ﰡ
Kwa hakika wamefaulu wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wenye kuzitumia sheria Zake.
Wale ambao miongoni mwa sifa zao ni kwamba wao ni wanyenyekevu kwenye Swala zao, nyoyo zinajishughulisha na hiyo Swala tu na viungo vyao vimetulia kwayo.
Na wale ambao wanaacha kila lisilo na wema ndani yake, la maneno na la vitendo.
Na wale ambao wanazitakasa nafsi zao na mali zao kwa kutoa Zaka za aina mbalimbali za mali zao.
Na wale ambao wanazihifadhi tupu zao kwa kuziepusha na mambo Al;iyoyafanya haramu Mwenyezi Mungun ya uzinifu, ulawiti na machafu mengine.
Isipokuwa kwa wake zao au wajakazi waliomilikiwa na mikono yao ya kulia. Hao, Waumini hawana lawama wala makosa kuwaingilia na kujistarehesha nao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewahalalishia.
Basi mwenye kutaka kujistarehesha na asiyekuwa mkewe au mjakazi wake, huyo ni miongoni mwa wenye kuikiuka halali na kuijia haramu na atakuwa amejiorodhesha nafsi yake kwenye mateso ya Mwenyezi Mungu na hasira Zake.
Na wale ambao wanavitunza vitu vyote walivyoaminiwa nazo na wanatekeleza ahadi zao zote.
Na wale ambao daima wanazitekeleza Swala zao kwa nyakati zake na kwa namana iliyowekwa na Sheria iliyokuja kutoka kwa Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye.
Hao ndio Waumini wenye kuirithi Pepo.
Ambao watairithi Pepo ya juu kabisa na ya kati na kati, nayo ndiyo yenye mashukio bora zaidi kuliko zote, wao humo watakaa milele, neema zao hazitakatika wala hazitaondoka.
Na kwa hakika tulimuumba Ādam kutokana na udongo uliochukuliwa kutoka ardhi yote.
Kisha tukawaumba watoto wake wakiwa ni wenye kuzaana kutokana na tone la maji: nalo ni manii ya wanaume, yanatoka kwenye migongo yao na yanatulia ndani ya zao za wanawake.
Kisha tukaliumba hilo tone kwa kuligeuza kulifanya pande la damu iliyo nyekundu, kisha tukaliumba pande la damu kwa kuligeuza kulifanya kinofu cha nyama kadiri ya kutafunika baada ya siku arubaini, na tukakiumba kinofu cha nyama kilicho laini kwa kukigeuza kukifanya mifupa, na tukaivisha nyama ile mifupa, kisha tukamfanya ni kiumbe kingine kwa kuvuvia roho ndani yake. Ametukuka Mwenyezi Mungu Mwenye kheri nyingi Ambaye Ametengeneza umbo la kila kitu.
Kisha nyinyi, enyi binadamu, baada ya vipindi vya maisha na umri kukoma, mtakufa.
Kisha nyinyi, baada ya kufa na dunia kumalizika, mtafufuliwa mkiwa hai kutoka makaburini mwenu muhesabiwe na mlipwe.
Kwa hakika tuliziumba juu yenu mbingu saba, moja juu ya nyingine, na hatukuwa tumeghafilika na viumbe, hatughafiliki na kiumbe wala hatumsahau.
Na tumeteremsha kutoka mbinguni maji kwa kadiri ya mahitaji ya viumbe, na tumeifanya ardhi kuwa ni mahali pa kutulia haya maji, na sisi niwaweza wa kuyaondoa maji haya yaliyotulia. Katika haya pana kitisho na onyo kwa wenye udhalimu.
Tukawafanyia kwa maji haya mashamba ya mitende na mizabibu, mukawa nayo nyinyi kutokana na mashamba hayo matunda ya aina nyingi na sampuli mbalimbali, na katika hayo munakula.
Na tukawatolea nyinyi kwa maji hayo mizaituni ambayo inatoka kandokando ya jabali la Tūr Ṣīnā’ ambao unakamuliwa mafuta ya kujipaka na kutumia kwa chakula.
Na nyinyi, enyi watu, muna mazingatio katika ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo ya kulizingatia namna ya kuumbwa kwao. Tunawanywesha maziwa yanayotoka matumboni mwao. Na munayo nyinyi kutokana nao manufaa mengine mengi kama sufi na ngozi na mfano wa hivyo, na miongoni mwao mnakula.
Na juu ya ngamia na majahazi, katika nchi kavu na baharini munabebwa.
Kwa hakika, tulimtumiliza Nūḥ kwa watu wake kuwalingania kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, (alipokwenda) akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu peke Yake, nyinyi hamuna muabudiwa yoyote isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, basi mtakasieni ibada. Kwani nyinyi hamuiogopi adhabu yake?»
Basi wale waheshimiwa wa watu wake walimkanusha na wakasema kuwaambia watu wa kawaida wao, «Yeye ni mwanadamu kama nyinyi, hana ubora wowote wa kutafautiana na nyinyi, na hataki kwa maneno yake isipokuwa uongozi na utukufu juu yenu, na lau Mwenyezi Mungu Alitaka kutuletea mtume, Angalimtuma Malaika kwetu, hatujasikia mfano wa hili kwa watu waliotutangulia miongoni mwa mababa na mababu. Na huyu Nūh
hakuwa isipokuwa ni mwanamume aliyeshikwa na wazimu, basi ngojeeni mpaka atakapopata fahamu auache ulinganizi wake au afe mupumzike na yeye.»
Nūḥ akasema, «Mola wangu! Niokoe na watu wangu kwa sababu ya kunikanusha mimi kwa yale niliyowafikishia ya ujumbe wako.»
Hapo tukamletea wahyi na kumwambia, «Tengeneza jahazi chini ya uangalizi wetu na amri yetu kwako na usaidizi wetu, na wewe uko kwenye utunzi wetu na hifadhi yetu. Basi amri yetu itakapokuja ya kuwaadhibu watu wako kwa kuwazamisha, na mafuriko yakaanza, na maji yakatembuka kwa nguvu kwenye tanuri, napo ni mahali pa kuchomea mikate, ikiwa ni alama ya kuja kwa adhabu, hapo basi watie ndani ya jahazi, kati ya kila kilicho hai, kiume na kike, ili kizazi kisalie. Na uwatie watu wako pia, isipokuwa yule aliyestahili kuadhibiwa kwa ukafiri wake, kama mke wako na mwano wa kiume, na usiniombe kuokolewa watu wako waliodhulumu, kwani wao hapana budi ni wenye kuzamishwa. Na katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya jicho kwa Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kama inavyonasibiana na Yeye, Aliyetukuka, bila kufananisha wala kulifanya liko namna gani.
‘’Basi ukiwa juu ya jahazi na ukatulia humo wewe na walio pamoja na wewe, mukiwa mumesalimika na kuzama, sema, ‘Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyetuokoa na watu makafiri.’»
Na useme, «Mola wangu! Nifaniye wepesi uteremkaji uliobarikiwa wenye amani, na wewe ndiye bora wa wenye kuteremsha.» Katika hili pana mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, kwa waja Wake wasome dua hii wateremkapo mahali.
Kwa hakika, katika kuwaokoa Waumini na kuwaangamiza makafiri, pana dalili wazi zakuonesha ukweli wa Mitume wa Mwenyezi Mungu katika yale waliokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na sisi ni wenye kuwapa mtihani watu kwa kuwapelekea Mitume kwao kabla mateso hayajawashukia.
Kisha tukawaleta baada ya watu wa Nūḥ kizazi kingine, nacho ni kile cha watu wa kabila la ‘Ād.
Tukampeleka kwao Mtume miongoni mwao, naye ni Hūd, amani imshukiye, akawaambia, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, hamuna muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Je, hamuogopi mateso Yake mtakapomuabudu asiyekuwa Yeye?»
Watukufu na viongozi waliomkufuru Mwenyezi Mungu miongoni mwa watu wake na waliokataa kuwa kuna maisha ya Akhera na zikawafanya wakiuke mipaka zile neema walizoneemeshwa ulimwenguni za maisha ya anasa za kupindukia, «Huyu anayewaita mumpwekeshe Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, si lolote isipokuwa ni mwanadamu kama nyinyi, anakula chakula cha aina mnachokula nyinyi, na anakunywa aina ya kinywaji mnachokunywa.
«Na lau mtamfuata binadamu kama nyinyi, basi nyinyi mtakuwa wakati huo ni wenye kupata hasara kawa kuwaacha waungu wenu na kumfuata yeye.
«Vipi mtayaamini yale anayowaahidi kwamba nyinyi mkifa na mkawa mchanga na mifupa iliyovunjika vipande-vipande, kuwa mtatolewa kutoka kwenye makaburi yenu mkiwa hai?
«Kwa hakika, liko mbali sana hilo mnaloahidiwa, enyi watu, la kwamba nyinyi mtatolewa makaburini mwenu mkiwa hai baada ya kufa kwenu.
«Maisha yetu ni ya hapa duniani tu, wazazi wanakufa na watoto wanaishi. Na sisi si wenye kutolewa tukiwa hai mara nyingine.
«Na huyu, Anayewalingania kwenye Imani, hakuwa isipokuwa ni mtu amemzulia Mwenyezi Mungu urongo. Na sisi si wenye kuyaamini anayoyasema.»
Hapo Mtume wao Alimuomba Mola wake akisema, «Ewe Mola wangu! Ninusuru juu yao kwa kuwa wamenikanusha.»
Mwenyezi Mungu Akasema Akiyakubali maombi yake, «Kwa muda mchache watakuwa ni wenye kujuta.» Yaani, baada ya kipindi cha muda mchache watakuwa na majuto hao wakanushaji.»
Hawakupitiwa na muda, uliwajia wao ukelele mkali pamoja na upepo ambao kwa upepo huo Mwenyezi Mungu Aliwaangamiza, wakafa wote na wakawa ni kama takataka za mtiririko wa maji zinazoelea juu ya maji. Basi maangamivu ni ya hawa madhalimu, na kuwa mbali na rehema ya Mwenyezi Mungu ni kwao. Kwa hivyo, na wajihadhari wenye kusikia, wasije wakawakanusha Mitume wao, ikawashukia wao adhabu ilyowashukia waliowatangulia.
Kisha tukawaleta, baada ya hawa waliokanusha, ummah na viumbe wengine, kama watu wa Lūṭ, Shu'ayb, Ayyūb na Yūnus, rehema za Mwenyezi Mungu na amani Yake ziwashukie.
Hautangulii ummah wowote, miongoni mwa ummah hawa wanaokanusha Mitume wao, muda uliowekewa kuangamia kwake, wala hauchelewi.
Kisha tukawapeleka Mitume wetu waende kwa ummah hao, wakifuatana: hawa baada wengine. Na kila Mtume akiwalingania watu wake, wanamkanusha. Basi tukawafuatisha, kundi baada ya kundi, kwa kuwaangamiza na kuwamaliza, na hakuna kilichosalia isipokuwa ni habari za kuangamia kwao.Na tukazifanya habari hizo ni maneno ya kuzungumzwa na watu waliokuja baada yao, wakizichukuwa kuwa ni mazingatio. Basi maangamivu na kuepushwa na kila kheri ni kwa watu wasiowaamini Mitume wala kuwatii.
Kisha tukampeleka Mūsā na ndugu yake Hārūn kwa alama zetu tisa, nazo ni fimbo, mkono, nzige, chawa, vyura, damu, mafuriko, shida za maisha na upungufu wa matunda, zikiwa ushahidi uliyo wazi wenye kuzishinda nyoyo, zipate kulainika kwa alama hizo nyoyo zaWaumini, na isimame hoja juu ya washindani. Tuliwapeleka wao wawili
kwa Fir'awn, hakimu wa Misri, na watukufu wa watu wake ambao walifanya kiburi wakakataa kumuamini Mūsā na ndugu yake. Na wao walikuwa ni watu wanaojiona bora kuliko watu wengine na walikuwa wakiwanyanyasa kwa kuwadhulumu.
Wakasema, «Je, tuwaamini watu wawili kama sisi, na jamaa zao Wana wa Isrāīl wako chini ya amri yetu, wanatutii na wanajidhalilisha kwetu.?»
Basi wakawakanusha katika yale waliyokuja nayo, wakawa ni wenye kuangamizwa kwa kuzamishwa baharini.
Hakika tulimletea Mūsā Taurati, ili watu wake wajiongoze nayo kwenye haki.
Na tulimjaalia Īsā mwana wa Maryam na mamake ni alama yenye kuonesha uweza wetu, kwani tulimuumba bila ya baba, na tulimfanyia makao kwenye ardhi iliyopo mahali pa juu palipolingana ili apate utulivu juu yake, penye urutuba na maji yapitayo yanayoonekana waziwazi kwa macho.
Enyi Mitume! Kuleni riziki ya halali na fanyeni matendo mema, kwani mimi kwa mnayoyafanya ni mjuzi, hakuna kitu chochote chenye kufichika kwangu katika matendo yenu. Wanaohutubiwa katika aya hii ni Mitume wote kwa jumla, amani iwashukie, na wafuasi wao. Na katika aya pana dalili kwamba kula halali inasaidia kufanya matendo mema na kwamba mwisho wa haramu ni mbaya na miongoni mwa ubaya wake ni kurudishwa dua kwa kutokubaliwa.
Na kwa hakika Dini yenu, enyi Mitume, ni Dini moja, nayo ni Uislamu, na mimi ni Mola wenu niogopeni kwa kufuata maamrisho yangu na kujiepusha na makatazo yangu.
Na wafuasi walipambanukana katika dini wakawa makundi na mapote, wakaifanya dini yao kuwa dini nyingi baada ya kuamrishwa wajikusanye pamoja. Kila kundi linajigamba kwa maoni yake, linadai kuwa kundi hilo liko kwenye haki na lingine liko kwenye batili. Katika haya pana onyo la kujiweka kwenye makundi na kupambanukana katika Dini.
Basi waache , ewe Mtume, kwenye upotevu wao na ujinga wao wa kutoijua haki hadi pale adhabu itakapowashukia.
Kwani wanadhani hawa makafiri kwamba yale tunayowapa ya mali na watoto ulimwenguni ni mazuri waliyoharakishiwa na kwamba wao wanastahiki hayo?
Hakika tunawaharakishia haya mazuri kwa kuwatahini na kwa kuwavuta kidogo kidogo, lakini wao hawalihisi hilo.
Hakika wale ambao kwa kumcha Mola wao wanayaogopa na kujitahadhari na yale Aliyowaogopesha nayo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Na wale ambao wao wanaziamini aya za Mwenyezi Mungu katika Qur’ani na wanazitumia.
Na wale ambao wao wanaitakasa ibada kwa Mwenyezi Mungu , Peke Yake, na hawamshirikishi na Yeye mwingine asiyekuwa Yeye.
Na wale wanaojibidiisha kufanya matendo ya kheri na wema, mioyo yao ina kicho cha kuogopa yasikubaliwe matendo yao na yasiwaokoe na adhabu ya Mola wao warejeapo Kwake kwa kuhesabiwa.
Hao wanaojibidiisha kutii, dasturi yao ni kukimbilia kufanya kila kitendo chema, na wao kwa kuyaendea mambo mema ni wenye kutangulia.
Hatumlazimishi mja yoyote miongoni mwa waja wetu isipokuwa kile kinachomkunjukia kukifanya, na matendo yao yamesajiliwa kwetu ndani ya Kitabu cha kudhibiti matendo, ambacho Malaika watakiinua, kitakachosema ukweli juu yao, na hakuna yoyote kati yao Atakayedhulumiwa.
Lakini nyoyo za makafiri ziko kwenye upotevu uliowafinika, zimejiepusha na Qur’ani na yaliyomo ndani yake. Na wao, pamoja na ushirikina wao, wana matendo mabaya, Mwenyezi Mungu Anawapa muhula wayafanye, ili ziwapate wao hasira za Mwenyezi Mungu na mateso Yake.
Mpaka tutakapowashika wenye gogi na kiburi miongoni mwao kwa adhabu yetu, hapo ndipo watainua sauti zao wakinyenyekea na wakiomba waokolewe.
Na hapo waambiwe, «Msipige kelele wala msiombe kuokolewa leo! Nyinyi hamuwezi kuziokoa nafsi zenu, na hakuna yoyote atakayewaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
«Zilikuwa aya za Qur’ani zikisomwa kwenu, ili mupate kuziamini, na mlikuwa mnazikimbia hamtaki kuzisikia na kuzikubali na kuzitumia, kama anavyofanya mwenye kurudi nyuma kwa kule kurudi kwake nyuma.
«Mnalifanya hilo na huku mnawaonesha watu kiburi pasi na haki kwa sababu ya Nyumba ya Mwenyezi Mungu tukufu. Mnasema, ‘Sisi ni watu wa Nyumba hiyo, hatushindwi tukiwa hapo,’ na mnakesha mkiwa kando-kando yake kwa maneno maovu.»
Kwani hawayafikirii yaliyomo ndani ya Qur’ani wakapata kujua ukweli wake au limewazuia wao kuamini kwa kuwa wamejiwa na Mtume na kitabu ambacho mfano wake hakikuwajia baba zao wa mwanzo, wakakikanusha kwa ajili hiyo na wakakipa mgongo?
Au limewazuia wao kuifuata haki kwa kuwa Mtume wao, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hajulikani kwao na kwa hivyo wanamkataa?
Au wanamdhania kuwa ni mwendawazimu? Kwa hakika wamedanganya. Ukweli ni kuwa amewajia na Qur’ani, upwekeshaji Mwenyezi Mungu na dini ya kweli. Na wengi wao wanaichukia haki kwa uhasidi na uadui.
Lau kama Mwenyezi Mungu Angaliwawekea sheria inayolingana na mapendeleo yao, zingaliharibika mbingu na ardhi na vilivyomo humo. Bali tumewaletea yale ambayo ndani yake muna alama za nguvu yao na utukufu wao, nayo ni Qur’ani, na wao wanaipa mgongo.
Au limewazuia wao kukuamini kwa kuwa wewe, ewe Mtume, unawaomba malipo juu ya ulinganizi wako kwao, hivyo basi wakafanya ubahili? Hukufanya hivyo, kwa kuwa zile thawabu zilizoko kwa Mwenyezi Mungu na vipewa ni bora zaidi. Na Yeye ni bora wa wanaoruzuku, hakuna awezaye kuruzuku kama Yeye Anavyoruzuku, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake.
Kwa hakika wewe, ewe Mtume, unawalingania watu wako na wengineo kwenye Dini iliyolingana sawa, nayo ni Dini ya Uislamu.
Na kwa hakika, wale ambao hawaamini kufufuliwa na kuhesabiwa wala hawayafanyii kazi hayo mawili, basi hao wamepotoka kando ya njia ya Dini iliyonyoka, nayo ni dini ya Uislamu.
Na lau tungaliwahurumia na tukawaaondolea ukame na njaa, wangaliendelea kwenye ukafiri na ushindani, wakiwa katika hali ya kuduwaa na kukosa muelekeo.
Na kwa hakika, tuliwajaribu wao kwa kuwaonja kwa aina mbalimbali za mikasa, pamoja na hivyo wasimnyenyekee Mola wao na wasimuombe kwa unynyekevu wakati wa kushukiwa na hiyo mikasa.
Mpaka tulipowafungulia juu yao mlango wa adhabu kali huko Akhera, wakitahamaki wamo ndani yake, wamekata tamaa kupata kheri yoyote, wamechanganyikiwa hawajui wafanye nini.
Na yeye Ndiye Aliyewaumbia masikizi ya kuvisikia venye kusikika, na macho ya kuviona venye kuonekana, na nyoyo ili muelewe. Pamoja na hayo, shukrani zenu kwa hizi neema za mfululizo juu yenu bado ni chache hata hazitajiki.
Na yeye Ndiye Aliyewaumba watu wote katika ardhi, na Kwake Yeye mtakusanywa baada ya kufa kwenu, na hapo Atawalipa kwa mliyoyatenda, mema au maovu.
Na Yeye , Peke Yake, Ndiye Anayehuisha kutoka katia hali ya kutokuweko, na Ndiye Atakayefisha baada ya uhai. Na ni kwake Yeye kufuatana usiku na mchana na pia kupishana. Basi hamuuweki akilini mwenu uweza Wake na upweke Wake?
Lakini makafiri hawakuamini kuwa kuna kufufuliwa, lakini waliyakariri maneno ya wakale wao wakanushaji.
walisema «Ati tutakapokufa na miili yetu ikatangamana na mchanga wa ardhi pamoja na mifupa yetu tutafufuliwa mara nyingine? Hili haliwi wala haliingii akilini.»
Yameshasemwa maneno haya kuambiwa wazee wetu kitambo, kama vile unavyotuambia, ewe Muhammad, hatukuyaona kuwa yana uhakika. Hayakuwa haya isipokuwa ni porojo za watu wa kale.
Waambie, «Ni ya nani Ardhi hii na walio ndani yake iwapo muna ujuzi?»
Watakubali kwa lazima kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, Yeye Ndiye Muumba wake na Ndiye Mwenye kuimiliki. Waambie, «Je, haliwi hilo kwenu ni lenye kuwafanya mukumbuke kuwa Yeye ni Muweza wa kuwafufua wafu na kuwarudishia uhai?»
Sema, «Ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa ‘Arsh iliyo kubwa, ambayo ndiyo kiumbe kikubwa kabisa na kilichoko juu kabisa?»
Watasema kwa lazima kuwa hizo ni milki ya Mwenyezi Mungu. Basi waambie, «Mbona hamuogopi adhabu ya Mwenyezi Mungu mnapomuabudu asiyekuwa Yeye?»
Sema, «Ni nani mmiliki wa kila kitu? Na ni nani Ambaye mkononi Mwake kuna hazina za kila kitu? Na ni nani Anayempa himaya mwenye kutaka himaya Yake, ambapo hakuna anayeweza kumhami na kumlinda yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuangamiza wala hakuna anayekinga shari Aliyoikadiria Mwenyezi Mungu, iwapo mnalijua hilo?»
Watajibu kuwa hayo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Sema uwaambie, «Vipi zinaondoka akili zenu na mnadanganywa na mnaepushwa njia ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtii na kuyaamini mambo ya kufufuliwa na kurudishiwa uhai?»
Ilivyo ni kwamba tumewaletea wakanushaji hawa ukweli wa yale tuliyompeleka kwayo Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na kwa hakika wao ni warongo kwenye ushirikina wao na ukanushaji wao kufufuliwa.
Mwenyezi Mungu Hakujifanyia mwana, na hakukuwa pamoja na Yeye muabudiwa mwingine, kwani kama kungalikuwa huko kuna waabudiwa zaidi ya mmoja pamoja na Yeye, basi kila muabudiwa angalijitenga na alivyoviumba na kungalikuwa na ushindani kati yao kama ilivyo kwa watawala wa ulimwnguni. Hapo mpango wa ulimwengu ungaliharibika. Ametakasika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuepukana na sifa wanazompa za kuwa Yeye ana mshirika au mwana.
Yeye, Peke Yake, Ndiye Anayejua yanayofichika kwa viumbe vyake na wanayoyaona. Basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameepukana na mshirika ambaye wanadai kuwa Anaye.
Sema, ewe Mtume, «Mola wangu! Unioneshapo kwa hawa washirikina ile adhabu yako uliyowaonya nayo,
basi usiniangamize kwa ile uliyowaangamiza nayo. Na uniokoe na adhabu yako na hasira zako. Usiniweke pamoja na watu washirikina na madhalimu. Bali niingize kwa wale uliokuwa radhi nao.»
Na kwa hakika sisi tunaweza kukuonesha yale tunayowaahidi ya adhabu.
Pindi wanapokufanyia ubaya maadui zako, ewe Mtume, kwa maneno au vitendo, basi usiwalipe ubaya, lakini uondoshe ubaya wao kwa kuwafanyia wema. Sisi tunayajua mno yale wanayokubandika washirikina ya sifa za ushirikina na kukukanusha, na Atawalipa kwa hayo malipo maovu mno.
Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Najilinda kwako na upotezaji wa Mashetani unaoupelekea kwenye ubatilifu na uharibifu na kuzuia watu wasiifuate haki.
Na ninajilinda kwako, ewe Mola wangu, na kuingiliwa na wao kwenye mambo yangu.»
Mwenyezi Mungu Anawatolea habari makafiri au waliokiuka mipaka ya amri Yake, Aliyetukuka, walioko kwenye hali ya kusongwa na kifo, mauti yalipowafikia na wakaishuhudia adhabu waliyoandaliwa, hapo huwa akisema kila mmoja wao, «Mola wangu! Nirudisha ulimwenguni.
«Huenda mimi nikayarekebisha yale niliyoyapoteza ya imani na utiifu.» Hatolipata hilo, kwani hatakubaliwa hilo aliloliomba wala hatapewa muhula. Hilo ni neno tu atalisema. Ni neno lisilomnufaisha, na yeye kwa neno hilo si mkweli, kwani lau angalirudishwa ulimwenguni angaliyarudia yale aliyokatazwa. Na Wenye kufa watasalia kwenye kizuizi na kitengo kilichoko kati ya Akhera na duniani mpaka Siku ya kufufuliwa na kukusanywa.
Basi Siku ya Kiyama itakapokuwa, na Malaika anayehusika akavivia kwenye baragumu, na watu wakafufuliwa kutoka makaburini mwao, hapo hakuna kujigamba kwa nasaba kama walivyokuwa wakijigamba nazo duniani wala hapana yoyote atakayemuuliza yoyote.
Basi yule ambaye mema yake yatakuwa mengi na zikawa nzito kwayo mizani za matendo yake Siku ya kuhesabiwa, basi hao ndio wenye kufaulu kupata Pepo.
Na yule ambaye mema yake yatakuwa machache kwenye mizani na maovu yake yatakuwa mengi zaidi, na kubwa zaidi ya hayo maovu ni ushirikina, basi hao ndio ambao wamepita patupu na wakaziangamiza nafsi zao kwenye moto wa Jahanamu, watasalia humo milele.
Moto huo utaunguza nyuso zao, na wao humo watakuwa ni wenye kufinya nyuso, midomo yao imekauka na meno yao yamejitokeza nje.
Wataambiwa, «Je, hamkuwa mkisomewa aya za Qur’ani huko duniani, mkawa mnazikanusha?»
Wakikubali kuwa Mitume wao waliwapelekea ujumbe na wakawaonya, watasema Siku ya Kiyama, «Mola wetu! Raha zetu, na pia matamanio yetu yalikadiriwa kwetu kwenye ujuzi wako uliotangulia, zilitutawala na kwa hivyo tukawa, katika matendo yetu, ni wenye kupotea na kuwa kando ya njia ya uongofu.
«Mola wetu! Tutoe Motoni na uturudishe duniani. Na huko, tukirudi upotevuni, basi kwa kweli sisi ni madhalimu tunastahili kuadhibiwa.»
Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Atawaambia, «Kaeni Motoni mkiwa wanyonge wala msiseme na mimi.» Hapo yatakatika maombi yao na matumaini yao.
«Kulikuwa na kundi la waja wangu, nao ni Waumini, wakiomba kwa kusema, ‘Mola wetu! Tumeamini, basi yasitiri madhambi yetu na uturehemu, na wewe ndiye bora wa kurehemu.’
«Mkajishughulisha kuwacheza shere, mpaka mkasahau kumtaja Mwenyezi Mungu na mkasalia kwenye ukanushaji wenu, na kwa kweli mlikuwa mkiwacheka kwa shere na dharau.
«Mimi nilililipa kundi hili la waja wangu Waumini kwa kuwafanya wafuzu kupata Pepo kwa sababu ya uvumilivu wao juu makero na utiifu kwa Mwenyezi Mungu»
Na watu waovu wataulizwa wakiwa Motoni, «Mlisalia miaka mingapi ulimwenguni? Na mlipoteza mangapi huko ya kumtii Mwenyezi Mungu?»
Watasema kwa kituko cha Kisimamo na ukali wa adhabu, «Tulikuwa huko kwa siku moja au sehemu ya siku. Waulize washika hesabu wenye kuhesabu miezi na siku.»
Hapo Atawaambia «Hamkuketi isipokuwa kipindi kichache, na lau mlivumilia juu ya kumtii Mwenyezi Mungu mungalifaulu kuipata Pepo, kama mungalikuwa na ujuzi wa hilo.» Hivyo ni kwamba kipindi cha kukaa kwao duniani ni kichache sana kulingana na kipindi cha kukaa kwao Motoni milele.
Je, mlidhania, enyi viumbe, ya kwamba sisi tuliwaumba nyinyi mkiwa mumepuuzwa: hakuna maamrisho wala makatazo wala malipo mema wala mateso, na kwamba nyinyi hamtorudishwa kwetu Akhera kwa Hesabu na Malipo?
Ametukuka Mwenyezi Mungu Aliye Mfalme, Anayepelekesha kila kitu, Ambaye Yeye ni Kweli, ahadi Yake ni kweli na onyo Lake ni kweli na kila kitu kutoka Kwake ni kweli. Ametakasika na kuwa Ataumba kitu kwa upuuzi au pasi na maarifa. Hapana mola isipokuwa Yeye, Mola wa ‘Arsh tukufu ambayo ndicho kiumbe kikubwa kuliko vyote.
Na yoyote atakayeabudu, pamoja na Mwenyezi Mungu Aliyepwekeka, mungu mwingine, asiyekuwa na hoja yoyote juu ya ustahiki wake kuabudiwa. Basi kwa kweli malipo yake juu ya kitendo chake hicho kiovu yako mbele ya Mola wake huko Akhera. Ukweli ni kwamba hakuna kufuzu wala kuokoka kwa makafiri Siku ya Kiyama.
Na useme, ewe Nabii, «Mola wangu! Samehe madhambi na urehemu. Na wewe ndiye bora wa anayemrehemu mwenye dhambi, akaikubali toba yake na asimtese kwa dhambi zake