ﮛ
surah.translation
.
ﰡ
(Alif, Lām, Rā) Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa. Hizo ni aya tukufu miongoni mwa aya za Kitabu kitukufu kilichoteremshwa kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Nazo ni aya za Qur’ani zenye kufafanua kweli kwa matamko mazuri zaidi na yaliyo wazi zaidi na yenye kuonyesha zaidi makusudio. Kitabu na Qur’ani ni kitu kimoja ; na hapa Mwenyezi Mungu Ameyakusanya pamoja majina mawili.
Makafiri watatamani, watakapowaona Waumini walioasi wakitoka Motoni, lau wao walikuwa ni wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wakawa ni wenye kutoka kama wao.
Waache, ewe Mtume, hao makafiri wapate kula na wastarehe na ulimwengu wao na iwashughulishe tamaa ya huo ulimwengu wasimtii Mwenyezi Mungu, watakuja kujua mwisho wa mambo yao ambayo ni hasara ya duniani na Akhera.
Na wakiomba kuteremshiwa adhabu, kwa kukukanusha, ewe Mtume, basi sisi hatuuangamizi mji, isipokuwa uwapo wakati wa kuangamizwa umeshapangwa; hatutawaangamiza mpaka waufikie mfano wa wale waliowatangulia.
Hakuna watu wowote watakaoupita muda wao uliowekwa wakauzidisha wala kuutangulia wakaupunguza.
Na wenye kumkanusha Muhammad, rehema na amani zimshukie, walisema kwa njia ya shere, «Ewe yule ulioteremshiwa Qur’ani, ‘wewe umerukwa na akili.’
Si utuletee Malaika iwapo wewe ni mkweli wapate kutoa ushahidi kwamba Mwenyezi Mungu Amekutumiliza.»
Na Mwenyezi Mungu Akawajibu: Sisi hatuwateremshi Malaika isipokuwa kwa adhabu ambayo haina kucheleweshwa kwa asiyeamini na hawakuwa ni wenye kuachwa wakati Malaika watakapoteremka.
Hakika sisi tumeiteremsha Qur’ani kwa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukiye, na hakika sisi tunachukua ahadi kuitunza isiongezwe, isipunguzwe wala sehemu yoyote katika hiyo isipotee.
Na kwa hakika tulitumiliza kabla yako, ewe Mtume, Wajumbe kati ya makundi ya wa mwanzo.
Hakuna Mjumbe yoyote aliwajia wao isipokuwa walikuwa wakimfanyia shere.Katika haya pana kumliwaza Mtume, rehema na amani zimshukie. Na kama walivyokufanyia hawa, hivyo ndivyo walivyofanyiwa Mitume kabla yako.
Kama tulivyoutia ukafiri kwenye nyoyo za ummah waliotangulia kwa sababu ya kuwafanyia shere Mitume na kuwakanusha, hivyo ndivyo tunavyofanya kwenye nyoyo za washirikina miongoni mwa watu wako waliofanya uhalifu wa kumkanusha Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake;
hawauamini Ukumbusho ulioteremshwa kwako. Na umeshapita mwendo wa wamwanzo wa kuwaangamiza wakanushaji. Na hawa ni kama wao, wataangamizwa wenye kuendelea na ukafiri na ukanushaji miongoni mwao.
Na lau tuliwafungulia makafiri wa Makkah mlango wa mbingu, wakaendelea kupanda kuingia ndani wapate kuyashuhudia yaliyomo mbinguni ya ajabau za ufalme wa Mwenyezi Mungu, hawangaliamini
na wangalisema, «Macho yetu yamerogwa mpaka tumekuwa tunaona tusiyoyaona. Sisi tumerogwa tu na Muhammad kwenye akili zetu.»
Na miongoni mwa dalili za uweza wetu ni kwamba sisi tumeweka kwenye uwingu wa karibu vituo ya sayari kushukia, ambayo kwayo zinajulikana njia, nyakati, urutuba na ukavu, na tumeupamba uwingu huu kwa nyota ili wenye kuziangalia wataamali na wazingatie.
Na tumeuhifadhi uwingu huo na kila Shetani Aliyetolewa na aliyefukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu ili asiufikie.
Isipokuwa aliyetega sikio kusikiliza maneno ya watu wa juu baadhi ya nyakati, akafikiwa na sayari inayotoa mwangaza na kumchoma.Na huenda Shetani akamddokeza rafiki yake baadhi ya habari alizozisikia kwa kutegea kabla hajateketezwa na kimondo.
Na ardhi tumeinyosha ikawa kunjufu, tukaweka juu yake majabali yenye kuiimarisha , tuakaotesha kila aina ya mimea ambayo waja wanaihitajia kwa kipimo kinachojulikana.
Na tukawawekea nyinyi humo vitu mnavyovihitajia katika maisha yenu miongoni mwa makulima, wanyama, aina mbalimbali ya shughuli za kujipatia maisha na vinginevyo. Na tukawaumbia nyinyi watoto, watumishi na wanyama manaonufaika nao. Na riziki zao haziko juu yenu, bali ziko juu ya Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe vyote kwa wema utokao Kwake na ukarimu.
Na hakuna chochote cha manufaa ya waja isipokuwa ziko kwetu hazina zake za kila aina, na hatukiteremshi isipokuwa kwa kadiri iliyowekewa mpaka, kama vile tutakavyo. Hazina zote ziko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, Anampa Anayemtaka na Anamzuilia Anayemtaka, kulingana na rehema Yake kunjufu na hekima Yake kubwa.
Na tunatuma upepo na tunaufanya uwe mtiifu kwetu uyajaze mawingu yabubujishe maji na yanyeshe na yanywesheze miti, hapo majani yake yafunguke na mafumba yake yajitokeze. Na mvua inabeba heri na nafuu na tunayateremsha maji yake tuliyowatayarishia nyinyi kwa ajili ya kunywa kwenu, ardhi yenu na wanayama wenu. Na nyinyi si waweza wa kuyahifadhi na kuyaweka akiba, lakini sisi tunawahifadhia kwa kuwahurumia na kuwafanyia hisani.
Ndio sisi tunaompa uhai aliyekufa kwa kumpatisha kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na tunamfisha aliyekuwa hai baada ya ajali yake kukoma. Na sisi ndio wenye kuirithi ardhi na walioko juu yake.
Kwa hakika tunawajua walioangamia miongoni mwenu tangu Ādam, walio hai na watakaokuja mpaka Siku ya Kiyama.
Na hakika Mola wako Ndiye Atakayewakusanya wao wahesabiwe na walipwe. Hakika Yeye ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo, ni Mwingi wa ujuzi, hakuna kinachofichika Kwake.
Kwa hakika tulimuumba Ādam kwa udongo mkavu, ukigongwa unasikiwa sauti. Na udongo huu mkavu ni miongoni mwa udongo mweusi uliogeuka rangi yake na harufu yake kwa kipindi kirefu cha kukaa kwake.
Na tulimuumba baba wa majini, naye ni Iblisi, kabla ya kuumbwa Ādam, kwa moto mkali sana, usio na moshi.
Kumbuka, ewe Mtume, pindi Mola wako Aliposema kuwaambia Malaika, «Mimi nitamuumba mtu kutokana na udongo mkavu. Na udongo huu mkavu unatokana na udongo mweusi uliogeuka rangi.
«Basi nitakapomtengeneza na kulikamilisha umbo lake na nikapuliza roho ndani yake, mwangukieni hali ya kusujudu,» sijida ya maamkizi na heshima na si sijida ya ibada.
Na Malaika wote walisujudu kwa umoja wao, kama Alivyowaamrisha Mola Wao.. Hakuna yoyote kati yao aliyekataa.
Lakini Iblisi alikataa kumsujudia Ādam pamoja na Malaika waliosujudu.
Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia Iblisi, «Una nini wewe kutosujudu pamoja na Malaika?»
Iblisi akasema akionyesha kiburi chake na uhasidi wake, «Hainasibiani na mimi nimsujudie mtu uliyempatisha kutokana na udongo mkavu, uliokuwa mweusi na uliogeuka.»
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Akamwambia, «Basi toka Peponi, wewe ushafukuzwa na umeepushwa na kila jema,
umeshukiwa na laana na umewekwa mbali na rehema yangu mpaka Siku ya kufufuliwa watu ili wahesabiwe na walipwe..»
Iblisi akasema, «Ewe Mola wangu! Nipatie muda mpaka siku ya wewe kuwafufua waja wako , nayo ni Siku ya Kiyama.»
Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Wewe ni miongoni mwa wale niliowapa muda na kuchelewesha kuwaangamiza mpaka siku ambayo viumbe wote watakufa baada ya Mpulizo wa kwanza,
na siyo mpaka siku ya Ufufuzi. Na alikubaliwa hilo kwa njia ya kulegezewa na kuachiliwa, na ni mtihani kwa binadamu na majini.
Akasema Iblisi, «Mola wangu, kwa sababu ya vile ulivyonipoteza na kunipotosha nitawapambia vizazi vya Ādam kukuasi katika ardhi na nitawapoteza wote wasiione njia ya uongofu,
isipokuwa waja wako ambao umewaongoa wakakutakasia ibada peke yako pasi na viumbe wako wengine.»
Akasema Mwenyezi Mungu , «Hii ni njia nyofu iliyolingana inayofikisha kwangu na kwenye Nyumba ya ukarimu wangu.
Kwa kweli, wale waja wangu ambao wamenitakasia mimi sitakupatia uwezo juu ya nyoyo zao ili uwapoteze kwa uwezo huo na njia iliyonyoka. Lakini uwezo wako utakuwa ni juu ya yule aliyekuandama miongoni mwa wapotofu washirikina ambao wameukubali usimamizi wako na kukutii badala ya kunitii mimi.»
Hakika Moto mkali ndio agizo la Iblisi na wafuasi wake wote.
Una milango saba , kila mlango uko chini ya mwengine. Kila mlango utakuwa na fungu na sehemu la wafuasi wa Iblisi kulingana na matendo yao.
Hakika wale waliomcha Mwenyezi Mungu, kwa kuyafuata Aliyoyaamrisha na kujiepusha na aliyoyakataza.watakuwa kwenye mabustani ya Pepo na mito ipitayo.
Wataambiwa, «Ingieni Mabustani haya mkiwa watulivu mumesalimika na kila ovu mumeaminika na kila adhabu.
Na tutawaondolea yaliyomo ndani ya nyoyo zao ya chuki na uadui, wataishi Peponi wakiwa ndugu wapendanao, watakaa kwenye vitanda vikubwa na nyuso zao zitaelekeana katika hali ya kuungana na kupendana.
Haitawapata humo tabu wala uchovu. Na wao ni wenye kusalia humo milele.
Wapashe habari, ewe Mtume, waja wangu kwamba mimi ni mwenye kuwasamehe Waumini wenye kutubia, ni mwenye huruma kwao,
na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iumizayo yenye kutia uchungu kwa wasiotubia.
Na wapashe habari, ewe Mtume, kuhusu wageni wa Ibrāhīm miongoni mwa Malaika ambao walimpa habari njema za kupata mwana na za kuangamia kwa jamaa za Lūṭ.
Pindi walipoingia kwake na wakamwamkia kwa kusema, «Amani.» Hapo naye akawarudishia maamkizi ya amani. Kisha akwaletea chakula na wao wasikile, na hapo akasema, «Sisi ni wenye kicho na nyinyi.»
Malaika wakamwambia, «Usiwe na kicho. Sisi tumekuja kukupa habari njema kwamba utapata mwana atakayekuwa na ujuzi mwingi wa Dini, naye ni Is’ḥāq.»
Ibrāhīm akasema, huku yuwaona ajabu, «Mnanipa habari njema za kupata mwana na mimi nishakuwa mtu mzima, na mke wangu pia, ni kwa njia gani mnanipa habari njema hizo za kushangaza?»
Wakasema, «Tunakupa habari njema kwa kweli ambayo Mwenyezi Mungu Ametujulisha nayo. Basi usiwe miongoni mwa waliokata tamaa ya wewe kupata mwana.»
Ibrāhīm akasema, «Hakika hawakati tamaa na rehema za Mola wao isipokuwa walio na makosa waliojitenga na njia ya haki.»
Na akasema, «Ni jambo gani kubwa mlilolijia, enyi mliotumwa, kutoka kwa Mwenyezi Mungu?»
Wakasema, «Hakika Mwenyezi Mungu Ametutuma kuwaangamiza watu wa Lūṭ walio washirikina wapotofu,
isipokuwa Lūṭ na watu wake waliomuamini, hao hatutawaangamiza na tutawaokoa wote.
Ama yule mke wake aliye kafiri, tumepitisha kwa amri ya Mwenyezi Mungu kumwangamiza pamoja na watakaosalia kwenye adhabu.»
Basi walipofika kwa Lūṭ Malaika waliotumwa,
Aliwaambia, «Kwa kweli, nyinyi ni watu msiojulikana na mimi.»
Wakasema, «Usiogope. Kwani hakika yetu sisi tumekujilia na adhabu ambayo jamaa zako walikuwa na shaka nayo na hawakuwa wakiikubali kuwa ni kweli.
Na tumekujia na haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwa hakika sisi ni wasema kweli.
Kwa hivyo, toka miongoni mwao , wakiwa pamoja na wewe watu wako waumini, baada ya kupita sehemu ya usiku. Na wewe nenda nyuma yao isije mmoja wao akasalia nyuma ikampata adhabu. Na jichungeni asije mmoja wenu akageuka na akatazama nyuma yake asije akaona adhabu na pia naye ikampata. Na kimbilieni kule ambako Amewaamrisha Mwenyezi Mungu, ili mpate kuwa mahali salama penye amani.
Na tukampelekea wahyi Lūṭ kwamba watu wako(waliokukanusha) wataangamizwa wote, hakuna atakayesalia, pindi kutakapoanza kupambazuka.
Na wakaja wakazi wa mji wa Lūṭ mpaka kwa Lūṭ pindi walipojua kwamba kwake kuna wageni, huku wana furaha na nderemo kwa wageni wake, ili wawachukue wafanye nao machafu.
Lūṭ akawaambia, «Hawa ni wageni wangu, na wako kwenye himaya yangu, basi msiniaziri,
na yaogopeni mateso ya Mwenyezi Mungu, wala msiwasumbue mkaniingiza kwenye unyonge na madharau kwa kuwaudhi wageni wangu.»
Watu wake wakasema, «Kwani sisi si tulikukataza kumkaribisha mgeni yoyote miongoni mwa walimwengu - na walikuwa wakiwakatia njia wasafiri - kwa kuwa sisi tunataka kufanya machafu na wao?»
Lūṭ akasema kuwaambia, «Hawa wanawake wenu ni mabinti zangu, waoeni iwapo mnataka kumaliza hamu zenu, wala msiyafanye mliyokatazwa na Mwenyezi Mungu ya kuwajia wanaume.» Amewaita hao wanawake kuwa ni mabinti zake, kwa kuwa Nabii wa ummah ana cheo cha baba kwao.
Muumba Anaapa kwa Anayemtaka na kwa Anachokitaka. Ama muumbwa haifai kwake kuapa isipokuwa kwa jina la Mwenyezi mungu. Na Ameapa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa uhai wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumtukuza kwa watu, kwamba watu wa Lūṭ wako kwenye sahau kali, wana shaka na wako kwenye ushindani.
Walikuwa hivyo mpaka kilipowashukia kimondo cha adhabu katika kipindi cha kutoka jua.
Hapo tulivipindua vijiji vyao tukavifanya juu yake kuwa chini yake, na tukawanyeshea mawe ya udongo uliokauka ulio mgumu.
Kwa hakika, katika yale yaliyopwapata pana mawaidha kwa wenye kuangalia na kuzingatia.
Na kwa hakika, vijiji vyao viko kwenye njia ya kudumu ambayo wasafiri wanaopitia huko wanaviona.
Kwa hakika, katika kule kuwaangamiza kwetu pana ushahidi waziwazi kwa wenye kuamini na wenye kutenda matendo yanayoambatana na sheria za Mwenyezi Mungu.
Na kwa hakika, wakazi wa mji uliozingirwa na miti, nao ni watu wa Shu'ayb, walikuwa ni wenye kuzidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume wao mtukufu.
Hivyo basi tuliwaadhibu kwa mtetemeko na adhabu ya siku ya uvuli. Na kwa hakika, makazi ya watu wa Lūṭ na watu wa Shu'ayb yako katika njia iliyo wazi, watu wanayapitia katika safari zao na wanapata mazingatio.
Na kwa hakika, walimkanusha Mtume Ṣāliḥ, amani imshukiye, watu wa bonde la Hijr, nao ni kina Thamūd, wakawa kwahilo ni wenye kuwakanusha Mitume wote. Kwani mwenye kumkanusha Mtume mmoja huwa amewakanusha Mitume wote, kwani wao wako kwenye Dini moja.
Na tuliwapa watu wa Ṣāliḥ aya zetu zinazojulisha usahihi wa mambo ya haki ambayo amekuja nayo kwao Mtume Ṣāliḥ, na miongoni mwayo ni ngamia, waszingatie kwa aya hizo na wakawa ni wenye kujiweka mbali nazo na kuzipa mgongo.
Na walikuwa wakiyachonga majabali na wakifanya humo majumba, na huku wao wanajiaminisha kwamba hayatawaangukia na hayataharibika.
Kikawachukua wao kimondo cha adhabu kipindi cha kucha mapema.
Na hazikuwatetea wao mali zao wala zile ngome kwenye mlilima ya mawe wala zile nguvu na heshima walizopewa.
Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake isipokuwa kwa haki, zikiwa ni zenye kujulisha ukamilifu wa muumba wake na uweza Wake, na kwamba Yeye Ndiye Ambaye ibada yoyote haifai kufanyiwa isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiyekuwa na mshirika. Na ule wakati ambao Kiyama kitasimama hauna budi ni wenye kuja, ili kila mtu apate kulipwa kwa yale aliyoyatenda. Basi wasamehe, ewe Mtume, hao washirikina, usiwachukulie na uyaachilie mbali wanayoyatenda.
Hakika Mola wako Ndiye Muumba wa kila kitu, Ndiye Anayekijua, kwa hivyo hakuna kitu chochote kinachomshinda wala kufichika Kwake katika ardhi wala mbinguni.
Na kwa kweli tumekupa, ewe Mtume, ufunguo wa Qur,ani, nao ni hizo aya saba (za sura ya Fatiha) zinazokaririwa katika kila Swala, na tumekupa Qur,ani tukufu.
Usiziangalie kwa macho yako mawili zile starehe za duniani ambazo tuliwastarehesha nazo makafiri aina mbalimbali, na usisikitike juu ya ukafiri wao, na uwanyenyekee wenye kumuamini MwenyeziMungu na Mtume wake.
Na sema, «Mimi ndiye muonyaji mwenye kuyafunua wazi yale ambayo watu wanaongokea kwayo kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu.
Na ni mwenye kuwaonya nyinyi isije ikawapata adhabu kama ile Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa wale walioigawanya Qur,ani, wakaiamini baadhi yake na wakaikanusha baadhi nyingine miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara na makafiri wa Kikureshi.
«Na wao ni wale walioifanya Qur’ani kuwa ni vigawannyo na mafungu.» Kati yao kuna wanaosema, ‘ni uchawi’ na kati yao kuna wanaosema, ‘ni ukuhani’ na kati yao kuna wanaosema yasiyokuwa hayo ili wawazuie watu kufuata uongofu.
Naapa kwa Mola wako, tutawahesabu tena tutawahesabu Siku ya Kiyama, na tutawalipa tena tutawalipa wote kwa kuigawanya kwao Qur’ani, kwa kuzua kwao urongo, kuibadilisha, kuipotoa na yasiyokuwa hayo
ambayo wao walikuwa wakiyatenda ya kuabudu mizimu, maasia na madhambi. Na katika haya pana kuwatisha na kuwaonya wao wasidumu nayo haya matendo mabaya.
Na utangaze waziwazi ulinganizi wa haki ambao Amekuamrisha nao Mwenyezi Mungu, wala usiwajali washirikina, kwani kwa kweli Amekutakasa Mwenyezi Mungu kutokana na hayo wanayoyasema.
Sisi, kwa hakika, tumekutosheleza hao wacheza shere wenye kufanya dharau kati ya viongozi wa Kikureshi
ambao wameifanya mizimu na vinginevyo kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Basi watakuja kuujua mwisho wa vitendo vyao, hapa duniani na kesho Akhera.
Na kwa kweli, tunaujua unyongekaji wa kifua chako, ewe Mtume, kwa yale wayasemayo washirikina kuhusu wewe na kuhusu ulinganizi wako.
Kimbilia kwa Mola wako pindi unaponyongeka moyo wako, na uitakase dhati Yake kwa kumshukuru na kumsifu. Na uwe ni miongoni mwa wenye kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na wenye kumuabudu, kwani kwa kweli hilo litakutosheleza na lile lenye kukutia kero.
Na uendelee kumuabudu Mola wako muda wa uhai wako mpaka ikujie yakini isiyokuwa na shaka nayo ni kifu. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alitekeleza amri ya Mola Wake, kwani hakuacha kuendelea kumuabudu Mwenyezi Mungu mpaka ikamjia yakini ya kifo kutoka kwa Mola Wake.