ترجمة سورة إبراهيم

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة إبراهيم باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Alif, Lām, Rā. Hii Qur’ani ni kitabu tulichokuletea wahyi ili uwatoe binadamu kutoka kwenye upotevu na upotovu kuwapeleka kwenye uongofu na mwangaza, kwa idhini ya Mola wao na taufiki Yake kwao, kwenye Uislamu ambao ndio njia ya Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda Anayehimidiwa kwa kila hali.
Mwenyezi Mungu Ambaye ni Vyake vilivyoko mbinguni na vya ardhini, kwa kuviumba, kuvimiliki na kuviendesha. Yeye Ndiye Ambaye ni lazima ibada Afanyiwe Yeye Peke Yake. Na wale waliogeuka na wasimuamini Mwenyezi Mungu na wasiwafuate Mitume Wake watapata maangamivu na adhabu kali Siku ya Kiyama.
Na hawa wenye kugeuka wasimuamini Mwenyezi Mungu na wasimfuate Mtume Wake ndio wanaochagua maisha ya dunia yenye kutoeka na wanaacha Akhera yenye kusalia, wanawakataza watu kufuata dini ya Mwenyezi Mungu na wanaitaka iwe ni njia iliyopotoka ili iafikiane na mapendeleo yao. Hao waliosifiwa kwa sifa hizi wamo ndani ya upotevu wa kutoiona haki, wako mbali na njia zote za uongofu.
Na hatukutuma Mitume kabla yako, ewe Nabii, isipokuwa kwa lugha ya watu wake, ili awafafanulie sheria ya Mwenyezi Mungu, ili Mwenyezi Mungu Apate kumpoteza Anayemtaka awe kando na uongofu na Amwongoze Anayemtaka kwenye ukweli. Na yeye Ndiye Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwenye hekima Anayeyaweka mambo mahali pake kulingana na hekima.
Na kwa hakika tulimtuma Mūsā kwa Wana wa Isrāīl na tukamsaidia kwa miujiza yenye kuonyesha ukweli wake na tukammpa amri awalinganie wao kwenye Imani, ili awatoe wao kutoka kwenye upotevu awatie kwenye uongofu na awakumbushe neema za Mwenyezi Mungu na mateso Yake katika wakati wake. Katika kukumbusha huku mambo hayo kuna dalili nyingi kwa kila mvumilivu sana juu ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, kuyaepuka yaliyoharamishwa na Yeye na kuyakubali maandiko Yake, mwenye kushukuru sana, mwenye kusimama kutekeleza haki za Mwenyezi Mungu na anayemshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake. Aina mbili hizi za watu zimetajwa mahsusi, kwa kuwa wao ndio wanaozingatia hizo dalili na hawaghafiliki nazo.
Na watajie, ewe Mtume, watu wako kisa cha Mūsā pindi alipowaambia watu wake, «Tajeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu alipowaokoa kutokana na Fir'awn na wafuasi wake waliokuwa wakiwaonjesha adhabu kali zaidi, wakiwaua watoto wenu wa kiume, ili asitokee kati yao atakayeuvamia ufalme wa Fir'awn, na walikuwa wkiwaacha wanawake wenu kwa kutumika na kudharauliwa. Na katika misukosuko hiyo na kuokolewa huko ni mtihani mkubwa utokao kwa Mola wenu.»
Mūsā aliwaambia, «Na kumbukeni pindi Mola wenu alipowajulisha kwa kuwasisitiza kwamba mkimshukuru kwa neema Zake Atawazidishia nyongeza Zake, na mkikanusha neema ya Mwenyezi Mungu, Atawaadhibu adhabu kali.»
Na akawaambia, «Mkimkanusha Mwenyezi Mungu , nyinyi na watu wa ardhini, hamtamdhuru Mwenyezi Mungu kitu chochote. Kwani Mwenyezi mungu ni Mkwasi kutowahitajia viumbe Vyake, ni mstahiki wa kushukuriwa na kusifiwa, ni mshukuriwa kwa hali zote.»
Kwani haikuwajia, enyi ummah wa Muhammad, habari za ummah waliowatangulia: watu wa Nūḥ, watu wa Hūd, watu wa Ṣāliḥ na ummah waliokuja baada yao? Hakuna anayeidhibiti idadi yao isipokuwa Mwenyezi Mungu. Mitume wao waliwajia kwa hoja waziwazi, wakaiuma mikono yao kwa hasira na kwa kiburi cha kutoikubali Imani, na wakasema kuwaambia Mitume wao, «Sisi hatuyaamini mliyotuletea, na sisi tuko kwenye shaka yenye kutia wasiwasi juu ya yale unayotuitia kwayo ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha.»
Mitume wao wakasema kuwaambia, «Je, pana shaka yoyote juu ya Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye Ndiye Muabudiwa Peke Yake, na hali Yeye ni Muumba wa mbingu na ardhi na Mwenye kuzifanya zipatikane kutoka kwenye hali ya kutokuwako bila ya kuwa na mfano uliotangulia, na hali Yeye Anawaita kwenye Imani Apate kuwasamehe mliyoyatanguliza ya ushirikina na Awaepushie adhabu ya kumaliza kabisa, Awape nafasi ya kusalia ulimwenguni mpaka muda Aliyoupanga ambao ni kikomo cha nyakati za maisha yenu, Asiwaadhibu duniani? Wakawaambia Mitume wao, «Hatuwaoni nyinyi isipokuwa ni binadamu, hali zenu ni kama zetu, hamna ubora wowote juu yetu wa kuwafanya muwe Mitume. Mnataka kutuzuia kuviabudu vitu ambavyo baba zetu walikuwa wakiviabudu miongoni mwa masanamu na mizimu. Basi tuletee hoja iliyo wazi yenye kuonyesha usahihi wa yale mnayoyasema.
Mitume waliposikia yale yaliyosemwa na watu wao waliwaambia, «Ni kweli kwamba sisi hatukuwa isipokuwa ni binadamu kama nyinyi, kama mlivyosema. Lakini Mwenyezi Mungu Anawafanyia wema Anaowataka miongoni mwa waja wake kwa kuwapa neema Zake na kuwateua kwa kuwapa utume Wake. Na hizo dalili waziwazi mlizozitaka, haiwezekani sisi kuwaletea isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na taufiki Yake. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake wanategemea Waumini katika mambo yao yote.
«Na vipi sisi tusimtegemee Mwenyezi mungu , na hali Yeye Ndiye Aliyetuongoza njia ya kuokoka na adhabu Yake kwa kufuata hukumu za dini Yake? Na sisi tutavumilia sana makero yenu kwetu kwa maneno maovu na mengineyo. Na kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake ni lazima Waumini wamtegemee Awapatie nusura ushindi juu ya maadui zao.»
Nyoyo za makafiri ziliingia dhiki kwa maneno ya Mitume na wakasema kuwaambia, «Hakika tutawatoa kutoka miji yetu mpaka mrudi kwenye dini yetu.» Mwenyezi Mungu Akatuma wahyi kwa Mitume kwamba Atawaangamiza wenye kukataa wenye kumkanusha Yeye na Mitume Wake.
«Na tutaufanya mwisho mwema uwe ni wa Mitume na wafuasi wao kwa kuwakalisha kwenye ardhi ya makafiri baada ya kuwaangamiza. Kuwaangamiza huko na kuwakalisha Waumini ardhi yao ni jambo la uhakika kwa anayeogopa kisimamo chake mbele yangu Siku ya Kiyama na akaoogopa unyo langu na adhabu yangu.»
Mitume wakaelekea kwa Mola wao wakamuomba Awape ushindi juu ya maadui wao na Ahukumu baina yao, na Yeye Akawakubalia na Akamwangamiza kila mwenye kujiona asiyekubali haki, Asiyeiandama na Asiyetaka kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasia ibada.
Mbele yake, huyu kafiri, patakuwa na Jahanamu, ataikuta na adhabu yake na atanyweshwa humo usaha na damu zinazotoka kwenye miili ya watu wa Motoni.
Mwenye kiburi atajaribu kumeza usaha na damu na vinginevyo vinavyotiririka mara kwa mara kutoka kwa watu wa Motoni, na hataweza kuzimeza kwa uchafu wake, umoto wake na uchungu wake. Na adhabu kali ya kila aina itamjia kwenye kila kiungo katika mwili wake. Hatakuwa ni mwenye kufa akapumzika. Na baada ya adhabu hii atapatiwa adhabu nyingine yenye kuumiza.
Hali ya matendo mazuri ya makafiri ulimwenguni, kama vile kufanya wema na kuunga zao, ni kama hali ya jivu lililopigwa na upepo wa nguvu katika siku yenye upepo mkali usiache hata alama yake. Hivyo ndivyo yatakavyokuwa matendo yao, hawatapata kwa matendo hayo kitu cha kuwanufaisha mbele ya Mwenyezi Mungu; kwani ukafiri umeyaondoa kama vile upepo ulivyoondoa jivu. Kushughulika huko na kufanya matendo mema huko bila ya msingi, ndio kupotea kuliko mbali na njia ya sawa
Je, hujui, ewe mwenye kwambiwa,- na makusudiwa ni watu kwa jumla- kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyepatisha mbingu na ardhi kwa namna thabiti yenye kuonyesha hekima Yake , na kwamba Yeye Hakuziumba kwa mchezo, bali ni kwa ajili ya kutolea ushahidi juu ya upweke Wake na ukamilifu wa uweza Wake, ili wamuabudu Peke Yake, na wasimshirikishe na kitu chochote? Basi Akitaka Atawaondoa na Awalete watu wasiokuwa nyinyi wanaomtii Mwenyezi Mungu.
Na kuwaangamiza nyinyi na kuwaleta watu wengine wasiokuwa nyinyi si jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu, bali ni jambo lilio pesi.
Na watatoka viumbe kwenye makaburi yao na watajitokeza waziwazi Siku ya Kiyama kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja Mwenye kutendesha nguvu, ili Awahukumu baina yao. Hapo wafuasi watasema kuwaambia viongozi wao , «Sisi tulikuwa kwenu nyinyi ulimwenguni ni wafuasi, tukifuata amri zenu. Je, nyinyi ni wenye kututetea na kuizuia chochote miongoni mwa adhabu ya Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkituahidi? Viongozi watasema, «Lau Mwenyezi Mungu Alituongoza kwenye Imani tungaliwalekeza kwenye hiyo, lakini Yeye Hakutuafikia ndipo tukapotea na tukawapoteza. Ni sawa kwetu sisi na kwenu kuwa na babaiko au kuvumilia, kwani hatuna pa kukimbilia kuepukana na adhabu wala pa kupata uokozai.
Shetani atasema baada ya Mwenyezi Mungu kuamua jambo Lake na kuwahesabu viumbe Vyake, na kuingia watu wa Peponi Peponi na watu wa Motoni Motoni, «Mwenyezi Mungu Aliwaahidi nyinyi ahadi ya kweli ya kufufuliwa na kulipwa, na mimi niliwaahidi ahadi ya urongo kwamba hakuna kufufuliwa wala kulipwa, nikakawaendea kinyume na ahadi yangu. Na mimi si kuwa na nguvu zozote za kuwalazimisha kunifuata, wala si kuwa na hoja. Isipokuwa mimi niliwaita kwenye ukafiri na upotevu mkanifuata. Basi msinilaumu, jilaumuni nyinyi wenyewe. Dhambi ni dhambi zenu wenyewe. Mimi si mwenye kuwaokoa na nyinyi si wenye kunokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Mimi nimejiepusha na jambo la nyinyi kunifanya mimi ni mshirika pamoja na Mwenyezi Mungu katika kutiiwa ulimwenguni. Hakika madhalimu, katika kuupa mgongo kwao ukweli na kuufuata urongo, watakua na adhabu kali iumizayo.
Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema, watatiwa ndani ya mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake na majumba yake ya fahari inapita mito. Hawatatoka humo milele, kwa idhini ya Mola wao na uweza Wake na nguvu Zake. Watasalimiwa humo kwa salamu itokayo kwa Mwenyezi Mungu, Malaika Zake na Waumini.
Kwani huoni, ewe Mtume, namna gani Mwenyezi Mungu alivolipiga mfano neno la tawhīd «Lā ilahā illā Allāh» wa mti mkubwa, nao ni mtende, ambao shina lake limejikita imara ndani ya ardhi na kilele chake kiko juu kimeelekea mbiguni?
Unatoa matunda yake kila kipindi kwa idhini ya Mola wake. Namna hiyo ndivyo ulivyo mti wa Imani: msingi wake umejikita imara ndani ya moyo wa Muumini kiujuzi na kiitikadi, na tagaa zake za matendo mema na tabia za kuridhisha zinapaishwa juu kwa Mwenyezi Mungu, na malipo yake mema yanapatikana kila kipindi. Na Mwenyezi Mungu Anawapigia watu mfano ili wakumbuke na wawaidhike wapate kuzingatia.
Na mfano wa neno ovu, nalo ni neno la ukafiri, ni kama mti muovu wa chakula na ladha, nao ni mti wa subili, uliong’olewa juu ya ardhi, kwa kuwa mizizi yake iko karibu na uso wa ardhi, hauna mizizi iliyojikita ndani wala hauna tagaa zenye kwenda juu. Hivo ndivyo kafiri alivyo, hana uthabiti wala hana wema na wala hakuna tendo lema lake lolote litakalopaishwa kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu Anawathibitisha wale waloamini kwenye neno la ukweli lenye uimara nalo ni kukubali kwamba hakuna mola anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhaamad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwamba Atawathibitisha kwenye dini ya kweli aliyokuja nayo katika huu ulimwengu, Atawapa mwisho mwema wakati wa kufa, na Atawaongoza watoe jawabu ya sawa watakapoulizwa na Malaika wawili kaburini. Na Mwenyezi Mungu Atawapoteza madhalimu wasiuone usawa ulimenguni na Akhera. Na Mwenyezi Mungu Anafanya Analolitaka kwa kuwaafikia wenye kuamini na kutowaongoza wenye kukufuru na kuasi.
Kwani hutazami, ewe mwenye kuambiwa (makusudio ni jumla ya wenye kuambiwa), hali ya wakanushaji miongoni mwa makafiri wa Kikureshi waliochagua kumkanusha Mwenyewzi Mungu badala ya kumshukuru kwa neema ya amani na kutumilizwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwao wao? Na kwa hakika waliwashukisha wafuasi wao nyumba ya maangamivu, waliposababisha kuwatoa wao kwenda Badr wakauawa, na mwisho wao ukawa ni nyumba maangamivu,
nayo ni Moto wa Jahanamu ambao watauingia na wataungulika na joto lake. Na mahali pabaya pa kukaa na kutulia ni hapo penye makao yao.
Na hawa makafiri walimfanya Mwenyezi Mungu ana washirika ambao waliwaabudu pamoja na Yeye, ili wawaepushe watu na Dini Yake. Waambie, «Stareheni katika maisha ya ulimwengu, kwani hayo ni upesi kuondoka, na marejeo yenu na kurudi kwenu ni kwenye adhabu ya Jahanamu.»
Waambie, ewe Mtume, waja wangu walioamini watekeleze Swala kwa namna yake inayotakikana na watoe sehemu ya mali tuliyowapa katika njia za heri, za lazima na za zinazopendekezwa, watoe kwa siri au waziwazi, kabla ya kuja Siku ya Kiyama ambayo haitafaa kitu fidia wala urafiki.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi, Akazifanya zipatikane baada ya kutokuwako, Akateremsha mvua kutoka mawinguni Akaihuisha Ardhi kwa hiyo baada ya kuwa imekufa, Akawatolea nyinyi kutoka ndani ya ardhi vyakula vyenu, Akawadhalilishia majahazi yapate kuenda baharini kwa amri Yake kwa ajili ya manufaa yenu, Akawadhalilishia mito ili munywe nyinyi na wanywe wanyama wenu na kwa ajili ya mimea yenu na manufaa yenu mengine.
Na Akawadhalilishia nyinyi jua na mwezi, haviachi kutembea kwake, ili maslahi yenu yatimie kwa viwili hivyo. Na Akwadhalilishia nyinyi usiku, ili mtulie humo na mpumzike, na mchana ili mtafute fadhila Zake na mpange maisha yenu.
Na Akawapa nyinyi kila mlichomuomba. Na mkihesabu ili kujua idadi ya neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, hamtaweza kuzihesabu na kudhibiti idadi yake wala kusimama itakikanavyo kushukuru kwa hizo kwa wingi wake na aina zake. Hakika Binadamu ni mwingi wa kujidhulumu nafsi yake, ni mwingi wa kukanusha neema za Mola wake.
Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Ibrāhīm aliposema akimuomba Mola Wake, baada ya kumfanyia makao mwanawe wa kiume, Isma'il, pamojaa na mamake, Hajar, kwenye bonde la Makkah, «Ewe Mola ijaalie Makkah ni mji wa amani, awe kila aliye humo yuko kwenye amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.
«Ewe Mola wangu! Masanamu wamesababisha kuwaepusha watu wengi na njia ya ukweli. Basi mwenye kunifuata mimi katika kumpwekesha Mwenyezi Mungu, yeye atakuwa kwenye Dini yangu na mwendo wangu, na mwenye kwenda kinyume na mimi, katika mambo ambayo si ya ushirikina, basi wewe ni Mwingi wa kusamehe dhambi za wenye kufanya madhambi, kwa fadhila zako, ni Mwingi wa huruma kwao, unamsamehe unayemtaka miongoni mwao.
«Ewe Mola wetu! Mimi nimewafanya watoto wangu wakae kwenye bonde lisilo na mimea wala maji, penye ujirani na mji wako mtakatifu. Mola wetu! Mimi nimefanya hilo kwa amri Yako, ili wasimamishe Swala kwa namna yake itakikanayo, basi ifanye myoyo ya baadhi ya viumbe vyako ilemee kwao na ipendelee, na uwape riziki ya kila aina ya matunda wakiwa mahali hapa, ili wakushukuru kwa neema zako.» Mwenyezi Mungu Akakubali maombe yake.
«Ewe Mola wetu! Hakika wewe unajua kila tunachokificha na tunachokionyesha. Na hakuna chochote chenye kupotea na kuwa nje ya ujuzi wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa vilivyoko ardhini na mbinguini.»
Ibrāhīm anamsifu Mola wake na anasema, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu Aliyeniruzuku, pamoja na uzee wangu, wanangu wawili, Ismā'īl na Isḥāq, baada ya maombi yangu Anitunuku miongoni mwa wema, kwani Mola wangu ni mwenye kusikia maombi ya mwenye kumuomba; na mimemuomba na Hakuyapitisha patupu matarajio yangu.
«Ewe Mola wangi! Nijaalie ni mwenye kuendelea kutekeleza Swala kwa njia ya ukamilifu zaidi na ujaalie katika kizazi changu wenye kuendelea nayo. Ewe Mola wetu! Na uyakubali maombi yangu na uikubali ibada yangu.
«Ewe Mola wetu! Nisamehe iwapo yametukia kutoka kwangu mambo ambayo binadamu hawasalimiki nayo, na uwasamehe wazazi wangu wawili (Hapa ni kambla haijamfunukia kwamba baba yake ni adui wa Mwenyezi Mungu) na uwasamehe Waumini wote Siku ambayo watu watasimama kuhesabiwa na kulipwa..»
Na usidhani, ewe Mtume, kwamba Mwenezi Mungu ni mwenye kughafilika na yale wanayoyafanya madhalimu, ya kukukanusha wewe na Mitume wengine na kuwakera Waumini na maasia mengineyo. Kwa kweli, Anachelewsha kuwatesa mpaka Siku ngumu ambayo macho yao yatakodoka na hayatafumbika kwa kitisho cha yale yanayoyaona. Katika hii pana kumliwaza Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukiye.
Siku watakaosimama madhalimu kutoka makaburini mwao wakikimbilia kumwitika mlinganizi wakiinua vichwa vyao, hawaoni chote kwa kituko cha kisimamo, na hali nyoyo zao ni tupu hazina kitu ndani yake, kwa kicho kingi na kuogopa ktuko cha wanayoyaona.
Na waonye, ewe Mtume, wale watu ambao wewe umetumilizwa kwao, adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama. Na hapo wale waliojidhulumu kwa kukanusha watasema, «Ewe Mola,wetu! Tupe muhula wa muda mchache, tutakuamini na tutawasadiki Mitume wako. Na wataambiwa kwa kujereshwa, «Je, hamkuapa katika uhai wenu kwamba hamtaondoka ulimwenguni kwenda Akhera, na msiamini kufufuliwa huku?
«Na mkakaa kwenye makao ya makafiri waliopita waliojidhulumu nafsi zao, kama vile watu wa Hūd na Ṣāliḥ, na mkajua, kwa mlivyoona na mlivyombiwa, maangamivu tuliyowateremshia na tukawapigia mifano katika Qur’ani msizingatie?»
Na kwa kweli, washirikina walimpangia njama Mtume, rehema na amani zimshukie, za kumuua. Na vitimbi vyao vilikuwako kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Yeye Amewazunguka. Na vitimbi vyao vikawarudia wenyewe. Na havikuwa vitimbi vyao ni vyenye kuondoa majabali wala vitu vinginevyo kwa udhaifu wake na unyonge wake. Na wao hawakumdhuru Mwenyezi Mungu, lakini walijidhuru wenyewe.
Basi usidhanie, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu Atakwenda kinyume na vile Alivyowaahidi Mitume Wake, kuwa Atawapa ushindi na Atawaangamiza wenye kuwakanusha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi, hakuna kitu kinachomshinda kukifanya, ni Mwenye kuwalipiza maadui wake kwa kuwapa mateso makali kabisa. Maneno haya ingawa anaambiwa Nabii, rehema na amani zimshukie, yanaelekezwa kwa ummah wote.
Na malipizo ya Mwenyezi Mungu ya kuwatesa maadui Wake Siku ya Kiyama yatakuwa kwenye siku ambayo itabadilishwa hii ardhi kwa ardhi nyingine nyeupe iliyotakata kama fedha, na vilevile zitatabadilishwa mbingu kwa nyingine, na watatoka viumbe makaburini mwao wakiwa hai wakiwa wamejitokeza kukutana na Mwenyezi Mungu Aliye Mmoja, Mwenye kutendesha nguvu, Aliyepwekeka kwa utukufu Wake, majina Yake, sifa Zake na matendo Yake na kulazimisha Kwake kila kitu.
Na utawaona,ewe Nabii, waasi Siku ya Kiyama wamefungwa pingu, mikono yao miguu yao yamekutanishwa pamoja kwa minyonyoro, na hali wakiwa watwevu.
Nguo zao ni za rojo la mafuta linalochomeka sana, na hapo moto utaziramba nyuso zao na kuzichoma.
Mwenyezi Mungu Atawafanyia hayo yakiwa ni malipo yao kwa madhambi waliyoyachuma duniani. Na Mwenyezi Mungu Atamlipa kila binadamu kwa alilolitenda, baya au zuri. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpesi wa kuhesabu.
Hii Qur’ani tuliyokuteremshia, ewe Mtume, ni maelezo na ni tangazo kwa watu, kwa kuwashauri na kuwatisha, na ili wawe na yakini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mola Mmoja, wapate kumuabudu, Peke Yake, Asiye na Mshirika, na wapate kuwaidhika kwayo wenye akili timamu.
Icon