ﰡ
Shukrani ni za Mwenyezi Mungu kwa sifa Zake ambazo zote ni sifa za ukamilifu, na kwa neema Zake za nje na za ndani za kidini na za kidunia, Ambaye Ana ufalme wa vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na ni Zake Yeye sifa njema zilizotimia huko Akhera, na Yeye Ndiye Mwenye hekima katika matendo Yake, Aliye Mtambuzi wa mambo ya viumbe Vyake.
Anakijua kila kinachoingia ardhini miongoni mwa matone ya maji na kinachotoka humo miongoni mwa mimea, madini na maji, na kinachoshuka kutoka juu miongoni mwa mvua, Malaika na Vitabu, na vinavyopanda huko miongoni mwa Malaika na matendo ya waja. Na Yeye Ndiye Mwenye kuwarehemu waja Wake, Hawaharakishii mateso wale wenye kuasi kati yao, ni Mwingi wa msamaha wa dhambi za wenye kutubia Kwake, wenye kujitegemeza Kwake.
Na makafiri wenye kukanusha kufufuliwa walisema. «Kiyama hakitatujia.» Sema, ewe Mtume, uwaambie, «Kwani! Ninaapa kwa Mola wangu, kitawajia! Lakini hakuna yoyote anayejua wakati wa kuja kwake isipokuwa Mwenyezi Mungu, Mjuzi wa visivyoonekana, Ambaye haufichamani Kwake uzito wa kadiri ya chungu mdogo uliyo mbinguni au ardhini, hata mdogo zaidi kuliko huo na hata mkubwa, isipokuwa uko kwenye Kitabu kilichotunzwa, nacho ni Ubao Uliohifadhiwa.
Ili Awalipe mema wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakamfuata Mtume Wake na wakafanya matendo mema, hao watakuwa na msamaha wa dhambi zao na riziki njema, nayo ni Pepo.»
Na wale wanaotembea katika kuizuia njia ya Mwenyezi Mungu, kuwakanusha Mitume Wake na kuzitangua aya zetu huku wakiteta na Mwenyezi Mungu wakipinga amri Zake, hao watakuwa na adhabu mbaya zaidi na yenye ukali mwingi zaidi.
Na wale waliopatiwa elimu wanajua kwamba Qur’ani uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako ndiyo haki na kwamba inaongoza kwenye njia ya Mwenyezi Mungu, Aliye Mshindi Asiyeshindwa wala kuzuiliwa, bali Amekitendesha nguvu kila kitu na Amekishinda, Ndiye Mwenye kusifiwa katika maneno Yake, matendo Yake na Sheria Zake.
Na makafiri wanasema, wakiambiana wao kwa wao kwa njia ya shere, «Je, tuwaoneshe mtu ( wakimkusudia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie) atakayewaambia kwamba nyinyi mkifa na miili yenu ikawa mbalimbali kabisa kuwa nyinyi mtahuishwa na mtafufuliwa kutoka makaburini mwenu» wanasema hayo kwa kupita kiasi katika kukanusha kwao.
Kwani mtu huyu amemzulia Mwenyezi Mungu urongo, au ana wazimu na kwa hivyo anasema jambo asilolijua? Mambo si vile kama wanavyosema makafiri, bali Muhammad ni mkweli wa wakweli. Na wale wasioamini kufufuliwa na wasiofanya matendo ya kuwafaa huko, watakuwa kwenye adhabu ya milele huko Akhera, na wako kwenye upotevu wa mbali hapa duniani.
Kwani hawaoni makafiri hawa wasioamini Akhera ukubwa wa uweza wa Mwenyezi Mungu juu ya vilivyoko mbele yao na nyuma yao, miongoni mwa mbingu na ardhi, vinavyoshangaza akili, na kwamba viwili hivyo vimewazunguka? Tutakapo tutawazamisha ndani ya ardhi, kama tulivyomfanyia Qārūn, au tutawateremshia vipande vya adhabu, kama tulivyowafanyia watu wa Shu'ayb, kwa hakika mbingu iliwanyeshea moto ukawaunguza. Hakika katika hilo tulilolitaja la uwezo wetu kuna ushahidi wazi kwa kila mja mwenye kurudi kwa Mola wao kwa kutubia, mwenye kukubali upweke Wake na mwenye kumtakasia ibada.
Hakika tulimpa Dāwūd unabii, Kitabu na ujuzi, na tukayaambia majabali na ndege, «Takaseni pamoja naye!» (Dāwūd anapomtakasa Mwenyezi Mungu kwa kuleta tasbihi, fanyeni hivyo pamoja naye). Na tulimlainishia chuma kikawa ni kama unga uliokandwa, anakisinyanga anavyotaka.
(Na tulikwambia, ewe Dāwūd,) «Tengeneze nguo za chuma zilizotimia na zilizo pana, na ukadirie vipimo vya misumari katika vikuku vya kuunganisha nguo hizo za chuma, na usikifanye kikuku kuwa kidogo kwani kitakuwa dhaifu, na kwa hivyo hizo nguo za chuma hazitaweza kumkinga (mwenye kuzivaa). Na usizifanye kubwa zikawa nzito kwa mwenye kuzivaa. Na ufanye, ewe Dāwūd, wewe na watu wako, vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, kwani mimi kwa mnayoyafanya ni Mwenye kuyaona, hakifichamani kwangu kitu chochote katika hivyo.»
Na tulimdhalilishia Sulaymān upepo, ukawa unatembea kutoka mwanzo wa mchana mpaka katikati yake mwendo wa mwezi, na kutoka katikati ya mchana mpaka usiku mwendo wa mwezi kwa mwendo wa kawaida. Na tulimyayushia shaba ikawa inatiririka kama vile maji yanavyotiririka, akawa anafanya kwa shaba hiyo anachotaka. Na tulimdhalilishia miongoni mwa majini wenye kutumika mbele yake, na yoyote kati yao anayesita kufuata amri yetu tuliomuamrisha ya kumtii Sulaymān tutamuonjesha kutokana na adhabu ya Moto unaowaka.
Majini wanamfanyia Sulaymān anachotaka miongoni mwa misikiti ya ibada, picha za shaba na ukoa, madishi makubwa kama mabirika ya kukusanyika maji ndani yake na vyungu vilivyojikita visivyotikisika kutoka mahali pake kwa ukubwa wake, na tukasema, «Enyi jamii ya Dāwūd! Fanyeni kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kile Alichowapa, kwa kumtii na kufuata amri Yake.» Na ni wachache, miongoni mwa waja wangu, wenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na Dāwūd, yeye na jamii yake, alikuwa miongoni mwa hao wachache.
Tulipopitisha kuwa Sulaymān afe, hakuna kilichowafahamisha majini juu ya kifo chake isipokuwa mchwa kuila fimbo yake ambayo alikuwa ameitegemea, basi Sulaymam akaanguka chini, na hapo majini wakajua kwamba wao lau walikuwa wanajua ghaibu hawangalikaa kwenye adhabu yenye kudhalilisha na kazi ngumu kumfanyia Sulaymān, kwa wao kudhania kuwa yeye ni katika walio hai. Katika hii aya kuna kubatilisha itikadi ya baadhi ya watu kwamba majini wanayajua yasiyoonekana. Kwani lau wao wangaliyajua yasiyoonekana wangalijua kifo cha Sulaymān, amani imshukie, na hawangalikaa kwenye adhabu yenye kunyongesha.
Kwa hakika, kabila la Saba’ la huko Yaman, kwenye makazi ya watu wake kuna dalili ya uweza wetu: mabustani mawili kuliani na kushotoni, «Kuleni riziki ya Mola wenu na mumshukuruni kwa neema Zake juu yenu, kwani nchi yenu ina mchanga bora na hewa nzuri, na Mola wenu ni Mwingi wa msamaha kwenu.»
Wakaipa mgongo amri ya Mwenyezi Mungu, wakaacha kumshukuru na wakawakanusha Mitume, tukawatumia mafuriko yenye kubomoa yaliyo na nguvu, yaliyoliharibu bwawa la maji na yakayazamisha mabustani. Na tukawageuzia mabustani yao mawili yenye kutoa matunda yakawa ni mabustani mawili yenye miti michache ya khamṭ, nayo ni miti ya matunda machungu yenye ladha ya kuchukiza, na athl, nayo ni miti inayofanana na ṭarfā ’isiyokuwa na matunda, na mikunazi michache yenye miba mingi.
Mabadiliko hayo, kutoka kwenye mambo mazuri kwenda kwenye mabaya, ni kwa sababu ya kukanusha kwao na kutoshukuru kwao neema za Mwenyezi Mungu. Na hatumtesi mateso haya makali isipokuwa mkanushaji sana aliyeendelea kwenye ukanushaji; atalipwa kulingana na matendo yake, sawa kwa sawa.
Na tulijaalia, baina ya watu wa Saba’ na hali wao wako Yaman, na ile miji tuliobarikia, nayo ni Shām, kuwe na miji iliyoshikana, aliye kwenye mji wowote kati ya hiyo huuona mji mwingine. Na tukafanya mwendo wa kutembea humo ni mwendo uliokadiriwa, kutoka nyumba hadi nyumba, bila mashaka, na tukawaambia, «Endeni kwenye miji hiyo , wakati mnapotaka wa usiku au mchana, mkiwa mko kwenye amani hamuogopi adui, njaa wala kiu.
Kwa sababu ya kuruka mipaka kwao, walichoka na raha na amani na maisha ya neema na wakasema, «Mola wetu! Ifanye miji yetu iwe mbali mbali ili safari zetu zirefuke baina ya miji hiyo, tusipate mji ulioimarika njiani tunapokwenda.» Na wakajidhulumu nafsi zao kwa kukanusha kwao, na kwa hivyo tukawaangamiza na tukawafanya ni mazingatio na mazungumzo kwa wanaokuja baada yao, na tukawatenganisha kila namna ya kuwatenganisha, na miji yao ikawa magofu. Kwa hakika yale yaliyoikumba Saba’ ni mazingatio kwa kila mwingi wa uvimilivu juu ya shida na mambo magumu, mwingi wa kushukuru neema za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Na kwa hakika alidhani Iblisi dhana isiyo ya ukweli kuwa atawapoteza wanadamu na kwamba wao watamtii yeye katika kumuasi Mwenyezi Mungu, na dhana yake kwao ikawa ya kweli, kwa kuwa wao walimtii yeye na wakamuasi Mola wao , isipokuwa kundi la wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, kwani wao walijikita kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu.
Na wala hakuwa iblisi na uwezo wa kuwalazimisha wakanushaji kukufuru, lakini hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha awapambie wanadamu ili ujitokeze ujuzi Wake wa kale tupate kumpambanua anayeamini kufufuliwa, thawabu na adhabu na kumtenganisha na yule mwenye shaka na hilo. Na Mola wako ni Mtunzi wa kila jambo, Analihifadhi na kutoa malipo yake.
Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina, «Waiteni wale ambao mlidai kuwa wao ni washirika wa Mwenyezi Mungu mkawaabudu badala Yake , miongoni mwa masanamu , malaika na binadamu, na wakusudieni katika haja zenu. Kwani wao hawatawaitika. Wao hawamiliki chochote, mbinguni wala ardhini, hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo, na wala hawana ushirika katika hizo mbili. Na hakuna yoyote miongoni mwa hawa washirikina mwenye kumsaidia kuumba chochote. Bali Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, ndiye Aliyepwekeka kwa upatishaji.Yeye Ndiye Anayeabudiwa Peke Yake, na hakuna mwingine yoyote asiyekuwa Yeye anayestahiki kuabudiwa.
Na maombezi ya mwenye kuombea hayafal kitu hayanufaishi mbele Yake, isipokuwa kwa yule Aliyemruhusu. Na miongoni mwa utukufu Wake na utisho Wake, Aliyeshinda na kutukuka, ni kuwa Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Anapotamka wahyi na watu wa mbinguni wakayasikia maneno Yake, wanakuwa katika hali ya kutetemeka kwa utisho, mpaka wanakuwa katika hali kama ile ya kukosa fahamu. Na kibabaiko kinapowaondokea kwenye nyoyo zao wanaulizana wao kwa wao, «Amesema nini Mola wenu?» Malaika watasema, «Amesema kweli! Na Yeye Yuko juu kwa dhati Yake, utendaji nguvu Wake na utukufu wa cheo Chake, Aliye Mkubwa juu ya kila kitu.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Ni nani anayewaruzuku kwa mvua kutoka mbinguni, na kwa mimea na madini na vinginevyo kutoka ardhini?» Hivyo basi hawana budi kukubali kuwa Yeye ni Mwenyezi Mungu. Na iwapo hawatakubali hilo, waambie, «Mwenyezi Mungu Ndiye Mwingi wa kuruzuku, na kwa hakika mojawapo wa mapote mawili, kati ya sisi na nyinyi, limejikita kwenye uongofu au limevama kwenye upotevu ulio wazi.»
Sema, «Hamtaulizwa kuhusu dhambi zetu, wala hatutaulizwa kuhusu matendo yenu, sababu sisi tumejitenga na nyinyi na ukanushaji wenu.»
Sema, «Mola wetu Atatukusanya baina yetu na nyinyi Siku ya Kiyama, kisha Atatoa uamuzi wa uadilifu baina yetu. Na Yeye Ndiye Mfunguzi Mwenye kutoa uamuzi baina ya viumbe Vyake, Mwingi wa ujuzi wa yale yanayotakikana yatolewe uamuzi na hali ya viumbe Vyake. Hakuna kinachofichicana Kwake chochote.»
Sema, «Nionesheni kwa hoja na dalili wale mliomshikanisha na Mwenyezi Mungu mkawafanya ni washirika Wake katika kuabudiwa, je wao wameumba chochote? Mambo si kama walivyoeleza.Bali Yeye Ndiye Mwenye kuabudiwa kwa haki, ambaye hana mshirika wake, aliye Mshindi katika kuwatesa waliomshirikisha, na mwenye hekima katika maneno Yake, vitendo Vyake na upelekeshaji mambo ya viumbe Vyake.
Na hatukukutumiliza, ewe Mtume, isipokuwa ni kwa watu wote, uwabashirie malipo mema ya Mwenyezi Mungu na uwaonye mateso Yake. Lakini wengi wa watu hawaijui haki, hivyo basi wao wanaipa mgongo.
Na hawa washirikina wanasema kwa njia ya shere, «Ni lini wakati wa Ahadi hii ambayo unatuahidi kuwa Mwenyezi Mungu Atatukusanya ndani yake kisha Ahukumu baina yetu, iwapo nyinyi ni wakweli katika kile mlichotuahidi kwacho?»
Waamnbie, ewe Mtume, «Nyinyi muna maagano ambayo hapana budi yatawajia, nayo ni maagano ya Siku ya Kiyama, hamtachelewa nayo hata muda mchache wa kupata kutubia, na wala hamtatangulia mbele yake mkaadhibiwa hata kwa muda mchache. Basi jihadharini na Siku hiyo na jitayarisheni kwa vifaa vyake.»
Na waliokanusha walisema, «Hatutaiamini hii Qur’ani wala vile vilivyoitangulia, kina Taurati, Injili na Zaburi.» Kwa hakika washakanusha vitabu vyote vya Mwenyezi Mungu. Na lau utaona pindi madhalimu wamefungwa mbele ya Mola wao ili wahesabiwe, huku wakirudishiana maneno baina yao, kila mmoja anamtupia lawama mwingine, utaona jambo la kutisha! Watakuwa waliokuwa wakifanywa wanyonge wakisema kuwaambia wale waliokuwa na kiburi, nao ni wale viongozi na wakubwa waliopotea na kupoteza, «Lau si nyinyi kutupoteza njia tungalikuwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.»
Viongozi watasema kuwaambia wale waliofanywa wanyonge, «Kwani ni sisi tuliowazuia uongofu baada ya kuwajia? Bali ni nyinyi wenyewe mlikuwa wahalifu kwa kuwa mliingia kwenye ukafiri kwa matakwa yenu na hiyari yenu.»
Watasema waliofanywa wanyonge kuwaambia wakubwa wao katika upotevu, «Bali ni kule kutupangia kwenu ubaya usiku na mchana ndiko kulikotutia sisi katika majanga. Kwa kuwa mlikuwa mkitutaka tumkanushe Mwenyezi Mungu na tumfanye kuwa ana washirika katika kuabudiwa.» Na watu wa kila mojawapo ya makundi mawili wataficha majuto watakapoiona adhabu ilioandaliwa wao. Na tutaweka minyororo kwenye shingo za wale waliokanusha. Na wao hawatateswa kwa adhabu hii isipokuwa ni kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu na kufanya kwao matendo mabaya duniani. Katika hii aya kuna onyo kali dhidi ya kuwafuata walinganizi wa upotevu na viongozi wa ukiukaji Sheria.
Na hatukutumiliza Mtume yoyote katika mji wowote alinganie kwenye kumwahidisha Mwenyezi Mungu na kumpwekesha katika ibada, isipokuwa wale wenye kuvama kwenye starehe na matamanio miongoni mwa watu wake huwa wakisema, «Hakika sisi kwa haya mliokuja nayo, enyi Mitume, ni wenye kukanusha.»
Na wanasema, «Sisi ni wengi zaidi wa mali na watoto, na Mwenyezi Mungu hakutupa neema hizi isipokuwa ni kuwa anaridhika na sisi, na sisi si wenye kuadhibiwa duniani wala Akhera.»
Sema uwaambie, ewe Mtume, «Hakika Mola wangu Anawakunjulia riziki hapa duniani anaowataka miongoni mwa waja Wake, na Anawabania Anaowataka, si kwa mapenzi wala chuki, lakini Anafanya hivyo kwa kuwatahini. Lakini wengi wa watu hawajui kwamba huo ni mtihani kwa waja Wake kuwa wao hawataamali.»
Hayakuwa mali yenu na watoto wenu ni vitu vya kuwafanya nyinyi muwe karibu na sisi, na daraja zenu ziwekwe juu, lakini wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo mema, basi hao watapata malipo ya nyongeza: kwa jema moja kwa kumi mfano wake mpaka kiwango cha nyongeza Anachokitaka Mwenyezi Mungu. Na wao watakuwa kwenye Pepo ya juu kwa juu, wakiwa wamesalimika na adhabu, kifo na mambo ya huzuni.
Na wale wanaokimbilia kuzibatilisha hoja zetu na wanaozuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe wakiwa wapinzani na washindani, hawa wataingia ndani ya adhabu ya Jahanamu Siku ya Kiyama, watahudhuriwa na Zabāniyah, ambao ni askari wa Motoni, na hawatatoka humo.
Waambie, ewe Mtume, hawa waliodanganyika kwa mali na watoto, «Mola wangu anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake na Anambania Anayemtaka, kwa hekima Anayoijua. Na namna mtakavyotoa kitu chochote, Yeye Atawapa badala yake duniani na huko Akhera Atawapa malipo mema. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye bora wa wenye kuruzuku, basi tafuteni riziki Kwake Peke Yake na zungukeni kwa kufuata sababu zake Alizowaamuru.
Kumbuka, ewe Mtume, Siku ambayo Mwenyezi Mungu Atawafufua washirikina na waabudiwa badala Yake miongoni mwa Malaika, kisha Awaambie Malaika kwa njia ya kuwalaumu wale waliowaabudu, «Je ni hawa waliokuwa wakiwaabudu badala yetu sisi?»
Malaika watasema, «Tunakutakasa, ewe Mwenyezi Mungu, na kuwa na mshirika wa kuabudiwa! wewe Ndiye Msimamizi wetu tunayemtii na kumuabudu Peke Yake. Bali hawa walikuwa wakiwaabudu mashetani, wengi wao wanawaamini na kuwatii.»
Basi Siku ya Ufufuzi, hao waabudiwa hawatakuwa na mamlaka ya kuwanufaisha au kuwadhuru wenye kuwaabudu. Na tutasema kuwaambia wale waliozidhulumu nafsi zao, «Onjeni adhabu ya Moto ambao mlikuwa mkiukanusha!»
Na wanaposomewa makafiri wa Makkah aya za Mwenyezi Mungu zikiwa wazi wao wanasema, «Hakuwa Muhammad isipokuwa ni mtu anayependa kuwakataza nyinyi kuwaabudu waungu ambao baba zenu walikuwa wakiwaabudu,» na wanasema, «Haikuwa hii Qur’ani isipokuwa ni urongo uliozuliwa, umeuleta wewe mwenyewe na sio kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu.» Na makafiri walisema kuhusu Qur’ani ilipowajia, «Haikuwa hii isipokuwa uchawi uliojitokeza wazi.»
Na hatukuwateremshia wakanushaji vitabu vya wao kuvisoma kabla ya Qur’ani vikawa vitawaonyesha wao yale wanayoyadai kwamba kile alichokuja nacho Muhammad ni uchawi, na hatukumtuma kwao kabla yako wewe, mjumbe yoyote wa kuwaonya wao adhabu yetu.
Na walikanusha wale waliokuwa kabla yao, kama vile 'Ād na Thamūd, Na watu wa Makkah hawakufikia ushuri wa kile tulichowapa ummah waliopita cha nguvu, wingi wa mali, umri mrefu na neema nyiginezo, na tukawaangamiza. Basi angalia, ewe Mtume! Ni namna gani yalivyokuwa makemeo yangu na adhabu yangu kwao?
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji washindani, «Mimi ninawapa ushauri mmoja: msimame kumtii Mwenyezi Mungu wawili-wawili na mmoja-mmoja, kisha mfikirie kuhusu hali ya mwenzenu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kile alichonasibishwa nacho. Yeye hana wazimu. Hakuwa Yeye isipokuwa ni mwenye kuwatisha na kuwaonya adhabu ya Jahanamu kabla joto lake halijawasumbua.»
Sema, ewe Mtume, uwaambie wakanushaji, «Malipo niliyowaomba kwa wema huu niliowaletea ni yenu nyinyi. Malipo yangu mimi ninayoyangojea hayapo isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Mwenye kuyaona matendo yangu na matendo yenu.Hakuna chochote kinachofichamana Kwake. Yeye Anawalipa wote: kila mmoja kwa anachostahiki.»
Sema, ewe Mtume, umwambie anayekanusha upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Uislamu, «Hakika Mola wangu Anauvurumiza ubatilifu kwa hoja za ukweli, hivyo basi ukaufedhehi na ukauangamiza. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa vitu visivyoonekana, hakuna kinachofichamana Kwake chochote ardhini na mbinguni.»
Sema, ewe Mtume, «Ukweli na Sheria tukufu itokayo kwa Mwenyezi Mungu umekuja, na ubatilifu umeondoka na mamlaka yake yamepotea, hivyo basi ubatilifu haukusaliwa na kitu cha kukianzisha wala kukirudisha.»
Sema, «Nikipotoka nikawa kando na haki, basi dhambi la upotevu wangu liko juu ya nafsi yangu, na nikiwa nitalingana sawa juu ya haki, ni kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu Ambao Ananiletea mimi. Hakika Mola wangu ni Msikizi wa ninayowaambia, Yuko karibu na yule anayemlingania na kumuomba.»
Na lau ungaliona, ewe Mtume, pindi watakapobabaika wakanushaji pale watakapoishuhudia adhabu ya Mwenyezi Mungu, ungaliona jambo kubwa! Hawatakuwa na uokozi wala makimbilio na watachukuliwa hadi Motoni kutoka mahali karibu pa kutwaliwa.
Na wakanushaji watasema watakapoiona adhabu huko Akhera, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu, Vitabu Vyake na Mitume Wake. Vipi wao waipate Imani na hali ni kwamba kuifikia kwao hiyo Imani ni kutoka mahali mbali?» kushawekwa kizuizi baina yao na hiyo, kwani mahali pake ni ulimwenguni, na huko walikanusha.
Kwa hakika waliikanusha haki duniani na wakawakanusha Mitume. Na wanajisemea kwa kudhani wakiwa mbali na kuifikia haki, hawana tegemezi la dhana yao ya ubatilifu, kwa hivyo hawana njia ya kuifikia haki kama vile mfumaji asivyo na njia ya kulenga shabaha kutoka mahali mbali.
Na kutawekwa kizuizi baina ya wakanushaji na kile wanachokitamani cha toba na kurudi ulimwenguni wapate kuamini, kama vile Mwenyezi Mungu Alivyowafanya wale wanaofanana na wao miongoni mwa wakanushaji wa watu wa mataifa yaliyopita. Kwa kweli wao walikuwa duniani wako kwenye shaka yenye kutia wasiwasi na babaiko kuhusu jambo la Mitume, kufufuliwa na kuhesabiwa, na kwa hivyo hawakuamini.