ﯧ
surah.translation
.
ﰡ
Ashasikia Mwenyezi Mungu neno la Khawalah binti ya Tha’labah anayekurudiarudia kuhusu mumewe Aws mwana wa al-Ṣāmit na kuhusu kile kilichotokea upande wake cha kufanya ẓihār nako ni kule kutamka mumewe kumwambia yeye, «wewe kwangu mimi ni kama mgongo wa mamangu», yaani katika uharamu wa kumuingilia, na huku anamnyenyekea Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amtatulie shida yake, na Mwenyezi Mungu Anayasikia maneno yenu na marudiano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila neno, ni Muoni wa kila kitu, hakifichiki Kwake chochote chenye kufichika.
wale wanaowafananisha wake zao na mama zao, kwa kutoka mwanamume miongoni mwao kumwambia mkewe, «Wewe kwangu ni kama mgongo ya mamangu» yaani kuwa kumuingilia ni haramu, wamemuasi Mwenyezi Mungu na wameenda kinyume na Sheria. Na wake zao si mama zao kihakika, bali wao ni wake zao; mama zao ni wale tu waliowazaa wao. Na hawa wanaowafananisha wake zao na mama zao, kwa hakika, wanasema neno la urongo lililo baya lisilo sahihi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamahe na kusitiri kwa wale ambao yametokea kwao baadhi ya mambo ya uvunjaji Sheria kisha wakayarakebisha kwa kutubia kidhati.
Na wale wanaojiharamishia wake zao kwa kuwafananisha na migongo ya mama zao kisha wakarudi nyuma na hilo neno na wakataka kuwaingilia, basi ni juu ya yule mume aliyetoa tamshi la ẓihār, katika hali hii, atoe kafara ya kule kujiharamishia, nayo ni kuacha shingo huru yenye Imani: mtumwa au kijakazi, kabla hajamuingilia yule mkewe aliyemfananisha na mgongo wa mamake. Hiyo ndiyo hukumu ya Mwenyezi Mungu kwa anayemfananisha mkewe na mgongo wa mamake, mnakumbushwa mwaidhike nayo, enyi Waumini, ili msiingie kwenye kosa la kuwafananisha wake zenu na mama zenu na kusema neno la uzushi, na mtoe kafara mnapoingia kwenye kosa hilo, na ili msirudie tena kufanya hilo. Na Mwenyezi Mungu hakifichamani chochote Kwake Yeye katika matendo yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwayo
Na Asiyepata shingo ya kuiacha huru, basi lililo wajibu kwake ni kufunga miezi miwili iliyofuatana kabla hajamuundama mkewe. Na asiyeweza kufunga miezi miwili kwa udhuru wa kisheria, basi na awalishe masikini sitini chakula kinachowashibisha. Hayo tuliyoyaelezea nyinyi ya hukumu ya kujiharamishia mke wake kwa kumfananisha na mgongo wa mamake ni kwa sababu mmuamini Mwenyezi Mungu na mumfuate Mtume Wake na mfanye matendo yanayoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu na muache yale ambayo mlikuwa mkiyafanya wakati mlipokuwa kwenye ujinga. Hukumu hizo zilizotajwa ndizo amri za Mwenyezi Mungu na mipaka Yake, basi msiikiuke. Na wenye kuzikataa watapata adhabu yenye uchungu.
Hakika ya wale wanaomfanyia uadui na Mwenyezi mungu na Mtume Wake na wakaenda kinyume na amri zao, watadhalilishwa na watatwezwa kama walivyodhalilishwa ummah waliokuwa kabla yao waliopingana na Mwenyezi Mungu na Mitume Wake. Na tumeteremsha aya zenye hoja zilizo wazi zinazoonyesha kuwa Sheria ya Mwenyezi Mungu na mipaka Yake ni kweli. Na wenye kuzikanusha aya hizo watapata adhabu yenye kudhalilisha ndani ya moto wa Jahanamu.
Na kumbuka, ewe Mtume, Siku ya Kiyama, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawahuisha wafu wote na Atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho katika uwanja mmoja, Awape habari ya yale waliyoyafanya ya kheri na shari. Mwenyezi Mungu Ameyadhibiti hayo na Ameyaandika katika Ubao Uliohifadhiwa, na Amewatunzia wao katika kurasa za matendo yao na hali wao wameyasahau. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila jambo, hakuna chochote kinachofichamana Kwake.
Kwani hujui kwamba Mwenyezi Mungu Yuwajua kila kitu kilicho mbinguni na ardhini? Hawanong’oni watu watatu, kati ya viumbe Vyake, maneno ya siri isipokuwa Mwenyezi Mungu ni wanne wao , wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, wala wachache kuliko idadi hiyo iliyotajwa wala wengi kuliko idadi hiyo isipokuwa Yeye Huwa Yuko pamoja nao kwa ujuzi wake, mahali popote waliopo. Hakuna chochote kinachofichamana Kwake kuhusu mambo yao. Kisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, Atawapa habari ya kile walichokifanya chema au kibaya na Atawalipa kwa walichokifanya. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi.
Je, huwaoni, ewe Mtume, Mayahudi waliokatazwa wasizungumze kwa siri maneno yanayowatia shaka Waumini, kisha wanarudi kufanya yale waliyokatazwa, na wanazungumza kwa siri maneno ya dhambi, uadui na kuenda kinyume na amri ya Mtume? Na wanapokujia hawa Mayahudi kwa jambo lolote miongoni mwa mambo, wanakuamkia kwa maamkizi ambayo siyo yale Mwenyezi Mungu Aliyoyafanya ni maamkizi yako, na wanasema, «As-sām ‘alayka» yaani, Mauti yakushukie! Na wanasema wakiambiana wao kwa wao, «Si Atuangamize Mwenyezi Mungu kwa yale tunayomuambia Muhammad, iwapo ni Mtume kikweli.» Moto wa Jahanamu utawatosha: wataungia na watalihisi joto lake, na ubaya wa marejeo ni huo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mnapozungumza baina yenu kwa siri, msizungumze maneno ya dhambi au yenye uadui kwa wengine msiokuwa nyinyi au yanayoenda kinyume na amri ya Mtume. Na zungumzeni yale yenye kheri, utiifu na wema, na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake, Kwani Kwake Yeye Peke Yake ndipo mtakaporudi na matendo yenu yote na maneno yenu Aliyowadhibitia, na Atawalipa kwayo.
Hakika kuzungumza kwa siri maneno ya dhambi na uadui ni katika ushawishi wa Shetani. Yeye ndiye anayeyapamba na kuyahimiza ili atie masikitiko kwenye nyoyo za Waumini. Na hilo halikuwa ni lenye kuwaudhi Waumini kitu chochote isipokuwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na mapendeleo Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu na wajitegemeze wenye kumuamini katika mambo yao yote.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mkitakiwa mpanane nafasi kwenye mabaraza basi peaneni nafasi, na mkifanya hivyo Mwenyezi Mungu Atawakunjulia nafasi duniani na Akhera. Na mkitakiwa kwenu, enyi Waumini, muinuke katika mabaraza yenu kwa jambo lolote lenye kheri kwenu, basi inukeni. Mwenyezi Mungu Anavipandisha vyeo vya Waumini miongoni mwenu, na Anavipandisha vyeo vya wenye elimu daraja nyingi kwa kuwapatia malipo mema na daraja za kupata radhi. Na Mwenyezi Mungu Anayatambua matendo yenu, hakuna chochote kinachofichamana Kwake katika hayo, na Yeye ni mwenye kuwalipa nyinyi kwayo. Katika aya pana kutukuza cheo cha wanavyuoni na utukufu wao na kutukuzwa daraja zao.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Mkitaka kusema na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa siri baina yenu na yeye, basi tangulizeni kabla ya hilo kutoa sadaka kwa wahitaji. Hilo ni bora kwenu, kwa kuwa lina thawabu, na lenye kusafisha zaidi nyoyo zenu na madhambi. Basi mkitopata cha kutoa sadaka hamna makosa juu yenu. Kwani Mwenyezi Mungu, kwa hakika, ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake Waumini, ni Mwenye huruma kwao.
Je, mmeogopa kuwa mtafukarika mkitanguliza sadaka kabla ya kunong’ona na Mtume wa Mwenyezi Mungu? Basi msipofanya hilo mliloamrishwa, na Mwenyezi Mungu Amewasamehe na Amewaruhusu msilifanye hilo, basi simameni imara na muendelee kusimamisha Swala, kutoa Zaka na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika kila lile mliloamrishwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa Matendo yenu na ni Mwenye kuwalipa kwayo.
Je, huwaoni wanafiki waliowafanya Mayahudi ni marafiki na wakawategemea? Na wanafiki kihakika si miongoni mwa Waislamu wala mayahudi, na wanaapa urongo kuwa wao ni Waislamu na kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na hali wanajua kuwa wao ni warongo kwa kile walichokiapia.
Mwenyezi Mungu Amewatayarishia hawa wanafiki adhabu iliyofikia upeo wa ukali na uchungu. Hakika wao ni mabaya sana yale waliokuwa wakiyafanya ya unafiki na uapaji mayamini ya urongo.
Wanafiki wameyafanya yale mayamini yao ya urongo ni kinga yao wasipate kuuawa kwa ukafiri wao na kuwazuia Waislamu wasiwapige vita na kuchukua mali yao. Na kwa ajili hiyo wanajizuia wao na kuwazuia wengine njia ya Mwenyezi Mungu, nayo ni Uislamu. Basi watapata adhabu yenye kudhalilisha Motoni kwa kufanya kiburi kwao kwa kujiepusha na kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kwa kuzuia kwao njia Yake isifuatwe.
Hayatawakinga wanafiki hawa mali yao wala watoto wao kitu chochote na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hao ni watu wa Motoni, watauingia na wasalie humo milele, hawatatoka humo kabisa. Malipo haya yanamkusanya kila anayeiwekea kizuizi Dini ya Mwenyezi Mungu kwa maneno yake au vitendo vyake.
Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atawafufua wanafiki wote kutoka makaburini mwao wakiwa hai, na hapo wamuapie Yeye kuwa wao walikuwa Waumini kama walivyokuwa wakiwaapia nyinyi, enyi Waumini, duniani. Na watadhani kuwa hilo litawanufaisha kwa Mwenyezi Mungu kama lilivyokuwa linawanufaisha ulimwenguni kwa Waislamu. Basi jua na utanabahi kuwa wao ndio waliofikia upeo katika urongo ambao hawakuufikia wasiokuwa wao.
Hao Shetani aliwaghilibu na akawatawala mpaka wakaacha amri za Mwenyezi Mungu na kufanya matendo ya utiifu Kwake. Hao ni kundi la Shetani na wafuasi wake. Jua utanabahi kwamba watu wa kundi la Shetani ndio wenye kupata hasara duniani na Akhera.
Hakika wale wanaoenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hao ni miongoni mwa wadhalilifu walioshindwa na kufanywa wanyonge duniani na Akhera.
Ameandika Mwenyezi Mungu kwenye Ubao Uliohifadhiwa na Amepitisha kuwa ushindi ni Wake Yeye, Kitabu Chake, Mitume Wake na waja Wake Waumini. Hakika mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake, ni Mwenye nguvu, hakuna kitu kinachomuelemea, ni Mwenye ushindi juu ya viumbe Vyake.
Hutakuta, ewe Mtume, watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na wanaofanya matendo waliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, wakiwapenda na kuwategemea wale wanaomsimamishia uadui Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wanaoenda kinyume na amri zao, ingawa ni baba zao au wana wao au ndugu zo au jamaa zao wa karibu. Hao wanaofunga urafiki kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wanaosimamisha uadui kwa ajili Yake ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Ameithibitisha Imani ndani ya nyoyo zao na Akawatia nguvu kwa kuwapa ushindi utokao Kwake na msaada dhidi ya adui yao duniani, na Atawaingiza huko Akhera kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya miti yake inapita mito, hali ya kukaa humo muda mrefu usiomalizika, Amewapa radhi Zake na hatawakasirikia na wao wameridhika na Mola wao kwa yale Aliyowapatia ya utukufu na daraja kubwa. Hao ndio kundi la Mwenyezi Mungu na walioshikana na Yeye, na hao ndio wenye kufaulu kwa kupata furaha ya duniani na Akhera.