ترجمة معاني سورة الملك
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
Zimekithiri kheri za Mwenyezi Mungu na wema Wake kwa viumbe Vyake, Ambaye mkononi Mwake upo ufalme wa duniani na Akhera na mamlaka ya viwili hivyo, Anapitisha amri Yake na uamuzi Wake kwenye mamlaka Yake hayo, na Yeye kwa kila jambo ni Muweza. Faida inayopatikana katika aya hii ni kuwa inathibitisha sifa ya mkono kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kutukuka, kwa namna inavyonasibiana na utukufu Wake.
Aliyeumba mauti na uhai ili awatahini nyinyi, enyi watu, ni yupi miongoni mwenu aliye mwema wa matendo na utakasaji wa nia? Na Yeye Ndiye Mshindi Ambaye hakuna chochote kinachomshinda, Ndiye Mwingi wa msamaha kwa anayetubia miongonu mwa waja Wake. Katika aya hii pana kuhimiza kufanya utiifu na makaemeo ya kutenda maasia.
Aliyeumba mbingu saba zilizopangika, baadahi yake juu ya nyingine, huoni katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, ewe mwenye kuangalia, tofauti yoyote wala mpambanuko, basi rudia tena kuangalia mbinguni: je unaona pasuko zozote au nyufa?
Kisha rudia kuangalia tena, mara baada ya mara, yatakurudia hayo macho yakiwa manyonge na matwevu hayakuona upungufu wowote na hali yakiwa ni yenye usumbufu na uchovu.
Na hakika tumeupamba uwingu wa karibu unaoonekana na macho kwa nyota kubwa zenye kung’ara, na tumezifanya nyota hizo ni vimondo zenye kuwachoma wenye kusikiliza kwa kuiba miongoni mwa mashetani, na tumewaandalia wao huko Akhera adhabu ya Moto wenye kuwaka wakawa ni wenye kuadhibika kwa joto lake.
Na wenye kumkanusha Mola wao watapata adhabu ya moto wa Jahanamu, na ubaya zaidi wa mahali pa mtu kurejea ni ni huo moto wa Jahanamu!
Waingizwapo hao wakanushaji ndani ya moto wa Jahanamu, watausikia ukitoa sauti kali yenye kutisha , huku ukichemka machemko makali sana.
unakaribia huo moto wa Jahanamu kurarukararuka kwa ukali wa hasira ulizonazo juu ya wakanushaji. Kila linapotiwa humo kundi la watu, wale wawakilishi wa kusimamia mambo ya huo moto wa Jahanamu watawauliza kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia: Je kwani hakuwajia nyinyi, huko duniani, mjumbe wa kuwatahadharisha na adhabu hii ambayo nyinyi mmo ndani yake?
Watawajibu kwa kusema, «Ndio! Tumejiwa na Mjumbe anayetoka kwa Mwenyezi mungu akatuonya na tukamkanusha na tukasema kuhusu miujiza aliyokuja nayo: Mwenyezi Mungu hakumteremshia binadamu kitu chochote. Hamkuwa nyinyi, enyi Mitume, isipokuwa mmeenda mbali na haki.
Na watasema kwa kukubali makosa, «Lau tungalikuwa tunasikia usikivu wa mwenye kutafuta haki, au tunafikiria juu ya yale tunayoitiwa kwayo, hatungekuwa ni kati ya watu wa Motoni.»
Hivyo basi wakakubali kukanusha kwao na kukufuru kwao kulikowafanya wastahili adhabu ya Moto. Basi kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwa watu wa Motoni!
Hakika wale wanaomuogopa Mola wao, wakamuabudu na wasimuasim na hali wako mbali na macho ya watu na wanaiogopa adhabu ya Akhera kabla hawajaiona, watapata msamaha wa dambi zao katoka kwa Mwenyezi Mungu na malipo mema makubwa ambayo ni Pepo.
Na yaficheni maneno yenu, enyi watu, katika jambo lolote miongoni mwa mambo yenu , au yadhihirisheni, kwani yote mawili mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa. Hakika Yeye , kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi wa yaliyomo ndani ya vifua, basi yatafichamana vipi maneno yenu na matendo yenu Kwake Yeye!
Je, kwani hajui, Mola wa viumbe, viumbe Vyake na mambo yao na hali ni kuwa Yeye Ndiye Aliyewaumba, Akalitengeneza umbo lao na Akalifanya zuri? Na Yeye Ndiye Mpole kwa waja Wake, Ndiye Mwenye kuwatambua wao na matendo yao.
Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Aliyewafanyia ardhi iwe nyepesi iliyotayarishwa mpate kutulia juu yake. Basi tembeeni sehemu zake na pande zake na mle riziki ya Mwenyezi Mungu Anayowatolea humo. Na Kwake Yeye Peke Yake ndio Ufufuzi kutoka makaburini mwenu ili mhesabiwe na mlipwe. Katika hii aya pana ishara ya kuhimiza utafutaji riziki na uchumaji. Pia pana dalili kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Muabudiwa wa haki Peke Yake Asiye na mshirika, na pana dalili ya uweza Wake, kukumbusha neema Zake na kuonya kuelemea duniani.
Je mmesalimika, enyi makafiri wa Makkah, na Mwenyezi Mungu Aliye mbinguni kuwa Hatawadidimiza ardhini ikawa inatetemeka na nyinyi mpaka mkaangamia?
Au mmesalimika kuwa Mwenyezi Mungu Aliye juu ya mbingu kuwa Hatawatumia upepo wenye kuwapiga mawe madogomadogo na hapo mkajua, enyi makafiri, ni vipi onyo langu kwenu mnapoiona adhabu? Na huko kujua wakati huo hakutawanufaisha. Katika hii aya pana kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Yuko juu kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake, kutakasika ni Kwake.
Kwa hakika walikanusha wale waliokuwa kabla ya makafiri wa Makkah kama vile watu wa Nuchouh, 'Ād na Thamūd walivyowakanusha Mitume wao. Basi kulikuwa namna gani kule kuwakasirikia kwangu na kuwageuzia kwangu neema waliyokuwa nayo kwa kuwateremshia adhabu na kuwaangamiza?
Je kwani walighafilika hawa makafiri wasiwatazame ndege juu yao wakiwa wanazikunjua mbawa zao angani na wakati mwingine wanazikunja na kuzitia mbavuni mwao? Hakuna mwenye kuwatunza wasianguke wakiwa katika hali hiyo isipokuwa Mwingi wa rehema.
Hakika Yeye Anaona kila kitu, hakuna upungufu wala tofauti.Bali ni nani huyu ambaye, kulingana na madai yenu, enyi makafiri, kuwa ni kundi lenu, anayewanusuru asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, iwapo Yeye Atawatakia baya? Makafiri hawakuwa, katika madai yao isipokuwa wako katika kudanganywa na kupotezwa na Shetani.
Bali ni nani huyo mpaji anayedaiwa atakayewapa nyinyi riziki iwapo Yeye Atazuia riziki Yake na Atawakatalia kuwapa? Bali makafiri wanaendelea kwenye ukiukaji wao na upotevu wao wakiwa katika hali ya ushindani, kujiona na kuikimbia haki, hawaisikii wala hawaifuati.
Je huyu anayetembea akiwa kichwa chake kimeinama hajui pa kuelekea wala namna ya kwenda yuko katika kulingana zaidi kwenye njia na ameongoka zaidi au ni yule anayetembea sawasawa, akiwa na kimo kilicholingana, aliye mzima, afuataye njia iliyofunuka wazi isiyokuwa na mpeteko? Na huu ni mfano Mwenyezi Mungu Amempigia kafiri na na Muumini.
Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewapatisha nyinyi kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na akawafanya nyinyi muwe na mashikio ili msikie kwayo, macho ili muonee na nyoyo ili muelewe kwazo. Basi ni uchache, enyi makafiri, mnavyomtekelezea shukrani Mola wenu kwa neema hizi alizowaneemesha.
Waambie, «Mwenyezi Mungu ndiye Aliyewaumba na Akawaeneza ardhini. Na Kwake Yeye, PekeYake, mtakusanywa baada ya huku kutengana, ili mhesabiwe na mlipwe.»
Na wanasema hao makafiri, «Ni lini itakapohakikika ahadi hii, ewe Muhammad? Tupeni habari ya kipindi chake, enyi Waumini, iwapo nyinyi ni wakweli katika yale mnayoyadai.»
Waambie hao, ewe Mtume, «Hakika ujuzi wa kipindi cha kusimama Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake Ndiye Anayehusika nacho. Na hakika si lingine ni kwamba mimi ni muonyaji kwenu, ninawaogopesha mwisho mbaya wa ukafiri wenu na ninawaeleza kile Alichoniamrisha Mwenyezi Mungu nikibainishe upeo wa kubainisha.
Watakapoiona makafiri adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa iko karibu nao na wakaishuhudia, utajitokeza unyonge na unguliko kwenye nyuso zao na waambiwe, kwa njia ya kuwalaumu na kuwakaripia, «Hii ndiyo ile mliokuwa mkitaka iharakishwe ulimwenguni.»
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa makafiri, «Nipasheni habari, iwapo Mwenyezi Mungu Atanifisha pamoja na Waumini walio pamoja na mimi, kama mnavyotamani, au Ataturehemu avicheleweshe vipindi vyetu vya kufa na Atuepushie adhabu yake, basi ni nani huyo ambaye atawahami aizuie adhabu kali yenye kuumiza isiwafikie?»
Sema, «Ni Mwenyezi Mungu! Yeye Ndiye Mwingi wa rehema. Tumemuamini na tumeifuata Sheria Yake kivitendo na tumemtii. Na Kwake yeye, Peke Yake, tumetegemea katika mambo yetu yote. Basi mtajua, enyi makafiri, itakapoteremka adhabu, ni yupi kati ya makundi mawili miongoni mwetu: sisi na nyinyi, yuko mbali waziwazi na njia ya Mwenyezi Mungu iliyonyoka.»
Sema, ewe Mtume, Uwaambie hawa washirikina, «Nipasheni habari iwapo maji yenu mnayokunywa ni yenye kupotea ndani ya ardhi, mkawa hmyafikii kwa namna yoyote, basi ni nani asiyekuwa Mwenyezi Mungu Atakayewaletea maji yenye kutembea ardhini na yenye kuonekana na macho»