ﰡ
«Tā Sīn» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah. Hizi ni aya za Qur’ani, nazo ni aya za Kitabu kitukufu zenye maana yaliyofunuka wazi zenye ushahidi waziwazi wa kuonyesha elimu zilizomo, hekima na Sheria.
Nazo ni aya zenye kuongoza kwenye njia ya kufuzu duniani na Akhera, na zinatoa bishara ya malipo mazuri kwa Waumini walioziamini na wakaongoka kwa uongofu wake.
Ambao wanasimamisha Swala tano zilizotimia nguzo, zilizokamilika masharti, na wanatekeleza Zaka za lazima kwa wanaostahiki kupewa, na wao wanaamini kwa yakini maisha ya Akhera na yaliyomo ndani yake ya malipo mema na mateso.
Hakika ya wale wasioamini nyumba ya Akhera na hawafanyi matendo ya kuwafaa huko, tutawapambia wao matendo yao mabaya wayaone ni mazuri, na wao watakuwa wakizunguka kwenye matendo hayo wakiwa wameduwaa.
Hao ndio watakaopata adhabu mbaya duniani, kwa kuuawa, kutekwa, kudhalilika na kushindwa. Na wao huko Akhera watakuwa ni wenye hasara kubwa zaidi.
Na kwa hakika wewe , ewe Mtume, unapewa Qur’ani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa hekima katika kuumba Kwake na upelekeshaji Wake Ambaye Amekizunguka kila kitu kwa kukijua.
Taja habari ya Mūsā aliposema kuwaambia watu wa nyumbani kwake katika safari yake kutoka Madyan kwenda Misri, «Mimi nimeuona moto. Nitawajia kutoka huko na habari ya kutuonyesha njia, au nitawajia na kinga cha moto mupate mvuke wake mjihami na baridi.
Mūsā alipoujia moto, Mola wake Alimwita na akampa habari kwamba hapa ni mahali Alipopatakasa Mwenyezi Mungu na Akapabariki na Akapafanya ni mahali pa kusema na Mūsā na kumtumiliza, na kwamba Mwenyezi Mungu Amewabariki waliopo motoni na waliopo pambizoni mwake miongoni mwa Malaika, na kumtakasa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe, kwa kumuepusha na sifa zisizonasibiana na Yeye,
«Ewe Mūsā! Hakika yangu mimi ni Mwenyezi Mungu ninayestahiki kuabudiwa peke yangu, ni Mshindi Mwenye nguvu wa kuwaadhibu maadui zangu, niliye na hekima katika upelekeshaji wa viumbe vyangu.
Na itupe fimbo yako!» Akaitupa ikawa nyoka. Alipoiona inatikisika kwa ulaini kama vile nyoka mwepesi anavyojitikisa, alizunguka kukimbia na asiirudie. Hapo Mwenyezi Mungu Akamtuliza kwa neno Lake, «Ewe Mūsā! Usiogope. Hakika mimi hawaogopi mbele yangu wale niliowatuma na ujumbe wangu.
Isipokuwa yule aliyepitisha mpaka kwa kufanya dhambi kisha akatubia, akabadilisha toba njema baada ya dhambi baya, kwani mimi ni mwenye kumsamehe ni mwenye kumrehemu.» Basi asikate tamaa mtu yoyote na rehema ya Mwenyezi Mungu na msamaha Wake.
«Na utie mkono wako kwenye uwazi wa kanzu yako uliofunuliwa kifuani, utatoka ukiwa mweupe kama barafu, bila ya kuwa na mbalanga, ikiwa ni moja ya miujiza tisa, nayo, pamoja na huo mkono, ni fimbo, miaka ya ukame, upungufu wa matunda, mafuriko, nzige, chawa, vyura na damu, ili kukupa nguvu wewe katika ujumbe wako utakaoupeleka kwa Fir’awn na watu wake. Hakika wao walikuwa ni watu waliotoka nje ya amri ya Mwenyezi Mungu na kumkanusha.»
Miujiza hii ilipowajia, hali ya kuwa imefunuka wazi, inamfanya mwenye kuitazama auone uhakika wa yale inayoyatolea ushahidi, walisema, «Huu ni uchawi uliofunuka waziwazi.»
Na waliikanusha, Fir’awn na watu wake, miujiza tisa yenye kuonyesha wazi ukweli wa Mūsā katika unabii wake na ukweli wa ulinganizi wake, na walikanusha kwa ndimi zao kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu, na hali wana yakini nayo ndani ya nyoyo zao, kwa kuifanyia uadui haki na kuwa na kiburi cha kutoikubali. Basi angalia , ewe Mtume, ulikuwa vipi mwisho wa wale waliozikanusha aya za Mwenyezi Mungu na wakafanya uharibifu kwenye ardhi? Mwenyezi Mungu aliwazamisha baharini. Na katika hilo kuna mazingatio kwa anayezingatia.
Na kwa kweli, tulimpa Dāwūd na Sulaymān elimu wakaitumikia na wakasema, ‘Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetufanya bora kuliko wengi miongoni mwa waja Wake Waumini. Katika hii aya kuna dalili ya utukufu wa elimu na daraja ya juu ya wenye elimu.
Na Sulaymān alimrithi baba yake Dāwūd unabii na elimu. Na alisema Sulaymān kuwaambia watu wake, «Enyi watu! Tumefundishwa na kufahamishwa maneno ya ndege, na tumepewa kila kitu kinachohitajika. Kwa hakika, huu ambao Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ametupa ndio wema ulio waziwazi ambao Anatufadhilisha nao juu ya wasiokuwa sisi.
Na akakusanyiwa Sulaymān askari wake miongoni mwa majini, binadamu na ndege katika matembezi yao. Na wao, pamoja na wingi wao, hawakua wamepuuzwa, bali palikuwa, juu ya kila jinsi, mwenye kuwasimamia wa mwanzo wao kwa wa mwisho wao ili wasimame wote wakiwa wamejipanga.
Mpaka walipofika kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja «Enyi chungu! Ingieni kwenye makazi yenu ili Sulaymān na askari wake wasije wakawaua na hali wao hawajui hilo.»
Akatabasamu akicheka kwa neno la huyu chungu, kwa kufahamu kwake na kuwa na akili ya kuwaonya chungu, na akatambua neema ya Mwenyezi Mungu juu yake. Hapo akaelekea Kwake akiomba, «Mola wangu! Nipe muelekeo na uniafikie nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu wawili, na nifanye matendo mema ambayo wewe utaridhika nayo kutoka kwangu na unitie, kwa rehema zako, ndani ya starehe ya Pepo yako pamoja na waja wako wema ambao uliridhika na matendo yao.
Na akakagua Sulaymān hali ya ndege waliofanywa watiifu kwake na hali ya wale wasiokuweko miongoni mwao, na kulikuwa hapo kwake kuna ndege anayetambulikana na kujulikana aina ya hud-hud asimpate hapo. Akasema, «Kwa nini mimi simuoni yule hud-hud nimjuwae? Je, kuna kitu kilichomfanya afichike nisimuone? Au huyu ni miongoni mwa wale ambao hawapo hapa kwangu, ndio nisimuone kwa kuwa hayupo?» Ilipofunuka wazi kuwa hayupo,
alisema, «Nitamuadhibu hud-hud huyu adhabu kali kwa kumtia adabu ya kutokuweko kwake, au nitamtesa kwa kumchinja kwa kitendo alichokifanya kwa kuwa aliharibu nidhamu aliyowekewa aifuate, au ni lazima anijie na hoja iliyo wazi ya sababu ya kughibu kwake.
Akakaa hud-hud muda usio mrefu kisha akahudhuria, na Sulaymān akamlaumu juu ya kughibu kwake na kutokuwako kwake. Hud-hud akamwambia, «Nimejua jambo usilolijuwa kikamilifu, na nimekujia kutoka mji wa Saba’ na habari ya jambo muhimu sana, na mimi nina yakina nalo.
«Mimi nimemkuta mwanamke anawatawala watu wa Saba ’, na amepatiwa kila kitu katika mahitaji ya utawala wa kidunia, na ana kitanda cha heshima kubwa anakalia juu yake kuendesha mambo ya ufalme wake.
«Nimemkuta Yeye na watu wake wanaabudu jua, wakiacha kumuabudu Mwenyezi Mungu. Na Shetani Amewapambia matendo yao mabaya waliokuwa wakiyafanya, akawaepusha na kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha, hivyo basi wao hawaongoki kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, kumpwekesha na kumuabudu Peke Yake.»
Shetani amewapambia hilo, ili wasimsujudie Mwenyezi Mungu Ambaye Anakitoa kilichofichwa na kufinikwa mbinguni na ardhini miongoni mwa mvua, mimea na visivyokuwa hivyo, na Anayajua mnayoyafanya kwa siri na mnayoyafanya kwa dhahiri.
Mwenyezi Mungu, Ambaye hakuna muabudiwa anayestahiki ibada isipokuwa Yeye, ni Mola wa ‘Arsh iliyo kubwa ambayo ni kubwa kuliko viumbe vyote.
Sulaymān alisema kumwambia hud-hud, «Tutaichunguza habari uliyotuletea tujue: unasema kweli katika hiyo au umekuwa ni katika warongo ndani yake?
Enda na barua yangu hii kwa watu wa Saba’ uwapatie, kisha jiepushe kando na wao ukiwa karibu nao mahali unapoweza kusikia maneno yao na uyatie akilini maneno yatakayopitika baina yao.»
Hud-hud alienda akamrushia malkia ile barua. Papo hapo akaisoma na akawakasunya watukufu wa watu wake, na akamsikia akisema, «Mimi nimefikiwa na barua tukufu yenye cheo kutoka kwa mtu mkubwa wa cheo.»
Kisha akayaeleza yaliyomo ndani akasema, «Hiyo inatoka kwa Sulaymān, nayo imeanza na ‘Bi ism Allāh al-Rahmān al-Rahīm» (Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwenye kuwarehemu wema na waovu ulimwenguni, Mwenye kuwarehemu wema watupu kesho Akhera)
Msifanye kiburi wala msijifanye wakubwa mkakataa kuyakubali haya ninayowalingania. Na njooni kwangu mkiwa ni wenye kukubali upweke wa Mwenyezi Mungu na kujisalimisha Kwake kwa utiifu.»
Akasema, «Enyi watukufu! Nipeni shauri kuhusu jambo hili. Sikuwa mimi ni mwenye kuamua jambo isipokuwa mbele yenu na kwa ushauri wenu.»
Wakasema kumjibu ,»Sisi ni wenye nguvu wa idadi na silaha, na ni watu wa utetezi na ushujaa katika vita vikali, na uamuzi ni wako, na wewe ndiye mwenye maoni, basi fikiria unatuamrisha nini. Sisi ni wenye kusikiliza maneno yako na ni watiifu kwako.»
Akasema akiwatahadharisha kukabiliana na Sulaymān kwa uadui na akiwaelezea mwisho mbaya wa kupigana, «Kwa hakika, wafalme wakiingia na majeshi yao kwenye mji kwa nguvu na ushindi, wanauharibu, wanawafanya watukufu wake kuwa wanyonge, wanauwa na wanachukua mateka. Na hii ndiyo desturi yao inayoendelea na inayojikita ili kuwafanya watu wawaogope.
Na mimi nitamtumia Sulaymān tunu iliyokusanya mali ya thamani ili kufanya urafiki naye kwayo, na nitangojea watarudi na nini hao wajumbe.»
Mjumbe wa malkia alipokuja na tunu kwa Sulaymān, alisema Sulaymān, akilikataa hilo na akizungumzia neema za Mwenyezi Mungu juu yake, «Mnanipatia mali ili kuniridhisha? Yale aliyonipa Mwenyezi Mungu ya unabii, ufalme na mali mengi ni mazuri zaidi na ni bora zaidi kuliko hayo Aliyowapa nyinyi, bali nyinyi ndio mnaofurahia tunu mnayotunukiwa, kwa kuwa nyinyi ni watu wa kuonyeshana kwa kujifahiri na dunia na kuipapia kwa wingi.»
Na Sulaymān, amani imshukiye, akasema kumwambia mjumbe wa watu wa Saba’, «Rejea kwao, kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu, tutawajia wao na askari wasioweza kupambana nao na kukabiliana nao, na tutawatoa kutoka nchini mwao wakiwa wadhalilifu, hali ya kuwa wanyonge wenye kudharauliwa, iwapo hawatafuata Dini ya Mwenyezi Mungu Peke Yake na hawataacha kumuabudu asiyekuwa Yeye.»
Sulaymān akasema akiwahutubia wale ambao Mwenyezi Mungu Amemdhalilishia miongoni mwa majini na binadamu, «Ni nani kati yenu ataniletea kitanda cha ufalme wake kabla hawajanijia wakiwa katika hali ya kufuata na kutii?»
Akasema afriti wa kijini mwenye nguvu na ukali, «Mimi nitakuletea kabla hujainuka kutoka kwenye kikao chako hiki unachokaa kuhukumu baina ya watu. Na mimi ni mwenye nguvu na uwezo wa kukibeba, ni muaminifu wa kuvitunza vilivyomo ndani yake, nitakuja nacho kama kilivyo, sikipunguzi kitu chake chochote wala sikigeuzi.»
Akasema yule ambaye alikuwa na ujuzi kutoka kwenye Kitabu, «Mimi nitakuletea hiko kitanda kabla ya kupepesa macho yako yanapogeuka kuangalia kitu.» Sulaymān akamruhusu, naye akamuomba Mwenyezi Mungu na akakileta kitanda cha kifalme. Alipokiona Sulaymān kimehudhurishwa mbele yake na kimethibiti alisema, «Huu ni miongoni mwa wema wa Mola wangu Aliyeniumba na akaumba ulimwengu wote ili kunitahini mimi nitalishukuru hilo kwa kutambua neema Yake Aliyetukuka au nitakufuru kwa kuacha kushukuru? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake, nafuu ya hilo itamrudia yeye mwenyewe, na mwenye kukanusha neema na akaacha kushukuru, basi hakika Mola wangu Ametosheka Hahitajii shukrani yake, ni Karimu ambaye kheri Yake inamuenea hapa duniani mwenye kushukuru na mwenye kukufuru, kisha Atawahesabu huko Akhera na awalipe.
Sulaymān akasema kuwaambia walioko mbele yake, «Kibadilisheni kitanda cha ufalme wake ambacho anakaa juu yake kwa namna ya yeye kutokitambua akikiona, tuone: ataelekezeka kukijua au atakuwa ni kati ya wale wasioelekezeka?»
Alipokuja malkia wa Saba ’.kwa Sulaymān kwenye kikao chake aliambiwa, «je, kitanda cha ufalme wako kiko hivi?» Akasema, «Hicho kinafanana nacho.» Ikambainikia Sulaymān kuwa amejibu jawabu la sawa na ameshajua uweza wa Mwenyezi Mungu na usahihi wa unabii wa Sulaymān , amani imshukiye. Na tulipewa elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na kujuwa uweza Wake kabla yake yeye, na tulikuwa ni wenye kuifuata amri ya Mwenyezi Mungu ni wenye kuifuata dini ya Uislamu.»
Na kilimzuia yeye kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake kile alichokuwa akikiabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka,. Kwa hakika yeye alikuwa ni kafiri na alikulia kati ya watu makafiri na akaendelea kwenye dini yao, isipokuwa hivyo, yeye ana werevu na busara ya kuijua haki na kuipambanua na batili, lakini itikadi za ubatilifu zinaondoa nuru ya moyo.
Akaambiwa, «Ingia kwenye jumba.» na ukumbi wake ulikuwa wa ukoa, chini yake palikuwa na maji. Alipouona ukumbi alidhania ni maji yanayopiga mawimbi, na akafunua miguu yake ili kuingia majini. Sulaymān akamwambia, «Huo ni ukumbi laini wa ukoa ulio safi na maji yako chini yake.» Akatambua ukubwa wa ufalme wa Sulaymān na akasema, «Mola wangu! Nimeidhulumu nafsi yangu kwa ushirikina niliokuwa nao, na nimesalimu amri kwa kumfuata Sulaymān kwa kuingia kwenye dini ya Mola wa viumbe wote.»
Hakika tulimtumiliza kwa watu wa Thamūd ndugu yao Ṣāliḥ kwamba: Mpwekesheni Mwenyezi Mungu na musimchukue mungu mwingine mukamuabudu pamoja na Yeye. Alipowajia Ṣāliḥ kuwalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake, watu wake walikuwa mapote mawili: mojawapo ya mapote mawili lilimuamini na lingine liliukanusha ulinganizi wake, kila mmoja kati ya watu wa mapote hayo mawili alikuwa akidai kwamba haki iko pamoja na yeye.
Ṣāliḥ alisema kuliambia pote lililokanusha, «Kwa nini mnaharakisha ukanushaji na kufanya matendo mabaya ambayo yatawaletea adhabu na mnachelewesha kuamini na kufanya matendo mema ambayo yatawaletea malipo mazuri? Si mutake msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwanzo na mtubie kwake kwa matumaini ya kurehemewa.»
Wakasema watu wa Ṣāliḥ kumwambia, «Tumepata ukorofi kwa sababu yako wewe na watu walioko na wewe kati ya wale walioingia katika dini yako.» Ṣāliḥ aliwaambia, «Wema Anaowapatia Mwenyezi Mungu au uovu, basi hua umekadiriwa kwenu na Mwenyezi Mungu na Atawapa malipo yake. Bali nyinyi ni watu ambao mtapewa mtihani wa mambo ya furaha na maudhiko na mema na maovu.
Na katika mji wa Ṣāliḥ, nao ni mji wa Ḥijr, ulioko Kaskazini magharibi ya bara Arabu, kulikuwa na wanaume tisa, shughuli yao ni kufanya uharibifu katika ardhi usiochanganyika na wema wowote wa kutengeneza.
Watu tisa hawa wakaambiana wao kwa wao, «Apianeni kwa Mwenyezi Mungu, kila mmoja awaapie wengine:’Tunaapa tutamjia Ṣāliḥ kwa ghafla, kipindi cha usiku, tumuue yeye na tuwaue watu wake kisha tutamuambia atakayesimama kutaka kisasi cha damu yake miongoni mwa jamaa zake: ‘Hatukushuhudia kuuawa kwao.’ Na sisi tutakuwa ni wakweli kwa tuliyoyasema.»
Basi wakazipanga hila hizi za kumuangamiza Ṣāliḥ na watu wake kwa kuwafanyia vitimbi, tukamuokoa Nabii wetu Ṣāliḥ, amani imshukie, na tukawapatiliza kwa mateso kwa ghafla na hali wao hawatazamii vitimbi vyetu kwao kama malipo ya vitimbi vyao.
Basi tazama , ewe Mtume, mtazamo wa mazingatio, mwisho wa njama za ukatili za kundi hili kumfanyia Nabii wao Ṣāliḥ. Sisi tuliwaangamiza wao na watu wao wote.
Hayo ni makazi yao, yako matupu, hakuna yoyote ndani yake. Mwenyezi Mungu Amewaangamiza kwa sababu ya wao kuzidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na kumkanusha Nabii wao. Kwa kweli, katika uvunjaji huo na uangamizaji pana mawaidha kwa watu wanaokijua kile tulichowafanya. Na huu ndio mwendo wetu kwa wenye kuwakanusha Mitume.
Na tukamuokoa, na yale maangamivu yaliyowafika kina Thamūd, Ṣāliḥ na waliomuamini waliokuwa wakijikinga, kwa Imani yao, na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na mkumbuke na umtaje Lūṭ, aliposema kuwaambia watu wake, «Hivi nyinyi mnaleta kitendo ambacho ni upeo wa ubaya, nanyi mnajua ubaya wake?
Hivi nyinyi mnawajia wanaume kwenye tupu zao za nyuma kwa matamanio badala ya wanawake? Bali nyinyi ni watu msiojua haki ya Mwenyezi Mungu juu yenu, ndipo mkaenda kinyume na amri Yake na mkamuasi Mtume Wake kwa kitendo chenu kibaya ambacho hakuwatangulia nacho yoyote katika viumbe.»
Watu wa Lūṭ hawakuwa na jawabu la kumpa isipokuwa ni kuambiana wao kwa wao, «Watoeni wafuasi wa Lūṭ kwenye mji wenu, kwani wao ni watu wanaojiepusha na kuwajilia wanaume.» Waliwaambia hilo kwa njia ya kuwafanyia shere.
Tukamuokoa Lūṭ na watu wake waliomfuata na adhabu ambayo itawashukia watu wa Lūṭ waliomkanusha, isipokuwa mkewe tuliomkadria kuwa ni mwenye kusalia kwenye adhabu mpaka aangamie pamoja na wenye kuangamia, kwa kuwa yeye alikuwa ni msaidizi wa watu wake kwa matendo yao mabaya na alikua akiridhika nayo.
Na tukawateremshia kutoka mbinguni mvua ya mawe ya udongo yenye kuangamiza. Ilikuwa mbaya mno mvua ya hao walioonywa ambao hoja iliwasimamia.
Sema, ewe Mtume, «Sifa njema na shukrani ni za Mewenyezi Mungu, na amani kutoka Kwake na usalama ziwashukie waja Wake Aliowateua kwa kuwapa utume.» Kisha waulize washirikina wa watu wako, «Je, Mwenyezi Mungu Anayemiliki kunufaisha na kudhuru ni bora au ni yule wanayemshirikisha badala Yake kati ya wale wasiojimilikia wenyewe wala kuwamilikia wengine nafuu yoyote wala madhara yoyote?»
Na waulize wao , «Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na Akawateremshia maji kutoka mbinguni, Akaotesha kwa hayo maji mabustani yenye mandhari mazuri?» Hamkuwa nyinyi ni wenye kuipanda miti yake lau si Mwenyezi Mungu kuwateremshia maji kutoka mbinguni. Kumuabudu Mwenyezi Mungu ndio ukweli na kumuabudu asiyekuwa Yeye ndio urongo. Je, kuna muabidiwa pamoja na Mwenyezi Mungu alifanya vitendo hivi mpaka aabudiwe pamoja na Yeye na ashirikishwe na Yeye? Bali washirikina hawa ni watu wanapotoka na njia ya haki na Imani ndio wakamfanya Mwenyezi Mungu ni sawa na asiyekuwa Yeye katika kuabudiwa na kutukuzwa.
Je, kuviabudu vile mnavyovishirikisha na Mola wenu ni bora au Yule Aliyewafanyia ardhi kuwa ni mahali pa kutulia, Akaitoa mito kati yake, Akaiwekea majabali yaliyojikita na Akaweka kizuizi baina ya bahari mbili, ya tamu na chumvi, ili mojawapo isiiharibu nyingine? Je kuna muabudiwa yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu alifanya hilo hata mumshirikishe na Yeye katika kuabudu kwenu? Bali wengi wa hawa washirikina hawajui kadiri ya ukubwa wa Mwenyezi Mungu, hivyo basi wanamshirikisha Yeye kwa kuiga na kwa udhalimu.
Je, kuviabudu vile mnavyovishirikisha na Mwenyezi Mungu ni bora au Yule Anayemjibu mwenye shida anapomuomba, Anayemuondolea maovu yaliyomshukia na Anayewafanya nyinyi ni wenye kushikilia nafasi za waliowatangulia nyinyi katika ardhi? Je, kuna muabudiwa yoyote pamoja na Yeye Anayewaneemesha neema hizi? Ni uchache sana kwenu nyinyi kukumbuka na kuzingatia, na kwa hivyo, mlimshirikisha Mwenyezi Mungu na mwingine katika kumuabudu.
Je, kuviabudu vile mnavyomshirikisha navyo Mwenyezi Mungu ni bora au Yule Anayewaongoza katika giza la bara na bahari mnapopotea na njia ikawa na giza kwenu, Ambaye Anapeleka upepo wenye kutoa bishara njema ya kile ambacho Mwenyezi Mungu Anawarehemu waja Wake kwacho, nacho ni mvua yenye kuhuisha ardhi iliyokufa? Je, kuna muabudiwa yoyote pamoja na Mwenyezi Mungu anayewafanyia chochote katika hayo mkamuomba badala yake? Ameepukana Mwenyezi Mungu na kutakasika na hivyo ambavyo wao wanamshirikisha navyo asiyekuwa Yeye.
Na waulize wao: Ni nani anayeanzisha kuumba viumbe, kisha anaviondosha akitaka, kisha anavirudisha? Na ni nani anayewaruzuku nyinyi kutoka mbinguni kwa kuiteremsha mvua? Na ni nani anayehuisha ardhi kwa kuotesha mimea na vinginevyo? Je, kuna muabudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu anafanya hayo? Sema, Leteni hoja yenu iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu Ana mshirika katika mamlaka Yake na ibada Yake.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Hakuna yoyote ajuwaye, mbinguni wala ardhini, jambo lolote lililofichika ambalo Mwenyezi Mungu Amejihusisha Mwenyewe kulijua. Na wao hawajui ni lini watafufuliwa kutoka makaburini mwao wakati wa Kiyama kusimama.»
Bali ujuzi wao wa Kiyama utakamilika huko Akhera, huko watakuwa na yakini juu ya Nyumba ya Akhera na vituko vilivyomo watakapoishuhudia. Na wao walipokuwa duniani walikuwa na shaka nayo, bali akili zao zilikuwa zimepofuka hawaiyoni.
Na walisema wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, «Je, sisi na wazazi wetu tutafufuliwa, tukiwa hai kama tulivyo, baada ya kufa kwetu, baada ya sisi kuwa mchanga?
Tuliahidiwa kufufuliwa huku, sisi na wazazi wetu, hapo kabla(tulipokuwa duniani) hatukuuona uhakika wake wala kutokea kwake. Hatukuona ahadi hii isipokuwa ni hadithi za urongo zilizozuliwa na kuandikwa na watu wa kale ndani ya vitabu vyao.
Waambie, ewe Mtume, hawa wakanushaji, «Tembeeni kwenye ardhi mziangalie nyumba za wahalifu waliokuwa kabla yenu muone ulikuwa vipi mwisho wa wenye kuwakanusha Mitume? Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa ukanushaji wao, na Mwenyezi Mungu Atawafanya nyinyi kama wao iwapo hamtaamini.»
Usiwe na masikitiko juu ya kukupa mgongo kwao, hao washirikina, na kukukanusha, na usiwe na dhiki moyo wako juu ya vitimbi vyao wanavyokufanyia, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukupa ushindi juu yao.
Na washirikina wa watu wako, ewe Mtume, wanasema «Itakuwa lini ahadi hii ya adhabu mnayotuahidi kwayo, wewe na wafuasi wako, mkiwa nyinyi ni wakweli katika yale mnayotuahidi?»
Waambie, ewe Mtume, «Huenda yakawa ni karibu kwenu baadhi ya yale mnayoyafanyia haraka ya adhabu ya Mwenyezi Mungu.»
Na hakika ya Mola wako ni Mwenye nyongeza za wema kwa watu, kwa kuacha kuwaharakishia wao adhabu kwa kumuasi kwao Yeye na kumkanusha. Lakini wengi wao hawamshukuru kwa hilo wakamuamini na wakamtakasia ibada.
Na kwa hakika, Mola wako ni Yeye Anayekijua kile ambacho vifua vyao vinakificha na kile ambacho vinakifichua wazi.
Na hakuna kitu chochote kilichofichika na macho ya viumbe, kilichoko mbinguni na ardhini,isipokuwa kiko kwenye Kitabu kilicho waziwazi kilichoko kwa Mwenyezi Mungu. Kitabu hiko kimevizunguka vyote vilivyokuwa na vitakavyokuwa.
Kwa hakika, hii Qur’ani inawapa Wana wa Isrāīl habari ya ukweli katika mambo mengi zaidi ambayo wao wametafautiana juu yake.
Na kwa hakika, hii Qur’ani ni uongofu kutoka kwenye upotevu na ni rehema inayotoa kwenye adhabu kwa mwenye kuiamini na akajiongoza kwa uongofu wake.
Hakika Mola wako Anahukumu baina ya wanaotafautiana, miongoni mwa Wana wa Isrāīl na wasiokuwa wao, kwa uamuzi wake kati yao. Akamlipiza kwa kumtesa mtenda makosa na kumlipa mema mtenda wema. Na Yeye Ndiye Mwenye nguvu Anayeshinda, uamuzi Wake haurudishwi, Aliye Mjuzi, kwa hivyo ukweli na urongo hazimchanganyikii.
Jitegemeze, ewe Mtume, katika mambo yako yote kwa Mwenyezi Mungu na uwe na imani Kwake, kwani Yeye ni Mwenye kukutosha. Hakika wewe uko kwenye njia iliyo wazi isiyokuwa na shaka.
Hakika yako wewe, ewe Mtume, huwezi kumsikilizisha haki yule ambaye Mwenyezi Mungu Amepiga mhuri juu ya moyo wake Akaufisha, na humsikilizishi ulinganizi wako yule ambaye Mwenyezi Mungu Ameyafanya masikizi yake kuwa kiziwi asiisikie haki, pindi wanapogeuka kukupa mgongo wewe. Kwani kiziwi hasikii ulinganizi akiwa amekuelekea, basi itakuwa vipi akiwa katika hali ya kupa mgongo na kugeuka?
Na wewe, ewe Mtume, hukuwa ni mwenye kuongoa kutoka kwenye upotevu yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemfanya kipofu asiuone uongofu na unyofu. Na haimkini kwako wewe umsikilizishe isipokuwa yule anayeziamini aya zetu, basi hao ni wenye kusalimu amri, watiifu na wenye kuyakubali yale ninayowalingania wao.
Na itakapopasa adhabu juu yao, kwa sababu ya kuvama kwao ndani ya madhambi na uasi na kuzipa mgongo kwao sheria za Mwenyezi Mungu na hukumu Zake mpaka wakawa ni miongoni mwa wabaya wa viumbe vyake, tutawatolea wao, katika kipindi cha mwisho wa zama, alama, miongoni mwa alama kubwa za Kiyama, nayo ni Mnyama atakayesema na wao kwamba watu wanaokanusha kufufuliwa ni wakanushaji wa Qur’ani na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hawaaamini wala hawafanyi matendo mema.
Na siku tutakayokusanya- Siku ya Ufufuzi- katika kila jamii, kundi la watu, miongoni mwa wale wanaozikanusha aya zetu na hoja zetu, watazuiliwa wa mwanzo wao wachanganywe na wa mwisho wao, wapate kukusanyika wote, kisha waongozwe hadi pale pa kuhesabiwa.
Mpaka litakapokuja, miongoni mwa kila jamii, pote la wale wanaozikanusha aya zetu na wakakusanyika, Mwenyezi Mungu Atasema, «Je, mumezikanusha aya zangu nilizoziteremsha kwa Mitume wangu na alama nilizozisimamisha zenye kuonyesha upweke wangu na ustahiki wangu peke yangu kuabudiwa na hali nyinyi hamkuwa na ujuzi wa kutosha kuwa ni batilifu, hata iwafanye mzipe mgongo na mzikanushe au ni kitu gani mlikuwa mkifanya?»
Hapo lithibiti juu yao neno la adhabu kwa sababu ya udhalimu wao na ukanushaji wao, na watakuwa hawatamki neno lenye hoja ya wao kujitetea nafsi zao ili kujiepushia adhabu kali iliyowashukia.
Je, hawakuona hawa wakanushaji wa aya zetu kwamba sisi tumeufanya usiku ni kipindi cha wao kutulia ndani yake na kulala, na mchana ni kipindi cha wao kuona ili waende kutafuta maisha yao? Hakika katika kuvipelekesha hivyo viwili kuna ushahidi kwa watu wanaoamini ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu, upweke Wake na ukubwa wa neema Zake.
Na kumbuka, ewe Mtume, siku ambayo Malaika atakapovuvia kwenye pembe, hapo wababaike walioko mbinguni na ardhini babaiko kubwa sana kwa kituko cha Mvuvio huo, isipokuwa yule aliyevuliwa na Mwenyezi Mungu kati ya wale Aliyowakirimu na Akawahifadhi na hilo babaiko. Na viumbe wote watamjia Mwenyezi Mungu wakiwa wanyonge watiifu.
Na utayaona majabali ukidhania kuwa yamesimama na yametulia na hali yanatembea mwendo wa kasi kama vile yanavyotembea mawingu yanayopelekwa na upepo. Na huu ni katika utengenezaji wa Mwenyezi Mungu Ambaye Ametengeneza uumbaji wa kila kitu na Akaufanya mzuri madhubuti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, enyi watu, yawe mazuri au mabaya na Atawalipa kwa hayo.
Mwenye kuja na upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na kumuamini na kumuabudu Peke Yake na matendo mema Siku ya Kiyama, basi Atakuwa na malipo mema makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yatakaokuwa mema na bora zaidi, nayo ni Pepo. Na wao, Siku ya babaiko kubwa, watakuwa kwenye amani,
Na mwenye kuja na ushirikina na matendo mabaya yanayochukiza, basi malipo yao ni awatupe Motoni Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Na wataambiwa kwa kulaumiwa, «Je, mtalipwa isipokuwa kile mliokuwa mkikifanya duniani?»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mola wa mji huu, nao ni Makkah, ambao Ameuharamisha kwa viumbe wake wasimwage humo damu iliyo haramu kuimwaga au kumdhulumu yoyote ndani yake au kuwinda viindwa vyake au kukata mti wake. Na ni Chake Yeye kila kitu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Na nimeamrishwa nimuabudu Yeye Peke Yake, na sio mwingine, na niwe mtiifu Kwake,
na niwasomee watu Qur’ani, basi mwenye kuongoka kuyajua yaliyomo ndani yake na akayafuata niliokuja nayo, wema wa hilo na malipo yake yatamfaa mwenyewe. Na mwenye kupotea akapotoka na njia ya haki, basi wewe sema, «Mimi ni muonyaji kwenu, nawaonya na adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake iwapo hamtaamini, kwani mimi ni mmoja wa Mitume waliowaonya watu wao, na uongofu wa aina yoyote hauko mikononi mwangu.
Na sema, ewe Mtume, «Sifa nzuri ni za Mwenyezi Mungu, atawaonyesha alama Zake ndani ya nafsi zenu na kwenye mbingu na ardhi, na mtazijua ujuzi wenye kuwaonyesha haki na kuwafafanulia ubatilifu. Na Mola wako si mwenye kughafilika na hayo mnayoyafanya na Atawalipa nyinyi kwa hayo.