ﯛ
ترجمة معاني سورة الأحقاف
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
ﮑ
ﰀ
“Ḥā, Mīm” Maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa yametangulia mwanzo wa sura ya Al-Baqarah.
Hii Qur’ani ni teremsho kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengezaji Wake.
Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina ya viwili hivyo isipokuwa kwa haki, si kwa mchezo na upuuzi, bali tumeziumba ili waja wapate kujua ukubwa wa Muumba wa hizo na wamuabudu Peke Yake na wajue kuwa Yeye ni Muweza wa kuwarudishia waja uhai baada ya kufa kwao, na ili wasimamishe haki na uadilifu baina yao, mpaka wakati huo uaojulikana Kwake. Na wale waliokanusha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mungu wa Kweli, wanayapa mgongo yale ambayo Qur’ani inawaonya kwayo; wao hawawaidhiki wala hawafikirii.
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa makafiri, “Je, mnawaona waungu na masanamu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Hebu nionesheni, ni sehemu gani waliyoiumba katika ardhi? Au kwani wao wana fungu katika uumbaji mbingu? Nileteeni kitabu kinachotoka kwa Mwenyezi Mungu kabla ya hii Qur’ani au athari iliyosalia ya elimu, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»
Hakuna aliyepotea zaidi wala aliye mjinga zaidi kuliko yule anayewaomba waungu wengine badala ya Mwenyezi Mungu, wasioitikia maombi yake kabisa mpaka Siku ya Kiyama, kwa kuwa waungu hao ni wafu au mawe au miti na mfano wa hivyo, na hali hivyo havina habari ya maombi ya huyo mwenye kuviabudu, havina uwezo wa kumnufaisha au kumdhuru.
Na pindi watu watakapokusanywa Siku ya Kiyama ili wahesabiwe na walipwe, wale waungu waliokuwa wakiwaomba duniani watakuwa ni maadui zao, wakiwalaani na kujiepusha nao na kukanusha kuwa wao walikuwa wanajua kuwa wale wanawaabudu wao.
Na washirikina wanaposomewa aya zetu zilizobainishwa waziwazi, wanasema hao makafiri wakati ule Qur’ani inapowajia, “Huu ni uchawi waziwazi.”
Au je wanasema hawa washirikina kwamba Muhammad ameizua Qur’ani? Waambie, ewe mtume, “Iwapo mimi nimemzulia Mwenyezi Mungu hii Qur’ani, basi nyinyi hamuwezi kunikinga mimi na adhabu ya Mwenyezi Mungu kitu chochote Akiwa atanitesa kwa hilo. Yeye, kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi zaidi wa kile mnachokisema juu ya hii Qur’ani kuliko kitu chochote kingine. Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu yangu mimi na nyinyi, na Yeye Ndiye Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwingi wa rehema kwa waja Wake Waumini.”
Sema, ewe Mtume, uwambie washirikina wa watu wako, “Sikuwa ni wa mwnzo wa wajumbe wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe Wake. Na sijui Atakalofanya Mwenyezi Mngu kwangu wala kwenu hapa duniani. Sifuati katika yale ninayowaamrisha nyinyi na katika yale ninayoyafanya isipokuwa wahyi wa Mwenyezi Mungu Anaoniletea mimi. Na sikuwa mimi isipokuwa ni mwenye kuonya ambaye uonyaji wake uko wazi.»
Sema , ewe Mtume, uwaambie washirikina wa watu wako, “Nipasheni habari: ikiwa hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu na mkaikanusha, na hali ameshuhudia shahidi kati ya Wana wa Isrāīl, kama ‘Abdullāh bin Salām, kwa mfano wa hii Qur’ani, nayo ni yaliyomo ndani ya Taurati ya kusadikisha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, akaiamini na akayafuata kivitendo yaliyokuja ndani ya Qur’ani, na nyinyi mkakanusha hilo kwa njia ya kiburi. Basi ni upi huu isipokuwa ni udhalimu mkubwa na ukafiri mwingi?” Hakika Mwenyezi Mungu Hawaongozi kwenye Uislamu na kuifikia haki wale watu waliojidhulumu kwa kumkanusha Mwenyezi Mungu.
Na wale walioukanusha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, walisema wakiwaambia wale waliomuamini, “Lau huko kumuamini Muhammad kwa aliyokuja nayo ni kheri hamngalitutangulia kuamini.” Na kwa kuwa hawakujiongoza na hii Qur’ani wala hawakunufaika na ukweli uliyomo ndani yake, watasema, “Huu ni urongo uliopokewa kwa watu wa kale.”
Na kabla ya hii Qur’ani, tuliiteremsha Taurati ikiwa ni muongozo kwa Wana wa Isrāīl waiandame na ni rehema kwa wenye kuiamini na kuifuata kivitendo. Na hii Qur’ani inasadikisha Vitabu vilivyokuwa kabla yake. Tumeiteremsha kwa lugha ya Kiarabu ili iwaonye wale waliozidhulumu nafsi zao kwa kukanusha na kuasi. Na bishara njema ni ya wale waliomtii Mwenyezi Mungu na wakafanya wema katika Imani yao na utiifu wao duniani.
Hakika wale waliosema, “Mola wetu ni Mwenyezi Mungu” kisha wakalingana sawa katika kumuamini, basi hao hawatakuwa na khofu ya babaiko la Siku ya Kiyama na vituko vyake, wala hawatasikitka juu ya hadhi za duniani walizoziacha nyuma yao
Hao ni wa watu wa Peponi, watakaa humo milele kwa rehema za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, juu yao , na kwa yale waliyoyatanguliza ya matendo mema katika dunia yao.
Na tumemuusia binadamu asuhubiane na wazazi wake wawili kwa vizuri, kwa kuwatenda wema wanapokuwa hai na baada ya kufa kwao. Kwa kuwa mamake alimbeba akiwa mwana wa matumboni kwa mashaka na tabu, na akamzaa kwa mashaka na tabu pia. Na muda wa kubeba mimba yake na mpaka kumaliza kumnyonyesha ni miezi thelathini. Katika kutaja mashaka haya anayoyabeba mama, na siyo baba, pana dalili kuwa haki yake juu ya mtoto wake ni kubwa zaidi kuliko haki ya baba. Mpaka alipofikia binadamu upeo wa nguvu zake za kimwili na kiakili na akafikia miaka arubaini, huwa akimuomba Mola wake kwa kusema, “Mola wangu! Niafikie nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu wawili, na nijaalie nifanye matendo mema unayoridhika nayo, na unisuluhishie wanangu. Hakika mimi nimetubia dhambi zangu kwako, na hakika mimi ni miongoni mwa wanyenyekevu kwako kwa utiifu na ni miongoni mwa wenye kujisalimisha kufuata amri zako na kuepuka makatazo yako, wenye kuandama hukumu yako.”
Hao ndio ambao tutayapokea kutoka kwao mazuri zaidi ya matendo mema waliyoyafanya, na tutasamehe dhambi zao, wakiwa ni miongoni mwa watu wa Peponi. Ahadi hii tuliyowaahidi ni ahadi ya ukweli na haki isiyokuwa na shaka.
Na yule aliyesema kuwaambia wazazi wake wawili walipomlingania kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na kuamini kuwa kuna kufufuliwa, “ Ubaya wenu! Je mnaniahidi kuwa nitatolewa kaburini mwangu nikiwa hai na hali kwamba makame ya ummah kabla yangu yashapita, na hakuna hata mmoja miongoni mwao aliyefufuliwa?” Na hali wazazi wake wanamuomba Mwenyezi Mungu Amuongoze na huku wakimwambia, “Ole wako! Amini na usadiki na ufanye matendo mema, hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli isiyokuwa na shaka.” Hapo awaambie, “Hayakuwa haya mnayoyasema isipokuwa ni mambo ya urongo waliyoyaandika watu wa mwanzo, yamenukuliwa kwenye vitabu vyao.”
Hao ambao sifa zao ni hizi imepasa juu yao adhabu ya Mwenyezi Mungu, na yamewashukia mateso Yake na hasira Zake, wakiwa ni katika jumla ya ummah waliopita kabla yao, miongoni mwa majini na binadamu, waliokuwa kwenye ukafiri na ukanushaji. Kwa kweli wao ni wenye hasara kwa kuchagua upotevu na kuacha uongofu, na kuchagua adhabu na kuacha starehe.
Na kila kundi la watu wema na watu waovu watakuwa tabaka mbalimbali mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, kwa matendo yao waliyoyatenda duniani, kila mmoja kulingana na daraja yake, ili Mwenyezi Mungu Awatekelezee malipo ya matendo yao. Na wao hawatadhulumiwa kwa kuongezewa maovu yao wala kupunguziwa mema yao.
Na Siku ambayo wataorodheshwa Motoni wale waliokufuru ili kuadhibiwa na waambiwe kwa kulaumiwa, “Mmeyapoteza mazuri yenu katika uhai wenu wa duniani na mmestarehe nayo. Basi leo, enyi makafiri, mtalipwa adhabu ya hizaya na unyonge ndani ya Moto, kwa kuwa mlikuwa na kiburi kwenye ardhi bila ya haki na kwa kuwa mlitoka kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu.”
Na kumbuka, ewe Mtume, Nabii wa Mwenyezi Mungu Hūd, ndugu yao kina 'Ād kinasaba na siyo kidini, alipowaonya watu wake kuwa watashukiwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakiwa kwenye nyumba zao hapo Aḥqāf (mahali kwenye mchanga mwingi) kusini mwa Arabuni. Na kwa hakika wamepita Mitume wakawaonya watu wao kabla ya Hūd na baada yake wakiwaambia, «Msimshirikishe Mwenyezi Mungu na kitu chochote mnapomuabudu. Mimi nawachelea nyinyi adhabu ya Mwenyezi Mungu katika Siku yenye kituko kikubwa , nayo ni Siku ya Kiyama.»
Wakasema, «Je, umetujia kwa ulinganizi wako ili kutuepusha na ibada ya Mola wetu? Basi tuletee hiko unachotuahidi cha adhabu, iwapo wewe ni katika watu wa ukweli wa kauli yako na ahadi yako.»
Hūd, amani imshukie, akasema, “Hakika ujuzi wa adhabu mliyoahidiwa uko kwa Mwenyezi Mwenyezi Mungu, na kwa kweli mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninawafikishia ujumbe Alionituma nao, na lakini mimi ninawaona kuwa ni watu mlio wajinga kwa kuifanyia haraka adhabu na kuwa na ujasiri juu ya Mwenyezi Mungu.
Walipoiona adhabu walioifanyia haraka imejitokeza juu ikielekea kwenye mabonde yao, walisema, “Hiki ni kiwingu chenye kutunyesheza mvua.” Hūd, amani imshukie, aliwaambia, «Hiki si kiwingu cha mvua na rehema kama mlivyodhania, bali hiki ni kiwingu cha adhabu mliyoitaka kwa haraka, huo ni upepo ambao ndani yake muna adhabu yenye uchungu na yenye kuumiza.
«Unaangamiza kila kitu unachokipitia katika vitu ambavyo ulitumwa uviangamize kwa amri ya Mola wake na matakwa Yake.» Wakawa hakuna kinachoonekana chochote katika miji yao isipokuwa nyumba zao walizokuwa wakizikaa. Mfano wa malipo haya ndiyo tunayowalipa makafiri kwa sababu ya uhalifu wao na kupita kiasi kwao.
Na tuliwarahisishia hao 'Ād sababu za kumakinika duniani kwa namna ambayo hatukuwamakinisha nyinyi, enyi Makureshi, na tukawafanya wawe na masikio ya wao kusikia na macho ya wao kuonea na nyoyo za wao kufahamia, wakavitumia katika mambo yanayomfanya Mwenyezi Mungu Awe na hasira nao. Na hilo halikuwafalia kitu chochote kwa kuwa walikuwa wakikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, na hiyo adhabu ambayo walikuwa wakiifanyia shere na kuiharakisha. Hili ni onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, imetukuka shani Yake, na ni tahadharisho kwa wenye kukufuru.
Hakika tuliiangamiza miji iliyokuwa pambizoni mwenu, enyi watu wa Makkah, kama ile ya kina 'Ād na Thamūd, tukazifanya kuta za nyumba za miji hiyo zimeanguka na kulalia sakafu zake zilizovunjika, na tuliwabainishia watu wa miji hiyo aina za hoja na dalili wapate kurudi nyuma na kuyaacha yale waliokuwa nayo ya ukanushaji Mwenyezi Mungu na aya Zake.
Basi si wangaliwasaidia wao, hao tuliowaangamiza miongoni mwa ummah waliopita, waungu wao ambao walichukua kule kuwaabudu ni ibada ya wao kujikurubisha kwa Mola wao, ili wawaombee mbele Yake. Lakini waungu wao waliwapotea, hawakuwaitikia wala hawakuwatetea. Huo ni urongo wao tu na uzushi walioupanga wa kuwafanya wao ni waungu.
Na kumbuka, ewe Mtume, pindi tulipokutumia kundi la majini kusikiliza Qur’ani kutoka kwako. Walipohudhuria, na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yuwasoma, waliambiana wao kwa wao, «Nyamazeni tusikilize Qur’ani! Na Mtume Alipomaliza kusoma Qur’ani, na wao wakawa wameielewa na ikawa imewaathiri, walirudi kwa majini wenzao wakawaonya na kuwahadharisha adhabu ya Mwenyezi Mungu wasipoamini.
walisema, «Enyi jamaa zetu! Sisi tumesikia Kitabu kilichoteremshwa baada ya Mūsā, chenye kusadikisha Vitabu vya Mwenyezi Mungu vlivyokuwa kabla yake, ambavyo Mwenyezi Mungu Ameviteremsha kwa Mitume Wake, (Kitabu) ambacho kinaongoza kwenye haki na usawa na kwenye njia sahihi iliyonyoka.
«Enyi jamaa zetu! Muitikieni Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad kwa kile anachowaitia, na muaminini yeye na myafuate kivitendo yale aliyoyaleta, Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu na Atawaokoa na adhabu yenye uchungu inayoumiza.
«Na asiyemuitikia Mtume wa Mwenyezi Mungu katika yale aliyoyalingania, basi yeye hatamshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi Akitaka kumuadhibu, wala hatakuwa na wasaidizi badala ya Mwenyezi Mungu, wenye kumkinga na adhabu Yake. Hao watakuwa wametoka nje ya haki waziwazi.
Je, wameghafilika na wasijue kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyeumba mbingu na ardhi pasi na mfano uliotangulia na bila kuelemewa na kuziumba, ni Muweza wa kuhuisha wafu ambao Aliwaumba hapo mwanzo? Ndio, hilo ni jambo jepesi kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Ambaye hakuna chochote kinachomshinda. Hakika Yeye kwa kila jambo ni Muweza.
Na Siku ya Kiyama, wataorodheshwa waliokufuru juu ya Moto wa Jahanamu ili waadhibiwe na waambiwe, «Je, hii adhabu si kweli?». watajibu kwa kusema, «Ndio. Tunaapa kwa Mola wetu kuwa hii ndiyo kweli.» Hapo waambiwe, «Basi onjeni adhabu kwa kuwa mlikuwa mkiikataa adhabu ya Moto na kuikanusha duniani.»
Basi vumilia, ewe Mtume, kwa yanayokupata ya makero ya watu wako wenye kukukanusha kama vile walivyovumilia Mitume wenye nia thabiti kabla yako wewe, nao, kwa kauli mashuhuri, ni Nūḥ, Ibrāhīm, Mūsā na Īsā, na wewe ni miongoni mwao, wala usiwafanyie haraka watu wako ya kuadhibiwa. Kwani itapotokea na wakaiona, watajihisi kama kwamba hawakukaa duniani isipokuwa muda mchache wa mchana. Haya ni mafikisho kwao na kwa wasiokuwa wao. Na haangamizwi kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa watu waliotoka nie ya amri Yake na twaa Yake.