Hili ni elezo la kujiepusha litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na ni tangazo la kuachana kabisa na makubaliano yaliyokuwako kati ya Waislamu na Washirikina.
Tembeeni, enyi washirikina, katika ardhi muda wa miezi minne, mutembee mnapotaka mkiwa kwenye amani bila kusumbuliwa na Waumini, na mjue kwamba nyinyi hamtayaponyoka mateso. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwatweza Makafiri na ni Mwenye kuwatia aibu hapa ulimwenguni na Moto kesho Akhera. Aya hii inawahusu wale waliokuwa na mapatano huru yasiyokuwa na muda au yule ambaye alikuwa kwenye makubaliano chini ya miezi mine, akamilishiwe miezi yake minne, au aliyekuwa na mapatano akayavunja.
Na ni ujulisho kutoka kwa Mwenyezi Mungu na ni onyo kwa watu siku ya kuchinja kwamba Mwenyezi Mungu Amejitenga na washirikina; na Mtume Wake pia Amejitenga na wao. Basi ikiwa mtarudi kwenye haki, enyi washirikina, na mkauacha ushirikina wenu, hilo ni bora kwenu. Na mkiipa mgongo haki kwa kutoukubali na mkakataa kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu, basi jueni kwamba nyinyi hamtaiponyoka adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na waonye, ewe Mtume, hawa wenye kuupa mgongo Uislamu, adhabu ya Mwenyezi Mungu iumizayo.
Na wanavuliwa, kwenye hukumu iliyopita, washirikina walioingia pamoja na nyinyi kwenye makubaliano yenye muda ujulikanao, na wakawa hawakufanya hiana kwenye mapatano, wala hawakumsaidia yoyote katika maadui, basi watimizie ahadi yao mpaka mwisho wake uliowekwa Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wachamungu ambao wanatekeleza waliyoamrishwa. Na ogopeni ushirikina na uhaini na maasia mengineyo.
Basi pindi itakapomalizika miezi minne, ambayo ndani yake mliwapa amani washirikina, basi tangazeni vita juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu popote walipo, na muwalenge kwa kuwazingira kwenye vituo vyao na muwavizie kwenye njia zao. Na iwapo watarudi nyuma kuacha ukafiri wao, wakaingia kwenye Uislamu na wakajilazimisha na sheria zake za kusimamisha Swala na kutoa Zaka, basi waacheni, kwani wameshakuwa ndugu zenu katika Uislamu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waliotubia na wakarudi nyuma, ni Mwenye huruma kwao.
Na pindi yoyote, miongoni mwa washirikina ambao damu zao na mali zao zimehalalishwa, akiomba kuingia kwenye himaya yako, ewe Mtume, na akataka amani, basi mkubalie maombi yake ili apate kuisikia Qur’ani tukufu na auone uongofu wake, kisha mrudishe alikotoka akiwa kwenye usalama. Hilo ni kwa sababu ya kumsimamishia hoja, kwa kuwa Makafiri hawaujui uhakika wa Uislamu, kwani huenda wakauchagua pindi ujinga wao ukiwaondokea.
Haitakikani kwa washirikina wawe na makubaliano, mbele ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, isipokuwa wale mliofanya makubaliano nao kwenye msikiti wa Ḥarām katika mapatano ya Hudaibiyah. Basi wakiendelea kutekeleza makubaliano yenu, na nyinyi endeleeni na wao kama hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu, wenye kutekeleza ahadi zao.
Tabia ya Makafiri ni kujilazimisha na makubaliano iwapo ushindi uko kwa wengine wasiokuwa wao. Lakini wakijihisi kuwa wana nguvu juu ya Waumini, basi wao hawachungi ujamaa wala makubaliano. Basi msidanganyike na vile wanavyowafanyia wawapo na kicho na nyinyi. Kwani wao wanawaambia maneno kwa ndimi zao ili mridhike na wao, lakini nyoyo zao zinakataa hilo. Na wengi wao ni wenye kuupiga vita Uislamu, ni wenye kuvunja ahadi.
Wameziacha aya za Mwenyezi Mungu na wakachukua badala yake vitu vya kilimwengu vilivyo duni, wakaipa mgongo haki na wakawazuia wale wanaotaka kuingia kwenye Uislamu wasiingie. Ni jambo ovu walilolifanya na ni kitendo cha kuchukiza walichokitenda.
Washirikina hawa wako kwenye vita dhidi ya Imani na watu wake, hawauekei uzito wowote ujamaa wa Muumini wala mapatano yake; walilonalo wao ni uadui na udhalimu.
Na iwapo watakomeka na ibada ya asiyekuwa Mwenyezi mungu, wakalitamka neno la kumpwekesha, wakajilazimisha na sheria za Kiislamu za kusimamisha Swala na kutoa Zaka, basi hao ni ndugu zenu katika Uislamu. Na tunazieleza waziwazi aya na kuzifafanua kwa watu wenye kufaidika nazo.
Na iwapo washirikina hawa watayavunja makubaliano ambayo mliyowekeana ahadi nao na wakaitukana dini ya Uislamu waziwazi, basi wapigeni vita, kwani wao ni viongozi wa upotevu, hawana ahadi wala dhamana, mpaka wakomeke na ukafiri wao na uadui wao juu ya Uislamu.
Msiwe kwenye hali ya kutoamua kuhusu kupigana na hawa watu ambao walivunja ahadi zao na wakafanya hima kumtoa Mtume kutoka Maka, na wao ndio walioanza kuwaudhi hapo mwanzo. Je mnawaogopa? Au mnaogopa kupambana nao vitani? Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye haki zaidi ya nyinyi kumuogopa, iwapo kweli nyinyi ni Waumini.
Enyi mkusanyiko wa Waumini,piganeni vita na maadui wa Mwenyezi Mungu, kwani Aliyetukuka na kushinda Atawaadhibu wao kwa mikono yenu na Atawafanya wanyonge kwa kushindwa na kutwezwa, Atawanusuru juu yao, Ataliinua neno Lake, Atavipoza, kwa kushindwa kwao, vifua vyenu ambavyo kwa muda mrefu viliingiwa na sikitiko na kero kutokana na vitimbi vya washirikina hawa.
Na Ataziondoa hasira kwenye nyoyo za Waumini. Na yoyote mwenye kutubia, miongoni mwa wajeuri hawa, basi Mwenyezi mungu Humkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa ujuzi wa ukweli wa toba ya mwenye kutubia, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo, utengenezaji Wake na sheria Zake Alizowaekea waja Wake.
Ni katika mipango ya Mwenyezi Mungu kuwajaribu waja Wake. Basi msidhani, enyi mkusanyiko wa Waumini, kwamba MwenyeziMungu Atawaacha bila ya mtihani ili Apate kuwajua, ujuzi uliyofunuka wazi kwa viumbe, waja Wake ambao wamemtakasia Mola wao katika jihadi yao na hawakuwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waumini kuwa ni washauri na marafiki. Na Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa vitendo vyenu vyote na Atawalipa kwa vitendo hivyo.
Si katika mambo ya washirikina kuziamirisha Nyumba za Mwenyezi Mungu huku wao wanautangaza ukafiri wao wa kumkanusha Mwenyezi Mungu na wanamfanya kuwa Ana washirika. Washirikina hawa, Siku ya Kiyama, vitendo vyao vyote vitaharibika na mwisho wao ni kukaa milele Motoni.
Hawawi na hamu ya kujishughulisha na Nyumba za Mwenyezi Mungu na kuziamirisha. isipokuwa wale ambao wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wanasimamisha Swala, wanatoa Zaka na hawaogopi, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, lawama ya yoyote mwenye kulaumu. Hawa waamirishaji ndio waongofu wa njia ya haki.
Mnayafanya, enyi watu, yale mnayoyasimamia ya kuwanwyesha mahujaji na kuuamirisha msikiti wa Ḥarām ni kama Imani ya aliyemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Haziwi sawa hali za Waumini na hali za makafiri mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu halikubali tendo lolote bila ya Imani. Na Mwenyezi Mungu hawaelekezi watu wanaozidhulumu nafsi zao kwa ukafiri kwenye mambo mema.
Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakaiacha Nyumba ya ukafiri wakielekea kwenye Nyumba ya Uislamu na wakatoa mali zao na nafsi zao katika jihadi ili kulikuza neno la Mwenyezi Mungu. Hawa wana daraja kubwa mno kwa Mwenyezi Mungu, na wao ndio wenye kufaulu kuzipata radhi Zake.
Hakika Waumini hawa waliohama wana habari njema kutoka kwa Mola wao za rehema kunjufu na radhi ambayo hapatakuwa na hasira baada yake; na mwisho wao ni kwenda kwenye mabustani ya Pepo ya milele na neema zisizokoma.
Hali ya kukaa kwenye mabustani hayo ya Pepo neema hizo kikao kisicho na kikomo. Na hayo ni malipo ya yale waliyoyatanguliza ya utiifu na vitendo vyema katika maisha yao ya ulimwenguni. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ana malipo makubwa kwa aliyeamini na akafanya mema kwa kuzifuata amri Zake na kuyaepuka Makatazo Yake.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiwafanye jamaa zenu, miongoni mwa kina baba, watoto na wengineo, kuwa ni marafiki (mnaowategemea) mkawa mnawasambazia siri za Waislamu na mnawataka ushauri katika mambo yenu, iwapo bado wako kwenye ukafiri na kuufanyia uadui Uislamu. Na yoyote atakayewafanya wao kuwa ni marafiki na akawapa mapenzi, atakuwa amemuasi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na ameidhulumu nafasi yake dhuluma kubwa.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Waumini, «Iwapo mtawafanya kina baba, watoto, ndugu , wake na jamaa wa karibu, mali mlizozikusanya, biashara ambazo mnaogopa zisikose soko na majumba yanayopendeza ambayo mumekaa ndani yake, (iwapo mtayafanya hayo) ni bora kuliko kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na jihadi katika njia Yake, basi yangojeni mateso ya Mwenyezi Mungu na adhabu Yake kwenu. Na Mwenyezi Mungu hawapi taufiki wenye kutoka nje ya utiifu Wake.
Hakika Mwenyezi Mungu Amewasaidia kwa kuwapa ushindi katika matukio ya vita mengi mlipozishikilia sababu za ushindi na mkamtegemea Mwenyezi Mungu. Na siku ya vita vya Hunayn mlisema, «Hatutashindwa leo kwa uchache.» Hapo wingi wenu ukawadanganya usiwafae, na adui yenu akawalemea msipate pa kukimbilia kwenye ardhi iliyo pana, mkakimbia katika hali ya kushindwa.
Kisha Mwenyezi Mungu Alimteremshia utulivu Mtume Wake na Waumini wakasimama imara, na Mwenyezi Mungu Akawaongezea askari wasiowaona miongoni mwa Malaika. Hapo Aliwapa ushindi juu ya adui yao na akawaadhibu wale waliokufuru. Hayo ni mateso ya Mwenyezi Mungu kwa wenye kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu isifuatwe, wenye kuwakanusha Mitume Wake.
Na atakayerudi nyuma akaacha ukafiri wake baada ya hilo, na akaingia kwenye Uislamu, basi Mwenyezi Mungu Anaikubali toba ya Anayemtaka katika wao na Anamsamehe dhambi zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, ni mwingi wa kurehemu.
Enyi mkusanyiko wa Waumini, hakika washirikina ni najisi na ni wachafu, hivyo basi msiwape nafasi kusongea kwenye eneo la Ḥarām baada ya mwaka huu wa tisa wa hijria (kalenda ya Kiislamu). Na iwapo mtachelea umasikini, kwa kukatikiwa na biashara zao, Mwenyezi Mungu Atawapa badala yake na Atawatosheleza kwa fadhila Zake Atakapo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa hali zenu, ni Mwingi wa hekima katika kuyapeleka mambo yenu.
Enyi Waislamu, wapigeni vita Makafiri ambao hawamuamini Mwenyezi Mungu, wala hawaamini Kufufuliwa na Kulipwa, wala hawajiepushi na yale ambayo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameyakataza, wala hawajilazimishi na hukumu za sheria ya Uislamu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, mpaka watoe jizia, ambayo nyinyi mnawalazimisha nayo, kwa mikono yao wakiwa wanyenyekevu na wanyonge.
Hakika wamemshirikisha Mwenyezi Mungu Mayahudi walipodai kwamba 'Uzayr ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Na wamemshirikisha Mwenyezi Mungu Wanaswara walipodai kwamba Al-Masīh( ni mwana wa Mwenyezi Mungu, Neno hili wamelizua wao wenyewe, na wao kwa hili wanafananisha na neno la washirikina kabla yao. Mwenyezi Mungu Awalaani washirikina wote. Vipi wao wajiepusha na ukweli na kuelekea kwenye urongo?
Mayahudi na Wanaswara wamewafanya wanavyuoni na watu wema kuwa ni waola wenye kuwaekea hukumu za sheria, wakawa wanajilazimisha kuzifuata na wanaacha sheria za Mwenyezi Mungu. Na pia walimfanya Al- Masīḥ, 'Īsā mwana wa Maryam, kuwa ni mungu, wakamuabudu. Na hakika Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wao wamuabudu Yeye Peke Yake, bila ya mwingine. Yeye Ndiye Mungu wa haki. Hakuna mungu anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Amejiepusha na Ametakasika na kila kile wanachokizua watu wa ushirikina na upotevu.
Makahfiri, kwa kukanusha kwao, wataka kuutangua Uislamu na kuzitangua hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake, juu ya upweke Wake, Alizokuja nazo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Na Mwenyezi Mungu Anakataa isipokuwa kuikamilisha dini Yake na kuipa nguvu, na kuliinua neno Lake, hata kama wenye kukanusha watalichukia hilo.
Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa Qur’ani na dini ya Uislamu, ili Aifanye kuwa juu ya dini zote, ingawa washirikina wanaichukia dini ya haki-Uislamu- na kushinda kwake dini nyingine.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, hakika wengi wa wanavyuoni wa watu waliopewa Vitabu na watu wema wao wanakula mali za watu kwa njia isiyokuwa ya haki, kama hongo na vinginevyo, na wanakataza watu wasiingie kwenye Uislamu na wanazuia njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe. Na wale wanaozuia mali wakawa hawatekelezi Zaka zake wala hawatoi katika mali hizo haki za lazima, basi wape bishara ya adhabu iumizayo.
Siku ya Kiyama yatawekwa mapande ya dhahabu na fedha kwenye Moto, na yataposhika moto sana, watachomwa nayo, hao wenyewe, nyuso zao, mbavu zao na migongo yao. Na wataambiwa kwa kuwaumbua, «Haya ndiyo mali yenu mliyoyakumbatia na mkazuia, katika mali hayo, haki za Mwenyezi Mungu. Basi onjeni adhabu iumizayo, kwa sababu ya kukusanya kwenu na kuzuia.
Hakika idadi ya miezi, katika hukumu ya Mwenyezi Mungu na kulingana na ilivyoandikwa kwenye al-Lawḥ al-Maḥfūẓ (Ubao Uiohifadhiwa), ni miezi kumi na mbili, tangu siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo, kuna minne mitakatifu ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha ndani yake kupigana. Nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu. Hiyo ndyo Dini iliyolingana sawa. Basi ndani ya miezi hiyo msizidhulumu nafsi zenu, kwa kuwa uharamu wake umeongezwa. Na kwa kuwa kudhulumu katika miezi hiyo ni kubaya zaidi kuliko katika miezi mingineyo, haina maana kwamba kudhulumu katika miezi mingine kunaruhusiwa. Na wapigeni vita washirikina wote kama wanavyowapiga vita nyote. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye taqwā (uchajimungu) kwa msaada Wake na nusura Yake.
Hakika yale Waarabu walikuwa wakiyafanya katika kipindi cha ujinga kwa kuiharamisha miezi minne kila mwaka, kwa idadi na sio kwa kuyataja majina ya miezi iliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, wakawa waichelewesha baadhi yake au waitanguliza, na wakaiweka badala yake miezi ya uhalali kama wanavyotaka, kulingana na mahitaji yao ya kupigana. Hakika hayo ni katika kuzidisha ukafiri. Shetani anawapoteza kwa hayo wale waliokufuru :wanauhalalisha ule waliouchelewesha kuuharamisha kati ya miezi minne mwaka huu, na wanauhalalisha mwaka mwingine, ili walinganishe kiwango cha miezi minne, wapate kuihalalisha Aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu kati ya hiyo. Shetani amewapambia vitendo viovu. Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii watu Makafiri kufuata haki na usawa.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Mkafuata sheria Zake kivitendo, mna nini nyinyi pindi mkiambiwa, «Tokeni mwnde jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ili mkapigane na maadui wenu,» mnafanya uvivu na mnajikalia majumbani mwenu? Je mnapendelea mafungu yenu ya starehe za kilimwengu kuliko neema za kesho Akhera? Basi kile mnachostarehe nacho ulimwenguni ni kichache chenye kuondoka. Ama neema za Akhera ambazo Mwenyezi Mungu Ameziandalia Waumini ni nyingi zenye kudumu.
Iwapo hamtatoka, enyi Waumini, kwenda kupigana na adui yenu , Mwenyezi Mungu Atawateremshia mateso Yake na atawaleta watu wengine ambao watatoka kwenda vitani waambiwapo watoke, watamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na nyinyi hamtamdhuru Mwenyezi Mungu chochote kwa kuikimbia kwenu jihadi, kwani Yeye ni mwenye kujitosheleza na nyinyi, na nyinyi ndio wahitaji Wake. Na Analolitaka Mwenyezi Mungu litakuwa hapana budi. Na Mwenyezi Mungu, juu ya kila kitu, ni Muweza, miongoni mwa kutetea dini Yake na Mtume Wake pasi na nyinyi.
Enyi mkusanyiko wa Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, msipotoka pamoja na yeye anapowataka mtoke, na msipomtetea, basi Mwenyezi Mungu Alimsaidia na kumtetea siku ile Makafiri wa Kikureshi walipomtoa kwenye mji wake wa Maka, na yeye ni wapili kati ya wawili( yeye na Abu Bakr al-Siddiq, radhi ya Mwenyezi Mungu imshukiye) wakawafanya ibidi waingie pangoni katika jabali la Thawr, wakakaa humo siku tatu, pindi alipomwambia rafiki Yake Abu Bakr, alipomuona ameingiwa na kicho juu yake, «Usihuzunike, Mungu Yupo pamoja na sisi» kwa kutunusuru na kutupa nguvu. Hapo Mwenyezi Mungu Aliteremsha utulivu kwenye moyo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, na akamsaidia kwa askari ambao hakuna aliowaona kati ya wanadamu, nao ni Malaika. Hapo Mwenyezi Mungu Alimuokoa na adui yake, Akawafanya wanyonge maadui wake, Akalifanya neno la waliokanusha ndilo la chini na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na hilo ni kwa kuliinua juu jambo la Uislamu. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika kuyaendesha mambo ya waja Wake. Katika aya hii pana kitambulisho cha cheo cha Abu Bakr, radhi ya Mwenyezi Mungu zimshukie.
Tokeni, enyi Waumini, kwenda kwenye jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, vijana kwa wazee, katika uzito na wepesi, vyovyote mtakavyokuwa, mtoe mali zenu katika njia ya Mwenyezi Mungu na mupigane kwa mikono yenu ili kulitangaza neno la Mwenyezi Mungu. Kutoka huko na kupigana huko ni bora kwenu katika hali zenu za sasa na za baadaye kuliko kuwa wazito, kuacha kutoa na kujikalisha nyuma. Basi iwpo nyinyi ni miongoni mwa walio na ujuzi wa ubora wa jihadi na thawabu zake mbele ya Mwenyezi Mungu, fanyeni mliyoamrishwa na muitikie mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Mwenyezi Mungu, uliotukuka utukufu Wake, Ameliumbua kundi la wanafiki waliomtaka ruhusa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, ya kusalia nyuma na kutoenda kwenye vita vya Tabūk, kwa kueleza kwamba lau kutoka kwao kulikuwa ni kwa kuandama ngawira ya karibu iliyo nyepesi kuipata, wangalikuandama. Lakini walipoitwa kwenda kupigana na Warumi pambizoni mwa miji ya Shām katika kipindi cha joto, walitiana uvivu na wakajiweka nyuma. Na watatoa nyudhuru za kusalia kwao nyuma na kuacha kutotoka wakiapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao hawaliwezi hilo; wanaziangamiza nafsi zao kwa urongo na unafiki, na hali kwamba Mwenyezi Mungu yuwajua kuwa wao ni warongo katika zile nyudhuru zao wanazozitoa.
Mwenyezi Mungu Amekusamehe, ewe Nabii, kwa yale yaliyotokea kwako, ya kuliacha lililo bora zaidi na la ukamilifu zaidi, nayo ni yale ya kuwaruhusu wanafiki kukaa wasiende kwenye jihadi. Ni kwa nini uwaruhusu hawa wakae wasiende vitani, usingojee mpaka wakufunukie waziwazi wale waliosema kweli katika kutaja nyudhuru zao na uwajue warongo miongoni mwao katika hilo?
Si katika misimamo ya wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Siku ya Mwisho kukutaka ruhusa, ewe Nubii, ya kusalia nyuma kwa kutoshiriki kwenye jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi na mali. Hiyo ni misimamo ya wanafiki tu. Na Mwenyezi Mungu Anamjua Anayemuogopa Yeye na kumcha kwa kuzitekeleza faradhi Zake na kujitenga na Makatazo Yake.
Kwa hakika wanaoomba ruhusa ya kusalia nyuma kutoenda kwenye jihadi ni wale ambao hawamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho wala hawafanyi mema, na nyoyo zao zimekuwa na shaka kuhusu usahihi wa uliyokuja nayo, ewe Nabii, ya Uislamu na sheria zake. Wao wako kwenye shaka yao wanashangaa.
Na lau wanafiki walitaka kutoka pamoja na wewe, ewe Nabii, kwenye jihadi, basi wangalijiandaa kwa matayarisho ya vyakula na vipando. Lakini Mwenyezi Mungu Amechukia kutoka kwao, ndipo ikawa ni uzito kwao kutoka, kwa mapitisho na Makadirio Yake, ingawa kisheria Amewaamrisha, na wakaambiwa, «Bakieni nyuma pamoja na waliokaa miongoni mwa wagonjwa, madhaifu, wanawake na watoto.»
Lau wanafiki wangalitoka pamoja na nyinyi, enyi Waumini, kwenye jihadi, wangalieneza mgongano katika safu zenu, ubaya na uharibifu, na wanagalikimbilia kueneza fitina na chuki baina yenu, kwa lengo la kutaka kuwafitini kwa kuwazorotesha msipigane jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na katika nyinyi, enyi Waumini, kuna wapelelezi wa makafiri, wanazisikia habari zenu na wanazipeleka kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa wanafiki walio madhalimu na Atawalipa kwa hilo.
Walipendelea wanafiki kuwafitini Waumini na Dini yao na kuwazuia wasiiifuate njia ya Mwenyezi Mungu kabla ya vita vya Tabūk, na mambo yao yakafunuka wakajulikana. Na walikuchafulia mambo, ewe Nabii, katika kuyavunja uliyokuja nayo, kama walivyofanya siku ya vita vya Uḥud na siku ya vita vya Khandaq. Na walikufanyia vitimbi mpaka usaidizi ukaja kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Akawatia nguvu askari Wake na Akaipa ushindi dini Yake, pamoja na kuwa wao wanaichukia.
Miongoni mwa wanafiki hawa, kuna wale wanaoomba ruhusa ya kuketi wasiende kwenye jihadi na wanasema, «Usiniingize kwenye mtihani utakaonifikia, katika hali ya kutoka, wa fitina ya kuvutiwa na wanawake.» Hakika wanafiki hawa wameanguka kwenye fitina kubwa ya unafiki. Na kwa hakika, Moto wa jahanamu ni wenye kuwazunguka wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho; hakuna atakayeponyoka.
Ewe Nbii! Unapofikiwa na furaha na ngawira, wanafiki wanasikitika, na unapopatwa na kero la kushindwa au matatizo, wanasema,»Sisi ni wenye busara na uhodari wa kupanga, tulijipangia kwa maslahi yetu kubakia nyuma na kutomfuata Muhammad.» Na hapo wanaondoka hali ya kuwa na furaha kwa waliyoyafanya na kwa mabaya yaliyokufika.
Sema, ewe Nabii, uwaambie hao wanaovunja moyo kwa kujitoa, kwa kuwakemea na kuwaumbua, «Hakuna litakalotupata isipokuwa lile Alilolipitisha Mwenyezi Mungu juu yetu na Aliloliandika katika al-Lawḥ al-Maḥfūẓ (Ubao Uliohifadhiwa). Yeye Ndiye Mwenye kutupa ushindi juu ya maadui wetu.» Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na wajitegemeze wale wanaoumuamini.
Waambie, ewe Nabii, «Kwani kuna mnachokitazamia kwetu isipokuwa tufe mashahidi au tuwashinde? Na sisi tunatazamia kwenu kwamba Mwenyezi Mungu Atawapatia mateso ya haraka yanayotoka Kwake yawaangamize, au yanayotokana na mikono yetu tuwaue. Basi ngojeeni, na sisi tunalingojea, pamoja na nyinyi, lile ambalo Mwenyezi Mungu ni Mwenye kulifanya kwa kila kundi kati yetu na nyinyi.»
Sema, ewe Nabii, kuwaambia wanafiki, «Toeni mali zenu vile mtakavyo na namna mtakavyo, kwa hiari yenu au kwa kulazimishwa, Mwenyezi Mungu hatavikubali kutoka kwenu mnavyovitoa, kwa kuwa nyinyi ni watu mliotoka kwenye dini ya Mwenyezi Mungu na utiifu Kwake.
Na sababu ya kutokubaliwa wanavyovitoa ni kwamba wao wameficha ukanushaji wao Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na ukataaji wao ukweli wa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kwamba wao hawaendi kuswali isipokuwa huku wanaona uzito, na kwamba hawatoi mali yao isipokuwa huku wao ni wenye kuchukia hilo. Wao hawana matarajio ya kupata malipo ya faradhi hizi wala hawaogopi mateso kwa kuziacha kwa ukafiri wao walionao.
Zisikushangaze, ewe Nabii, mali za wanafiki hawa wala watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu Anataka kuwaadhibu kwa hizo hapa ulimwenguni, kwa tabu ya kuzipata na kwa mikasa inayozifikia kwa kuwa yatokeyapo hayo hawatarajii malipo mema kwa Mwenyezi Mungu, na zitoke nafsi zao wapate kufa juu ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Na wanawaapia wanafiki hawa, enyi Waumini, kwa urongo na ubatili, kwamba wao ni katika nyinyi, wala wao kamwe si katika nyinyi. Lakini wao ni watu waoga, wanaapa kwa kujikinga na nyinyi.
Lau wanafiki hawa wapata mahala pa usalama na ngome ya kuwahifadhi, au pango kwenye jabali litakalowapa makao au handaki ndani ya ardhi itakaowaokoa na nyinyi, basi wangalikwenda huko mbiombio.
Na miongoni mwa wanafiki, kuna wale wanaokutia kombo katika kugawanya sadaka: wapatapo fungu wanaridhika na wananyamaza, na wasipobahatika kupata fungu wanakukasirikia na kukuumbua.
Na lau hawa wanaokutia kombo katika ugawaji wa sadaka waliridhika na kile ambacho Mwenyezi Mungu na Mtume Wake waliwagawia na wakasema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Anayetutosha. Mwenyezi Mungu Atatupa kutokana na nyongeza Zake, na Mtume Wake atatupa kutokana na kile Mwenyezi Mungu Alichompa. Sisi tuna hamu Mwenyezi Mungu Atukunjulie na Atukwasishe tusihitajie sadaka wala tusichukue sadaka za watu.» Lau walifanya hivyo, ingalikuwa bora na yenye manufaa zaidi kwao.
Zaka za lazima zinapewa wahitaji wasiomiliki kitu, masikini wasiomiliki kiwango kinachowatosha kwa mahitaji yao, wenye kuzishughulikia kwa kuzikusanya,wale ambao mwazizoeza nyoyo zao, miongoni mwa wale mnaotarajia wasilimu au ipate nguvu Imani yao au wawe na manufaa kwa Waislamu au mzuie kwazo madhara ya mtu yoyote yasiwafikie Waislamu. Pia zinatolewa katika kuacha huru watumwa na wale wenye mikataba ya uhuru. Na zinatolewa kupewa wenye kuingia kwenye madeni kwa sababu ya kuleta maelewano baina ya watu na wenye kulemewa na madeni waliyokopa kwa lengo lisiliokuwa la uharibifu au utumiaji wa kupita kiasi kisha wakashindwa kulipa. Na zinapewa wapiganaji katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na zinapewa msafiri aliyeishiwa na matumizi. Ugawaji huu ni lazima Aliyoifaradhia Mwenyezi Mungu na Akaikadiria. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa mambo yanayowafaa waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na sheria Zake.
Miongoni mwa wanafiki kuna watu wanaomkera Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa maneno na wanasema, «Yeye anasikiliza kila aambiwalo na analiamini.» Waambie, «Muhammad ni sikio linalosikiliza kila jema. Anamuamini Mwenyezi Mungu na anawasadiki Waumini kwa yale wanayomwambia. Na yeye ni rehema kwa aliyemfuata na akaongoka kwa uongofu Wake. Na wenye kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa namna yoyote ya kumkera, watakuwa na adhabu yenye kuumiza.
Wanafiki wanaapa viapo vya urongo na wanatoa nyudhuru za kupanga ili kuwafanya Waumini waridhike na wao. Na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanastahiki zaidi na inafaa zaidi wawaridhie kwa kuwaamini na kuwatii, iwapo kweli wao ni Waumini.
Kwani hawakujua wanafiki hawa kwamba mwisho wa wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume Wake ni Moto wa Jahanamu, watakuwa na adhabu kali ndani yake? Mwisho huo ndio utwevu na unyonge mkubwa. Na miongoni mwa kupiga vita kwao huko ni kumkera Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumtukana na kumtia kombo; Mwenyezi Mungu Atulinde na hilo.
Wanafiki wanaogopa kuteremshwa sura kuhusu wao, yenye kuwapa habari ya ukafiri waliyouficha ndani ya nyoyo zao. Waambie, ewe Nabii, Endeleeni juu ya yale ambayo muko nayo ya kufanya shere na masihara. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuutoa nje ukweli wa yale mliokuwa na hadhari nayo.
Na lau unawauliza, ewe Nabii, kuhusu yale matukano waliyokutukana wewe na Maswahaba zako watasema, «Sisi tulikuwa tukizungumza maneno bila kuyakusudia. Waambie, ewe Nabii, «Je ni Mwenyezi Mungu mlikuwa mkimcheza shere na aya Zake na Mtume Wake?»
Msitoe sababu, enyi mkusanyiko wa wanafiki! Kwani hakuna faida ya kutoa udhuru kwenu. Hakika mumekufuru kwa maneno haya mliyoyafanyia shere. Iwapo tutalisamehe kundi miongoni mwenu lililotaka msamaha na likatubia kidhati, tutaliadhibu kundi la watu wengine kwa sababu ya uhalifu wao wa kusema maneno haya maovu ya makosa.
Wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike ni aina moja katika kutangaza kwao Imani na kuficha kwao ukafiri. Wanaamrisha kukufuriwa Mwenyezi Mungu na kuasiwa Mtume Wake, na wanakataza Imani na utiifu, na wanaizuia mikono yao kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na kwa hivyo hawamtaji, na Yeye Amewasahau na rehema Yake hakuwaelekeza kwenye wema. Hakika wanafiki ndio waliotoka nje wakaacha kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Mwenyezi Mungu Amewaahidi wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na Makafiri kwamba mwisho wao ni kwenda kwenye Moto wa Jahanamu, wakae humo milele kabisa. Moto huo ni wenye kuwatosha, ukiwa ni mateso yao kwa kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Amewafukuza kwenye rehema Yake. Na watakua na adhabu ya daima.
Hakika vitendo vyenu, enyi wanafiki, vya kucheza shere na ukafiri ni kama vitendo vya watu waliotangulia, waliokuwa na nguvu nyingi na mali na watoto zaidi kushinda nyinyi, wakajimakini na maisha ya kilimwengu, wakasterehe na vitu na ladha zilizomo. Basi na nyinyi, enyi wanafiki, mumestarehe kwa sehemu yenu ya matamanio yenye kumalizika kama starehe ya waliokuwa kabla yenu kwa mafungu yao ya vitu vya kilimwengu venye kumalizika. Na mumejiingiza katika kumzulia Mwenyezi Mungu urongo kama walivyojiingiza wale watu waliokuwa kabla yenu. Hao wenye kusifiwa kwa tabia hizi, ndio wale ambao mema yao yameondoka duniani na Akhera. Na wao ndio wenye kupata hasara kwa kuuza kwao sterehe za Akhera kwa vyeo na starehe za ulimwenguni.
Kwani haikuwajia wanafiki hawa habari ya wale waliopita, miongoni mwa watu wa Nūḥ, kabila la 'Ād, kabila la Thamūd, watu wa Ibrāhīm, watu wa Madyan na watu wa Lūṭ, walipowajia Mitume na wahyi na aya za Mwenyezi Mungu wakawakanusha? Wote hawa Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu Yake, kuwalipiza wao kwa matendo yao mabaya. Mwenyezi Mungu Hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini ni wao wenyewe walijidhulumu nafsi zao kwa kukanusha na kupinga.
Na wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, waume na wake, wanasaidiana wao kwa wao, wanaamrisha watu kuamini na kufanya vitendo vyema na wanawakataza kukanusha na kufanya maasia, wanatekeleza Swala, wanatoa Zaka, wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wanakomeka kufanya yale waliyokatazwa. Hao Mwenyezi Mungu Atawarehemu, Atawaokoa na adhabu Yake na Atawatia Peponi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika sheria Zake na hukumu Zake.
Mwenyezi Mungu Amewaahidi wenye kumuaumini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, waume na wake, mabustani ya Pepo ambayo chini yake inapita mito, hali ya kukaa humo milele. Starehe zake haziwaondokei. yana majumba yaliojengwa vizuri yenye utulivu mzuri katika mabustani ya makao. Na radhi itokayo kwa Mwenyezi Mungu watakayoipata ni kubwa zaidi na ni bora zaidi kuliko starehe walizonazo. Ahadi hiyo ya malipo mema ya Akhera ndio kufaulu kukubwa.
Ewe Nabii! Pigana vita na makafiri kwa upanga, na wanafiki kwa ulimi na kusimamisha hoja, na ukazane juu hayo mapote mawili. Na mahala pao pa kutulia ni Motoni; na ubaya wa mahala pa kuishia ni hapo watakapoishia wao.
Wanafiki wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao hawakusema kitu cha kumkosea Mtume na Waislamu. Wao ni warongo. Hakika wamesema neno la ukafiri na wametoka kwa hilo kwenye Uislamu, na wamejaribu kumdhuru Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye, Mwenyezi Mungu hakuwawezesha kulifanya hilo. Na wanafiki hawakupata kitu chochote cha kumtia kombo na kumkosoa, isipokuwa ni kwamba Mwenyezi Mungu Aliwaneemesha akawapa utajiri kwa milango ya heri na baraka Aliyomfungulia Nabii Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Basi wakirudi makafiri hawa kwenye Imani na kutubia, hilo ni bora kwao, na wakigeuka nyuma au wakasalia hali ile walivyo, Mwenyezi Mungu Atawaadhibu adhabu iumizayo hapa duniani, kupitia mikono ya Waislamu, na kesho Akhera kwa Moto wa Jahanamu, na hapatakuwa na mwokoaji wa kuwaokoa wala msaidizi wa kuwakinga na janga la adhabu.
Na miongoni mwa mafukara wa wanafiki, kuna wanaojipa ahadi ya mkazo wenyewe kwamba lau Mwenyezi Mungu Atampa mali, atayatolea sadaka, atafanya vile watu wema wanafanya katika mali yao na atafuata njia ya wema.
Alipowapa Mwenyezi Mungu kutokana na hisani yake, walifanya ubakhili kutoa sadaka na kutumia mali katika wema, na waligeuka nyuma hali ya kuupa mgongo Uislamu.
Ikawa malipo ya mambo waliyoyafanya na mwisho wao ni kwamba aliwaongezea unafiki juu ya unafiki wao, hawataweza kujisafisha nao mpaka Siku ya kuhesabiwa. Hayo ni kwa sababu ya kwenda kwao kinyume na ahadi walioitoa juu ya nafsi zao na kwa sababu ya unafiki wao na urongo wao.
Kwani hawakujua wanafiki hawa kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua wanayoyaficha ndani ya nafsi zao na yale wanayoyazungumza kwenye mabaraza yao ya vitimbi na njama na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa yaliyofichika yote? Basi Atawalipa kwa matendo yao ambayo Amewahifadhia na kuwadhibitia.
Na pamoja na ubahili wawanafiki, wale wanaotoa sadaka hawavuki salama na kero lao. Pindi wale matajiri wakitoa sadaka ya mali mengi, wanawatia kombo na kuwatuhumu kuwa wanajionesha. Na pindi mafukara wakitoa sadaka kulingana na uwezo wao, wanawafanyia shere na kusema kwa njia ya kuwachezea, «Sadaka yao hii itafalia nini?» Basi Mwenyezi Mungu Anawafanyia shere wanafiki hawa. Na wao watakuwa na adhabu kali iumizayo.
Waombee msamaha hao wanafiki, ewe Mtume, au usiwaombee msamaha, Mwenyezi Mungu Hatawasamehe, namna yatakayokuwa mengi na kukaririka maombi yako kutaka wasamehewe, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Hawaafikii kwenye uongofu wale waliotoka nje ya utiifu Wake.
Walifurahi wale waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani ziwashukiye, kwa kujikalia Madina wakienda kinyume na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na walichukia kupigana jihadi pamoja na Yeye kwa mali zao na nafsi Zao katika njia ya Mwenyezi Mungu na waliambiana wao kwa wao, «Msitoke katika kipindi cha joto.» Waambie, ewe Mtume, «Moto wa Jahanamu una joto zaidi,» lau wao wanalijua hilo.
Basi na wacheke hao wanafiki waliojiweka nyuma wasimwandame Mtume wa Mwenyezi Mungu katika vita vya Tabūk, kidogo katika uhai wao wa kilimwengu wenye kumalizika, na walie sana katika Moto wa Jahanamu, ukiwa ni malipo ya yale ambayo walikuwa wakiyachuma duniani ya unafiki na ukafiri.
Basi Akikurudisha Mwenyezi Mungu, ewe Mtume, kutoka kwenye vita ulivyopigana ukaja kwenye kundi la wanafiki waliothibiti juu ya unafiki, na wakakutaka ruhusa watoke na wewe kwenye vita vingine baada ya vita vya Tabūk, waambie, «Hamtatoka pamoja na mimi kabisa kwenye vita vyovyote, na hamtapigana pamoja na mimi na adui yoyote. Nyinyi mumeridhika kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na wale waliojiweka nyuma wakaacha kupigana jihadi pamoja na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.»
Na usimswalie kabisa, ewe Mtume, yoyote aliyekufa miongoni mwa wanafiki na usisimame kwenye kaburi yake kumuombea, kwa kuwa wao wamemkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wamekufa na wao wametoka kwenye utiifu. Hii ni hukumu yenye kuenea kwa kila mtu ambaye unafiki wake umejulikana.
Na zisikushangaze mali za wanafiki hawa na watoto wao. Mwenyezi Mungu Anataka kuwaadhibu wao kwa hizo ulimwenguni, kwa kupambana kwao na shida katika kuzipata na kwa kufa kwao katika hali ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Na pindi sura yoyote ikiteremshwa kwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, inayoamrisha kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtakasa na kupigana jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, wale wenya uwezo wa kifedha miongoni mwa wanafiki wanakuomba ruhusa na wanasema, «Tuache pamoja na waliokaa wasioweza kutoka.»
Wanafiki hawa wameridhika na aibu, nayo ni kukaa majumbani pamoja na wanawake na watoto na wenye nyudhuru. Na Mwenyezi Mungu Amezipiga muhuri nyoyo zao kwa sababu ya unafiki wao na kujiweka kwao nyuma kuacha jihadi na kutoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wao hawayaelewi yale ambayo yana maslahi yao na uongofu wao.
Iwapo wanafiki hawa watajikalisha nyuma waache kupigana, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, amepigana jihadi, yeye na Waumini pamoja naye, kwa mali zao na nafsi zao. Wao wamepata ushindi na ngawira ulimwenguni, na watapata Pepo na mapokezi mema kesho Akhera. Na wao ndio wenye kufaulu.
Amewatayarishia Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, mabustani ya Pepo ambayo inapita mito chini ya miti yake, hali ya kukaa humo milele. Huko ndiko kufaulu kukubwa.
Na kilikuja kikundi, miongoni mwa watu wa vitongoji vya Waarabu wa majangwani, kandokando ya mji wa Madina wakitoa nyudhuru kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, wakimuelezea udhaifu walionao na kutoweza kwao kutoka kwenda vitani. Na kuna watu waliojikalia bila kutoa udhuru wowote kwa kumfanyia ujasiri Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema wa Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Basi wale waliokufuru miongoni mwa hawa itawatapata adhabu kali, ya kuuawa na nyinginezo hapa duniani, na ya Moto kesho Akhera.
Watu wenye nyudhuru, miongoni mwa madhaifu, wagonjwa na mafukara ambao hawamiliki mali ya kuwawezesha kufanya matayarisho ya kutoka, hawana makosa ya kujikalia, iwapo wamemtakasia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wameifuata sheria Yake kivitendo. Hapana njia yoyote kwa wale waliozuiliwa na udhuru kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kupatiwa mateso na kutiwa makosani, iwapo wao ni waaminifu kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa watenda wema (muhsinūn), ni Mwenye kuwarehemu.
Pia hapana makosa kwa wale ambao wakikujia kutaka uwasaidie kuwachukua kwenda kwenye jihadi, unawaambia, «Sina wanyama wa mimi kuwapatia muwapande», hapo wakakuacha na kugeuka kwenda zao, na macho yao yanabubujika machozi kwa masikitiko ya kukosa utukufu wa jihadi na thawabu zake kwa kuwa hawakupata cha kutumia na cha kuwabeba lau walitoka kwenda kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Hakika makosa na lawama ni kwa wale matajiri waliokujia, ewe Mutme, kukutaka ruhusa ya kujikalia, nao ni wanafiki matajiri waliojichagulia kuketi pamoja na wanawake na wenye nyudhuru. Na Mwenyezi Mungu Amezipiga mhuri nyoyo zao kwa unafiki, haziingiwi na Imani. Wao hawajui mwisho wao mbaya kwa kubakia kwao nyuma na kuacha kwao kupigana jihadi pamoja na wewe.
Watataka udhuru kwenu, enyi Wumini, hawa waliojikalisha nyuma na kuacha kupigana jihadi na washirikina, kwa kutumia maneno ya urongo, mtakaporudi kutoka kwenye jihadi ya vita vya Tabūk. Waambie, ewe Mtume, «Msitoe udhuru, hatutawaamini katika yale mnayoyasema. Mwenyezi Mungu Ashatupa habari, kuhusu mambo yenu, ambazo zimetupa uthibitisho wa urongo wenu. Mwenyezi Mungu Atayaona matendo yenu na Mtume Wake, iwapo mtatubia unafiki wenu au mtaendelea nao. Na Mwenyezi Mungu Atawaonesha watu matendo yenu waziwazi hapa duniani kisha mtarudishwa, baada ya kufa kwenu, kwa Yule Ambaye hayafichiki Kwake mambo yenu ya ndani na ya nje, ili Awape habari ya matendo yenu yote na Awape malipo yake.
Mtakaporejea kwao kutoka vitani, wanafiki watawaapia nyinyi kwa Mwenyezi Mungu, wakitoa udhuru hali ya kuwa ni warongo, ili muwaache bila kuwauliza. Basi jiepusheni nao na muwape mgongo kwa kuwadharau, kwani wao ni wachafu wa ndani. Na mahali pao pa kushukia kesho Akhera ni Moto wa Jahanamu, ukiwa ni malipo ya yale waliokuwa wa kiyatenda ya madhambi na makosa.
Wanawaapia nyinyi, enyi Waumini, wanafiki hawa kwa urongo ili mridhike nao. Basi mkiridhika nao, kwa kuwa hamjui urongo wao, hakika Mwenyezi Mungu Haridhiki na hawa wala wengineo kati ya wale walioendelea na uasi na kutoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Mabedui, wakazi wa jangwani, ni washupavu zaidi wa ukafiri na unafiki kuliko wakazi wa mjini. Hivyo ni kwa sababu ya ugumu wa tabia za, ususuavu wa nyoyo zao na kuwa mbali kwao na elimu, wanavyuoni, vikao vya mawaidha na dhikr (kumtaja Mwenyezi Mungu). Kwa hivyo wao wanastahilii zaidi wasijue mipaka ya Dini na zile sheria na hukumu ambazo Mwenyezi Mungu Ameziteremsha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali za hawa wote, ni Mwenye hekima Katika uendeshaji Wake mambo ya waja Wake.
Na miogoni mwa Mabedui kuna wanaohesabu wanachokitoa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni kodi na ni hasara, hawatazamii, kwa kile wakitoacho, thawabu wala kujikinga na adhabu, na wana hamu mupatwe na misiba na maafa. Lakini mabaya yatawazunguka wao, sio Waislamu. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa wanayoyasema, ni Mjuzi wa nia zao mbaya.
Na miongoni mwa Mabedui kuna wanaomuamini Mwenyezi Mungu na kukubali upweke Wake, kufufuliwa baada ya kufa na kuwa kuna thawabu na adhabu, na wanatarajia malipo mema kwa kile chochote wanachokitoa cha matumizi katika kupigana jihadi na washirikina, kwa kusudia radhi za Mwenyezi Mungu na mapenzi Yake, na kukifanya ni njia ya kumfanya apate maombi ya Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Jua utanabahi kwamba matendo haya yatawaweka wao karibu na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Mwenyezi Mungu Atawatia kwenye Pepo Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha wa maovu waliyoyafanya, ni Mwenye kuwarehemu.
Wale waliowatangulia watu mwanzo kwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake miongoni mwa Muhājirūn waliowagura watu wao na jamaa zao wakaondoka kwenda kwenye Nyumba ya Uislamu, na Anṣār waliomhami Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, dhidi ya maadui wake makafiri, na wale waliowafuata wao kwa wema, katika usawa wa itikadi, maneno na vitendo, kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa pungufu na kutukuka, Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu Ameridhika na wao kwa kumtii kwao Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na wao wameridhika na Yeye kwa malipo mazuri mengi Aliyowapatia kwa utiifu wao na Imani yao. Amewaandalia wao mabustani ya Pepo ambayo inapita mito chini yake, hali ya kukaa milele humo daima. Huko ndiko kufaulu kukubwa. Katika aya hii pana kuwasafisha Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwaendee, kuwafanya waadilifu na kuwasifu. Na kwa hivyo, kuwaheshimu wao ni katika misingi ya Imani.
Miongoni mwa watu ambao wako pambizoni mwa Madina kuna Mabedui wanafiki, na miongoni mwa watu wa Madina pia kuna wanafiki waliojikita kwenye unafiki na kuzidi kuendelea nao kwa kupita mipaka katika uasi, kwa namna ambayo yanafichamana kwako, ewe Mtume, mambo yao. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kwa kuuawa na kutekwa na kukashifiwa duniani, na kwa adhabu ya kaburi baada ya kufa, kisha watapelekwa, Siku ya Kiyama, kwenye adhabu kubwa ndani ya Moto wa Jahanamu.
Na wengine wa Madina na walio pambizoni mwake, walikubali makosa yao, wakajuta na wakatubia kwa hayo, walichanganya matendo mazuri, nayo ni kutubia, kujuta, kukubali makosa na mengineyo miongoni mwa matendo mema, kwa mengine mabaya, nayo ni kujikalia nyuma kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mengineyo miongoni mwa matendo mabaya. Basi hao yatarajiwa Mwenyezi Mungu Awaelekeze kutubia na aikubali toba yao kutoka kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu.
Chukua, ewe Mtume, kwenye mali za hawa waliotubia, waliochanganya matendo mema na matendo mengine maovu, sadaka itakayowasafisha wao na uchafu wa madhambi yao na itakayowainua wao na kuwaondoa kwenye daraja za wanafiki kuwapeleka kwenye daraja za wenye ikhlasi; na watakie wao msamaha wa madhambi yao na uwaombee sitara ya hayo, kwani maombi yako na utakaji msamaha wako ni rehema na utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa kila maombi na kila neno, ni Mjuzi wa hali za waja Wake na nia zao, na Atamlipa kila mwenye kutenda kwa matendo aliyoyatenda.
Kwani hawajui, hawa wenye kujikalisha nyuma na kuacha kwenda kwenye jihadi na wengineo, kwamba Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Ambaye Anakubali toba ya waja Wake, Anachukua sadaka na Anatoa malipo yake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba ya waja Wake warejeapo Kwake, ni Mwenye kuwarehemu warudipo kutaka radhi Zake.?
Na sema, ewe Nabii, kuwaambia hawa wenye kujikalisha nyuma na kuacha kwenda kwenye jihadi, «Mfanyieni Mwenyezai Mungu yale ya kumridhisha ya kumtii na kutekeleza mambo ya lazima Aliyoyaweka na kuepuka maasia. Na Mwenyezi Mungu Atayaona matendo yenu na Mtume Wake na Waumini, na yatakuwa wazi mambo yenu, na mtarejeshwa Siku ya Kiyama kwa Anayejua yaliyofichika yenu na yaliyo wazi yenu, na hapo Atawapa habari ya yale ambayo mlikuwa mkiyafanya. Katika hii kuna tishio na onyo kwa anayeendelea kwenye ubatilifu wake na ukiukaji mipaka wake.
Na miongoni mwa hawa waliojikalisha nyuma wakaacha kuwafuata, enyi Waumini, katika vita vya Tabūk kuna wengine walioahirishwa, ili Mwenyezi Mungu Aaamue juu yao uamuzi Atakaoutoa: ima Awaadhibu Mwenyezi Mungu au Awasamehe. Hawa ni wale waliojuta kwa yale ambayo walifanya. Nao ni Murarah mwana wa al-Rabī‘, Ka‘b mwana wa Mālik na Hilāl mwana wa Umayyaha. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa Anayestahili mateso au msamaha. Ni Mwingi wa hekima katika maneno Yake yote na vitendo Vyake.
Na wanafiki waliojenga msikiti, kwa kuwadhuru Waumini, kumkanusha Mwenyezi Mungu na kuwagawanya Waumini, ili waswali humo baadhi yao na wauache msikiti wa Qubā’ ambao Waislamu wanaswali ndani yake, ili Waislamu watafautiane na wagawanyike kwa hilo, na kwa ajili ya kumngojea yule aliyempiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kabla ya hapo, naye ni Abū ‘Āmir al-Rāhib aliyeasi, ili pawe ni mahali pa kuwafanyia vitimbi Waislamu. Na wataapa tena wataapa, wanafiki hawa, kwamba wao hawakukusudia kwa kuujenga isipokuwa kuwafanyia wema na kuwahurumia Waislamu na kuwapa nafasi wanyonge wasioweza kwenda msikiti wa Qubā’.Na Mwenyezi Mungu Anashuhudia kwamba wao ni warongo katika yale wanayoyaapia. Msikiti huo ulivunjwa na ukatiwa moto.
Usisimame, ewe Nabii, kuswali katika msikiti huo kabisa. Kwani msikiti uliojengwa kwa misingi ya uchamungu kuanzia siku ya mwanzo, nao ni msikiti wa Qubā’, unafaa zaidi kwa wewe kusimama humo kwa kuswali. Kwani katika msikiti huu kuna watu wanapenda kujisafisha na najisi na uchafu kwa maji, kama wanavyojisafisha kwa kujiepusha na mambo yanayopelekea kufanya mambo yaliyoharamishwa na kuomba msamaha kutokana na madhambi na maasia. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kujisafisha.Na iwapo msikiti wa Qubā’ ulijengwa juu ya misingi ya uchaji-Mungu, basi Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kama hivyo kwa njia ya ubora zaidi na ustahiki zaidi.
Hawalingani: yule aliyeweka msingi wa jengo lake juu ya kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kutaka radhi Zake na yule aliyeweka msingi wa jengo lake kandokando ya shimo linalokaribia kuanguka akajenga msikiti wa kudhuru, kukufuru na kuleta mgawanyiko baina ya Waislamu, ikampelekea yeye aanguke kwenye Moto wa Jahanamu. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu madhalimu waliokiuka mipaka Yake.
Haliachi kuendelea, lile jengo wanafiki walilolijenga liwe ni madhara kwa msikiti wa Qubā’, kuwa ni ishara ya shaka unafiki uliojikita ndani ya nyoyo zao, mpaka nyoyo zao zikatike-katike kwa wao kuuawa au kufa au kwa kujuta kwao upeo wa kujuta nakurejea kwao kwa Mola wao na kumuogopa Yeye upeo wa kuogopa.Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa shaka waliyonayo hawa wanafiki na yale waliyoyakusudia kwa jengo lao, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo ya viumbe Vyake.
Hakika Mwenyezi Mungu Amenunua kutoka kwa Waumini, nafsi zao na kuwapa wao , badala yake, Pepo na yale Aliyoyatayarisha ya starahe humo ndani, kwa kutoa kwao nafsi zao na mali zao katika kupigana jihadi na maadui wake kwa ajili ya kulitukuza neno Lake na kuidhihirisha dini Yake, wakaua na wakauawa. Hiyo ikiwa ni ahadi juu ya Mwenyezi Mungu iliyothibiti ndani ya Taurati iliyoteremshwa kwa Mūsā, amani imshukiye, na Injili iliyoteremshwa kwa ‘Īsā, amani imshukiye, na Qur’ani iliyoteremshwa kwa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukiye. Na hakuna yoyote mwenye utekelezaji zaidi wa ahadi Yake kuliko Mwenyezi Mungu, kwa yule aliyetimiza ahadi yake kwa Mwenyezi Mungu. Basi onesheni furaha, enyi Waumini, kwa biashara yenu mliyoifanya na Mwenyezi Mungu na kwa ahadi Yake, ya Pepo na Radhi, kwenu. Na mapatano hayo ya biashara ndiyo kufaulu kukubwa.
Na miongoni mwa sifa za Waumini hawa waliopewa bishara njema ya kuingia Peponi ni kwamba wao ndio wanaotubia, wenye kuondoka kwenye yale ambayo Mwenyezi Mungu Ameyakataza kwenda kwenye yale ambayo Mwenyezi Mungu Anayapenda na Anayaridhia, wale waliomtakasia ibada Mwenyezi Mungu Peke Yake na wakapindana katika kumtii, wale wenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote yale ambayo Aliwatahini nayo ya uzuri au ubaya, wenye kufunga, wenye kurukuu katika swala zao, wenye kusujudu katika hizo, wale ambao wanawaamrisha watu kila lile ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wameliamrisha na wanawakataza kila lile ambalo Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wamelikataza, wenye kutekeleza faradhi za Mwenyezi Mungu, wenye kumalizikia kwenye kufuata amri Yake na kuepuka katazo Lake, wenye kusimama imara katika kumtii na wenye kukomea pale penye mipaka Yake. Na wape bishara njema, ewe Nabii, waumini hawa waliosifika na sifa hizi ya radhi za Mwenyezi Mungu na Pepo Yake
Haifai kwa Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, hata kama ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwa imefunuka waziwazi kwamba wao ni watu wa Moto wa Jah(Im, kwa kufa kwao katika hali ya ushirikina. Na Mwenyezi Mungu Hawasamehe washirikina, kama alivyosema Aliyetukuka, «Hakika Mwenyezi Mungu Hasamehe Ashirikishwapo» na kama Alivyosema Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, «Hakika yule anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu Ashamharimishia Pepo»
Na hakukuwa kwa Ibrāhīm kule kumuombea msamaha babake mshirikina isipokuwa ni yatokana na ahadi aliyeitoa kwake, nayo ni neno lake, «Nitakuombea msamaha Mola wangu, kwani Yeye kwangu mimi Ana ukarimu mwingi.» Basi ilipomfunukia wazi Ibrāhīm kwamba babake ni adui wa Mwenyezi Mungu na kwamba kusihi na kukumbusha hakukufaa kitu kwake na kwamba yeye atakufa akiwa kafiri, alimuacha, akaacha kumuombea msamaha na akamwepuka. Kwa kweli, Ibrāhīm, amani imshukiye, ana unyenyekevu mkubwa kwa Mwenyezi Mungu, ni mwenye msamaha mwingi kwa kasoro zinazotoka kwa watu wake.
Na Mwenyezi mungu Hakuwa ni Mwenye kuwapoteza watu baada ya kuwapa neema uongofu na taufiki, mpaka awaelezee waziwazi yale ambayo yatawapelekea kumcha Yeye na yale wanayoyahitajia ya misingi ya Dini na tagaa zake. Hakika Mwenyezi Mungu, kwa kila jambo, ni Mjuzi; Amewafundisha nyinyi yale ambayo hamkuwa mkiyajua, amewaelezea waziwazi yale ambayo mtanufaika nayo na Amewasimamishia hoja kwa kuwafikishia ujumbe Wake.
Hakika Mwenyezi Mungu ni mmiliki wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Hana mshirika katika uumbaji, uendeshaji, ustahiki wa kuabudiwa na uwekaji sheria. Anampa uhai Anayemtaka na anamfisha Anayemtaka. Na hakuna yoyote, isipokuwa Mwenyezi Mungu, wa kuyasimamia mambo yenu wala wakuwapa ushindi juu ya adui wenu.
Mwenyezi Mungu Alimuelekeza Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kurudi Kwake na kumtii, na Aliwakubalia toba Muhājirūn, waliogura nyumba zao na jamaa zao wakaenda kwenye Nyumba ya Uislamu, na pia Aliwakubalia toba waliomuhami Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, waliotoka pamoja na yeye kupambana na maadui katika vita vya Tabūk katika kipindi cha joto kali na shida ya chakula na vipando. Mwenyezi Mungu Aliwakubalia toba yao baada ya hali kufikia kiwango kwamba nyoyo za baadhi yao zilikaribia kuiyepuka haki na kupendelea ulegevu na utulivu. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwathibitisha na Akawapa nguvu na Akawakubalia toba. Hakika Yeye kwao ni Mwingi wa upole ni mwenye huruma. Na miongoni mwa huruma Yake kwao ni kwamba Aliwapa neema ya kutubia, Akaikubali toba yao na Akawathibitisha juu yake.
Na pia Alikubali toba ya wale watu watatu walioachwa nyuma - nao ni Ka‘b mwana wa Mālik, Hilāl mwana wa Umayyah na Murarah mwana wa a-Rabī'-. Wao walijikalisha nyuma wakaacha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakasikitika masikitiko makubwa. Mpaka ilipofikia hadi ya ardhi kuwa dhiki na wao, pamoja na kuwa ni kunjufu, kwa majonzi na majuto kwa sababu ya kujikalisha nyuma kwao, na nafsi zao zikaingiwa na dhiki kwa hamu iliyowapata na wakahakikisha kwamba hakuna mahali pa kuhamia kumkimbia Mwenyezi Mungu isipokuwa ni Kwake, hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na sifa za upungufu na kutukuka, Aliwaafikia kwenye utiifu na kurejea kwenye yale yanayomridhisha Yeye. Hakika Yeye ni Ndiye Mwingi wa kukubali toba za waja Wake, Ndiye Mwenye kuwahurumia.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkaitumia sheria Yake! Fuateni maamrisho ya Mwenyezi Mungu na epukeni makatazo Yake katika kila kitu mnachokitenda na mnachokiacha, na kuweni pamoja na wakweli katika Imani zao na ahadi zao na katika kila jambo miongoni mwa mambo yao.
Haikuwa inafaa kwa watu wa mji wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na walio pambizoni mwao miongoni mwa wanaokaa jangwani, kujikalisha nyuma pamoja na watu wao majumbani mwao na kuacha kumfuata Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye. Na haikuwa inafaa kwao kuzipendelea nafsi zao mapumziko huku Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yuko kwenye tabu na usumbufu. Hayo ni kwamba wao hawapatikani na kiu wala usumbufu wala njaa kwenye safari yao na jihadi yao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wala hawakanyagi ardhi yoyote ambayo kuikanyaga kwao inawatia hasira makafiri, na wala hawafaulu kumuua au kumshinda adui wa Mwenyezi Mungu na adui wao isipokuwa wataandikiwa, kwa hayo yote, thawabu ya tendo jema. Hakika Mwenyezi Mungu Hapotezi malipo ya muhsinūn: waliofanya wema kwa kukimbilia kwao kufuata amri ya Mwenyezi Mungu na kusimama kwao imara kutekeleza haki Yake inayowalazimu na haki ya viumbe Vyake.
Na wala hawatoi matumizi, madogo au makubwa, katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawayapiti mabonde katika kutembea kwao pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, katika kupigana kwake jihadi, isipokuwa wataandikiwa thawabu ya tendo lao, ili Mwenyezi Mungu Awalipe mazuri zaidi ya wao kulipwa kwa matendo yao mema.
Na haikuwa inafaa kwa Waumini watoke wote kupigana na adui yao, pia hailingani na wao wakae wote. Basi si watoke kupigana jihadi, katika kila kundi, watu ambao itapatikana kwao kutosheleza kufikia malengo. Hivyo ili wapate kujifunza, wale waliokaa wasiende vitani, na kujua hukumu mpya za dini ya Mwenyezi Mungu na zile zilizoteremshiwa Mtume Wake, na wapate kuwaonya jamaa zao kwa yale waliojifunza watakaporejea kwao, huenda wao wakajihadhari na adhabu ya Mwenyezi Mungu, kwa kutekeleza maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkaifuata sheria Yake kivitendo, anzeni kupigana na walio karibukaribu na Nyumba ya Uislamu , miongoni mwa makafiri, na wakute kutoka kwenu ushupavu na ukali. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wachamungu kwa msaada Wake na nusura Yake.
Na pindi Mwenyezi Mungu Aiteremshapo sura, miongoni mwa sura za Qur’ani, kwa Mtume Wake, basi kati ya hawa wanafiki kuna wanaosema, kwa kukanusha na kufanya shere, «Ni nani wenu ambaye sura hii ilimfanya imani yake, kwa Mwenyezi Mungu na aya Zake, iongezeke? Basi wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake,, kule kuteremka sura, kuliwaongezea waolmani kwa kuijua na kuizingatia na kuiamini na kuitumia, na hali wao wanafurahia Imani na yakini Alizowapa Mwenyezi Mungu.
Ama wale ambao wana unafiki na shaka ndani ya nyoyo zao katika dini ya Mwenyezi Mungu, basi kule kuteremka sura kunawaongezea unafiki na shaka juu ya unafiki na shaka walizokuwa nazo kabla ya hapo. Na hawa wataangamia wakiwa katika hali ya kumkanusha Mwenyezi Mungu na aya Zake.
Kwani hawaoni wanafiki kwamba Mwenyezi Mungu Anawapa mitihani, kwa kuwaletea ukame na matatizo na kwa kuyatoa nje yale wanayoyaficha ya unafiki, mara moja au mara mbili kila mwaka? Kisha wao, pamoja na hayo, hawatubii kutokana na ukafiri wao na unafiki wao, wala hawazingatii wala hawakumbuki aya za Mwenyezi Mungu wazionazo.
Na iteremshwapo sura, wanafiki huwa wakishiriana kwa macho, kwa kukataa kuteremka kwake, kucheza shere na kuwa na hasira, kwa yale yaliyoteremka humo ya kutaja aibu zao na matendo yao, kisha wanasema, «Je, kuna yoyote anayewaona mkiondoka kwa Mtume?» Iwapo hakuna yoyote aliyewaona huinuka na kuondoka kwa Mtume, rehema na amani zimshukiye, wakiogopa fedheha. Mwenyezi Mungu Amezipindua nyoyo zao Ameziepusha na Imani kwa sababu wao hawaelewi wala hawazingatii.
Hakika amewajia nyinyi, enyi Waumini, mjumbe atokanao na watu wenu, Azionea uzito shida mlizonazo na masumbuko, ana pupa kwamba muamini na mambo yenu yafaulu na yeye kwa Waumini ni mwingi wa upole na huruma.
Basi washirikina na wanafiki wakikupa mgongo kwa kuacha kukuamini, ewe Mtume, sema kuwaambia, «Mwenye kunitosha ni Mwenyezi Mungu; Ananitosheleza yote yanayonitia hamu, hapana muabudiwa yoyote wa haki isipokuwa Yeye, Kwake yeye nimetegemea na Kwake Yeye nimeyategemeza mambo yangu yote. Kwani Yeye Ndiye Mwenye kuninusuru na Mwenye kunisaidia. Na Yeye Ndiye Mola wa Arsh iliyo kubwa, ambayo ndiyo kiumbe kikubwa kabisa.»