أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٖ مِّن رَّبِّهِۦ وَيَتۡلُوهُ شَاهِدٞ مِّنۡهُ وَمِن قَبۡلِهِۦ كِتَٰبُ مُوسَىٰٓ إِمَامٗا وَرَحۡمَةًۚ أُوْلَـٰٓئِكَ يُؤۡمِنُونَ بِهِۦۚ وَمَن يَكۡفُرۡ بِهِۦ مِنَ ٱلۡأَحۡزَابِ فَٱلنَّارُ مَوۡعِدُهُۥۚ فَلَا تَكُ فِي مِرۡيَةٖ مِّنۡهُۚ إِنَّهُ ٱلۡحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَٰكِنَّ أَكۡثَرَ ٱلنَّاسِ لَا يُؤۡمِنُونَ
Basi je, mtu aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake Mlezi, inayo fuatwa na shahidi anaye toka kwake, na kabla yake kilikuwa Kitabu cha Musa kilicho kuwa mwongozi na rehema - hao wanamuamini, na anaye mkataa katika makundi, basi Moto ndio pahala pa miadi yao. Basi usiwe na shaka juu ya hayo. Hii ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi; lakini watu wengi hawaamini.
Ali Muhsin Al - Swahili translation
Je, yule aliyekuwa kwenye hoja na uangalifu kutoka kwa Mola wake katika kile anachokiamini na anachokilingania kwa wahyi ambao ndani yake Mwenyezi Mungu Ameuteremsha ushahidi huu, na ukafuatiwa na hoja nyingine kutoka Kwake yenye kuutolea ushahidi, nayo ni Jibrili au ni Muhammad, rehema na amani ziwashukie, na ukatiliwa nguvu na dalili ya tatu kabla ya Qur’ani, nayo ni Taurati - Kitabu alichotemshiwa Mūsā chenye uongozi na rehema kwa waliokiamini- (je yeye) ni kama yule ambaye hamu yake ilikuwa ni maisha yenye kutoweka na pambo lake? Hao wanaiamini hii Qur’ani wanazifuata hukumu zake kivitendo. Na mwenye kuikanusha hii Qur’ani, miongoni mwa wale waliojikusanya kumpinga Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, basi malipo yake ni Moto, hapana budi atauingia. Basi usiwe na shaka juu ya jambo la Qur’ani na kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka baada ya dalili na hoja kulitolea ushahidi hilo. Na ujue kwamba Dini hii ndio ukweli unaotoka kwa Mola wako, lakini wengi wa watu hawaamini wala hawayatendi yale wanayoamrishwa. Huu ni muongozo unaowaenea ummah wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس