ترجمة سورة الأحزاب

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الأحزاب باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Ewe Nabii! Endelea daima kwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwa kuyafanya maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, na waumini wakufuate kwa kuwa wao wanahitajia hilo zaidi kuliko wewe, na usiwatii makafiri na watu wa unafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, ni Mwenye hekima katika uumbaji Wake, amri Zake na uendeshaji mambo Wake.
Na uyafuate yale uliyoletewa wahyi kutoka kwa Mola wako, ya Qur’ani na Sunnah. Hakika Mwenyezi Mungu Anayaona mnayoyafanya na ni Mwenye kuwalipa kwa hayo, hakuna kitu kinachofichamana Kwake katika hayo.
Na umtegemee Mola wako, na umuachie Yeye mambo yako, na Yeye Anatosha kuwa Mtunzi kwa anayemtegemea na kurudia Kwake.
Mwenyezi Mungu hakumfanya yoyote miongoni mwa wanadamu awe na nyoyo mbili kifuani mwake, na hakuwafanya wake wenu mnaojiharamisha nao kwa njia ya ẓihār kama vile uharamu wa mama zenu. (Ẓihār ni mwanamume kumwambia mkewe, ‘Wewe ni haramu kwangu kama vile mgongo wa mamangu.’ Na hii ilikuwa ni talaka katika kipindi cha ujinga (kabla ya kuja Uislamu) na Mwenyezi Mungu Akabainisha kwamba mke hawi mama kwa namna yoyote. Na Mwenyezi Mungu Hakuwafanya watoto wa kubandika kuwa ni wana katika sheria. Bali ufananishaji na mgongo na ubandikaji wana, viwili hivyo havina uhakika katika uharamishaji wa milele, kwani mke aliyefananishwa na mgongo wa mama hawi ni kama mama katika uharamu, na nasaba haithubutu kwa kujibandika wana kwa mtu kusema kuhusu mwana wa kubandika, «Huyu ni mwanangu». Kwani haya ni maneno ya mdomo yasiyo na ukweli na hayazingatiwi. Na Mwenyezi Mungu Anasema haki na Anawabainishia waja Wake njia Yake na Anawaongoza njia ya uongofu.
Wale mnaodai kuwa ni wana wenu wanasibisheni na baba zao, hilo ni jambo la uadilifu zaidi na la sawa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Mkiwa hamuwajui baba zao wa kihakika, basi hapo waiteni kwa undugu wa Dini ambayo inawakusanya nyinyi na wao, kwani wao ni ndugu zenu katika Dini na pia ni marafiki zenu. Na nyinyi hamna dhambi kwa makosa mliyoyafanya bila kukusudia, lakini Mwenyezi Mungu Atawapatiliza mkifanya hilo kwa kusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa aliokosea, ni Mwingi wa rehema kwa mwenye kutubia dhambi Zake.
Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni bora kwa Waumini na ni karibu na wao zaidi kuliko nafsi zao katika mambo ya dini na dunia. Na heshima ya wake za Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa ummah wake, kama vile heshima ya mama zao, haifai kuwaoa wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada yake. Na wenye ujamaa wa ukaribu, miongoni mwa Waislamu, baadhi yao wana haki zaidi ya kuwarithi wengine katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake kuliko kurithi kwa (misingi ya) Imani na uhamiaji. (Waislamu hapo mwanzo wa Uislamu walikuwa wakirithiana kwa misingi ya hijrah (uhamiaji) na Imani au Dini na si kwa kizazi, kisha hilo likaondolewa kwa aya ya urathi), isipokuwa iwapo nyinyi, enyi Waislamu, mtawafanyia wema kwa kuwahami, kuwafanyia wema, kuwaunga na kuwaachia wasia wa kuwafaidisha. Hukumu hii iliyotajwa imekadiriwa, imeandikwa kwenye Ubao uliyohifadhiwa, basi ni lazima kwenu muifuate kivitendo. Ndani ya aya hii pana ulazima wa kuwa Mtume, rehema na amani zimshukie, awe ni mwenye kupendwa zaidi na mja kuliko nafsi yake, na ulazima wa kumfuata yeye kikamilifu. Na ndani yake pana ulazima wa kuwaheshimu mama za Waumini, wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kwamba mwenye kuwatukana atarudi na hasara.
Na kumbuka utaje, ewe Nabii, tulipochukua kutoka kwa Manabii ahadi ya mkazo kutekeleza ujumbe, na tukachukua ahadi kutoka kwako, na kutoka kwa Nūḥ, Ibrāhīm, Mūsā na Īsā mwana wa Maryam (nao ndio Mitume wenye nyoyo thabiti, katika kauli iliyo mashuhuri), na tukachukua kutoka kwao ahadi ya mkazo ya kufikisha ujumbe na kutekeleza amana na kuaminiana wao kwa wao.
Mwenyezi Mungu Alichukua ahadi hiyo kutoka kwa Mitume hao, ili Apate kuwauliza waliotumwa vile walivyojibiwa na ummah wao, ili Mwenyezi Mungu Awalipe Pepo wenye kuamini. Na Amewaandalia makafiri, Siku ya Kiyama, adhabu kali ndani ya Jahanamu.
Enyi Waumini! Ikumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliyowaneemesha nyinyi katika Madina siku ya vita vya Makundi (Aḥzāb), navyo ndivyo vita vya Shimo (Khandaq), walipojikusanya dhidi yenu washirikina kutoka nje ya Madina, na Mayahudi na wanafiki wakiwa ndani ya Madina na pambizoni mwake, wakawaviringa nyinyi, hapo tukayatumia yale makundi upepo mkali uliong’oa mahema yao na kuvirusha vyungu vyao, na tukawatumia Malaika kutoka mbinguni msiowaona, hapo basi nyoyo zao zikaingia kicho. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mnayoyatenda, hakuna chochote kinachofichamana kwake katika hayo.
Kumbukeni pindi walipowajia kwa juu yenu kutoka sehemu ya juu ya bonde lilioko upande wa mashariki na kwa chini yenu kutoka sehemu ya kati ya bonde lilioko upande wa magharibi, na pindi macho yalipokodoka kwa kuduwaa sana na kushutuka, na nyoyo zikafika kwenye magorombo (ya koo) kwa kitisho kikali, na wanafiki wakajawa na ukataji tamaa na uvumi ukazidi, na mkawa mnamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya ya kuwa Yeye Hataiokoa Dini Yake na Hatalikuza jina Lake.
Katika msimamo huo mgumu, Imani za Waumini zilijaribiwa na watu wakakaguliwa, na akajulikana mnafiki kwa kutengwa na Muumini, na wakasukikasukika msukosuko mkali kwa kuingiwa na kicho na babaiko, ili Imani yao ibainike na yakini yao izidi
Na pindi waliposema wanafiki na wale ambao ndani ya nyoyo zao mna shaka, nao ni wale madhaifu wa Imani, «Ahadi ya Mwenyezi Mungu Aliyotuahidi ya kupata ushindi na utulivu, haikuwa isipokuwa ni maneno ya urongo na udanganyifu, basi msimuamini.»
Na kumbuka, ewe Nabii, neno la kipote cha wanafiki wakiwaita Waumini miongoni mwa watu wa Madina, «Enyi watu wa Yathrib (nalo ni jina la zamani la Madina), ‘Msikae kwenye vita ambavyo mtashindwa, rudini majumbani mwenu ndani ya Madina’» Na pote lingine la wanafiki linamuomba ruhusa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kurudi majumbani mwao kwa kisingizio kuwa hayako imara, na kwa hivyo wanayaogopea, na ukweli ni kwamba hayo si hivyo, na lengo lao halikuwa isipokuwa ni kukimbia vita.
Na lau jeshi la makundi lingaliingia Madina kupitia pambizoni mwake, kisha wakatakwa hawa wanafiki wamshirikishe Mwenyezi Mungu na warudi kutoka kwenye Uislamu, wangalilikubali hilo kwa haraka, na hawangalichelewesha kurudi kwenye ushirikina isipokuwa kwa muda mchache.
Na kwa hakika, wanafiki hawa walimuahidi Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume Wake kabla ya vita vya Shimo (Khandaq) kuwa hawatakimbia watakapohudhuria vita na hawatachelewa watakapoitwa kwenda Jihadi, lakini wao walihini ahadi yao. Na Mwenyezi Mungu Atawahesabu kwa hilo na Atawauliza kuhusu ahadi hiyo. Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu itaulizwa na itahesabiwa.
Sema, ewe Nabii, kuwaambia hawa wanafiki, «Kukimbia kwenu vitani kwa kuogopa kufa au kuuawa, huko hakutachelewesha muda wenu wa kuishi katika dunia hii, na mkikimbia hamtastarehe katika dunia hii isipokuwa kwa kadiri ya umri wenu uliowekewa kikomo, nacho ni muda mchache sana ukilinganishwa na Akhera.»
Sema, ewe Nabii, kuwaambia wao, «Ni nani Atakayewazuia na Mwenyezi Mungu Au Atakayewaokoa na adhabu Yake Akiwa Anawatakia ubaya au Akiwa Anawatakia rehema?» Na hakika Yeye Ndiye Mpaji, Mzuiliaji, Mwenye kudhuru, Mwenye kunufaisha? Na hawatapata hawa wanafiki, isipokuwa Mwenyezi Mungu, msaidizi wa kuwasaidia wala mnusuru wa kuwapa ushindi.
Hakika Mwenyezi Mungu Anawajua wale wenye kuwavunja watu moyo wasipigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wenye kuwaambia ndugu zao, «Njooni mjiunge na sisi na muacheni Muhammad! Msihudhurie vitani pamoja na yeye.» Kwani sisi tunachelea msije mkaangamia anapoangamia yeye. Na wao, pamoja na uvunjaji moyo wao huu, hawaji vitani isipokuwa kwa tukizi, kwa kujionyesha na kutaka kusikika na kuogopa fedheha.
Wanawafanyia nyinyi, enyi Waumini, ugumu wa mali, nafsi, juhudi na mapenzi kwa uadui na chuki walizonazo ndani ya nafsi zao, kwa kupenda kuishi na kuogopa kufa. Na vita vikisimama huwa wakiogopa kuangamia, na utawaona wanakuangalia, macho yao yanazunguka kwa kuwa akili zao zimeondoka kwa kuogopa na kukimbia kuuawa, kama vile macho ya mtu aliyekaribia kufa yanavyozunguka. Na vita vinapomalizika na hofu kuondoka wanawarushia nyinyi matamshi makali yenye kukera. Na utawakuta wao, zinapogawiwa ngawira, ni wachoyo na ni mahasidi. Hao hawakuamini kwa nyoyo zao ndipo Mwenyezi Mungu Akawaondolea thawabu za matendo yao, na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.
Wanafiki wanadhani kwamba mapote ya watu ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwafanya washindwe, hawakuondoka kwenda zao, hivyo ni kwa sababu ya kicho na uoga. Na lau hayo mapote yangalirudi Madina wangalitamani wanafiki hao kuwa wao hawako Madina, wako pamoja na mabedui wa jangwani wantafuta habari zenu na wanauliza kuhusu wana wenu wakiwa mbali. Na lau wangalikuwa wako na nyinyi hawangalipigana pamoja na nyinyi isipokuwa kidogo, kwa uoga wao mwingi, unyonge wao na uchache wa Imani yao.
Hakika yenu nyinyi, enyi Waumini, mna mfano mwema wa kuiga katika maneno ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, matendo yake na mwenendo wake. Basi jilazimisheni na mwenendo wake, kwani anaoufuata na kuuiga ni yule anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, Akamtaja Mwenyezi Mungu na kumuomba msamaha kwa wingi na akamshukuru kwa kila namna.
Na Waumini walipoyashuhudia mapote ya watu waliojikusanya pambizoni mwa mji wa Madina na wakauzunguka, walikumbuka kwamba ahadi ya ushindi imekaribia na wakasema, «Haya ndiyo yale Aiyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ya maonjo, shida na (kisha) ushindi. Mwenyezi Mungu Alitekeleza ahadi Yake na Mtume Wake alisema kweli katika bishara njema aliyoitoa. Na hakukuwaongezea kule kuyatazama yale mapote isipokuwa kumuamini Mwenyezi Mungu na kujisalimisha na uamuzi Wake na kufuata amri Yake.
Miongoni mwa Waumini kuna wanaume waliotekeleza ahadi zao walizomuahidi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakasubiri juu ya shida, madhara na wakati wa vita. Kati yao kuna aliyetekeleza nadhiri akafa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu au akafa juu ya ukweli na utekelezaji ahadi, na kati yao kuna anayengojea mojawapo ya mema mawili, ushindi au kufa shahidi, na hawakuigeuza ahadi ya Mwenyezi Mungu wala hawakuitangua wala hawakuibadilisha kama vile wanafiki walivyogeuza.
Ili Mwenyezi Mungu Awalipe mema watu wa ukweli kwa ukweli wao na kujitolea kwao, nao ni Waumini, na ili Awaadhibu wanafiki Akitaka kuwaadhibu, kwa kutowapa taufiki ya kutubia toba ya kidhati kabla ya kufa, hivyo basi wafe kwenye ukafiri na wastahili Moto, au Awape taufiki ya kutubia na kurejea, kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za wenye kuzidhulumu nafsi zao, ni Mwingi wa huruma kwao kwa kuwapa taufiki ya kutubia toba ya kidhati.
Na Akayarudisha Mwenyezi Mungu mapote ya ukafiri kutoka Madina yakiwa yamepita patupu, yamepata hasara na yamejawa na hasira, hayakupata kheri yoyote duniani wala Akhera, na Mwenyezi Mungu Akawatosheleza Waumini (wasilazimike) kupigana kwa kuwasaidia kwa sababu Alizowatolea. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Hashindwi wala Halazimishwi, ni Mshindi katika ufalme Wake na mamlaka Yake.
Na Mwenyezi Mungu Akawateremsha Mayahudi wa Banū Qurayẓah kutoka kwenye ngome zao kwa kuwa waliyasaidia Mapote katika kupigana na Waislamu, na Akatia hofu ndani ya nyoyo zao wakashindwa, mkawa mnaua kundi katika wao na mnateka kundi lingine.
Na Akawamilikisha nyinyi, enyi Waumini, ardhi yao, makazi yao na mali yao yanayohamishika kama vile pambo, silaha na wanyama na yasiyohamishika kama vile mashamba, nyumba na ngome zilizojikita. Na Akawarithisha ardhi ambayo hamkuweza kuikanyaga kabla ya hapo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, hakuna kinachomshinda.
Ewe Nabii! Waambie wake zako waliojikusanya mbele yako wakitaka kwako ongezo la matumizi, «Mkiwa mnataka maisha ya kilimwengu na pambo lake, basi njooni niwastareheshe kwa kitu kichache cha kilimwengu nilicho nacho na niwatenge bila ya kuwadhuru wala kuwaudhi.
«Na mkiwa mnataka radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na yale aliyowaandalia Mwenyezi Mungu katika Nyumba ya Akhera, basi vumilieni juu ya hali mliyonayo, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, kwani hakika Mwenyezi Mungu Amewaandalia walio wema katika nyinyi malipo makubwa.» (Na walimchagua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na yale Aliyowaandalia Mwenyezi Mungu katika Nyumba ya Akhera).
Enyi wake za Mtume! Yoyote miongoni mwenu Atakayefanya maasia yaliyo wazi ataongezewa adhabu mara mbili zaidi.( Na kwa kuwa cheo chao ni cha juu, imenasibiana na cheo hicho Mwenyezi Mungu Alifanye dhambi linalotokana na wao liwe zito, ili kuhifadhi heshima yao na heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Na kuadhibu huko ni rahisi kwa Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kati yenu na akafanya matendo Aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu , tutampa malipo mema ya matendo yake mara mbili zaidi ya malipo ya asiyekuwa yeye kati ya wanawake wengine, na tumemuandalia yeye riziki nzuri, nayo ni Pepo.
Enyi wake wa Nabii! Nyinyi, katika utukufu na cheo, si kama wanawake wasiokuwa nyinyi iwapo mtafanya matendo ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mtajiepusha na mambo ya kumuasi yeye. Basi msizungumze na wanaume wa kando kwa sauti nyororo yenye kumtia tamaa mwanamume ambaye kuna ubaya ndani ya moyo wake na ugonjwa wa kutamani haramu, (Hii ni adabu ya lazima kwa kila mwanamke Anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.) na semeni maneno yaliyo mbali na shaka yasiyokatazwa na Sheria.
Najilazimisheni kuwa majumbani mwenu, na msitoke humo isipokuwa kwa mahitaji, na msionyeshe uzuri wenu kama vile wanawake wa kipindi cha ujinga wa mwanzo walivyokuwa wakifanya, katika zama zilizotangulia Uislamu. Na maneno haya wanaambiwa wanawake wa kila zama. Na tekelezeni, enyi wake wa Nabii, Swala kwa ukamilifu katika nyakati zake, na toeni Zaka kama Alivyoamrisha Mwenyezi Mungu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika maamrisho yao na makatazo yao. Hakika si lingine Mwenyezi Mungu Amewausia haya ili Awasafishe nyinyi na Awaondolee udhia na ubaya enyi watu wa nyumba ya Nabii!, ambao miongoni mwao ni wake zake na wanaozalikana na yeye, rehema na amani zimshukie, na Azitakase nafsi zenu upeo wa kuzitakasa.
Na yatajeni yale yanayosomwa ndani ya majumba yenu, ya Qur’ani na hadithi za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiena muyafanyie kazi na muyape cheo ambacho yanastahiki., kwani hayo ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole kwenu, kwa kuwa Amewaweka majumbani ambako aya za Mwenyezi Mungu zinasomwa na Sunnah, ni Mtambuzi wa kuwatambua nyinyi kwa kuwachagua muwe wake wa Mtume Wake.
Hakika wale wanaume na wanawake wenye kufuata amri za Mwenyezi Mungu, na wanaume na wanawake wenye kuamini, na wanaume na wanawake wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na wakweli wa kiume na wa kike, na wanaume na wanawake wenye kusubiri katika kujiepusha na matamanio na juu ya kufanya matendo ya utiifu na juu ya shida, na wanaume na wanawake wenye kumcha Mwenyezi Mungu, na wanaume na wanawake wenye kutoa sadaka za lazima na za ziada, na wanaume na wanawake wenye kufunga saumu za lazima na za ziada, na wanaume na wanawake wenye kuzihifadhi tupu zao na uzinifu na vitangulizi vyake na kujihifadhi ufunuaji uchi, na wanaume na wanawake wenye kumtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi kwa nyoyo zao na ndimi zao, Hao Mwenyezi Mungu Amewaandalia msamaha wa dhambi zao na malipo mema makubwa, nayo ni Pepo.
Na haipasi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke iwapo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wametoa uamuzi wawe wataenda kinyume nao, kwa kuchagua lile ambalo silo alilolihukumu kwao. Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, amekuwa mbali na njia ya sawa umbali ulio wazi.
Na pindi unaposema, ewe Nabii, kumwambia yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemneemesha kwa Uislamu, naye ni Zayd bin Harithah ambaye Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wewe ukamneemesha kwa kumuacha huru, «Baki na mke wako, Zaynab binti Jahsh, na usimuache! na muogope Mwenyezi Mungu , ewe Zayd!» na huku unaficha, ewe Nabii, katika nafsi yako kile Alichokuletea wahyi nacho Mwenyezi Mungu cha Zayd kumuacha Zaynab na kuwa wewe utamuoa. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye kudhihirisha ulichokificha, na unaogopa wasije wanafiki wakasema kwamba Muhammad amemuoa mtalaka wa mwanawe wa kubandika, na Mwenyezi Mungu Anastahiki zaidi umuogope. Basi Zayd alipomaliza haja yake kwa Zaynab na akamuacha kisha eda lake likamalizika, tulikuoza wewe, ili uwe ni kiigizo katika kubatilisha mila ya uharamishaji wa kuoa mke wa mwana wa kubandika baada ya kuachwa, wala haitakuwa kosa na dhambi kwa Wamini kuwaoa wake za wale watoto wao wa kubandika baada kuwaacha iwapo wamemaliza haja yao kwao. Na kwa hakika amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kufanyika, hakuna mwenye kuiwekea pingamizi wala kuizuia. Ada ya kujibandika mtoto ilikuwako zama za kijinga (kabla ya Uislamu) kisha ikabatilishwa kwa neno lake Mwenyezi Mungu, «Waiteni wao kwa kuwanasibisha na baba zao..».
Haikuwa ni dhambi kwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika kile Alichomhalalishia Mwenyezi Mungu cha kumuoa mke wa mwanawe wa kujibandika baada ya kumuacha, kama vile alivyowahalalishia hilo Manabii kabla yake yeye, ni mwenendo uliowekwa na Mwenyezi Mungu kwa wale waliopita kabla. Na kwa kweli, amri ya Mwenyezi Mungu ni mpango uliokadiriwa , hauna budi kutokea.
Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Aliwataja Manabii waliopita na Akawasifu kwamba wao ni wale wanaozifikisha jumbe za Mwenyezi Mungu kwa watu, na wanamuogopa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na hawamuogopi yoyote asiyekuwa Yeye. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwahesabu waja Wake kwa matendo yao yote na ni Mwenye kuyaona.
Hakuwa Muhammad ni baba wa yoyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini yeye ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii, hakuna unabii baada yake mpaka Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo miongoni mwa matendo yenu ni mjuzi, hakuna chenye kufichamana Kwake.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mtajeni Mwenyezi Mungu kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu utajo mwingi sana.
Na zishughulisheni nyakati zenu kwa kumtaja Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, asubuhi na jioni, baada ya Swala za faradhi na nyakati za matukio maalumu na sababu, kwani huko kumtaja Mwenyezi Mungu ni ibada iliowekwa na Sheria, inapelekea kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kujizuia na madhambi, na inasaidia kila kheri.
Yeye Ndiye Anayewarehemu na kuwasifu, na Malaika Wake wanawaombea dua, ili awatoe kutoka kwenye giza la ujinga na upotevu kuwaelekeza kwenye nuru ya Uislamu.Na ni Mwenye kuwarehemu Waumini duniani na Akhera, hawaadhibu wao maadamu wao waendelea kumtii na kumtakasa.
Maamkizi ya hawa Waumini kutoka kwa Mwenyezi Mungu huko Peponi Siku ya wao kukutana na Yeye ni Salām na amani kwao kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Amewaandalia wao malipo Mazuri, nayo ni Pepo.
Ewe Nabii! Sisi tumekutumiza uwe ni shahidi juu ya ummah wako kwa kuwafikishia ujumbe, na kuwabashiria Waumini miongoni mwao rehema na Pepo, na uwe ni mwenye kuwaonya na Moto waasi na wakanushaji.
Na uwe ni mlinganizi kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumuabudu Yeye Peke Yake, na uwe ni taa yenye kung’ara kwa anayetaka kupata mwangaza kwako. Kwani jambo lako la haki ambalo umekuja nalo liko wazi kama vile jua katika kuchomoza na kutoa mwangaza, hakuna mwenye kulikanusha isipokuwa mshindani.
Na uwape bishara njema, ewe Nabii, watu wa Imani kuwa watakuwa na malipo makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nayo ni mabustani ya Peponi.
Na usilitii, ewe Nabii, neno la kafiri au mnafiki na uuache udhia wao, na hilo lisikuzuie kufikisha ujumbe, na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu katika mambo yako yote, na umtegemee Yeye, kwani Yeye Atakutosheleza yanayokutia hamu miongoni mwa mambo yote ya ulimwengu na Akhera.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, mfungapo ndoa na wanawake na msiwaingilie, kisha mkawaacha kabla hamjawaingilia, basi hawalazimiki wakae eda lenu la nyinyi kuwahesabia, basi wapeni kitu cha kuwastarehesha katika mali yenu kulingana na ukunjufu mlionao ili kuwapa maliwazo, na wafungueni washike njia waende zao pamoja na sitara nzuri, bila ya udhia wala madhara.
Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake uliowapa mahari yao, na tumekuhalalishia wajakazi waliomilikiwa na mkono wako miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amekuneemesha nao, na tumekuhalalishia kuwaoa wana wa kike wa ami zako na wana wa kike wa shangazi zako na wana wa kike wa khalati zako waliohama (kuja Madina) pamoja na wewe, na tumekuhalalishia mwanamke Muumini aliyekutunukia nafsi yake bila mahari, iwapo unataka kumuoa, hili ni lako wewe peke yako, na haifai kwa asiyekuwa wewe kumuoa mwanamke kwa kutunukiwa. Tushajua kile tulichowalazimisha Waumini kuhusu wake zao na wajakazi wao kuwa wasioe isipokuwa wake wanne, idadi wanayoitaka ya wajakazi na ulazima wa walii, mahari na mashahidi juu yao. Lakini tumekuruhusu wewe na tumekupa nafasi ambayo hatukumpa mtu mwingine asiyekuwa wewe, ili kifua chako kisiingie dhiki juu ya kuwaoa wale uliowaoa kati ya aina hizi. Hii ni miongoni mwa ziada ya utunzi wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na takrima Yake kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe dhambi za waja Wake Waumini, ni Mwenye huruma kwa kuwapanulia (milango ya riziki).
Unamkalisha nyuma unayemtaka miongoni mwa wake zako katika ugawaji wa kulala, na unamleta karibu nawe unayemtaka miongoni mwao. Na yoyote unayemtaka kati ya wale uliochelewesha ugawaji wao, huna dhambi katika hilo. Kwani hiyari hiyo iko karibu zaidi ya kuwafanya wao wafurahike wala wasihuzunike na waridhike wote kwa kile ulichowagawia. Na Mwenyezi Mungu Anavijua vilivyomo ndani ya nyoyo za wanaume, vya kuelemea upande wa baadhi ya wake na kutoelekea upande wa wengine. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyomo ndani ya nyoyo, ni Mpole, Hafanyi haraka ya kuwatesa wanaomuasi.
Haifai kwako kuwaoa wanawake baada ya wake zako walio mama wa Waumini, na usiwaache wao ukawaoa wengine badala yao, kwa kuwakirimu na kushukuru mazuri waliyoyatenda ya kumchagua Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Nyumba ya Akhera, hata kama utavutiwa na uzuri wa hao wanawake wengine, isipokuwa kile ambacho mkono wako wa kulia umemiliki, miongoni mwa wajakazi, kwani hao ni halali kwako. Na Mwenyezi Mungu anakiona kila kitu, hakuna chochote kilicho nje ya ujuzi Wake.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiingie nyumba za Mtume, isipokuwa kwa ruhusa yake, kwa kula chakula bila ya kungoja kuiva kwake. Lakini mkiitwa ingieni, na mkimaliza kula ondokeni, bila ya kujipumbaza kwa mazungumzo baina yenu. Kwani kule kungoja kwenu na kujipumbaza kwenu kunamkera Nabii, naye anawaonea haya kuwatoa kwenye hizo nyumba pamoja na kuwa hiyo ni haki yake, na Mwenyezi Mungu Haoni haya kuieleza haki na kuifunua. Na mkiwaomba wake za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wawapatie kitu chochote mnachokihitajia katika vyombo vya nyumbani na mfano wake, basi waombeni mkiwa nyuma ya pazia. Kufanya kwenu hivyo kunatakasa zaidi nyoyo zenu na nyoyo zao na kuziepusha na mawazo ambayo yanawapitia wanaume kuhusu mambo ya wanawake na wanawake kuhusu mambo ya wanaume, kwani kuona ndio sababu ya kufitinika. Na haifai kwenu kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu wala kuwaoa wake zake baada ya kufa kwake kabisa, kwa kuwa wao ni mama zenu, na haifai mtu kumuoa mamake. Hakika kumkera kwenu Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuwaoa wake zake baada yake ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Ummah huu ulitekeleza amri hii na ulijiepusha na kile Mwenyezi Mungu Aliukataza nacho.
Mkidhihirisha chochote kwa ndimi zenu, enyi watu, kati ya vitu vinavyomkera Mtume katika vile alivyowakataza navyo au mkakificha ndani ya nafsi zenu, basi Mwenyezi Mungu, aliyetukuka anavijua vilivyomo ndani ya nyoyo zenu na vile mlivyovidhihirisha, na Atawalipa kwa hayo.
Hakuna dhambi kwa wanawake kutojifinika mbele ya baba zao, wana wao wa kiume,ndugu zao wa kiume, wana wa kiume wa ndugu zao wa kiume, wana wa kiume wa ndugu zao wa kike, wanawake waumini na watumwa waliomilikiwa na wao kwa kuwa wanahitaji utumishi wao sana. Na muogopeni Mwenyezi Mungu , enyi wanawake, msipite mpaka mliowekewa mkaonyesha pambo lenu msiofaa kulionyesha, au mkaacha kujifinika mbele ya yule ambaye ni lazima mjifinike mbele yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu, Anashuhudia matendo ya waja , ya nje na ya ndani, na Atawalipa kwayo.
Hakika Mwenyezi Mungu Anamsifu Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mbele ya Malaika waliokurubishwa. Na Malaika Wake wanamsifu Nabii na wanamuombea Mwenyezi Mungu, basi enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, mswalieni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mtakieni amani, kwa kumwamkia na kumtukuza. Na namna ya kumswalia Nabii, rehema na amani zimshukie, imethibiti kwenye Sunnah kwa aina mabalimbali, miongoni mwazo ni: «Ewe Mola! Mrehemu Muhammad na watu wa Muhammad, kama ulivyowarehemu watu wa Ibrāhīm, hakika wewe ni Mwingi wa kushukuriwa ni Mwingi wa kutukuzwa. Ewe Mola! Mbariki Muhammad na watu wa Muhammad kama ulivyowabariki watu wa Ibrāhīm, hakika wewe ni Mwingi wa kushukuriwa, ni Mwingi wa kutukuzwa.»
Hakika ya wale wanaomuudhi Mwenyezi Mungu kwa kumshirikisha na kufanya maasia mengine, na wakamuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno na vitendo, Mwenyezi Mungu atawafukuza na Atawaweka mbali na kheri duniani na Akhera, na Amewaandalia, huko Akhera, adhabu kali yenye kuwadhalilisha na kuwafanya wanyonge.
Na wale wenye kuwaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwa maneno au vitendo bila ya kosa walilolifanya, basi watakuwa wametenda tendo la urongo na uzushi mbaya kabisa, na wamefanya kosa chafu waziwazi, ambalo kwalo watastahili kupewa adhabu huko Akhera.
Ewe Nabii! Waambie wake zako, watoto wako wa kike na wanawake Waumini wateremshe juu ya vichwa vyao na nyuso zao mashuka yao na mitandio yao, ili kufinika nyuso zao, vifua vyao na vichwa vyao. Kufanya hivyo kuko karibu zaidi kuwafanya wao watenganishwe kwa kusitirika na kuhifadhika, wasiwe ni wenye kusumbuliwa kwa kukerwa wala kuudhiwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na kurehemu kwa kuwa Amewasamehe yaliyopita na Akawarehemu kwa kuwabainishia halali na haramu.
Wasipokomeka, wale wanaoficha ukafiri na kudhihirisha Imani, wale ambao ndani ya nyoyo zao muna shaka na wasiwasi na wale wanaoeneza habari za urongo katika mji wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mabaya yao na shari zao, tutakupa uwezo juu yao, kisha hawatakaa pamoja na wewe humo isipokuwa muda mchache.
Hali ya kuwa wamefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu; mahali popote watakapopatikana watekwe na wawe ni wenye kuuawa muda wa kuendelea kwao katika unafiki na kueneza habari za urongo baina ya Waislamu kwa lengo la kuleta fitina na uharibifu.
Huu ndio mpango wa Mwenyezi Mungu na njia Yake kuhusu ummah waliopita, ni kuwa watekwe na wawe ni wenye kuuawa popote waliopo. Na hutapata , ewe Nabii, mageuzi wala mabadiliko katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Wanakuuliza watu , ewe Mtume, kuhusu kipindi cha Kiyama kwa njia ya kukiona ni kitu ambacho ni mbali kutokea na kwa njia ya kukikanusha. Waambie, «Hakika ya mambo ni kwamba Ujuzi wa kipindi cha Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu.» Na ni lipi linalokujuza wewe, ewe Mtume kwamba huenda Kiyama kikawa karibu?
Mwenyezi Mungu Amewafukuza makafiri kwenye rehema Yake duniani na Akhera na Amewaandalia huko Akhera Moto wenye kuwashwa ulio na joto kali,
hali ya kukaa milele humo. Hawatapata mtegemewa wa kuwasaidia na kuwatetea, wala mwenye himaya wa kuwahami, Akawatoa Motoni.
Siku zitakapogeuzwa nyuso za makafiri Motoni, huku wakisema kwa kujuta na kuduwaa, «Tunatamani lau tungalimtii Mwenyezi Mungu na tungalimtii Mtume Wake duniani tukawa watu wa Peponi.»
Na watasema makafiri Siku ya Kiyama, «Mola wetu! Kwa kweli sisi tumewatii viongozi wetu katika upotevu na wakubwa wetu katika ushirikina wakatuepusha na njia ya uongofu na Imani.
Mola wetu! Waadhibu Motoni mara mbili zaidi ya adhabu unayotuadhibu kwayo, na uwafukuze kutoka kwenye rehema mafukuzo makali.» Katika hii pana dalili ya kwamba kumtii asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika kuenda kinyume na amri Yake na amri ya Mtume Wake, kunapasisha kupata hasira za Mwenyezi Mungu na mateso Yake, na kwamba mfuasi na mfuatwa watashirikiana kwenye adhabu. Basi ajihadhari na hilo Muislamu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, msimkere Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno wala kwa vitendo, wala msiwe mfano wa wale waliomkera Nabii wa Mwenyezi Mungu Mūsā, Mwenyezi Mungu Akamuepusha na kile walichokisema cha urongo na uzushi, na yeye alikuwa kwa Mwenyezi Mungu ni mwenye cheo kikubwa na utukufu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, fanyeni matendo ya kumtii na mjiepushe na matendo ya kumuasi, ili msistahili kupata mateso hayo. Na semeni, katika hali zenu zote na mambo yenu yote, maneno ya kunyoka na yanayolingana na usawa, yasiyokuwa na urongo na ubatilifu.
Mkimuogopa Mwenyezi Mungu na mkasema maneno ya sawa, Mwenyezi Mungu Atawasamehe dhambi zenu, Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, katika kile alichokiamrisha na akakikataza, basi huyo amefaulu kupata utukufu mkubwa duniani na Akhera.
Sisi tuliiorodhesha amana- ambayo Mwenyezi Mungu Amewapatia waliokalifishwa na Sheria waitunze, nayo ni kufuata maamrisho na kujiepusha na makatazo- kwa mbingu, ardhi na majabali, vikakataa kuibeba na vikaogopa visiweze kusimama kuitekeleza, na akaibeba binadamu na akashikamana nayo pamoja na udhaifu Wake. Hakika yeye ni mwingi wa udhalimu na ujinga wa nafsi yake.
Ili mwisho wa binadamu kuibeba amana uwe ni Mwenyezi Mungu kuwaadhibu wanafiki wa kiume wanaodhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri na wanafiki wa kike, na wanaume wanaomshirikisha katika ibada ya Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye na wanawake washirikina, na ili Awakubalie toba Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwa kuzificha dhambi zao na kuacha kuwaadhibu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa wenye kutubia miongoni mwa waja Wake, ni Mwenye huruma kwao.
Icon