ترجمة سورة السجدة

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة السجدة باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

«Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwazo wasua ya Al-Baqarah.
Hii Qur’ani aliyokuja nayo Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, haina shaka kuwa imeteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote.
Kwani je, wanasema washirikina kuwa Muhammad Ameizua Qur’ani? Wamesema urongo, bali hiyo Qur’ani ndiyo ukweli uliothibiti ulioteremshwa kwako, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako, ili uwaonye nayo watu ambao hawakujiwa na muonyaji kabla yako wewe, huenda wao wakaongoka: wakaijua haki, wakaiamini, wakaitanguliza na wakakuamini wewe.
Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye aliumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa Siku sita kwa hekima Anayoijua. Na Yeye ni Muweza wa kuziumba kwa neno «Kuwa» na likawa, kisha Akalingana, Kutakasika na kuwa juu ni Kwake - nako ni kuwa juu na kunyanyuka- juu ya ‘Arsh Yake , kulingana kunakonasibiana na utukufu Wake, hakusemwi kuko namna gani wala hakufananishwi na vile binadamu wanavyolingana. Hamna nyinyi, enyi watu, mtegemewa wa kumtegemezea mambo yenu, au muombezi wa kuwaombea nyinyi mbele ya Mwenyezi Mungu, ili muokoke na adhabu Yake. Basi kwani nyinyi hamwaidhiki na mkafikiria, enyi watu, mkampwekesha Mwenyezi Mungu kwa uungu na mkamtakasia ibada?
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaendesha mambo ya viumbe kutoka mbinguni hadi ardhini, kisha mambo hayo yanapanda kwa Mwenyezi Mungu pamoja na mapelekesho kwa kipindi cha siku moja ambayo kadiri yake ni miaka elfu moja ya siku za duniani mnazozihesabu.
Huyo Muumbaji Mwenye kuendesha mambo ya viumbe ni Mjuzi wa kila kinachofichamana na macho, miongoni mwa mambo yanayohifadhiwa na vifua na kufichwa na nafsi, na ni Mjuzi wa vitu vinavyoonekana na macho, na Yeye Ndiye Mwenye nguvu, Ndiye Mwenye kushinda Asiyeshindwa, Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake Waumini.
Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye Ametengeneza uumbaji wa kila kitu, na Alianza kumuumba binadamu, naye ni Ādam, kwa udongo.
Kisha Akavifanya vizazi vya Ādam vizalikane na tone dhaifu lililo dogo na twevu.
Kisha Aliukamilisha uumbaji wa binadamu na Akaufanya upendeze na Akalifanya zuri umbo lake, na Akapuliza ndani yake roho Yake kwa kumtuma Malaika kwake ili apulize roho, na Akawapa nyinyi, enyi watu, neema ya masikizi na maangalizi ya kupambanua sauti, rangi, vitu na watu, na neema ya akili ya kupambanua jema na baya na lenye kunufaisha na kudhuru. Ni kuchache kule kumshukuru kwenu Mola wenu kwa neema Alizowapatia.
Na wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu wenye kukanusha kufufuliwa wamesema, «Je, itakapokuwa mchanga nyama yetu na mifupa yetu, je, tutafufuliwa tuwe umbo lingine?» huku wakiona kuwa hilo liko mbali kutokea na huku hawataki kuifikia haki. Na hilo kwao ni udhalimu na ushindani, hii ni kwamba wao wanakanusha kukutana na Mola wao Siku ya Kiyama.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Atakayewafisha nyinyi ni Malaika wa kifo aliyewakilishwa kwenu, atakayezichukua roho zenu utakapokoma muda wenu wa kuishi, na hamtachelewa hata nukta moja, kisha mtarudishwa kwa Mola wenu, Awalipe kwa matendo yenu, yakiwa ni mema Awalipe wema na yakiwa maovu Awalipe uovu.
Na lau ungaliona, ewe mhutubiwa, pindi wahalifu waliokanusha kufufuliwa wakiwa wameviinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao kutokana na hizaya na aibu huku wanasema, «Mola wetu! Tumeyaona machafu yetu na tumesikia kutoka kwako ukweli wa yale waliokuwa Mitume wako wakituamrisha duniani, na tumeshatubia kwako, basi turudishe duniani ili tufanye matendo ya utiifu kwako. Sisi tushayaamini sasa yale tuliokuwa tukiyakanusha ya kuwa wewe ni mmoja na kwamba wewe utawafufua walio makaburini. Na lau ungaliyaona, ewe mhutubiwa, haya yote ungaliona jambo kubwa na janga zito.
Na lau tungalitaka tungaliwapa washirikina hawa uongofu wao na Angaliwaonyesha njia ya Imani, lakini limethibiti neno linalotoka kwangu na limepasa kwamba nitaujaza, moto wa jahanamu, watu wote wa aina mbili, ya kijini na kibanadamu, wenye kukufuru na kuasi, kwa kuwa walichagua upotevu na kuacha uungofu.
Wataambiwa washirikina hawa kwa njia ya kulaumiwa, watakapoingia Motoni, «Basi onjeni adhabu kwa sababu ya kughafilika kwenu na Akhera na kujiingiza kwenu kwenye ladha za dunia, sisi tutawaacha kwenye adhabu leo, na onjeni adhabu ya moto wa Jahanamu isiyomalizika kwa yale mliokuwa mkiyafanya duniani ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na kumuasi.»
Kwa kweli, wanaoziamini aya za Qur’ani na kuzifuata kivitendo ni wale ambao wanapowaidhiwa nazo au wanaposomewa, wanamsujudia Mola wao kwa kumnyenyekea na kumtii na wanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsifu katika kusujudu kwao, na hali wao hawaoni kiburi wakaacha kumsujudia na kumtakasa na kumuabudu Yeye Peke Yake Asiyekuwa na mshirika.
Mbavu za hawa wanaoziamini aya za Mwenyezi Mungu zinajiepusha na magodoro ya kulalia, wakiswali kwa Mola wao swala ya usiku, wakimuomba kwa kuogopa adhabu na kutarajia malipo mema, na katika kile tulichowaruzuku wanatumia katika kumtii Mwenyezi Mungu na katika njia Yake.
Hakuna nafsi yoyote inayoyajua yale aliyowawekea Mwenyezi Mungu hawa Waumini ya kutuliza macho na kufurahisha moyo, yakiwa ni malipo yao kwa matendo yao mema.
Je, Yule Aliyekuwa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mwenye kuamini agizo lake la kuwalipa mema wema wenye kufanya mema na kuwalipa ubaya wenye kufanya mabaya, ni kama yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Yake na akaikanusha Siku ya Kiyama? Hawalingani mbele ya Mwenyezi Mungu.
Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na wakayafanya yale waliyoamrishwa kwayo, basi malipo yao ni mabustani ya Pepo watashukia huko na watakaa kwenye starehe zake wakiandaliwa, yakiwa malipo yao kwa yale waliokuwa wakiyafanya ulimwenguni ya utiifu Kwake.
Na ama wale waliotoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo ya kumuasi, basi mahali pao pa kutulia ni moto wa Jahanamu, kila wakitaka kutoka wanarudishwa ndani. Na wataambiwa, kwa kulaumiwa na kukaripiwa, «Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkiikanusha ulimwenguni.»
Na tutawaonjesha, tena tutawaonjesha, hawa waasi wenye kukanusha adhabu ndogo ya matatizo, shida na misiba ya duniani kabla ya adhabu kubwa zaidi Siku ya Kiyama, ambako wataadhibiwa ndani ya moto wa Jahanamu, huenda wao wakarejea na wakatubia dhambi zao kwa Mola wao.
Hakuna hata mmoja aliye dhalimu zaidi wa nafsi yake kuliko yule aliyekumbushwa dalili za Mwenyezi Mungu kisha akazipa mgongo zote, asiwaidhike kwa mawaidha yake, bali akayafanyia kiburi. Hakika sisi ni wenye kuwatesa wale wahalifu waliozipa mgongo aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake na wasinufaike nazo.
Hakika tulimletea Mūsā Taurati kama tulivyokuletea wewe, ewe Mtume, Qur’ani. Basi usiwe na shaka ya kukutana na Mūsā usiku wa Isrā’ (safari ya kwenda Bayt al- Maqdis) na Mi’rāj (safari ya kwenda mbinguni), na tukaifanya Taurati ni uongofu kwa Wana wa Isrāīl, Unawalingania kwenye haki na kwenye njia iliyonyoka.
Na tuliwafanya, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, ni waongozi na walinganizi kwenye wema, watu wanawafuata na wao wanawalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake na kumtii. Na walipata daraja hii ya juu waliposubiri juu ya amri za Mwenyezi Mungu, kuyaacha makemeo Yake na kuwalingania na kuvumilia makero katika njia Yake, na walikuwa wanaziamini kikweli aya za mwenyezi Mungu na hoja Zake.
Hakika Mola wako, ewe Mtume, Atatoa uamuzi baina ya Waumini na makafiri miongoni mwa Wana wa Isrāīl na wasiokuwa wao Siku ya Kiyama kwa uadilifu katika yale waliotafautiana juu yake miongoni mwa mambo ya dini, na Atamlipa kila binadamu kwa matendo yake kwa kuwatia watu wa Peponi Peponi na watu wa Motoni Motoni.
Kwani haikuwabainikia hawa wenye kumkanusha Mtume ni mara ngapi tuliwaangamiza ummah waliotangulia kabla yao na huku wanatembea kwenye makazi yao, wakawa wanayaona waziwazi, kama vile watu wa Hūd, Ṣāliḥ na Lūṭ? Hakika katika hayo kuna alama na mawaidha ya kutolea ushahidi ukweli wa Mitume waliowajia na urongo wa ushirikina walionao. Basi kwani hawasikii, hawa wenye kuwakanusha Mitume, mawaidha ya Mwenyezi Mungu na dalili Zake wakapata kunufaika nayo?
Kwani hawakuona wenye kukanusha kufufuliwa baada ya kufa kwamba sisi tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu iliyo ngumu ambayo haina mimea, tukatoa kwa maji hayo mimea yenye rangi mbalimbali yenye kuliwa na wanyama wao na miili yao ikapata chakula cha kuwafanya wao waishi kwayo? Kwani hawazioni neema hizi kwa macho yao wakajua kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwahuisha wafu na kuwafufua kutoka makaburini mwao?
Hawa washirikina wanaifanyia haraka adhabu, wanasema, «Ni lini hukumu hii ya kutuadhibu, kama mnavyodai, ambayo itaamua baina yetu na nyinyi, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu?»
Waambie, ewe Mtume, «Siku ya hukumu ambayo mtateswa na mtashuhudia kifo, makafiri hakutawafaa kuamini kwao, wala hawatacheleweshwa ili watubie na warudie.»
Basi wape mgongo, ewe Mtume, hawa washirikina, na usiujali ukanushaji wao, na ungojee vile Mwenyezi Mungu Atawafanya. Hakika wao ni wenye kungojea na kutaraji mpatikane na ubaya. Basi Mwenyezi Mungu Atawapa hizaya na Atawadhalilisha na Akupe ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu Ashalifanya hilo, sifa njema ni Zake na wema ni Wake.
Icon