يُوصِيكُمُ ٱللَّهُ فِيٓ أَوۡلَٰدِكُمۡۖ لِلذَّكَرِ مِثۡلُ حَظِّ ٱلۡأُنثَيَيۡنِۚ فَإِن كُنَّ نِسَآءٗ فَوۡقَ ٱثۡنَتَيۡنِ فَلَهُنَّ ثُلُثَا مَا تَرَكَۖ وَإِن كَانَتۡ وَٰحِدَةٗ فَلَهَا ٱلنِّصۡفُۚ وَلِأَبَوَيۡهِ لِكُلِّ وَٰحِدٖ مِّنۡهُمَا ٱلسُّدُسُ مِمَّا تَرَكَ إِن كَانَ لَهُۥ وَلَدٞۚ فَإِن لَّمۡ يَكُن لَّهُۥ وَلَدٞ وَوَرِثَهُۥٓ أَبَوَاهُ فَلِأُمِّهِ ٱلثُّلُثُۚ فَإِن كَانَ لَهُۥٓ إِخۡوَةٞ فَلِأُمِّهِ ٱلسُّدُسُۚ مِنۢ بَعۡدِ وَصِيَّةٖ يُوصِي بِهَآ أَوۡ دَيۡنٍۗ ءَابَآؤُكُمۡ وَأَبۡنَآؤُكُمۡ لَا تَدۡرُونَ أَيُّهُمۡ أَقۡرَبُ لَكُمۡ نَفۡعٗاۚ فَرِيضَةٗ مِّنَ ٱللَّهِۗ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمٗا
Mwenyezi Mungu anakuusieni juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na ikiwa wanawake zaidi ya wawili, basi watapata thuluthi mbili za alicho kiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi ya alicho kiacha, ikiwa anaye mtoto. Akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wamekuwa ndio warithi wake, basi mama yake atapata thuluthi moja. Na akiwa anao ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alicho usia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani baina yao aliye karibia zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
Ali Muhsin Al - Swahili translation
Mwenyezi Mungu Anawausia na kuwaamrisha, kuhusu wana wenu atakapokufa mmoja wenu na akaacha watoto wa kiume na wa kike, kwamba urithi wote ni wao: mtoto wa kiume atapata mfano wa fungu la watoto wawili wa kike, iwapo itakuwa hakuna mawarithi wengine isipokuwa ni wao tu. Iwapo atawaacha watoto wa kike peke yao, basi watoto wa kike wawili au zaidi watapata theluthi mbili ya alichokiacha.. Na iwapo mrithi ni binti mmoja, basi atapata nusu ya mali, na wazazi wawili wa maiti, kila mmoja atapata sudusi. Hii ni iwapo maiti ana mtoto wa kiume au wa kike, mmoja au zaidi. Iwapo maiti hana mwana, na wakawa mawarithi wake ni wazazi wake wawili, basi mamake atapata theluthi na babake atapata kilichosalia. Na iwapo maiti ana ndugu, wawili au zaidi, wawe ni wanawake au ni wanaume, basi mamake atapata sudusi, baba atapata kilichosalia na ndugu hawatapata kitu. Mgawanyo huu wa mali yalioachwa hufanyika baada ya kutoa wasia aliousia maiti katika kiwango cha theluthi, au baada ya kutoa deni adaiwalo. Baba zenu na watoto wenu ambao wamepangiwa kurithi, hamjui ni yupi katika wao mwenye manufaaa ya ukaribu zaidi na nyinyi katika dunia yenu na Akhera yenu. Kwa hivyo, msimfanye mmoja kati yao ni bora kuliko mwengine. Hili mliousiwa nalo limefaradhiwa kwenu na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa viumbe Wake, ni Mwenye hekima katika Sheria Alizowaekea.
الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس