ترجمة سورة الفتح

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الفتح باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Sisi tumekufungulia wewe, ewe Mtume, ufunguzi ulio waziwazi, ambao ndani yake Mwenyezi Mungu Ataipa nguvu Dini Yako na Atakupa ushindi juu ya maadui wako, nao ni mapatano ya Ḥudaybiyah ambayo kwayo watu walikuwa katika hali ya amani, na likapanuka duara la ulinganizi wa Dini ya Mwenyezi Mungu, na watu wakaingia kwenye Dini ya Mwenyezi Mungu mapote kwa mapote. Kwa hivyo, Mwenyezi Mung Aliyaita mapatano hayo “Ufunguzi uliofunuka” yaani uliokuwa wazi wenye kujitokeza.
Tumekufungulia ufunguzi huo na tukakufanyia sahali, ili Mwenyezi Mungu Akusamehe dhambi zako zilizotangulia na zitakazofanyika baadaye, kwa sababu ya utiifu mwingi ulioufanya unaotokana na ufunguzi huu na kwa usumbufu ulioubeba, na ili Akutimizie neema Zake kwako kwa kuipa ushindi Dini yako,
Akunusuru juu ya maadui wako na Akuongoze njia ya Dini iliyolingana sawa isiyopotoka , na Mwenyezi Mugu Akunusuru kwa nguvu kwa namna ambayo Uislamu hautakuwa mnyonge.
Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Aliyeteremsha utulivu ndani ya nyoyo za wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika siku ya Ḥudaybiyah zikatulia na yakini ikajidhatititi ndani ya hizo nyoyo, ili wazidi kumuamini Mwenyezi Mungu na kumfuata Mtume Wake pamoja na kuamini kwao na kufuata kwao. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ana askari wa mbinguni na ardhini, Anawanusuru kwa askari hao waja Wake Waumini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa maslahi ya viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na utengezaji Wake.
Apate kuwaingiza Waumini wa kiume na Waumini wa kike kwenye mabustani ya Peponi ambayo mito inapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, hali ya kukaa humo milele, na Awafutie baya walilolifanya asiwaadhibu kwalo. Malipo hayo kwa Mwenyezi Mungu ndio kuokoka na kila kero na ndio kupata kila linalotafutwa.
Na Apate kuwaadhibu wanafiki wa kiume na wanafiki wa kike na washirikina wa kiume na washirikina wa kike wanaomdhania Mwenyezi Mungu dhana mbaya ya kuwa yeye Hatamnusuru Mtume na waliokuwa pamoja na yeye dhidi ya maadui wao na kuwa Yeye Hataipa ushindi Dini Yake. Basi juu ya hao utazunguka mzunguko wa adhabu na kila kilicho kibaya kwao, na Amewaandalia moto wa Jahanamu; na mashukio mabaya ya mtu kuishia ni hayo.
Na Mwenyezi Mungu, Alyetakasika na kutukuka, Ana askari wa mbinguni na ardhini. Anawanusuru kwa askari hao waja Wake Waumini. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi Mwenye uweza juu viumbe Vyake, ni Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo yao.
Hakika yetu sisi tumekutumiliza, ewe Mtume, uwe shahidi kwa umati wako juu ya ufikishaji ujumbe, uwabainishie kile ulichotumilizwa kwao, uwabashirie Pepo wanaokutii na uwaonye mateso ya sasa na ya baadaye,
mpate kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, mumnusuru Mwenyezi Mungu kwa kuinusuru Dini Yake, mumtukuze na mumtakase mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Hakika ya hao wanaokupa mkono , ewe Mtume, wa ahadi ya kupigana hapo Ḥudaybiyah, wao kwa kweli wanampa mkono wa ahadi Mwenyezi Mungu na wanafanya mapatano na Yeye kwa kutaka Pepo Yake na radhi Zake. Mkono wa Mwenyezi Mungu uko juu ya mikono yao. Hivyo basi Yupo na wao anayasikia maneno yao, Anawaona mahali walipo na Anayajua mambo yao ya ndani na ya nje. Basi mwenye kuivunja ahadi yake aliyoitolea mkono, maangamivu ya jambo hilo yatamrudia mwenyewe; na atakayetekeleza ahadi aliyomuahidi Mwenyezi Mungu ya kuvumilia wakati wa mapambano na adui katika njia ya Mwenyezi Mungu na kumnusuru Nabii wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Mwenyezi Mungu Atampa malipo mema mengi, nayo ni Pepo. Katika aya pana kuthibitisha sifa ya mkono kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inayonasibiana na Yeye, Aliyetakasika, bila kufananisha wala kueleza vile ulivyo.
Watakwambia, ewe Nabii, wale mabedui waliojikalisha nyuma wasitoke na wewe kwenda Makkah utakapowalaumu, «Tulishughulishwa na mali yetu na watu wa nyumbani kwetu, basi tuombee Mola Wako Atusamehe kosa letu la kujikalisha nyuma.» Wanasema hayo kwa ndimi zoa na hayana ukweli wowote maneno yao ndani ya nyoyo zao. Waambie, «Ni nani atakayemiliki kuwafanyia chochote kwa Mwenyezi Mungu iwapo Amewatakia nyinyi kheri au shari?» mambo sivyo kama vile hawa wanafiki wanavyodhania kuwa Mwenyezi Mungu hayajui yale ya unafiki yaliyomo ndani yao. Bali kwa hakika, Yeye Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya, hakuna chochote kinachofichamana Kwake katika matendo ya viumbe Vyake.
Pia mambo sivyo kama mlivyodai kuwa mlishughulishwa na mali na watu wa nyumbani, bali kwa kweli nyinyi mlidhani kuwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wale Maswahaba waliokuwa na yeye wataangamia na hawatarudi kwenu kabisa, na Shetani aliwapambia hilo ndani ya nyoyo zenu. Na pia mlidhani dhana mbaya kuwa Mwenyezi Mungu Hatampa ushindi Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Maswahaba wake juu ya maadui wao, na mlikuwa ni watu wenye kuangamia msiokuwa na kheri yoyote.
Na asiyemuamini Mwenyezi Mungu na yale aliyokuja nayo Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akazifuata Sheria Zake kivitendo, basi huyo ni kafiri anayestahili kuteswa, kwani hakika sisi tumewaandalia makafiri adhabu yenye kuunguza ndani ya Moto.
Ni ya Mwenyezi Mungu mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili, Anamsamehe, kwa rehema Zake, Anayemtaka Akamfinikia dhambi zake, na Anamuadhibu, kwa uadilifu Wake, Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na kutukuka ni Kwake, ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia Kwake, ni Mwingi huruma kwake.
Watasema wale walioachwa nyuma utakapoondoka, ewe Nabii, wewe na Maswahaba wako kuelekea kwenye ngawira za Khaybar ambazo Mwenyezi Mungu Aliwaahidi nyinyi kuwa mtazipata, «Tuacheni tuende na nyinyi huko Khaybar» wakiwa wanataka kwa hilo kubadilisha ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu. Waambie, «Hamtatoka pamoja na sisi kwenda Khaybar, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alitwambia kabla hatujarudi Madina kwamba ngawira za Khaybar ni za wale waliohudhuria Ḥudaybiyah pamoja na sisi.» Watasema, «Mambo sivyo kama mnavyosema. Mwenyezi Mungu Hakuwaamrisha nyinyi hili. Nyinyi mnatukataza kutoka na nyinyi kwa uhasidi wenu tusije tukapata ngawira pamoja na nyinyi.» Mambo sivyo kama walivyodai, bali wao walikuwa hawaelewi amri za Mwenyezi Mungu kuhusu haki zao na wajibu wao wa kidini isipokuwa kidogo.
Waambie wale waliojikalisha nyuma miongoni mwa al-a'rāb (nao ni mabedui) ili kujiepusha na kupigana, «Mtaitwa mwende mpigane na watu wenye nguvu nyingi za kupigana, mpigane nao au wasalimu amri bila ya kupigana. Basi mkimtii Mwenyezi Mungu katika hilo Alilowaitia la kupigana na watu hao Atawapa Pepo, na mkimuasi kama mlivofanya mlipojikalisha nyuma msiende Makkah pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na Amani zimshukie, Atawaadhibu adhabu yenye kuumiza.»
Yule aliye kipofu kati yenu, enyi watu, hana dhambi, wala aliye kiguru hana dhambi, wala aliye mgonjwa hana dhambi, wanapojikalisha nyuma wasishiriki katika kupigana jihadi pamoja na Waumini, kwa kuwa wao hawawezi. Na Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, Atamtia kwenye mabustani ya Pepo ambayo chini ya miti yake na majumba yake ya fahari itakuwa ikipita mito. Na Mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake akajikalisha nyuma ili kuhepa kupigana jihadi pamoja na Waumini, Atamuadhibu adhabu yenye uchungu na kuumiza.
Mwenyezi Mungu Ameridhika na Waumini pale walipokupa mkono wa ahadi, ewe Mtume, chini ya mti (Hii ndio hiyo Bay 'ah al-Ridwān ya hapo Ḥudaybiyah). Mwenyezi Mungu Alijua yaliyomo ndani ya nyoyo za Waumini hawa ya Imani, ukweli na utekelezaji ahadi, basi Mwenyezi Mungu Akawateremshia utulivu, Akaziimarisha nyoyo zao na Akawapa, badala ya kile kilichowapita katika mapatano ya Ḥudaybiyah, ufunguzi wa karibu, nao ni ufunguzi wa kuiteka Khaybar
na ngawira nyingi za mali za Mayahudi wa Khaybar walizozichukua. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika kuwatesa maadui Zake, ni Mwingi wa hekimakatika kuendesha mambo ya viumbe Vyake.
Mwenyezi Mungu Amewaahidi nyinyi ngawira nyingi mtakazozichukua katika nyakati zake alizowakadiria, Akawaharakishia ngawira za Khaybar na Akaizuia mikono ya watu isiwafikie nyinyi, lisiwapate ovu lolote kati ya yale maovu ambayo maadui wenu waliwadhamiria ya vita na mapigano, na lisiwapate wale mliowaacha Madina, na ili kule kushindwa kwao, kusalimika kwenu na kughanimu kwenu kuwe ni alama ya nyinyi kuizingatia na kuchukua dalili kwayo kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwahifadhi nyinyi na kuwanusuru, na yeye Ndiye Anayewaongoza kwenye njia iliyolingana sawa isiyokuwa na mpotoko.
Na hakika Mwenyezi Mungu Amewaahidi nyinyi ngawira nyingine ambayo hamna uwezo nayo, Mwenyezi Mungu, kutakasika na kutukuka ni Kwake, Ndiye Mwenye uweza nayo, nayo iko chini ya mpango Wake na mamlaka Yake, na Ashawaahidi nyinyi kuwapatia, na hapana budi kwamba kile Alichoahidi kitakuwa. Na Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu ni Muweza, hakuna chochote kinachomshinda.
Na lau makafiri wa Makkah wangalipigana vita na nyinyi, wangalishindwa na nyinyi na wangaliwapa migongo yao kama vile anavyofanya anayeshindwa vitani, kisha hawatapata, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, rafiki wa kushikana na wao kuwapiga vita nyinyi wala msaidizi wa kuwasaidia wao wapigane na nyinyi.
Huo ndio mpango wa Mwenyezi Mungu Alioupanga kwa viumbe Vyake hapo tangu kuwa Atawanusuru askari Wake na Atawashindisha maadui Wake, na hutapata, ewe Nabii, katika mipango ya Mwenyezi Mungu mabadiliko.
Na Yeye Ndiye Aliyeizuia mikono ya washirikina isiwafikie nyinyi, na mikono yenu isiwafikie wao katika bonde la Makkah baada nyinyi kuwaweza wao wakawa chini ya mamlaka yanu. (washirikina hawa ndio wale waliotoka kuishambulia kambi ya askari wa Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hapo Ḥudaybiyah, Waislamu wakawakamata kisha wakawaachilia wasiwaue, na walikuwa ni kiasi cha wanaume themanini.) Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yenu, hakuna chochote kinafichamana Kwake.
Makafiri wa Kikureshi ndio waliokataa kumpwekesha Mwenyezi Mungu, wakawazuia nyinyi, Siku ya Ḥudaybiyah, kuingia Msikiti wa al-Ḥarām, wakakataza wanyama na wakawafunga wasifike mahali pa wao kuchinjwa, napo ni Ḥarām. Na lau si wanaume Waumini walio wanyonge na wanawake Waumini msiowajua, walio kati ya hawa makafiri wa Makkah, wanaoificha Imani yao kwa kuzichelea nafsi zao, msije mkawakanyaga kwa jeshi lenu mkawaua, mkapata dhambi, aibu na gharama kwa mauaji hayo bila kujua, tungaliwapa nyinyi uwezo juu yao, ili Mwenyezi Mungu Apate kumtia kwenye rehema Zake Anayemtaka kwa kumpa neema ya kuamini baada ya kukanusha. Lau hawa Waumini wa kiume na Waumini wa kike wangalitenganika na washirikina wa Makkah na wakajitoa kati yao, tungaliwaadhibu wale waliokufuru na kukanusha miongoni mwao adhabu yenye uchungu na kuumiza.
Pindi wale waliokanusha walipoingiza ndani ya nyoyo zao ghera, ghera za watu wa zama za ujinga, ili wasikubali utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na miongoni mwa hayo ni kule kukataa kwao kwandika «Bi ism Allāh al-Raḥmān al-Raḥīm» katika mapatano ya Ḥudaybiyah, na wakakataa kuandika, «Haya ndiyo yale aliyoyapitisha Muhammad, Mtume wa Mwenyezi Mungu.» Na Mwenyezi Mungu Akamteremshia utulivu Mtume Wake na Waumini pamoja na yeye, Akawathibitishia neno «Lā ilāha illā Allāh» ambalo ndio kichwa cha ya kila uchamungu. Na Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Waumini pamoja na yeye ndio wanaostahiki zaidi neno la uchamungu kuliko washirikina. Na hivyo ndivyo walivyokuwa, walistahiki neno hili na sio washirikina. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa ujuzi wa kila kitu, hakuna kitu chochote kinachofichamana Kwake.
Kwa hakika Mwenyezi Mungu Alimsadikishia Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndoto yake aliyomuotesha kwa haki kwamba utaingia, wewe na Maswahaba wako, Nyumba takatifu ya Mwenyezi Mungu hali ya kuwa mko katika amani, hamuwaogopi watu wa ushirikina, hali ya kuwa mnanyoa vichwa vyenu na mnapunguza. Mwenyezi Mungu Alijua kheri na maslahi ya kuwaepusha nyinyi na Makkah mwaka wenu huo na kuingia huko baadae, msiyoyajua nyinyi, na Akajaalia, kabla ya kuingia kwenu Makkah mliyoahidiwa, ufunguzi wa karibu, nao ni mapatano ya amani ya Ḥudaybiyah na ufunguzi wa Khaybar.
Yeye Ndiye Aliyemtumiliza Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa ubainufu ulio wazi na Dini ya Uislamu, ili aifanye kuwa juu ya mila zote. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi kwamba Yeye ni Mwenye kukupa ushindi na kuidhihirisha Dini yako juu ya kila dini.
Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wale walio pamoja na yeye katika dini yake, ni wakali juu ya makafiri, wanahurumiana wao kwa wao, utawaona wakirukuu na kumsujudia Mwenyezi Mungu katika Swala yao, wakimtarajia Mola wao Awatunuku fadhila Zake, Awatie Peponi na Awe radhi nao. Alama ya utiifu wao kwa Mwenyezi Mungu iko wazi kwenye nyuso zao kwa alama ya kusujudu na kuabudu. Hiii ndiyo sifa yao kwenye Taurati. Na sifa yao katika Injili ni kama sifa ya mmea wa nafaka uliotoa kijiti chake na tawi lake, kisha matawi yakawa mengi baada ya hapo, na mmea ukashikana, ukapata nguvu na ukasimama juu ya kigogo chake ukiwa na mandhari mazuri yanayowapendeza wakulima, ili kuwatia hasira kwa Waumini hawa, kwa wingi wao na uzuri wa mandhari yao, makafiri. Katika haya pana dalili ya ukafiri wa wenye kuwachukia Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, kwa kuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Anamtia hasira kwa Maswahaba basi ishapatikana kwake sababu ya hasira nayo ni ukafiri. Mwenyezi Mungu Amewaahidi waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake kati yao kusamehewa dhambi zao na kupewa malipo mema mengi yasiyokatika, nayo ni Pepo. (Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya ukweli unaoaminiwa usioenda kinyume. Na kila mwenye kufuata nyayo za Maswahaba, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie, basi yeye anaingia kwenye hukumu yao ya kustahiki msamaha na malipo makubwa, na wao wana ubora, kutangulia mbele na ukamilifu ambao hakuna yoyote katika ummah huu atakayewafikia, radhi za Mwenyezi Mungu ziwashukie na Awaridhishe).
Icon