ترجمة معاني سورة يونس
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
(Alif, Lām, Rā’.) Yametangulia maelezo juu ya herufi zilizotajwa kimkato mwanzo wa sura ya Al- Baqarah. Hizi ni aya za Kitabu kilichopangwa vizuri ambacho Mwenyezi Mungu Amekipanga na kukifafanua kwa waja Wake.
Je, lilikuwa jambo la ajabu kwa watu lile la kuteremsha kwetu wahyi wa Qur’ani kwa mtu miongoni mwao anayewaonya mateso ya Mwenyezi Mungu na kuwapa habari njema wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake kwamba wao watapata malipo mazuri kwa matendo mema waliyoyatanguliza? Alipowajia Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu na akawasomea, wakanushaji walisema, «Muhammad ni mchawi, na aliyokuja nayo ni uchawi wenye ubatilifu waziwazi.»
Hakika Mola wenu ni Mwenyezi Mungu Ambaye Alizipatisha mbingu na ardhi katika kipindi cha Siku Sita, kisha Akalingana, yaani Akawa juu ya 'Arsh, mlingano unaonasibiana na utisho Wake na utukufu Wake. Anaendesha mambo ya viumbe Vyake. Hakuna yoyote Anayempinga katika uamuzi Wake na hakuna muombezi yoyote anayeombea mbele Yake Siku ya Kiyama isipokuwa baada ya Yeye kumpa idhini kuombea. Basi muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wenu, Anayesifika kwa sifa hizi na mtakasiyeni ibada. Je, hamwaidhiki na mkazizingatia aya hizi na hoja?
Kwa Mola wenu ndio marejeo yenu nyote Siku ya Kiyama. Na hili ndilo agizo la Mwenyezi Mungu lililo kweli. Yeye Ndiye Ambaye Anaanza kuumba viumbe kisha Atawarudisha baada ya kufa, Awafanye wawe hai kama walivyokuwa mwanzo, ili Awalipe waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akafanya matendo mazuri malipo mazuri zaidi kwa uadilifu. Na wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Mtume Wake watakuwa na vinywaji vya maji moto sana yanayochoma nyuso na kukata tumbo; na watakuwa na adhabu inayoumiza kwa sababu ya ukafiri wao na upotevu wao.
Mwenyezi Mungu Ndiye ambaye Alilifanya jua kuwa d,iyā’ (mwangaza), Akaufanya mwezi kuwa ni nūr (mng’aro) na Akaupangia mwezi njia zake za kupita. Ikawa kwa jua zinajulikana siku, na kwa mwezi inajulikana miezi na miaka. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hakuumba jua na mwezi isipokuwa ni hekima kubwa, na kuonesha ukamilifu wa uwezo wa Mwenyezi Mungu na ujuzi Wake; Anafafanua hoja na dalili kwa watu wanaojua hekima ya utengenezaji wa uumbaji.
Hakika katika kupishana usiku na mchana na Alichokiumba Mwenyezi Mungu, katika mbingu na ardhi na zilizomo ndani yake zilizopangika na kutengenezeka miongoni mwa maajabu ya uumbaji, ni dalili na hoja zilizo wazi kwa watu wanaoogopa mateso ya Mwenyezi Mungu, ghadhabu Zake na adhabu Yake.
Hakika ya wale ambao hawana matumaini ya kukutana na sisi Akhera kwa kuhesabiwa na yanayofuatia ya malipo juu ya matendo kwa kuwa wanakanusha kufufuliwa, wakaridhika na maisha ya ulimwenguni kuwa ni badala ya Akhera, wakajitegemeza nao huo ulimwengu, na wale ambao wao ni wenye kughafilika na alama zetu zilizoko ulimwenguni na zilizomo kwenye Sheria.
Hao makao yao ni Moto wa Jahanamu huko Akhera, yakiwa ni malipo kwa yale ambayo wao walikuwa wakiyatenda katika ulimwengu wao ya madhambi na hatia.
Hakika ya wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya mema, Mola wao Atawaonesha njia ya Pepo na Atawaafikia kufanya matendo yenye kuwafikisha kwake, kwa sababu ya Imani yao , kisha Atawapa malipo mema kwa kuingia Peponi na kuwashushia wao radhi Zake; chini ya sebule zao na majumba yao itakuwa ikipita mito, wakiwa ndani ya mabustani ya Pepo ya starehe.
Maombi yao Peponi ni kuleta tasbihi (kusema Subhānaka Allāhumma), na maamkizi ya Mwenyezi Mungu na Malaika Wake kuwaamkia wao, na maamkizi yao, wao kwa wao, huko Peponi ni Salām. Na mwisho wa maombi yao ni kusema kwao, «Al-hamdu li Llāhi Rabbil- 'ālamīn» Yaani, shukrani na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba viumbe na Mwenye kuvilea kwa neema Zake.
Na lau Mwenyezi Mungu Awaharakishia watu kuyakubali maombi yao ya kujitakia mabaya kama Anavyowaharakishia katika kuwakubalia maombi yao ya kujitakia mazuri wangaliangamia. Hivyo basi tunawaacha, wale ambao hawaogopi mateso yetu wala hawaamini kidhati kufufuliwa na kuhuishwa, ndani ya uasi wao na ujeuri wao hali ya kuwa wanashangaa na kuduwaa.
Na impatapo binadamu shida, anatuomba tumsaidiye katika kumuondolea hiyo akiwa katika hali ya kuwa amelala kwa ubavu wake au ameketi au amesimama, kulingana na hali ile alivyo wakati mashaka yalipomshukia. Na tunapomuondolea ile shida iliyompata, huendelea kuifuata ile njia yake ya mwanzo kabla hajapatwa na mashaka na huyasahau yale aliokuwa nayo ya shida na matatizo na huacha kumshukuru Mola Wake aliyemuondolea yale aliyokuwa nayo ya matatizo. Na kama alivyopambiwa binadamu huyu kuendelea katika kukanusha kwake na kuwa na ujeuri baada ya Mwenyezi Mungu kukuondolea mashaka aliyokuwa nayo , vilevile walipambiwa wale waliopita kiasi katika kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na Manabii Wake yale ambayo walikuwa wakiyafanya ya kumuasi Mwenyezi Mungu na kumshirikisha.
Hakika tuliwaangamiza watu waliowakanusha Mitume wa Mwenyezi Mungu kabla yenu, enyi mliomshirikisha Mola wenu, waliposhirikisha na wakawajia Mitume wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu wakiwa na miujiza iliyo wazi na hoja zenye kubainisha ukweli wa yale aliyekuja nayo. Basi watu hawa hawakuwa ni wenye kuwaamini Mitume wao na kuwafuata, kwa hivyo walistahili maangamivu. Na mfano wa maangamivu hayo ndivyo atakavyolipwa kila mhalifu mwenyekukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Kisha tukawafanya nyinyi, enyi watu, ni badala yao katika ardhi baada ya makame ya wale walioangamizwa, ili tuangalie vipi mtafanya: mema au maovu, tupate kuwalipa kwa hayo, kulingana na matendo yenu.
Na wasomewapo washirikina aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi tulizokuteremshia wewe, ewe Mtume, husema wale ambao hawaogopi Hesabu wala hawatarajii malipo wala hawaamini Siku ya kufufuliwa na kuhuishwa, «Lete qur’ani isiyokuwa hii, au tugeuze hii Qur’ani: uifanye halali kuwa haramu na haramu kuwa halali, ahadi kuwa onyo na onyo kuwa ahadi, na uondoe yaliyomo ndani yake ya kukashifu waungu wetu na kuzifanya za kipumbavu akili zetu.» Waambie, ewe Mtume,»Hilo haliko kwangu. Kwani mimi nafuata, katika kila ninalowaamrisha na ninalowakataza, yale ambayo Mola wangu Ameniteremshia na kuniamrisha kwayo. Mimi naogopa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nikienda kinyume na amri Yake, adhabu ya siku iliyo kubwa , nayo ni Siku ya Kiyama.
Waambie, ewe Mtume, «Lau Mwenyezi Mungu Alitaka, singaliwasomea hii Qur’ani, wala Mwenyezi Mungu Hangaliwajulisha nayo. Basi jueni kuwa hiyo ni haki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwani nyinyi mnajua kwamba mimi nimekaa na nyinyi muda mrefu kabla Mola wangu Hajauleta wahyi wa hiyo (Qur’ani) kwangu, na kabla sijaisoma kwenu. Basi hamtumii akili zenu kwa kuzingatia na kufikiri?»
Hapana yoyote mwenye udhalimu mkubwa zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo au akazikanusha aya Zake. Hakika ni kwamba hawatafuzu waliowakanusha Manabii wa Mwenyezi Mungu na Mitume Wake wala hawatafaulu.
Na hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye wanaviabudu visivyowadhuru chochote wala kuwanufaisha ulimwenguni wala Akhera, na wanasema, «Sisi tunawaabudu wao ili watuombee mbele ya Mwenyezi Mungu.» Waambie, ewe Mtume, «Je, mnampa habari Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, jambo Asilolijua, katika mbingu au katika ardhi, kuhusu mambo ya waombezi hawa?» Kwa hakika lau kulikuwa na waombezi katika hizo wa kuwaombea nyinyi mbele Yake, Angalikuwa na ujuzi zaidi kuhusu wao kuliko nyinyi.» Kwani Mwenyenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameepukana na wanachokifanya washirikina hawa cha kushirikisha kwao, katika ibada Yake, vitu visivyodhuru wala kunufaisha.
Watu walikuwa kwenye dini moja, nayo ni Uislamu, kisha wakatafautiana baada ya hapo, wakakufuru baadhi yao na wengine wakasimama imara juu ya haki. Na lau kwamba si neno lilitangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu la kuwapa muhula wenye kuasi na kutowafanyia haraka kuwapatiliza kwa madhambi yao, basi wangaliamuliwa baina yao kwa kuwaangamiza watu wa ubatilifu miongoni mwao na kuwaokoa watu wa ukweli.
Na makafiri hawa wakaidi wanasema «Basi si ateremshiwe Muhammad ujuzi, dalili na miujiza inayoonekana, kutoka kwa Mola wake, ambayo kwayo tutajua kuwa yeye yuko juu ya haki katika yale anayoyasema.» Waambie, ewe Mtume, «Hakuna ajuwaye ghayb (yasioonekena) isipokuwa ni Mwenyezi Mungu. Akitaka (kufanya wanayoyataka) Atafanya na akitaka (kutofanya) hatafanya. Basi ngojeni, enyi watu, uamuzi wa Mwenyezi Mungu baina yetu na nyinyi wa kuyaharakisha mateso Yake kwa wakosa kati yetu na kumnusuru mwenye haki; mimi nalingojea hilo.
Na tunapowaonjesha washirikina usahali, faraja na neema baada ya uzito, shida na dhiki zilizowapata, punde si punde wanakanusha na kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Sema uwaambie, ewe Mtume, washirikina hawa wanaofanya shere, «Mwenyezi Mungu ni ni mpesi wa vitimbi, kuwavuta nyinyi kidogokidogo na kuwatesa.» Hakika watunzi wetu tunaowatuma kwenu, wanayasajili kwenu yale mnayoyafanyia vitimbi kuhusu aya zetu kisha tutawahesabu kwa hayo.
Yeye Ndiye Anayewaendesha nyinyi, enyi watu, juu ya wanyama na vinginevyo barani, na ndani ya majahazi baharini, hata mnapokuwa humo na yakatembea kwa upepo mzuri na abiria wa hayo majahazi wakafurahi kwa huo upepo mzuri, ghafla majahazi hayo yanajiwa na upepo mkali, na mawimbi yakawajia abiria kutoka kila mahali, na wakawa na hakika kuwa maangamivu yamewazunguka, hapo wanamtakasia dua Mwenyezi Mungu Peke Yake, na wakaviacha vile ambavyo walikuwa wakiviabudu na wanasema, «Ukituokoa kutoka kwenye shida hii ambayo tuko nayo, kwa kweli tutakuwa ni miongoni mwa wale wenye kukushukuru kwa neema yako.»
Mwenyezi Mungu Alipowaondolea shida na mikasa, punde si punde wakawa wanafanya uharibifu na maasia katika ardhi. Enyi watu, hakika ukorofi wa udhalimu wenu unawarudia nyinyi wenyewe. Chukueni starehe katika uhai wa kilimwengu wenye kuondoka, kisha kwetu ndio mwisho wenu na marejeo yenu, hapo tutawapa habari ya matendo yenu yote na tutawahesabu juu ya hayo.
Hakika mfano wa uhai wa kilimwengu na yale mnayojifahiri nayo baina yenu ya mapambo na mali ni kama mfano wa mvua tulioiteremsha kutoka juu kushuka ardhini, tukaotesha kwayo aina za mimea zilizochanganyika miongoni mwa zile zinazoliwa na watu katika matunda na zinazoliwa na wanyama katika nyasi, mpaka ulipoonekana wazi uzuri wa hii ardhi na mng’aro wake, na watu wa ardhi hii wakadhani kwamba wao ni waweza wa kuyavuna na kufaidika nayo, hapo amri yetu na hukumu yetu iliyajia kuwa ile mimea iliyoko juu yake iangamie na uzuri wake uondoke, kipindi cha usiku au mchana, tukaifanya mimea hii na miti imevunwa imekatwa, hakuna kitu katika ardhi hiyo, kama kwamba hapakuwa na mazao na mimea iliokuwa imesimama kabla ya hapo juu ya uso wa ardhi. Hivyo ndivyo kutoweka kunakomaliza yale mnayojigamba nayo baina yenu ya ulimwengu wenu na pambo lake, Mwenyezi Mungu Akayamaliza na kuyaangamiza. Na kama tulivyowafafanulia, enyi watu, mfano wa ulimwengu huu, na tukawajulisha uhakika wake, ndivyo tunavyofafanua hoja zetu na dalili zetu kwa watu wanaofikiri juu ya aya za Mwenyezi Mungu na wanaozingatia yanayowafaa duniani na Akhera.
Na Mwenyezi Mungu Anawaita kwenye mabustani ya Pepo Yake Aliyowaandalia wanaojitegemeza Kwake, na Anawaongoza Anaowataka miongoni mwa viumbe vyake, Akawaafikia kuipata njia iliyolingana sawa, nayo ni Uislamu.
Ni ya Waumini, waliofanya vizuri kumuabudu Mwenyezi Mungu,wakamtii katika yale Aliyowaamrisha na Akayakataza, Pepo na zaidi yake ambayo ni kuutazama Uso wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, huko Peponi, na kupata msamaha na radhi. Na wala nyuso zao hazitafinikwa na vumbi wala unyonge kama itakavyo kuwapata watu wa Moto. Hawa wanaosifika na sifa hizi ndio watu wa Peponi, ni wenye kukaa milele kabisa humo.
Na wale waliofanya maovu ulimwenguni, wakakanusha na wakamuasi Mwenyezi Mungu, watapata mateso ya Mwenyezi Mungu huko Akhera ambayo ni malipo yanayofanana na matendo yao maovu waliyoyafanya, na watafinikwa na unyonge na utwevu. Na hawatapata yoyote mwenye kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwafikie Akitaka kuwatesa. Nyuso zao zitakuwa ni kama zilizovishwa sehemu za weusi wa usiku wenye giza. Hawa ndio watu wa Motoni wenye kukaa milele humo.
Kumbuka, ewe Mtume, Siku ambayo tutawafufua viumbe wote ili wahesabiwe na walipwe, kisha tuseme kuwaambia waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, «Jilazimisheni mahali mliopo, nyinyi na washirika wenu ambao mlikuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, mpaka tuangalie mtafanya nini.» Hapo tutapambanua baina ya washirikina na wale wanaowaabudu, na watajitenga, wale walioabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu, na wale waliokuwa wanawaabudu, na watasema kuwaambia washirikina «Hamkuwa mkituabudu sisi ulimwenguni.»
Basi yatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Shahidi baina yetu na nyinyi. Hakika sisi hatukuwa tunayajua yale mliokuwa mkiyafanya. Na hakika sisi tulikuwa ni wenye kughafilika kuwa nyinyi mnatuabudu, hatukuwa tunalihisi hilo.
Katika kisimamo hiko cha kuhesabiwa, kila nafsi itazipekua na kuziona hali zake na matendo yake, na italipwa kulingana na hayo :yakiwa ni mema atalipwa mema na yakiwa ni maovu atalipwa maovu. Na wote watarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu Aliye Muamuzi Muadilifu. Hapo watu wa Peponi watatiwa Peponi, na watu wa Motoni watatiwa Motoni, na vitawaondokea washirikina vile ambavyo walikua wakiviabudu badala ya Mwenyezi Mungu kwa kumzulia Yeye urongo.
Waambie, ewe Mtume, washirikina hawa, «Ni nani anayewaruzuku kutoka juu kwa mvua anayoiteremsha, na kutoka ardhini kwa mimea na miti aina mbalimabali anayoiotesha kutoka humo, ambayo miongoni mwayo mnakula nyinyi na wanyama wenu? Na ni nani anayemiliki hisia za kusikia na za kuona mnazostarehea, nyinyi na wengineo? Na ni nani anayemiliki uhai na kifo, katika ulimwengu wote, akawatoa wenye uhai na wafu, baadhi yao kutoka kwa wengine, katika viumbe mnavyovijua na msivyovijua? Na ni nani anayeyaendesha mambo ya mbinguni na ardhini na yaliyomo ndani yake, (anayeyaendesha) mambo yenu nyinyi na mambo ya viumbe vyote?» Watakujibu kwamba anayefanya yote hayo ni Mwenyezi Mungu. Waambie, «Basi si muogope mateso ya Mwenyezi Mungu mnapomuabudu mwingine pamoja na Yeye?»
Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu! Yeye Ndiye kweli isiyo na shaka, Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake, Asiye na Mshirika. Basi ni kitu gani kisichokuwa kweli isipokuwa ni upotevu? Basi vipi nyinyi mtaepushwa na kumuabudu Yeye muelekezwe kumuabudu asiyekuwa Yeye?
Kama walivyokanusha washirikina hawa na walivyoendelea kwenye ushirikina wao, ndivyo lilivothibiti neno la Mola wako, hukumu Yake na uamuzi Wake juu ya wale waliotoka nje ya utiifu Wake wakaenda kumuasi na wakamkanusha, kwamba wao hawataamini upweke wa Mwenyezi Mungu wala unabii wa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amawni zimshukiye, wala hawatafanya matendo yanayolingana na uongofu Wake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Je, kuna yoyote, miongoni mwa waungu wenu na waabudiwa wenu, mwenye kuanzisha kuumba chochote kisicho na asili (ya mfano uliotangulia) kisha akifanye kitoweke baada ya kukianzisha, kisha akirudishe kama namna kilivyokuwa kabla hajakifanya kitoweke?» Kwa hakika, wao hawawezi kufanya madai hayo. Sema, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Anayeanzisha kuumba kisha Akakifanya kitoweke kile Alichokiumba, kisha Akakirudisha. Basi ni vipi nyinyi mnajiepusha na njia ya haki na kufuata ubatilifu, nao ni kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu?»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Je, kuna yoyote, miongoni mwa washirika wenu, mwenye kuongoza kwenye njia iliyolingana sawa?» Hakika wao hawawezi hilo. Waambie, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Anamuongoza aliyepotea njia ya uongofu na kumuelekeza kwenye haki. Basi ni yupi anayefaa zaidi kufuatwa: ni yule anayeongoza, peke yake, kwenye njia ya haki au ni yule ambaye haongoki, kwa kutojua kwake na kwa upotevu wake, nao ndio hao washirikina wenu ambao hawaongozi wala hawaongoki mpaka waongozwe? Basi muna nini nyinyi, vipi mnamsawazisha Mwenyezi Mungu na viumbe vyake?» Huu ni uamuzi uliotanguka.
Na wengi wa washirikina hawa hawafuati, katika kuwafanya masanamu ni waungu na kuitakidi kwao kwamba hao masanamu wanawaleta karibu na Mwenyezi Mungu, isipokuwa urongo na dhana, nazo hazifai kitu mbele ya ukweli. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya washirikina hawa ya ukafiri na kukanusha.
Haikuwa ni yenye kumkinika kwa yoyote kuja nayo Qur’ani hii kutoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, sababu ni kwamba hakuna yoyote awezae kufanya hilo miongoni mwa viumbe. Lakini Mwenyezi Mungu Aliiteremsha kusadikisha vitabu alivyowateremshia Manabii Wake, kwa kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni moja. Na katika hii Qur’ani kuna maelezo na ufafanuzi wa sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyowaekea ummah wa Muhammad. Hapana shaka kwamba hii Qur’ani ni wahyi unaotoka kwa Mola wa viumbe wote.
Au kwani wao wanasema kwamba Muhammad ameizua hii Qur’ani yeye mwenyewe? Wao wanajua kwamba yeye ni mwanadamu kama wao. Waambie, «Basi leteni sura moja inayofanana na hii Qur’ani katika mpango wake na uongozi wake, na takeni usaidizi wa kufanya hilo kwa mnayemuweza, badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa majini na binadamu, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.»
Bali wao walifanya haraka kuikanusha Qur’ani mwanzo walipoisikia, kabla hawajazizingatia aya zake, na wakakikanusha kitu ambacho wao hawana ujuzi nacho, miongoni mwa habari ya Ufufuzi, Malipo, Pepo, Moto na vinginevyo, na bado haujawajia wao uhakika wa yale waliyoahidiwa katika Kitabu. Na kama walivyokanusha washirikina mambo Aliyowaonya nayo Mwenyezi Mungu, ndivyo walivyokanusha watu waliopita kabla yao. Basi tazama, ewe Mtume, ulikuwaje mwisho wa madhalimu? Baadhi yao Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza kwa kuwadidimiza ardhini, wengine kwa kuwazamisha majini na wengine kwa kuwapa mateso mengineyo.
Na miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, kuna anayeiamini Qur’ani na miongoni mwao kuna asiyeiamini mpaka afe kwenye msimamo huo na afufuliwe juu yake. Na Mola wako ni Anawajua zaidi hao waharibifu ambao hawaiamini kwa njia ya udhalimu, ushindani na uharibifu, na Atawalipa juu ya uharibifu wao kwa adhabu iliyo kali zaidi.
Na wakikukanusha, ewe Mtume, washirikina hawa waambie, «Mimi nina Dini yangu na matendo yangu, na nyinyi muna dini yenu na matendo yenu; nyinyi hamtaadhibiwa kwa matendo yangu, na mimi sitaadhibiwa kwa matendo yenu.»
Na miongoni mwa makafiri kuna wanaosikia maneno yako ya kweli na usomaji wako Qur’ani, lakini wao hawaongoki. Je, kwani wewe unaweza kuwasikizisha viziwi? Vilevile, huwezi kuwaongoa hawa isipokuwa Mwenyezi Mungu Atake kuwaongoa, kwa kuwa wao ni viziwi, hawaisikii haki na hawaielewi.
Na miongoni mwao kuna wanaokutazama wewe na dalili za unabii wako wa kweli, lakini wao hawaioni nuru ya Imani Aliyokupa Mwenyezi Mungu. Je, unaweza , ewe Mtume, kuwaumbia vipofu macho ya kuwafanya wao waongoke. Vilevile huwezi kuwaongoa wao iwapo hawana busara. Hakika yote hayo yako kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu Hawadhulumu watu kitu chochote, kwa kuwaongezea makosa yao na kuwapunguzia mema yao, lakini watu ndio wanaojidhulumu nafsi zao kwa kukufuru, kuasi na kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo Yake.
Na siku Mwenyezi Mungu Atawakusanya washirikina hawa, Siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa, kama kwamba wao kabla ya hapo hawakukaa katika maisha ya duniani isipokuwa kadiri ya muda mchache wa kipindi cha mchana, watajuana wao kwa wao kama walivyokuwa duniani, kisha kujuana huko kutakatika na muda huo utapita. Hakika wamepata hasara wale waliokataa na kukanusha kuwa watakutana na Mwenyezi Mungu na kuwa Ana thwabu na Ana adhabu. Na hawakuwa ni wenye kuafikiwa kupata uongofu katika yale waliyoyafanya.
Na iwapo tutakuonesha, ewe Mtume, katika uhai wako baadhi ya mateso tunayowaahidi duniani, au tukakufisha kabla hatujakuonesha hayo kwao, ni kwetu sisi peke yetu marejeo ya mambo yao katika hali zote mbili, kisha Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa vitendo vyao waliokuwa wakivifanya duniani, hakuna chochote kati ya hivyo kinafichika Kwake, na Atawalipa malipo yao wanayostahiki kwa vitendo vyao hivyo.
Na kila ummah uliopita kabla yenu, enyti watu, ulikuwa na mjumbe niliyemtuma kwao, kama nilivyomtuma Muhammad kwenu Alinganie kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu na kuwa na utiifu Kwake. Basi huyo mjumbe wao atakapokuja Akhera, hapo kutaamuliwa baina yao kwa uadilifu, na wao hawatadhulumiwa katika malipo ya matendo yao chochote.
Na washirikina katika watu wako, ewe Mtume, wanasema, «Ni lini kitasimama Kiyama iwapo wewe na waliokufuata ni miongoni mwa wakweli katika yale mnayotuahidi kwayo?»
Waambie, ewe Mtume, «Siwezi kuiepushia nafsi yangu madhara wala kuiletea manufaa isipokuwa Akiwa Mwenyezi Mungu Ametaka kuniepushia madhara au kuniletea manufaa. Kila watu wana wakati wa kumalizika muda wao na kipindi chao cha kuishi, basi ujapo wakati wa kumalizika kipindi chao cha kuishi na kukoma umri wao, hawatachelewa hata kwa muhula wa saa moja wala hautatangulia muda wa maisha yao mbele ya wakati maalumu.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Nipeni habari ikiwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu mchana au usiku, ni kitu gani mnachokifanyia haraka, enyi wahalifu, kuwa adhabu iteremke?
Je, baada ya kushuka adhabu ya Mwenyezi Mungu kwenu, enyi washirikina, ndipo mtaamini, wakati ambapo Imani haitawafaa? Wakati huo mtaambiwa, ‘Je, sasa ndipo mnaamini na hapo nyuma mlikuwa mnaifanyia haraka?’»
Kisha wataambiwa waliozidhulumu nafsi zao kwa kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu, «Onjeni adhabu ya Mwenyezi Mungu ya daima milele kwenu, kwani mnateswa isipokuwa ni kwa yale matendo ya kumuasi Mwenyezi Mungu mliokuwa mkiyafanya katika maisha yenu.
Na hao washirikina miongoni mwa watu wako, ewe Mtume, wanataka uwape habari kuhusu adhabu Siku ya Kiyama, «Je, ni kweli hiyo? Waambie, ewe Mtume, «Ndio, naapa kwa Mola wangu, hiyo ni kweli isiokuwa na shaka.Na nyinyi si wenye kumlemea Mwenyezi Mungu Asiwafufue na kuwalipa, kwani nyinyi muko kwenye udhibiti wa Mwenyezi Mungu na mamlaka Yake.
Na lau kwamba kila nafsi iliyomshirikisha na kumkanusha Mwenyezi Mungu itakuwa na vyote vilivyomo ardhini, na ikamkinika kuvifanya ni fidia yake ya kujikomboa na adhabu hiyo, ingalijikomboa kwavyo. Na wale ambao walidhulumu wataficha majuto yao watakapoiona adhabu ya Mwenyezi Mungu imewashukia wao wote. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atahukumu baina yao kwa uadilifu, na wao hawatadhulumiwa, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Hamuadhibu yoyote isipokuwa kwa dhambi zake.
Jua utanabahi kwamba kila kilichoko mbinguni na ardhini ni milki ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, hakuna kitu chochote kati ya hivyo ni cha yoyote isipokuwa Yeye. Jua utanabahi kwamba kukutana na Mwenyezi Mungu kuko na adhabu Yake kwa washirikina ni yenye kuwa, lakini wengi wao hawaujui uhakika wa hilo.
Hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha, Hashindwi kuwahuisha watu baada ya kufa kwao, kama ambavyo hakumshindi Yeye kuwafisha Atakapo hilo. Na wao ni wenye kurejea Kwake baada ya kufa kwao.
Enyi watu yamewajia nyinyi mawaidha kutoka kwa Mola wenu yanayowakumbusha mateso ya Mwenyezi Mungu na yanayowaonya makamio Yake, nayo ni Qur’ani na yale iliyoyakusanya ya miujiza na mawaidha ili kuzitengeneza tabia zenu na matendo yenu. Na ndani yake muna dawa ya yaliyomo nyoyoni ya ujinga na ushirikina na magonjwa mengineyo, na muna uongofu kwa viumbe wenye kuifuata iwaokoe na maangamivu. Mwanyezi mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Ameijaalia ni neema na rehema kwa Waumini. Na Amewahusu Waumini kwa hilo, kwa kuwa wao ndio wenye kunufaika na Imani. Ama makafiri, hiyo Qur’ani kwao ni giza.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wote, «Kwa wema wa Mwenyezi Mungu na rehema Yake, basi na wawe na furaha.» Wema wa Mwenyezi mungu na rehema Yake ni Uislamu ambao ni uongofu na ni Dini ya haki aliyokuja nayo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwani Uislamu ambao Mwenyezi Mungu Amewaita wao waufuate, na Qur’ani ambayo Aliiteremsha kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye ni bora kuliko taka za ulimwengu wanazozikusanya na anasa zilizomo ndani yake zenye kutoeka kuondoka.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaokataa wahyi, «Nipeni habari juu ya hii riziki ya wanyama, mimea na vitu vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu Amewaumbia nyinyi, mkajihalalishia baadhi ya hivyo na mkajiharamishia vinginevyo.» Waambie, «Je, Mwenyezi Mungu Amewaruhusu hilo au mnaongea maneno ya ubatilifu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na mnasema urongo?» Hakika wao wanaongea maneno ya ubatilifu ya kumzulia Mwenyezi Mungu na wanasema urongo.
Na hawa wanaomzulia Mwenyezi Mungu urongo, wakamnasibishia uharamishaji wa vitu ambavyo Yeye Hakuviharamisha kati ya riziki na vyakula, wanadhani kuwa Mwenyezi Mungu Atawafanya nini Siku ya Kiyama, siku ya wao kuhesabiwa, kwa urongo wao waliomzulia? Je,wanadhani kwamba Yeye Atawaacha na Atawasamehe? Mwenyezi Mungu Ana wema mwingi kwa viumbe Wake kwa kuacha Kwake kuyaharakisha mateso duniani kwa aliyemzulia urongo, na badala yake kumpa muhula. Lakini wengi zaidi wa watu hawamshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema wake juu yao kwa hilo.
Na huwi, ewe Mtume, kwenye jambo lolote katika mambo yako, na husomi chochote kile katika aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na hafanyi yoyote katika ummah huu tendo lolote lema au baya, isipokuwa sisi huwa ni mashahidi juu yenu ni wenye kuliona hilo, mnapolichukua na kulitenda, tukawahifadhia na tukawalipa kwalo. Na haufichamani na ujuzi wa Mwenyezi Mungu uzito wa chungu mdogo ardhini wala mbinguni, wala kitu kidogo kabisa wala kikubwa kabisa, isipokuwa kiko kwenye Kitabu kilichoko kwa Mwenyezi Mungu kilicho waziwazi chenye ufafanuzi, ujuzi Wake umekizunguka na Kalamu Yake imekiandika.
Jueni mtanabahi kwamba mawalii wa Mwenyezi Mungu hawatakuwa na kicho cha mateso ya Mwenyezi Mungu Akhera, wala wao hawatasikitika juu ya hadhi za kilimwengu walizozikosa.
Sifa za Mawalii hawa ni kwamba wao wamemuamini Mwenyezi Mungu na wamemfuata Mtume Wake na yale ambayo alikuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba wao wanamcha Mwenyezi Mungu kwa kuzifuata amri Zake na kuyaepuka matendo ya kumuasi.
Mawalii hawa wana bishara njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa watapata ya kuwafurahisha katika maisha ya kilimwengu, na miongoni mwayo ni ndoto njema anayoiona mwenyewe au akaonewa na duguye, na watapata Pepo kesho Akhera. Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake wala Haigeuzi. Huko ndiko kufaulu kukubwa, kwa kuwa bishara hiyo imekusanya kuokoka na kila lifanyiwalo hadhari na kufaulu kupata kila litakwalo na kupendwa.
Na yasikusikitishe, ewe Mtume, maneno ya washirikina juu ya Mola wao na kumzulia kwao Yeye urongo na kuishirikisha kwao mizimu ya masanamu pamoja na Yeye. Kwani Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyepwekeka kwa nguvu zilizokamilika na uwezo uliotimia, ulimwenguni na Akhera; na Yeye Ndiye Msikizi wa maneno yao Ndiye Mjuzi wa nia zao na matendo yao.
Jueni mtanabahi kwamba ni wa Mwenyezi Mungu kila aliye mbinguni au ardhini miongoni mwa Malaika, binadamu, majini na wengineo. Na ni nini wanachofuata wale wanaowaomba asiyekuwa Mwenyezi Mungu katika hao washirika? Hawana wanachokifuata isipokuwa shaka, na wao hawana lolote isipokuwa wanasema urongo katika yale ambayo wanamnasibisha nayo Mwenyezi Mungu.
Yeye Ndiye Ambaye Amewaekea nyinyi, enyi wtu, usiku ili mtuliye ndani yake na mpumzike na usumbufu wa harakati za kutafuta maisha , na Amewaekea mchana ili muone ndani yake na muende mbio kutafuta riziki yenu. Hakika katika kupishana usiku na mchana na hali ya watu katiaka vipindi viwili hivyo pana dalili na hoja, kwa watu wanaozisikia hoja hizi na kuzitafakari, kwamba Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa.
Washirikina walisema, «Mwenyezi Mungu amejifanyia mwana» kama vile wanavyosema: ‘Malaika ni watoto wa kike wa Mwenyezi Mungu’, au ‘Al-Masīh( ni mwana wa Mwenyezi Mungu’. Mwenyezi Mungu Ametakasika na hayo yote na Ameepukana nayo! Yeye Ndiye Mkwasi Asiyemuhitajia kila asiyekuwa Yeye. Ni Vyake Yeye vyote vilivyoko kwenye mbingu na ardhi. Vipi basi Atakuwa na mwana miongoni mwa Aliyewaumba na hali ni kwamba kila kitu kinamilikiwa na Yeye? Na nyinyi hamuna dalili yoyote juu ya urongo mnaouzua. Je, mnasema kuhusu Mwenyezi Mungu maneno msiyoyajua ukweli wake na usawa wake?
Sema, «Hakika wale ambao wanamzulia Mwenyezi Mungu urongo, kuwa Amejifanyia mwana na kumuengezea mshirika, hawatapata matakwa yao ulimenguni wala Akhera.»
Hakika wao wanastarehe ulimwenguni, kwa ukafiri wao na urongo wao, starehe fupi. Kisha ukomapo muda wao wa kuishi, kuja kwetu ndio mwisho wao. Kisha tutawaonjesha adhabu ya Jahanamu kwa kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu, kumkanusha kwao Mitume wa Mwenyezi Mungu na kupinga kwao aya Zake.
Wasimulie, ewe Mtume, makafiri wa Maka habari ya Nūḥ, amani imshukiye, pamoja na watu wake alipowaambia, «Ikiwa imekuwa ni uzito kwenu kukaa kwangu na nyinyi kuwakumbusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, basi ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mategemeo yangu, na matumaini yangu yako Kwake Yeye. Basi tayarisheni mambo yenu na waiteni washirika wenu, kisha msiyafanye mambo yenu yafichike bali yawe waziwazi yenye kuonekana, kisha amueni juu yangu mateso na mabaya mnayoyaweza wala msinipe muhula wa saa moja ya mchana.
«Mkiupuuza mwito wangu, basi sikuwaomba malipo, kwa kuwa thawabu zangu ziko kwa Mwenyezi Mungu na malipo yangu yako juu Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Peke Yake hakuna mwenye ushirika na Yeye, na nimeamrishwa niwe miongoni mwa wenye kufuata hukumu Yake.»
Basi wakamkanusha Nūḥ, watu wake katika yale Aliyowaitia kwayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo tulimuokoa Yeye na waliokuwa na Yeye kwenye jahazi, na tukawafanya wao washikilie nafasi ya waliokanusha katika ardhi, na tukawazamisha wale waliokataa hoja zetu. Hivyo basi, fikiria, ewe Mtume, namna ulivyokuwa mwisho wa watu wale ambao Mtume wao Aliwaonya adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake?
Kisha tukatuma, baada ya Nūḥ, Mitume kwenda kwa watu wao (Hūd, Ṣāliḥ„ Ibrāhīm, Lūṭ„ Shu'ayb na wengineo), kila Mtume Alikuja kwa watu wake kwa miujiza yenye kuonesha dalili ya utume Wake na ukweli wa yale aliyowaitia. Hawakuwa ni wenye kuyaamini wala kuyafanya yale ambayo watu wa Nūḥ na waliowatangulia miongoni mwa ummah waliopita. Na kama alivyopiga mhuri Mwenyezi Mungu juu ya nyoyo za hawa watu wasiamini, hivyo ndivyo anavyopiga mhuri juu ya nyoyo za wanaofanana na wao kati ya waliokuwa baada yao, miongoni mwa wale ambao walivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu na wakaenda kinyume na yale, ambayo Mitume wao waliwaitia kwayo, ya kumtii Yeye, ikiwa ni mateso kwao kwa sababu ya matendo yao ya uasi.
Kisha tukawatuma, baada Mitume hao, Mūsā na Hārūn, amani iwashukie, kwenda kwa Fir'awn na watukufu wa watu wake, wakiwa na miujiza yenye kuonesha dalili ya ukweli wao, wakafanya kiburi kwa kukataa kuikubali haki na wakawa ni watu washirikina, wahalifu na wakanushaji.
Huo ukweli, ambao Alikuja nao Mūsā, ulipomfikia Fir'awn na watu wake, walisema, «Hakika miujiza aliyokuja nayo Mūsā ni uchawi mtupu ulio waziwazi.»
Mūsā aliwaambia akiona ajabu kwa maneno yao, «Mnaiyambia haki ilipowajia kuwa ni uchawi? Tazameni sifa za kitu kilichowajia na vilivyomo ndani yake, mtakikuta ni ukweli. Na wachawi hawafaulu wala hawafuzu ulimwenguni wala Akhera.»
Fir'awn na kundi lake wakasema kumwambia Mūsā, «Je, umetujia kutuepusha na yale ambayo tuliwakuta nayo wazazi wetu ya kuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, mupate kuwa na utukufu na mamlaka, wewe na Hārūn, katika ardhi ya Misri? Basi sisi si wenye kukubali kwamba wawili nyinyi ni Mitume mliotumwa kwetu ili tumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika.»
Na akasema Fir'awn, «Nileteeni kila mchawi mwenye uhodari wa uchawi.»
Wachawi walipomjia Fir'awn, Mūsā aliwaambia, «Tupeni chini kamba zenu na fimbo zenu mlizonazo.»
Walipozitupa kamba zao na fimbo zao, Mūsā aliwaambia, «Mlivyokuja navyo mkavitupa ni uchawi. Mwenyezi Mungu Ataviondoa mlivyokuja navyo na atavitangua. Hakika Mwenyezi Mungu Hakitengenezi kitendo cha anayetembea katika ardhi ya Mwenyezi Mungu kufanya mambo Anayoyachukia na kufanya uharibifu humo kwa kumuasi.
Na Mwenyezi Mungu Atauimarisha ukweli niliokuja nao kutoka Kwake Ataufanya uwe juu ya ubatilifu wenu kwa maneno Yake na amri Yake, ingawa watu wahalifu wenye kufanya maasia, miongoni mwa jamaa za Fir'awn, wanachukia.
Na hawakumuamini Mūsā, amani imshukiye, pamoja na hoja na dalili alizowaletea, isipokuwa kizazi cha watu wake, Wana wa Isrāīl, hali ya kuwa wao wana uoga na Fir'awn na kundi lake wasiwatese kwa kuwaadhibu na wasiwazuie na Dini yao. Na hakika Fir'awn ni mjeuri mwenye kiburi katika ardhi, na hakika Yeye ni miongoni mwa waliopita mpaka katika ukafiri na uharibifu.
Na akasema Mūsā, «Enyi watu wangu, mkimuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, na mkafuata sheria Yake, kuweni na imani na Yeye na jisalimisheni kwa amri Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu jitegemezeni iwapo nyinyi ni wenye kumdhalilikia kwa utiifu.
Watu wa Mūsā walisema kumwambia, «Tumemtegemea Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika na tumemwachia Yeye mambo yetu. Ewe Mola wetu, usiwape ushindi juu yetu ikawa ni mtihani kwetu katika Dini yetu, au ikawa ni mtihani kwa makafiri kwa kupata ushindi wakasema: lau wao (wenye kumuamini Mūsā) wako kwenye haki hawangalishindwa.
«Na utuokoe, kwa rehema yako, kutokana na watu makafiri, Fir'awn na kundi lake.» Kwani wao walikuwa wakiwalazimisha kufanya kazi ngumu.
Na tuliwapelekea wahyi Mūsā na Hārūn kwamba watengezeeni watu wenu katika Misri majumba yenye kuwa ni makao na mahali pa hifadhi pa kukimbilia, na myafanye majumba yenu kuwa ni mahali pa kuswali ndani yake mkiwa na uoga, na tekelezeni Swala za faradhi kwa nyakati zake. Na wape Waumini wenye kumtii Mwenyezi Mungu bishara njema ya nguvu ya ushindi na thawabu nyingi kutoka Kwake, kutakata ni Kwake na kutukuka.
Na Mūsā akasema, «Mola wetu, hakika wewe umempa Fir'awn na watukufu wa watu wake pambo la vitu vya duniani wasikushukuru, na wamejisaidia kwa vitu hivyo katika kupotoa watu na njia Yako. Mola wetu, yageuze Mali yao wasifaidike nayo, na uzipige mhuri nyoyo zao zisipate kuikunjukia Imani, wasiamini mpaka waione adhabu kali iumizayo.»
Akasema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwambia wao wawili, «Yameshakubaliwa maombi yenu juu ya Fir'awn na kundi lake na mali zao,- Mūsā alikuwa akiomba, na Hārūn akiitika maombi yake, ndipo ikafaa kuyanasibisha maombi kwa wao wawili,- basi jikiteni kwenye Dini yenu na muendelee kumlingania Fir'awn na watu wake kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii, na msifuate njia ya asiyejua ahadi yangu njema na onyo langu.»
Na tuliwakatia bahari Wana wa Isrāīl mpaka wakaivuka, wakafuatwa na Fir'awn na askari wake, kwa udhalimu na uadui, wakafuata njia ya bahari nyuma yao, mpaka Fir'awn alipozungukwa na hali ya kuzama alisema kwamba hapana Mola isipokuwa yule ambaye Wana wa Isrāī wamemuamini, na mimi ni miongoni mwa wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu wenye kujisalimisha Kwake kwa kufuata na kutii.
Je, sasa hivi, ewe Fir'awn, wakati kifo kimekushukia ndipo, unakubali kuwa wewe ni mja wa Mwenyezi Mungu na hali ulimuasi na ukawa ni miongoni mwa waharibifu wenye kuzuia njia Yake kabla ya adhabu Yake kukushukia! Basi toba haitokunufaisha wakati wa kukata roho na kushuhudia kifo na adhabu.
Leo tutakujaalia uwe kwenye muinuko wa ardhi kwa mwili wako, akutazame mwenye kukanusha kuangamia kwako, ili uwe ni mazingatio kwa watu wenye kuja baada yako kuwaidhika na wewe. Na hakika wengi zaidi kati ya watu ni wenye kughafilika na hoja zetu na dalili zetu, hawazifikirii wala hawazizingatii.
Hakika tuliwashukisha Wana wa Isrāīl mashukio mazuri yaliyoteuliwa katika miji ya Sham na Misri na tukawaruzuku riziki ya halali iliyo nzuri itokanayo na mazuri ya ardhi iliyobarikiwa. Na hawakutafautiana, katika mambo ya Dini yao isipokuwa baada ya kujiwa na ujuzi wa kuwafanya wao wawe pamoja na washikane, miongoni mwao ni yale yaliyomo ndani ya Taurati kuhusu habari ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Kwa kweli, Mola wako, ewe Mtume, Atahukumu baina yao Siku ya Kiyama na Atatoa uamuzi katika yale waliokuwa wakitafautiana juu yake kuhusu mambo yako, wapate kuingia wakanushaji Motoni na Waumini Peponi.
Basi uwapo na shaka,ewe Mtume, juu ya ukweli wa yale tuliyokupa habari yake, waulize wanaosoma Kitabu kabla yako miongoni mwa watu wa Taurati na Injili. Kwani hilo limethibiti kwenye vitabu vyao. Hakika umejiwa na ukweli wa yakini, kutoka kwa Mola wako, kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba hawa Mayahudi na Wanaswara wanajua ukweli wa hilo na wanapata sifa zako katika vitabu vyao, lakini wao wanalikataa hilo pamoja na kuwa walijua. Basi usiwe ni miongoni mwa wenye kufanya shaka juu ya usawa wa hilo na ukweli wake. Makusudio ya aya hii ni kusimamisha hoja kwa washirikina kwa ushahidi wa Watu wa Kitabu kati ya Wayahudi na Wanaswara ili kuukata udhuru wao.
Na usiwe, wala usiwe, ewe Mtume, ni miongoni mwa waliokanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, ukawa ni katika waliopata hasara ambao Mwenyezi Mungu Amewakasirikia na wamepata mateso Yake.
Hakika ya wale ambao limethibiti kwao neno la Mola Wako la kuwafukuza kwenye rehema Yake na kuwaadhibu, hawaziamini hoja za Mwenyezi Mungu, hawaukubali upweke Wake wala hawazifuati sheria Zake kivitendo.
Hata kama yatawajia wao kila mawaidha na mazingatio mpaka waishuhudie adhabu yenye kuumiza. Hapo wataamini, na haitawafaa Imani yao.
Imani haikuwafaa watu wa mji wowote walioamini walipoishuhudia adhabu isipokuwa watu wa mji wa Yunus mwana wa Matta. Kwani wao walipohakikisha kwamba adhabu ni yenye kuwashukia, walirejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kutubia kidhati; na ulipofunuka ukweli wa toba yao, Mwenyezi Mungu aliwaondolea adhabu ya hizaya baada ya kuwa karibu na wao, na Akawaacha ulimwenguni wakisterehe mpaka muda wao wa kuishi kukoma.
Na lau Mola wako, ewe Mtume, Aliwatakia Imani watu wa duniani wote, wangaliyaamini, kwa umoja wao, yale uliyokuja nayo, lakini Yeye ana hekima katika hilo. Yeye Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka, kulingana na hekima Yake, na haliko kwenye uwezo wako jambo la kuwatendesha nguvu watu juu ya kuamini.
Haikuwa nafsi yoyote ni yenye kumuamini Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa idhini Yake na taufiki Yake. Basi usiisumbue nafsi yako katika hilo, kwani mambo yao yako kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Ataajaalia adhabu na hizaya kwa wale ambao hawayatii akilini maamrisho Yake na makatazo Yake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wako, «Fikirini na mzingatie kwa yaliyomo mbinguni na ardhini miongoni mwa aya za Mwenyezi Mungu zilizo waziwazi.» Lakini aya, mazingatio na Mitume wenye kuwaonya waja wa Mwenyezi Mungu adhabu Yake, vyote hivyo havikuwa ni vyenye kuwanufaisha watu wasioamini chochote katika hivyo, kwa sababu ya kupa mgongo kwao na ujeuri wao.
Je, hawa wanangojea isipokuwa hiyo siku watakapoishuhudia adhabu ya Mwenyezi Mungu mfano wa siku za wakale wao waliokanusha waliopita kabla yao? Sema, ewe Mtume, «Ingojeeni adhabu ya Mwenyezi Mungu; hakika mimi ni mwenye kuingojea pamoja na nyinyi kuteswa kwenu.»
Kisha tutawaokoa Mitume wetu na wale walioamini pamoja na wao. Na kama tulivyowaokoa hao tutakuokoa wewe, ewe Mtume, na waliokuamini wewe kwa wema utokao kwetu na rehema.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu hawa, «Iwapo muko kwenye shaka juu ya usawa wa Dini yangu ambayo nimewaitia kwayo, nayo ni Uislamu, na juu ya uthabiti wangu na kujikita kwangu juu yake, pamoja ya kuwa nyinyi muna matumaini ya kuniepusha nayo, basi mimi sitamuabudu katika hali yoyote ile, yoyote miongoni mwa wale mnaowaabudu mkajifanyia masanamu na mizimu, lakini namuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Mwenye kuwafisha na kuzitwaa roho zenu, na nimeamrishwa niwe ni miongoni mwa wenye kumuamini na wenye kufuata Sheria Zake kivitendo.»
Na ujisimamishe imara, ewe Mtume, juu ya dini ya Uislamu, hali ya kulingana sawa juu yake, usiwe ni mwenye kupotoka na kuwa kando nayo ukaelekea kwenye Uyahudi au Unaswara wala kumuabudu asiyekuwa Yeye. Wala usiwe ni miongoni mwa wale wanaoshirikisha, katika ibada ya Mola wao, waungu na wale wanaodai kuwa wanafanana na Yeye, kwani ufanyapo hilo utakuwa ni miongoni mwa watakaoangamia. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pia wanaambiwa umma wote.
Wala usiwaombe, ewe Mtume, wasiokuwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa mizimu na masanamu, kwani wao hawanufaishi wala hawadhuru. Na ufanyapo hilo na ukawaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu, hapo wewe utakuwa ni miongoni mwa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ushirikina na kufanya maasia. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, pia wanaambiwa umma wote.
Na Mwenyezi Mungu Akikupatia, ewe Mtume, shida au mitihani, basi hakuna wa kuyaondoa hayo isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, na Akikutakia furaha na neema, basi hakuna yoyote mwenye kuyazuia hayo. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Anampatia furaha na shida Anayemtaka kati ya waja Wake. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha wa dhambi za wenye kutubia, ni Mwingi wa rehema kwa wanaomuamini na kumtii.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa watu, «Amewajia nyinyi Mtume wa Mwenyezi Mungu na Qur’ani ambayo ndani yake muna maelezo ya kuwaongoa nyinyi. Basi mwenye kuongoka kwa uongofu wa Mwenyezi Mungu, hakika matunda ya kitendo chake yatamrudia yeye mwenyewe. Na mwenye kupotoka akawa kando na haki na akaendelea kwenye upotevu, hakika upotevu wake na madhara yake yatamshukia yeye mwenyewe. Na mimi si kuwakilishwa kwenu mpaka muwe Waumini. Mimi ni mjumbe mwenye kufikisha , nawafikishia yale niliyotumwa kwayo.
Na uufuate, ewe Mtume, wahyi wa Mwenyezi Mungu Aliokutumia wewe na uutumie kivitendo. Na uwe na subira katika kumtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na katika kujiepusha na mambo ya kumuasi na kwa kuvumilia makero ya wenye kukukera katika kuufikisha ujumbe Wake, mpaka Mwenyezi Mungu Atoe uamuzi Wake kwao na kwako. Na Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye mbora wa kutoa uamuzi, kwa kuwa uamuzi Wake unakusanya uadilifu uliokamilika.