ﯯ
surah.translation
.
ﰡ
Ewe Mtume! Mbona unajizuia nafsi yako na halali Aliyokuhalalishia Mwenyezi Mungu kwa kuwa unataka kuwaridhisha wake zako? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukusamehe, ni Mwenye huruma kwako.
Kwa hakika Amepasisha Mwenyezi Mungu kwenu, enyi Waumini, kuvihalalisha viapo vyenu kwa kuvitolea kafara. Kafara yenyewe ni kuwalisha masikini kumi au kuwavisha au kuacha shingo huru. Na asiyepata cha kutoa, basi afunge siku tatu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwanusuru nyinyi na kuyasimamia mambo yenu. Na Yeye Ndiye Mjuzi wa mambo yanayowafaa Akayapitisha kwenu, Ndiye Mwingi wa hekima kwenye maneno Yake na matendo Yake.
Na pindi Mtume alipompa siri mke wake Hafsah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, ya mazungumzo fulani, na yeye alipomwambia maneno hayo mke mwenzake 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, na Mwenyezi Mungu Akamjulisha Mtume Wake kuwa mkewe ameitoa siri yake, alimjulisha Hafsah sehemu ya maneno aliyoyatoa na akayanyamazia mengine asimwambie kwa kuchunga heshima. Basi Mtume alipomwambia Hafsah yale mazungumzo aliyoyatangaza, alisema huyo mke, «Ni nani aliyekwambia maneno hayo?» Akasema Mtume, «Aliyenambia hayo ni Mwenyezi Mungu, Aliye Mwingi wa ujuzi na utambuzi, Ambaye hakifichamani Kwake chenye kujificha chochote.
Iwapo mtarudi kwa Mwenyezi Mungu (ewe Hafsah na 'Aishah) basi yatakuwa yamepatikana kwenu yanayopelekea kukubaliwa toba yenu, kwa kuwa nyoyo zenu zilielekea kwenye kuyapenda yale aliyoyachukia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ya kutoa siri yake. Na mtakaposaidiana juu yake kwa kufanya yanayomuudhi, basi Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wake na Mtetezi wake na Jibrili na Waumini wema. Na Malaika, baada ya usaidizi wa Mwenyezi Mungu, ni wasaidizi wake na watetezi juu ya yoyote anayemuudhi na kumfanyia uadui.
Linalotarajiwa kwa Mola wake iwapo atawaacha nyinyi, enyi wake zake, ni amuoze yeye, badala yenu nyinyi, wake wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu kwa kumtii, wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kumtii Mwenyezi mungu, wenye kurudi kwenye yale anayoyapenda Mwenyezi Mungu ya kumtii Yeye, wenye kumuabudu kwa wingi, wenye kufunga sana, wakiwa wake wakuu miongoni mwao na wanawali.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Zilindeni nafsi zenu kwa kuyatenda yale ambayo Amewaamrisha kwayo Mwenyezi Mungu na kuyaepuka yale ambayo Amewakataza nayo, na walindeni watu wenu kwa kile mnachotumia kujilinda nyinyi wenyewe na Moto ambao kuni zake ni watu na majiwe. Watasimamia kuadhibiwa watu wa Motoni Malaika wenye nguvu walio thabiti katika usimamizi wao, wasioenda kinyume na Mwenyezi Mungu katika maamrisho Yake na wanaotekeleza yale wanayoamrishwa.
Na wataambiwa wale waliokanusha kwamba Mwenyezi mungu Ndiye Mola wa haki na wakamkufuru, watakapoingizwa Motoni, «Msitafute nyudhuru Siku ya Leo, ukweli ni kwamba nyinyi mnapewa malipo ya yale ambayo mlikuwa mkiyafanya duniani.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Acheni madhambi yenu na mrudi kwenye kumtii Mwenyezi Mungu, kurudi kwa mwisho kusikokuwa na ufanyaji maasia tena kwa kutarajia Mola wenu Awafutie maovu ya matendo yenu na Awaingize kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya majumba yake ya fahari inapita mito ya maji, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Hatamfedhehi Nabii na walioamini pamoja naye wala hatawatesa, bali Atavipandisha juu vyeo vyao. Nuru ya watu hawa itakuwa inatembea mbele yao na kuliani mwao huku wakisema, «Mola wetu! Tukamilishie sisi nuru yetu mpaka tuvuke Ṣirāṭ na tuongoke njia ya kwenda Peponi, na utusamehe na uyatupilie mbali madhambi yetu na uyasitiri, kwani wewe Kwa hakika ni Muweza juu ya kila kitu.»
Ewe Nabii! Pigana jihadi na wale waliouonyesha ukafiri waziwazi na wakautangaza, na pigana nao kwa upanga, na pigana jihadi na wale waliouficha ukafiri na kuufinika kwa hoja na kwa kusimamisha hukumu za Sheria na vitambulisho vyaa Dini. Na utumie ukali na ugumu katika kupigana jihadi na makundi mawili hayo. Na makazi yao ambayo watakwenda kukaa huko Akhera ni moto wa Jahanamu. Na ni marejeo maovu mno hayo watakayoyarejea!
Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa hali ya makafiri- katika kutangamana kwao na Waislamu, kuwa karibu na wao na kutangamana nao na kwamba hilo halitawanufaisha kwa kuwa wamemkufuru Mwenyezi Mungu- kuwa ni kama hali ya mke wa Nabii wa Mwenyezi Mungu, Nūḥ, na mke wa Nabii wa Mwenyezi mungu, Lūṭ, kwa kuwa wote wawili walikuwa chini ya hifadhi ya ndoa ya waja wawili wema miongoni mwa waja wetu, ukapatikana kutoka kwao kuwafanyia uhaini wa kidini, kwani wote wawili walikuwa makafiri. Mitume wawili hawa hawakuweza kuwatetea wake zao na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na wakaambiwa wake wawili hao, «Ingieni Motoni pamoja na wenye kuingia huko.» Katika kupiga mfano huu pana dalili ya kwamba kuwa karibu na Manabii na watu wema hakufai kitu iwapo mtu mwenyewe ana matendo mabaya.
Na Mwenyezi Mungu Anapiga mfano wa hali ya Waumini- waliomuamini Mwenyezi Munmgu, wakamuabudu Peke Yake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo na kwamba wao hakuwadhuru wao kule kutangamana kwao na makfiri katika maingilaiano yao- kuwa ni kama hali ya mke wa Fir'awn aliyekuwa kwenye hifadhi ya ndoa ya aliyekuwa muovu mno miongoni mwa wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu, na hali yeye alikuwa anamuamini Mwenyezi Mungu, pindi aliposema, «Mola wangu! Nijengee Nyumba huko kwako Peponi na uniokoe na utawala wa Fir'awn na ukafiri wake na yale matendo maovu yanayotokana na yeye, Na uniokoe na watu wenye kumfuata katika udhalimu na upotevu, na uniokoe na mateso yao.
Na Mwenyezi Mungu Anapiga mfano kwa walioamini. Mfano wenyewe ni Maryam binti 'Imran aliyeihifadhi tupu yake na akailinda na uzinifu, basi mwenyezi Mungu Akamuamrisha Jibrili, amani imshukie, apulize kwenye mfuko wa nguo yake. Na ule mpulizo ukafika kwenye uzao wake. Hapo akabeba mimba ya ‘Īsā, amani imshukie, akayaamini maneno ya Mola wake, akafuata kivitendo Sheria Zake Alizozipasisha kwa waja Wake na vitabu Vyake Alivyoviteremsha kwa Mitume Wake, na akawa ni miongoni mwa wale wenye kumtii Yeye.