ترجمة سورة الحديد

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الحديد باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viumbe Vyake vyote vilivyoko mbinguni na ardhini. Na Yeye ni Mshindi juu ya viumbe Vyake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo yao.
Ni Yake mamlaka ya mbinguni na ardhini na vilivyomo ndani yake. Yeye Ndiye Mmiliki Mwenye kuendesha mambo ya viumbe Vyake, Anahuisha na kufisha, na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna kinachomshinda Akikitaka kifanyike, Anachokitaka kinakuwa, na Asichokitaka hakiwi.
Yeye Ndiye wa Mwanzo Ambaye hakukuwa na chochote kabla Yake, na Ndiye wa Mwisho Ambaye hakuna kitu chochote baada Yake, na Ndiye Aliyejitokeza Ambaye hakuna kitu chochote juu Yake, na Ndiye wa ndani Ambaye hakuna kitu chochote kilicho karibu kuliko Yeye, na hakuna chochote kinachofichamana Kwake ardhini wala mbinguni, na Yeye ni Mjuzi wa kila kitu.
Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi kisha Akawa juu ya 'Arsh Yake iliyo juu ya viumbe Vyake vyote kuwa Juu kunakonasibiana na utukufu Wake. Anavijua vinavyoingia ardhini, miongoni mwa mbegu, mvua na visivyokuwa hivyo, na vinavyotoka humo miongoni mwa mimea, nafaka na matunda, na vinavyoshuka kutoka mbinguni, miongoni mwa mvua na vinginevyo, na vinvyopanda huko, miongoni mwa Malaika na matendo ( ya awaja), na Yeye , kutakasika ni Kwake, Yuko pamoja na nyinyi kwa ujuzi Wake popote mnapokuwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu mnayoyafanya na Atawalipa kwayo.
Ni Yake mamlaka ya mbinguni na ardhini, na Kwake Mwenyezi Mungu ndiko mwisho wa mambo ya viumbe huko Akhera na Atawalipa wao kwa matendo yao.
Anazitia saa za usiku zilizopungua ndani ya mchana na hivyo basi mchana ukaongezeka, na Anazitia saa za mchana ndani ya usiku, na hivyo basi usiku ukaongezeka. Na Yeye , kutakasika ni Kwake, ni Mjuzi wa yaliyomo ndani ya vifua vya viumbe Vyake.
Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mtoe katika mali amabayo Mwenyezi Mungu Amewaruzuku na Akawafanya nyinyi ni wasimamizi wa mali hayo. Basi wale walioamini miongoni mwenu, enyi watu, na wakatoa mali yao watapata malipo makubwa.
Na mna udhuru gani ya nyinyi kutokaubali upweke wa Mwenyezi Mungu na kutofuata sheria Zake kivitendo na hali Mtume anawalingania juu ya hilo na Mwenyezi Mungu Ashachukua ahadi zenu juu ya hilo, iwapo nyinyi ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu Muumba wenu?
Yeye Ndiye Anayemteremshia mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, aya za Qur’ani zilizopambanuliwa zilizo wazi, ili Awatoe nyinyi kwa hizo kwenye giza la ukafiri na kuwatia kwenye mwangaza wa Imani. Na hakika Mwenyezi Mungu, kwa kule kuwatoa nyinyi kwenye giza na kuwatia kwenye mwangaza, Anawarehemu rehema kunjufu katika maisha yenu ya sasa ya ulimwenguni na maisha yenu ya baadaye, na awalipe malipo mazuri kabisa.
Na ni kitu gani kinachowazuia nyinyi kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu? Hakika ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye urithi wa mbingu na ardhi, Anavirithi vyote vilivyomo humo, na hatasalia yoyote kuwa ni mwenye kumiliki chochote humo. Hawalingani kimalipo na thawabu wale waliotoa kabla ya ufunguzi wa Makkah na wakapigana na wakanushaji na wasiokuwa wao, kwani wao wana daraja kubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wale waliotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu baada ya ufunguzi na wakapigana na wakanushaji, na kila mojawapo ya makundi mawili haya Mwenyezi Mungu Ameliahidi Pepo. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa matendo yenu, hakuna chchote katika hayo kinachofichamana Kwake, na Atawalipa nyinyi kwa hayo.
Ni yupi yule anayetoa katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kutaka thawabu kutoka ndani ya moyo wake bila kusimanga wala kuudhi, ili Amuengezee Mola wake malipo na thawabu na apate malipo mema nayo ni Pepo?
Siku utakapowaona Waumini wa kiume na Waumini wa kike ikitembea nuru yao juu ya njia ya Ṣirāṭ mbele yao na upande wao wa kulia kwa kadiri ya matendo yao mema na waambiwe, «Bishara yenu leo ni kuingia kwenye mabustani ya Peponi yaliyo makunjufu ambayo chini ya miti yake inapita mito, hamtatolewa humo milele.» Malipo hayo ndiyo kufuzu kwenu kukubwa huko Akhera.
Siku watakaposema wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike wakiwaambia Waumini, «Tungojeeni tupate mwangaza wa nuru yenu!» Hapo Malaika wawaambie, «Rudini nyuma yenu mtafute nuru (kwa njia ya kuwafanyia shere). Hapo watenganishwe baina yao kwa kuwekwa kizuizi cha ukuta wenye mlango ambao ndani yake , upande wa Waumini, mna rehema, na nje yake, upande wa wanafiki kuna adhabu.
Hapo wale wanafiki wawaite Waumini kwa kusema, «Kwani hatukuwa na nyinyi duniani tukitekeleza ibada za Dini kama nyinyi?» Na Waumini wawaambie, «Ndio, mlikuwa na sisi kidhahiri, lakini nyinyi mlijiangamiza wenyewe kwa unafiki na kufanya maasia, na mkingojea kwa hamu Nabii afe na Waumini wapatikane na mikasa, mkakufanyia shaka kule kufufuliwa baada ya kufa, na yakawadanganya nyinyi matumaini yenu ya urongo na mkasalia katika hali hiyo mpaka mauti yakawajia. Na Shetani aliwadanganya nyinyi kuhusu Mwenyezi Mungu.
Leo haitakubaliwa badala kutoka kwa yoyote miongoni mwenu, enyi wanafiki, ili ajifidie kwayo na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala kutoka kwa wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. mwisho wenu nyote ni Moto, huo ni makao mnayostahili zaidi kuliko makao yoyote, na mwisho mbaya kabisa ni huo.
Je haujafika wakati kwa wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafuata uongofu Wake kulainika nyoyo zao anapotajwa Mwenyezi Mungu na kuisikia Qur’ani, na wasiwe ni wenye ugumu wa nyoyo kama walivyokuwa wale waliopewa Vitabu kabla yao, kati ya Mayahudi na Wanaswara, ambao walipitiwa na muda mrefu wakayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu na nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi miongoni mwao wakatoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu? Katika aya hii pana kuhimiza ulainifu na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, wakati wa kuyasikia yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu ya Kitabu na Hekima, na kujihadhari na kujifananisha na Mayahudi na Wanaswara katika ususuwavu wa nyoyo zao na kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu.
Jueni kwamba Mwenyezi mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anaihuisha ardhi kwa mvua baada ya kufa kwake ikatoa mimea. Basi vilevile Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuhuisha wafu Siku ya Kiyama, na Ndiye Muweza wa kuzilainisha nyoyo baada ya kususuwaa kwake. Kwa hakika tumewafunulia wazi dalili za uweza wetu, huenda nyinyi mkazielewa na kwa hivyo mkawaidhika.
Hakika ya wale wanaume na wanawake wanaotoa sadaka kutokana na mali yao na wakatumia katika njia ya Mwenyezi Mungu matumizi zikiwa radhi nyoyo zao, kwa kutafuata radhi za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, wataongezewa malipo mema ya hayo, na juu ya hayo watapata malipo mengi, nayo ni Pepo.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wasimbague yoyote miongoni mwao, hao ndio wakweli iliyokamilika imani yao kwa kile walichokuja nacho Mitume, kiitikadi, kimaneno na kivitendo, na ndio mashahidi mbele ya Mola wao; watapata malipo yao mengi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na nuru yao kubwa Siku ya Kiyama. Na wale waliokufuru na kukanusha dalili zetu na hoja zetu, wao ndio watu wa Motoni, hawatakuwa na malipo mema wala nuru.
Jueni, enyi watu, kwamba uhai wa kilimwengu ni mchezo na pumbao ya miili kuchezea na nyoyo kupumbaa, na pambo la nyinyi kujipamba nalo, na kuoneshana baina yenu kwa vitu vyake vya starehe, na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama ule wa mvua ambayo mimea yake iliwafurahisha wakulima, kisha ikasinyaa na kukauka, ukaiona imekuwa rangi ya manjano baada ya kuwa rangi ya kijani, kisha ikawa ni yenye kukatikakatika na kuwa mikavu na kusagikasagika. Na huko Akhera kuna adhabu kali kwa makafiri na msamaha wa Mwenyezi Mungu na radhi Zake kwa watu wenye kuamini. Na haukuwa uhai wa kilimwengu, kwa mwenye kuushughulikia hali ya kusahau Akhera yake, isipokuwa ni starehe yenye udanganyifu.
Shindaneni, enyi watu, katika kukimbilia sababu za kusamehewa kwa kutubia kidhati na kujiepusha na maasia, ili mlipwe msamaha kutoka kwa Mola wenu na Pepo ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, nayo imetayarishiwa wale waliompwekesha Mwenyezi mungu na wakawafuata Mitume Wake. Hizo ni nyongeza za Mwenyezi Mungun Anazompa Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake. Pepo haipatikani isipokuwa kwa rehema ya mwenyezi Mungu na nyongeza Zake na matendo mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nyongeza kubwa kwa waja Wake Waumini.
Hampatikani na msiba wowote, enyi watu, kwenye ardhi wala ndani ya nafsi zenu, utokanao na magonjwa, njaa na ndwele, isipokuwa umeandikwa kwenye Ubao Uliyohifadhiwa kabla ya kuumbwa viumbe. Hakika hilo, kwa Mwenyezi Mungu, ni jambo sahali.
Ili msisikitike kwa mlichokikosa cha ulimwengu na msifurahike furaha ya kiburi na majivuno. Na mwenyezi mungu Hampendi kila mwenye kujiona kwa alichopewa cha ulimwengu, mwenye kujifahiri nacho juu ya wengine.
Hawa wenye kujiona ndio wale wanaoyafanyia ubahili mali yao, wasiyatoe katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wakawaamuru watu wawe mabahili kwa kuwapambia huo ubahili. Na yoyote anayezunguka nyuma kwa kuacha kumtii Mwenyezi mungu hamdhuru yoyote isipokuwa nafsi yake, na hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, kwani Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Asiyehitajia viumbe vyake, Mwenye kuhimidiwa Ambaye Ana kila sifa njema iliyokamilika na kila tendo zuri ambalo Anastahiki kushukuriwa kwalo.
Hakika tumetumiliza Mitume wetu kwa hoja zilizo wazi na kuwateremshia Vitabu vyenye hukumu na sheria, na tukateremsha mizani ili watu waamiliane baina yao kwa uadilifu, na tukateremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa mengi kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu Amjue, ujuzi wenye kujitokeza kwa watu, yule anayetetea Dini Yake na Mitume Wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Asiyetendeshwa nguvu, ni Mshindi hakuna anayeweza kushindana na Yeye.
Na hakika tuliwatumiliza Nūḥ na Ibrāhīm kwa watu wao, na tukajaalia kwenye kizazi chao unabii na vitabu vilivyoteremshwa. Basi miongoni mwa watu wa kizazi chao kuna walioongoka kwenye haki, na wengi kati yao wametoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu.
Kisha tukafuatisha, kwenye athari za Nūḥ na Ibrāhīm, Mitume wetu tiliowatumiliza kwa hoja zilizo wazi, na tukamfuatisha 'Īsā mwana wa Maryam na tukampa Injili, na tukajaalia ndani ya nyoyo za wale waliomfuata na kuwa kwenye dini yake ulaini na huruma, wakawa wanapendana wao kwa wao, na walizusha taratibu za kuabudu, kwa kupitisha kiasi katika ibada, ambazo hatukuwalazimisha nazo isipokuwa ni wao wenyewe waliojilazimisha nazo kwa lengo la kupata radhi za Mwenyezi Mungu, lakini hawakusimama nazo vile inavyotakiwa kusimama. Basi tukawapa wale walioamini miongoni mwao malipo yao kulingana na Imani yao, na wengi miongoni mwao ni wenye kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na ni wenye kumkanusha Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Enyi mlioamini! Fuateni amri za Mwenyezi Mungu na mjiepushe na makatazo Yake na muaminini Mtume Wake, Atawapa rehema Zake mara mbili zaidi, na Atawafanya muwe na nuru ambayo kwayo mnajiongoza na Atawasamehe dhambi zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewapa haya yote ili wapate kujua watu waliopewa Vitabu ambao hawakumuamini Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwamba wao hawawezi chochote kujipa wao wenyewe nyongeza za kheri za Mwenyezi Mungu wala kuwapatia wengine, na kwamba nyongeza zote ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wema mkubwa na vipewa vingi kwa viumbe Vyake.
Icon