ترجمة سورة ص

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة ص باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

«Ṣād» Yametangulia maelezo kuhusu herufi zilizotengwa na kukatwa mwanzoni mwa sura ya Al-Baqarah.
Anaapa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, kwa Qur’ani inayokusanya ukumbushaji kwa watu kwa yale ambayo wao wameghafilika nayo. Lakini makafiri wanaifanyia kiburi haki na wanaenda kinyume nayo.
Kuna ummah wengi tuliowaangamiza kabla ya hawa washirikina, wakaomba waokolewe na wakaita kutaka toba, na wakati si wakati wa kukubaliwa toba wala wakati wa kukimbia na kuokolewa na yaliyowapata.
Na wameona ajabu washirikina hawa kuwa Mwenyezi Mungu Amewatumia binadamu miongoni mwao awalinganie kwa Mwenyezi Mungu na awaogopeshe adhabu Yake na wakasema, «Hakika yeye si Mtume bali yeye ni mrongo katika maneno yake, anawafanyia uchawi watu wake.
Ni vipi atawafanya waungu wengi kuwa ni mungu mmoja? Hili alilolileta na akalingania kwalo ni jambo la ajabu.
Wakatoka viongozi wa watu na wakubwa wao wakiwahimiza watu wao kuendelea kwenye ushirikina na kuvumilia juu ya waungu wengi, «Hili alilokuja nalo huyu Mtume ni jambo la kupangwa, lengo lake ni uongozi na ukubwa.
Hatujasikia hili analolingania katika dini ya baba zetu wa Kikureshi wala katika Unaswara; halikuwa hili isipokuwa ni urongo na uzushi.
«Je, amehusishwa Muhammad peke yake kwa kuteremshiwa Qur’ani bila ya sisi?» Bali wao wako kwenye shaka ya kuwa mimi nimekuletea wahyi wewe, ewe Mtume, na kukupa utume. Bali wao walisema hilo kwa kuwa hawajaonja adhabu ya Mwenyezi Mungu, na lau wangaliionja adhabu hawangalithubutu kusema waliyosema.
Au kwani wao wanamiliki mahazina ya fadhila za Mola wako, Aliye Mshindi katika ufalme Wake, Aliye Mpaji wa Anachokitaka miongoni mwa riziki Yake na fadhila Zake kwa Anayemtaka miongoni mwa viumbe Vyake?
Au kwani washirikina hawa wana mamlaka ya mbinguni na ardhini na vilivyoko baina ya viwili hivyo, hivyo basi wakatoa na kuzuia? Basi wazishikilie kamba zenye kuwafikisha mbinguni wapate kutoa uamuzi wanaoutaka wa kutoa na kuzuia.
Askari hawa wanaokanusha ni askari wenye kushindwa, kama walivyoshindwa wengineo miongoni mwa mapote ya watu waliokuwa kabla yao.
Walikanusha kabla yao watu wa Nūḥ, 'Ād, Fir'awn mwenye nguvu kubwa,
Thamūd, watu wa Lūṭ, watu wa miti na mabustani nao ni watu wa Shu'ayb. Hao ndio ummah walioshirikiana wakawa pote moja juu ya ukafiri na ukanushaji na wakajikusanya juu yake.
Hakuna watu wa pote lolote kati ya hawa isipokuwa walikanusha Mitume na kwa hivyo wakastahiki kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu na yakawashukia wao mateso Yake.
Na hawangojei washirikina hawa, ili adhabu iwashukie wakisalia kwenye ushirikina wao, isipokuwa Mvuvio mmoja ambao hauna kurudi.
Na wanasema, «Mola wetu! Tuharakishie sehemu yetu ya adhabu duniani kabla ya Siku ya Kiyama.» Kusema huku kulikuwa ni uchezaji shere kutoka kwao.
Vumilia, ewe Mtume, kwa unayoyachukia katika hayo wanayoyasema, na umtaje mja wetu Dāwūd, mwenye nguvu juu ya maadui wa Mwenyezi Mungu na uvumilivu juu ya kumtii Yeye. Hakika yeye ni mwingi wa kutubia, ni mwingi wa kurejea kufanya yale yanayomridhisha Mwenyezi Mungu. Katika haya pana kumliwaza Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Hakika sisi tuliyadhalilisha majabali pamoja na Dāwūd, yakawa yanamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumsabihi wakati anapomtakasa kwa kumsabihi mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Na tukawadhalilisha ndege pamoja naye, kwa mkusanyiko wao, wakawa wanatakasa kwa kusabihi na kuwa watiifu kwake
Tukamtilia nguvu ufalme wake kwa haiba, uwezo na ushindi, na tukampa unabii na upambanuzi wa maneno na utoaji hukumu.
Na je, ilikujia, ewe Mtume, habari ya watesi wawili walioparaga ukuta wakamuingilia Dāwūd mahali pake pa kuabudu.
Na Dāwūd akashutuka kwa wao kumuingilia? Walimwambia, «Usiogope! Sisi ni watesi, mmoja wetu amemdhulumu mwenzake. Basi hukumu baina yetu kwa uadilifu, wala usitoe hukumu ya maonevu juu yetu, na utuongoze kwenye njia ya sawa.»
Mmoja wa wale wawili alisema, «Huyu ni ndugu yangu; ana kondoo tisini na tisa na mimi sina isipokuwa kondoo mmoja, akafanya tamaa kumtaka na akasema, ‘Nipe mimi!’ Na akanishinda kwa hoja.»
Dāwūd akasema, «Kwa hakika ndugu yako amekudhulumu kwa kutaka kwake kumchukua kondoo wako awe pamoja na kondoo wake. Na kwa hakika, wengi wa washirika, baadhi yao wanadhulumu wengine: wanawadhulumu kwa kuchukua haki zao na kukosa kuwa waadilifu wa nafsi zao. Isipokuwa watu wema walioamini, kwani wao hawadhulumiani, nao ni wachache.» Na Dāwūd akajua kwa yakini kuwa sisi tumemtahini kwa utesi huu, hivyo basi akamuomba msamaha Mola wake, akasujudu kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na akarejea Kwake na akatubia.
Tukamsamehe hilo na tukamfanya ni miongoni mwa watu waliosogezwa karibu na sisi, na tumemuandalia mwisho mwema huko Akhera.
Ewe Dāwūd! Sisi tumekufanya ni msimamizi ardhini na tumekupa mamlaka huko, basi hukumu baina ya watu kwa uadilifu na uchungaji haki, na usifuate matamanio katika kuhukumu, kwani hilo litakupotosha na Dini ya Mwenyezi Mungu na Sheria Yake, hakika wale wanaopotea njia ya Mwenyezi Mungu watapata adhabu ya uchungu humo Motoni, kwa kughafilika kwao na Siku ya kulipwa na kuhesabiwa. Katika haya pana ushauri kwa viongozi wahukumu kwa haki iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, wala wasipotoke nayo wakapotea njia Yake.
Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa upuuzi na mchezo. Hiyo ndiyo dhana ya waliokufuru. Basi ole wao na Moto wa Siku ya Kiyama, kwa dhana yao ya ubatilifu na ukanushaji wao Mwenyezi Mungu.
Je, tuwafanye walioamini wakafanya matendo mema ni kama waharibifu kwenye ardhi? Au je, tuwafanye wachamungu wenye kuamini ni kama waharibifu waliokufuru? Kusawazisha huku hakulingani na hekima ya Mwenyezi Mungu na hukumu yak, kwani hao hawalingani kwa Mwenyezi Mungu. Bali Mwenyezi Mungu Atawalipa wachamungu malipo mema na Atawatesa waharibifu walio waovu.
Hiki ulicholetewa kwa njia ya wahyi, ewe Mtume, ni Kitabu tulichokuteremshia kilichobarikiwa, ili wafikirie juu ya aya zake na wazitumie njia zake za uongofu na ishara zake njema, na ili wapate kukumbuka watu wenye akili timamu yale Aliyowalazimisha Mwenyezi Mungu.
Na tulimtunukia Dāwūd mwanawe Sulaymān, tukamneemesha yeye (Dāwūd) kwa kumpa Sulyman, na tukamtuliza jicho lake kwake. Neema ya mja ni Sulaymān. Yeye alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu na kutubia Kwake.
Kumbuka pindi walipoorodheshwa mbele yake kipindi cha alasiri farasi wa asili wenye kasi za kukimbia, waliosimama kwa miguu mitatu na kuinua mguu wa nne kwa kuwa ni farasi bora na wapesi. Waliendelea kuorodheshwa mbele yake mpaka jua likachwa.
Akasema, «Mimi nimehiari kupenda farasi kuliko kumtaja Mola wangu mpaka jua likachwa na macho yangu yakawa hayalioni.
Warudisheni hao farasi walioorodheshwa hivi punde.» Wakarudishwa, na akaingia kuipiga miguu yao na shingo zao kwa upanga kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwa wao walikuwa ni sababu ya Swala yake kumpita, Na ilikuwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuchinja farasi yakubaliwa katika Sheria yake.
Hakika tulimpa mtihani Sulaymān na tukamrushia kwenye kiti chake kipande cha mtoto aliyezaliwa katika kipindi alichoapa kuwa atawapitia wake zake na kila mmoja katika wao atamzalia shujaa atakayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na hakuseme «in shāa Allāh» (Mungu Akitaka). Akawapitia wake zake wote, na hakuna hata mmoja katika wao aliyeshika mimba isipokuwa mmoja aliyezaa mtoto nusu. Kisha Sulaymān alirudi kwa Mola Wake, akatubia
na akasema, «Mola wangu! Nisamehe dhambi zangu na unipe ufalme mkubwa unaohusika na mimi ambao mfano wake hautakuwa kwa binadamu yoyote baada yangu. Hakika yako wewe, uliotakasika na kutukuka, ni Mwingi wa upaji na utoaji.
Tukamkubalia maombi yake na tukamdhalilishia upepo ukawa unapita kwa amri yake ukiwa mtiifu kwake, hali ya kuwa na nguvu na kasi, ukielekea pale anapotaka,
Na tukamdhalilishia Mashetani, akawa anawatumia katika kazi zake. Katika wao kulikuwa na wajenzi na wazamiaji baharini.
Na wengine, nao ni waasi wa kijini, walikuwa wamefungwa pingu.
Ufalme huu mkubwa na udhalilishiaji huu wa kipekee ni upaji wetu kwako, ewe Sulaymān, basi mpe unayemtaka na umnyime unayemtaka, hapana hesabu juu yako.
Na hakika Sulaymān kwetu sisi, huko Akhera, atakuwa na ukaribu na marejeo mazuri.
Mkumbuke, ewe Mtume, mja wetu Ayyūb alipomlingania Mola wake kwa kusema, «Shetani amenisababishia tabu, mashaka na maumivu katika mwili wangu, mali yangu na watu wangu!»
Tukamwambia, «Ipige ardhi kwa mguu wako! Yatabubujika kutoka humo maji baridi. Basi kunywa katika maji hayo na uoge, na madhara na maudhiko yatakuondokea.»
Tukamuondolea shida yake na tukamtukuza, na tukamtunukia watu wake :mke na watoto, na tukamuongezea wana na wajukuu mfano wao. Yote hayo yalikuwa ni huruma kutoka kwetu na takrima kwake kwa uvumilivu wake, na pia ni mazingatio kwa wenye akili timamu, wapate kujua kwamba mwisho wa subira ni faraja na kuondokewa na shida.
Na tukamwambia yeye, «chukua kwa mkono wako mrundiko wa nyasi au mfano wake umpige nao mke wako, ili utekeleze yamini lako na usilivunje. Kwani yeye alikuwa ameapa kuwa atampiga mbati mia moja Mwenyezi Mungu Akimponyesha, alipomkasirikia mkewe kwa jambo dogo alipokuwa mgonjwa. Na alikuwa ni mwanamke mwema na Mwenyezi Mungu Akamhurumia yeye na Akamhurumia mumewe kwa uamuzi huu. Hakika sisi tumemkuta Ayyūb ni mvumilivu katika mitihani. Mja bora ni yeye, kwani yeye ni mwingi wa kurudi kwenye utiifu wa Mola wake.
Wakumbuke, ewe Mtume, waja wetu na Manabii wetu: Ibrāhīm, Is’ḥāq na Ya’qūb. Hakika wao ni watu wenye nguvu katika kumtii Mwenyezi Mungu na ujuzi katika Dini Yake.
Sisi tumewahusisha wao kwa jambo kubwa ambalo ni mahsusi kwao, kwa kuwa tumejaalia ukumbusho wa Nyumba ya Akhera uko ndani ya nyoyo zao, na kwa hivyo wakaifanyia kazi kwa kututii sisi na wakawalingania watu kwenye jambo hilo na kuwakumbusha.
Na kwa hakika, wao kwetu sisi ni miongoni mwa wale tuliowachagua ili watutii na tuliowateua kubeba ujumbe wetu.
Wakumbuke, ewe Mtume, waja wetu: Ismā'īl, Ilyasa' na Dhulkifl kwa utajo mzuri sana. Na kila mmoja miongoni mwao ni katika watu wema ambao Mwenyezi Mungu Aliwachagua miongoni mwa viumbe na Akawachagulia hali na sifa kamilifu kabisa.
Hii Qur’ani ni utajo na utukufu kwako, ewe Mtume, na kwa watu wako. Na wale watu wa uchaji Mwenyezi Mungu na utiifu Kwake watakuwa na mwisho mwema kwetu sisi
kwenye Pepo za kukaa daima, milango yake ikiwa tayari imefunguliwa kwa ajili yao,
watakuwa ni wenye kutegemea kwenye Pepo hizo juu ya viti vya fahari vilivyopambwa, watataka na kupatiwa kila wanachokitamani miongoni mwa aina nyingi za matunda na vinywaji, kutokana na kila ambacho nafsi zao zitakitamani na macho yao yatapendezwa nacho.
Na huko watakuwa nao wanawake ambao macho yao yanawatazama waume zao tu hali wakiwa marika na wao kimiaka.
Starehe hii ndiyo ile mliokuwa mkiahidiwa, enyi wachamungu, Siku ya Kiyama.
Hiyo ndiyo riziki yetu tuliyowaandalia nyinyi, haina kumalizika wala kukatika.
Hayo, yaliyotangulia kutajwa sifa zake, ni ya wachamungu. Ama wale wenye kuruka mpaka na kuingia ukafirini na maasi, wao watakuwa na marejeo maovu kabisa na mwisho mbaya sana,
nao ni Moto ambao ndani yake wataadhibiwa, utawafinika pande zao zote, basi tandiko baya mno ni tandiko lao.
Adhabu hii ni maji yaliyo moto sana, na usaha unaotiririka kutoka kwenye miili ya watu wa Motoni, basi na wanywe.
Na wao watakuwa na adhabu nyingine ya namna hii, aina na sampuli mbalimbali.
Na watakapoufikia Moto, hao wenye kupita vipimo katika uasi, watatukanana wao kwa wao na watasema baadhi yao kuwaambia wengine, «Hili ni kundi kubwa la watu wa Motoni ni wenye kuingia pamoja na nyinyi.» Na wao wajibu, «Hawana makaribisho mema wala nyumba zao haziwaenei ndani ya Moto. Wao ni wenye kuungulika kwa joto lake kama tunavyoungulika sisi.»
Hapo kundi la wafuasi litasema kuwaambia wale waliopita vipimo katika uasi, «Bali ni nyinyi msiokaribishwa vyema, kwa kuwa nyinyi ndio mliotusababishia makao ya Motoni kwa kule kutupoteza kwenu duniani, basi ubaya wa nyumba ya mtu kutulia ni Moto wa Jahanamu!»
Na kundi la wafuasi liendelee kusema, «Mola wetu! Yoyote yule aliyetupoteza duniani akatuepusha na uongofu, muongezee adhabu yake Motoni maradufu.»
Na watasema wale waliopita vipimo katika uasi, «Mbona hatuwaoni pamoja na sisi Motoni wale watoto ambao tulikuwa tukiwahesabu duniani kuwa ni miongoni mwa watu waovu wakorofi?
Je, kwani kule kuwadharau kwetu na kuwachezea kulikuwa ni makosa Au wao wako pamoja na sisi Motoni lakini macho yetu bado hayajawaona?»
Kwa hakika, hili la kujadiliana watu wa Motoni na kuteta kwao ni jambo litakalotokea bila shaka.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia watu wako, «Hakika mimi ninawaonya nyinyi na adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwashukie kwa sababu ya kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu, hakuna mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye Peke Yake, Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa ukubwa Wake, majina Yake, sifa Zake na matendo Yake, Mwenye kutendesha nguvu Anayekilazimisha kila kitu na kukishinda.
Mwenye kumiliki mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake, Aliye Mshindi katika kutesa Kwake, Mwingi wa kusamehe dhambi za aliyetubia na kurudi kutafuta radhi Zake.»
Sema, ewe Mtume kuwaambia watu wako, «Kwa hakika hii Qur’ani ni habari yenye manufaa makubwa.
Nyinyi mmeghafilika nayo, mmejiepusha nayo na hamuitumii.
«Mimi sikuwa na ujuzi wa utesi wa Malaika wa mbinguni kuhusu kuumbwa kwa Ādam, lau si Mwenyezi Mungu kunijulisha na kuniletea wahyi kwa hilo.
«Mwenyezi Mungu haniletei wahyi unaokusanya ujuzi wa kitu ambacho sina ujuzi nacho isipokuwa ni kwa kuwa mimi ni muonyaji wenu kutokana na adhabu Yake, ni mwenye kuwabainishia sheria Yake.»
Kumbuka pindi Aliposema Mola wako kuwaambia Malaika, «Hakika mimi nitamuumba kiumbe kutokana na mchanga.
Basi nitakapousawazisha mwili wake na umbo lake na nikapuliza roho ndani yake na uhai ukatambaa humo, msujudieni» sijida ya heshima na kukirimu, na siyo sijida ya ibada na kutukuza. Kwani ibada haiwi isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Na Mwenyezi Mungu Ameharamisha, katika Sheria ya Kiislamu, kusujudu kwa njia ya maamkizi.
Hapo Malaika wote wakasujudu kwa kutii na kufuata amri ya Mwenyezi Mungu,
isipokuwa Iblisi Yeye hakusujudu kwa ujeuri na kiburi, na alikuwa, katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ni miongoni mwa makafiri.
Mwenyezi Mungu Akamwambia Iblisi, «Ni lipi lililokukataza kumsujudia yule niliyemkirimu nikamuumba kwa mikono yangu miwili? Je, umemfanyia kiburi Ādam au umekuwa ni miongoni mwa wale waliomfanyia kiburi Mola wako?» Katika aya hii pana kumthibitishia Mwenyezi Mungu, Mwenye kheri nyingi na kutukuka, sifa ya mikono miwili, kwa namna inayolingana na Yeye, kutakasika ni Kwake.
Iblisi akasema akimpinga Mola wake, «Mimi sikumsujudia kwa kuwa mimi ni bora kuliko Yeye, kwa kuwa umeniumba kwa moto na umemuumba yeye kwa udongo (na moto ni bora kuliko udongo).
Mwenyezi Mungu Akamwambia, «Basi toka peponi! Wewe, kwa neno lako hilo, umefukuzwa, umeepushwa na kulaaniwa.
Na huko kukufukuza kwangu na kukuepusha na mimi kutaendelea mpaka Siku ya Malipo na Hesabu.»
Iblisi akasema, «Mola wangu! ucheleweshe ukomo wa maisha yangu wala usiniangamize mpaka wakati ambapo viumbe watafufuliwa kutoka makaburini mwao».
Mwenyezi Mungu Akasema kumwambia, «Wewe ni miongoni mwa watakaocheleweshwa mpaka Siku ya kipindi maalumu,
nayo ni Siku ya Mvuvio wa Kwanza ambapo viumbe watakufa.»
Iblisi akasema, «Naapa kwa enzi yako, ewe Mola wangu, na utukufu wako! Nitawapoteza binadamu wote,
isipokuwa wale uliowatakasa miongoni mwa waja wako na ukawalinda nisiwapoteze, na usinipatie njia yoyote ya kuwaathiri.»
Mwenyezi Mungu Akasema, «Ukweli watoka kwangu , na sisemi isipokuwa ukweli.
Nitaujaza moto wa Jahanamu ukukusanye wewe na kizazi chako na wale wote wenye kukufuata miongoni mwa wanadamu.»
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina miongoni mwa watu wako. «Sitaki kwenu ujira au malipo kwa kuwalingania nyinyi na kuwaongoza, na sidai jambo ambalo si langu, bali mimi nafuata yale ninayoletewa kwa njia ya wahyi, wala sijikalifishi kuleta mambo ya dhana na uzushi.»
Haikuwa hii Qur’ani isipokuwa ni ukumbusho kwa viumbe vyote: majini na binadamu, wapate kujikumbusha kwayo mambo yanayowanufaisha wao ya maslahi ya Dini yao na dunia yao.
Na mtajua, tena mtajua, enyi washirikina, habari ya hii Qur’ani na ukweli wake, pindi utakaposhinda Uislamu na watu kuingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu mapote kwa mapote, na pia pindi mtakaposhukiwa na adhabu na kamba zote kuwakatikia.
Icon