ترجمة سورة الإسراء

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الإسراء باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Mwenyezi Mungu Anajisifu na kujitukuza kwa uweza Wake juu ya yasiyowezekana na yoyote isipokuwa Yeye, hapana Mola isipokuwa Yeye, hapana Mlezi isipokuwa Yeye. Yeye Ndiye ambaye Aliyempeleka mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kipindi cha usiku, kwa mwili wake na roho yake, katika hali ya kuangaza na siyo ya kulala, kutoka msikiti wa Ḥarām Uliyoko Makkah, kwenda msikiti wa Aqṣā uliyoko Bayt al- Maqdis, ambao Mwenyezi Mungu Amezibariki sehemu zinazouzunguka kwa matunda, nafaka na vinginevyo, na Akaufanya ni mahali pa Manabii wengi, ili ajionee maajabu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na dalili za upweke Wake. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Ndiye Mwenye kuzisikia sauti zote, Ndiye Mwenye kukiona kila cha kuonekana, na Atampa kila mmoja anachofaa kupata duniani na Akhera.
Na kama Mwenyezi Mungu Alivyomtukuza Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kumpeleka safari hiyo ya usiku, Alimtukuza Mūsā, amani imshukiye, kwa kumpa Taurati na Akaifanya ni yenye kuufafanua ukweli na kuwaongoza Wana wa Isrāīl na Akaifanya ni yenye kukusanya makatazo kwao ya kumfanya asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni mtegemewa au ni muabudiwa wakawa wamtegemezea mambo yao.
Enyi kizazi cha wale tuliowaokoa na tukawabeba pamoja na Nūḥ katika jahazi, msimshirikishe Mwenyezi Mungu katika kumuabudu, na kuweni ni wenye kushukuru neema Zake na ni wenye kumfuata Nūḥ, amani imshukiye, kwani yeye alikuwa ni mja mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa moyo wake, ulimi wake na viungo vyake.
Na tuliwapasha habari Wana wa Isrāīl katika Taurati ambayo waliteremshiwa kwamba yeye hapana budi itatukia kutoka kwao uharibifu mara mbili katika Bayt al- Maqdis na sehemu zinazofuatia kwa kudhulumu, kuua Manabii, kufanya kiburi, kupita kiasi na kufanya uadui.
Ukitukia kutoka kwenu uharibifu wa kwanza, tutawasaliti nyinyi na waja wetu wenye ushujaa na nguvu kali, watawashinda, watawaua na watawafukuza, hapo wazunguke kwenye nyumba zenu wakifanya uharibifu. Hiyo ilikuwa ni ahadi isiyokuwa na budi kutukia kwa kupatikana sababu zake kutoka kwenu.
Kisha tukawarudishia ushindi, enyi wana wa Isrāīl, na kuwa juu ya maadui zenu waliowasaliti, na tukawazidishia riziki zenu na watoto wenu na tukawapa nguvu na tukawafanya muwe wengi wa idadi kuliko adui yenu. Hiyo ni kwa sababu ya wema wenu na unyenyekevu wenu kwa Mola wenu.
Mkifanya matendo yenu na maneno yenu kuwa mazuri,basi mimejifanyia vizuri nyinyi wenyewe, kwa kuwa malipo ya hayo yatarudi kwenu; na mkifanya vibaya, basi mateso ya hayo ni yenye kuwarudia nyinyi. Na utakapofika wakati wa uharibifu wa pili, tutawasaliti maadui wenu mara nyingine, ili wawadhalilishe na wawashinde na idhihiri athari ya udhalilifu na utwevu kwenye nyuso zenu na wawaingilie kwenye Bayt al Maqdis waiharibu kama walivyoiharibu mara ya kwanza na wavunjevunje kila kilichoko chini ya mikono yao uvunjaji kamili.
Inatarajiwa kuwa Mola wenu, enyi Wana wa Isrāīl, Atawarehemu baada ya kuwatesa, mkitubia na mkatengenea, na mkirudi kufanya uharibifu na maonevu, tutarudi kuwatesa na kuwadhili. Na tumeufanya moto wa Jahanamu, kwenu na kwa makafiri kwa jumla, ni gereza ambalo hakuna kutoka humo kabisa. Katika aya hii na ile kabla yake pana onyo kwa ummah huu dhidi ya kufanya maasia ili lisiwapate lile lililowapata Wana wa Isrāīl, basi mipango ya Mwenyezi Mungu ni mimoja, haina kubadilika wala kugeuka.
Hii Qur’ani tuliyoiteremsha kwa mja wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, inawaongoza watu kwenye njia nzuri kabisa nayo ni mila ya Kiislamu, na inawapa bishara njema Waumini, wanaofanya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaamrisha kwayo na wanaokomeka na yale ambayo Amewakataza nayo, kwamba watakuwa na malipo makubwa,
na kwamba wale ambao hawaamini Nyumba ya Akhera na malipo yaliyoko huko, tumewatayarishia adhabu yenye kuumiza ndani ya Moto.
Na binadamu wakati mwingine hujiapiza mabaya nafsi yake au mtoto wake au mali yake awapo na hasira kama vile anavyoomba mema. Hii ni kwa sababu ya ujinga wa mwanadamu na pupa lake. Na miongoni mwa rehema ya Mwenyezi Mungu kwake ni kwamba Yeye Anayakubali maombi yake mema na sio mabaya na kwamba Yeye anajua kuwa yeye hakukusudia kutaka hilo. Hakika binadamu ana tabia ya kuwa na pupa sana.
Na tumefanya usiku na mchana kuwa ni alama mbili zenye kuonyesha upweke wetu na uweza wetu, tukaifuta alama ya usiku, nayo ni mwezi, na tukaifanya alama ya mchana, nayo ni jua, ni yenye mwangaza, ili binadamu apate kuona kwenye mwangaza wa mchana namna ya kupekesha mambo ya maisha yake na ili aingie kwenye utulivu na mapumziko wakati wa usiku, na ili watu wajue, kwa kupishana mchana na usiku, idadi ya miaka na hesabu ya miezi na siku, wakaweka juu ya hiyo mipango wanayoitaka ya maslahi yao. Na kila kitu tumekifafanua ufafanuzi wa kutosha.
Na kila binadamu Mwenyezi Mungu Anayajaalia yale anayoyatenda, yawe mema au maovu, ni yenye kuwa na yeye wakati wote, hatahisabiwa kwa matendo ya mtu mwingine, wala mwingine hatahesabiwa kwa matendo yake yeye. Na Mwenyezi Mungu Atamtolea , Siku ya Kiyama, kitabu kilichoandikwa ndani yake yale aliyoyatenda; atakiona kimefunguliwa mbele yake.
Ataambiwa, «Soma kitabu cha matendo yako.» Hapo atasoma, hata kama hakuwa akijua kusoma ulimwenguni, «Leo nafsi yako itakutosheleza kuwa ni yenye kukuhesabia matendo yako, upate kujua malipo yake.» Huu ni miongoni mwa uadilifu na uchungaji haki mkubwa kabisa kwamba mja aambiwe, ‘jihesabu nafsi yako, kwani inatosha kuwa ni yenye kukuhesabu. ’
Mwenye kuongoka akafuata njia ya haki, basi malipo mema yake yatamrudia yeye peke yake; na mwenye kupotoka akafuata njia ya ubatilifu, basi mateso ya kufanya hivyo yatamrudia yeye peke yake; na hakuna nafsi yoyote iliyofanya dhambi itabeba makosa ya nafsi nyingine iliyofanya dhambi. Na Mwenyezi Mungu Hatamuadhibu yoyote isipokuwa baada ya kumsimamishia hoja kwa kutuma Mitume na kuteremsha Vitabu.
Na tukitaka kuwaangamiza watu wa mji kwa udhalimu wao, tunawaamrisha wenye gogi wao wamtii Mwenyezi Mungu, wampwekeshe na wawaamini Mitume Wake, na wasokuwa wao wako nyuma yao kwa kuwafuata, wakaasi amri ya Mola wao na wakawakanusha Mitume Wake, hapo likapasa juu yao neno la adhabu ambalo hakuna namna ya kurudishwa, na tukawamaliza kwa maangamivu yaliyotimia.
Na ni wengi tuliowaangamiza miongoni mwa watu waliokanusha Mitume wao baada ya Nabii wa Mwenyezi Mungu, Nūḥ. Na inatosha kwamba Mola wako, ewe Mtume, ni Mjuzi wa matendo yote ya waja Wake, hakifichamani Kwake chochote chenye kufichamana.
Yoyote ambaye matakwa yake ni ulimwengu huu wa sasa na akaushughulikia huo peke yake, asiiamini Akhera na asifanye matendo ya kumfaa huko, Mwenyezi Mungu Atamharakishia, hapa ulimwenguni, Anayoyataka Mwenyezi Mungu na kuyapendelea miongoni mwa yale aliyoyaandika kwenye Ubao Uliohifadhiwa (Al- Lawḥ Al-Mahfūḍ) kisha Mwenyezi Mungu Atamjaalia huko Akhera moto wa Jahanamu, atauingia akiwa ni mwenye kulaumiwa, ni mwenye kufukuzwa kwenye rehema Yake Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka. Hiyo ni kwa sababu ya kutaka kwake ulimwengu na kujishughulisha nao bila ya Akhera.
Na yoyote aliyekusudia kwa matendo yake mema kupata malipo ya Nyumba ya Akhera yenye kusalia na akajishughulisha nayo kwa kumtii Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na hali yeye ni mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu na kuamini thawabu Zake na malipo Yake makubwa, basi hao matendo yao ni yenye kukubaliwa ni yenye kuhifadhiwa kwa ajili yao mbele ya Mola wao na watapata malipo yake.
Kila kundi, miongoni mwa wenye kuufanyia kazi ulimwengu wenye kumalizika na wenye kuifanyia kazi Akhera yenye kusalia, tunalipatia riziki yetu: tunawaruzuku Wauminiu na makafiri ulimwenguni. Kwani riziki inatokana na vipawa vya Mola wako kwa wema Wake; na vipawa vya Mola wako hanyimwi mtu yoyote, awe ni Muumini au ni kafiri.
Taamali, ewe Mtume, vile Mwenyezi Mungu Alivyowatukuza baadhi ya watu juu ya wengine ulimwenguni kiutajiri na kimatendo. Na Akhera in daraja kubwa zaidi kwa Waumini na ina matukuzo makubwa zaidi.
Usimfanye, ewe mwanadamu, pamoja na Mwenyezi Mungu mshirika yoyote katika ibada Yake, kwani ukifanya hivyo utarudi uwe ni mwenye kutukanika na kuhizika.
Na Mola wako, ewe mwanadamu, Ameamrisha na kulazimisha na kupasisha Apwekeshwe, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, kwa kuabudiwa Peke Yake, na Ameamrisha kuwafanyia wema baba na mama, hasa wakiwa katika hali ya ukongwe: usione dhiki wala uzito kwa jambo lolote ulionalo kwa mmoja wao au kwa wao wawili, wala usiwasikizishe neno baya, hata kama ni sauti ya kuonesha kutoridhika ambayo ni neno baya la daraja ya chini kabisa, wala usiwafanyie tendo baya, lakini kuwa mpole kwao na uwaambie wao daima maneno mapesi yenye ulaini.
Na uwe, kwa mamako na babako, mdhalilifu na mnyenyekevu kwa kuwahurumia, na umuombe Mola wako awarehemu kwa rehema Zake kunjufu wakiwa hai na wakiwa wamekufa, kama walivyovumilia juu ya kukulea ulipokuwa mdogo usiokuwa na uwezo wala nguvu.
Mola wenu, enyi watu, ni Mjuzi zaidi wa mazuri na mabaya yaliyomo ndani ya nyoyo zenu. Iwapo matakwa yenu na makusudio yenu ni kumridhisha Mwenyezi Mungu na kujikaribisha Kwake, basi Yeye, kutakata na sifa mbaya ni Kwake, kwa wenye kurejea Kwake katika nyakati zote ni Mwingi wa kusamehe. Basi yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Amejua kwamba hakuna katika moyo wake isipokuwa ni kurejea Kwake na kumpenda, Yeye Atamsamehe na Atamghufiria yatakayotukia miongoni mwa madhambi madogo yanayolingana na tabia za kibinadamu.
Na umfanyie wema kila mwenye ukaribu wa ujamaa na wewe, na umpe haki yake ya wema na hisani, na umpe masikini mwenye uhitaji na msafiri aliyeepukana na watu wake na mali yake, na usitumie mali yako katika njia isiyokuwa ya kumtii Mwenyezi Mungu au kwa njia ya kupita kiasi na ufujaji.
Hakika wale wenye kupita kiasi katika matumizi na wenye kutoa mali yao katika kumuasi Mwenyezi Mungu wanafanana na Mashetani kwenye uovu, uharibifu na maasia, na Shetani ni mwingi wa kukufuru, ni mkanushaji sana neema za Mola wake.
Na ukiwaepuka hawa ambao uliamrishwa uwape, kwa kuwa hakuna kitu cha kuwapa, kwa kungojea riziki kutoka kwa Mola wako, basi waambie maneno laini ya upole kama vile kuwaombea dua awatajirishe na awape riziki kunjufu, na uwaahidi kwamba Mwenyezi Mungu Akiyafanya mambo ya riziki kuwa mapesi kwa wema Wake basi wewe utawapatia nao.
Wala usiuzuie mkono wako kutumia katika njia njema, ukaidhiki nafsi yako na watu wako na wahitaji, na wala usipite kiasi katika matumizi ukatoa zaidi ya uwezo wako, kwani ukifanya hivyo utaketi hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa, kwani watu watakulaumu na watakutukana, na ni mwenye kujuta juu ya ufujaji wako na mali yako kupotea.
Hakika Mola wako nawakunjulia riziki baadhi ya watu na Anawabania wengine kulingana na ujuzi Wake na hekima Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake. Yeye Ndiye Mwenye kuyaona mambo ya ndani ya waja Wake, hakuna chochote katika hali zao kilicho nje ya ujuzi Wake.
Na mkijua kwamba riziki iko kwenye mkono wa Mwenyezi Mungu, kutkata na sifa za upungufu ni Kwake, basi msiwaue watoto wenu kwa kuchelea umasikini, kwani Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye kuwaruzuku waja Wake, Anawruzuku wana kama Anavyowaruzuku wazazi. Hakika kuua watoto ni dhambi kubwa.
Wala msikaribie uzinifu na mambo yanayopelekea huko ili msiingie ndani yake, hakika hilo ni tendo baya sana, na njia mbaya zaidi ni njia ya tendo hilo.
Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, isipokuwa kwa haki ya kisharia, kama kisasi au kumpiga mawe mzinifu aliyeingia kwenye hifadhi ya ndoa au kumuua aliyeritadi. Na mwenye kuuawa pasi na haki ya kisheria, basi tumempa msimamizi wa mambo yake , awe ni mrithi au ni hakimu, uwezo wa kutaka muuaji auawe au kutaka dia. Na haifai kwa msimamizi wa mambo ya aliouawa kupita mpaka wa Mwenyezi Mungu katika kuchukua kisasi, kama vile kuua watu wawili au wengi kwa mmoja au kumua muuaji kwa njia ya kumtesa. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumsaidia msimamizi wa aliyeuawa juu ya aliyeua mpaka aweze kumuua kwa njia ya kisasi.
Wala msitumie mali ya watoto waliofiliwa na wazazi wao nao wako chini ya miaka ya kubaleghe na wakawa wako chini ya usimamizi wenu, isipokuwa kwa njia ambayo ni nzuri kwao, nayo ni kuyazalisha na kuyakuza, mpaka afikie mtoto yatima miaka ya kubaleghe na utumiaji mzuri wa mali. Na timizeni utekelezaji wa kila ahadi mliyojilazimisha nayo, kwani Mwenyezi Mungu Atamuuliza mwenye kuweka ahadi kuhusu hiyo ahadi Siku ya Kiyama, Atamlipa akiitimiza na kuitekeleza na Atamtesa akienda kinyume nayo.
Na timizeni kipimo wala msikipunguze mnapowapimia wasiokuwa nyinyi, na mfanye mizani ya sawa, kwani kufanya uadilifu katika upimaji wa vibaba na mizani ni bora kwenu nyinyi ulimwenguni na kuna mwisho mwema mbele ya Mwenyezi Mungu kesho Akhera.
Na usiyafuate, ewe binadamu, usiyoyajua, lakini hakikisha na uthibitishe. Hakika ya biadamu ni mwenye kuulizwa juu ya yale ambayo alitumia masikizi yake, maangalizi yake na moyo wake kuyafikia. Basi akivitumia vitu hivyo katika wema atapata malipo mema na akivitumia katika uovu atapata mateso.
Na usitembee ardhini kwa kujigamba na kujivuna, kwani wewe hutaipasua ardhi kwa kutembea juu yake kwa namna hiyo na hutaifikia milima katika urefu kwa kujigamba kwako, kujivuna kwako na kutakabari kwako.
Yote yaliyotangulia kutajwa, ya maamrisho na makatazo, Mwenyezi Mungu Anayachukia mabaya yake na hayaridhii kwa waja wake.
Hayo tuliyoyaeleza na kuyafafanua kati ya hizi hukumu tukufu za kuamrisha matendo mema na kukataza tabia duni, ni miongoni mwa yale tuliyokutumia wahyi nayo. Na usimfanye, ewe binadamu, pamoja na Mwenyezi Mungu yoyote kuwa ni mshirika Wake katika kumuabudu, ukaja kutiwa ndani ya moto wa Jahanamu, hali ukilaumiwa na nfsi yako na watu, na ukawa ni mwenye kufukuzwa na kuepushwa na kila kheri.
Je, kwani Amewahusu nyinyi Mola wenu, enyi washirikina, kwa kuwapa watoto wa kiume na Yeye Akajichukulia kutokana na Malaika watoto wa kike? Neno lenu hili ni upeo wa ubaya na linachukiza sana, halinasibiani na Mwenyezi Mungu, kuepukana na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake.
Hakika tumeelza katika hii Qur’ani aina mbalimbali za hukumu, mifano na mawaidha, ili watu wapate kuwaidhika na kuzingatia yanayowafaa wayachukue na yenye kuwadhuru wayaache. Na haya maelezo na ufafanuzi hayawaongezei madhalimu isipokuwa kuwa mbali na haki na kughafilika kutia mambo akilini na kuzingatia.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Lau kulikuwa na waungu wengine pamoja na Mwenyezi Mungu, basi wangalitafuta waungu hao njia ya kushindana na Mwenyezi Mungu Mwenye 'Arshi iliyo kubwa.»
Mwenyezi Mungu Ameepukana na kutakata na hayo wanayoyasema washirikina, na Ametukuka utukufu mkubwa.
Zinamtakasa Yeye, kutakata ni Kwake, mbingu saba na ardhi na viumbe wote waliyo humo. Na kila kitu kilichoko katika ulimwengu huu kinamuepusha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na sifa za upungufu, maepusho yanayofungamana na kumsifu na kumshukuru, kutakata ni Kwake, lakini nyinyi,enyi watu, hamtambui hilo. Kwa kweli, Yeye ni Mpole kwa waja Wake, hawaharakishii adhabu wanaomuasi, ni Mwingi wa msamaha kwao.
Na usomapo Qur’ani wakaisikia hawa washirikina, tunaweka baina yako wewe na hawa wasioiamini Akhera pazia yenye kusitiri ili kuziziba akili zao wasiifahamu Qur’ani, ikiwa ni mateso kwao kwa ukafiri wao na kukanusha kwao.
Na tumeweka juu ya nyoyo za washirikina vifiniko, wasipate kuifahamu Qur’ani, na tumejaalia uziwi ndani ya mashikio yao, wasipate kuisikia. Na umtajapo Mola wao katika Qur’ani uwalinganiapo kwenye kumpwekesha Yeye na ukatazapo kushirikishwa, wao hurudi kinyumenyume kwa kuyakimbia maneno yako, kwa kutakabari na kujiona kuwa ni wakubwa mno wa kutofaa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Peke Yake, katika kumuabudu.
Sisi tunayajua zaidi yale wanayoyasikiliza viongozi wa Kikureshi pale wakusikilizapo na hali nia zao ni mbovu. Kusikiliza kwao si kwa ajili ya kutaka kuogoka na kuikubali haki. Na sisi tunajua kule kunong’onezana kwao wanaposema, «Hamumfuati isipopkuwa ni mwanamume aliyerogwa na akili yake ikabadilika.»
Fikiri, ewe Mtume, kwa kulionea ajabu neno lao kwamba Muhammad ni mchawi mshairi mwenye wazimu. Hivyo basi wamekiuka mpaka na wamepotoka na hawakuongokea njia ya haki na usawa.
Wasirirkina walisema wakikanusha kwamba wataumbwa umbo jipya baada ya mifupa yao kuoza na kuwa mbalimbali, «Je, sisi tutafufuliwa ufufuzi mpya Siku ya Kiyama?»
Waambie, ewe Mtume, kwa njia ya kuwafanya washindwe, «Kuweni na nguvu na ugumu kama mawe au chuma mkiweza hilo.
Au kuweni umbo lolote kubwa ambalo akili zenu zaliona kuwa liko mbali na uhakika.» Na watasema kwa kukanusha, «Ni nani atakayeturudisha kwenye uhai baada ya kufa?» Waambie, «Atakayewarudisha na kuwarejesha ni Mwenyezi Mungu Aliyewaumba kutoka kwenye hali ya kutokuwako mara ya kwanza.» Na wasikiapo majibu haya watatikisa vichwa vyao kwa njia ya shere, huku wakiona ajabu na watasema, wakiliona jambo hilo kuwa ni mbali kukubalika, «Ufufuzi huu utatukia lini?» Sema, «Ni lipi linalowajulisha kwamba Ufufuzi huu, mnaoukanusha na mnaouona kuwa uko mbali, huenda ukawa ni wenye kutukia kipindi cha karibu?»
Siku Atakapowaita Muumba wenu mtoke kwenye makaburi yenu na mkaitika amri ya Mwenyezi Munguna na mkaiyandama, na shukrani ni Zake kwa kila namna, na mkadhani, kwa kituko cha Siku ya Kiyama na kwa kipindi kirefu cha kukaa kwenu Akhera, kwamba nyinyi hamkukaa duniani isipokuwa muda mchache.
Na waambie waja wangu Waumini waseme, katika mazungumzo yao na kushauriana kwao wao kwa wao, maneno mazuri, kwani wao wakitofanya hivyo Shetani atatia ugomvi, uharibifu na utesi baina yao. Hakika Shetani kwa binadamu ni adui aliyeudhihirisha uadui.
Mola wenu Anawajua nyinyi zaidi, enyi watu, Akitaka Atawarehemu Awaafikie kwenye Imani au Akitaka atawafisha kwenye ukafiri kisha Awaadhibu. Na hatukukutumiliza, ewe Mtume, uwe ni muwakilishi juu yao, unayapanga mambo yao na unawalipa kwa matendo yao, jukumu lako ni kuyafikisha uliyotumilizwa kwayo na kuieleza njia iliyolingana sawa.
Na Mola wako, ewe Mtume, Anawajua zaidi walioko mbinguni na ardhini, na tumewafadhilisha baadhi ya Mitume juu ya wengine kwa matukufu, wingi wa wafuasi na kuwateremshia Vitabu, na Dawud, amani imshukiye, tumempa Zaburi.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina wa Makkah, «Hawa masanamu mnaowaita wawaondolee shida hawawezi hilo wala hawawezi kuiyepusha kwenu nyinyi kuipeleka kwa wengine, na pia hawawezi kuigeuza kutoka namna ilivyo kuifanya namna nyingine, Mwenye kuweza hilo ni Mwenyezi Mungu Peke Yake.» Aya hii inakusanya kila anayeombwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, miongoni mwa Manabii, watu wema na wasiokuwa hao, kwa tamko la istighāthah (kutaka uokozi) au du'a’ (maombi) au mfano wake, kwani hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Hao ambao washirikina wanawaomba, miongoni mwa Manabii, watu wema na Malaika, wao wenyewe wanashindana kujiweka karibu na Mola wao kwa matendo mema wanayoyaweza, wanatarajia rehema Yake na wanaogopa adhabu Yake. Hakika adhabu ya Mola wako ndiyo ambayo inatakikana kwa waja wawe na hadhari nayo na waiogope.
Na Mwenyezi Mungu Anawaonya wanaokufuru kwamba hakuna mji wowote wenye kukufuru na kukanusha Mitume isipokuwa mateso Yake yataushukia kwa maangamivu hapa duniani kabla ya Siku ya Kiyama au kwa adhabu kali juu ya watu wake. Hayo ni maandishi Aliyoyaandika Mwenyezi Mungu na hukumu Aliyoipitisha, hapana budi kujiri, nayo imeandikwa kwenye Al-Lawḥ Al-Mahfūḍ (Ubao Uliohifadhiwa).
Hakuna kilichotuzuia kuteremsha miujiza ambayo washirikina waliitaka isipokuwa ni kwamba ummah waliowatangulia waliikanusha, Mwenyezi Mungu Aliwajibu kwa waliyotaka wakakanusha na wakaangamia. Na tuliwapa Thamūd, nao ni watu wa Ṣāliḥ, miujiza iliyo wazi, nayo ni ngamia, wakaikanusha na tukawaangamiza. Na huku kutuma kwetu Mitume wakiwa na alama, mazingatio na miujiza tuliyoipitisha kwenye mikono yao, hakukuwa isipokuwa ni kuwatisha waja wapate kuzingatia na wakumbuke.
Kumbuka, ewe Mtume, pindi tulipokwambia kwamba Mola wako Amewazunguka watu kwa ujuzi na uweza. Na hatukuijaalia ndoto tuliyokuonyesha waziwazi usiku wa isrā’ (kwenda Bayt al- Maqdis) na mi'rāj (kupaa kwenda mbinguni) miongoni mwa maajabu ya viumbe isipokuwa ni kuwatahini watu. Na tunawatisha washirikina kwa aina mbalimbali za adhabu na miujiza, lakini kuwatisha huko hakuwaongezei isipokuwa ni kuendelea zaidi kwenye ukafiri na upotevu.
Na ukumbuke neno tulilowaambia Malaika wamsujudie Ādam kwa kumwamkia na kumuhishimu, wakamsujudia wote isipokuwa Iblisi, alifanya kiburi na akakataa kusujudu, na huku akisema kwa njia ya kupinga na kujiona, «Je, nimsujudie huyu dhaifu aliyeumbwa kwa udongo?»
Iblisi akasema akionesha ujasiri wake na ukafiri kwa Mwenyezi Mungu, «Unamuona kiumbe huyu uliyemfadhilisha juu yangu? Ukinibakisha hai mpaka Siku ya Kiyama nitawatawala wale wanaozalikana na yeye kwa kuwapoteza na kuwaharibu isipokuwa wale waliotakaswa katika Imani, nao ni wachache.»
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Akasema Akimuonya Iblisi na wafuasi wake, «Enda! Yoyote mwenye kukufuata miongoni mwa kizazi cha Ādam, basi mateso yako na mateso yao ndani ya moto wa Jahanamu ni mengi.
«Na uwalaghai wale unaoweza kuwalaghai miongoni mwao kwa kuwaita kuniasi, na uwakusanyie askari zako unaowaweza, kati ya kila aliye juu ya kipando na anayetembea kwa miguu, na ujishirikishe nao katika mali yao wanayoyachuma kwa njia za haramu, na ujishirikishe nao katika watoto wao kwa kuwapambia uzinifu na uasi na kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu mpaka uenee uchafu na uharibifu, na uwaahidi wafuasi wako, miongoni mwa wale wanaozalikana na Ādam, ahadi za urongo, na kila ahadi za Shetani ni ubatilifu na udanganyifu.
«Hakika waja wangu Waumini waliyotakaswa ambao walinitii, wewe huna uwezo wa kuwapoteza.» Na inatosha kuwa Mola wako , ewe Mtume, kuwa Ndiye Mwenye kuwalinda na kuwahifadhi Waumini kutokana na vitimbi vya Shetani na udanganyifu wake.
Mola wenu, enyi watu, Ndiye Anayewaendeshea vyombo vya kusafiria baharini ili mtafute riziki ya Mwenyezi Mungu katika safari zenu na biashara zenu. Hakika Mwenyezi Mungu , kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwingi wa huruma kwa waja Wake.
Na mkipatikana na shida baharini mkakaribia kuzama na kuangamia, wanapotea kwenye akili zenu wale waungu ambao mlikuwa mkiwaabudu, na mkamkumbuka Mwenyezi Mungu Muweza, Peke Yake, Awasaidie na Awaokoe, hapo mnamtakasia katika kutaka msaada na uokzi, na Yeye Anawasaidia na Anawaokoa. Anapowaokoa kwa kuwaegesha kwenye nchi kavu, mnageuka mkaacha Imani, kumtakasia Mwenyezi Mungu na matendo mema. Na huu ni katika ujinga wa binadamu na ukafirir wake, kwani binadamu ni mkanushaji sana neema za Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka.
Je, mumeghafilika, enyi watu, na adhabu ya Mwenyezi Mungu, ndipo mkajiaminisha kwamba ardhi haitawaporomokea ikawadidimiza au kwamba Mwenyezi Mungu Hatawanyesheza mvua ya mawe itokayo juu iwaue kisha msipate yoyote wa kuwalinda na adhabu Yake?
Au mumejiaminisha, enyi watu, kwamba Mola wenu, na hali nyinyi mumemkanusha, hatawarudisha baharini mara nyingine kisha akawaletea kimbunga kikali chenye kuvunjavunja kila kitu kinachokifikia, kikaja kikawazamisha kwa ukanushaji wenu, kisha msipate kitu chochote cha madai au malalamiko juu yetu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu kitu chochote hata wizani wa chungu mdogo?
Kwa hakika tumewatukuza watu wa kizazi cha Ādam kwa akili na kuwapelekea Mitume, na tukawadhalilishia vilivyoko ulimwenguni vyote: tukawadhalilishia wanyama barani wa kuwapanda na vyombo baharini vya kuwabeba, tukawaruzuku vilaji na vinywaji vizuri na tukawapa daraja kubwa juu ya viumbe wengi.
Na kumbuka, ewe Mtume, Siku ya Kufufuliwa, kwa njia ya kutoa bishara na kuogopesha, pindi Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na ktukuka, Atakapoliita kila kundi la watu pamoja na kiongozi wao ambaye walikuwa wakimfuata ulimwenguni. Basi aliyekuwa mwema kati yao , na akapewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, hawa watasoma kitabu cha mema yao wakiwa katika hali ya kufurahika na kuterema, na kamwe hawatapunguziwa chochote katika malipo ya matendo yao mazuri, hata kama ni kadiri ya uzi unaokuwa kwenye mpasuko wa koko ya tende.
Na aliyekuwa kipofu wa moyo, katika ulimwengu huu, wa kutoziona dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, asiyaamini yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukiye, basi yeye, Siku ya Kiyama, atakuwa kipofu zaidi wa kutoiona njia ya Peponi na atapotea zaidi njia ya uongofu na usawa.
Na kwa hakika washirikina walikaribia kukuepusha, ewe Mtume, na Qur’ani Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ili utuzulie isiyokuwa hiyo tuliyokuletea wahyi nayo. Na lau ulifanya walivyotaka, wangalikufanya ni kipenzi msafiwa.
Na lau si sisi kukuimarisha kwenye haki na kukuhifadhi usikubaliane nao, ungalikaribia kuelemea kwao kidogo katika yale waliyokushauri kwa nguvu za udanganyifu wao na wingi wa hila zao na kuwa na hamu kwako waongoke.
Na lau ulielemea, ewe Mtume, upande wa hawa washirikina maelemeo madogo katika yale waliyotaka kwako, basi tungalikuonjesha mara mbili zaidi ya adhabu ya duniani na mara mbili zaidi ya adhabu ya baada ya kufa kesho Akhera, hivyo ni kwa ajili ya kutimia neema ya Mwenyezi Mungu kwako na ukamilifu wa kumjua Mola wako, kisha hutampata yoyote mwenye kukuepushia adhabu yetu.
Na makafiri walikaribia kukutoa Makkah kwa kukukera, na lau walikutoa huko hawangalikaa huko baada yako isipokuwa muda mchache, hadi iwashukie adhabu ya ulimwenguni.[6]
____________________
[6]Tafsiri ya aya hii yategemea moja ya sababu zilizotajwa za kuteremka kwake, nayo ni kuwa makafiri wa kikureshi walitaka kumtoa Mtume (s.a.w) kwenye mji, Mwenyezi Mungu Akawaonya kwa aya hii na kwamba wao lau walimtoa hawangalikaa kwenye mji wa Makkah baada yao isipokuwa muda mchache. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, kwani haukupita muda mrefu baada ya kugura kwa Mtume (s.a.w) kwenda Madīnah mpaka Mwenyezi Mungu Akawakusanya na wao hapo Badr, hapo wakubwa wao wakauawa na wengine kutekwa. Tazama Ibn Kathīr katika kufasiri aya hii.
Huo ndio mwendo uliowekwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika kuwaangamiza watu wanaomtoa Mtume wao kutoka kwao, na hutapata mabidiliko kwenye mwendo wetu, kwani hatuendi kinyume na ahadi yetu.
Simamisha Swala itimie kuanzia kipindi cha kupinduka jua wakati wa mchana mpaka kipindi cha usiku. Inaingia hapa Swala ya Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na Isha. Na simamisha Swala ya Alfajiri na urefushe kisomo chake, kwani Swala ya Alfajiri inahudhuriwa na Malaika wa usiku na Malaika wa mchana.
Na inuka, ewe Nabii, kutoka kwenye usingizi sehemu ya usiku, usome Qur’ani katika Swala ya usiku, ipate kuwa, hiyo Swala ya usiku, ni nyongeza kwako katika utukufu wa cheo na kupandishiwa daraja. Huenda Mwenyezi Mungu Akakuleta uwe ni mwenye kuwashufaia watu Siku ya Kiyama, ili Mwenyezi Mungu Awarehemu kwa kuwaondolea waliokuwa nayo, na usimame kisimamo ambacho watakushukuru kwacho wa mwanzo na wa mwisho.
Na useme, «Mola wangu! Nitia matio mazuri katika jambo lililo lema kwangu na unitoe matoko mazuri kwenye mambo yaliyo mabaya kwangu, na unipatie hoja thabiti kutoka kwako yenye kuniokoa na wote wanaoenda kinyume na mimi.»
Na useme, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Uislamu umekuja na ushirikina umeondoka. Kwani ubatilifu hauna kusalia wala kujikita, na ukweli ndio wenye kuimarika na kusalia ambao hauondoki.»
Na tunateremsha miongoni mwa aya za Qur’ani yanayopoza magonjwa ya nyoyo kama shaka , unafiki na ujinga, na yanayopoza miili kwa kujizungua nayo, na yanayokuza Imani ambayo ni sababu ya kufaulu kupata rehema ya Mwenyezi Mungu. Na hii Qur’ani haiwaongezei makafiri wanapoisikia isipokua ukafiri na upotevu, kwa kuikanusha kwao na kutoiamini.
Na tunapompa mwanadamu, vile alivyo, neema ya mali na afya na mfano wa hizo, anageuka na kujiweka mbali na kumtii Mwenyezi Mungu, na akipatikana na shida ya ufukara au ugonjwa huwa ni mwenye kukata tamaa, kwa kuwa yeye haamini kuwa atapata nyongeza njema za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuhifadhi katika hali yake ya raha na ya shida.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu, «Kila mmoja miongoni mwenu anatenda kulingana na hali zinazonasibiana na yeye , na Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa yule aliyeongoka zaidi njia ya haki.»
Na makafiri wanakuuliza juu ya uhakika wa roho kwa njia ya ushindani, basi wajibu kwamba uhakika wa roho na hali zake ni katika mambo ambayo Mwenyezi Mungu Ameufanya ujuzi wake uweko Kwake. Na hamukupewa ujuzi, nyinyi na watu wote, isipokuwa kitu kichache.
Na lau tulitaka kuifuta Qur’ani moyoni mwake, tungaliliweza hilo, na hungalimpata mwenye kukuhami ambaye atatuzuia kufanya hivyo au akurudishie Qur’ani.
Lakini Mwenyezi Mungu Alikurehemu, Akaithibitisha moyoni mwako, hakika wema Wake juu yako ni mkubwa. Yeye Amekupa hii Qur’ani tukufu, Al-Maqām al-Maḥmūd (Kisimamo Kishukuriwacho) na mengineyo miongoni mwa yale ambayo Hakumpa yoyote katika viumbe.
Sema, «Lau wataafikiana majini na binadamu kujaribu kuleta mfano wa hii Qur’ani yenye kuelemea, hawataweza kuileta, hata kama watashirikiana na kusaidiana kufanya hivyo.»
Na tumewafafanulia watu katika hii Qur’ani kila aina ya mfano unaopasa kuzingatiwa, kwa njia ya kuwasimamishia hoja, ili waifuate na waitumie, lakini wengi wa watu walikataa isipokuwa ni kuipinga haki na kuzikanusha hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake.
Na Qur’ani ilipowaelemea washirikina na ikawashinda, waliingia kutaka miujiza kulingana na mapendeleo yao wakasema, «Hatutakuamini, ewe Muhammad, na hatutafanya vile unavyosema mpaka utupasulie kwenye ardhi ya Makkah chemchemu ya maji yenye kupita.
«Au uwe na shamba lenye aina za mitende na mizabibu, na uifanye mito ni yenye kupita kati yake kwa wingi.
«Au uiangushe mbingu juu yetu iwe vipande-vipande kama ulivyodai, au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika Wake tuwaone wametukabili waziwazi.
«Au uwe na nyumba ya dhahabu, au upande daraja za kukupaisha mbinguni, na hatutaamini kupaa kwako mpaka urudi ukiwa na kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kilichofunguliwa tusome ndani yake kwamba wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kikweli.» Sema, ewe Mtume, kwa kushangaa juu ya ushindani wa makafiri hawa, «Kutakata na sifa za upungufu ni kwa Mola wangu! Kwani mimi ni nani, isipokuwa ni mja miongoni mwa waja Wake mwenye kufikisha ujumbe Wake? Basi vipi mimi nitaweza kuyafanya mnayoyataka?»
Na hakuna kilichowazuia makafiri kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuwatii, pindi ulipowajia wao ufafanuzi wa kutosha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa ni kule kusema kwao kwa ujinga na kwa njia ya kukanusha, «Je, kwani Mwenyezi Mungu Ametumiliza Mtume miongoni mwa jinsi ya binadamu?»
Waambie, ewe Muhammad, ukiwarudi washirikina kule kukanusha kwao kuwa Mtume ni miongoni mwa wanadamu, «Lau juu ya hii ardhi kulikuwa na Malaika wanatembea kwa kujituliza, tungaliwapelekea mtume miongoni mwa jinsi yao,» lakini watu wa ardhi ni wanadamu, basi mtume wa kupelekewa inatakiwa awe ni miongoni mwa jinsi yao, ili iwezekane kwao kuzungumza naye na kufahamu maneno yake.
Waambie, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi baina yangu mimi na nyinyi juu ya ukweli wangu na uhakika wa unabii wangu. Hakika Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mtambuzi wa hali za waja Wake ni Muoni wa matendo yao, na Atawalipa kwa hayo.»
Na yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Anamuongoza ndiye mwenye kuongoka kwenye haki, na yoyote yule ambaye Yeye Anampoteza, Akamdhili na Akamuachia yeye na nafsi yake basi huyo hakuna mwenye kumuongoza badala ya Mwenyezi Mungu. Hawa wapotevu Mwenyezi Mungu Atawafufua Siku ya Kiyama na Awakusanye kwa nyuso zao hali wakiwa hawaoni wala hawatamki wala hawasikii. Mwisho wao ni moto wa Jahanamu wenye kuwaka, kila kutuliapo kuwaka kwake na kuzimika mroromo wake, tunawazidishia moto wenye kuwaka na kuroroma.
Adhabu hii iliyosifiwa ni mateso kwa washirikina kwa sababu ya kukanausha kwao aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake, kukanusha kwao Mitume Wake waliowaita kumuabudu Yeye na kule kusema kwao kwa njia ya kukataa, waamrishwapo kuamini kuwa kuna Ufufuzi, «Tutakapokufa na tukawa mifupa iliyochakaa na vipande vilivyotengeka mbalimbali, je tutafufuliwa baada yake hali ya kuwa ni viumbe vipya?»
Je, kwani wameghafilika hawa washirikina, wasiangalie na kujuwa kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyeumba mbingu na ardhi na viumbe vilivyomo ndani yake bila ya mfano uliotangulia, ni muweza wa kuumba mfano wao baada ya kumalizika kwao? Mwenyezi Mungu Amewaekea washirikina hawa wakati maalumu wa kufa kwao na kuadhibiwa, hapana shaka wakati huo utawafikia. Na pamoja na uwazi wa haki na dalili Zake walikataa washirikina isipokuwa ni kuikanusha Dini ya Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Lau nyinyi mnamiliki hazina za rehema ya Mola wangu ambazo hazimaliziki wala hazitoeki, basi mungalizifanyia ubahili msitoe katika hizo kuwapa wengine kwa kuchelea zisimalizike mkawa mafukara.» Na ni katika tabia ya binadamu kuwa yeye ni mgumu wa kile kilicho mkononi mwake, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu.
Na hakika tulimpa Mūsā miujiza tisa iliyo waziwazi, yenye kutolea ushahidi wa ukweli wa unabii wake, nayo ni fimbo, mkono, ukame, upungufu wa matunda, mafuriko, nzige, chawa, vyura na damu. Basi waulize Mayahudi, ewe Mtume, suala la kuthibitisha, pale Mūsā alipowajia mababu zao na miujiza iliyo wazi, Fir'awn akasema kumwambia Mūsā, «Mimi nadhani, ewe Mūsā, kwamba wewe ni mchawi uliodanganywa na kutekwa akili yako kwa vitendo hivyo vya ajabu unavyovileta.»
Mūsā akamjibu, «Umeshajua kwa yakini, ewe Fir'awn, kwamba hakuiteremsha miujiza hiyo tisa yenye kuutolea ishahidi unabii wangu isipokuwa Mola wa mbingu na ardhi, ipate kuwa ni dalili ambazo wenye busara watazitumia kuonyesha upweke wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika uola Wake na uungu Wake, na mimi nina yakini kwamaba wewe, ewe Fir'awn, ni mwenye kuangamia, kulaaniwa na kushindwa.»
Hapo Fir'awn akataka kumbabaisha Mūsā na kumtoa pamoja na Wana wa Isrāīl kwenye ardhi ya Misri, tukamuanagamiza baharini yeye na askari waliokuwa pamoja na yeye kwa kuwatesa.
Na tukasema, baada ya kuangamia Fir’awn na askari wake, kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Kaeni ardhi ya Sham. Na itakapo kuja Siku ya Kiyama, tutawaleta nyote kutoka makaburini mwenu kufika kwenye kisimamo cha kuhesabiwa.»
Na tumemteremshia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, hii Qur’ani ili kuwaamrisha waja, kuwakataza, kuwalipa mema na kuwaadhibu; na imeteremka kwa ukweli, uadilifu na utunzi isibadilishwe na isigeuzwe. Na hatukukutumiliza wewe, ewe Mtume, isipokuwa ni uwabashirie Pepo waliotii na uwatishe na Moto walioasi na kukanusha.
Na tumekuteremshia, ewe Mtume, Qur’ani tuliyoieleza, tukaipanga na kuifafanua ikawa ni yenye kutenganisha baina ya uongofu na upotevu na ukweli na ubatilifu, ili upate kuwasomea watu kwa umakinifu na upole; na tumeiteremsha mafungu-mafungu kidogo-kidogo kulingana na matukio ya wakati na mahitaji yake.
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji, «Iaminini Qur’ani au msiiamini, kwani kuiamini kwenu hakuiongezei ukamilifu, na kuikanusha kwenu hakuifanyi iwe na upungufu, kwani wanavyuoni waliopewa Vitabu vilivyotangulia kabla ya Qur’ani na wakajua uhakika wa wahyi, wanaposomewa Qur’ani wananyenyekea na wanamsujudia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa nyuso zao kwa kumtukuza na kwa kumshukuru.
Na wanasema, hawa waliopewa ujuzi, wanapoisikia Qur’ani, «Kuepukana na kutakasika ni kwa Mola wetu na kila sifa wanazompa washirikina; halikuwa agizo la Mwenyezi Mungu Aliyetukuka isipokuwa ni lenye kutukia kikweli.»
Na hapo hawa wanapomoka hali ya kusujudu kwa nyuso zao, huku wakilia kwa kuathirika na mawaidha ya Qur’ani. Na kule kuisikia Qur’ani na mawaidha yake kunawafanya wazidi kuinyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu na kuunyenyekea uweza Wake mkubwa.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina wa watu wako waliokupinga kutumia kwako neno la Yā Allāh , Yā Raḥmān, katika maombi, «Muombeni Allāh (Mwenyezi Mungu) au muombeni Raḥmān (Mwingi wa rehema), kwani kwa majina yoyote yake mkimuomba huwa mnamuomba Mola Mmoja, kwa kuwa majina Yake yote ni mazuri. Wala usidhihirishe kisomo katika Swala yako wakakusikia washirikina, wala usisome kwa siri wasikusikie masahaba zako, na uwe kati na kati baina ya kudhihirisha na kusirisha.»
Na useme, «Shukrani zote ni za Mwenyezi Mungu, ukamilifu na sifa njema ni Zake, Aliyeepukana na mwana na mshirika katika uungu Wake. Na Mwenyezi Mungu Hana msaidizi yoyote kati ya viumbe vyake, Yeye Ndiye Mkwasi na Ndiye Mwenye nguvu., na wao ndio mafukara wanaomhitajia.» Na umtukuze matukuzo yaliyotimu, kwa kumsifu, kumuabudu Peke Yake bila ya mshirika, na kumtakasia Dini yote.»
Icon