ترجمة معاني سورة التغابن
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
Vinamtakasa Mwenyezi Mungu na sifa zisizonasibiana na Yeye vyote vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini. Ni Wake Yeye Mwenyezi Mungu, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, uendeshaji mambo usio na kizuizi katika kila kitu. Na Yeye Ndiye Mwenye sifa njema zilizo nzuri. Na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.
Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafanya nyinyi mpatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako, kati yenu kuna wenye kuukanusha uungu Wake na baadhi yenu kuna wenye kuuamini na kufuata Sheria Zake kivitendo. Na Yeye, kutakasika na kila sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuviona vitendo vyenu, hakuna chochote chenye kufichamana Kwake, na Atawalipa kwavyo.
Ameumba mbingu na ardhi kwa hekima kubwa, na Akawaumba nyinyi katika sura nzuri, na Kwake Yeye ndio marejeo Siku ya Kiyama, Amlipe kila mtu kwa matendo yake.
Anajua, kutakasika na kutukuka ni Kwake, kila kilichoko mbinguni na ardhini, na Anakijua mnachokificha, enyi watu, na mnachokidhihirisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yale yanayodhamiriawa na vifua na kufichwa na nafsi
Je haikuwajia nyinyi, enyi washirikina, habari ya wale waliokufuru miongoni mwa watu waliopita kabla yenu, ulipowafikia wao mwisho mbaya wa ukafiri wao na uovu wa vitendo vyao hapa ulimwenguni na kuwa wao kesho Akhera watakuwa na adhabu kali iumizayo?
Hayo yaliyowapata duniani na yatakayowapata kesho Akhera ni kwamba wao walikuwa wakijiliwa na Mitume wa Mwenyezi Mungu na alama waziwazi na miujiza iliyofunuka wazi, huwa wakisema, «Je binadamu kama sisi wanatuongoza? Hapo wakamkufuru Mwenyezi Mungu, wakaukanusha ujumbe wa Mitume Wake na wakaipa mgongo haki wasiikubali. Na Mwenyezi Mungu Hana haja na kuamini kwao wala kuabudu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Ana utajiri uliotimia usio na mpaka, ni Mwenye kusifiwa kwa maneno Yake, matendo Yake, na sifa Zake, Hawajali wao wala haumdhuru Yeye upotevu wao chochote.
Walidai wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu kwa ubatilifu kwamba wao hawatatolewa kwenye makaburi yao baada ya kufa. Waambie, ewe Mtume, «Ndio. Naapa kwa Mola wangu! Mtatolewa makaburini mwenu mkiwa hai, kisha mtapewa habari ya yale mliyoyafanya duniani. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni sahali na rahisi.
Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, enyi washirikina, na mjiongoze kwa Qur’ani Aliyomteremshia Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu kwa mnayoyafanya ni Mtambuzi, hakuna kinachofichamana na Yeye cha matendo yenu na maneno yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa kwa hayo Siku ya Kiyama.
Ikumbukeni Siku ya Mkusanyo ambayo Mwenyezi Mungu Atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho. Siku hiyo ambayo ina mpunjano na mtengano kati ya viumbe: Waumini wawapunje makafiri na wenye kuasi, na wao hao( hao makafiri na waasi) iwadhihirikie wazi kuwa wao ndio waliopata hasara. Basi wenye Imani wataingia Peponi kwa rehema za Mwenyezi Mungu, na wenye ukafiri wataingia Motoni kwa uadilifu Wake. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na akafanya matendo ya utiifu Kwake, Atamfutia dhambi zake na Amtie kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya majumba yake ya fahari inapita mito ya maji, hali ya kukaa milele humo. Kukaa milele huko Peponi ndiko kufaulu kukubwa ambako hakuna kufaulu kushinda huko.
Na wale ambao wanapinga kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Mola wa haki na wakazikanusha dalili za kuwa Yeye Ndiye Mola na hoja za uungu Wake Alizowatuma nazo Mitume Wake, hao ni watu wa Motoni, ni wenye kukaa humo milele. Moto huo wa Jahanamu ni marejeo maovu mno watakayofikia.
Halimpati yoyote jambo lolote la shida isipokuwa kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu na mapitisho Yake na makadirio Yake. Na yoyote anayemuamini Mwenyezi Mungu, Atauongoza moyo Wake ufuate amri Zake na uridhike na mapitisho Yake. Atauongoza kwenye njia nzuri ya maneno, vitendo na hali. Kwani uongofu hasa ni wa moyo, na viungo vinafuata. Na Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, hakifichamani Kwake chochote miongoni mwa hivyo.
Na mtiini Mwenyezi Mungu, enyi watu, na muongokee Kwake katika yale Aliyoyaamrisha na Aliyoyakataza, na mfuateni Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika yale aliyowafikishia kutoka kwa Mola wake. Na iwapo mtaupa mgongo utiifu wenu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi Mjumbe wetu hana madhara yoyote kutokana na kupa mgongo kwenu. Jukumu lake yeye ni kuwafikishia nyinyi yale Aliyotumilizwa kwayo ufikishaji wenye maelezo ya waziwazi.
Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Ambaye hukuna muabudiwa wa kweli isipokiuwa Yeye. Na kwa Mwenyezi Mungu tu na wategemee Waumini, kwa upweke Wake, katika mambo yao yote.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake! Kwa kweli miongoni mwa wake zenu na wana wenu ni maadui wenu, wanawazuia nyinyi na njia ya Mwenyezi Mungu na wanawavunja moyo ya kumtii Mwenyezi Mungu, basi jihadharini nao wala msiwasikilize. Na iwapo mtayasamehe makosa yao, mkayapa mgongo na mkayaficha msiyatangaze, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe ni Mwingi wa rehema, Atawasamehe nyinyi madhambi yenu, kwani Yeye, Aliyetakasika na kila upungufu, ni Mkubwa wa kusamehe ni Mkunjufu wa rehema.
Hayakuwa mali yenu na watoto wenu isipokuwa ni majaribio na mtihani kwenu. Na Mwenyezi Mungu, Kwake Yeye kuna thawabu kubwa kwa aliyechagua kumtii Yeye kuliko kumtii asiyekuwa Yeye na akatekeleza haki ya Mwenyezi Mungu katika mali yake.
Fanyeni juhudi zenu, enyi Waumini, na tumieni nguvu zenu katika kumcha Mwenyezi Mungu, na msikilizeni Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, usikilizaji wa kuzingatia na kufikiri, zifuateni amri Zake na myaepuke makatazo Yake na mtoe katika kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, hilo litakuwa bora kwenu. Na atakayeepukana na uchoyo na kubania kilichozidi katika mali, basi hao ndio watakaozipata kheri zote, watakaofaulu kupata kila wanalolitaka.
Iwapo mtatoa mali yenu katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Yeye na kwa moyo mzuri, Atawaongezea Mwenyezi Mungu thawabu za ambacho mmekitoa na Atawasamehe madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kurudisha shukrani kwa watoaji kwa kuwapa malipo mema ya kile walichokitoa, ni Mpole kwa kutoharakisha mateso kwa wanaomuasi.
Na Yeye, kutakasika na kila upungufu ni Kwake, ni Mjuzi wa kila lililofichika lisionekane na lile lililojitokeza likaonekana, ni Mshindi Asiye na mshindani, ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake na matendo Yake.