ﯘ
surah.translation
.
ﰡ
ﮀ
ﰀ
“Hā, Mīm” maelezo yametangulia mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa.
ﮂﮃ
ﰁ
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ameapa kwa Qur’ani ambayo matamshi yake na maana yake yako waziwazi.
Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa lugha ya Kiarabu , huenda nyinyi mkaelewa na mkazingatia maana yake na hoja zake.
Nayo , kwa hakika, katika Ubao Uliohifadhiwa kwetu sisi ina cheo na heshima za juu, iko thabiti, haina tafauti ndani yake wala kugongana.
Je tuwape nyinyi mgongo na tuache kuwateremshia Qur’ani kwa ajili ya kupuuza kwenu, kutofuata na kupita mipaka kwenu katika kukataa kuiamini?
Tumewatumiliza Manabii wengi katika kame za mwanzo zilizopita kabla ya watu wako, ewe Nabii.
Hawajiwi na Nabii yoyote isipokuwa huwa wakimcheza shere kama vile watu wako walivyokucheza shere, basi tukawaangamiza wale waliowakanusha Mitume wetu, nao walikuwa ni wenye nguvu kali na ushujaa wa kivita kuliko watu wako, ewe Mtume.
Na yashapita mateso ya wa mwanzo kwa kuangamizwa kwa sababu ya ukanushaji wao, ujeuri wao na kuwacheza shere Mitume wao. Katika haya pana maliwazo kwa Nabii, rehema na amani zimshukie.
Na unapowauliza, ewe Mtume, hawa washirikina miongoni mwa watu wako, «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi? Wanasema , «Aliyeziumba ni Yule Aliye Mshindi katika mamlaka Yake, Aliye Mjuzi wa hizo na vitu vilivyomo ndani yake, hakuna chochote kinachofichamana Kwake.
Aliyewafanyia ardhi kuwa ni (kama) tandiko na mkeka, Akawasahilishia humo njia za maisha yenu na biashara zenu, ili mjiongoze kwa njia hizo kwenye maslahi yenu ya kidini na ya kidunia.
Na Aliyeteremsha kutoka mawinguni mvua kwa kipimo, Asiifanye mafuriko yenye kuzamisha wala pungufu isiyotosheleza haja, ipate kuendesha maisha yenu na yale ya wanyama wenu, tukahuisha kwa maji hayo sehemu kubwa ya ardhi kavu isiyokuwa na mimea. Na kama tulivyotoa kwa maji hayo tuliyoyateremsha kutoka juu, kwenye ardhi hiyo iliyokufa, mimea na mazao, hivo ndivyo mtakavyotolewa, enyi watu, makaburini mwenu baada ya kutoweka kwenu.
Na Aliyeumba aina zote za wanyama na mimea, na Akawawekea majahazi mnayoyapanda baharini, na Akawaumbia wale mnaowapanda barani miongoni mwa wanyama, kama vile ngamia, farasi, nyumbu na punda.
Mpate kujituliza juu ya migongo ya hivyo mnavyovipanda, kisha mkumbuke neema ya Mola wenu kwenu hapo mnapopanda na mseme, «Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetudhalilishia (kipando) hiki, na hatukuwa ni wenye uwezo juu yake.»
Na ili mseme pia, «Na sisi baada ya kufa kwetu ni wenye kuelekea Kwake na kurejea. Hapa pana dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwaneemesha waja Wake kwa neema mbalimbali, Ndiye Mwenye kustahiki kuabudiwa kwa kila hali.
Na hawa washirikina wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa na fungu miongoni mwa waja Wake. Nako ni kule kusema kwao kuhusu Malaika kuwa ni watoto wa kike wa mwenyezi Mungu. Kwa hakika, binadamu ni mwingi wa kukanusha neema za Mola Wake Alizowaneemesha kwazo, ni mwenye kudhihirisha kukataa kwake na kukanusha kwake, anahesabu misiba na anasahau neema.
Je, kwani nyinyi mnadai, enyi wajinga, kuwa Mola wenu Amejichagulia, katika vile Anavyoviumba, watoto wa kike, na hali nyinyi hamliridhii hilo kwenu, na Akawahusu nyinyi kwa kuwapatia watoto wa kiume? Haya ni makaripio kwao.
Na anapopewa bishara mmoja wao ya mtoto wa kike ambaye amemnasibishia Mwingi wa rehema, alipodai kwamba Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu, uso wake unageuka ukawa mweusi kwa bishara mbaya aliyopewa ya mtoto wa kike, na huwa na huzuni na kujawa na hamu na unguliko.(Basi vipi wataridhika kwa Mwenyezi Mungu kitu ambacho wao wenyewe hawaridhiki nacho? Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na Ametakasika na kile wanachosema hao makafiri.)
Je, mnajasiri na kumnasibishia Mwenyezi Mungu mtu anayelelewa katika pambo asiyeweza kutasua hoja kwenye mjadala kwa sababu ya kukulia kwake kwenye pambo na starehe?
Na hawa washirikina waliwafanya Malaika ambao ni waja wa Mwenyezi Mungu kuwa ni wanawake. Je, wao walihudhuria wakati Mwenyezi Mungu Alipowaumba mpaka waamue kuwa wao ni wanawake? Ushahidi wao utasajiliwa, na wataulizwa kuhusu hilo kesho Akhera.
Na hawa washirikina wa Kikureshi wanasema, «Lau Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Angalitaka, hatungalimuabudu yoyote asiyekuwa Yeye.” Na hii ni hoja iliyotanguka, kwani Mwenyezi Mungu Ashasimamisha hoja juu ya waja kwa kuwatumiliza Mitume na kuteremsha Vitabu, basi kujisimamishia hoja ya Mapitisho na Makadirio ni ubatilifu mkubwa zaidi baada ya Mitume kuwaonya. Wao hawana ujuzi wa hakika ya yale wanayoyasema. Hakika ni kwamba wao wanayasema kwa kudhania na kuzua urongo, kwa kuwa hawana habari wala dalili kuhusu hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Je, walishuhudia uumbaji wa Malaika au tuliwapatia kitabu kabla ya hii Qur’ani tuliyoiteremsha, wakawa wameshikamana nacho, wakifanyia kazi na wanajijengea kwa hicho hoja za kukupinga, ewe Mtume?
Bali walisema, «Sisi tuliwakuta baba zetu kwenye njia, madhehebu na dini, na sisi tunafuata na kuandama nyayo za baba zetu katika yale waliyokuwa nayo.”
Hivyo ndivyo ilivyo, hatukutumiliza kabla yako wewe, ewe Mtume, muonyaji yoyote kwenye kijiji chochote, mwenye kuwaonya adhabu yetu kwa kutukanusha, na akawaonya na kuwahadharisha adhabu yetu, isipokuwa wale ambao ziliwatia kiburi neema miongoni mwa viongozi na wakubwa huwa wakisema, ”Sisi tuliwakuta baba zetu kwenye mila na dini, na sisi ni wenye kufuata mwenendo wao na njia yao.”
Huyo Muonyaji, akiwa ni Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale Mitume waliomtangulia, huwa akisema kuwaambia waliompinga wakitumia udanganyifu huu uliyotanguka, «Je, mtawafuata baba zenu , hata kama mimi nimewajia kutoka kwa Mola wenu na kitu chenye kuongoza zaidi kwenye njia ya haki na chenye kuonyesha zaidi njia ya uongofu kuliko kile mlichowakuta baba zenu wakikifuata cha dini na mila?” Na wao huwa wakisema kwa ushindani, ”Sisi ni wenye kuyapinga na kuyakanusha hayo mliyotumilizwa kwayo.”
Basi tukawalipiza hao ummah waliowakanusha Mitume wao kwa kuwateremshia mateso ya kuwadidimiza, kuwazamisha na mengineyo. Basi angalia, ulikuwa vipi mwisho wa mambo yao walipozikanusha hoja za Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Basi na wajihadhari watu wako wasiendelee kwenye ukanushaji wao ili yasiwapate wao yale yaliyowapata wale.
Kumbuka, ewe Mtume, pindi aliposema Ibrāhīm alipomwambia baba yake na watu wake waliokuwa wakiabudu vitu ambavyo watu wako , ewe mtume, wanaviabudu, ”Hakika mimi nimejiepusha na vile mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu.
«Isipokuwa Yule Aliyeniumba , kwani Yeye Ataniafikia kufuata njia ya uongofu.”
Na Ibrāhīm, amani imshukie, alilifanya neno la kumpwekesha Mwenyezi Mungu (Lā ilāha illā Allāh) ni lenye kusalia baada yake, kwa kutarajiwa warudi kumtii Mola wao na kumpwekesha. Na kutubia kutokana na ukanushaji wao na dhambi zao.
Bali niliwastarehesha hawa washirikina wa watu wako, ewe mtume, na wazazi wao kabla yao kwa uhai, sikuwaharakishia adhabu kwa ukanushaji wao mpaka ikawajia Qur’ani na Mtume wa kuwabainishia wanachokihitajia katika mambo ya Dini yao.
Na ilipowajia Qur’ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu walisema, «Hii uliyotuletea ni uchawi wa kuturogea nao, na si wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, na sisi tunaukanusha.”
Na hawa washirikina wa Kikureshi walisema, «Iwapo hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu kikweli, basi si ateremshiwe mtu mkuu kutoka miji hii miwili: Makkah au Ṭāif.
Je, wao ndio wanaougawa huu utume wakauweka wanapotaka? Sisi tumewagawia wao maisha yao katika uhai wao wa kilimwengu ya riziki na vyakula, na tumewainua daraja baadhi yao juu ya wengine :huyu ni tajiri na huyu ni masikini, huyu ana nguvu na huyu ni mnyonge, ili baadhi yao wawe ni wenye kutumiwa na wengine katika maisha. Na rehema ya Mola wako, ewe Mtume, ya kuwatia wao Peponi ni bora kuliko takataka za dunia zenye kutoweka.
Na lau si kuwa watu watajumuika pamoja kwenye ukafiri, tungalizifanya nyumba za wale wenye kumkanusha Mwingi wa Rehema ziwe na ghorofa za fedha na ngazi za wao kupandia.
Na tukazifanya nyumba zao ziwe na milango ya fedha, tukawafanyia vitanda ambavyo juu yake wanakaa na kutegemea
na tukawafanya wawe na dhahabu. Na vyote hivyo havikuwa isipokuwa ni sterehe za maisha ya kilimwengu, nazo ni starehe chache zenye kuondoka. Na starehe za Akhera zimehifadhiwa kwa Mola wako kwa wale wachamungu na si kwa wengine.
Na mwenye kuupa mgongo utajo wa Mwingi wa Rehema, nao ni Qur’ani, asiogope mateso yaliyotajwa ndani yake na asijiongoze kwa uongofu wake, tutamwekea Shetani hapa duniani wa kumpoteza, ikiwa ni malipo yake ya kuupa mgongo kwake utajo wa Mwenyezi Mungu. Shetani huyo atakuwa na yeye wakati wote na kufuatana naye, akimkataza ya halali na kumsukuma afanye ya haramu.
Na kwa hakika, Mashetani wanawazuia hawa wanaoupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu wasifuate njia ya haki, wanawapambia upotevu na wanawafanya wachukie Kumuamini Mwenyezi Mungu na kufanya matendo ya utiifu Kwake. Na wanadhani hawa wenye kupa mgongo, kutokana na vile Mashetani wanavyowapambia upotevu walionao, wanadhani kuwa wao wako kwenye haki na uongofu.
Mpaka pale atakapotujia yule aliyeupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu pamoja na yule mwenzake Shetani, ili kuhesabiwa na kulipwa, atasema yule mwenye kupa mgongo kumwambia mwenzake, «Natamani lau baina yangu mimi na wewe pana umbali wa baina ya Mashariki na Magharibi, kwani mwenza mbaya zaidi kwangu ni wewe kwa kuwa umenipoteza.”
Haitawafalia kitu leo, enyi mlioupa mgongo utajo wa Mwenyezi Mungu, kwa kushirikisha kwenu duniani, kuwa mmeshirikiana na wenzenu (wa Kishetani) katika adhabu. Basi kila mmoja ana fungu lake kamili la adhabu kama mlivyoshirikiana katika ukanushaji.
Je, kwani wewe, ewe mtume, unamsikilizisha yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemfanya kiziwi akawa haisikii haki, au unamuongoza kwenye njia ya uongofu yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameupofusha moyo wake akawa haioni haki, au unamuongoza yule aliyepotoka waziwazi akawa kando ya haki? Hayo si yako. Lako wewe ni kufikisha ujumbe, na si juu yako kuwafanya waongoke, lakini Mwenyezi Mungu Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka.
Na iwapo tutakufisha, ewe Mtume, kabla hujanusuriwa juu ya wakanushaji wa watu wako, basi sisi ni wenye kuwalipiza wao kwa kuwaadhibu huko Akhera.
Au tutakuonyesha lile tulilowaahidi la adhabu yenye kuwashukia, kama ilivyokuwa siku ya Badr, kwani sisi tuna uweza juu yao tutakupa ushindi juu yao na tutawafedhehi kwa mkono wako na kwa mikono ya wenye kukuamini,
Basi shikamana, ewe Mtume, na kile alichokuamrisha Mwenyezi Mungu katika hii Qur’ani ambayo Mwenyezi Mungu amekuletea, kwa njia ya wahyi. Hakika wewe uko kwenye njia iliyonyoka, nayo ni Dini ya Mwenyezi Mungu aliyoamrisha ifuatwe ambayo ni Uislamu. Hapa pana kumpa moyo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumsifu.
Na hii Qur’ani ni utukufu kwako na kwa watu wako miongoni mwa washirikina wa Kikureshi, kwa kuwa imeteremshwa kwa lugha yao, kwa kuwa wao wanaifahamu zaidi kuliko watu wengine na kwa hivyo inatakiwa wawe ni watu wenye kusimama nayo zaidi na ni wenye kufanya matendo yanayoambatana nayo zaidi. Na mtaulizwa , wewe na walio pamoja na wewe, kuhusu vile mlivyomshukuru kuletewa hiyo Qur’ani na mlivyoifanyia kazi.
Na uwaulize, ewe Mtume, wafuasi wa wale tuliowatumiliza kabla yako miongoni mwa Mitume wetu na wabebaji sheria zao, «Je walikuja Mitume wao na ujumbe wa kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu?” Wao watakupasha habari kuwa hilo halikutukia, kwani Mitume wote walilingania kile ulichowaitia watu cha kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake Asiye na mshirika, na wakakataza kuabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Kwa hakika tulimtumiliza Mūsā kwa hoja zetu aende kwa Fir’awn na watukufu wa watu wake kama tulivyokutumiliza wewe, ewe mtume, kwa hawa washirikina wa watu wako, na Mūsā akawaambia, «Mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa viumbe wote.”
Na alipowajia na dalili zilizo wazi zenye kuonyesha ukweli wake katika ulinganizi wake, hapo Fir’awn na viongozi wa utawala wake wakawa wanazicheka zile hoja na mazingatio alivyokuja navyo Mūsā.
Na hatukuwa tukimuonyesha Fir’awn hoja yoyote isipokuwa huwa ni kubwa zaidi kuliko ile iliyokuwa kabla yake na inautolea dalili zaidi usahihi wa kile ambacho Mūsā alikuwa akiwalingania kwacho. Na tuliwapatiliza kwa aina mbalimbali za adhabu , kama vile Nzige, chawa, vyura, mafuriko na nyinginezo ili wapate kurudi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kuacha kumkanusha.
Na Fir’awn na viongozi wa utawala wake wakasema kumwambia Mūsā, ”Ewe mjuzi! (Na mchawi alikuwa kwao ni mtu mkubwa wanayemheshimu, na haukuwa uchawi ni sifa ya mtu kutukanika), ’Tuombee Mola wako, kwa ile ahadi Aliyokuahidi na yale matukufu Aliyokutunukia wewe mahsusi, Atuepushie adhabu, kwani tukiepushiwa adhabu, kwa hakika sisi ni wenye kuongoka na kuayaamini yale uliotujia nayo.
Basi Mūsā alipoomba adhabu iondolewe kwao na tukawaondolea hiyo adhabu, ghafla wanavunja ahadi na wanaendelea kwenye upotevu wao.
Na Fir’awn aliita mbele ya wakubwa wa watu wake kwa kujigamba na kujisifu kwa ufalme wa Misri, «Je, kwani mimi sina ufalme wa Misri na mito hii inayopita chini yangu? Kwani hamuoni utukufu wangu na nguvu zangu na unyonge wa Mūsā na umasikini wake?
«Bali mimi ni bora kuliko huyu asiye na utukufu. Kwani yeye anajidhalilisha katika kuataka haja zake kwa udhaifu wake na unyonge wake, na hafafanui maneno kwa ajili ya uzito wa ulimi wake.» Na lililomfanya Fir’awn atoe kauli hii ni ukafiri, ushindani na uzuiaji njia ya Mwenyezi Mungu.
«Basi si apewe huyo Mūsā, iwapo ni mkweli kuwa yeye ni Mjumbe wa Mola wa viumbe wote, vikuku vya dhahabu, au waje Malaika pamoja na yeye wameshikana na kukutana na wakafuatana wakimtolea ushahidi kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwetu sisi.»
Fir’awn akazichezea akili za watu wake, akawaita kwenye upotevu na wao wakamtii na wakamkanusha Mūsā. Kwa hakika, wao walikuwa ni watu waliotoka kwenye utiifu wa Mwenyezi Mugu na njia yake ya sawa.
Walipotukasirisha, kwa kutuasi na kumkanusha Mūsā na miujiza aliyokuja nayo, tuliwatesa kwa adhabu ya duniani tuliyowaharakishia na tukawazamisha wote baharini.
Tukawafanya hao tuliowazamisha baharini kuwa ni mfano uliotangulia kwa anayefanya matendo kama yao katika wale watakaokuja baada yao kwa kustahiki adhabu, na ni mazingatio na mawaidha kwa watu wa nyuma.
Na washirikina walipopiga mfano wa Īsā mwana wa Maryam walipomjadili Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumhoji kuwa Wanaswara wanamuabudu, unawakuta watu wako wanainua sauti zao na kupiga kelele kwa furaha na kuterema. Napo ni pale neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka lilipoteremka (Nyinyi na vile mnavyoviabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Moto, nyinyi nyote ndani ya Moto huo mtaingia). Na washirikina wakasema, «Tumeridhika kwa waungu wetu wawe na cheo cha Īsā, Mwenyezi Mungu Akateremsha neno lake (Hakika wale ambao ilitangulia kutoka kwetu kuwa wao ni wema, hao ni wenye kuepushwa nao huo Moto). Yule anayetupwa Motoni, miongoni mwa waungu wa makafiri, ni yule aliyeridhika kuabudiwa na wao.
Na walisema washirikina wa watu wako, ewe Mtume, ” Je waungu wetu tunaowaabudu ni bora au ni Īsā ambaye watu wake wanamuabudu? Akiwa Īsā atakuwa Motoni, basi nasi natuwe na waungu wetu pamoja na yeye. Hawakukupigia mfano huu isipokuwa kwa kujadili, bali wao ni wabishi kwa njia ya ubatilifu.
Hakuwa Īsā mwana wa Maryam isipokuwa ni mja, tulimneemesha kwa utume na tukamfanya ni alama ya kutolea ushahidi uweza wetu.
Na lau tungakiataka tungaliwajaalia badala yenu Malaika , hawa baada ya wengine, badala ya wanadamu.
Kwa hakika kuteremka kwa Īsā, amani imshukie, kabla ya Siku ya Kiyama, ni dalili ya kukaribia Wakati huo, basi msitie shaka kuwa hilo ni lenye kuwa hapana budi. Na nifuateni mimi katika yale ninayowatolea habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Hii ni njia imara inayoelekea Peponi, isiyo na mpeto.
Na asiwazuie Shetani, kwa kutia kwake wasiwasi kwa watu, kunitii mimi katika yale ninayowaamrisha na ninayowakataza, kwani yeye ni adui kwenu ambaye uadui wake uko waziwazi.
Na Īsā alipowajia Wana wa lsrāīl kwa dalili zilizofunuka wazi alisema, «Nimewajia na unabii, na ili niwaeleze baadhi ya mambo ya yale mnayotafautiana kwayo katika mambo ya Dini. Basi mcheni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo Yake, na mnitii mimi katika yale ninayowaamrisha ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii.
«Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Mola wangu na Mola wenu nyote, basi muabuduni Yeye Peke Yake na msimshirikishe na Yeye kitu chochote. Hili nililowaamrisha la kumcha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ustahiki wa kuabudiwa ndio njia iliolingana sawa, nayo ni Dini ya Mwenyezi Mungu ya kweli Ambaye Hakubali kutoka kwa yoyote dini isiyokuwa hiyo.”
Hapo makundi ya watu yakatafautiana kuhusu jambo la Īsā, amani imshukie, na wakawa mapote: kati yao kuna waliokubali kuwa yeye ni mja wa Mwenyezi Mungu na ni Mtume Wake, na hiyo ndio kauli ya kweli, na kati yao kuna wanaodai kuwa yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu , na kati yao kuna wanaosema kwamba yeye ni Mwenyezi Mungu, Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na kutakasika na neno lao hilo. Basi maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama ni yenye kuwapata wale waliomsifu Īsā kwa sifa ambazo sizo zile Mwenyezi Mungu Alizomsifu nazo.
Je, kwani wana kutu chochote wanachokingojea watu wa makundi hayo waliotafautiana kuhusu Īsā isipokuwa ni kujiwa na Kiyama kwa ghafla na hali wao hawahisi wala hawatambui?
Marafiki katika kumuasi Mwenyezi Mungu duniani watatengana wao kwa wao Siku ya Kiyama. Lakini wale waliofanya urafiki juu ya uchaji Mwenyezi Mungu, urafiki wao utadumu duniani na Akhera.
Wataambiwa hawa wachamungu, «Enyi waja wangu! Hamna khofu yoyote Leo ya kupata mateso yangu, wala nyinyi hamtahuzunika juu ya hadhi za kilimwengu mlizozikosa.”
Wale walioziamini aya zetu na wakayafuata kivitendo yale walioletewa na Mitume wao, wakawa ni wenye kumtii Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote, kwa nyoyo zao na viungo vyao,
wataambiwa, «Ingieni Peponi , nyinyi na wendani wenu Waumini, mkistareheshwa humo na mkifurahishwa.”
Watazungushiwa, hawa waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, chakula ndani ya vyombo vya dhahabu na vinywaji ndani ya gilasi za dhahabu. Na humo watakuwa na kila ambacho nafsi zao zinakitamani na macho yao yanapendezwa nacho, na wao humo watakaa milele.
Na hii Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewarithisha, ni kwa sababu ya kile mlichokuwa mkikifanya ulimwenguni cha mambo ya kheri na matendo mema, na akaifanya, kwa wema Wake na rehema Yake, ni malipo yenu.
Mtakuwa nayo, humo Peponi, matunda mengi ya kila aina ya nyinyi kuyala.
Hakika ya wale waliochuma dhambi kwa ukanushaji wao, ni wenye kukaa ndani ya adhabu ya Jahanamu.
Hawatasahilishiwa, na wao wakiwa ndani yake watakuwa ni wenye kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu.
Na hatukuwadhulumu wahalifu hawa kwa kuwaadhibu , isipokuwa ni wao wenyewe ndio waliojidhulumu nafsi zao kwa kushirikisha kwao na kukataa kuwa Mwenyezi Mungu Ndie Mola wa haki, Aliye Peke Yake, Asiye na Mshirika na kuacha kuwafuata Mitume wa Mola wao.
Na hao wahalifu waliomkanusha Mwenyezi Mungu, baada ya Mwenyezi Mungu kuwatia kwenye moto wa jahanamu, watamwita Malik, mshika hazina za Moto kwa kusema, «Ewe Malik! Basi na Atufishe Mola wako, tupate kupumzika na haya tuliyonayo,” Hapo Malik awajibu, «Nyinyi ni wenye kukaa, hamna kutoka Motoni na hamna makimbilio ya kujiepusha nao.”
Kwa hakika, tumewaletea haki na kuibainisha kwenu, lakina wengi wenu mliichukia walipokuja nayo Mitume.
Je, kwani hawa washirikina wamepanga mambo madhubuti ya kuichimba haki tuliyowaletea? Sisi tunawapangia adhabu na mateso.
Au kwani wanadhani, hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, kuwa sisi hatusikii yale wanayoyaficha ndani ya nafsi zao na kunong’onezana baina yao? Basi sivyo hivyo, sisi tunasikia na tunajua, na wajumbe wetu ambao ni Malaika watukufu na watunzi wanawaandikia yote waliyoyafanya.
Sema, ewe mtume, uwaambie washirikina wa watu wako wanaodai kuwa Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu, «Iwapo Mwingi wa rehema Alikuwa na mtoto, kama vile mnavyodai, lakini hili halikuwa wala halitakuwa, basi mimi ni wa mwanzo kumuabudu mtoto huyo mnaodai, Ametakasika Mwenyezi Mungu na kuwa na mke na mtoto.”
Kuepukana na kila sifa ya upungufu na kutakasika ni kwa Mola wa mbingu na ardhi, Mola wa ’Arsh kubwa, na kuwa mbali na urongo na uzushi wanaomzulia washirikina ya kuwa Mwenyezi Mungu Ana mwana na mengineyo ya ubatilifu wanayodai.
Basi waache, ewe Mtume, hao wenye kumzulia Mwenyezi Mungu urongo wavame kwenye ubatilifu wao na wacheze katika dunia yao mpaka wapambane na hiyo Siku yao ambayo wanaahidiwa kuwa wataadhibiwa: ima hapa duniani au kesho akhera au kote kuwili.
Na Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anayeabudiwa kwa haki, mbinguni na ardhini, na Yeye Ndiye Mwingi wa hekima Aliyeimarisha kuumba Kwake na kuitengeneza Sheria Yake, Mwenye ujuzi wa kila kitu kuhusu hali ya viumbe Vyake. Hakuna chochote kinachofichamana katika hivyo.
Ni nyingi mno baraka za Mwenyezi Mungu na kheri Zake na ni mkubwa mno ufalme Wake, Ambaye ni Yake, Peke Yake, mamlaka ya mbingu saba na ardhi saba na vitu vilivyoko baina yake, na Kwake Yeye Ndiko uliyoko ujuzi wa Wakati ambapo Kiyama kitasimama na viumbe wafufuliwe kutoka makaburini mwao wapelekwe kwenye Kisimamo cha Hesabu, na Kwake Yeye mtarudishwa, enyi watu, baada ya kufa kwenu, na hapo alipwe kila mmoja kwa anayostahiki.
Na hawamiliki, wale ambao washirikina wanawaabudu, uwezo wa kumuombea yoyote mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa wale waliyoishuhudia haki na wakakubali upweke wa Mwenyezi Mungu na unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakawa na yakini ya uhakika wa kile walichokikubali na kukitolea ushahidi.
Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina wa watu wako, ”Ni nani aliyewaumba?” watasema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyetuumba.” Basi vipi wao wanageuka na wanapotoka kwa kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na kumshirikisha na asiyekuwa Yeye?
Na Atasema Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu amani zimshukie, huku akimshtakia watu wake waliomkanusha kwa Mola Wake kwa kusema, «Hawa ni watu hawakuamini wewe wala kile ulichonituma kwao.
Basi wasamehe, ewe Mtume, na uyapuuze makero yao, na lisitokee lolote kutoka kwako isipokuwa amani ambalo ni neno linalosemwa na wenye akili na busara kuambiwa wajinga, kwani wao hawatukanani na wao wala hawawalipizi kwa vitendo vyao vibaya waliowafanyia. Basi watajua watakachokikuta cha balaa na adhabu. Hapa pana onyo na kitisho kikubwa kwa makafiri hawa wenye kushindana na mfano wao.