ترجمة سورة العنكبوت

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة العنكبوت باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

«Alif, Lām, Mīm.» Yametangulia maelezo juu ya herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah.
Je wanadhani watu kwamba wakisema «Tumeamini» Mwenyezi Mungu Atawaachilia bila ya kuwajaribu wala kuwatahini?
Kwa hakika, tuliwajaribu wale waliokuwa kabla yao miongoni mwa ummah mbalimbali na tukawatahini kwa Mitume wetu tuliowatumiliza kwao. Basi hakika ni kwamba Mwenyezi Mungu Atawajua, ujuzi wa kujitokeza nje kwa viumbe, ukweli wa wale wakweli katika Imani yao na urongo wa warongo, ili Alipambanue kila kundi na lingine.
Je, kwani wanadhani wale wanaofanya mambo ya uasi, ya ushirikina na mengineyo, kuwa watatushinda wajikwepeshe na sisi tusiwaweze? Ni uamuzi mbaya mno wanaouamua.
Yoyote mwenye kuwa na matumaini ya kukutana na Mwenyezi Mungu na akawa na matarajio ya kupata malipo Yake mema, basi muda Aliouweka Mwenyezi Mungu wa kuwafufua viumbe Wake ili wahesabiwe na walipwe ni wenye kuja hivi karibuni. Na Yeye Ndiye Msikizi wa maneno, Mjuzi wa vitendo.
Na mwenye kupigana jihadi katika njia ya kuinua neno la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na akapigana jihadi na nafsi yake kwa kuisukuma ifanye vitendo vya utiifu, basi anapigana jihadi kwa maslahi ya nafsi yake. Kwa kuwa yeye anafanya hilo kwa kutaka thawabu ya kupigana kwake jihadi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja ya matendo mema ya waja Wake, kwani mamlaka ni Yake, uumba na mapitisho.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, kwa hakika tutawafutia makosa yao na tutawalipa kwa matendo yao mema, mazuri zaidi ya yale waliokuwa wakiyafanya.
Na tumemsihi binadamu awatendee wema wazazi wake wawili na awe mwema kwao wa maneno na vitendo. Na wakikusukuma kwa bidii, ewe binadamu, umshirikishe mwingine na mimi katika ibada yangu, basi usifuate amri yao. Matakwa ya kuwa Mwenyezi Mungu ashirikishwe yanashikanishwa na matakwa ya kuwa vitendo vingine vya maasia vifanywe. Kwani hakuna kutiiwa kiumbe namna atakavyokuwa katika jambo la kumuasi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama lilivyothibiti hilo kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Kwangu mimi ndio mwisho wenu, Siku ya Kiyama, na huko niwape habari ya matendo mema na mabaya ambayo mlikuwa mkiyafanya duniani na niwalipe kwa hayo.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wakafanya matendo mema, tutawatia Peponi wakiwa ni katika jumla ya waja wa Mwenyezi Mungu wema.
Na miongoni mwa watu, kuna anayesema, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu.» Na afanyiwapo udhia na washirikina huwa akipapatika kutokana na mateso yao na makero yao, kama anavyopapatika kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu na asivumilie makero yake, akaritadi na akaiacha Imani yake. Na lau waja ushindi kutoka kwa Mola wako, ewe Mtume, kwa watu wenye kumuamini, watasema hawa wenye kuritadi kuiacha Imani yao, «Sisi tulikuwa pamoja na nyinyi, enyi Waumini, tukiwasaidia dhidi ya maadui wenu.» Je, si Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi kuliko yoyote wa kuyajua yaliyomo ndani ya vifua vya viumbe wake wote?
Na Atawajua Mwenyezi Mungu, tena atawajua, ujuzi wenye kujitokeza kwa viumbe, wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo, na Atawajua, tena Atawajua, wanafiki, ili Alipambanue kila kundi na lingine.
Na wanasema wale waliokataa upweke wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa Makureshi, na wasiliamini onyo la Mwenyezi Mungu na ahadi Yake, kuwaambia wale waliomuamini Mwenyezi Mungu miongoni mwao na wakafuata Sharia Zake kivitendo, «Iacheni Dini ya Muhammad, na fuateni dini yetu, kwani sisi tutayabeba makosa yenu,» na wao si wenye kubeba chochote katika dhambi zao. Kwa kweli, wao ni warongo kwa yale waliyoyanena.
Na wataibeba, tena wataibeba, washirikina hawa mizigo ya nafsi zao na madhambi yake na mizigo ya wale waliowapoteza na wakawazuia wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu pamoja na mizigo yao wenyewe, bila ya wale waliowafuata nyinyi kupunguziwa mizigo yao kitu chochote. Na wataulizwa, tena wataulizwa, Siku ya Kiyama, kuhusu yale ya urongo waliokuwa wakiyazua.
Na hakika tulimtumiliza Nūḥ kwa watu wake, akakaa kwao miaka elfu moja kasoro miaka hamsini, akiwaita kwenye upwekeshaji wa Mwenyezi Mungu na akiwakataza ushirikina, na wao wasimuitikie. Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwa mafuriko, na wao wako katika hali ya kujidhulumu wenyewe kwa ukafiri wao na kupita kiasi kwao katika uasi.
Hivyo basi tukamuokoa Nūḥ na waliomfuata miongoni mwa wale waliokuwa naye jahazini. Na tukalifanya hilo kuwa ni mazingatio na mawaidha kwa viumbe wote.
Mkumbuke na umtaje, ewe Mtume, Ibrāhīm, amani imshukie, alipowalingania watu wake kwamba: mtakasieni Ibada Mwenyezi Mungu Peke Yake, na muogope hasira Zake kwa kutekeleza faradhi Zake na kujiepusha na vitendo vya kumuasi. Hilo ni bora kwenu ikiwa mnakijua kilicho chema kwenu kutokana na kilicho kibaya kwenu.
Hamuabudu, enyi watu, badala ya Mwenyezi Mungu isipokuwa masanamu na mnazua urongo kwa kuwaita wao waungu. Kwa hakika, hawa masanamu wenu mnaoaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, hawawezi kuwaruzuku nyinyi kitu chochote, basi tafuteni riziki kwa Mwenyezi Mungu na sio kwa masanamu wenu na mumtakasie ibada na shukrani kwa kuwaruzuku. Ni kwa Mwenyezi Mungu mtarudishwa baada ya kufa kwenu, na hapo awalipe kwa yale ambayo mlifanya.
Na mkimkanusha, enyi watu, Mtume wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika kile alichowalingania mkifuate cha kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake, basi kuna makundi ya watu kabla yenu waliowakanusha Mitume wao katika kile walichowaitia, na kwa hivyo zikawashukia hasira za Mwenyezi Mungu. Na Mtume Muhammad hana jukumu lingine isipokuwa ni kuwafikishia nyinyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ujumbe Wake ufikishaji wenye uwazi, na ashafanya hilo.
Kwani hawa hawajui ni vipi Mwenyezi Mungu Anaanzisha uumbaji viumbe kutoka katika hali ya kutokuwako, kisha Atawarudisha baada ya kutoweka kwao, kama alivyoanzisha mara ya kwanza uumbaji mpya na kwamba kulifanya hili si jambo lisilowezekana na Yeye? Hakika hilo kwa Mwenyezi Mungu ni lepesi kama lilivyokuwa lepesi lile la kuanzisha uumbaji wake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wenye kukanusha kufufuliwa baada ya kufa, «Endeni katika ardhi, muangalie namna Mwenyezi Mungu Alivyoanzisha uumbaji na Asielemewe kuuanzisha hapo mwanzo?» Hivyo basi Hataelemewa na kule kuuanzilisha upya uanzilishaji mwingine. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hakuna jambo lolote Alitakalo linalomshinda.
Anamuadhibu Anayemtaka kati ya viumbe Vyake kwa makosa waliyoyafanya siku za uhai wao, na Anawarehemu Anaowataka miongoni mwao, kati ya wale waliotubia, wakaamini na wakafanya matendo mema. Na Kwake Yeye mtarejeshwa muhesabiwe na mulipwe kwa mliyoyafanya.
Na hamkuwa nyinyi, enyi watu, ni wenye kumshinda Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu iwapo mtamuasi. Na nyinyi hamuna badala ya Mwenyezi Mungu mtegemewa yoyote wa kuyasimamia mambo yenu, wala msaidizi wa kuwaokoa nyinyi na Mwenyezi Mungu iwapo Anawatakia mabaya.
Na wenye kukanusha hoja za Mwenyezi Mungu na kupinga dalili Zake, hao hawatakuwa na matarajio ya rehema yangu huko Akhera watakapoishuhudia adhabu iliyoandaliwa kwao, na wao watakuwa na adhabu yenye uchungu na iumizayo.
Basi jawabu ya watu wa Ibrāhīm haikuwa isipokuwa ni kuambiana wao kwa wao, «Muueni au mchomeni kwa moto!» Wakamtupa motoni, na Mwenyezi Mungu Akamuokoa nao, na akaufanya kuwa ni baridi na salama kwake. Hakika katika kumuokoa kwetu Ibrāhīm kutokana na moto pana dalili na hoja kwa watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kufanya matendo yanayoambatana na Sheria Yake.
Na Akasema Ibrāhīm kuwaambia watu wake, «Enyi watu wangu! Kwa hakika, nyinyi mumewaabudu waungu wa ubatilifu, mumewafanya wao ni waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, mnapendana juu ya kuwaabudu na mnajipendekeza kwa kuwatumikia. Kisha, Siku ya Kiyama, baadhi yenu watajiepusha na wengine na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi, na mwisho wenu ni Moto, na hamtakuwa na msaidizi wa kuwazuia kuuingia.
Lūṭ akamuamini Ibrāhīm na akaufuata mwenendo wake. Na Ibrāhīm akasema, «Mimi nitaiwacha nchi ya watu wangu na nitaenda kwenye ardhi iliyobarikiwa, nayo ni Shām, kwani Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake.
Na tukamtunukia yeye Isḥāq, mtoto wake, na Y'qub, mtoto wa mtoto wake. Na tukawafanya, katika kizazi chake, Mitume na tukawaletea Vitabu. Na tukampa yeye malipo mema ya mitihani aliyoipata kwa ajili yetu, nayo ni kutajwa vizuri na kuwa na wana wema duniani. Na kwa hakika, yeye huko Akhera ni miongoni mwa watu wema.
Mkumbuke na umtaje Lūṭ, ewe Mtume, alipowaambia watu wake, «Kwa hakika, nyinyi mnaleta kitendo kichafu, hakuna yoyote katika viumbe aliyetangulia kukifanya.
Je, ni vipi nyinyi mnawajilia wanaume kupitia sehemu zao za nyuma, mnavamia njia za wasafiri kwa kitendo chenu kiovu na mnafanya vitendo vibaya kwenye mabaraza yenu, kama vile kuwacheza shere watu, kuwarushia mawe wapita njia na kuwakera kwa maneno na vitendo kwa namna isiyofaa?» Katika haya kuna tangazo kwamba haifai watu kukusanyika juu ya jambo baya ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wamelikataza. Watu wa Lūṭ hawakuwa na jawabu la kumpa isipokuwa ni kusema, «tuletee adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli katika hayo unayoyasema na ni miongoni mwa watekelezaji katika ahadi unayoitoa.»
Akasema, «Mola wangu! Nipe ushindi juu ya watu waharibifu kwa kuwateremshia adhabu, kwa kuwa wameuzua uchafu huu na wameendelea nao» Na Mwenyezi Mungu Akaikubali dua yake.
Na Malaika walipomjia Ibrāhīm na habari ya furaha itokayo kwa Mwenyezi Mungu ya (kuzaliwa) Isḥāq, na nyuma ya Isḥāq ni mwanawe, Ya’qūb, walisema wale Malaika, «Sisi ni wenye kuwaangamiza watu wa kijiji cha watu wa Lūṭ, nacho ni Sadūm, kwa kuwa watu wake wamekuwa ni wenye kujidhulumu wenyewe kwa kumuasi Mwenyezi Mungu.»
Akasema Ibrāhīm kuwaambia Malaika, «Huko kuna Lūṭ, na yeye si miongoni mwa madhalimu.» Malaika wakasema, «Sisi tunamjua zaidi aliye huko. Tutamuokoa, yeye na watu wa nyumbani kwake, na maangamivu yatakayowashukia watu wa kijiji chake, isipokuwa mke wake atakayesalia kwenye maangamivu.
Na Malaika walipomjia Lūṭ, hilo lilimkera, kwa kuwa yeye aliwadhania ni wageni wanadamu na akaingiwa na masikitiko kwa kuwako kwao kwa kuwa ajua ubaya wa kitendo cha watu wake, na wao wakamwambia, «Usituogopee, kwani watu wako hawatatufikia. Na wala usiwe na masikitiko kwa kuwa tunakupasha habari kuwa sisi ni wenye kuwaangamiza wao. Sisi ni wenye kukuokoa wewe na hiyo adhabu itakayowashukia watu wako na ni wenye kuwaokoa watu wa nyumbani kwako pamoja nawe isipokuwa mke wako, kwani yeye ni mwenye kuangamia akiwa na wale wenye kuangamia katika watu wake.
«Sisi ni wenye kuwateremshia watu wa kijiji hiki adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kumuasi kwao Mwenyezi Mungu na kufanya kwao machafu.»
Na tulizibakisha, katika nyumba za watu wa Lūṭ, athari zilizo wazi kwa watu wanaoelewa mambo ya kuwapa mazingatio na kunufaika kwayo.
Na tulimtumiliza, kwa watu wa Madyan, ndugu yao, Shu'ayb. Akawaambia, «Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu Peke Yake, na mumtakasie Ibada, kwani nyinyi hamuna Mola isipokuwa Yeye. Na kuweni na matarajio mema, kwa ibada mnazofanya, kupata malipo mazuri ya Siku ya Akhera, na msifanye uharibifu na maasia kwa wingi, na msijikite juu ya hayo. Lakini tubieni kwa Mwenyezi Mungu kwa makosa hayo na mrudi Kwake.
Wakamkanusha Shu'ayb watu wa Madyan kwa yale aliyokuja nayo ya utume kutoka kwa Mweyezi Mungu, basi wakapatikana na msukosuko mkali, wakawa wamelala chini kwenye nyumba zao hali ya kuwa wameangamia.
Na tukawaangamiza kina 'Ād na Thamūd, na yameshaonekana na nyinyi magofu ya nyumba zao, vile yalivyokuwa matupu, hayana mtu yoyote katika wakazi wake, na vile mateso yetu yalivyowashukia wao wote. Na Shetani aliwapambia wao matendo yao maovu, na kwa hivyo akawazuia wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu na njia ya kumuamini Yeye na Mitume Wake, na walikuwa wakijiongoza kuona njia katika ukafiri wao na upotevu wao wakijifurahisha nayo, wakidhani kwamba wao wako kwenye uongofu na usawa, ilhali wao wamezama kwenye upotevu.
Na tulimuangamiza Qārūn, Fir'awn na Hāmān. Na wote hao Mūsā aliwajia na dalili waziwazi, wakajifanya wakubwa katika ardhi na wakafanya kiburi humo. Na hawakuwa wao ni wenye kutuponyoka, bali sisi tulikuwa tuna uweza juu yao.
Kila mmoja, kati ya hao waliotajwa, tulimkamata kwa dhambi zake: kati yao kuna wale tuliyowatumia mawe ya udongo ulioshikana, nao ni watu wa Lūṭ, na kati yao kuna waliopatwa na ukelele, nao ni watu wa Ṣāliḥ na watu wa Shu'ayb , na kati yao kuna tuliowadidimiza ardhini kama vile Qārūn, na katika wao kuna tuliowazamisha majini, nao ni watu wa Nūḥ na Fir'awn na jamaa zake. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kuwaangamiza hawa kwa dhambi wengine akawa ni mwenye kuwadhulumu kwa kuwaangamiza wao bila kustahili, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe kwa kujistarehesha kwa neema za Mola wao na kumuabudu asiyekuwa Yeye.
Mfano wa wale waliowafanya masanamu ni wategemewa badala ya Mwenyezi Mungu, wakawa wanatarajia msaada wao, ni kama mfano wa buibui aliyejitengenezea nyumba ili imuhifadhi, isimfalie kitu alipokuwa na haja nayo. Hivyo basi ndivyo walivyo hawa washirikina, hawakuwafalia kitu wale waliowachukuwa kuwa ni wasaidizi wao badala ya Mwenyezi Mungu. Na kwa hakika, nyumba iliyo dhaifu zaidi ni nyumba ya buibui, na lau wao wangalikuwa wakilijua hilo hawangaliwafanya wao ni wasaidizi wenye kutegemewa badala ya Mwenyezi Mungu, kwani wao hawawanufaishi wala hawawadhuru.
Hakika Mwenyezi Mungu Anavijua vile wanavyomfananisha navyo washirikina na kumshirikisha navyo, na kwamba hivyo , kwa hakika, si kitu chochote, bali ni majina tu waliyoyaita, havinufaishi wala havidhuru. Na Yeye Ndiye Mshindi Mwenye uweza wa kuwatesa waliomkufuru, Ndiye Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengenezaji Wake.
Na mifano hii tunawapigia watu , ili wanufaike nayo na wajifunze kwayo. Na hawaielewi isipokuwa wale wanaomjua Mwenyezi Mungu na kuzijua aya Zake na Sheria Zake.
Mwenyezi Mungu Ameumba mbingu na ardhi kwa uadilifu na usawa. Hakika katika uumbaji Wake huo kuna ushahidi mkubwa, kwa wanaoamini, wa uweza Wake na kupwekeka kwake kwa uungu. Na Amewahusu Waumini kwa kuwataja kwa kuwa wao ndio wanaonufaika na huo ushahidi.
Isome hii Qur’ani iliyoteremshwa kwako, na uifuate kivitendo, na utekeleze Swala kwa mipaka yake, kwani utunzaji wa Swala unamkataza mtu kuingia kwenye vitendo vya uasi na makatazo. Hivyo ni kwamba mwenye kuzitimiza nguzo zake na masharti yake, moyo wake unang’ara, Imani yake inazidi, hima yake ya kufanya mema inapata nguvu na matamanio yake ya kufanya mabaya yanapungua au yanaondoka. Na kwa hakika, kumtaja Mwenyezi Mungu katika Swala na isiyokuwa Swala ni jambo kubwa na bora kuliko kitu chochote. Na Mwenyezi Mungu Anayajua mnayoyatenda ya uzuri na ubaya, hivyo basi Atawalipa kwa hayo malipo makamilifu zaidi na yanayotosha zaidi.
Na wala msijadiliane, enyi Waumini, na Mayahudi na Wanaswara isipokuwa kwa njia nzuri na maneno mazuri na kulingania kwenye haki kwa njia sahali yenye kupelekea kwenye lengo hilo, isipokuwa wale ambao wamekaa kando na haki wakafanya ushindani na kiburi na wakatangaza vita juu yenu, basi hao piganeni nao kwa upanga mpaka waamini au watoe jizia (kodi maalumu) kwa mkono na wao wakiwa katika hali ya unyonge. Na semeni, «Tumeiamini Qur’ani iliyoteremshwa kwetu, na tumeiamini Taurati na Injili ambazo mliteremshiwa, na Mola wetu na Mola wenu ni Mmoja Hana mshirika Wake katika uungu Wake, wala katika sifa Yake ya kuwa ni Mola, wala majina Yake na sifa Zake. Na sisi ni wenye kunyenyekea na kujifanya wanyonge Kwake kwa kumtii katika yale Aliyotuamrisha na Aliyotukataza.
Na kama tulivyowateremshia Kitabu, ewe Mtume, wale Mitume waliokuwa kabla yako, vilevile tumekuteremshia Kitabu hiki chenye kusadikisha Vitabu vilivyotangulia. Basi wale tuliyowapa Kitabu miongoni mwa Wana wa Isrāīl wakamjua vile inavyotakikana wamjue, wanaiamini Qur’ani. Na kati ya hawa Warabu wa Kikureshi kuna wanaomuamini. Na hawaikanushi Qur’ani au kuzifanyia shaka dalili zake na hoja zake zenye ushahidi uliyo wazi isipokuwa makafiri ambao mienendo yao ni kukataa na kufanya ushindani.
Na miongoni mwa miujiza yako iliyo wazi, ewe Mtume, ni kuwa wewe hukusoma kitabu wala hukuandika herufi zozote kwa mkono wako wa kulia kabla ya hii Qur’ani kukuteremkia, na hali wao wanalijua hilo. Na lau ungalikuwa ni mwenye kusoma au kuandika kabla hujaletewa wahyi wangalilifanyia shaka hilo hao wapotofu na wangalisema, «Amejifunza hiyo (Qur’ani) au ameinakili kutoka kwenye vitabu vilivyotangulia.»
Lakini Qur’ani ni aya zilizofunuka zilizo wazi katika kuutolea ushahidi ukweli, wanavyuoni wanaihifadhi. Na hawazikanushi aya zetu na kuzikataa isipokuwa washindani wanaoijua haki na kuiepuka.
Na washirikina walisema, «Si ateremshiwe Muammad dalili na hoja kutoka kwa Mola wake, kama vile ngamia wa Ṣāliḥ na fimbo ya Mūsā!» Waambie, «Jambo la miujiza hii liko kwa Mwenyezi Mungu, Akitaka Ataiteremsha na Akitaka Ataizuia. Na hakika ni kwamba mimi ni muonyaji, ninawatahadharisha na ukali wa adhabu Yake na mateso Yake, na ni mwenye kuwaonyesha njia ya haki na batili.»
Kwani haikuwatosha washirikina hawa ili wajue ukweli wako, ewe Mtume, kuwa sisi tumekuteremshia Qur’ani inayosomwa kwao? Hakika katika hii Qur’ani kuna rehema kwa Waumini, ulimwenguni na Akhera, na kuna ukumbusho wa kujikumbusha nao wa mazingatio na mawaidha.
Sema, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi baina yangu mimi na nyinyi juu ya ukweli wangu wa kuwa mimi ni Mtume Wake, na juu ya kunikanusha kwenu mimi na kuirudisha kwenu haki niliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Anavijuwa vilivyomo mbinguni na ardhini», hakuna kinachofichamana na Yeye chochote kile kilichoko ndani ya hivyo viwili. Na wale waliouamini urongo na wakamkanusha Mwenyezi Mungu, pamoja na kuwepo dalili hizi zilizo wazi, hao ndiyo wenye hasara ulimwenguni na Akhera.
Na wanakuharakisha, ewe Mtume, hawa washirikina wa watu wako uwaletee adhabu kwa kukufanyia shere. Na lau si Mwenyezi Mungu kuwa Amewawekea wakati wa kuadhibiwa wao duniani usiotangulia wala kuchelewa, ingaliwajia wao adhabu pale walipoitaka. Na kwa hakika itawajia ghafula na hali wao hawaitambui wala kuihisi.
Wanakuharakisha uwaletee adhabu ulimwenguni, na hali hiyo ni yenye kuwajia hapana budi, ima hapa ulimwenguni au huko Akhera. Na kwa hakika adhabu ya Jahanamu huko Akhera ni yenye kuwazunguka, hawana makimbilio nayo.
Hiyo Siku ya Kiyama, adhabu ya Jahanamu itawafinika makafiri upande wa juu ya vichwa vyao na upande wa chini ya nyayo zao. Hivyo basi Moto utawazunguka pande zao zote, na Mwenyezi Mungu Atasema kuwaambia wakati huo, «Onjeni malipo ya yale mliokuwa mkiyafanya ulimwenguni, ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kufanya uhalifu na madhambi.
«Enyi waja wangu mlioamini! Iwapo muna shida ya kudhihirisha Imani na ibada ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, basi hamieni kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu iliyo kunjufu na munitakasie ibada mimi peke yangu.»
Kila nafsi iliyo hai ni yenye kuonja kifo, kisha kwetu sisi mtarejea muhesabiwe na mulipwe.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema waliyoamrishwa kwayo, tutawatayarishia katika Pepo vyumba vilivyo juu, ambavyo chini yake inapita mito, hali ya kukaa humo milele.Neema ya malipo ya wenye kufanya utiifu kwa Mwenyezi Mungu ni Vyumba hivi vilivyoko ndani ya Mabustani ya starehe.
Mabustani hayo yaliyotajwa ni ya Waumini waliovumilia katika kumuabudu Mwenyezi Mungu, wakashikamana na dini yao na wakawa wanamtegemea Mwenyezi Mungu katika riziki zao na kupigana jihadi na maadui wao.
Ni viumbe vingapi vitambaavyo visivyojiwekea akiba ya chakula chao cha kesho, kama vile mwanadamu anavyofanya. Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kuwa juu, Anaviruzuku kama Anavyowaruzuku nyinyi. Na Yeye ni Msikizi wa maneno yenu, ni Mjuzi wa vitendo vyenu na mawazo ya nyoyo zenu.
Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina,»Ni nani aliyeumba mbingu na ardhi kwa mpango huu mzuri na akalidhalilisha jua na mwezi?» Watasema, «Aliyeviumba hivyo ni Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Basi vipi wao watapotoshwa waache kumuamini Mwenyezi Mungu, Muumba na Muendeshaji wa kila kitu, na wakawa wanamuabudu asiyekuwa Yeye? Basi uonee ajabu uzushi wao na urongo wao!
Mwenyezi Mungu, aliyetakasika na kuwa juu, Anampanulia riziki Anayemtaka na Anawabania wengine katika wao, kwa kuwa Anayajua yanayowafaa waja Wake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, katika hali zenu na mambo yenu, ni Mjuzi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake.
Na ukiwauliza, ewe Mtume, hao washirikina, «Ni nani anayeteremsha maji kutoka mawinguni, yakaotesha mimea juu ya ardhi baada ya kuwa imekauka?» watakwambia huku wakikubali, «Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Anayeyateremsha hayo.» Sema, «Shukrani ni za Mwenyezi Mungu Aliyedhihirisha hoja yako kwao. Lakini wengi wao hawafahamu yanayowafaa wala yanayowadhuru, na lau waelewa hawangalimshirikisha Mwenyezi Mungu na Mwengine.
Na haukuwa uhai huu wa ulimwengu isipokuwa ni pumbao na mchezo wa kuzifanya nyoyo zipumbae na miili icheza, kwa sababu ya pambo na matamanio, kisha yanaondoka haraka. Na kwa hakika, nyumba ya Akhera ndiyo uhai wa kikweli na wa daima usikokuwa na kifo ndani yake. Lau watu wanalijua hilo hawangalifadhilisha nyumba ya kutoweka juu ya Nyumba ya kusalia.
Na wanapopanda makafiri kwenye majahazi baharini, na wakaogopa kuzama, wanampwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia dua wakati wa shida yao. Na Anapowaokoa akawafikisha kwenye nchi kavu, na shida ikawaondokea, wanarudi kwenye ushirikina wao. Hakika yao wao, kwa kufanya hivi, wanagongana, wanampwekesha Mwenyezi Mungu kipindi cha shida na wanamshirikisha kipindi cha raha.
Na kushirikisha kwao baada ya sisi kuwaneemesha kwa kuwaokoa na bahari, ni ili iwe mwisho wake ni kuzikanusha zile tulizowaneemesha katika nafsi zao na mali zao na ili wakamilishe kujistarehesha kwao katika hii dunia. Basi wataujua uharibikaji wa matendo yao na kile Alichowaandalia wao Mwenyezi Mungu cha adhabu kali Siku ya Kiyama. Na katika hilo pana onyo na tahadharisho kwao.
Kwani hawakushuhudia makafiri wa Makkah kwamba Mwenyezi Mungu Amewawekea Makkah kuwa ni mahali patakatifu penye amani, watu wake wanapata amani humo ya nafsi zao na mali zao, hali watu walio pambizoni mwake, nje ya eneo takatifu, wananyakuliwa hawana amani? Je, ni ushirikina wanaouamini na ni neema ya Mwenyezi Mungu Aliyowahusu wao nayo, wanayoikanusha, wakawa hawamuabudu Yeye, Peke Yake, bila mwingine?
Hakuna yoyote aliye na udhalimu mkubwa kuliko yule aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na akamnasibishia Mwenyezi Mungu upotevu alio nao na ubatilifu, au akaikanusha haki ambayo Mwenyezi Mungu Amemleta nayo Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Hakika ndani ya Moto ni makao ya aliyemkanusha Mwenyezi Mungu na akaukataa upweke Wake na akamkanusha Mtume Wake Muhammad,rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Na Waumini waliopigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu, nafsi na Shetani na wakavumilia kwenye misukosuko na makero katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Atawaongoa kwenye wema na kuwasimamisha imara juu ya njia iliyolingana sawa. Na yoyote ambaye sifa yake ni hii, basi yeye amejifanyia wema nafsi yake na amewafanyia wema wengine. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kuwa juu, Yupo pamoja na wale viumbe wake waliofanya wema, kwa kuwapa ushindi, kuwatilia nguvu, kuwahifadhi na kuwaongoza.
Icon