ﮡ
surah.translation
.
ﰡ
Umekaribia wakati wa kuhesabiwa watu juu ya matendo waliyoyatanguliza, pamoja na hivyo, makafiri wanaishi wakiwa kwenye hali ya kupumbaa, wameghafilika na uhakika huu, wakiwa kwenye hali ya kulipa mgongo onyo hili.
Hakuna kitu chochote katika Qur’ani chenye kuteremka, kinachosomwa kwao na chenye kuwakumbusha upya, isipokuwa huwa wakikisikia wakiwa katika hali ya kucheza na kufanya shere.
Nyoyo zao zimeghafilika na Qur’ani, zimeshughulika na ubatilifu wa dunia na matamanio yake, hawayafahamu yaliyomo ndani yake. Lakini madhalimu miongoni mwa Makureshi wamejikusanya pamoja juu ya jambo lililofichika, nalo ni kueneza yale ambayo kwayo wanawazuia watu kumuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kuwa yeye ni binadamu mfano wao, hatafautiani na wao katika kitu chochote, na kwamba Qur’ani aliyoileta ni uchawi. (Wanawaambia kwa kusema) «Vipi mutakuja kwake na mumfuate na hali kwamba mnaona kwamba yeye ni binadamu kama nyinyi?»
Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, analirudisha kila jambo kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, akasema, «Mola wangu Analijua jambo la mbinguni na la ardhini na Anayajua maneno yenu mnayoyasema kwa siri, na Yeye Ndiye Mwenye kuyasikia maneno yenu, Ndiye Mwenye kuzijua hali zenu.» Katika hiya pana tishio kwao na onyo.
Lakini makafiri wameikanusha Qur’ani: kuna wanaosema kwamba ni mchanganyiko wa ndoto zisizo na ukweli, kuna wanaosema kwamba ni uzushi na urongo na si wahyi na kuna wanaosema kwamba Muhammad ni mshairi na kwamba haya ambayo amekuja nayo ni mashairi, na akiwa anataka tumuamini basi na atuletee miujiza yenye kuonekana kama vile ngamia wa Ṣāliḥ na miujiza ya Mūsā na 'Īsā na yale ambayo walikuja nayo Mitume kabla yake.
Hakuna mji wowote ulioamini kabala ya makafiri wa Makkah ambao watu wake walitaka miujiza kutoka kwa Mtume wao na ikatokea kweli, bali walikanusha na tukawaangamiza. Basi je, makafiri wa Makkah wataamini iwapo itakuwa miujiza waliyoitaka? Sivyo, wao hawataamini.
Na hatukuwatumiliza kabla yako , ewe Mtume, isipokuwa wanaume wa kibinadamu ambao tunawaletea wahyi, na hatukuwatumiliza Malaika. Basi waulizeni, enyi watu wa Makkah, wenye ujuzi wa vitabu vilivyoteremshwa huko nyuma iwapo hamjui hilo.
Na hatukuwafanya wale Mitume kabla yako wawe nje ya tabia ya binadamu, wasihitaji chakula na kinywaji, na hawakuwa ni wenye kukaa milele wakawa hawafi.
Kisha tuliwatimizia Manabii na wafuasi wao yale tuliyowaahidi ya ushindi na kuokolewa, na tukawaangamiza wenye kuzionea nafsi zao kwa kumkanusha kwao Mola wao.
Kwa kweli tumekuteremshia hii Qur’ani; ndani yake kuna enzi yenu na utukufu wenu katika ulimwengu na Akhera iwapo mtajikumbusha nayo. Je, hamuyafahamu yale ambayo kwayo niliwatukuza nyinyi juu ya wasiokuwa nyinyi?
Na kuna miji mingi ambayo watu wake walikuwa madhalimu kwa kukanusha kwao yale ambayo Mitume wao walikuja nayo. Ndipo tukawaangamiza kwa adhabu iliyowamaliza wote, na tukafanya wapatikane watu wengine wasiokuwa wao.
Walipoiyona, madhalimu hawa, adhabu yetu kali ikiwashukia na wakaziona ishara zake, wakitahamaki wakawa wanakimbia kwa haraka kutoka mjini mwao.
Wakaitwa wakiwa katika hali hii na kuambiwa, «Msikimbieni, na rudini kwenye ladha zenu na starehe zenu katika ulimwengu wenu wenye kupumbaza na nyumba zenu zilizojengwa, kwani huenda mkaulizwa jambo kuhusu ulimwengu wenu. Na hiyo ni kwa njia ya kuwafanyia shere na ubishi.»
Hawakuwa na majibu yoyote isipokuwa ni kukubali makosa yao na kusema, «Ee maangamivu yetu! Tumejidhulumu nafsi zetu kwa ukafiri wetu.»
Yaliendelea maneno hayo - nayo ni yale ya kujiapiza wenyewe maangamivu na kukubali kuwa wamejidhulumu wenyewe- kuwa ndiyo mwito wao wanaoukariri mpaka tukawafanya kama mimea ya ukulima iliyovunwa, wakiwa wametulia hawana uhai. Basi kuweni na hadhari, enyi mnaoambiwa, na kuendelea kumkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, isije ikawashukia nyinyi yale yaliyowashukia watu waliopita kabla yenu.
Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa upuuzi na ubatilifu, lakini ni kwa kusimamisha hoja juu yenu, enyi watu, na ili mzingatie kwa hayo yote mpate kujua kwamba Yule Aliyeziumba hizo mbingu na ardhi hafanani na chochote, na hakuna anayefaa kuabudiwa isipokuwa Yeye.
Lau tulitaka kujifanyia kipumbazi cha mtoto au mke tungalikifanya kutoka kwetu, na sio kwenu. Hatukuwa ni wenye kufanya hilo kwa kuwa ni muhali kwetu kuwa na mtoto au mke.
bali tunaisukuma haki na tunaifafanua, na hapo urongo unapomoka, na punde si punde unaondoka na kupotea. Na nyinyi, enyi washirikina, mtapata adhabu huko Akhera kwa kumsifu kwenu Mola wenu kwa sifa zisizonasibiana na Yeye.
Ni milki ya Mweyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, kila aliye mbinguni na ardhini. Na wale Malaika walioko mbele Yake hawafanyi kiburi kumuabudu Yeye wala hawachoki kufanya hivyo. Basi vipi itafaa Ashirikishwe na kitu ambacho ni mja wake na kiumbe chake.
Wao (hao Malaika) wanamtaja Mwenyezi Mungu na wanamtakasa daima, hawadhoofiki wala hawachoki.
Itakuwa sawa vipi kwa washirikina kujifanyia waungu walemevu kutoka ardhini wasioweza kuhuisha wafu?
Lau mbinguni na ardhini kulikuwa na waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, wenye kuyaendesha mambo yake, ungaliharibika mpango wake. Basi Mwenyezi Mungu, Bwana wa 'Arsh, Ameepukakana na sifa za upungufu na Ametakasika na kila sifa ambayo wakanushaji makafiri wanamsifu nayo ya urongo, uzushi na kila aibu.
Miongoni mwa dalili za kupwekeka Kwake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, kwa kuumba na kustahiki kuabudiwa ni kwamba Yeye Haulizwi kuhusu uamuzi Wake kwa viumbe Wake na kwamba viumbe Wake wote ndio wenye kuulizwa kuhusu matendo yao.
Je, hawa washirikina waliwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu wanaonufaisha na kudhuru na wanaohuisha na kufisha? Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Leteni dalili zenu mlizonazo juu ya hao mliowafanya waungu.» Kwani hakuna, ndani ya Qur’ani niliyokuja nayo wala ndani ya Vitabu vilivyotangulia, dalili yoyote ya yale mliyoyafuata.» Na wao hawakushirikisha isipokuwa ni kwa sababu ya ujinga wao na kuigiza, kwa hivyo wao ni wenye kuupa mgongo ukweli na ni wenye kuukataa.
Na hatukutumiliza kabla yako, ewe Mtume, mjumbe yoyote isipokuwa tunampatia wahyi kwamba hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu. Basi mtakasieni ibada Yeye Peke Yake.
Na washirikina walisema, «Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto» kwa madai yao kwamba Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu. Ametakasika Mwenyezi Mungu na hilo! Malaika ni waja wa Mwenyezi Mungu waliokurubishwa waliohusishwa kwa kupewa matukufu,
na wao kwa utiifu wao mzuri hawasemi isipokuwa lile ambalo Mola wao Amewaamrisha kwalo, na hawafanyi tendo lolote mpaka Awaruhusu.
Na hakuna tendo lolote miongoni mwa matendo ya Malaika, lililopita au linalofuatia, isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Analijua na anawahesabia kwalo. Na hawatangulii kumuombea yoyote isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameridhika wamuombee. Na wao kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu wana hadhari ya kuenda kinyume na maamrisho Yake na makatazo Yake.
Na yoyote miongoni mwa Malaika atakayedai kwamba yeye ni mungu pamoja na Mwenyezi Mungu, kwa kukadiria, basi malipo yake ni moto wa Jahanamu. Na mfano wa malipo hayo ndivyo tunavyomlipa kila dhalimu mshirikina.
Kwani hawakujua hawa ambao wamekufuru kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeshikana, hakuna kipambanuzi baina yao, hakuna mvua kutoka juu wala mimea kutoka kwenye ardhi, kisha tukazipambanua kwa uweza wetu, tukateremsha mvua kutoka juu na tukatoa mimea kutoka kwenye ardhi na tukajaalia kutokana na maji kila kitu chenye uhai. Basi je hawaamini hawa wakanushaji, wakayasadiki wanayoyaona na wakamuhusuMwenyezi Mungu tu kwa ibada?.
Na tumeumba kwenye ardhi majabali yenye kuituliza isitikisike na tumetoa, kwenye hayo majabali, njia kunjufu, ili viumbe waongoke kwenye njia za kujitafutia maisha yao na kumpwekesha Muumba wao.
Na tumeifanya mbingu ni sakafu ya ardhi, haiinuliwi na nguzo, nayo imetunzwa, haianguki wala haipenywi na mashetani. Na makafiri wameghafilika na kupumbaa kutozizingatia alama za mbnguni (Jua, mwezi na nyota) na kutozifikiria.
Na mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, Ndiye Aliyeumba usiku ili watu wapate kutulia, na mchana ili wapate kutafuta maisha. Na Ameumba jua, likiwa ni alama ya mchana, na mwezi, ukiwa ni alama ya usiku. Na kila kimojawapo ya hivyo viwili kina njia ya kupitia na kuogelea hakiendi kando nayo.
Hatukumfanya mwadamu yoyote kabla yako, ewe Mtume, asalie duniani milele. Basi ufapo wewe, kwani wao wana matumaini ya kuishi daima baada yako? Hili haliwi. Katika aya hii pana dalili kwamba Al-Khadhir, amani imshukie, ameshakufa, kwa kuwa yeye ni mwanadamu.
Kila nafsi ni yenye kuonja kifo hapana budi namna utakavyorefuka umri wake duniani. Na kuweko kwake maishani hakukuwa isipokuwa ni mtihani wa majukumu ya maamrisho na makatazo na mabadiliko ya hali, mazuri na mabaya, kisha baada ya hapo kuna kurudi na kurejea kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ili kuhesabiwa na kulipwa.
Na makafiri wanapokuona, ewe Mtume, wanakuashiria kwa kukufanyia shere, huwa wakiambiana wao kwa wao, «Je, ni huyu yule mtu anayewatukana waungu wenu?» Wao wamemkanusha Mwingi wa rehema na wamezikanusha neema Zake na yale Aliyoyateremsha ya Qur’ani na uongofu.
Ameumbwa mwanadamu akiwa na pupa, anayafanyia haraka mambo na anakuwa na pupa yawe. Na kwa kweli, Makureshi waliifanyia haraka adhabu na wakaona kuwa imechelewa kutokea., Mwenyezi Mungu Akawaonya kwamba Atawaonesha adhabu waliyoifanyia haraka, basi wasimuombe Mwenyezi Mungu awaharakishie na awaletee kwa upesi.
Na makafiri wanasema, wakiifanyia haraka adhabu kwa njia ya shere, «Ni lini itapatikana ile unayotuonya nayo, ewe Muhammad, iwapo wewe na aliyekufuata wewe ni miongoni mwa wakweli.»
Lau makafiri wanajua watakayoyakuta watakapokuwa hawawezi kuzilinda nyuso zao na migongo yao na Moto na wasiipate wenye kuwanusuru, hawangalibaki kwenye ukafiri wao na hawangaliifanyia haraka adhabu yao.
Hakika Kiyama kitawajia ghafla, hapo wataduwaa na watakuwa na kicho kikubwa na hawataweza kuizuia adhabu isiwapate, na hawatapewa nafasi ya kutubia wala kutoa udhuru.
Mitume kabla yako, ewe Mtume, walifanyiwa shere, ikawafikia wale waliokuwa wakiifanyia shere adhabu ambayo walikiifanyia dhihaka na kejeli.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaoifanyia haraka adhabu, «Hakuna anayewahifadhi na kuwalinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia , usiku wenu au mchana wenu, katika kulala kwenu au kuangaza kwenu?» Bali wao wamepumbaa na wameghafilika na Qur’ani na mawaidha.
Je wao wanao waungu wenye kuwazuia wao na adhabu yetu? Kwa hakika, waola wao hawawezi kujinusuru wenyewe, vipi wataweza kuwanusuru wenye kuwaabudu? Na wao hawatanusuriwa kutokana na sisi.
Kwa hakika makafiri na baba zao walighurika na muhula waliopewa kwa kile walichokiona cha mali, watoto na maisha marefu, ndipo wakajikita kwenye ukafiri wao wasiepukane nao, na wakadhani kwamba wao hawataadhibiwa. Kwa kweli, wameghafilika na mpango uliopita, kwani Mwenyezi Mungu anaipunguza ardhi kwenye pambizo zake kwa adhabu Anayoiteremsha kwa washirikina kila sehemu na kushindwa. Je, makafiri wa Makkah Wana nafasi ya kutoka nje ya uwezo wa Mwenyezi Mungu au kukataa kufa?
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wale uliotumilizwa kwao, «Siwatishii adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa ni kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu,» nao ni Qur’ani. «Lakini makafiri hawasikii yale wanayosomewa masikizi ya kuzingatia wanapoonya, na kwahivyo hawafaidiki nayo.»
Lau liliwapata makafiri fungu la adhabu ya Mwenyezi Mungu wangalijua mwisho wa kukanusha kwao na wangalilikabili hilo kwa kujiapiza maangamivu kwa sababu ya kujidhulumu kwao nafsi zao kwa kumuabudu kwao asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu Ataiweka Mizani ya uadilifu kwa ajili ya Hesabu katika siku ya Kiyama. Hawatadhulumiwa hawa wala wengine kitu chochote, hata kama ni kitendo, kizuri au kibaya, cha kadiri ya chungu mdogo, kitazingatiwa katika hesabu ya mwenyewe. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyadhibiti matendo ya waja Wake na ni Mwenye kuwalipa kwayo.
Kwa hakika, tulimpa Mūsā na Hārūn hoja na ushindi juu ya maadui wao na pia Kitabu, nacho ni Taurati, ambacho kwacho tumepambanua baina ya ukweli na urongo, na ambacho ni nuru ambayo kwayo wanajioongoza wachamungu wenye kuogopa adhabu ya Mola wao.
Na wao ni wenye kicho na hofu kwa kuuogopa wakati Kiyama kitasimama.
Na hii Qur’ani ambayo Mwenyezi Mungu Ameiteremsha kwa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukliye, ni ukumbusho kwa anayejikumbusha nayo na akatekeleza amri Zake na akajiepusha na makatazo Yake, ina kheri nyingi na manufaa makubwa. Je, mnaikanusha na hali ina upeo wa uwazi na ufunuzi.
Kwa hakika, tulimpa Ibrāhīm uongofu wake ambao yeye aliwalingania watu waufuate kabla ya Mūsā na Hārūn. Na sisi tulikuwa tunajua kwamba yeye anastahiki hilo.
Pindi aliposema kumwambia babake na watu wake, «Ni masanamu gani hawa mliowatengeneza kisha mkakaa kuwaabudu na mkajilazimisha nao.»
Wakasema, «Tuliwapata baba zetu wakiwaabudu, na sisi tunawaabudu kwa kuwaiga wao.»
Ibrāhīm akawaambia, «Kwa hakika nyinyi na wazee wenu, kwa kukuwaabudu kwenu hawa masanamu, muko mbali waziwazi na haki.»
Wakasema, «Je, neno hili ambalo umekuja nalo kwetu ni la usawa na ukweli, au neno lako ni la mtu anayefanya mzaha na shere, hajui analosema?»
Ibrāhīm, rehema na amani zimshukie, akasema, «Bali Mola wenu Ambaye ninawalingania mumuabudu Ndiye Mola wa mbingu na ardhi Ambaye Ameziumba, na mimi ni mwenye kulitolea ushahidi hilo.
«Na ninaapa kwa Mwenyezi Mungu, nitawachimba masanamu wenu niwavunjevunje baada ya nyinyi kuondoka kwenda zenu na kuwaacha.»
Hapo Ibrāhīm akawavunjavunja masanamu akawafanya vipande- vipande vilivyo vidogo na akamuacha mkubwa wao, ili watu wake wapate kumrudia kumuuliza, na ili ulemevu wao na upotevu wao upate kujulikana waziwazi, na ili hoja isimame kwao.
Na watu wakarudi na wakawaona masanamu wao wamevunjwa- vunjwa na wametwezwa. Hapo wakaulizana wao kwa wao, «Ni nani aliyefanya haya kwa waungu wetu? Huyo, kwa kweli, ni dhalimu kwa kuwa na ujasiri juu ya waungu wanaostahiki kuheshimiwa na kutukuzwa.»
Hapo wale waliomsikia Ibraim akiapa kwamba atawachimba masanamu wao, «Tulimsikia kijana akiwataja kwa ubaya, anaitwa Ibrāhīm.»
Viongozi wao wakasema, «Mleteni Ibrāhīm mbele ya watu aonekane, wapate kushuhudia kukubali kwake makosa ya aliyoyasema, ili iwe ni hoja dhidi yake.»
Ibrāhīm akaletwa, na wakamuuliza kwa njia ya kumpinga, «Je, ni wewe uliowavunjavunja waungu wetu?» Wakikusudia masanamu wao.
Ibrāhīm akalipata alitakalo la kuonesha wazi upumbavu wao na huku wakiona, akasema, «Aliyewavunjavunja ni huyu sanamu mkubwa, waulizeni hilo waungu wenu mnaowadai iwapo watasema au watawapa majibu.»
Hapo wakatahayari na ukawafunukia wazi upotevu wao, vipi wanawaabudu na ilhali wao wanashindwa kujitetea wenyewe kitu chochote wala kuwajibu mwenye kuwauliza? Na wakakubali wenyewe kuwa wamefanya udhalimu na ushirikina.
Punde si punde ukakamavu wao uliwarudia baada ya kushindwa hoja, wakageuka kurudi kwenye ubatilifu wao na wakatumia hoja dhidi ya Ibrāhīm ambayo ni hoja dhidi yao wakasema, «Vipi tutawauliza na hali wewe unajua kuwa hawa hawasemi?»
Ibrāhīm akasema kwa njia ya kudharau jambo la kuabubudu masanamu, «Vipi mnaabudu masanamu wasionufaisha wanapoabudiwa wala kudhurisha wanapoachwa?
Ubaya ni wenu na ni wa waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Kwani hamutii akili mkajua uovu wa haya mliyonayo?»
Ilipopomoka hoja yao na ukweli ukajitokeza, waliamua kutumia uwezo wao na wakasema, «Mchomeni Ibrāhīm kwa moto mkionesha hasira kwa ajili ya waungu wenu, iwapo nyinyi ni wenye kuwasaidia basi washeni moto mkubwa na mumtupe ndani yake.»
Mwenyezi Mungu Akamsaidia Mtume Wake na Akauambia moto, «Kuwa baridi na salama kwa Ibrāhīm!» Hivyo basi asiipate na udhia wala asifikiwe na jambo la kuchukiza.
Na wale watu walimtakia Ibrāhīm maangamivu na Mwenyezi Mungu Akavitangua vitimbi vyao na Akawafanya wao wawe ni wenye kushindwa na kuwa chini.
Na tukamuokoa Ibrāhīm na Lūṭ ambaye alimuamini kutoka 'Irāq na tukawatoa huko hadi Shām ambako tulikubariki kwa kheri nyinygi, na huko kulikuwa na Manabaii, rehema na amani ziwashukie, wengi zaidi.
Na Mwenyezi Mungu Alimneemesha Ibrāhīm kwa kumtunuku Isḥāq alipomuomba, na zaidi ya hilo Alimtunuku, kutokana na Isḥāq, Ya'qūb. Na kila mmoja kati ya Ibrāhīm na Isḥāq na Ya'qūb Mwenyezi Mungu Alimjaalia kuwa mwema na mtiifu Kwake.
Na tukamfanya Ibrāhīm, Isḥāq na Ya'qūb kuwa viongozi wa watu, wanawalingania wamuabudu Yeye na kumtii kwa idhini Yake Aliyetukuka, na tuliwaletea wahyi kufanya mema ya kuzifuata kivitendo sheria za Manabii, kusimamisha Swala kwa njia zake na kutoa Zaka. Na wao walizifuata amri hizo na walikuwa watiifu kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake bila Mwingine.
Na tulimpa Lūṭ unabii, kufanya uamuzi baina ya watesi na ujuzi wa amri za Mwenyezi Mungu na Dini Yake. Na tulimuokoa na kijiji chake Sadūm ambacho watu wake walikuwa wakifanya mambo machafu. Wao, kwa sababu ya machafu na maovu ambayo watu wa uovu na uchafu wakiyatenda, walikuwa nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu Akamkamilishia nema, Akamtia ndani ya rehema Yake kwa kumuokoa na kile kilichowafikia watu wake kwa kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa wale wanaofanya matendo ya utiifu Kwake.
Na mkumbuke Nūḥ, ewe Mtume, alipomuita Mola Wake kabla yako na kabla ya Ibrāhīm na Lūṭ, tukaitika mwito wake na tukamuokoa, yeye na watu wake waliomuamini, na makero makubwa.
Na tukamnusuru na vitimbi vya watu waliozikanusha alama zetu zenye kuonesha ukweli wake. Kwa haki, wao walikuwa ni watu wa ubaya, na hivyo basi tuliwazamisha wote kwa mafuriko.
Na kumbuka Nabii wa Mwenyezi Mungu Dāwūd na mwane Sulaiman, ewe Mtume, walipotoa uamuzi juu ya kesi iliyoletwa na wagonvi wawili, kondoo wa mmoja wao waliharibu mimea ya mwingine, walienea kwenye mimea hiyo kipindi cha usiku wakaiharibu. Dāwūd alitoa uamuzi kwamba wale kondoo wawe ni milki ya mwenye mimea wakiwa ni badala ya mimea yake iliyoharibiwa, kwa kuwa thamani ya viwili hivyo ni sawa. Na sisi tuliushuhudia uamuzi wao, haukufichamana kwetu.
Tukamfahamisha Sulaymān kuzingatia maslahi ya pande mbili na kufanya uadilifu, akatoa uamuzi kwamba yule mwenye kondoo ashughulike kutengeneza mimea iliyoharibika na kumalizika kwa muda maalumu ambapo katika muda huo yule mwenye mimea ajifaidishe kwa manufaa ya kondoo, kama vile maziwa, sufi na mfano wake, na baadaye kondoo warudi kwa mwenyewe na mimea irudi kwa mwenyewe, kwa kuwa thamani ya mimea iliyoharibiwa inalingana na manufaa ya wale kondoo. Na kila mmoja kati ya Dāwūd na Sulaymān tulimpa busara na ujuzi. Na tulimfanyia Dāwūd wema wa kumdhalilishia majabali yakawa yanaleta tasbihi anapoleta tasbihi, na vilevile ndege wakawa wanaleta tasbihi, na sisi tulikuwa ni wenye kulifanya hilo.
Na Mwenyezi Mngu Alimhusu Dāwūd, amani imshukiye, kwa kumfundisha kutengeneza nguo za kivita, akizifanya kwa kutunga vikuku vilivyoshikamana, kurahisisha harka ya mwili, ili kuwakinga wapiganaji wasiathiriwe na silaha wanazopigwa. Je, nyinyi ni wenye kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwenu kupitia kwa mkono wa mja Wake Dāwūd?
Na tulimdhalilishia Sulaymān upepo wenye kuvuma kwa kasi ukimchukua yeye na walio pamoja naye, ukawa unapita kwa amri yake kuelekea ardhi ya Bayt al-Maqdis iliyoko Shām amabayo tuliibariki kwa kheri nyingi. Na ujuzi wetu umeenea vitu vyote.
Na tulimdhalilishia Sulaymān, kati ya mashetani, mashetani ambao alikuwa akiwatuma kufanya yale ambayo wasiokuwa wao wanashindwa nayo, walikuwa wakipiga mbizi baharini wakimtolea lulu na johari, na walikuwa wakimtengenezea vitu avitakavayo kwao, hawakuwa wakiweza kukataa kufanya ayatakayo kutoka kwao. Mwenyezi Mungu Amewahifadhi kwa nguvu Zake na enzi Yake , kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake.
Na kumbuka, ewe Mtume, mja wetu Ayyūb, tulipomtahini kwa madhara na ugonjwa mkubwa mwilini mwake, na akakosa watu wake, mali yake na watoto wake, akasubiri kwa kutaka thawabu, na akamlingania Mola wake, Aliyetukuka na kushinda, kwa kumuomba, «Mimi nimepatikana na madhara, na wewe Ndiye Mwenye huruma kuliko wenye huruma, basi niepushie nayo!»
Hapo tukayakubali maombi yake, tukamuondolea matatizo na tukamrudishia alichokikosa miongoni mwa wake, watoto na mali mara mbili zaidi. Tulimfanyia hayo kwa huruma itokayo kwetu na ili awe ni kiolezo kwa kila mwenye kuvumilia mitihani, mwenye matumaini ya kupata rehema ya Mola wake na mwenye kumuabudu.
Na kumbuka Ismā'īl, Idrīs na Dhulkifl. Wote hao ni miongoni mwa wavumilivu katika kumtii Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, katika kujiepusha na kumuasi na juu ya makadirio Yake, na kwa hivyo walistahiki kutajwa kwa sifa nzuri.
Na tukawatia ndani ya rehema yetu. Kwa hakika wao ni miongoni mwa wale ambao imetengenea ndani yao na nje yao, wakamtii Mwenyezi Mungu na wakafanya matendo yanayolingana na maamrisho Yake.
Na kumbuka kisa cha mtu wa chewa, naye ni Yūnus mwana wa Mattā, amani imshukie, Mwenyezi Mungu Alimtumiliza kwa watu wake, akawalingania wasimuamini, akawaonya kuwa wataadhibiwa, lakikni hawakurudi nyuma. Na asiwavumilie kama vile Mwenyezi Mungu Alivyomuamrisha na akaondoka kutoka kwao akiwa na hasira juu yao, akiwa amebanwa na kifua kwa kuasi kwao. Na akadhani kwamba Mwenyezi Mungu Hatampa dhiki na kumuadhibu kwa ukiukaji huu. Mwenyezi Mungu Akamtahini kwa dhiki nyingi na kifungo na akamezwa na tewa baharini, na akamlingania Mola wake kwa kumuomba katika magiza ya usiku, bahari na tumbo la tewa hali ya kutubia na kukubali ukiukaji wake kwa kuacha kuwavumilia watu wake, huku akisema, «Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa wewe! Kutakasika na sifa za upungufu ni kwako! kwa hakika mimi nimekuwa miongoni mwa wenye kudhulumu!»
Basi hapo tukamkubalia maombi yake na tukamuondolea unguliko la shida. Na hivyo ndivyo tunavyowaokoa wakweli wenye kuzifuata sheria zetu kivitendo.
Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha mja wa Mwenyezi Mungu Zakariyya alipomuomba Mola wake Amtunukie wana, wakati umri wake ulipokuwa mkubwa, kwa kusema, «Mola wangu! Usiniache pweke ni siwe na mwana! Basi nitunuku mrithi wa kusimamia mambo ya Dini kwa watu baada yangu mimi, na wewe Ndiye bora wa wenye kusalia na bora wa wenye kusimamia mambo yangu baada yangu kwa uzuri!»
Tukamkubalia maombi yake na tukamtunuku yeye, akiwa katika hali ya uzee, mwanawe Yaḥyā, na tukamfanya mke wake ni mwema wa tabia na ni mwenye kufaa kushika mimba na kuzaa baada ya kuwa tasa. Kwa kweli, wao walikuwa wakiikimbilia kila kheri, na wakituomba wakitumai kupata mazuri yaliyoko kwetu wakiogopa mateso yetu na walikuwa wadhalilifu na wanyonge kwetu.
Na kumbuka, ewe Mtume, kisa cha Maryam binti ya 'Imran aliyeihifadhi tupu yake na haramu na asifanye uzinifu katika maisha yake. Mwenyezi Mungu Akamtuma Jibrili, amani imshukiye, kwake akapuliza katika mfuko wa kanzu yake, na ule mpulizo ukafika kwenye uzao wake, na Mwenyezi Mungu akamuumba Al-Masīḥ 'Īsā, amani imshukie. Hivyo basi akabeba mimba yake bila ya mume, na kwa ajili hiyo akawa , yeye na mwanawe, ni alama ya uweza wa Mwenyezi Mungu na mazingatio kwa viumbe mpaka kusimama Kiyama.
Manabii hawa wote, dini yao ni moja, nayo ni Uislamu. Nao ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kwa kuwa mtiifu na kumpwekesha Yeye kwa ibada. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Bwana wa viumbe, basi muabuduni, enyi watu, Peke Yake, Asiye na mshirika.
Lakini watu walitafautiana juu ya Mitume wao, na wengi wa wafauasi wao katika dini walipambanukana wakawa ni makundi na mapote, wakaabudu viumbe na matamanio. Na wote hao ni wenye kurejea kwetu na ni wenye kuhesabiwa juu ya yale waliyoyafanya.
Basi Mwenye kujilazimisha kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na akafanya awezayo ya matendo mema kwa kumtii Mwenyezi Mungu na kumuabudu. Kwani Mwenyezi Mungu Hayapotezi matendo Yake wala Hayabatilishi, bali Anayaongeza yote hayo mara nyingi, na atayakuta aliyoyatenda kwenye Kitabu chake siku atakayofufuliwa baada ya kufa kwake.
Haiwezekani kwa watu wa miji tuliyoiangamiza, kwa sababu ya ukanushaji wao na dhulma zao, kurudi duniani kabla ya Siku ya Kiyama ili kurakibisha kasoro zao ambazo walikuwa nazo.
Basi pindi kitakapofunguliwa kizuizi cha Ya’jūj na Ma’jūj, na wakatoka kwenye ardhi za juu wakaenea kwenye pande zake kwa haraka,
hapo Siku ya Kiyama itakuwa imekaribia na vituko vyake vitajitokeza, na hapo utayaona macho ya makafiri yamekodoka hayapepesi kwa kibabaiko kikali, huku wakiwa wanajiapiza maangamivu kwa majuto wakisema, «Ee ole wetu! Kwa hakika tulikuwa tumeghafilika na Siku hii na kujiandalia nayo na kwa hivyo tulikuwa madhalimu.»
Kwa hakika, nyinyi, enyi makafiri, na vitu ambavyo mlikuwa mkiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa masanamu, na wale walioridhia muwaabudu, kati ya majini na binadmu, ni viwashio vya moto wa Jahanamu na ni kuni zake, nyinyi na wao humo mtaingia.
Lau hawa ambao mliwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka walikuwa ni waungu wanaostahiki kuabudiwa, hawangaliingia moto wa Jahanamu pamoja na nyinyi, enyi washirikina. Kwa hakika, wote hao, waabudu na waabudiwa, ni wenye kukaa milele ndani ya moto wa Jahanamu.
Hawa wenye kuadhibiwa Motoni wataona uchungu unaooneshwa na mlio wa sauti zao ambapo pumzi zao zinatoka kwa nguvu sana kutoka kwenye vifua vyao. Na wao wakiwa Motoni hawasikii kwa ukali wa adhabu wanayopewa.
Kwa hakika, wale ambao kimetangulia kwetu sisi kitangulizi chema katika ujuzi wetu kuwa watakuwa ni watu wa Peponi, hao wataepushwa na Moto, hawataungia wala hawatakuwa karibu nao.
Hawatasikia sauti ya mroromo wake na kuchomeka kwa miili humo, kwani wameshakaa kwenye nyumba zao huko Peponi na wamekuwa ni wenye kukaa makao ya milele katika starehe na ladha zake zinazotamaniwa na nafsi zao.
Hakiwatishi wao kituko kikubwa Siku ya Kiyama, bali Malaika watawapa bishara njema kwa kuwaambia, «Hii ndiyo siku yenu mlioahidiwa maandalizi mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na thawabu nyingi.»
Siku ambayo tutaikunja mbingu kame vile ukurasa unaokunjiwa maandishi yaliyomo ndani na tutawafufua viumbe kama vile walivyokuwa mwanzo walipozaliwa na mama zao. Hiyo ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyokwenda kinyume. Tumeliahidi hilo ahadi ya kweli tuliyojilazimisha nayo. Hakika sisi daima ni wenye kufanya tunaloahidi.
Na kwa hakika, tuliandika kwenye vitabu vilivyoteremshwa, baada ya kuwa yashaandikwa katika Ubao Uliohifadhiwa, kwamba ardhi watairithi waja wa Mwenyezi Mungu walio wema, wale wanaosimama imara kwa yale waliyoamrishwa na wakajiepusha na yale waliyokatazwa, nao ni ummah wa Muhammad, rehema na amani ya Mwenyezi Mungu zishukiye.
Kwa hakika, kwenye mawaidha haya yanayosomwa pana mazingatio ya kutosha kwa watu wenye kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa namna Aliyowaekea na Anayoiridhia kutoka kwao.
Na hatukukutumiliza , ewe Mtume, isipokuwa ni rehema kwa watu wote. Mwenye kukuamini atakuwa mwema na ataokoka, na asiyeamini atapita patupu na atapata hasara.
Sema, «Kile nilicholietewa wahyi na nikatumilizwa kwacho ni kwamba mola wenu Anayestahiki kuabudiwa, Peke Yake, ni Mwenyezi Mungu. Basi jisalimisheni Kwake na mnyoshe shingo zenu kwa kumuabudu.»
Basi hawa wakiupuka Uislamu waambie, «Ninawafikishia nyote kile ambacho Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amenitumia wahyi nacho. Mimi na nyinyi tuko sawa katika kuyajua yale ninayowaonya nayo na kuwatahadharisha, na mimi sijui, baada ya hapo, ni lini adhabu mliyoagiziwa itawashukia?»
Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyadhihirisha miongoni mwa maneno yenu na mnayoyaficha ndani ya nyoyo zenu, na Atawahesabu kwayo.
Na sijui huenda kukawa kule kucheleweshwa adhabu mliyoitaka iwajie kwa haraka ni mavuto na mtihani kwenu, na ili mjistareheshe ulimwenguni mpaka muda ukome, mpate kuzidisha ukafiri, kisha hiyo iwe ni sababu ya nyinyi kupata mateso makubwa zaidi.
Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, akasema,» Mola wangu! Amua baina yetu na watu wetu walioukanusha Uamuzi wa haki, na tunamuomba Mola wetu Mwingi wa rehema, tunataka msaada Wake tuzibatilishe sifa mnazombandika, enyi makafiri, za ushirikina na ukanushaji na uzushi na juu ya maonyo mnayotuonya kuwa mtakuwa na nguvu na ushindi.