ﮔ
surah.translation
.
ﰡ
Masahaba Zako wanakuuliza, ewe Nabii, kuhusu ngawira siku ya Badr: utawagawia vipi? Waambie, «Jambo lake limeachiwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake» Mtume ndiye mwenye kusimamia ugawaji wake kwa amri ya Mola wake. Basi jikingeni na mateso ya Mwenyezi Mungu wala msithubutu kumuasi, na muache kubishana na kuteta kwa sababu ya mali, na mzitengeneze hali zenu, na mjilazimishe utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake iwapo nyinyi ni Waumini, kwani Imani inapelekea kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Hakika wenye kumuamini Mwenyezi Mungu kikweli ni wale ambao akitajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao zinaingiwa na kicho, wasomewapo aya za Mwenyezi Mungu zinawazidishia Imani pamoja na Imani waliyo nayo kwa kuyazingatia maana yake na kwa Mola wao wanategemea: hawamtaraji isipokuwa Yeye na hawamuogopi isipokuwa Yeye.
Wale ambao wanaendelea kutekeleza Swala zilizofaradhiwa kwa nyakati zake, na katika kile tulichowaruzuku wanatoa kwenye yale tuliyowaamrisha.
Hawa wanaofanya matendo haya ndio wenye kuyaamini kikweli, nje na dani, yale Aliyowateremshia Mwenyezi Mungu, watakuwa na daraja za juu mbele ya Mwenyezi Mungu, msamaha wa dhambi zao na riziki nzuri ambayo ni Pepo.
Na kama mlivyotafautiana juu ya ugawaji wa ngawira, na Mwenyezi Mungu Akauondoa kwenu na Akauweka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, rehema na amani zimshukiye, hivyo ndivyo Mola wako Alivyokuamrisha utoke Madina uende kupambana na msafara wa Makureshi kwa wahyi aliyokujia nao Jibrili, pamoja na kuwa kundi miongoni mwa Waumini walichukia kutoka.
Likawa linabishana na wewe, ewe Nabii, kundi hilo la Waumini kuhusu kupigana baada ya kuonekana wazi kwamba hilo ni lenye kutukia, wakawa kama kwamba wao wanaongozwa kupelekwa kwenye kifo na hali wakikitazama waziwazi.
Na kumbukeni, enyi wabishi, ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu kuwa mtapata ushindi juu ya moja ya mapote mawili: msafara na bidhaa unazozibeba au jeshi la maadui, mpigane nalo na mlishinde. Na nyinyi mnapenda kupata ushindi juu ya msafara badala ya kupigana. Na Mwenyezi Mungu Anataka kuuthibitisha Uislamu na kuukuza kwa kuwaamuru nyinyi kupigana na makafiri na kuwamaliza makafiri kwa kuwaangamiza.
Ili Mwenyezi Mungu Aupe nguvu Uislamu na watu wake na auondoe ushirikina na watu wake ingawa washirikina watalichukia hilo.
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu siku ya Badr mlipoomba mpate ushindi juu ya adui yenu, Mwenyezi Mungu Akakubali maombi yenu kwa kusema, «Mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja kutoka mbinguni wakifuatana hawa baada ya wengine.
Mwenyezi Mungu Hakuufanya msaada huo usipokuwa ni bishara kwenu ya ushindi na ili nyoyo zenu zitulie na muwe na yakini ya kupata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwani ushindi watoka kwa Mwenyezi Mungu tu, si kwa ukali wa zana zenu na nguvu zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake ni Mwenye hekima katika upelekeshaji Wake na uwekaji sheria Wake.
Kumbukeni pindi Mwenyezi Mungu Alipowatia usingizi, ili kuwapa hisia ya amani ya kutoogopa kwamba adui yenu atawashinda, na kuwateremshia kutoka mawinguni maji safi, ili mjisafishe kwayo na uchafu wa nje na Awaondolee, ndani, wasiwasi na mawazo yanayoletwa na Shetani, na ili Aziimarishe nyoyo zenu kwa kuvumilia kwenye vita, na ili nyayo za Waumini ziwe thabiti zisiteleze kwa kuifanya ngumu ardhi ya mchanga kwa mvua hiyo.
Pindi Mola wako, ewe Nabii, Alipowapelekea wahyi Malaika ambao Mwenyezi Mungu Aliwasaidia nao Waislamu katika vita vya Badr, «Mimi nipo na nyinyi, nawasaidia na kuwahami, watieni hima wale walioamini, nitaweka kwenye nyoyo za waliokanusha kicho kingi, unyonge na utwevu.» Vipigeni, enyi Waumini, vichwa vya makafiri na wapigeni wao kila ncha na kila kiungo.
Hayo yaliyojiri ya kuwapiga makafiri vichwa vyao, shingo zao na ncha zao ni kwa kuwa wao walienda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na yoyote mwenye kwenda kinyume cha amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwake ulimwenguni na Akhera.
Adhabu hiyo niliyoiharakisha kwenu, enyi makafiri mnaoenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu ulimwenguni, ionjeni katika maisha ya kilimwengu, na huko Akhera mtakuwa na adhabu ya Moto.
Enyi wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Yake kivitendo, mpambanapo na waliokanusha katika vita wakawa wanasongea karibu yenu msiwape migongo yenu na mkakubali kushindwa na wao, lakini kuweni imara na wao, kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja na nyinyi na ni Mwenye kuwapa ushindi juu yao.
Na yoyote katika nyinyi atawapa mgongo wake kwenye vita, isipokuwa kwa kupenya kama mbinu ya vita ya kuwachimba makafiri au kujiunga na mjumuiko wa Waislamu waliyo vitani popote waliopo, basi huyo amestahili kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu, na makao yake ni Moto wa Jahanamu ambao ni mahali pabaya sana pa kuishia na kukomea.
Nyinyi, enyi Waumini, hamukuwaua washirikina siku ya Badr, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Aliwaua, kwa kuwa Aliwasaidia nyinyi kufanya hilo. Na hukurusha uliporusha, ewe Nabii, lakini ni Mwenyezi Mungu Aliyerusha, kwa kuwa Alikifikisha kile ulichokirusha kwenye nyuso za washirikina; na ili Mwenyezi Mungu Awafanyie mtihani wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na Awafikishe kwa sababu ya jihadi kwenye daraja za juu, na Awajulisha wao neema Zake kwao wapate kumshukuru, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa hilo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa dua zenu na maneno yenu mliyoyaficha na mliyoyafanya waziwazi, ni Mjuzi wa yenye nafuu kwa waja Wake.
Kitendo hiki cha kuwaua washirikina na kuwarushia waliposhindwa na mtihani mzuri wa kuwapa ushindi Waumini juu ya maadui zao, huo unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuja kwa Waumini, na kwamba Mwenyezi Mungu, mbeleni, ni mwenye kuvikosesha nguvu na kuvimaliza vitimbi vya makafiri mpaka wawe wanyonge na wafuate haki au waangamie.
Muombapo, enyi makafiri, kwa Mwenyezi Mungu Ayalete mateso na adhabu Yake kwa wale wenye kupita mipaka na kudhulumu, basi Mwenyezi Mungu Ameshaitikia maombi yenu Alipowaletea mateso Yake yaliyokuwa ni adhabu kwenu na ni mazingatio kwa wacha-Mungu. Na iwapo mtakomeka, enyi makafiri, kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kumpiga vita Nabii Wake, rehema na amani zimshukiye, hilo ni bora kwenu katika ulimwengu wenu na Akhera yenu. Na mkirudi vitani na kumpiga vita Muhammad, rehema na amani zimshukiye, na kuwapiga vita wafuasi wake Waumini, basi tutarudia kuwashinda kama mlivyoshindwa Siku ya Badr. Na hautawafaa mkusanyiko wenu kitu chochote kama ambavyo haukuwafaa siku ya Badr, pamoja na wingi wa idadi yenu na zana zenu na uchache wa idadi ya waumini na zana zao. Na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na Waumini kwa kuwasaidia na kuwapa ushindi.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kuweni na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika yale Aliyowaamrisha kwayo na Akawakataza nayo, na msiache kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake na hali nyinyi mnazisikia hoja na dalili zinazosomwa kwenu kwenye Qur’ani.
Wala msiwe, enyi Waumini, katika kwenda kinyume kwenu na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, rehema na amani zimshukiye, ni kama washirikina na wanafiki ambao wakisikia Kitabu cha Mwenyezi Mungu kinasomwa kwao huwa wakisema, «Tumesikia kwa masikio yetu,» na hali wao kwa hakika hawayazingatii wanayoyasikia wala hawayatii akilini.
Hakika waovu zaidi wa wanaotembea kwenye ardhi, miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu, mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi ambao masikio yao yamezibana kutoisikia haki wakawa hawasikii, mabubu ambao ndimi zao zimeshikwa kutoitamka haki wakawa hawatamki. Hawa ndio wale wasioelewa maamrisho na makatazo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na lau Mwenyezi Mungu Alijua kwamba ndani ya hawa kuna kheri yoyote Angaliwafanya wasikie mawaidha ya Qur’ani na mazingatio yake mpaka wazifahamu hoja na dalili za Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka. Lakini Yeye Alijua kwamba hamna kheri kwao na kwamba wao hawataamini. Na lau Aliwasikilizisha, kwa kukadiria na kukisia, wangaliipa mgongo Imani kwa kusudi na ujeuri, baada kuielewa. Na wao ni wenye kuipa mgongo, hawazunguki kuitazama haki kwa njia yoyote.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola na Muhammad kuwa ni Nabii na ni Mtume, Itikieni mwito wa Mwenyezi Mungu na wa Mtume kwa kumtii awaitapo kwenye haki yenye kuwapa uhai. Kwani katika kuitikia mwito huo kunatengeneza maisha yenu katika ulimwengu na Akhera. Na mjue, enyi Waumini, kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Mwenye kuendesha kila kitu na Ndiye Muweza, Anaingilia kati baina ya mtu na kile ambacho moyo wake unakitamani. Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayestahiki kuitikiwa Akiwaita, kwani mamlaka ya kila kitu yako mkononi Mwake. Na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwa Siku isiyo na shaka, ambapo kila mmoja atalipwa kwa analostahili kulipwa.
Na jihadharini, enyi Waumini, na mtihani na mkasa yenye kuwaenea waliofanya makosa na wasiofanya, hawahusishwi nayo wenye maasia wala aliyefanya dhambi; bali yanawapata watu wema pamoja nao iwapo wanaweza kukataza udhalimu wasiukataze. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwa mwenye kwenda kinyume na maamrisho Yake na makatazo Yake.
Na kumbukeni, enyi Waumini, neema za Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa ndani ya Maka ni wachache wa idadi mnanyanyaswa, mnaogopa msije mkanyakuliwa na makafiri kwa haraka, Akawapatia makao ya nyinyi kuhamia nayo ni Madina na akawapa nguvu kwa kuwapa ushindi juu yao siku ya Badr na Akawapa vyakula kati ya vitu vizuri ambavyo ngawira ni miongoni mwavyo, ili mumshukuru Yeye kwa alichowaruzuku nacho na kuwaneemesha.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na makazifuata sheria Zake kivitendo, msimhini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kwa kuyaacha Aliyowalazimisha nayo na kuyafanya Aliyowakataza nayo, na wala msifanye kasoro katika yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaamini nayo, na hali nyinyi mnajua kwamba ni amana inayopasa kutekelezwa.
Na mjue, enyi Waumini, kwamba mali yenu ambayo Mwenyezi Mungu Amewapa jukumu la kuyasimamia, na watoto wenu ambao Mwenyezi Mungu Amewapa, ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni majaribio kwa waja Wake, ili Ajue: watamshukuru kwa neema hizo na kumtii au watashughulika nazo wamsahau Yeye? Na jueni kwamba mbele ya Mwenyezi Mungu kuna heri na thawabu kubwa kwa anayemcha na kumtii.
Enyi wale ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata sheria Zake kivitendo, mkimuogopa Mwenyezi Mungu, kwa kufanya maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake, Atawafanya muwe na upambanuzi baina ya ukweli na urongo, Atawafutia madhambi yenu yaliyopita na Atawafinikia, Hatawaadhibu kwayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye hisani na vipewa vyingi vyenye kuenea.
Na kumbuka, ewe Mtume, wanapofanya njama washirikina wa Maka wakufunge au wakuue au wakuhamishe kutoka mjini kwako. Wanakufanyia njama, na Mwenyezi Mungu Aliwarudushia njama zao, ikiwa ni malipo yao, na Mwenyezi Mungu Anafanya njama; na Mwenyezi Mungu ni bora wa wenye kufanya njama.[5]
____________________
[5]Kwa kuwa njama za washirikina zinajulikana na Mwenyezi Mungu na kwa hivyo hazina athari yoyote, ndio maana ya kuwa Mwenyezi Mungu anafanya njama na kuwa njama zake zinashinda zao.
____________________
[5]Kwa kuwa njama za washirikina zinajulikana na Mwenyezi Mungu na kwa hivyo hazina athari yoyote, ndio maana ya kuwa Mwenyezi Mungu anafanya njama na kuwa njama zake zinashinda zao.
Na pindi wanaposomewa, hawa ambao walimkanusha Mwenyezi Mungu, aya za Qur’ani tukufu, wao husema kwa ujinga wao na kuikejeli kwao haki, «Tumeshalisikia hili hapo nyuma, na lau tunataka tungalisema maneno yafananayo na hii Qur’ani. Haikuwa Qur’ani hii unayotusomea, ewe Muhammad, isipokuwa ni maneno ya urongo ya watu wa kale.
Na kumbuka, ewe Mtume, neno la washirikina miongoni mwa watu wako wakimuomba Mwenyezi Mungu, «Iwapo hili alilokuja nalo Muhammad ndio haki itokayo kwako, basi tuteremshie mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu inayoumiza.»
Na hakuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka, ni Mwenye kuwaadhibu washirikina hawa na hali wewe, ewe Mtume, uko pamoja nao, na hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaadhibu wao na hali wao wanaomba msamaha wa madhambi yao.
Na vipi wao wasistahili adhabu ya Mwenyezi Mungu na hali wao wanawazuia mawalii wake Waumini kutufu Alkaba na kuswali ndani ya msikiti wa H(arām. Na wao hawakuwa ni mawalii wa Mwenyezi Mungu. Mawalii Wake si wengine isipokuwa wale wanaomuogopa Yeye kwa kutekeleza faradhi Alizoziweka na kujiepusha na mambo ya kumuasi. Lakini wengi zaidi wa makafiri hawajui, na kwa hivyo walidai kwamba wana jambo ambalo wasiokuwa wao wana haki nalo zaidi.
Hakukuwa kuswali kwao kwenye Msikiti wa H(arām isipokuwa ni kupiga mbinja na kupiga makofi, basi onjeni adhabu ya kuuawa na kutekwa siku ya Badr kwa sababu ya kukanusha kwenu na vitendo vyenu ambavyo hakuna mwenye kujitokeza kuvitenda isipokuwa makafiri wenye kukataa upweke wa Mola wao na utume wa Nabii wao.
Hakika ya wale wenye kukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na wakamuasi Mtume Wake wanatoa mali yao kuwapa washirikina na watu wa upotevu wanaofanana na wao ili kuzuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe na kuwazuia Waumini wasimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Basi watatoa mali yao kwa lengo hilo, kisha mwisho wa utoaji wao utakuwa ni majuto na hasara juu yao, kwani mali yao yatamalizika na hawatapata wanaoyatarajia ya kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu na kuzuia njia Yake isifuatwe, kisha mwishowe Waumini watawashinda. Na wale waliokufuru watakusanywa wapelekwe kwenye Jahanamu waadhibiwe humo.
Mwenyezi Mungu Atawakusanya na Atawatweza hawa ambao walimkanusha Mola wao na wakatoa mali yao kuwazuia watu kumuamini Mwenyezi Mungu na kuzuia njia Yake isifuatwe, ili Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Apate kukipambanua kichafu na kizuri, na ili Ayakusanye Mwenyezi Mungu mali ya haramu, yaliyotumiwa kuwazuia watu na dini ya Mwenyezi Mungu, Ayaweke baadhi yake juu ya mengine yawe yamekusanyikana na kupandana kisha Ayatie kwenye Moto wa Jahanamu. Makafiri hawa ndio wenye kupata hasara duniani na Akhera.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Washirikina wa watu wako kwamba watakomeka na ukafiri na kumfanyia uadui Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wakarudi kumuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake na kutompiga vita Mtume na Waumini, Mwenyezi Mungu Atawasamehe madhambi yaliyopita, kwani Uislamu unafuta yaliyopita. Na watakaporudia washirikina hawa kukupiga vita baada ya tukio ambalo ulipata ushindi juu yao siku ya Badr, basi mwendo wa watu wa mwanzo umetangulia, nao ni kwamba wao wakikanusha na wakaendelea kwenye ukaidi wao, tutawaletea adhabu na mateso kwa haraka.
Na piganeni na washirikina, enyi waumini, mpaka usiweko ushirikina na uzuiliaji wa njia ya Mwenyezi Mungu na kusiabudiwe isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika, ili chuki ziwaondokee waja wa Mwenyezi Mungu katika ardhi na mpaka dini, utiifu na ibada vitakasiwe Mwenyezi Mungu tu bila mwingine. Wakiwa watakomeka na kuwafitini Waumini na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na wakawa kwenye dini ya haki pamoja na nyinyi, basi Mwenyezi Mungu hakifichiki Kwake wanachokifanya cha kuacha ukafiri na kuingia kwenye Uislamu.
Na wakiyapa mgongo hawa washirikina yale mliyowaitia, enyi Waumini, ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuacha kuwapiga vita nyinyi, na wakakataa isipokuwa kuendelea kwenye ukafiri na kuwapiga vita nyinyi, basi kuweni na yakini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasaidia na kuwapa ushindi juu yao. Yeye Ndiye bora wa kuwasaidia na kuwapa nyinyi ushindi na wale wenye kujitegemeza Kwake juu ya maadui zenu.
Na jueni, enyi Waumini, kwamba kile mlichokipata kutoka kwa adui yenu kupitia jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi mafungu manne kati ya mafungu yake matano yapewe wapiganaji ambao walishiriki vitani, na fungu moja lililosalia kati ya yale mafungu matano litagawanywa sehemu tano: ya kwanza ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, iwekwe kwenye manufaa ya Waislamu wote; ya pili ni ya jamaa wa karibu na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, nao ni waliozalikana na Hashim na waliozalikana na Muttalib. Wamwekewa sehemu hiyo ya tano mahali pa sadaka, kwani sadaka si halali kwao. Ya tatu ni ya mayatima; ya nne ni ya masikini, na ya tano ni ya msafiri aliyemalizikiwa na matumizi, iwapo nyinyi mnaukubali upweke wa Mwenyezi Mungu, mnamtii Yeye, ni wenye kuyaamini yale Aliyomteremshia mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, miongoni mwa aya, usaidizi na ushindi katika siku Aliyopambanua baina ya haki na upotofu hapo Badr, siku lilipokutana kundi la Waumini na kundi la washirikina. Na Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Mwenye uwezo, Hashindwi na chochote.
Na kumbukeni pindi mlipokuwa kwenye upande wa bonde lililokuwa karibu sana na mji wa Madina na maadui zenu wameshukia kwenye upande wa bonde la mbali, na msafara wa biashara upande wenu wa chini unaelekea kwenye ufuo wa Bahari Nyekundu. Na lau kama mungalijaribu kuweka maelewano ya makutano hayo mungalitafautiana, lakini Mwenyezi Mungu Aliwakusanya bila kuagana ili Alipitishe jambo ambalo ililazimu lifanyike kwa kuwaokoa vipenzi Vyake na kuwadhalilisha maadui Wake kwa kuuawa na kushikwa mateka. Na hili lilifanyika ili apate kuangamia mwenye kuangamia kati yao kutokamana na hoja ya Mwenyezi Mungu iliyomthibitikia akaiyona na ikaondoa udhuru wake, na apate kuishi mwenye kuishi kutokamana na hoja ya Mwenyezi Mungu iliyomthibitikia na kujitokeza wazi kwake. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya makundi mawili hayo, hakifichiki Kwake chochote, ni Menye kuzijua nia zao.
Na kumbuka, ewe Nabii, pindi Mwenyezi Mungu Alipokuonyesha uchache wa maadui zako ukiwa usingizini na ukawajulisha Waumini kuhusu hilo, ndipo nyoyo zao zikapata nguvu na wakawa na ujasiri wa kupigana nao. Na kama Anagalikuonyesha Mola wako wingi wa maadui zako, basi wangalisita Maswahaba wako kupambana nao, na mungalipatwa na uoga na mkatafautiana kuhusu kupigana, lakini Mwenyezi Mungu Aliepusha jambo la nyinyi kushindwa na Akaokoa na mwisho mbaya wa hilo. Hakika Yeye ni Mjuzi mno wa yaliyofichika nyoyoni na maumbile ya nafsi.
Na kumbuka pia pindi walipojitokeza maadui kwenye ardhi ya mapigano mkawaona kuwa ni wachache mkawa na ujasiri juu yao, na Akawafanya nyinyi ni wachache kwenye macho yao, ili waache kujiandaa kupigana na nyinyi, ili Mwenyezi Mungu Alipitishe jambo ambalo hapana budi lifanyike, ili itimie ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu ya himaya na ushindi. Hapo likawa neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu, na neno la wale waliokanusha ndilo la chini, Na kwa Mwenyezi Mungu ndiko marudio ya mambo yote, Apate kumlipa kila mmoja kwa anachostahili kulipwa.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, mkutanapo na kundi la watu wa ukafiri wakawa wamejitayarisha kupigana na nyinyi, basi thibitini na msishindwe na wao na mumtaje Mwenyezi Mungu kwa wingi, hali ya kuomba na kunyenyekea, Awateremshie ushindi na uwezo wa kumshinda adui yenu, ili mufaulu.
Na mjilazimishe kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake katika hali zenu zote. Wala msitafautiane ikawa ni chanzo cha neno lenu kuwa mbalimabali na nyoyo zenu kutengana, mkaja kuwa madhaifu na nguvu zenu kuondoka na ushindi wenu; na subirini mnapokutana na adui. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kusubiri, kwa kuwasaidia, kuwapa ushindi na kuwapa nguvu, na Hatawaacha.
Na Msiwe kama mfano wa washirikina ambao walitoka nchini mwao kwa majivuno na kujionyesha ili wawazuie watu wasiingie kwenye dini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu kwa wanayoyafanya ni Mwenye kuyazunguka. Hakifichiki Kwake chochote.
Na kumbukeni pindi Shetani Alipowapambia washirikina yale waliyoyajia na waliyoyakusudia na akawaambia, «Hamuna yoyote Atakayewashinda leo, na mimi ni msaidizi wenu.» Basi yalipopambana makundi mawili: washirikina wakiwa pamoja na Shetani, na Waislamu wakiwa pamoja na Malaika, alirudi nyuma Shetani akaienda zake na akasema kuwaambia washirikina, «Mimi ni mwenye kujitenga na nyinyi; mimi nawaona Malaika msiowaona waliokuja kuwasaidia Waislamu. Hakika mimi namuogopa Mwenyezi Mungu.» Basi akawaacha na akajitenga nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwa aliomuasi na asitubiye toba ya kidhati.
Na kumbukeni waliposema watu wenye shaka na unafiki na wagonjwa wa nyoyo, huku wauona uchache wa Waislamu na wingi wa maadui wao, «Imewadanganya hawa Waislamu dini yao, ndipo ikawaingiza kwenye matatizo haya.» Na hawa wanafiki hawakuelewa kwamba mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu na akawa na uhakika wa ahadi Yake, basi Mwenyezi Mungu Hatamuacha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye ushindi, hakuna chochote kinachomshinda, ni Mwenye hekima katika uendeshaji Wake mambo na utengezaji Wake.
Na lau ingalionekana, ewe Mtume, hali ya Malaika ya kuzichukua roho za Makafiri na kuzitoa, na huku wao wanawapiga nyuso zao wakiwaelekea, na wanawapiga migongo yao wakiwakimbia na wanawaambia, «Onjeni adhabu inayounguza», ungaliona jambo kubwa. Na msururu huu wa maneno ingawa sababu yake ni vita vya Badr, lakini unakusanya hali ya kila kafiri.
Malipo hayo ambayo yamewapata nyinyi, enyi washirikina, ni kwa sababu ya matendo yenu maovu katika maisha yenu ya duniani. Na Mwenyezi Mungu hamdhulumu yoyote, kati ya viumbe Wake, kitu chochote hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo. Bali Yeye Ndiye Mwamuzi Muadilifu Asiyedhulumu.
Hakika yale yaliyowapata washirikina siku hiyo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu katika kuwatia adabu wakiukaji mipaka miongoni mwa umma waliotangulia, mfano wa Fir'awn na waliomtangulia, walipowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakazipinga aya Zake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Aliwateremshia mateso Yake kwa sababu ya madhambi yao. Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyeshindwa, ni Mkali wa mateso kwa aliyemuasi na asitubie kutokana na dhambi zake.
Malipo hayo maovu ni kwamba Mwenyezi Mungu pindi Anapowaneemesha watu neema yoyote, hawaondolei mpaka wabadilishe hali yao njema iwe mbovu, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua hali zao, kwa hivyo huwapitishia yale yaliyolingana na ujuzi Wake na matakwa Yake.
Hali ya Makafiri hawa ni kama hali ya Makafiri wa jamaa za Fir'awn ambao walimkanusha Mūsā, na ni kama hali ya wale waliowakanusha Mitume wao miongoni mwa watu waliopita. Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa sababu ya madhambi yao na Akawazamisha jamaa za Fir'awn baharini. Na kila umma kati yao walikuwa wanatenda mambo ambayo haikufaa wao kuyatenda, ya kukanusha kwao Mitume wa Mwenyezi Mungu na kupinga kwao aya za Mwenyezi Mungu na kushirikisha kwao, katika ibada, asiyekuwa Yeye.
Hakika wabaya mno wa wale wanaotembea juu ya ardhi mbele ya Mwenyezi Mungu ni Makafiri wanaoendeleza ukafiri; wao hawawaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu, hawaukubali upweke Wake wala hawazifuati sheria Zake.
Miongoni mwa wabaya hao ni Mayahudi ambao waliingia pamoja na wewe katika mapatano kwamba hawatakupiga vita wala hawatamsaidia yoyote dhidi yako, kisha wanazivunja ahadi zao mara kwa mara hali ya kuwa wao hawamuogopi Mwenyezi Mungu.
Pindi utakapopambana na hawa, wanaovunja ahadi na mapatano, katika vita, wape adhabu ambayo itatia kicho kwenye nyoyo za wegine na itaitawanya mikusanyiko yao, huenda wao wakazingatia wasiwe na ujasiri wa kufanya kama yale waliyoyafanya waliotangulia.
Na ukiogopa, ewe Mtume, hiana ambayo ishara zake zimejitokeza, kutoka kwa kundi lolote, basi watupilie mbali ahadi yao, ili zote pande mbili ziwe zimelingana kwa kujua kwamba hapana tena mapatano baada ya leo. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kuenda kinyume na ahadi zao, wavunjaji ahadi na mapatano.
Na wasidhanie wale ambao walizikanusha aya za Mwenyezi Mungu kwamba wao washapita na washaokoka na kwamba Mwenyezi Mungu Hawawezi; hakika wao hawatakwepa adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na Tayarisheni, enyi makundi ya Waislamu,ili kukabiliana na maadui wenu, chochote mkiwezacho cha wingi wa watu na zana, ili muingize, kwa hio, kicho katika nyoyo za maadui wa Mwenyezi mungu na maadui wenu wanaowavizia; na muwatishe wengine ambao uadui wao bado haujajitokeza kwenu hivi sasa, lakini Mwenyezi Mungu Anawajua na Anayajua yale ambayo wanayadhamiria. Na mali yoyote na vinginevyo mnavyovitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, vingi au vichache, Mwenyezi Mungu Atawapa badala yake duniani na Atawaekea thawabu zake mpaka Siku ya Kiyama; na nyinyi hamtapunguziwa malipo ya hayo chochote.
Na wakielekea kuacha vita na wakapendelea kuishi kwa amani na nyinyi, basi nawe elekea huko, ewe Nabii, na uyategemeze mambo yako kwa Mwenyezi Mungu na uwe na imani na Yeye. Hakika Yeye Ndiye Mwenye kuyasikia maneno yao, Mwenye kuzijua nia zao.
Na pindi wakitaka kukufanyia njama, Mwenyezi Mungu Atakukinga na udanganyifu wao. Yeye Ndiye Aliyekuteremshia ushindi na Akakutia nguvu kwa Waumini miongoni mwa Muhājirūn (waliohamia Madina kutoka Maka) na Anṣār (wenyeji wa Madina)
na Akaziweka pamoja nyoyo zao baada ya utengano, lau ungalitoa mali yaliyoko duniani kote hungaliweza kuziweka pamoja, lakini Mwenyezi Mungu Aliziweka pamoja juu ya Imani wakawa ni ndugu wanaopendana. Hakika Yeye ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwenye hekima katika mambo Yake na uendeshaji Wake.
Ewe Nabii, hakika Mwenyezi Mungu Atakukinga wewe na Atawakinga wale walio pamoja na wewe shari ya maadui wenu.
Ewe Nabii, wahimize wanaokuamini kupigana vita. Iwapo watapatikana kati yenu watu ishirini wenye kusubiri kwenye kipindi cha kupambana na adui, watawashinda watu mia mbili kati yao. Na iwapo watapatikana kati yenu wapiganaji jihadi mia moja wenye subira, watawashinda Makahri elfu moja, kwa kuwa wao ni watu wasiokuwa na ujuzi na ufahamu wa yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaandalia wapiganaji jihadi katika njia Yake; kwani wao wapigania utukufu katika ardhi na kufanya uharibifu ndani yake.
Sasa hivi Mwenyezi Mungu Amewapunguzia, enyi Waumini, kwa udhaifu mlio nao. Basi ikiwa watakuwako miongoni mwenu watu mia moja wenye subira, watawashinda Makafiri mia mbili. Na iwapo watakuwako kati yenu watu elfu moja, watawashinda watu elfu mbili kati yao kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye subira kwa msaada Wake na nusura Yake.
Haifai kwa Nabii awe na mateka miongoni mwa maadui wake mpaka aue kwa wingi, ili kutia kicho ndani ya nyoyo zao na aimarishe misingi ya Dini. Mnataka, enyi mkusanyiko wa Waislamu, kwa kuchukuwa kwenu fidia kutoka kwa mateka wa vita vya Badr, starehe ya ulimwenguni, na Mwenyezi Mungu Anataka kuikuza dini Yake ambayo kwayo hupatikana Akhera. Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake.
Lau si Kitabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu chenye mapitisho na Makadirio yaliyotangulia ya kuhalalisha ngawira na kukomboa mateka kwa umma huu, basi ingaliwapata adhabu kubwa kwa kuchukuwa kwenu ngawira na fidia kabla ya kuletwa sheria kuhusu mambo mawili hayo.
Basi kuleni mlichokipata katika ngawira na fidia ya mateka, kwani hiyo ni halali nzuri. Na jilazimisheni na hukumu za Mwenyezi Mungu na sheria Zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye huruma nao.
Ewe Nabii, waambie mliowateka siku ya vita vya Badr, «Msisikitike juu ya fidia iliyochukuliwa kutoka kwenu. Iwapo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Atajua kwamba kwenye nyoyo zenu pana wema, basi Atawapa kilicho bora zaidi kuliko mali yaliyochukuliwa kutoka kwenu, kwa kuwarahisishia nyinyi, kwa hisani Yake, wema mwingi - Mwenyezi Mungu Alitekeleza ahadi Yake kwa 'Abbas, Mwenyezi Mungu Awe radhi naye, na wengineo- na Atawasamehe madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha wa madhambi ya waja Wake wanapotubia, ni Mwenye huruma kwao.
Na wakitaka kukwendea kinyume mara nyingine, wale uliowaacha huru miongoni mwa mateka, basi usikate tamaa. Kwani wao tangu hapo walikuwa wamefanya uhaini kwa Mwenyezi Mungu na wakakupiga vita., na Mwenyezi Mungu Akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani, ni Mwenye hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake.
Hakika wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata sheria Zake kivitendo, wakahama kwenda kwenye Nyumba ya Uislamu au nchi ambayo wataweza hapo kumuabudu Mola wao, wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali na nafsi, na Wale ambao waliowaweka Wahamiaji katika nyumba zao, wakawaliwaza kwa mali yao nawakaitetea dini ya Mwenyezi Mungu, hao ni wenye kusaidiana wao kwa wao. Ama wale walioamini na wasigure kutoka kwenye Nyumba ya ukafiri, basi nyinyi hamlazimishwi kuwahami na kuwatetea mpaka watakapogura. Na wakifanyiwa maonevu na Makafiri na wakataka msaada wenu, basi wakubalieni, isipokuwa iwapo ni dhidi ya watu ambao kuna makubaliano ya mkazo baina yenu na wao na hawajayavunja. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu, Atamlipa kila mtu kwa kadiri ya nia yake na tendo lake.
Na wale waliokanusha, ni wenye kusaidiana wao kwa wao. Na iwapo hamtakuwa, enyi Waumini, ni wenye kusaidiana nyinyi kwa nyinyi, basi kutapatikana katika ardhi kufitiniwa Waumini na dini ya Mwenyezi Mungu na uharibifu mkubwa wa kuzuiwa njia ya Mwenyezi Mungu na kutiwa nguvu misingi ya ukafiri.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wakaacha majumba yao wakaelekea Nyumba ya Uislamu au kwenye nchi ambayo ndani yake watapata utulivu wa kumuabudu Mola wao, wakapigana jihadi kwa kulikuza neno la Mwenyezi Mungu, na wale waliowahami ndugu zao Muhājirūn, wakawapa Makao na wakawaliwaza kwa mali na kwa kuwapa nguvu. Hao basi ndio Waumini wakweli kidhati. Watapata msamaha wa madhambi yao na riziki njema iliyo kunjufu katika mabustani ya Pepo ya starehe.
Na wale walioamini, baada ya hawa Muhājirūn na Anṣār, wakagura na wakapigana jihadi pamoja na nyinyi katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi hao ni katika nyinyi, enyi Waumini; wana haki mlizonazo nyinyi na wana majukumu mliyonayo. Na wenye ujamaa, kwenye hukumu ya Mwenyezi Mungu, baadhi yao wanapewa kipaumbele kwa wengine katika kurithiana kuliko Waislamu wa kawaida. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, Anayajua yanayowafaa waja Wake kuhusu kurithiana wao kwa wao kwa ujamaa na nasaba na kutorithiana kwa mapatano ya kujihami na yasiyokuwa hayo miongoni mwa yale yaliyokuwa mwanzo wa Uislamu.