ﰡ
Ni kubwa mno baraka za Mwenyezi Mungu na ni mengi sana mema Yake na ni kamilifu sifa Zake, Aliyetakasika na kutukuka, Ambaye Ameiteremsha Qur’ani, yenye kupambanua baina ya ukweli na ubatilifu, kwa mja Wake Muhammad, rehemea ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ili awe ni mjumbe kwa binadamu na majini na awe muonyaji wa adhabu ya Mwenyezi Mungu kwao.
Ambaye Ana ufalme wa mbingu na ardhi, Hakujifanyia mtoto na hakuwa na mshirika katika ufalme Wake. Na Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu, Akakisawazisha kulingana na umbo linalonasibiana nacho na inavyotakikana kulingana na hekima Yake, pasi na kupungua wala kwenda kombo.
Na washirikina wa kiarabu walitengeneza waungu, wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Waungu hao hawawezi kuumba chochote, na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyewaumba wao na wenye kuwaabudu, wala hawana uwezo wa kuzuia madhara wala kujiletea manufaa, wala hawawezi kukifisha kilicho hai wala kukihuisha kilichokufa au kumfufua yoyote, miongoni mwa wafu, akiwa hai kutoka kaburini mwake.
Na wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu walisema kwamba hii Qur’ani ni urongo tu na ni uzushi uliofanywa na Muhammad na akasaidiwa na watu wengine. Kwa hakika wamefanya udhalimu mbaya sana na wameleta uzushi wenye kuchukiza, kwani Qur’ani haikuwa inamkinika kwa binadamu yoyote kuizua.
Na walisema kuhusu Qur’ani, «Hiyo ni hadithi za wakale katika vitabu vyao, na Muhammad amezinakili. Basi hizo anasomewa asubuhi na jioni,»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwa hakika Aliyeiteremsha Qur’ani ni Mwenyezi Mungu Ambaye ujuzi Wake umevizunguka vilivyoko mbinguni na ardhini. Kwa hakika Yeye ni Msamehefu sana kwa waliotubia kutokana na madhambi na maasia, ni Mwenye huruma kwao kwa kuwa hakufanya haraka ya kuwatesa.»
Na walisema washirikina, «Ana nini huyu anayedai kwamba yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (wakimkusudia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie), anakula chakula kama sisi na aenda sokoni kutafuta riziki? Basi si angalimtuma Malaika awe naye ashuhudilie ukweli wake,
au imshukie kutoka mbinguni kanzi ya mali, au awe na shamba kubwa ambalo yeye anakula matunda yake.» Na wakaendelea kusema, hawa madhalimu wenye kukanusha, «Mumfuatao nyinyi si mwingine isipokuwa ni mtu aliyefanyiwa uchawi ulioathiri akili yake.»
Tazama, ewe Mtume, namna walivyosema, hawa wakanushaji, juu yako maneno hayo ya ajabu yanayofanana na mifano kwa ugeni wake, ili wafikie kukukanusha, kwa hivyo wakawa mbali na haki, na kwa hivyo hawapati njia ya kuifikia (hiyo haki) ili wayarakibishe maneno waliyoyasema kuhusu wewe, ya urongo na uzushi.
Ni kubwa mno baraka za Mwenyezi Mungu, na ni mengi sana mema Yake, Ambaye Akitaka Atakufanyia mema zaidi kuliko yale waliotamani uwe nayo, Angalikufanyia, ulimwenguni, mashamba mengi ambayo kati yake inapita mito, na Akufanye uwe na majumba makubwa ya fahari.
Na hawakukanusha, kwa kuwa unakula chakula na unaenda sokoni, lakini wameikanusha Siku ya Kiyama na malipo yake yaliyoko. Na tumewatayarishia waliokikanusha Kiyama Moto mkali, watachomwa nao.
Moto huo ukiwaona hawa wakanushaji Siku ya Kiyama, kutoka mahali mbali, watasikia sauti ya kuchemka kwake na mkoromo wake kwa ukali wa hasira zake kwao.
Na pindi wakitupwa kutoka mahali pembamba sana pa moto wa Jahanamu, ikiwa mikono yao imeshikanishwa na minyonyoro kwenye shingo zao, hapo watajiapiza kuangamia ili wajiokoe nayo.
Hapo wataambiwa kwa kukatishwa tamaa, leo msjiiombee maangamivu mara moja, lakini jiombeeni mara nyingi, kwani hilo halitawaongezea isipokuwa makero, hakuna maokozi kwenu.
Sema uwaambie, ewe Mtume, «Je, Moto huu mliosifiwa ni bora au ni Pepo ya neema za milele walioahidiwa wenye kuiogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu, ambayo itakuwa yao ikiwa ni malipo ya matendo yao na ni mahali watakapoishia huko Akhera?
Hawa wenye utiifu watavipata wanavyovitamani vya ladha za neema, starehe yao humo ni ya daima, na kuingia kwao humo ilikuwa ni ahadi ya Mola wako, ewe Mtume, yenye kuombwa, kwa kuwa waja wema wa Mwenyezi Mungu wanamuomba (hiyo Pepo). Na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake.
Na Siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu Atawakusanya washirikina na vile ambavyo walikuwa wakiviabudu badala Yake. Hapo awaambie waabudiwa, «Je, ni nyinyi mliowapoteza njia ya haki waja wangu hawa, au ni wao wenyewe waliopotea njia wakawaabudu nyinyi?»
Hapo waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu watasema, «Kutakasika ni kwako, ewe Mola wetu! Tunajiepusha na kitendo walichokifanya hawa. Haipasii kwetu sisi kuwategemea wasaidizi wa kutusaidia isipokuwa wewe. Lakini wewe uliwasterehesha hawa washirikina na baba zao kwa mali na afya nzuri, mpaka wakasahau utajo wako wakakushirikisha, na wakawa ni watu walioangamia walioghilibiwa na ubaya na hizaya.»
Hapo waambiwe washirikina, «Kwa kweli, wamewakanusha nyinyi, hawa mliowaabudu kwenye madai yenu juu yao. Enyi hawa, nyinyi hamuwezi kuzikinga nafsi zenu na adhabu wala kuziokoa. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, akajidhulumu nafsi yake, akamuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu na akafa katika hali hiyo, mwenyezi Mungu Atamuadhibu adhabu kali.
Na hatukumtumiliza yoyote kabla yako, ewe Mtume, miongoni mwa Mitume wetu, isipokuwa walikuwa binadamu, wanaokula chakula na wanaoenda sokoni. Na tumewafanya baadhi yenu, enyi watu, ni maonjo na mtihani kwa wengine, kwa uongofu na upotevu, utajiri na umasikini, uzima na ugonjwa. Basi je, mtavumilia msimame imara juu ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewalazimisha nayo na mumshukuru ili Mola wenu awape malipo mema au hamtavumilia mustahili kuteswa? Na Mola wako, ewe Mtume, Anamuona anayepapatika au anayevumilia, na anayekanusha au anayeshukuru.
Na walisema wale ambao hawatarajii kukutana na Mola wao baada ya kufa kwao kwa kuwa wanamkanusha, «Si angalau tuteremshiwe Malaika watueleze kwamba Muhammad ni mkweli au tumuone Mola wetu waziwazi Atuelezee habari ya ukweli wake juu ya utume wake.» Kwa kweli wamejiona nafsi zao na wamefanya kiburi kwa kuwa wamefanya ujasiri kusema hili na wamepita mpaka katika ujeuri wao na ukafiri wao.
Siku watakapowaona Malaika wakati wa kufa kwao, na wakiwa ndani ya makaburi yao na Siku ya Kiyama, kwa sura ambazo sizo zile walizozitaka, sio kuwapa bishara ya Pepo, lakini kuwaambia, «Mwenyezi Mungu Ameifanya Pepo ni mahali palipoharamishwa kwenu.»
Hapo tutayaleta yale waliyoyafanya yanayoonekana kuwa ni mazuri na ya kidini, tuyafanye ni yenye kubatilika na kupotea. Hayatawanufaisha na yatakuwa ni kama vumbi linalorushwa, nalo ni lile vumbi lembamba linaloonekana kwenye mwangaza wa jua. Hivyo ni kwamba matendo mema hayawi na manufaa yoyote huko Akhera isipokuwa mwenye kuyafanya awe na imani ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumtakasia na kumfuata Mtume Wake Muhammd, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Watu wa Peponi, Siku ya Kiyama, watakuwa na mahali pa kutulia bora zaidi kuliko watu wa Motoni, na watakuwa na mashukio mazuri kabisa. Raha yao imekamilika na starehe yao haitatangamana na chochote kile chenye kuharibu.
Ikumbuke, ewe Mtume, Siku hiyo ambayo mbingu zitapasuka-pasuka, na katika mwanya wa pasuko hizo yajitokeza mawingu meupe yaliyo membamba, na Siku hiyo Mwenyezi Mungu Awateremshe Malaika wa mbinguni wawazunguke viumbe katika Mkusanyiko, na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Aje kufanya uamuzi baina ya waja kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake.
Mamlaka ya kikweli katika Siku hii ni ya Mwingi wa rehema Peke Yake bila mwingine. Na Siku hii itakuwa ngumu kwa makafiri kwa mateso yatakayowapata na adhabu kali.
Na ikumbuke, ewe Mtume, Siku ambayo mwenye kujidhulumu nafsi yake ataiuma mikono yake kwa majuto na unguliko kwa kusema, «Laiti mimi niliandamana na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na nikamfuata katika kuufanya Uislamu kuwa ni njia ya Peponi,»
na atasema kwa maunguliko, «Laiti mimi sikumfanya fulani kuwa ni rafiki wa kumfuata na kumpenda.
Amenipoteza rafiki huyu na kuniepusha na Qur’ani baada ya kunijia» Na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu amekuwa daima ni mwenye kumtupa mwanadamu. Katika aya hizi kuna onyo kwamba rafiki mbaya asifuatwe, kwani yeye huenda akawa ni sababu ya kumtia, yule anayefuatana na yeye, Motoni.
Na Mtume atasema akishtakia matendo ya watu wake, «Ewe Mola wangu! Kwa kweli watu wangu wameiacha hii Qur’ani na wameigura, wameendelea sana katika kuipa mgongo na kuacha kuizingatia na kuitumia na kuifikisha. Katika aya hii pana kitisho kikubwa kwa anayeigura Qur’ani na asiitumie.
Na kama tulivyokufanya, ewe Mtume, uwe na maadui miongoni mwa wahalifu watu wako, tulimfanya kila Nabii, miongoni mwa Manabii, awe na adui kati ya wale wahalifu wa watu wake. Basi vumilia kama walivyovumilia. Na inatosha kuwa Mola wako ni Mwenye kuongoa, ni Mwenye kuilekeza, ni Mwenye kuonyesha njia na ni Mwenye kutoa msaada wa kukusaidia wewe dhidi ya maadui zako.Katika haya pana maliwazo kwa Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye.
Na Waliokanusha walisema, «Si hii Qur’ani ateremshiwe Muhammad kwa mara moja» kama ilivyokuwa Taurati, Injili na Zaburi? Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Akasema «Tumeiteremsha ikiwa hivyo, sehemu-sehemu, ili kuutia nguvu moyo wako na ili wewe uzidi utulivu, upate kuielewa na kuibeba, na tumeifunua wazi kwa kuithibitisha na kwa kuileta polepole.»
Na hawakujii, ewe Mtume, hawa washirikina na hoja yoyote au utata wowote isipokuwa tutakuletea majibu ya ukweli na ufafanuzi wake mzuri zaidi.
Hao makafiri ndio watakaoburutwa kwa nyuso zao hadi kwenye Moto wa Jahanamu. Hao ndio wenye mashukio mabaya kabisa miongoni mwa watu na ndio walioko mbali kabisa na njia ya haki.
Na kwa hakika, tulimpelekea Mūsā Taurati, tukamfanya ndugu yake Hārūn kuwa ni msaidizi wake
na tukawaambia wao wawili,»Endeni kwa Fir’awn na watu wake waliozikanusha dalili za uola[7] wetu na uungu wetu.» Basi wakawaendea na wakawalingania wamuamini Mwenyezi Mungu, wamtii na wasimshirikishe. Wakawakanusha, na kwa hivyo tukawaangamiza maangamivu makubwa.
____________________
[7]Dalili ya uola wa Mwenyezi Mungu ni dalili ya kuwa yeye Ndiye Mola
Na tuliwazamisha watu wa Nūḥ kwa mafuriko walipomkanusha. Na mwenye kumkanusha Mtume yoyote huwa amewakanusha Mitume wote. Na tulikufanya kule kuwazamisha ni mazingatio kwa watu. Na tutawapatia wao na wale waliofuata njia yao katika kukanusha, Siku ya Kiyama, adhabu yenye kuumiza.
Na tuliwaangamiza hao ‘Ād, watu wa Hūd, na Thamūd, watu wa Ṣāliḥ, na watu wa Kisimani na watu wengine wengi waliokuwako baina ya watu wa Nūḥ, kina ‘Ād, kina Thamūd na watu wa Rass(hapo kisimani) hakuna awajuao isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Na ummah wote hao tuliwabainishia hoja na kuwafafanulia dalili na tukawaondolea nyudhuru (za kutojua). Pamoja na hivyo, hawakuamini, na kwa ajili hiyo tuliwapa maangamivu kwa kuwaadhibu.
Na washirikina wa Makkah walikuwa wakikipitia kijiji cha watu wa Lūṭ katika safari zao, nacho ni kijiji cha Sadūm ambacho kiliangamizwa kwa mawe kutoka mbinguni, wasizingatie kwa hilo, bali walikuwa hawatazamii kuwa kuna marejeo Siku ya Kiyama ambapo wao watalipwa.
Na wakuonapo hao wakanushaji, ewe Mtume, wanakufanyia shere wakisema, «Je, ni huyu yule anayedai kwamba Mwenyezi Mungu Amemtumiliza kuwa ni mjumbe kwetu?
Yeye amekaribia kutuepusha na kuwaabudu masanamu wetu kwa hoja zake za nguvu na ufasaha wake, lau hatungalisimama imara juu ya kuwaabudu.» Na watajuwa, watakapoiona adhabu wanayoistahili, ni nani aliyepotoka zaidi kidini: ni wao au ni Muhammad?
Mwangalie, ewe Mtume, kwa kumuonea ajabu yule aliyeyatii matamanio yake kama kumtii Mwenyezi Mungu. Je, wewe utakuwa ni mwenye kumtunza mpaka umrudishe kwenye Imani?
Au unadhani kwamba wengi wao wanazisikia aya za Mwenyezi Mungu, kusikia kwa kuzingatia, au wanayaelewa yaliyomo ndani yake? Hawakuwa isipokuwa ni kama wanyama, katika kutonufaika kwa wanayoyasikia, bali wao wamepotea njia zaidi kuliko hao wanyama.
Kwani huoni vipi Mwenyezi Mungu Alivyokinyosha kivuli kuanzia kutokea alfajiri mpaka kutokea jua? Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka Angalikifanya kisimame na kitulie, kisiondolewe na jua kisha tungalilifanya jua kuwa ni alama ambayo kwa hali zake inachukuliwa dalili ya hali za kivuli.
Kisha kivuli kinapotea kidogo- kidogo, kila kunapoongezeka kupaa juu kwa jua ndipo kunapoongezeka kupungua kwake. Hilo ni miongoni mwa dalili za uweza wa Mwenyezi Mungu, ukubwa Wake na kwamba Yeye Peke Yake Ndiye Anayestahiki kuabudiwa, si mwengine.
Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyewawekea usiku kuwa ni wenye kuwasitiri nyinyi kwa giza lake, kama vile mavazi yanavyowasitiri. Na Amewawekea usingizi kuwa ni raha ya miili yenu, ndani yake mnatulia na mnapumzika. Na Amewawekea mchana ili mtapakae kwenye ardhi na mtafute maisha yenu.
Na Yeye Ndiye Aliyezituma pepo zinazobeba mawingu, zenye kuwabashiria watu mvua ikiwa ni rehema kutoka Kwake; na tumeyateremsha kutoka mbinguni maji ya kujisafisha nayo,
ili tutoe kwayo mimea mahali pasipo na mimea, ipate kuhuika ardhi ya ukame baada ya kuwa imekufa (kwa ukavu), na ili tuwanyweshe maji hayo wanyama howa na watu miongoni mwa viumbe vyetu vyingi.
Na hakika tunateremsha mvua juu ya sehemu ya ardhi bila ya nyingine, ili wale walioteremshiwa mvua wapate kukumbuka neema ya Mwenyezi Mungu juu yao na wamshukuru, na ili wale walionyimwa mvua wafanye haraka kutubia kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Apate kuwarehemu wao na kuwanywesha. Lakini wengi wa watu wanakataa isipokuwa ni kukanusha neema zetu juu yao, kama neno lao wanalolisema, «tumeletewa mvua kwa sababu ya nyota kadha na kadha.»
Na lau tungalitaka tungalimpeleka muonyaji katika kila mji, wa kuwalingania wao kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na kuwaonya wao adhabu Yake. Lakini tumekufanya wewe, ewe Mtume, ni mwenye kupelekwa kwa watu wote wa ardhini, na tumekuamrisha wewe uwafikishie hii Qur’ani.
Basi usiwatii makafiri kwa kuacha kitu chochote kile ambacho umetumilizwa nacho. Lakini fanya bidii yako katika kuufikisha ujumbe na upigane jihadi na wenye kuikanusha hii Qur’ani, kupigana jihadi kukubwa kusikochanganyika na udhaifu.
Na Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyezichanganya bahari mbili: ya tamu yenye ladha nzuri, na ya chumvi yenye uchumvi mwingi, na Akaweka baina ya hizo mbili kizuizi chenye kuzuia kila mojawapo ya hizo isiiharibu nyingine na pingamizi ili mojawapo isiifikie nyingine.
Na Yeye Ndiye Aliyeumba kizazi cha kiume na kike kutokamana na manii ya mwanamume, na kutokana na hayo ukapatikana ujamaa wa kinasaba na ujamaa wa ukwe. Na Mola wako ni Mwenye uweza wa kuumba Anachotaka.
Na pamoja na dalili hizi za uweza wa Mwenyezi Mungu na wema Wake kwa viumbe Wake, makafiri wanaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, kitu ambacho hakiwanufaishi wakikiabudu wala hakiwadhuru wakiacha kukiabudu. Na kafiri ni msaidizi wa Shetani juu ya Mola wake, kwa kufanya ushirikina katika ibada ya Mwenyezi Mungu, na ni mwenye kumpa nguvu huyo Shetani juu kumuasi Mwenyezi Mungu.
Na hatukukutumiliza wewe, ewe Mtume, isipokuwa uwe ni mwenye kuwabashiria Waumini Pepo na mwenye kuwaonya makafiri na Moto.
Waambie, «Sitaki kutoka kwenu, kwa kufikisha ujumbe, malipo yoyote. Lakini mwenye kutaka kuongoka na kufuata njia ya haki inayompeleka kwa Mola wake na kutumia katika mambo Anayoyaridhia, mimi sitawalazimisha hilo, isipokuwa hilo, kwa kweli, ni bora kwa maslahi ya nafsi zenu.»
Na jitegemeze kwa Mwenyezi Mungu Ambaye Ana uhai uliokamilika kwa namna zote, kama inavyonasibiana na utukufu Wake, Ambaye hafi, na umtakase na sifa za upungufu. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa madhambi ya viumbe Vyake. Hakuna chochote kinachofichika Kwake katika hayo. Na Atawahesabia na Atawalipa kwa hayo.
Aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa Siku sita, kisha akalingana juu ya '“Arsh - yaani Akawa juu na Akaangatika- kulingana kunakonasibiana na utisho Wake, Yeye Ndiye Mwingi wa rehema. Basi muulize, ewe Mtume, Mtambuzi kuhusu Yeye. Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, Anajikusudia Mwenyewe Aliyetukuka, kwani Yeye Ndiye Anayejua sifa Zake, ukuu Wake na utukufu Wake. Na hakuna yoyote, katika binadamu, anayemjua zaidi Mwenyezi Mungu wala anayetambua habari Zake zaidi kuliko mja Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye.
Na wakiambiwa makafiri, «Msujudieni Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema) na muabuduni,» wanasema, «Hatumjui Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema). Je, tukisujudie kila unachotuamrisha kukisujudia kwa kutii amri yako?» Basi hilo la kuwaita wao kumsujudia Al-Raḥmān (Mwingi wa rehema) linawaongezea wao kuikimbia imani na kuwa mbali nayo.
Ni kubwa baraka za Mwingi wa rehema na ni nyingi kheri Zake Aliyeziweka mbinguni nyota kubwa pamoja njia zake, na akaliweka, katika hizo mbingu, jua linalotoa mwangaza na mwezi unaong’ara.
Na Yeye Ndiye Aliyefanya usiku na mchana vipishane, kimoja baada ya kingine, kwa anayetaka kuzingatia hilo kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, Mpelekeshaji mambo na Muumbaji au anayetaka kumshukuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa neema Zake na mema Yake.
Na waja wa Mwingi wa rehema walio wema ni wale ambao wanatembea juu ya ardhi kwa utulivu wakiwa wanyenyekevu; na wajinga mafidhuli wanaposema nao maneno ya kuwaudhi wanawapa majibu mazuri na wanasema nao maneno ya kuwafanya wasalimike na dhambi na (pia wasalimike na) kukabiliana na mjinga kwa ujinga wake.
Na ambao wanaswali usiku kwa wingi wakimtakasia Mola wao wakiwa ndani ya Swala na wakijidhalilisha Kwake kwa kusujudu na kusimama.
Na ambao, pamoja na kujibidiisha kufanya ibada, wanamuogopa Mola wao na kwa hivyo wanamuomba Awaokoe na adhabu ya Jahanamu, kwani adhabu yake inalazimiana na muadhibiwa.
Kwa hakika moto wa Jahanamu ni mahali pabaya pa kutulia na kukaa.
Na ambao wakitumia mali zao hawapitishi kipimo katika kutoa wala hawabani katika matumizi, na kutumia kwao huwa kuko kati na kati baina ya kupitisha kipimo na kubana.
Na ambao wanampwekesha Mwenyezi Mungu na hawamuombi wala kumuabudu mola asiyekuwa Yeye, wala hawaiui nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa isipokuwa kwa kitu kinachopasisha kuuawa, kama vile kukufuru baada ya kuamini au kuzini baada ya ndoa au kumuua mtu kwa uadui, wala hawazini bali wanazihifadhi tupu zao isipokuwa kwa wake zao au wale ambao mikono yao ya kulia imemiliki. Na mwenye kuyafanya madhambi haya makubwa atakuta mateso huko Akhera.
Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Kiyama na ataketi milele akiwa mdhalilifu mnyonge. Onyo la kukaa milele ni kwa wale wanaoyafanya yote hayo au ni kwa yule aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu.
Lakini mwenye kutubia kutokana na madhambi haya toba ya dhati na akaamini imani ya kukata yenye kuambatana na matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu Atawafutia makosa yao na Atawaweka mahali Pake mema, kwa sababu ya kutubia kwao na kujuta kwao. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia, ni Mwingi wa rehema kwa waja Wake kwa kuwa Amewaita watubie baada ya kushindana na Yeye kwa kufanya maasia makubwa kabisa.
Na yoyote anayetubia kwa madhambi aliyoyafanya na akafanya matendo mema, basi yeye, kwa hilo, atakuwa amerudi kwa Mwenyezi Mungu kisawasawa, na hapo Mwenyezi Mungu Ataikubali toba yake na Atazifuta dhambi zake.
Na ambao hawatoi ushahidi wa urongo wala hawahudhurii vikao vyake, na wapitapo kwa watu wa ubatilifu na ulaghai bila ya kukusudia wanapita hali ya kupa mgongo na kupinga, wanajiepusha nao (huo ubatilifu na ulaghai) na hawauridhii kwa wengine.
Na ambao wakipewa mawaidha kwa aya za Qur’ani na dalili za upweke wa Mwenyezi Mungu hawajighafilishi nazo wakawa kama ambao ni viziwi hawakuzisikia na vipofu hawakuziona, lakini nyoyo zao zinazielewa na akili zao zinafunguka kuzikubali, na basi hapo wanajipomosha kwa Mwenyezi Mungu hali ya kusujudu na kutii.
Na ambao wanamuomba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wakisema, «Mola wetu! Tutunukie miongoni mwa wake zetu na wana wetu cha kutuliza macho yetu na chenye maliwazo na furaha kwetu, na utufanye ni kiigizo chema kwa wachamungu kutuiga.»
Hao waja wa Mwingi wa rehema, waliosifika kwa sifa zilizopita, watalipwa majumba ya Peponi ya juu kabisa, kwa rehema ya Mwenyezi Mungu na kwa sababu ya uvumilivu wao juu ya kufanya matendo ya utiifu, na watalakiwa humo Peponi kwa maamkizi na salamu kutoka kwa Malaika, na watakuta maisha mema na kusalimika na maafa,
hali ya kukaa milele humo bila ya kufa. Ni nzuri mno hiyo Pepo kuwa ni mahali pa wao kutulia na makao ya wao kukaa, hawatataka kuondoka hapo.
Mwenyezi Mungu Anatoa habari kuwa Yeye hawajali watu wala hashughuliki nao lau si wao kumlingania Yeye ulinganizi wa ibada na ulinganizi wa maombi. Hakika yenu nyinyi, enyi makafiri, mumekanusha, na ukanushaji wenu utapelekea mupate adhabu yenye kuwa na nyinyi kama vile mwenye kudai anavyokuwa na mdaiwa wake, na Atawaangamiza duniani na Akhera.