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuipa nguvu haki kwa kuitimiza Dini Yake japokuwa wale wapingaji wenye kukanusha watachukia.
Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad kwa Qur’ani na Dini ya haki ili Aifanye kuwa juu ya dini zilizo kinyume nayo japokuwa washirikina watachukia hilo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Je niwaonyeshe njia ya biashara yenye mapato makubwa ambayo itawaokoa na adhabu yenye kuumiza?
Ni mwendelee daima kumuamini kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na mpigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini Yake kwa mali mnayoyamiliki na nafsi zenu, hilo ni bora kwenu kuliko biashara ya duniani. Basi mkiwa mnajua vitu venye madhara na manufaa, fuateni amri hiyo.
Mkifanya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha nyinyi, enyi Waumini, Atayasitiri madhambi yenu na Atawatia kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake inapita mito, na makazi yaliyotakasika na kusafishika ndani ya Mabustani ya kukaa daima bila ya kukatika. Huko ndiko kufaulu ambako hakuna kufaulu zaidi yake.
Na kuna neema nyingine kwenu, enyi Waumini, mtaipenda, nayo ni msaada kutoka kwa mwenyezi Mungu utakaowajia na ushindi wa haraka utakaopatikana mikononi mwenu. Na wape bishara Waumini, ewe Mtume, ya kunusuriwa na kupata ushindi duniani na kupata Pepo kesho Akhera.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Kuweni watetezi wa dini ya Mwenyezi Mungu kama walivyokuwa marafiki wa kidhati wa ‘Īsā watetezi wa Dini ya Mwenyezi Mungu alipowaambia wao Īsā, «Ni nani atakayesimama kunihami na kunisaidia katika mambo ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu?» Wakasema, «Sisi ndio watetezi wa Dini ya Mwenyezi Mungu.» Hapo kundi moja la Wana wa Isrāīl likaongoka na kundi lingine likapotea, tukawapa nguvu wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na tukawapa ushindi juu ya wale waliowafanyia uadui miongoni mwa vipote vya Wanaswara, wakawa na nguvu juu yao kwa kutumilizwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.