ترجمة سورة الحشر

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الحشر باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Vimemtakasa Mwenyezi Mungu na kumuepusha na kila kisichonasibiana na Yeye, vilivyoko mbinguni na vilivyoko ardhini, na Yeye Ndiye Mshindi Asiyekuwa na mwenye kushindana na Yeye, Mwingi wa hekima katika makadirio Yake, uendeshaji Wake na utengezaji Wake na Sheria Zake, Anaweka kila jambo mahali pake panapostahiki.
Yeye, kutakasika ni Kwake, Ndiye Aliyewatoa wale walioukanusha unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa watu waliopewa Kitabu, nao ni Mayahudi wa ukoo wa Banū al Nadīr, kutoka majumbani mwao ambayo wakiwa humo walikuwa ni majirani na Waislamu pambizoni mwa Madina. Huko kulikuwa ndio mwanzo wa kutolewa nje ya Bara Arabu hadi Shām. Hamkudhani, enyi Waislamu, kuwa watatoka majumbani mwao kwa unyonge huu na utwevu, kwa silaha kali waliokuwa nazo na hifadhi ya nguvu waliokuwa nayo. Na walidhani Mayahudi kuwa ngome zao zitawakinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kuwa hakuna anayeziweza. Basi amri ya Mwenyezi Mungu ilizijilia kwa namna ambayo haikupita kwenye akili zao, na Mwenyezi Mungu Akawatia hofu na kicho kikubwa, wakawa wanazivunja nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini, basi zingatieni, enyi wenye busara timamu na akili nyingi kwa hayo yaliyowafika wao.
Na lau si Mwenyezi Mungu kupitisha na kuamua kuwa wao watoke majumbani mwao, Angaliwaadhibu duniani kwa kuuawa na kutekwa, na huko Akhera watakuwa na adhabu ya Motoni.
Hilo- lililowapata Mayahudi duniani na linalowangojea huko Akhera- ni kuwa wao walienda kinyume sana na amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume Wake, wakawapiga vita na wakafanya harakati za kuwaasi. Basi yoyote mwenye kuenda kinyume na Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hakika Mwenmyezi Mungu Atamtesa vikali.
Mitende mnayoikata au mnayoiacha imesimama juu ya mashina yake bila ya kuigusa , ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na amri Yake, na ili Awadhalilishe kwa hilo wale waliotoka nje ya utiifu Kwake wenye kuenda kinyume na amri Yake na makatazo Yake, kwa kuwapa nguvu nyinyi kuikata mitende yao na kuichoma.
Na yale mali ya Mayahudi wa Banū al- Nadīr ambayo Mwenyezi Mungu Amewaletea, hamkupanda farasi wala ngamia ili myapate, lakini Mwenyezi Mungu Anawapa nguvu wajumbe Wake juu ya anayemtaka miongoni mwa maadui Wake, wakajisalimsha bila ya vita. (Mali hayo yanaitwa fay’), na fay’ ni mali yaliyochukuliwa kwa makafiri kwa haki bila ya vita. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Muweza, hakuna kitu chochote kinachomshinda.
Hayo mali ya washirikina wa watu wa miji ambayo Mwenyezi Mungu Amewaletea bila kupanda farasi wala ngamia, basi hayo ni ya Mwenyezi Mungu na ya Mtume Wake, yatatumiwa kwa maslahi ya Waislamu kwa jumla, jamaa wa karibu wa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mayatima: nao ni watoto maskini waliofiliwa na baba zao, maskini: nao ni wenye uhitaji na ufukara, na ibn al-sabīl: naye ni mgeni msafiri ambaye matumizi yake yameisha na mali yake yamemalizika. Hiyo ni kwa sababu mali yasiwe ni milki inayozunguka kwa matajiri peke yao, na mafukara na maskini wakanyimwa nayo. Na mali yoyote ambayo Mtume Amewapatia au sheria yoyote aliyowawekea, basi chukueni, na chochote kile alichowakataza basi komekeni nacho. Na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kuepuka makatazo Yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye mateso makali kwa anayemuasi na kuenda kinyume na amri Yake na makatazo Yake. Na aya hii ni msingi wa ulazima wa kufuata Sunnah iwe ni ya maneno, ya vitendo au ya kukubali jambo lifanyike kwa kutolikataza.
Pia wanapewa mali hayo, ambayo Mwenyezi Mungu Amemletea Mtume Wake, mafukara waliohama, wale waliolazimishwa na makafiri wa Makkah watoke kwenye majumba yao na waache mali yao na huku wanaomba kwa mwenyezi Mungu Awafanyie hisani ya kuwapa riziki duniani na radhi kesho Akhera, na wanaitetea Dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kwa kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio wakweli ambao walikuwa wakweli wa maneno yao na vitendo vyao.
Na wale wakazi wa Madina na walioamini kabla ya Waumini wa Makkah hawajahamia Madina, nao ni Anṣār (Waumini wenyeji wa Madina) wanawapenda Muhājirūn (Waumini waliohamia Madina) na wanawaliwaza kwa mali yao wala hawaoni wivu juu yao kwa mali ya fay’ waliyopewa, na wanawatanguliza waliohama na wenye uhitaji na ufukara juu ya nafsi zao, japokuwa wao wana uhitaji na ufukara. Na yoyote aliyesalimika na ubahili na uzuiaji mali yaliyomzidi, basi hao ndio wenye kufuzu waliofaulu kupata matakwa yao.
Na waliokuja miongoni mwa Waumini baada ya Anṣār na Muhājirūn wanasema, «Mola wetu! Tusamehe dhambi zetu, na uwasamehe ndugu zetu katika Dini waliotutangulia katika kuamini, Na usitie ndani ya nyoyo zetu uhasidi na chuki kwa yoyote miongoni mwa wenye kuamini. Mola wetu! Wewe ni Mpole kwa waja wako. Unawarehemu waja wako rehema rehema kunjufu katika maisha yao ya hapa ulimwenguni ya kesho Akhera.» Katika hii aya pana dalili kwamba inapasa kwa Muislamu awataje kwa wema wale waliomtangulia na awaombee dua, na awapende maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na awataje kwa wema na awaombee radhi ya Mwenyezi Mungu.
Je huwatazami hao wanafiki wanawaambia ndugu zao katika ukafiri miongoni mwa Mayahudi wa Banū al Naḍī, «Tunaapa kwamba Muhammad na walio pamoja na yeye wakiwatoa kutoka majumbani mwenu tutatoka na nyinyi! Na hatutamfuata yoyote kuhusu nyinyi anayetutaka tusiwasaidie au tuache kutoka pamoja na nyinyi, na wakipigana na nyinyi tutawasaidia juu yao?» na Mwenyezi Mungu Anashuhudia kwamba wanafiki ni warongo katika yale waliyowaahidi Banū al Naḍī.
Lau Mayahudi watatolewa Madina, wanafiki hawatatoka pamoja na wao, na lau watapigwa vita hawatapigana pamoja na wao kama walivyoahidi. Na lau watapigana pamoja na wao wangalipa mgongo hali ya kukimbia kwa kushindwa, kisha Mwenyezi Mungu Hatawanusuru, bali Atawaacha bila kuwasaidia na Atawadhalilisha.
Kwa hakika, hofu ya wanafiki na Mayahudi kuwaogopa nyinyi, enyi Waumini, ni kubwa mno ndani ya nyoyo zao kuliko vile wanavyomuogopa na kumcha Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu ya kuwa wao ni watu wasiouelewa utukufu wa Mwenyezi Mungu na kuwa na Imani Kwake, na hawaogopi mateso Yake.
Hawatakabiliana na nyinyi Mayahudi wakiwa wamejikusanya isipokuwa wakiwa kwenye miji iliyohifadhiwa kwa ngome na mahandaki, au nyuma ya kuta ambazo wanazitumia kwa kujificha kwa uoga wao na kicho kilichojikita ndani ya nyoyo zao. Uadui wao baina yao ni mkubwa, utadhani kuwa wao wamekusanyika kwenye neno moja, lakini nyoyo zao ziko mbalimbali, na hiyo ni kwa sababu wao ni watu wasioitia akilini amri ya Mwenyezi Mungu wala kuzizingatia aya Zake.
Mfano wa hawa Mayahudi kwa mateso yaliyowashukia ni kama mfano wa makafiri wa Kikureshi siku ya Badr na Mayahudi wa Banū Qaynuqā'kwa kuwa walionja mwisho mbaya wa ukafiri wao na uadui wao kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, duniani, na huko Akhera watapata adhabu kali yenye uchungu.
Na mfano wa hawa wanafiki katika kule kuwashawishi Mayahudi wapigane na kuwaahidi kuwa watawatetea dhidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kama mfano wa Shetani alipompambia binadamu na kumlingania kwenye ukafiri, na alipokufuru alisema, «Mimi nimejiepusha na wewe; mimi namuogopa Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.»
Basi mwisho wa Shetani na yule binadamu aliyemtii na akakufuru ni kwamba wote wawili wataingia Motoni hali ya kukaa humo milele. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu na kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Zake kivitendo! Muogopeni Mwenyezi Mungu na jihadharini na mateso Yake kwa kuyafanya Aliyowaamrisha na kuyaacha Aliyowakataza, na kila mtu ayazingatie matendo aliyoyatanguliza kwa Siku ya Kiyama. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika kila mnachokitenda na mnachokiacha, hakika Mwenyezi Mungu , Aliyetakasika, ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, hakuna chochote kinachofichamana Kwake miongoni mwa matendo yenu, na Yeye ni Mwenye kuwalipa nyinyi kwa hayo.
Na msiwe, enyi Waumini, kama wale walioacha kutekeleza haki ya Mwenyezi Mungu Aliyoipasisha juu yao, na kwa sababu hiyo Akawasahaulisha wao kujifanyia wema nafsi zao kwa kufanya matendo mema yenye kuwaokoa wao na adhabu ya Siku ya Kiyama. Hao ndio wenye kusifika kwa uasi, wenye kutoka nje ya utiifu kwa Mwenyezi Mungu na utiifu kwa Mtume Wake.
Hawalingani sawa, watu wa Motoni wanaoadhibiwa na watu wa Peponi wanaostareheshwa. Watu wa Peponi ndio wenye kupata kila kinachotakiwa, ndio wenye kuokoka na kila kinachochukiwa.
Lau tungaliiteremsha hii Qur’ani juu ya jabali moja miongoni mwa majabali, na likaelewa yaliyo ndani yake ya ahadi ya malipo mema kwa watu wema na malipo mabaya kwa watu wabaya, ungaliliona, pamoja na nguvu zake, ugumu wake na ukuu wake, limenyenyekea, limejidhalilisha na limepasukapasuka kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na hiyo ni mifano tunawapigia watu na kuwabainishia, huenda wao wakafikiria juu ya uweza wa Mwenyezi Mungu na ukubwa Wake. Katika aya hii pana kuhimiza kuizingatia Qur’ani na kujifahamisha maana yake na kuitumia.
Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Anayeabudiwa kwa haki, Ambaye hakuna muabudiwa isipokuwa Yeye, Mjuzi wa yaliyofichika na yaliyojitokeza, Anayajua yaliyoghibu na yaliyoko. Yeye Ndiye Mwingi wa rehema Ambaye rehema Yake imeenea kila kitu, Anayewarehemu wenye kumuamini.
Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye kuabudiwa kwa haki, Ambaye hakuna Mola isipokuwa Yeye, Mmiliki wa vitu vyote, Anayeviendesha bila kizuizi chochote wala upinzani, Aliyetakasika na kila upungufu, Aliyeepukana na kila aibu, Anayewasadikisha Mitume Wake na Manabii kwa dalili zilizo wazi Alizowatuma nazo, Anayewatunza viumbe Wake katika matendo yao, Aliye Mshindi Ambaye hakuna wa kushindana na Yeye, Aliye Jebari Ambaye Amewatendesha nguvu waja wote, na Ambaye viumbe vyote vimemdhalilikia, Aliye Mkubwa Mwenye kiburi na utukufu. Ametakasika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kila kile ambacho wanamshirikisha nacho katika kumuabudu.
Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, kutakasika ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Aliye Muumba, Muanzilishi wa uumbaji kulingana na hekima Yake, Aliyewapa sura viumbe Wake kwa namna Atakavyo. Ni Yake Yeye, kutakasika ni Kwake, Majina Mema na sifa tukufu. Vinamatakasa Yeye vyote vilivyoko mbinguni na ardhini, na Yeye ni Mshindi, Mkali wa mateso kwa maadui Wake, Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo ya viumbe Vyake.
Icon