وَرَفَعَ أَبَوَيۡهِ عَلَى ٱلۡعَرۡشِ وَخَرُّواْ لَهُۥ سُجَّدٗاۖ وَقَالَ يَـٰٓأَبَتِ هَٰذَا تَأۡوِيلُ رُءۡيَٰيَ مِن قَبۡلُ قَدۡ جَعَلَهَا رَبِّي حَقّٗاۖ وَقَدۡ أَحۡسَنَ بِيٓ إِذۡ أَخۡرَجَنِي مِنَ ٱلسِّجۡنِ وَجَآءَ بِكُم مِّنَ ٱلۡبَدۡوِ مِنۢ بَعۡدِ أَن نَّزَغَ ٱلشَّيۡطَٰنُ بَيۡنِي وَبَيۡنَ إِخۡوَتِيٓۚ إِنَّ رَبِّي لَطِيفٞ لِّمَا يَشَآءُۚ إِنَّهُۥ هُوَ ٱلۡعَلِيمُ ٱلۡحَكِيمُ
Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mwenyezi Mungu ameijaalia iwe kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia wema kunitoa gerezani, na kukuleteni kutoka jangwani baada ya Shet'ani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Bila ya shaka Yeye ni Mjuzi Mwenye hikima.
Ali Muhsin Al - Swahili translation
Akawakalisha wazazi wake wawili kwenye kitanda cha ufalme wake kwa njia ya kuwatukuza. Na wazazi wake na ndugu zake kumi na moja wakamsalimia kwa kumuinamia kwa kumwamkia na kumtukuza na sio kumuabudu na kumnyenyekea. Na hilo lilikuwa linaruhusiwa katika Sheria yao, na limeharamishwa katika Sheria yetu, kwa ajili ya kuziba njia inayopelekea kwenye ushirikina. Na Yūsuf akamwambia baba yake, «Kusujudu huku ndio uaguzi wa ndoto yangu niliyokusimulia kabla, katika udogo wangu, Mwenyezi Mungu Ameifanya ni kweli. Na amenifadhili aliponitoa jela na akawaleta nyinyi kutoka jangwani, baada ya Shetani kuharibu uhusiano wa undugu baina yangu mimi na ndugu zangu. Hakika Mola wangu ni Mpole wa kupitisha Analolitaka. Yeye Anayajua sana maslahi ya waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na vitendo Vyake.»
الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس