ﰡ
«Ḥā, Mīm” Yametangulia maelezo kuhusu herufu zilizokatwa na kutengwa mwazo wa sura ya Al-Baqarah.
Ameapa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa Qur’ani iliyo wazi kimatamshi na kimaana.
Sisi tuliiteremsha katika Usiku wa Cheo uliobarikiwa wenye kheri nyingi, nao unapatikana katika mwezi wa Ramadhani. Sisi ni wenye kuonya watu kwa kile kinachowanufaisha na kuwadhuru, nako ni kule kupeleka Mitume na kuteremsha Vitabu, ili hoja ya Mwenyezi Mungu iwasimamie waja Wake.
Katika usiku huo linaamuliwa na kupambanuliwa, kutoka kwenye Ubao Uliohifadhiwa na kuletewa waandishi kati ya Malaika, kila jambo lililokadiriwa la muda wa kuishi na riziki katika mwaka huo na mambo mengine yatakayokuwa na kukadiriwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, mpaka mwisho wa mwaka, hayabadilishwi wala hayageuzwi.
Mambo haya yaliyopangwa kimadhubuti ni amri inayotoka kwetu, kwani yote yanayokuwa na Anayokadiria Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wahyi Anaouleta, vyote hivyo vinatokana na amri Yake na idhini Yake na ujuzi Wake. Hakika sisi tumetumiliza Mitume, Muhammad na waliokuwa kabla yake, kwa watu.
Hilo likiwa ni rehema kutoka kwa Mola wako, ewe Mtume, kuwafikia wale wenye kutumilizwa. Hakika Yeye ni Msikizi, Anasikia sauti zote, ni Mjuzi wa mambo yote ya waja Wake yaliyojitokeza nje na yanayofichika.
Muumba mbingu na ardhi na vitu vyote vilivyoko baina ya hivyo viwili. Iwapo nyinyi mna yakini na hilo, basi jueni kuwa Mola wa viumbe Ndiye Mola wa kweli,
hakuna Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Yeye, Peke Yake, Asiye na mshirika, Anayehuisha na kufisha, Mola wenu na Mola wa baba zenu wa mwanzo, basi muabuduni Yeye, na sio waungu wenu ambao hawawezi kudhuru wala kunufaisha.
Bali hawa washirikina wanaifanyia shaka haki; wao wanapumbaa na kucheza na hawaiamini.
Basi ngojea, ewe Mtume, uwaone hawa washirikina siku ambayo mbingu itakuja na moshi uliofunuka waziwazi
utakaowaenea watu, na hapo waambiwe, «Hii ni adhabu yenye uchungu na yenye kuumiza.”
Kisha waseme wakiomba iondolewe na iepushwe na wao, «Mola wetu! Tuepushie adhabu, kwani ukituepushia sisi ni wenye kukuamini.” (Na hilo lilifanyika na wasiamini kama walivyoahidi).
Vipi watakuwa ni wenye kukumbuka na kuwaidhika baada ya kuteremkiwa na adhabu, na hali wamejiwa na Mtume mwenye kufafanua, naye ni Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,
kisha wakaenda kinyume na yeye na wakasema kwamba alifundishwa na binadamu au makuhani au mashetani na kwamba yeye ni mwendawazimu na si Mtume?
Tutawaondolea nyinyi adhabu kidogo na mtaona kuwa nyinyi mtarudia yale ambayo mlikuwa mkiyafanya ya ukafiri, upotevu na ukanushaji, na kwa hakika sisi tutawaadhibu kwa hayo.
Siku tutakayowaadhibu makafiri wote adhabu kubwa kabisa Siku ya Kiyama, nayo ni Siku ya kuwatesa kwa kuwalipiza.
Hakika sisi tushawafanyia mtihani na kuwajaribu watu wa Fir’awn kabla ya hawa washirikina, na aliwajia wao Mtume mtukufu, naye ni Mūsā, amani imshukie, wakamkanusha na wakaangamia. Basi hivi ndivyo tutakavyowafanya maadui zako, ewe Mtume, wasipoamini.
Na Mūsā aliwaambia, «Nisalimishieni waja wa Mwenyezi Mungu kati ya Wana wa Isrāīl, na muwaachilie pamoja na mimi, wapate kumuabudu Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika. Mimi, kwenu nyinyi, ni mjumbe muaminifu juu ya wahyi Wake na ujumbe Wake.
Na msimfanyie kiburi Mwenyezi Mungu kwa kuwakanusha Mitume Wake, kwani mimi ni mwenye kuwajia na hoja waziwazi ya ukweli wa utume wangu.
Na mimi nimejihami kwa Mwenyezi Mungu msipate kuniua kwa kunipiga mawe.
Na iwapo hamniamini kwa haya niliokuja nayo, basi niacheni nifuate njia yangu na muache kuniudhi.
Hapo Mūsā akamuomba Mola wake, Fir’awn na watu wake walipomkanusha, akisema, «Hakika hawa ni watu wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumkanusha.”
Basi enda na waja wangu waliokuamini, wakakusadiki na wakakufuata, ewe Mūsā, katika kipindi cha usiku, kwani nyinyi mtafuatwa na Fir’awn na askari wake. Na nyinyi mtaokolewa, na Fir’awn askari wake watazama.
Na iache bahari hali ilivyo utakapopita, ikiwa imetulia haina mchafuko. Hakika Fir’awn na askari wake ni wenye kuzamishwa humo baharini.
Ni vingapi alivyoviacha Fir’awn na watu wake, baada ya kuangamia kwao na kuzamishwa baharini na Mwenyezi Mungu, miongoni mwa mabustani na mashamba yaliyostawi, chemchemi za maji yenye kupita,
Namazao na majumba mazuri na maisha
waliokuwa nayo ya neema na anasa.
Mfano wa mateso hayo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyowatesa wenye kukanusha na kubadilisha neema za Mwenyezi Mungu kwa kuzikanusha. Na tuliwarithisha neema hizo, baada ya Fir’awn na watu wake, watu wengine waliokuja baada yao wakashika nafasi yao miongoni mwa Wana wa Isrāīl.
Mbingu na ardhi hazikulia kwa kumsikitikia Fir’awn na watu wake, na hawakuwa ni wenye kucheleshewa adhabu iliyowashukia.
Kwa hakika, tuliwaokoa Wana wa Isrāīl kutokana na adhabu yenye kuwafanya wanyonge kwa kuuawa watoto wao wa kiume na kutumishwa wanawake wao.
Kutokana na Fir’awn. Hakika yeye alikuwa mjeuri, miongoni mwa washirikina, aliyepita mpaka katika kujigamba na kuwafanyia kiburi waja wa Mwenyezi Mungu.
Na kwa hakika, tuliwachagua Wana wa Isrāīl, kwa kuwajua kwetu, juu ya walimwengu wa zama zao.
Tukawapatia miujiza, kupitia kwa Mūsā, ambayo ilikuwa ni mtihani na maonjo kwao ya raha na shida.
Hakika hawa washirikina wa watu wako, ewe Mtume, wanasema,
”Hakuna kifo chochote ila kile kifo chetu tutakachokufia , nacho ndicho kifo cha mwanzo na cha mwisho, na sisi baada ya kufa kwetu hatutakuwa ni wenye kufufuliwa tuhesabiwe na tulipwe mema au tuteswe.”
Na wanasema pia, «Basi tuletee, ewe Muhammad: wewe na walio pamoja na wewe, wazazi wetu waliokufa, iwapo nyinyi ni wakweli kwamba Mwenyezi Mungu Atawafufua walio makaburini wakiwa hai.”
Je, hawa washirikina ni bora au watu wa Tubba’ wa Himyar na wale waliokuwa kabla yao miongoni mwa ummah waliomkanusha Mola wao? Tuliwaangamiza kwa uhalifu wao na kukanusha kwao. Hawa washirikina si bora kuliko hao ili tuwasamehe na tusiwaangamize, na hali wao wanamkanusha Mwenyezi Mungu.
Na hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake kwa mchezo.
Hatukuviumba hivyo viwili isipokuwa kwa haki ambayo ndiyo mpango wa Mwenyezi Mungu katika kuumba Kwake na kupelekesha mambo Kwake. Lakini wengi wa hawa washirikina hawalijui hilo, na kwa hivyo hawavitii akilini vitu viwili hivyo, kwa kuwa wao hawatarajii kupata malipo mema wala hawaogopi mateso.
Hakika Siku ya Uamuzi baina ya viumbe kwa waliyoyatanguliza katika dunia yao, ya kheri na ya shari, ndio wakati wa mkusanyiko wao wote.
Siku ambayo hakuna rafiki atayeweza kumuondolea rafiki yake shida yoyote, wala hawatasaidiana wao kwa wao,
isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemrehemu miongoni mwa Waumini, kwani yeye huenda akamuombea kwa Mola wake baada ya kuruhusiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mshindi katika kuwatesa maadui zake, Ndiye Mwenye kuwarehemu kwa wingi wale wenye kumtegemea na kumtii.
Hakika mti wa zaqqūm unatoka kwenye shina la moto wa Jaḥīm.
Matunda yake ni chakula cha mwenye dhambi nyingi, na dhambi kubwa zaidi kuliko dhambi zote ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu.
Matunda ya mti wa zaqqūm ni kama madini yaliyoyeyushwa.
Yanachoma ndani ya matumbo ya washirikina kama vile maji yaliyofikia upeo wa joto.
Mchukueni huyu mwenye dhambi aliyeasi mumsukume na mumuongoze kwa nguvu hadi katikati ya moto wa Jaḥīm Siku ya Kiyama.
Kisha mmimine juu ya kichwa cha huyu mfanya dhambi maji yaliyo moto sana hadi ya mwisho, na adhabu isimuepuke.
Ataambiwa mfanya dhambi huyo mbaya, «Onja adhabu hii unayoadhibiwa kwayo Leo! Hakika wewe ni mheshimiwa katika watu wako, ulio mtukufu kwao.» Katika haya kuna kumfanyia maskhara na kumlaumu.
Hakika adhabu hii mnayoadhibiwa kwayo Leo, ndiyo ile adhabu mliokuwa mna shaka nayo duniani na mkawa hamuiamini.
Hakika ya wale wanaomcha Mwenyezi Mungu, kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo yake duniani, watakuwa na mahali pa kukaa, hali ya kuwa wameaminika na magonjwa, masikitiko na mengineyo.
Kwenye mabustani ya Pepo.na maji yenye kupita.
Watakuwa wamevaa dibaji nyororo, hali ya kuwa wameelekeana kwa nyuso. Na hawatakuwa wakiangaliana visogo. Makao yao yatakuwa yakizunguka nao pale wanapozunguka.
Kama tutakavyowapa huko Akhera takrima ya kuwaingiza Peponi na kuwavisha hariri nzito na hariri yenye mng’aro, vilevile tutawakirimu kwa kuwaoza wanawake wazuri wenye macho makubwa ya kupendeza.
Wataka wachamungu hao huko Peponi waletewe kila aina ya matunda ya Peponi wanayoyatamani, wakiwa wamejiaminisha kuwa neema hizo hazitakatika wala hazitamalizika.
Hawataonja kifo, wachamungu hao, huko Peponi, baada ya kifo cha kwanza walichokionja duniani. Na Mwenyezi Mungu Atawakinga , hao wachamungu,na adhabu ya moto wa Jaḥīm, kwa wema Wake na hisani itokayo Kwake, Aliyetakasika na kuwa juu.
Takrima hii tutakayowapa wachamungu, huko Akhera, ndiyo kufuzu kukubwa ambako hakuna kufuzu kungine baada ya kufuzu huko.
Hakika sisi tumeyarahisisha matamshi ya Qur’ani na maana yake kwa lugha yao, ewe Mtume, kwani huenda wakawaidhika na wakakemeeka.
Basi ngojea, ewe Mtume, ushindi niliokuahidi juu ya hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na adhabu itakayowashukia. Wao ni wenye kungojea kufa kwako, kukushinda na kukulazimisha. Basi watajua utakuwa ni wa nani ushindi, kufaulu na sauti ya juu duniani na Akhera. Hivyo ni vyako wewe, ewe Mtume, na vya wale Waumini waliokufuata.