ترجمة معاني سورة الطلاق
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
Ewe Mtume! Pindi mnapotaka, wewe na Waumini, kuwapa talaka wake zenu, basi wapeni talaka wakiwa kwenye hali ya kukabili kipindi cha wao kukaa eda- yaani kwenye hali ya usafi ambao hakukupatikana kuingiliwa, au katika hali ya mimba iliyo wazi- na mshike hesabu ya eda, mpate kujua muda wa kuwarejea iwapo mtataka kuwarejea, na muogopeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu. Wala msiwatoe wanawake waliopewa talaka kwenye majumba wanayokaa mpaka eda lao limalizike, nalo ni hedhi tatu kwa asiyekuwa mdogo (asiyeingia damuni) na si kwa aliyekata tamaa ya kuingia damuni (kwa uzee) wala mwenye mimba. Na haifai kwa wanawake hao kutoka majumbani mwao wao wenyewe isipokuwa watakapofanya kitendo kiovu cha waziwazi kama vile uzinifu. Na hizo ndizo hukumu za Mwenyezi Mungu alizozipitisha kwa waja Wake. Na Mwenye kuzikiuka hukumu za Mwenyezi Mungu, basi huyo amejidhulimu nafsi yake na ameipeleka mahali pa maangamivu. Hujui, ewe mtoaji talaka, kwamba Mwenyezi Mungu huenda, baada ya talaka hiyo, Akaleta jambo usilolitazamia ukaja ukamrudia.
Na pindi kipindi cha eda la wanawake waliopewa talaka kinapokaribia kumalizika, basi warudieni na mtangamane nao kwa wema pamoja na kuwapatia matumizi, au waacheni pamoja na kuwatekelezea haki zao bila kuwafanyia mambo ya kuwadhuru. Na wekeni mashahidi mnaporejeana na mnapoachana, wanaume wawili waadilifu miongoni mwenu. Na tekelezeni, enyi mashahidi, ushahidi wenu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu na sio kwa kitu kingine. Hilo ambalo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha kwalo yuwawaidhiwa nalo yule anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na yoyote atakayemuogopa Mwenyezi Mungu akayafuata kivitendo yale ambayo Amemuamrisha nayo na akayaepuka yale ambayo Amemkataza nayo, Atamtolea njia ya kutoka kwenye kila dhiki
na Atamfanyia nyepesi njia za kupata riziki kwa namna ambayo haikupita akilini mwake wala haikuwa kwenye hesabu zake. Na yoyote atakayemtegemea Mwenyezi Mungu basi Yeye Atamtosheleza yale yanayomkera katika mambo yake yote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kulifikilia jambo Lake, Hapitwi na kitu chochote wala haelemewi na kitu chochote kinachotakikana na Yeye, hakika Mwenyezi Mungu Amekiwekea kila kitu muda wake wa kukomea na kipimo ambacho kitu hiko hakiwezi kukipita.
Na wanawake walioachwa ambao damu zao za hedhi zimekatika kwa utu uzima wao, mkitatizika mkawa hamjui: ni nini hukumu yao? Basi, eda lao ni miezi mitatu. Na wanawake wadogo ambao hawajaingia damuni, basi eda lao ni miezi mitatu vilevile. Na wanawake wajawazito, eda lao ni linamalizikia pale wanapozaa. Na yoyote atakayemuogopa mwenyezi Mungu na akatekeleza hukumu Zake, Atamfanyia mambo Yake yawe mepesi duniani na Akhera.
Hayo yailotajwa kuhusiana na mambo ya talaka na eda ni amri ya Mwenyezi Mungu Aliyoiteremsha kwenu, enyi watu, ili muitumie. Na yoyote mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu akawa anamcha kwa kuyaepuka yale ya kumuasi na kuzitekeleza faradhi Zake, basi Atamfutia madhambi yake, Atamuongezea kwa wingi malipo yake huko Akhera na amuingize Peponi.
Wakalisheni, wale walioachwa miongoni mwa wake zenu kwenye kipindi chao eda, mahali mfano wa pale mnapokaa nyinyi kwa kadiri ya ukunjufu wenu na uwezo wenu. Wala msiwafanyie mambo ya kuwadhuru mkawatilia mkazo katika makazi. Na iwapo wake zenu waliopewa talaka ni waja wazito, basi wapeni matumizi pindi wakiwa kwenye eda lao mpaka watakapozaa. Na iwapo watawanyonyeshea nyinyi watoto wao ambao ni wenu kwa malipo, basi wapeni malipo yao, na amrishaneni nyinyi kwa nyinyi wema na roho nzuri. Na iwapo hamkukubaliana juu ya unyonyeshaji wa mama mzazi, basi baba atanyonyeshewa na mnyonyeshaji mwingine asiyekuwa mama aliyepewa talaka.
Na atoe matumizi mume kulingana na kile alichokunjuliwa nacho na Mwenyezi Mungu kumpa mkewe aliyeachana naye na amlipie mwanawe, iwapo mume ana ukunjufu wa mapato. Na yule ambaye amebanika kimatumizi naye ni fukara, basi na atoe kulingana na kile alichopewa na Mwenyezi Mungu katika matumizi. Masikini halazimishwi kutoa kama kile anacholazimishwa tajiri. Mwenyezi Mungu Ataleta, baada ya dhiki na shida, ukunjufu wa maisha na kutosheka.
Na kuna vitongoji vingi ambavyo watu wake waliasi amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mitume Wake na wakaendelea kwenye ukiukaji wao na ukafiri wao,
tukawahesabu juu ya matendo yao duniani hesabu kali mno na tukawaadhibu adhabu kubwa na mbaya, wakauonja mwisho mbaya wa ujeuri wao na ukafiri wao, na mwisho wa ukafiri wao ulikuwa ni maangamivu na hasara, hapana hasara nyingine baada ya hiyo.
Mwenyezi Mungu Amewaandalia watu hawa, waliokiuka mipaka na wakaenda kinyume na amri za Mwenyezi Mungu na amri za Mitume Wake, adhabu kali sana. Basi muogopeni Mwenyezi Mungu na mjihadhari na mambo Anayoyachukia, enyi watu wenye akili zilizokomaa, mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo! Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ameteremsha kwenu, enyi Waumini, Ukumbusho wa kuwakumbusha nao na kuwazindusha juu ya fungu lenu la kumuamini Mwenyezi Mungu na kuwa watiifu Kwake kivitendo.
Na ukumbusho huu ni Mtume anayewasomea nyinyi aya za Mwenyezi Mungu zinazowafafanulia haki kwa kuitenga na ubatilifu, ili Apate kuwatoa, wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakazifuata Sheria Zake kivitendo na wakamatii, kutoka kwenye giza la ukafiri kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani. Na yoyote atakayemuamini Mwenyezi Mungu na akafanya matendo mema Atamuingiza kwenye mabustani ya Peponi ambayo chini ya miti yake inapita mito ya maji, wasalie humo milele. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ameifanya riziki ya Muumini mwema iwe nzuri huko Peponi.
Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyeziumba mbingu saba na Akaumba ardhi saba, na Akateremsha amri kupitia wahyi Aliyowateremshia Mitume Wake na kwa yale Anayowapangia viumbe Vyake kwayo kati ya mbingu na ardhi, ili mpate kujua , enyi watu, kwamba Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna kinachomshinda na kwamba Mwenyezi Mungu Amekizunguka kila kitu kiujuzi, basi hakuna kitu chochote kilichoko nje ya ujuzi Wake na uweza Wake.