ﮤ
surah.translation
.
ﰡ
Hii ni sura kubwa miongoni mwa sura za Qur’ani, tumeiteremsha na tumelazimisha kuzifanyia kazi hukumu zake, na tumeteremsha ndani yake hoja nyingi zilizo waziwazi ili mupate kujikumbusha, enyi Waumini, kwa aya hizi zilizo waziwazi na muzitumie.
Mzinifu mwanamume na mzinifu mwanamke ambao hawajawahi kuoa au kuolewa, adabu ya kila mmoja kati yao ni kupigwa mboko mia moja. Na imethibiti katika Sunnah (mapokezi kutoka kwa Mtume) kwamba pamoja na mboko hizi, ahamishwe kwa kipindi cha mwaka mmoja. Wala kusiwafanye nyinyi kule kuwahurumia kuacha kuwatia adabu hiyo au kuipunguza, iwapo munamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na munazifuata kivitendo hukumu za Kiislamu. Na waihudhurie adabu hiyo kikundi cha Waumini kwa kuwaumbua na iwe ni kitisho, mawaidha na mazingatio.
Mwanamume mzinifu haridhiki isipokuwa kumuoa mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina asiyekubali uharamu wa uhalifu wa uzinifu, na mwanamke mzinifu haridhiki isipokuwa kuolewa na mwanamume mzinifu mwanamume mshirikina asiyekubali uharamu wa uzinifu. Ama wanaume na wanawake wanaojizuia na uzinifu, wao hawaridhiki na hilo, na ndoa hiyo imeharamishwa kwa Waumini. Na huu ni ushahidi wazi wa uharamu wa kumuoa mwanamke mzinifu mpaka atubie, vilevile uharamu wa kumuoza mwanamume mzinifu mpaka atubie.
Na wale wanaowatuhumu watu waliojihifidhi, miongoni mwa wanaume na wanawake, kwa uchafu wa uzinifu pasi na kushuhudia pamoja na wao mashahidi wanne waadilifu, basi wapigeni mboko themanini na msiwakubalie ushahidi mwingine wowote kabisa, na hao ndio waliotoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu.
Lakini mwenye kutubia, akajuta, akarudi nyuma katika tuhuma yake na akatengeneza matendo yake, kwa kweli Mwenyezi Mungu Atamsamehe dhambi zake, Atamuonea huruma na Ataikubali toba yake.
Na wale wanaowatuhumu wake zao kwa uzinifu, na wakawa hawana mashahidi wa kutilia nguvu tuhuma yao isipokuwa wao wenyewe, basi ni juu ya mmoja wao hao wenye kutuhumu, atoe ushahidi mbele ya kadhi mara nne kwa kusema, «Ninashuhudia kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba mimi ni mkweli katika lile la uzinifu ambalo nimemtuhumu mke wangu kwalo.»
Na aongeze kwenye ushahidi wa tano kujiapiza nafsi yake kuwa inastahili kupata laana ya Mwenyezi Mungu iwapo yeye ni mrongo katika maneno yake hayo.
Na kwa ushahidi wake huu, itapasa kwa yule mke aliyetuhumiwa kutiwa adabu ya uzinifu, nayo ni kupigwa mawe mpaka kufa. Na haitamuepukia adabu hii mpaka atoe ushahidi wa kupinga ule ushahidi wa mumewe, mara nne kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba mumewe ni mrongo katika madai yake kuwa yeye amezini.
Na aongeze katika ushahidi wake wa mara ya tano kwa kujiapiza kuwa anapaswa kushukiwa na hasira za Mwenyezimngu iwapo mumewe ni mkweli katika madai yake kuwa yeye amezini. Na katika hali hii watatenganishwa baina ya wao wawili.
Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema Zake kwenu, enyi Waumini, kwa mapitisho haya ya kisheria kwa waume na wake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuitikia toba kwa aliyetubia miongoni mwa waja wake ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake na maongozi Yake, basi yangalimpata mmoja wa wale wawili wanaolaaniana yale aliyojiapiza.
Kwa hakika, wale waliokuja na urongo mbaya kabisa, nao ni kumsingizia Mama wa Waumini 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie, kuwa amefanya kitendo kichafu, ni kikundi cha watu wanaohusiana na nyinyi, enyi kongamano la Waislamu. Msidhanie maneno yao ni shari kwenu, ilivyo ni kuwa maneno yao ni kheri kwenu, kwa kuwa yalitokamana na maneno hayo kutakaswa Mama wa Waumini na uchafu, kusafika kwake na kuukuza utajo wake, kuzipandisha daraja, kuyafuta maovu na kuwasafisha Waumini. Kila mmoja aliyouzungumza urongo huo atapata malipo ya kitendo chake cha dhambi. Na yule aliyebeba jukumu kubwa zaidi katika uzushi huo, naye ni 'Abdullāh bin Ubayy bin Salūl, kiongozi wa wanafiki, Mwenyezi Mungu Amlaani, atakuwa na adhabu kubwa huko Akhera, nayo ni kukaa milele wakati waliposikia uzushi huo, nayo nikumuepushia kile ambacho hao (wazushi) walimsngizia nacho na kusema, «Huu ni urongo waziwazi juu ya 'Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimshukuie.
Si ingalikuwa bora kwa Waumini wanaume na wanawake wadhaniane kheri wao kwa wao pindi walikposikia uzushi huo, kuwa yale waliyosingiziwa hawanayo, na waseme, «Huu ni urongo ulio wazi» juu ya ‘Aishah, radhi za Mwenyezi Mungu zimfikie.
Si ingalikuwa walete mashahidi waadilifu wanne kuthibitisha maneno yao waliyoyasema. Na kwa kuwa hawakulifanya hilo, basi wao ni warongo mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu kwenu na rehema Zake, kwa kuwa wema Wake umewakusanya nyinyi katika Dini yenu na Akhera yenu, Asifanye haraka kuwaadhibu na aikubali toba ya mwenye kutubia miongoni mwenu, basi inagaliwapata adhabu kali kwa sababu ya maneno ya uvumi mliyojihusisha nayo.
Kipindi mlichokuwa mnaupokea uzushi na mnaueneza kwa midomo yenu, nao ni yale maneno ya urongo na ambayo hamuna ujuzi nao. Na mambo mawili haya yameharamishwa: kusema maneno ya urongo na kusema bila ya ujuzi. Na mnadhani kuwa hilo ni jambo dogo, nalo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika haya pana makemeo bayana juu ya kupuuza makatazo ya uenezaji ubatilifu.
Mbona hamukusema mlipousikia uzushi huo, «Haifai kwetu kuusema urongo huu. Kutakasika ni kwako, ewe Mola, kuyasema hayo juu ya mke wa Mtume wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Huu ni urongo uliobeba mzigo mkubwa wa madhambi.»
Mwenyezi Mungu Anawakumbusha na Anawakataza msirudie kitendo hiki cha kusingizia urongo, iwapo nyinyi ni wenye kumuamini Yeye.
Na Anawafafanulia nyinyi aya zinazokusanya hukumu za kisheria na mawaidha. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana matendo yenu, ni Mwenye hekima katika sheria Zake na uendeshaji Wake.
Kwa hakika,wale wanaopenda kuenea machafu kwa Waislamu, ya tuhuma za uzinifu au jambo lolote baya, watapata adhabu kali ulimwenguni, kwa kupigwa mboko, na mengineyo miongoni mwa mitihani ya kilimwengu, na watapata adhabu ya Motoni huko Akhera wakiwa hawakutubia. Na Mwenyezi Mungu, peke Yake, Ndiye Anayejua urongo wao na Ndiye Anayeyajua maslahi ya waja wake na mwisho wa mambo , na nyinyi hamyajui hayo.
Na lau kama si wema wa Mwenyezi Mungu juu ya wale waliohusika kwenye tukio la uzushi na rehema zake kwao na kwamba Mwenyezi Mungu Anawahurumia waja Wake Waumini huruma kunjufu katika yale wanaokuwa na pupu nayo (ya ulimwengu) na yale wanayoyasubiri (ya Akhera), hangalizifunua wazi hukumu hizi na mawaidha na Angalifanya haraka kumuadhibu yule aendaye kinyume na amri Yake.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitekeleza sheria Zake, msiziandame njia za Shetani. Na yoyote anayefuata njia za Shetani, basi (huyo Shetani) anamuamrisha vitendo viovu na vichafu. Na lau si wema wa Mwenyezi Mungu kwa Waumini na rehema zake kwao, hanagalitakasika yoyote katika wao kabisa na uchafu wa madhambi yake. Lakini Mwenyezi Mungu, kwa wema wake, Anamtakasa Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu , ni Mjuzi wa nia zenu na matendo yenu.
Wala wasiape watu wema katika Dini na wakunjufu wa mali kuacha kuwaunga watu wao wa karibu wasiokuwa na kitu na wahitaji na wageni waliogura makwao na kuwanyima matumizi kwa sababu kuna kosa walilifanya. Basi na wayasamehe maovu yao wala wasiwatese. Kwani nyinyi hamupendi Mwenyezi Mungu Awasamehe? Basi wasameheni. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao. Katika haya pana mahimizo juu ya kusamehe na kusahau kabisa, hata kama mtu atatendewa uovu.
Kwa kweli wale wanaowasingizia kitendo cha uzinifu wanawake wenye kujihifadhi, wasiofikiria machafu na walio Waumini ambao halijawapitia jambo hilo kwenye nyoyo zao, hao ni wenye kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu , duniani na Akhera, na watapata adhabu kubwa kwenye moto wa Jahanamu. Kwenye aya hii kuna ushahidi juu ya ukafiri wa mwenye kumtukana au kumtuhumu mke yoyote kati ya wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa jambo ovu lolote.
Hiyo ndiyo adhabu ya Siku ya Kiyama, siku ambayo ndimi zao zitatoa ushahidi kinyume na wao kwa yale ambayo hizo ndimi zimeyatamka, na itazungumza mikono yao na miguu yao kuhusu yale ambayo hiyo mikono na miguu iliyatenda.
Katika siku hiyo, Mwenyezi Mungu Atawalipa malipo yao kamili juu ya matendo yao kwa usawa, na watajua kwenye mkusanyiko huo mkubwa wa kisimamo kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Ukweli ulio wazi, Ambaye Yeye ni kweli, ahadi yake ni ya kweli, makemeo yake ni kweli na kila kitu kitokanao na yeye ni kweli, Ambaye hamdhulumu yoyote chochote hata kama ni kadiri ya uzani wa chungu mdogo.
Kila kiovu miongoni mwa wanaume na wanawake, maneno na vitendo, kinalingana na kiovu na kinaoana nacho. Na kila kizuri miongoni mwa wanaume na wanawake, maneno na vitendo, kinalingana na kizuri na kinaoana nacho. Na wanaume wazuri na wanawake wazuri ni wenye kutakaswa na uovu wanaowasingizia nao wale waovu. Watapata kutoka kwa Mwenyezi Mungu msamaha utakaoyafinika madhambi yote na riziki njema Peponi.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitumia sheria Zake, msiingie kwenye nyumba zisizokuwa zenu, mpaka muwatake ruhusa wenyewe ya kuingia na muwaamkie. Na matamshi ya maamkizi hayo yatokayo kwenye Sunnah ni, «Assalāmu ‘alaikum. Je, niingie?» Kutaka ruhusa huko ni bora kwenu nyinyi. Huenda mkazikumbuka, kwa kufanya kwenu hivyo, amri za Mwenyezi Mungu na mkapata kumtii.
Na iwapo hamtampata mtu kwenye nyumba za watu wengine, basi msizingie mpaka aweko mwenye kuwaruhusu. Asiporuhusu na akasema, «rudini,» basi rudini, wala msisisitize kutaka kuruhusiwa, kwani kurudi wakati huo ni jambo zuri zaidi kwenu, kwani mwanadamu ana nyakati na hali ambazo hapendi kwenye hali hizo kuonekana na mtu mwingine. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyatenda ni Mjuzi na Atamlipa kila mtendaji kitendo chake.
Lakini hapana ubaya kwenu kuiingia , bila ya kubisha hodi, nyumba ambazo hazikuwekwa kuwa ni makazi ya watu maalumu wajulikanao isipokuwa ziwe ni maliwazo kwa wenye kuzihitajia, kama nyumba zilizowekwa kuwa ni sadaka kwa mpita njia kwenye njia ya wasafiri na zisokuwa hizo katika huduma. Basi ndani ya nyumba hizo muna manufaa na mahitaji ya wenye kuyaingia, kwani kubisha kwenye hali hiyo ni usumbufu. Na Mwenyezi Mungu Anazijua hali zenu zilizo waziwazi na za zilizofichika.
Sema, ewe Nabii, uwaambie Waumini wanaume wayainamishe macho yao kutoangalia vitu visivyohalali kwao miongoni mwa wanawake na tupu, na wazilinde tupu zao na vile Alivyovifanya haramu Mwenyezi Mungu miongoni mwa uzinifu, ulawiti, kufunua tupu na mfano wa hayo. Kufanya hivyo ni usafi zaidi kwao. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa wanayoyafanya katika yale Anayowaamrisha na kuwakataza.
Na useme kuwaambia Waumini wanawake wayainamishe macho yao kutoyaangalia yasiokuwa halali kwao miongoni mwa tupu, na wazilinde tupu zao na yale Aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, wala wasionyeshe waziwazi pambo lao kwa wanaume, bali wajipinde kulificha pambo lao isipokuwa nguo za juu ambazo imezoeleka kuzivaa, iwapo hakuna kwenye nguo hizo kivutio cha kupelekea kufitinika nao, na waviangushe vifiniko vya vichwa vyao kwenye uwazi wa sehemu za juu za nguo zao kwenye sehemu za vifua vyao huku wamezifinika nyuso zao ili sitara yao itimie. Na wasiuonyeshe urembo uliofichika isipokuwa kwa waume zao, kwani wao wanaona kutoka kwao wasiyoyaona wengine. Na sehemu ya urembo huo, kama uso, shingo, mikono miwili na sehemu za begani za mikono, zinafaa kuonekana na baba zao au baba za waume zao au watoto wao au watoto wa waume zao au ndugu zao au watoto wa ndugu zao wa kiume, au watoto wa dada zao au wanawake wenzao, walio Waislamu na sio makafiri, au watumwa waliowatawala au wafuasi kati wanaume ambao hawana malengo wala haja ya wanawake, kama vile mapite wanaowafuata watu kwa sababu ya kula au kunywa tu, au watoto wadogo ambao hawana ujuzi wowote wa mambo yanayohusiana na tupu za wanawake na ambao bado hawana matamanio. Na wasipige miguu yao, hao wanawake, wanapotembea ili kuwasikilizisha watu mapambo yao yaliyofichika, kama vikuku(vinavovawa miguuni kama pambo) na mfano wake. Na rudini, enyi Waumini, kwenye kumtii Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha kwayo kati ya sifa hizi nzuri na tabia njema, na yaacheni yale ambayo walikuwa nayo watu wa zama za ujinga ya tabia na sifa mbovu kwa matarajio mufaulu kuzipata kheri mbili: ya ulimwenguni na ya Akhera.
Na waozeni, enyi Waumini, wanaume wasiokuwa na wake na wanawake wasiokuwa na waume, miongoni mwa waungwana na walio wema kati ya watumwa wenu na wajakazi wenu. Iwapo anayetaka kuoa kwa kujihifadhi ni masikini mwenye uhitaji, Mwenyezi Mungu Atamtosheleza kutokana na ukunjufu wa riziki Yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu, ni Mwingi wa kheri, ni Mkuu wa fadhila na ni Mjuzi mno wa nyenendo za waja Wake.
Na wale wasiokuwa na uwezo wa kuoa kwa ufukara wao au kwa jambo lingine, basi na wajizoeze uvumilivu wa kutoyafanya Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu, mpaka Mwenyezi Mungu Awatosheleze kwa wema Wake na Awasahilishie kuoa. Na wale wanaotaka kujikomboa na utumwa na ujakazi kwa kufanya mkataba na mabwana zao kwa kutoa kiasi maalumu cha pesa wawapatie, basi ni juu ya hao wamiliki wao waandikiane mapatano na wao kwa hilo, iwapo watajua kuwa kuna wema ndani yao ya uongofu, uwezo wa kujitafutia pesa na wema wa Dini. Na ni juu yao, hao wamiliki, wawape pesa, hao watumwa wao, au wawasamehe sehemu ya pesa walioandikiana. Na haifai kwenu kuwalazimisha wajakazi wenu kufanya uzinifu kwa lengo la kutaka kupata pesa. Na vipi litapatikana kwenu hilo na huku wao wenyewe wanataka kujilinda na uchafu huo, na nyinyi mnawakatalia hilo? Katika haya, pana kuonesha ubaya wa kitendo kiovu walichokifanya. Na yoyote mwenye kuwalazimisha wao kufanya uzinifu, basi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, baada ya kuwalazimisha wao, ni mwenye kuwasamehe (hao waliolazimishwa) na kuwaonea huruma, na dhambi ni kwa yule Aliyewalazimisha.
Na kwa hakika tumewateremshia, enyi watu, aya za Qur’ani zikiwa ni dalili wazwazi za kuonesha haki, na ni mfano wa matukio ya ummah uliopita wa Waumini kati yao na makafiri na yaliyowapitia ya kuwafaa na kuwadhuru ambayo ni mfano na mazingatio kwenu na ni mawaidha ya kuwaidhika mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na kujihadhari na adhabu Yake.
Mwenyezi Mungu ni Nuru ya mbinguni na ardhini, Anaendesha mambo humo na Anawaongoza watu wake. Kwa hivyo, Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Nuru, na pazia Yake ni Nuru. Kwayo zimeng’ara mbingu na ardhi na vilivyomo ndani. Na kitabu cha Mwenyezi Mungu na uongofu wake ni nuru kutoka Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Na lau si nuru Yake yeye Aliyetukuka, lingalishikamana giza na kupandana, hili juu ya lingine. Mfano wa nuru Yake ambayo inaongoza kupeleka Kwake, nayo ni Imani na Qura’ni ndani ya moyo wa mwenye kuamini, ni kama kishubaki, nacho ni kidirisha ukutani kisichoonyesha upande wa pili, kwenye kidirisha kuna taa, ambapo hapo kidirisha kinakusanya nuru ya ile taa, zote zikawa mwangaza wake ni mmoja. Na taa hiyo iko kwenye kiyoo, kama kawamba kiyoo hiko kwa usafi wake ni nyota ing’arao kama duri. Taa hiyo inawashwa kwa mafuta ya mti uliobarikiwa, nao ni mzaituni, si wa upande wa mashariki tu usiopatwa na jua mwisho wa mchana, wala si wa magharibi tu usiopatwa na jua mwanzo wa mchana, isipokuwa uko katikati kwenye sehemu ya ardhi, haukuelekea Mashariki wala Magharibi. Yanakaribia mafuta yake kwa usafi wake kuwaka yenyewe bila ya kuguswa na moto, na pindi yakiguswa na moto hung’ara mn’garo mkali mno, nuru juu ya nuru. Hiyo ni nuru kutokana na mwangaza utokao kwenye mafuta, ulioko juu ya nuru itokanayo na kuwasha moto. Basi huo ndio mfano wa uongofu, huwa unang’ara ndani ya moyo wa mwenye Imani. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza na kumuelekeza kuifuata Qur’ani Amtakaye, na Anawapigia watu mifano ili wapate kuifahamu mifano yake na hekima zake. Na Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi mno na hakuna chochote kinachofichamana Kwake.
Nuru hii inayong’ara kwenye misikiti ambayo Mwenyezi Mungu Ameamrisha itukuzwe, ijengwe na jina Lake litajwe humo kwa kusoma Kitabu Chake na kuleta tasbihi (subhān Allāh) na kuleta tahlili (Allāh Akbar) na yasiyokuwa hayo katika aina mbalimbali za kumtaja. Wanaswali kwenye misikiti hiyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.
Wanaume ambao hawapumbazwi na ununuzi wala uuzaji na jambo la kumtaja Mwenyezi Mungu, kusimamisha Swala na kutoa Zaka kwa anayestahiki kupewa; wanaiogopa Siku ya Kiyama ambayo nyoyo zinageukageuka baina ya matumaini ya kuokoka na kicho cha kuangamia, na macho yatakuwa yanageukageuka yanatazama ni mwisho gani yataishia?
Ili Mwenyezi Mungu Awape malipo mema ya matendo yao mazuri zaidi na Awaongezee kutokana na wema Wake. Na Mwenyezi Mungu Anamruzuku Anayemtaka bila kumhesabia, bali Anampa malipo ambayo matendo yake mema hayakuyafikia, na pasi na hesabu wala kipimo.
Na wale waliomkanusha Mola wao na wakawafanya warongo Mitume Wake, matendo yao waliyoyategemea kuwa yatawafaa huko Akhera, kama kuunga kizazi, kuwaacha huru mateka na yasiyokuwa hayo, yatakuwa ni kama mangati, nayo ni yale yanayoonekana kama maji juu ya ardhi tambarare kipindi cha mchana cha jua kali, mwenye kiu akiyaona anadhani ni maji, na akiyajia hakuti kuwa ni maji. Basi kafiri anadhani kwamba matendo yake yatamfaa, na ifikapo Siku ya Kiyama atakuta kuwa hayana malipo mema, na hapo atamkuta Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anamngojea Ampe malipo ya matendo yake kikamilifu. Na Mwenyezi Mungu ni Mpesi wa kuhesabu. Basi wajinga wasione kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu imekawia kuwa, kwani hiyo hapana budi kuja kwake.
Au matendo yao yawe mfano wa giza ndani ya bahari yenye kina, juu yake kuna mawimbi, na juu ya mawimbi kuna mawimbi mengine, na juu ya mawimbi hayo kuna mawingu mazito. Hilo ni giza kubwa sana, giza juu ya giza, pindi atowapo mkono wake mtazamaji, kamwe hakaribii kuuona kwa ukubwa wa giza. Limerundikana kwa makafiri giza la ushirikina, upotevu na uharibifu wa matendo. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu Hakumpatia nuru itokamanayo na Kitabu Chake na mwendo wa Mtume Wake, basi huyo hana wa kumuongoza.
Kwani hukujua, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa Yeye viumbe vilivyoko mbinguni na ardhini. Na ndege wamezikunjua mbawa zao huko juu angani wanamtakasa Mola wao? Kila kiumbe, Mwenyezi Mungu Amemfundisha namna ya kumswalia na ya kumtakasa. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Anayaona anayoyafanya kila mwenye kuabudu na kutakasa, hakuna chochote kinachofichika Kwake Yeye kuhusu hayo, na Atawalipa kwa hayo.
Ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ufalme wa mbinguni na ardhini. Ndiye Mwenye utawala wa hizo zote. Na Kwake Yeye ndio marejeo Siku ya Kiyama.
Kwani hukuona kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Anayapeleka mawingu pale Anapopataka, kisha Anayakusanya baada ya kuwa mbalimbali, kisha anayafanya yapandane na yarundikane, kisha Anaiteremshe mvua kutoka kwenye mrundiko huo? Na Anateremsha, kutoka kwenye mawingu yanayofanana na milima ya mawe kwa ukubwa wake, mvua ya barafu, Akaipeleka kwa amtakaye kati ya waja Wake na Akaiyondosha kwa Amtakaye kati yao kuambatana na hekima Yake na mpango Wake. Unakaribia mwangaza wa umeme huo umemetekao huko mawinguni, kwa ukali wake, kuyapofua macho ya wenye kuutazama.
Na miongoni mwa ushahidi wa kutolea dalili uweza wa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kwamba Yeye Anaugeuza usiku na mchana kwa kuja mmoja wapo baada ya mwingine na kutafautiana kwao kwa urefu na ufupi. Katika hilo pana ushahidi kwa mtu mwenye busara na kuizingatia.
Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amekiumba kila kitambaacho ardhini kutokana na maji, kwani maji ndio asili ya kuumbwa kwake. Na miongoni mwa vitambaavyo kuna anayetembea kwa matumbo yake kama vile nyoka na mfano wake, na katika hao kuna anayetembea kwa miguu miwli kama binadamu, na miongoni mwao kuna anayetembea kwa miguu minne kama wanyama na mfano wake. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Anaumba anachotaka, na Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Na kwa hakika tumeteremsha katika Qur’ani vitambulisho vilivyo waziwazi venye kuongoza kwenye haki. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza na kumuelekeza Anayemtaka katika waja wake kwenye njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu.
Na wanafiki wanasema, «Tumemuamuni Mwenyezi Mungu na yale ambayo amekuja nayo Mtume na tumezitii amri zao.» Kisha vinatoka vikundi kati yao, baada ya hapo, vikayapa mgongo hayo, visiukubali uamuzi wa Mtume. Basi hao hawakuwa ni Waumini.
Na wanapoitwa, wanapokuwa kwenye ugomvi baina yao, kwenye hukumu iliyo ndani ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu na waje kwa Mtume ili afanye uamuzi kati yao, ghafula hujitokeza kikundi kati yao kikajiepusha na kikawa hakikubali hukumu ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, pamoja na kuwa hiyo ndiyo haki isiyo na shaka.
Na iwapo haki iko upande wao, basi wao wanakuja kwa Nabii, rehema na amani zimshukie, wakiwa watiifu na kuwa tayari kuiandama hukumu yake, kwa kutambua kwao kwamba yeye atatoa uamuzi wa haki.
Je, sababu ya kupa mgongo kwao ni ule ugonjwa wa unafiki ulio ndani ya nyoyo zao au wanaushuku unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie? Au sababu ni kuchelea kwao isije ikawa hukumu ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni ya maonevu? Ukweli ni kwamba wao hawaogopei maonevu, isipokuwa kiini hasa ni kwamba wao wenyewe ndio madhalimu walio waovu.
Ama Waumini wa kweli, msimamo wao ni kwamba wanapoitwa kwenda kuhukumiwa, katika ugomvi ulio kati yao, na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na hukumu ya Mtume Wake, wanakubali uamuzi unaotolewa na wanasem, «Tumesikia tulioambiwa na tumemtii aliyetuita kwenye hilo.» Na hao ndio waliofaulu wenye kufuzu kupata matakwa yao kwenye mabustani ya Pepo yenye neema.
Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika kufuata maamrisho na kujiepusha na makatazo na akaogopa mwisho mbaya wa uasi na akajihadhari na adhabu ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio wenye kufuzu kupata neema Peponi..
Na wanafiki waliapa kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kwa upeo wa juhudi yao, viapo vizito, «Ukituamrisha, ewe Mtume, kutoka kwenda kwenye jihadi pamoja na wewe, tutatoka tena tutatoka» Sema uwaambie, «Msiape viapo vya urongo, kwani utiifu wenu unajulikana kuwa ni wa ulimini tu. Kwa kweli Mwenyezi Mungu Anayatambua mnayoyafanya, na Atawapa malipo yake.
Na useme, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume.» Na wakipa mgongo, basi jukumu la Mtume ni kufanya aliyoamrishwa ya kuufikisha ujumbe, na ni jukumu la watu wote kuyafanya waliyoamrishwa ya kufuata. Na mkimtii yeye mtaongoka. Na jukumu la Mtume ni kuufikisha ujumbe wa Mola wake mafikisho yaliyo wazi.
Mwenyezi Mungu Amewaahidi walioamini miongoni mwenu na wakafanya matendo mema kwamba atawarithisha ardhi ya washirikina na atawafanya ni wasimamizi wa hiyo ardhi, kama alivyofanya kwa waliokuja kabla yao kati ya wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, na Aifanye Dini yao ambayo Ameridhika nayo na Akawachagulia, nayo ni Uislamu, ni Dini yenye ushindi na uthabiti, na Azigeuze hali zao kwa kuwaondolea kicho na kuwaletea amani, iwapo watamuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na watasimama imara kwa kumtii, na wasimshirikishe na kitu chochote. Na Mwenye kukanusha baada ya hilo la kupewa usimamizi, amani, uthabiti na utawala kamili, na akakanusha neema za Mwenyezi Mungu, basi hao ndio waliotoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu.
Na isimamisheni Swala kwa kuitimiza, na toeni Zaka kuwapa wanaostahiki kupewa na mumtii Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kutarajia Mwenyezi Mungu Awarehemu.
Msidhani tena msidhani kwamba wale waliokufuru wanamshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi, kwani Yeye ni Muweza wa kuwaangamiza, na marejeo yao, huko Akhera ni Motoni. Na ni mabaya sana marejeo haya na mwisho huu. Maneno haya ni maelekezo kwa ummah wote, ingawa anayeambiwa hapa ni Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifanyia kazi sheria Zake! Waamrisheni watumwa wenu, wajakazi wenu na watoto waungwana mabao umri wao haujafikia wa kubaleghe waombe ruhusa wakitaka kuingia kwenu katika nyakati za mapumziko yenu na kuvua nguo zenu: kabla ya Swala ya Alfajiri, kwa kuwa huo ni wakati wa kuvua nguo za kulalia na kuvaa nguo za baada ya kuamka, na wakati wa kuvua nguo kwa mapumziko ya kipindi cha mchana wakati wa jua kali, na baada ya Swala ya Isha, kwa kuwa huo ni wakati wa kulala. Nyakati tatu hizi ni za kujifunua na kujiacha wazi na kunapungua kujisitiri. Lakini katika nyakati sizokuwa hizo, si makosa wakiingia bila ya idhini, kwa kuwa wao wanahitaji kuingia kwenu, wao ni wa kuingia na kutoka mara kwa mara kwa kutumika, na kwa kuwa dasturi iliyozoeleka ni kuwa nyinyi mnatembeleana nyakati hizi kwa kutimiza haja zenu zenye maslahi kwenu. Na kama Alivyowafafanulia Mwenyezi Mungu hukumu za kutaka ruhusa (ya kuingia majumbani), Anawafafanulia aya Zake, hukumu Zake, hoja Zake na Sheria za Dini Yake. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana yanayowafaa viumbe Wake, ni Mwingi wa hekima katika upelekeshaji Wake mambo yao.
Na pindi watoto wanapofikia miaka ya kubaleghe na kukalifishwa hukumu za kisheria, ni juu yao watake ruhusa wakitaka kuingia nyakati zote kama wanavyotaka ruhusa watu wazima. Na kama Mwenyezi Mungu Anavyowafafanulia adabu za kutaka ruhusa (kuingia majumbani), vilevile Anawafafanulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, aya Zake. Na Mwenyezi Mungu Anayajua sana yanayowafaa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake.
Na wanawake wakongwe ambao wamejikalia hawajistareheshi na hawana matamanio kwa sababu ya uzee wao, hawana hamu ya kuolewa na wanaume wala wanaume hawana hamu nao. Wanawake hawa hawana makosa kujitanda sehemu ya nguo zao kama vile shuka, bila kuonesha pambo wala kujirembesha. Na kuvaa kwao nguo hizi, kwa kujisitiri na kujihifadhi, ni uzuri kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno yenu, ni Mjuzi wa nia zenu na matendo yenu.
Hawana dhambi watu wenye nyudhuru miongoni mwa vipofu, viguru na wagonjwa, kuyaacha mambo ya lazima ambayo hawawezi kuyatekeleza, kama kupigana jihadi na mfano Wake katika vitu ambavyo vinahitajia kwa kipofu awe huona na kiguru awe mzima na mgonjwa awe na afya nzuri. Na nyinyi, enyi Waumini, hamuna makosa kula kwenye majumba ambayo ndani yake kuna wake zenu na watoto wenu, na hapa yanaingia majumba ya watoto, au majumba ya baba zenu au mama zenu au ndugu zenu wa kiume au dada zenu au ami zenu au mashangazi zenu au wajomba zenu au mama zenu wadogo au kwenye nyumba ambazo mliwakilishwa kuzisimamia wakati wenyewe hawapo kwa ruhusa yao au kwenye nyumba za marafiki. Hakuna makosa yoyote kwenu kula mkiwa pamoja au mbalimbali. Na muingiapo kwenye nyumba zinazokaliwa au zisizokaliwa, amkianeni nyinyi kwa nyinyi kwa maamkizi ya Kiislamu, nayo ni «As-salāmu ‘alaikum wa rahmatullāhi wa barakātuh, au As-salāmu ‘alainā wa ‘alā ‘ibādillāhi-s-sālihīn, iwapo hakuna yoyote. Maamkizi haya Mwenyezi Mungu Ameyaweka, nayo yana baraka, yanakuza kusafiana nia na kupendana, ni mazuri yanayopendeza kwa mwenye kuyasikia. Na kwa mfano wa ufafanuzi huu anawafafanulia Mwenyezi Mungu alama za Dini Yake na aya Zake, ili mzifahamu na mzitumie.
Kwa hakika Waumini kikwelikweli ni wale ambao Wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazitumia sheria Zake, na wakiwa wapo pamoja na Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika jambo ambalo amewakusanya kwalo la maslahi ya Waislamu, hawaondoki mpaka wamuombe ruhusa. Kwa hakika wale wanaokuomba ruhusa, ewe Nabii, ndio wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kikweli. Basi wakikuomba ruhusa kwa baadhi ya haja zao, mruhusu unayemtaka miongoni mwa wale waliokuomba ruhusa kuondoka kwa udhuru, na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake wenye kutubia, ni mwingi wa huruma kwao.
Msiseme, enyi Waumini, mnapomuita Mtume wa Mwenyezi Mungu, «Ewe Muhammad!» wala «Ewe Muhammad bin Abdillah!» kama wanavyosema hivyo baadhi yenu kuwaambia wengine. Lakini mtukuzeni na mseme, «Ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu! Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!» Kwa kweli Mwenyezi Mungu Anawajua wale wanaoondoka kutuka kwenye kikao cha Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa siri, bila ya ruhusa yake, wakisaidiana kujificha. Basi na wajihadhari wanaoenda kinyume na amri Yake wasije wakashukiwa na janga na shari au adhabu yenye uchungu iumizayo.
Jueni mtanbahi kwamba ni vya Mwenyezi Mungu vilivyoko mbinguni na ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki, kuvifanya vimdhalilikie. Ujuzi Wake umevizunguka vyote ambavyo muko navyo. Na Siku ya Akhera, ambayo waja watarejea Kwake, Atawapa habari ya matendo yao, na Atawalipa kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, hayafichamani Kwake Yeye matendo yao na hali zao.