ﮫ
surah.translation
.
ﰡ
ﭑ
ﰀ
«Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqrah.
Aya hizi ni aya za Qur’ani yenye hekima kubwa.
Aya hizi ni uongofu na ni rehema kwa waliofanya vizuri kuyafiuata kivitendo yale yaliyoteremshwa katika Qur’ani na aliyowaamrisha kwayo Mtume wao Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Wanaotekeleza Swala kikamilifu kwa nyakati zake na wanaotoa Zaka zilizo lazima juu yao kwa wanaostahiki kupewa. Na hali wao wana yakini kuwa kuna kufufuliwa na kulipwa Akhera.
Hao wanaosifika kwa sifa zilizotangulia wako kwenye ubainifu na nuru kutoka kwa Mola wao, na wao ndio wenye kufaulu ulimwenguni na Akhera.
Na miongoni mwa watu kuna anayenunua maneno ya pumbao, nayo ni kila chenye kumpumbaza mtu na utiifu wa Mwenyezi Mungu, ili awapoteze watu na njia ya uongofu wafuate njia ya matamanio na azifanye aya za Mwenyezi Mungu kuwa ni shere, basi hao watakuwa na adhabu yenye kuwadhalilisha na kuwatweza.
Na anaposomewa aya za Qur’ani anaupa mgongo utiifu wa Mwenyezi Mungu na anafanya kiburi bila kuzingatia, kama kwamba yeye hakusikia kitu, kama kwamba kwenye mashikio yake kuna uziwi. Na yoyote ambaye hali yake ni hii, mpe bishara, ewe Mtume, ya adhabu kali yenye kuumiza humo Motoni Siku ya Kiyama.
Hakika wale waliomuamini mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda mema waliyoamrishwa, hao wana starehe ya daima ndani ya mabustani ya Peponi.
Na uhai wao katika mabustani hayo ya Peponi ni uhai wa milele, haukatiki wala haumaliziki, Mwenyezi Mungu Amewaahidi hilo ahadi ya kweli. Na Yeye , kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Haendi kinyume na ahadi Yake. Na Yeye ni Mshindi katika amri Yake, ni Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake.
Ameumba mbingu, Akaziinua bila ya nguzo kama mnavyoziona. Na Ameweka ndani ya ardhi majabali yaliyojikita, ili zisipate kutikisika na kutetemeka yakaharibika maisha yenu. Na Ameeneza kwenye ardhi aina mbalimbali za wanyama. Na tumeteremsha kutoka mawinguni mvua, tukaotesha kwayo kwenye ardhi kila aina ya mimea mizuri yenye nafuu yenye mandhari mazuri.
Na vyote mnavyovishuhudia ni viumbe vya Mwenyezi Mungu, basi nionesheni, enyi washirikina, imeumba nini hiyo miungu yenu mnayoiabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Bali washirikina wameenda kando na haki na msimamo wa sawa waziwazi.
Na kwa hakika tulimpa mja mwema miongoni mwa waja wetu , naye ni Luqman, busara, nayo ni ufahamu wa Dini, akili na usawa wa maneno, na tulimwambia, «Zishukuru neema za Mwenyezi Mungu juu yako. Na Mwenye kumshukuru Mola wake, faida yake itamrudia mwenyewe, na Mwenye kukanusha neema Zake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hahitaji kushukuriwa, ni Zake Yeye shukrani na sifa njema kwa kila hali.
Na kumbuka na utaje, ewe Mtume, ushauri wa Luqman kwa mwanawe alipomuambia kwa kumwaidhia, «Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu ukajidhulumu nafsi yako, hakika ushirikina ni dhambi kubwa na ovu kabisa la madhambi makubwa.»
Na tulimuamuru binadamu kuwatendea wema wazazi wake wawili na kuwafanyia hisani, Mamake alimbeba tumboni, shida juu ya shida, na mimba yake na kumaliza kunyonya kwake ni ndani ya kipindi cha miaka miwili, na tukamwambia, «Mshukuru Mwenyezi Mungu kisha uwashukuru wazazi wako, kwangu mimi ndio marejeo nipate kumlipa kila mmoja kwa anachostahili.
«Na wakikusukuma kwa bidii wazazi wako wawili, ewe mtoto mwema, ili unishirikishe mimi na mwingine katika kuniabudu katika kitu ambacho huna ujuzi nacho, au wakakuamuru ufanye jambo miongoni mwa mambo ya kumuasi Mwenyezi Mungu basi usiwatii, kwani hakuna kutiiwa kiumbe kwa kuasiwa Muumba. Na suhubiana nao ulimwenguni kwa wema katika mambo mema yasiyo na madhambi. Na ufuate, ewe mwana mwenye Imani, njia ya aliyetubu kutokana na dhambi zake, akarudi kwangu na akamuamini Mtume wangu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kisha ni kwangu mimi marejeo yenu, niwape habari ya yale mliokuwa mkiyafanya duniani na nimlipe kila mtenda kwa matendo yake.
«Ewe mwanangu! Jua kwamba uovu au wema uwapo ni kadiri ya chembe ya hardali, nayo ni ile iliyo upeo wa udogo, iliyo ndani ya jabali au iliyo mahali popote, mbinguni au ardhini, Mwenyezi Mungu Ataileta Siku ya Kiyama na Ataihesabu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja Wake, ni Mtambuzi wa matendo yao.
«Ewe mwanangu! Simamisha Swala kikamilifu kwa kutimiza nguzo zake, sharti zake na mambo ya lazima yake, na uamrishe mema na ukataze maovu, na ujue kwamba nyasia hizi ni miongoni mwa mambo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu ambayo inatakiwa kuyafanyia pupa.
«Na usizungushe uso wako ukauepusha na watu unaposema na wao au wanaposema na wewe, kwa kuwadharau na kuwafanyia kiburi, wala usitembee kwenye ardhi baina ya watu kwa kujigamba na kujivuna. Hakika Mwenyezi Mungu Hampendi kila mwenye kiburi, mwenye kujifahiri katika nafsi yake, pambo lake na maneno yake.
«Na unyenyekee katika kwenda kwako na uishukishe chini sauti yako usiipandishe juu, kwani sauti mbaya zaidi na inayochukiza zaidi ni sauti ya punda wanaojulikana kwa upumbavu wao na sauti zao za juu.»
Kwani hamuoni, enyi watu, kuwa Mwenyezi Mungu amewadhalilishia vilivyoko mbinguni miongoni mwa jua, mwezi, mawingu na vinginevyo, na vilivyoko ardhini miongoni mwa wanyama, miti, maji na vinginevyo visivyodhibitika, na Akaeneza kwenu neema Zake za nje juu ya miili na viungo, na za ndani, kwenye akili na nyoyo, na zile Alizowawekea katika zile msizozijua? Na miongoni mwa watu kuna anayefanya ushindani juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada bila ya hoja wala ubainifu wala kitabu chenye kubainisha kinachofafanua uhakika wa madai yako.
Na wakiambiwa hawa wenye kufanya ushindani juu ya kumuwahidisha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ibada, «Fuateni yale Ailiyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,» wanasema, «Bali tutafuata yale tuliyowapata wazazi wetu wako nayo ya ushirikina na kuabudu masanamu.» Je, wanafanya hayo hata kama Shetani anawaita wao, kwa kuwapambia wao matendo yao mabaya na ukanushaji wao Mwenyezi Mungu, kwenye adhabu ya Moto unaowaka?
Na mwenye kumtakasia Mwenyezi Mungu ibada yake na kumkusudia kwake Mola wake Aliyetukuka, na akawa mwema katika maneno yake, mwenye kutengeneza matendo yake, basi huwa ameshikamana na kamba yenye kufikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake yanakuwa mambo yote, Akamlipa aliye mwema kwa wema wake na aliye mbaya kwa ubaya wake.
Na mwenye kukanusha, usimsikitikie, ewe Mtume, wala usiwe na huzuni, kwa kuwa wewe umetekeleza wajibu wako wa ulinganizi na ufikishaji, kwetu sisi ndio marejeo yao na mwisho wao Siku ya Kiyama, tuwapashe habari ya matendo yao maovu waliyoyafanya duniani, kisha tuwalipe kwa hayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale ambayo nyoyo zao zinayaficha, ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na kufadhilisha kumtii Shetani.
Tutawastarehesha wao kwenye ulimwengu huu wenye kutoweka kwa muda mchache, kisha Siku ya Kiyama tutawawapeleka kwa nguvu na kuwaongoza kwenye adhabu yenye kitisho, nayo ni adhabu ya Jahanamu.
Na lau unawauliza, ewe Mtume, hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi?» Watasema, «Ni Mwenyezi Mungu.» Basi wanaposema hilo, waambie, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyeonyesha ushahidi kutoka kwenu nyinyi wenyewe.» Lakini wengi wa hawa washirikina hawaangalii wala hawazingatii ni nani anayestahiki kusifiwa na kushukuriwa , kwa hivyo ndivyo wakamshirikisha mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Ni vya Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, vyote vilivyoko mbinguni na ardhini kwa kuvimiliki, kuvifanya vifuate amri, kuvipatisha na kuvipangia mambo yake, hivyo basi hakuna anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Anayejitosheleza mwenyewe Asiyehitaji viumbe Vyake. Ni Zake Yeye shukrani na sifa njema kwa kila namna.
Na lau miti ya ardhi yote ingalichongwa ikafanywa kalamu na bahari ikawa ni wino wake, na zikaongezwa juu yake bahari saba, na yakaandikwa, kwa kalamu hizo na wino huo, maneno ya Mwenyezi Mungu yatokanao na ujuzi wake na hukumu Zake na yale ambayo Amewaletea wahyi Malaika Wake na Mitume Wake, zingalivunjika- vunjika kalamu hizo na ungaliisha wino huo, na hayangaliisha maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia ambayo hakuna mwenye kuyazunguka kiujuzi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye nguvu katika kuwatesa wanaomshirikisha, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe Vyake. Katika aya hii pana kumthibitishia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka sifa ya Maneno kikweli, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake.
Hakukuwa kuwaumba nyinyi, enyi watu, na kuwafufua Siku ya Kiyama, vile ilivyo nyepesi na rahisi, isipokuwa ni kama kuumba nafsi moja na kuifufua. Hakika Mwenyezi Mungu Anayasikia maneno yenu, Anayaona matendo yenu, na Atawalipa kwa hayo.
Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu Anazichukua baadhi ya saa za usiku, hivyo basi mchana ukarefuka na usiku ukawa mfupi, na Anazichukua baadhi ya saa za mchana, hivyo basi usiku ukarefuka na mchana ukawa mfupi, na Amewadhalilishia jua na mwezi, kila mojawapo ya hivyo viwili kinatembea kwenye mzunguko wake hadi wakati maalumu uliopangiwa, na kwamba Mwenyezi Mungu Anayaona matendo yote ya viumbe, yawe mema au mabaya, hakuna chochote kati ya hivyo kinachofichamana Kwake?
Yote hayo ni miongoni mwa ukubwa wa uweza Wake. Mpate kujua na mkubali kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye wa kweli katika dhati Yake na sifa Zake na matendo Yake, na kuwa vile wanavyoviomba visivyokuwa Yeye ndio vya urongo, na kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyetukuka, kwa dhati Yake, uweza Wake na kutendesha nguvu Kwake, Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, Aliye Mkubwa juu ya kila kitu, na kila kisichokuwa Yeye kinanyenyekea Kwake, Yeye Peke Yake Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, na si mwingine.
Kwani huoni, ewe mtazamaji, kwamba majahazi yanayotembea baharini kwa amri ya Mwenyezi Mungu ni neema itokayo Kwake kwa viumbe Wake, Apate kuwaonyesha utendakazi Wake na hoja Zake kwenu za kuwafanya nyinyi mzingatie? Hakika katika kupitisha majahazi baharini kuna dalili nyingi kwa kila mvumilivu sana wa kuyaepuka yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na katika kumtii Yeye na kuyavumilia mambo yaliyokadiriwa na Yeye, mwingi wa kushukuru neema Zake.
Na washirikina wanapopanda majahazini na mawimbi makubwa yakawazunguka pambizoni mwao kama vile mawingu na majabali, huingiwa na hofu na babaiko la kuogopa kuzama, na hapo wanamkimbilia Mwenyezi Mungu na wanamtakasia dua zao, na Anapowaokoa Akawafikisha kwenye bara, kati yao kutakua na mtu wa kati na kati asiyemshukuru Mwenyezi Mungu kikamilifu, na kati yao kutakuwa na mwenye kukanusha neema za Mwenyezi Mungu na kuzikataa. Na hakanushi aya zetu na hoja zetu zenye kutolea ushahidi ukamilifu wa uweza wetu na upweke wetu isipokuwa kila mwingi wa kuvunja ahadi, mwingi wa kukataa neema za Mwenyezi Mungu juu Yake.
Enyi watu! Mcheni Mola wenu na mtiini kwa kufuata maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, na jihadharini na Siku ya Kiyama ambayo mzazi hatamfalia kitu mwane, wala mwana hatamfalia kitu babake. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli haina shaka, basi msihadaike na uhai wa duniani na pambo lake, ukawafanya msahau uhai mwingine. Na asiwahadae nyinyi yoyote mwenye kuhadaa miongoni mwa mashetani wa kibinadamu na wa kijini.
Hakika Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anajuwa ni lini Kiyama kitasimama. Na Yeye Ndiye Anayeteremsha mvua kutoka mawinguni, hakuna awezae hilo yoyote isipokuwa Yeye. Na Anajua vilivyomo ndani ya vizazi vya wanawake. Na Anajua kitakachotendwa na kila mtu wakati ujao. Na hakuna nafsi inayojua itakufa wapi. Ni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake Ndiye Anayehusika kwa kujua hayo yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi, Ameyazunguka mambo ya nje na ya ndani, hakuna chochote katika hayo kinachofichamana Kwake.