ﯣ
surah.translation
.
ﰡ
Kimekaribia Kiyama na mwezi umepasuka pande mbili, pale makafiri wa Makkah walipomtaka Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshikie, awaoneshe alama, na yeye akamuomba Mwenyezi Mungu na akawaonesha hiyo alama.
Na washirikina wakiiona dalili na ushahidi juu ya ukweli wa Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanakataa kuziamini na kuzisadiki hali ya kukanusha na kupinga, na wanasema baada ya dalili kujitokeza, «Huu ni uchawi wenye ubatilifu na wenye kuondoka na kupotea usiokuwa na sifa ya kudumu.
Na walimkanusha Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakafuata upotevu wao na kile cha ukanushaji ambacho matamanio yao yaliwavuta kwacho. Na kila jambo, la kheri au la shari, litawashukia wanaostahili Siku ya Kiyama yatakapodhihiri malipo na mateso.
Na hakika ziliwajia makafiri wa Kikureshi habari za ummah waliokanusha mitume wao na adhabu iliyowashukia zinazotosha kuwakemea na kuwafanya warudi nyuma waache ukafiri wao na upotevu wao.
Hii Qur’ani iliowajia ni hekima kubwa iliyofikia upeo. Basi yatawafalia nini maonyo wale watu waliyoipa mgongo na kuikanusha?
Kwa hivyo, wapuuze, ewe Mtume, na uingojee Siku kubwa, Siku Malaika Atakapoita, kwa kuvuvia kwenye baragumu, kwenye jambo linalotisha linalochukiza, nalo ni Kisimamo cha Hesabu.
Hali yakuwa macho yao yamedhalilika, wanatoka makaburini kama kwamba wao kwa kuenea kwao na upesi wa kuenda kwenye kuhesabiwa, ni nzige walioenea pambizoni mwa anga,
hali ya kukimbilia kile walichoitiwa. Hapo waseme makafiri, «Hii ni siku nzito yenye vituko vikubwa.»
Walikanusha kabla ya watu wako, ewe Mtume, watu wa Nūḥ wakamkanusha mja wetu Nūḥ na wakasema, «Yeye ni Mwendawazimu.» Wakamkaripia huku wakimtisha kwa aina nyingi za mateso iwapo hatakomeka na ulinganizi wake.
Nūḥ akamuomba Mola wake kwamba «mimi ni dhaifu wa kupambana na hawa, basi nisaidie mimi kwa kuwapa mateso yanayotoka kwako kwa kukukanusha wewe.»
Basi tukayakubali maombi yake, na tukafungua milango ya mbingu kwa maji mengi yenye kuteremka kwa nguvu,
na tukapasua ardhi tukatoa chemchemi za maji yanayotoka kwa kasi, yakakutana maji ya mbinguni na maji ya ardhini kuwaangamiza wao kwa vile Alivyowakadiria mwenyezi Mungu, yakiwa ni malipo ya ushirikina wao.
Tukambeba Nūḥ na waliokuwa pamoja naye juu ya jahazi ya mbao zilizopigwa misumari,
ikawa inatembea kwa uangalizi wetu na utunzi, na tukawazamisha waliokanusha, ikiwa ni malipo yao kwa ukafiri wao na kwa kumnusuru Nūḥ, amani imshukie. Hapa pana dalili ya kuthibitisha sifa ya macho mawili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, kama inavyonasibiana na Yeye.
Na kwa hakika tulikibakisha kisa cha Nūḥ pamoja na watu wake kiwe ni mazingatio na dalili ya uweza wetu kwa walio baada ya Nūḥ, ili wazingatie na wawaidhike kwa lililowapata ummah huu uliokanusha Mtume wao,
basi je kuna wakuwaidhika awaidhike? Na ilikuwa vipi adhabu yangu na maonyo yangu kwa aliyenikufuru mimi, akawakanusha Mitume wangu na asiwaidhike kwa walichokuja nacho? Hakika hiyo ilikuwa kubwa yenye uchungu.
Kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani ili isomwe na ihifadhiwe, na pia maana yake ili ieleweke na izingatiwe. Je kuna mwenye kuwaidhika nayo? Katika aya hii na mfano wake katika hii Sura kuna kuhimiza kusoma Qur’ani kwa wingi, kujifunza na kuifundisha.
Watu wa kabila la 'Ād walimkanusha Hūd tukawatesa, basi ilikuwa vipi vile nilivyowaadhibu wao kwa ukafiri wao na vile nilivyowaonya wao kwa kumkanusha Mtume wao na kutomuamini? Ilikuwa kubwa yenye uchungu.
Hakika sisi tuliwapelekea upepo wenye baridi kali katika siku korofi yenye kuendelea kwao kwa adhabu na maangamivu,
yenye kung’oa watu kutoka mahali walipo kwenye ardhi na kuwatupa kwa vichwa vyao, kuzivunja shingo zao na kuvipambanua vichwa vyao na miili yao na kuwaacha kama mitende iliyong’olewa kutoka mashinani.
Basi ilikuwa vipi adhabu yangu na onyo langu kwa aliyenikufuru na akawakanusha Mitume wangu na Asiwaamini? Hakika ilikuwa kubwa yenye uchungu!
Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ieleweke na izingatiwe kwa anayetaka kuwaaidhika na kuzingatia. Je kuna yoyote mwenye kuwaidhika nayo? Hapa pana kuhimiza kusoma Qur’ani kwa wingi, kujifunza na kufundisha.
Walizikanusha watu wa kabila la Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, alama ambazo walionywa nazo,
wakasema, «Je tumfuate binadamu mmoja miongoni mwetu na hali sisi ni wengi na yeye ni mmoja? Tukifanya hivyo tutakuwa mbali na usawa na tutakuwa ni wenye wazimu.
«Je Ameteremshiwa wahyi na kuhusishwa yeye pekee kwa utume miongoni mwetu, na hali yeye ni mmoja katika sisi? Bali yeye ana urongo mwingi na kiburi.»
Basi wataona wakati wa adhabu kuwateremkia hapa duniani na huko Akhera, ni nani mrongo mwenye kiburi?
Sisi tutamtoa ngamia waliomtaka kutoka kwenye jiwe, huo ukiwa ni mtihani kwao. Basi ingojee, ewe Ṣāliḥ, adhabu itakaowashukia, na usubiri katika kuwalingania na juu ya makero wanayokufanyia.
Na uwape habari kwamba maji yamegawanywa baina ya watu wako na ngamia: ngamia ana siku yake na nyinyi mna siku yenu, kila siku ya kunywa atakuja yule ambaye ni siku yake aliyogawanyiwa, na atakatazwa yule ambaye si siku yake aliyogawanyiwa.
Wakamuita mwenzao wakimshawishi amchinje, basi akamshika yule ngamia kwa mkono wake na akamchinja, na mimi nikawatesa,
basi ilikuwa vipi nilivyowaadhibu kwa ukafiri wao na nilivyowaonya waliowaasi Mitume wangu? Hakika hiyo ilikuwa adhabu kubwa yenye uchungu.
Sisi tuliwateremshia Jibrili, akawapigia ukulele mmoja, wakatoeka hadi wa mwisho wao, wakawa ni kama nyasi zilizokauka zilizo nyepesi kuvunjika, zinazofanyiwa boma la ngamia na mifugo.
Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ifahamike na izingatiwe kwa anayetaka kuwaidhika na kuzingatia. Basi je kuna yoyote mwenye kuwaidhika nayo?
Walizikanusha watu wa Lūṭ aya za Mwenyezi Mungu walioonywa nazo.
Sisi tuliwateremshia upepo mkali unaowarushia mawe, isipokuwa watu wa Lūṭ wa nyumbani, kwani wao tuliwaokoa na adhabu kipindi cha mwisho wa usiku,
ikiwa ni neema itokayo kwetu juu yao. Kama tulivyompa malipo mema Lūṭ na watu wake wa nyumbani, tukawapa neema na tukawaokoa na adhabu yetu ndivyo tunavyowalipa mema waliotuamini na kutushukuru.
Kwa hakika Lūṭ aliwaonya watu wake mateso ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake, wasimsikilize, bali walilifanyia shaka hilo na wakamkanusha.
Na kwa hakika walitaka kwake kufanya uchafu na wageni wake ambao ni Malaika, tukayafuta macho yao wasione chochote na wakaambiwa, «Onjeni adhabu yangu na onyo langu alilowaonya nalo Lūṭ, amani imshukie.»
Na iliwajia kipindi cha asubuhi adhabu ya kuendelea, imejikita kwao mpaka iwafikishe kwenye adhabu ya Akhera. Adhabu yenyewe ni kuvurumizwa mawe na kuipindua miji yao kwa namna ambayo kulikokuwa juu kukawa chini,
na wakaambiwa, «Onjeni adhabu yangu niliyowateremshia nyinyi kwa sababu ya ukafiri wenu na ukanushaji wenu onyo langu alilowaonya nalo Lūṭ, amani imshukie.
Na kwa hakika tumeyasahilisha matamko ya Qur’ani, ili isomwe na ihifadhiwe, na tumeyasahilisha maana yake, ili ifahamike na izingatiwe kwa anayetaka kuwaidhika na kuzingatia. Basi je kuna mwenye kuwaidhika nayo?
Kwa hakika lilimjia Fir'awn na watu wake onyo letu la kuwatesa kwa ukafiri wao.
Walizikanusha dalili zetu zote zenye kutolea ushahidi upweke wetu na unabii wa Manabii wetu, tukawatesa kwa adhabu mateso ya Mshindi Asiyeshindwa, Mweza wa Analolitaka.
Je makafiri wenu, enyi mkusanyiko wa Makureshi, ni bora kuliko wale waliotangulia kutajwa miongoni mwa wale walioangamia kwa sababu ya kukanusha kwao? Au nyinyi mmeepushwa na mateso ya Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo kwenye Vitabu vilivyoteremshwa kwa Mitume kwa kuwa mtasalimika na mateso?
Au kwani wanasema makafiri wa Makkah, «Sisi ndio wenye ushupavu na busara, na jambo letu ni la pamoja. Sisi ni watu wa ushindi, na hatatushinda anayetutaka kwa ubaya.?»
Utashindwa mkusanyiko wa makafiri wa Makkah mbele ya Waislamu na watakimbia. Na hili lilitokea siku ya vita vya Badr.
Na wakati wa Kiyama ambao ndio agizo la wao kulipwa wanachostahiki, na Wakati wa Kiyama ni mkubwa na mgumu zaidi kuliko adhabu iliyowafika siku ya Badr.
Hakika wahalifu wa ukafiri wako katika hali ya kuduwaa kutoijua haki na wako kwenye usumbufu na adhabu.
Siku watakapokokotwa ndani ya Moto kwa nyuso zao na waambiwe, «Onjeni ukali wa adhabu ya moto wa Jahanamu.»
Hakika sisi kila kitu tumekiumba kwa kipimo tulichokikadiri na kukipitisha, na ilitangulia elimu yetu ya kukijua kitu hiko na kukiandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa.
Na haikuwa amri yetu ya kuamuru jambo tukitaka liwe isipokuwa ni kuliambia neno moja nalo ni «kuwa» nalo likawa palepale kama vile kupeleka jicho kuangalia kitu, haichelewi hata kiasi cha jicho kupepesa.
Na kwa hakika tuliwaangamiza wale waliofanana na nyinyi katika ukafiri miongoni mwa ummah waliopita. Basi je, kuna mwenye kuwaidhika kwa mateso na adhabu?
Na kila kitu walichokifanya wale wanaofanana na nyinyi waliopita, cha kheri au cha shari, kimeandikwa kwenye Vitabu ambavyo Malaika watunzi wenye kudhibiti waliviandika.
Na kila dogo au kubwa katika matendo yao limesajiliwa ndani ya madaftari yao, na watalipwa kwayo.
Hakika wachamungu watakuwa kwenye mabustani ya Pepo makubwa na mito mipana Siku ya Kiyama.
Kwenye kikao cha haki, kisochokuwa na maneno ya upuuzi wala ya kuwatia madhambini, mbele ya Mwenyezi Mungu, Aliye Mfalme Mkubwa, Muumba vitu vyote, Mwenye uweza wa kila kitu, Aliyetukuka na kuwa juu.