ترجمة سورة الأعلى

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الأعلى باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Takasa Jina la Mola wako Aliyetukuka na kuepukana na mshirika na kila sifa pungufu kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake na utakatifu Wake.
Aliyeumba viumbe Akalitengeneza umbo lao na kulifanya zuri.
Na Aliyekadiria kila kitu na kukipeleka njia inayonasibiana nacho.
Na Aliyeotesha nyasi mbiti zenye rangi ya kijani,
Akazifanya baadaye kuwa kavu zilizobadilika rangi.
Tutakusomea, ewe Mtume, hii Qur’ani kisomo ambacho hutakisahau.
Isipokuwa iwapo Mwenyezi Mungu Ataka usahau kwa hekima na maslahi anayoyajua Yeye. Kwani Yeye ni Mjuzi wa yaliyo wazi na yaliyofichika, ya maneno na ya vitendo.
Tutakufanyia mapesi mambo yako yote; miongoni mwayo ni kukusahilishia kubeba majukumu ya utume na kuifanya nyepesi Dini uliyokuja nayo.
Basi wawaidhie kaumu zako, ewe Mtume, kwa namna tulivyokutayarishia ufanye kwenye wahyi ulioletewa, uwaongoze njia yenye kheri na wao na uwahusu kwa mawaidha yako wale wanaotarajiwa kuwaidhika nayo. Wala usijisumbue kuwashauri wale ambao mawidha hayawaathiri isipokuwa kuwatia ujeuri na kuwafanya wayakimbie.
Atanufaika kwa mawaidha anayemcha Mola wke,
na atajiepusha na mawaidha aliye mbaya asiyemuogopa Mola wake
atakayeingia kwenye Moto wa Jahanamu akiadhibika kwa ukali wake.
Kisha hatakuwa ni mwenye kufa akapumzika wala ni mwenye kuishi akanufaika.
Hakika amefuzu mwenye kuisafisha nafsi yake na tabia mbovu,
na akamtaja Mwenyezi Mungu, akampwekesha, akamuomba, akafanya vitendo vya kumridhisha na akasimamisha Swala kwa nyakati zake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kufuata sheria Aliyoiweka.
Hakika yenu, nyinyi watu, mnafadhilisha pambo la maisha ya kilimwengu juu ya starehe za Akhera.
Na hakika ya mambo ni kuwa nyumba ya Akhera na starehe zake ni bora zaidi kuliko ulimwngu na ni yenye kusalia zaidi.
Haya mlioosimuliwa ndani ya Sura hii ni miongoni mwa yaliyotajwa kimaana katika Kurasa zilizotangulia kuteremshwa kabla ya Qur’ani.
Nazo ni Kurasa za Ibrāhīm na Mūsā, amani ziwashukie.
Icon