ترجمة سورة البروج

Ali Muhsin Al - Swahili translation
ترجمة معاني سورة البروج باللغة السواحلية من كتاب Ali Muhsin Al - Swahili translation .

Al-Buruj


Naapa kwa mbingu yenye Buruji!

Na kwa siku iliyo ahidiwa!

Na kwa shahidi na kinacho shuhudiwa!

Wameangamizwa watu wa makhandaki

Yenye moto wenye kuni nyingi,

Walipo kuwa wamekaa hapo,

Na wao ni mashahidi wa yale waliyo kuwa wakiwafanyia Waumini.

Nao hawakuona baya lolote kwao ila kuwa wakimuamini Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Msifiwa,

Ambaye anao ufalme wa mbingu na ardhi; na Mwenyezi Mungu ni shaahidi wa kila kitu.

Hakika walio wafitini Waumini wanaume na Waumini wanawake, kisha hawakutubu, basi watapata adhabu ya Jahannamu na watapata adhabu ya kuungua.

Hakika walio amini na wakatenda mema watapata Bustani zenye mito ipitayo kati yake. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

Hakika kutesa kwa Mola wako Mlezi ni kukali.

Yeye ndiye anaye anzisha na ndiye anaye rejeza tena,

Naye ni Mwenye kusamehe, Mwenye mapenzi,

Mwenye Kiti cha Enzi, Mtukufu,

Atendaye ayatakayo.

Je! Zimekuwasilia khabari za majeshi?

Ya Firauni na Thamudi?

Lakini walio kufuru wamo katika kukadhibisha.

Na Mwenyezi Mungu nyuma yao amewazunguka.

Bali hii ni Qur'ani tukufu

Katika Ubao Ulio Hifadhiwa.
Icon