ترجمة معاني سورة المجادلة باللغة السواحلية من كتاب Ali Muhsin Al - Swahili translation

Ali Muhsin Al - Swahili translation


Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wane wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyo yatenda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

Kwani huwaoni wale walio katazwa kunong'onezana kisha wakayarudia yale yale waliyo katazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya dhambi, na ya uadui, na ya kumuasi Mtume? Na wakikujia hukuamkia sivyo anavyo kuamkia Mwenyezi Mungu. Na husema katika nafsi zao: Mbona Mwenyezi hatuadhibu kwa haya tuyasemayo? Basi Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo marejeo maovu yaliyoje!

Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

Huwakuti watu wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanao mpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio Hizbullahi, Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.
تقدم القراءة