ترجمة سورة الذاريات

Ali Muhsin Al - Swahili translation
ترجمة معاني سورة الذاريات باللغة السواحلية من كتاب Ali Muhsin Al - Swahili translation .

Az-Zariyat


Naapa kwa pepo zinazo tawanya,

Na zinazo beba mizigo,

Na zinazo kwenda kwa wepesi.

Na zinazo gawanya kwa amri,

Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli,

Na kwa hakika malipo bila ya shaka yatatokea.

Naapa kwa mbingu zenye njia,

Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitalifiana.

Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa.

Wazushi wameangamizwa.

Ambao wameghafilika katika ujinga.

Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo?

Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni.

Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza.

Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na chemchem.

Wanapokea aliyo wapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.

Walikuwa wakilala kidogo tu usiku.

Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.

Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba.

Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini.

Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?

Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa.

Basi naapa kwa Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, hakika haya ni kweli kama ilivyo kweli kuwa nyinyi mnasema.

Je! Imekufikia hadithi ya wageni wa Ibrahim wanao hishimiwa?

Walipo ingia kwake wakasema: Salama! Na yeye akasema: Salama! Nyinyi ni watu nisio kujueni.

Akenda kwa ahali yake na akaja na ndama aliye nona.

Akawakaribisha, akasema: Mbona hamli?

Akahisi kuwaogopa katika nafsi yake. Wakasema: Usiwe na khofu, nao wakambashiria kupata kijana mwenye ilimu.

Ndipo mkewe akawaelekea, na huku anasema na akijipiga usoni kwa mastaajabu, na kusema: Mimi ni kikongwe na tasa!

Wakasema: Ndivyo vivyo hivyo alivyo sema Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye hikima na Mwenye kujua.

AKASEMA: Basi ujumbe wenu ni nini, enyi mlio tumwa?

Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa watu wakosefu,

Tuwatupie mawe ya udongo,

Yaliyo tiwa alama kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa ajili ya wanao pindukia mipaka.

Kwa hivyo tutawatoa katika hao wale walio amini.

Lakini hatukupata humo ila nyumba moja tu yenye Waislamu!

Na tukaacha humo Ishara kwa ajili ya wanao iogopa adhabu chungu.

Na katika khabari za Musa, tulipo mtuma kwa Firauni na hoja wazi.

Lakini alipuuza kwa sababu ya nguvu zake na akasema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu!

Basi tukamkamata yeye na majeshi yake na tukawatupa baharini, na yeye ndiye wa kulaumiwa.

Na katika khabari za A'di tulipo wapelekea upepo wa kukata uzazi.

Haukuacha chochote ulicho kifikia ila ulikifanya kama kilio nyambuka.

Na katika khabari za Thamudi walipo ambiwa: Jifurahisheni kwa muda mdogo tu.

Wakaasi amri ya Mola wao Mlezi. Basi uliwanyakua moto wa radi nao wanaona.

Basi hawakuweza kusimama wala hawakuwa wenye kujitetea.

Na kaumu ya Nuhu hapo mbele. Hakika hao walikuwa watu wapotovu.

Na mbingu tumezifanya kwa nguvu na uwezo na hakika Sisi bila ya shaka ndio twenye uwezo wa kuzitanua.

Na ardhi tumeitandaza; basi watandazaji wazuri namna gani Sisi!

Na katika kila kitu tumeumba kwa jozi ili mzingatie.

Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.

Wala msifanye kuwa kuna mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu. Hakika mimi ni mwonyaji kwenu wa kubainisha nitokae kwake.

Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.

Je! Wameambizana kwa haya? Bali hawa ni watu waasi.

Basi waachilie mbali, nawe hulaumiwi.

Na kumbusha, kwani ukumbusho huwafaa Waumini.

Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.

Na sitaki kwao riziki, wala sitaki wanilishe.

Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kuruzuku, Mwenye nguvu, Madhubuti.

Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize.

Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa.
Icon