ترجمة معاني سورة الحجرات
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake msiamue jambo la Sheria za Dini yenu kinyume cha maamuzi ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mkaingia kwenye uzushi. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika maneno yenu na vitendo vyenu, isije amri ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ikaendewa kinyume. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno yenu , ni Mjuzi wa nia zenu na vitendo vyenu. Hapa pana onyo kwa Waumini wasifanye uzushi katika Dini au kuleta sheria ambazo Mwenyezi Mungu Hakuziruhusu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiinue sauti zenu juu ya sauti ya Nabii mnaposema naye, wala msipige kelele mnapomuita kama mnavyopigiana kelele nyinyi kwa nyinyi, na semeni na yeye kwa namna tafauti ya vile mnavyosema na wengine, kama alivyokuwa tafauti na wengine kwa kuteuliwa kuubeba ujumbe wa Mola Wake, ulazima wa kumuamini, kumpenda, kumtii na kumfuata kwa kuogopa yasitanguke matendo yenu mema na nyinyi hamfahamu wala hamlihisi hilo.
Hakika wale wanaoziteremsha sauti zao chini mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu , hao ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewatahini nyoyo zao na Akazitakasa kwa uchamungu wake, watapata msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Mola wao na malipo mema mengi, nayo ni Pepo.
Hakika ya wale wanaokuita, ewe Nabii, nyuma ya vyumba vyako kwa sauti ya juu, wengi wao hawana akili ya kuwapelekea kuwa na adabu nzuri pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumheshimu.
Na lau wangalisubiri mpaka ukawatokea ingalikuwa bora zaidi kwao mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wao kukuheshimu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa yale yaliyotokea kwao ya madhambi na utovu wa adabu kwa kutojua kwao, ni Mwingi wa rehema kwao kwa kutowaharakishia mateso.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, Akiwajia nyinyi mtu aliyetoka nje ya maadili ya Dini na habari yoyote, ihakikisheni habari yake kabla ya kuiamini na kuisambaza mpaka mjue usahihi wake, kwa kuchelea msiwatuhumu watu wasio na hatia kwa kosa litokalo na nyinyi mkaja kujuta kwa hilo.
Na mjue kuwa baina yenu yupo Mtume wa Mwenyezi Mungu, kuweni na adabu na yeye, kwani yeye anayajua zaidi mambo yanayowafaa kuliko nyinyi, anawatakia nyinyi kheri, na nyinyi huenda mkajitakia shari na madhara ambayo Mtume hawakubalii, na lau yeye angaliwafuata nyinyi katika mengi mnayoyachagua, hilo lingalipelekea muingie kwenye usumbufu. Lakini Mwenyezi Mungu Amewafanya nyinyi muipende Imani na Akaifanya ipambike ndani ya nyoyo zenu ndipo mkaamini, na Amewafanya nyinyi mchukie kumkanusha Mwenyezi Mungu, kutoka nje ya twaa Yake na kumuasi. Hao waliosifika kwa sifa hizi ndio waongofu wenye kufuata njia ya haki.
Kheri hii walioipata ni nyongeza njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu juu yao na ni neema. Na Mwenyezi Mungu Anamjua sana anayezishukuru neema Zake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya viumbe Vyake.
Na mapote mawili ya Waumini yakipigana, fanyeni upatanishi, enyi Waumini, baina yao kwa kuyaita yakubali kuamuliwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ya Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuridhika na uamuzi wa hivyo viwili. Iwapo pote mojawapo ya yale mawili litalifanyia uadui pote lingine na litakataa kukubali mwito huo wa upatanishi, basi lipigeni vita mpaka lirudi kwenye uamuzi wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na likirudi fanyani upatanishi baina ya hayo mawili kwa haki, na mfanyeni uadilifu katika uamuzi wenu kwa kutotoka nje ya hukumu ya wenyezi Mungu na hukumu ya Mtume Wake katika uamuzi wenu. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waadilifu katika uamuzi wao, wanaohukumu baina ya viumbe Vyake kwa haki. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya mapenzi kwa Mwenyezi Mungu kihakika, kama inavyonasibiana na utukufu Wake Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu.
Hakika Waumini ni ndugu katika Dini, basi fanyeni upatanishi baina ya ndugu zenu wawili wakipigana. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote , kwa kutarajia mrehemewe.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, wasitoke wanaume Waumini wakawacheza shere wanaume Waumini wengine, huenda akawa yule anayechezwa shere katika wao ni bora kuliko wale wenye kucheza shere, na wasitoke wanawake Waumini wakawacheza shere wanawake Waumini wengine, kwani huenda yule anayechezwa shere miongoni mwao ni bora kuliko wale wenye kucheza shere. Wala msitiane ila nyinyi kwa nyinyi, wala msiitane majina ambayo yanachukiwa na wenye kuitwa nayo, kwani ubaya wa sifa na jina ni utokaji nje wa maadili ya Dini, nao ni kucheza shere kwa njia ya dharau, kuaibisha kwa maneno au ishara na kupanana majina mabaya, baada ya kuwa mmeingia kwenye Uislamu na mmeufahamu. Na Asiyetubia na huku kuchezeana shere, kutiana ila, na kuitana majina mabaya na utokaji nje wa maadili ya Dini, basi hao ndio watu waliozidhulumu nafsi zao kwa kuyatenda mambo haya yaliyokatazwa.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo, Jiepusheni na dhana mbaya nyingi kwa Waumini, kwani dhana nyingine ni dhambi. Wala msipekue aibu za Waislamu, wala msisemane nyinyi kwa nyinyi maneno yenye kuchukiwa na wenye kusemwa na hali wao hawapo. Je, anapenda mmoja wenu kula nyama ya ndugu yake akiwa amekufa? Nyinyi mnalichukia hilo, basi lichukieni lile la kumsengenya. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha nyinyi na kuwakataza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba za waja Wake Waumini, ni Mwingi wa rehema kwao.
Enyi watu! Sisi tumewaumba nyinyi kutokana na baba mmoja, naye ni Ādam, na mama mmoja, naye ni Ḥawwā’, hivyo basi hakuna kufadhilishana baina yenu kinasaba, na tumewafanya nyinyi kwa kuzaana kuwa mataifa na makabila mbalimbali ili mjuane nyinyi kwa nyinyi, hakika mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemcha Yeye zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu Anawajua sana wachamungu na Anawatambua.
Waarabu wa majangwani, nao ni Mabedui, walisema, «Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Imani iliyokamilika.» Waambie, ewe Nabii, «Msijidai kuwa mna Imani kamilifu, lakini semeni, ‘Tumesilimu.’ na bado Imani haijaingia ndani ya nyoyo zenu. Na mkimtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Hatawapunguzia chochote katika thawabu za matendo yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa anayetubia dhambi zake, ni Mwingi wa rehema kwake.» Katika hii aya kuna makemeo kwa mtu anayedhihirisha kuamini na kufuata Sunnah, na hali matendo yake yanashuhudilia kinyume cha hayo.
Hakika ni kwamba Waumini ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Zake kivitendo, kisha wasiwe na shaka katika Imani yao, na wakatoa raali yao mazuri na roho zao kwa kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kumtii Yeye na kutafuta radhi Zake, basi hao ndio wakweli katika Imani Yao.
Waambie, ewe Mtume, hawa Mabedui, «Je mnampasha habari Mwenyezi Mungu kuhusu dini yenu na yaliyomo kwenye dhamiri zenu, na hali Mwenyezi Mungu Anavijua vilivyoko mbinguni na ardhini? Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, havifichamani Kwake vilivyomo ndani ya nyoyo zenu vya Imani au vya ukafiri na vya wema au vya ubaya.»
Hawa Mabedui wanakusimulia wewe, ewe Nabii, kusilimu kwao, kukufuata wewe na kukunusuru. Waambie, «Msinisimulie mimi kuingia kwenu kwenye Uislamu, kwani manufaa yake yanawarudia nyinyi wenyewe. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewafadhili nyinyi kwa kuwaafikia kumuamini Yeye na Mtume Wake, iwapo nyinyi ni wakweli katika kuamini kwenu.»
Hakika Mwenyezi Mungu Anayajua yasioonekana ya mbinguni na ardhini, hakuna chochote kinachofichamana kwake katika hayo. Na Mwenyezi Mungu Anayaona matendo yenu na Atawalipa kwayo, yakiwa mema Atawalipa wema, na yakiwa maovu Atawalipa uovu.