ﰡ
«Alif, Lām, Mīm» Yametangulia maelezo kuhusu matamko haya katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah.
Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana muabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Anayesifika kwa uhai mkamilifu unaonasibiana na utukufu Wake.Anayesimamia kila kitu.
Amekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa haki ambayo haina shaka, inayoshuhudia ukweli wa Vitabu na Mitume kabla yake. Na Aliiteremsha Taurati kwa Musa, amani imshukie, na Injili kwa Īsā, amani imshukie,
kabla ya kuteremka Qur’ani, ili kuwaongoza Wacha-Mungu kwenye Imani na kutengeneza dini yao na dunia yao. Na Aliteremsha yenye kupambanua baina ya haki na batili. Na wale ambao wamekanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa, wana adhabu kubwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi Asiyeshindwa, ni Mwenye kumtesa anayezikanusha hoja na dalili Zake na kupwekeka Kwake kwa uungu.
Hakika Mwenyezi Mungu, ujuzi Wake umewazunguka viumbe wote. Hakuna kitu chenye kufichika Kwake katika ardhi wala katika mbingu, kiwe kichache au kingi.
Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Anawaumba nyiyi katika zao za mamama zenu kama Atakavyo: wanaume, wanawake, wazuri, wabaya, waovu na wema. Hapana mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika amri Zake na uendeshaji mambo Wake.
Yeye Peke Yake Ndiye Ambaye Aliyekuteremshia Qur’ani ambayo katika hiyo kuna aya zenye maana yaliyo wazi; hizo ndizo msingi wa Kitabu ambao unategemewa ikitokea tashwishi, na ambao chochote kinachohalifiana nao kinarudishwa na kuoanishwa nao. Na katika hiyo kuna aya zingine mutashabihat: zinazoleta tashwishi kwa kuwa zinabeba zaidi ya maana mamoja, kwa namna ambayo haiwezekani kujuwa maana iliyokusudiwa isipokuwa kwa kuziambatanisha na muhkam: aya zenye maana yaliyo wazi. Basi wenye nyoyo zenye ugonjwa zilizopotoka, kwa ubaya wa nia zao, huzifuata hizi aya zenye tashwishi peke yake, ili kutia tashwishi kwa watu kwa lengo la kuwapoteza kwa kuzifasiri kuambatana na madhehebu yao yaliyo batili. Ilihali hakuna ajuwaye uhakika wa maana ya aya hizi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wale waliovama kwenye elimu wanasema, «Tumeiamini hii Qur’ani, kwani yote imetujia kutoka kwa Mola wetu kwa ulimi wa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.» na wanairudisha yenye tashwishi katika Qur’ani na kuiyoanisha na iliyo wazi yake. Hakika ni kwamba wanaoyafahamu na kuyazingatia maana kama ilivyo sahihi ipasavyo ni wale wenye akili timamu.
Na wanasema, «Ewe Mola wetu, usizipotoe nyoyo zetu na kukuamini Wewe, baada ya kutuneemesha kwa uongofu wa kufuata Dini Yako; na utupe miongoni mwa fadhila zako, rehema yenye kuenea. Kwani Wewe Ndiye Mpaji: Mwingi wa fadhila na vipaji vipaji., unampa unayemtaka bila ya hesabu.
Ewe Mola Wetu, sisi tunakubali na kushuhudia kwamba Wewe utawakusanya watu Siku isiyo na shaka , nayo ni Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huendi kinyume na ahadi uliyowapa waja Wako.»
Hakika wale waliokanusha Dini ya haki na wakaikataa, hayatawafaa wao mali yao wala watoto wao kuwaepushia chochote katika adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwashukia ulimwenguni, wala hayatawakinga wao na adhabu Yake Akhera. Na hawa ndio kuni za Moto Siku ya Kiyama.
Hali ya makafiri katika kukanusha kwao na adhabu itakayowashukia ni kama hali ya jamaa za Fir’aun na wale makafiri waliokuwa kabla yao. Wao walizikanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi, Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa kuwatesa kwa sababu ya kukanusha kwao na kushindana. Na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kutesa kwa aliyemkufuru Yeye na kuwakanusha Mitume Wake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia makafiri miongoni mwa Mayhudi na wengineo na wale ambao waliudharau ushindi wako katika Badr, «Nyinyi mtashindwa duniani na mtakufa ukafirini, na mtakusanywa mpelekwe kwenye Moto wa Jahanamu, ambao utakuwa ni tandiko la milele kwenu; tandiko baya sana ni hilo.»
Hakika yalikiwa kwenu, enyi Mayahudi wakaidi, ni ushuhuda mkubwa yale mapambano ya Badr yaliyotukia baina ya makundi mawili: kundi moja linapigana kwa ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu, nalo ni kundi la Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Masahaba wake, na kundi lingine lenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, linapigana kwa ajili ya batili. Ukiwatazama Waumini kwa macho utawaona kuwa ni mara mbili ya ile idadi yao. Na Mwenyezi Mungu Alilifanya hilo kuwa ni sababu ya ushindi wa Waislamu juu yao. Na Mwenyezi Mungu Anawasaidia kwa nusura Yake anaowataka katika waja Wake. Hakika katika tukio hili pana mazingatio makubwa kwa wenye busara ambao wanaongokea kujua hukumu zake na matendo Yake.
Wamepambiwa watu kupenda matamanio ya wanawake na watoto wa kiume na mali mengi ya dhahabu , fedha, farasi wazuri, wanyama wa mifugo miongoni mwa ngamia, ng’ombe na mbuzi na kondoo na ardhi inayotayarishwa kwa kupandwa miti na makulima. Hayo ni mazuri ya uhai wa kilimwengu na pambo lake lenye kutoweka. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna marejeo mazuri na thawabu, nayo ni Pepo.
Sema ,ewe Mtume, «Je, ni wape habari ya yaliyo bora kuliko yale waliyopambiwa watu katika maisha haya ya kilimwengu? Wale waliomchunga Mwenyezi Mungu na wakaogopa mateso Yake, watakuwa na Pepo ambazo inapita mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Watakaa milele humo. Na watakuwa nao humo wake waliotakasika na hedhi na nifasi na tabia mbaya. Na watakuwa na malipo makubwa zaidi kuliko hayo, nayo ni radhi za Mwenyezi Mungu.» Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuchungulia siri za viumbe wake, ni Mjuzi wa hali zao na atawalipa kwa hayo.
Waja hawa wacha-Mungu huwa wakisema, «Mola wetu, sisi tumekuamini Wewe na tumemfuata Mtume Wako Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, tusamehe madhambi tuliyoyatenda na utuepushe na adhabu ya Moto.»
Hawa ndio waliosifika kwa subira juu ya kumtii Mwenyezi Mungu, kuepuka maasia na juu ya shida zinazowafikia zilizokadiriwa na Mwenyezi Mungu. Na ndio waliosifika kwa ukweli wa maneno na vitendo na kutii kikamilifu. Na ndio waliosifika kwa utoaji, wa siri na wadhahiri, na kwa kuleta istighfar: kuomba msamaha, katika mwisho wa usiku, kwa kuwa wakati huo unatarajiwa zaidi kukubaliwa amali na kujibiwa dua.
Mwenyezi Mungu Ameshuhudia kuwa Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa uungu. Na Ameambatanisha ushahidi wake na ule wa Malaika na watu wa elimu juu ya kitu kitukufu zaidi chenye kushuhudiwa, nacho ni Tawhīd umoja Wake Aliyetukuka na kusimamia Kwake haki na uadilifu. Hapana Mola isipokuwa Yeye, Aliye Mshindi Ambaye hakuna kitu Atakacho kiwe kikakataa kuwa, Mwenye hekima katikia maneno Yake na vitendo Vyake.
Hakika dini ambayo Mwenyezi Mungu Aliwachagulia waja Wake na Akawatumiliza kwayo Mitume Wake na ambayo Hakubali isipokuwa hiyo ni Uislamu. Nao ni kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, Peke Yake, kwa kumtii na kujisalimisha Kwake kwa udhalilifu na kuwafuata Mitume katika yale waliotumilizwa kwayo katika kila kipindi mpaka wakahitimishwa kwa kuja Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambaye, Hakubali Mwenyezi Mungu dini kutoka kwa yoyote, baada ya kutumilizwa kwake, isipokuwa Uislamu ambao alitumilizwa nao. Na tafauti baina ya Watu wa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, iliyowafanya watengane wawe mapote na makundi, haikutokea ela baada ya kuthibiti hoja juu yao kwa kupelekwa Mitume na kuteremshwa Vitabu; hiyo ilitokana na uadui na uhasidi kwa kutafuta ulimwengu.Na yoyote mwenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu zilizoteremshwa na alama Zake zenye kujulisha uola Wake na uungu Wake, basi Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa hesabu, na Atawalipa kwa yale waliokuwa wakiyafanya.
Wakijadiliana na wewe, ewe Mtume, Watu wa Kitabu juu ya Tawhīd: kumuwahidisha na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, baada ya kuwasimamishia hoja, waambie, «Mimi nimemtakasia Mwenyezi Mungu Peke Yake, si mshirikishi Yeye na yoyote; na pia wale Waumini walionifuata wamemtakasia Mwenyezi Mungu na kumtii.» Na waambie wao na wale washirikina, Waarabu na wengineo, «Mkiingia kwenye Uislamu, basi nyinyi muko kwenye njia ya sawa, uongofu na haki. Na mkirudi nyuma, hesabu yenu iko kwa Mwenyezi Mungu. Mimi sina langu isipokuwa ni kufikisha ujumbe. Na mimi nimewafikishia na nimesimamisha hoja juu yenu.» Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja, hakuna chochote chenye kufichika kwake katika mambo yao.
Hakika wale wanaozikanusha dalili zilizo wazi na yale waliokuja nayo Mitume, wakawaua Manabii kwa udhalimu bila haki yoyote, na wakawaua wale ambao wanaamrisha uadilifu na kufuata njia ya Mitume, wape bishara ya adhabu yenye uchungu.
Hao ndio ambao amali zao zilitanguka ulimwenguni na Akhera. Hakuna amali yao yoyote itakubaliwa, na hawatakuwa na yoyote mwenye kuwanusuru kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Je, umeona, ewe Mtume, hali ya kustaajabisha zaidi kuliko hali ya hawa Mayahudi, ambao Mwenyezi Mungu Amewapa fungu katika Kitabu wakajua kuwa yale uliyoyaleta ni haki, wanaitwa wafuate yaliyokuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, nacho ni Qur’ani, ili kitoe uamuzi katika mambo waliotafautiana juu yake, kisha wengi wao wanakataa uamuzi huo iwapo haulingani na matamanio yao, kwa kuwa desturi yao ni ni kuipa mgongo haki?
kujiepusha huko na haki, sababu yake ni itikadi mbaya walionayo Watu wa Kitabu kwamba wao hawataadhibiwa isipokuwa siku chache. Itikadi hii iliwapelekea wao wamfanyiye ujasiri Mwenyezi Mungu na waidharau Dini Yake na waendelee na dini yao ya batili ambayo walijidanganya nayo nafsi zao.
Vipi hali zao zitakuwa, Atakapowakusanya Mwenyezi Mungu ili wahesabiwe katika Siku isiyo na shaka kuja kwake, nayo ni Siku ya Kiyama, na kila mmoja apate malipo ya aliyoyatenda, na wao bila kudhulumiwa kitu chochote?
Sema ,ewe Nabii, ukielekea kwa Mola wako kwa dua, «Ewe Ambaye Una ufalme wote, Wewe Ndiye Ambaye Unamtunuku ufalme, mali na umakinifu katika ardhi Umtakaye miongoni mwa waja Wako, na Unauondoa ufalme kutoka kwa Umtakaye. Na Unampa enzi ya ulimwengu na ya Akhera Unayemtaka, na Unamfanya awe na unyonge Unayemtaka. Kheri ipo mikononi mwako. Wewe, Peke Yako, juu ya kila kitu , ni Muweza.» Katika ayah hii pana kuthibitisha sifa ya Mkono kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inayonasibiana na Yeye, utakatifu ni Wake.
«Na miongoni mwa dalili za uwezo Wako, ni kuwa Wewe Unautia usiku ndani ya mchana, na Unautia mchana ndani ya uslku, huu ukarefuka na ule ukafupika. Na Unatoa chenye uhai kutoka kwa kilichokufa kisichokuwa na uhai, kama kutoa mazao kutokana na mbegu na kama kumtoa Muumini kutoka kwa kafiri. Na Unatoa kilichokufa kutoka kwa chenye uhai, kama kutoa yai kwenye kuku. Na Unamruzuku Unayemtaka katika waja Wako bila hesabu.»
Mwenyezi Mungu Anawakataza Waumini kuwafanya makafiri kuwa ni wategemewa, kwa mapenzi na kwa kutaka himaya, badala ya Waumini. Na yoyote mwenye kuwafanya wao ni wategemewa, huyo ameshakuwa mbali na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu Yuko mbali na yeye. Isipokuwa mkiwa ni madhaifu wenye kuogopa, hapo Mwenyezi Mungu Amewapa ruhusa muwasairi ili kujiepusha na shari lao, mpaka mtakapopata nguvu. Na Mwenyezi Mungu Anawatahadharisha nyinyi na Yeye. basi mcheni na muogopeni. Na Kwake Peke Yake ndio marejeo ya viumbe kwa kuhesabiwa na kulipwa.
Sema, ewe Nabii, Kuwaambia Waumini, «Mkiyaficha yaliyomo ndani ya nyoyo zenu ya kuwafanya makafiri ni wategemewa na wasaidizi au mkiyadhihirisha hayo, hakitafichika chochote katika hayo kwa Mwenyezi Mungu. Kwani ujuzi Wake umezunguka kila kilichoko mbinguni na kilichoko ardhini, na Ana uwezo kamili juu ya kila kitu.
Na katika Siku ya Kiyama, Siku ya Malipo, kila nafsi italikuta jema lolote ililolifanya linaingojea likiwa limeongezwa ili ilipwe nalo. Na pia baya iliolifanya italikuta linaingojea vilevile, hapo itatamani lau ilikuwa baina yake na hilo tendo baya zama zirefu. Basi jitayarisheni kwa Siku hii, na muogope mateso ya Mola Aliye Jabari. Na pamoja na ukali wa mateso Yake, Yeye, Aliyetakata na sifa za upungufu, ni Msifika kwa ukamilifu wa huruma kwa waja.
Sema, ewe Mtume, «Ikiwa nyinyi munampenda Mwenyezi Mungu kikweli, nifuateni mimi na kuniaminini, ndani na nje, ndipo Mwenyezi Mungu Atawapenda na Atawasamehe madhambi yenu.Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja Wake Waumini, ni Mwingi wa rehema kwao.» Aya hii tukufu yamhukumu kila anayedai kumpenda Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na akawa hamfuati Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kama ipasavyo kufuatwa, na wala hamtii katika maamrisho yake na makatazo yake, kuwa yeye ni mrongo katika madai yake mpaka amfuate Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kama ipasavyo kufuatwa.
Sema, ewe Mtume, «Mtiini Mwenyezi Mungu kwa kufuata Kitabu Chake, na mtiini Mtume kwa kufuata mwenendo wake wakati wa uhai wake na baada ya kufa kwake.Wakiwa watakupa mgongo na kukamaa kwenye ukafiri na upotevu walionao, wao hawatakuwa wanastahili mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu Hawapendi makafiri.
Hakika Mwenyezi Mungu Amemchagua Ādam, Nūḥ, jamii ya Ibrāhīm na jamii ya 'Imrān Akawafanya kuwa ni bora wa watu wa zama zao.
Manabii hawa na Mitume ni mlolongo wa usafi wenye kuungana katika kumtakasa Mwenyezi Munguna, kumpwekesha na kutenda vitendo vinavyoambatana na wahyi Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, ni Mjuzi wa vitendo vyao na Atawalipa kwavyo.
kumbuka, ewe Mtume, ilivyokuwa kuhusu mambo ya Maryam na mama yake na mtoto wake 'Īsā, amani imshukie, ili kuwarudi, kwa hayo, wale wanoadai uungu wa 'Īsā au kuwa yeye ni Mwana wa Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, aliposema mke wa 'Imran wakati aliposhika mimba, «Ewe Mola wangu, mimi nimekutakasia kilioko ndani ya tumbo langu kiwe ni chako Peke Yako kwa kutumikia Baitulmaqdis. Basi takabali kutoka kwangu. Hakika Wewe Peke Yako Ndiye Msikizi wa dua yangu, Ndiye Mjuzi wa nia yangu.»
Mimba yake ilipotimia na akamzaa mtoto wake alisema, «Mola wangu, mimi nimemzaa mwanamke ambaye hafai kwa kutumikia Baitulmaqdis,» Na Mwenyezi Mungu Anajua zaidi kwa alichokizaa na atamjaalia kuwa na jambo kubwa. Mke wa 'Imran aliendelea kusema, «Na Mwanamume niliyemtaka kwa kutumika si kama Mwanamke kwa hilo. Kwa kuwa mwanamume ni mwenye nguvu zaidi wa kutumika na kusimamia utumishi. Na mimi nimempa jina la Maryam. Na mimi nimemlinda kwako, yeye na watoto wake , kutokana na Shetani aliyefukuzwa kwenye rehema Yako.»
Mwenyezi Mungu Akamjibu maombi yake na Akaikubali nadhiri yake na kuipokea vizuri na Akamsimamia binti yake, Maryam, kwa kumtunza na Akamkuza makuzi mazuri. Mwenyezi Mungu Akamsahilishia kwa kumjaalia Zakaria, amani imshukie, kuwa ni mlezi wake; naye akamuweka mahali pake pa kuabudu. Na alikuwa kila akimjia mahali hapo, anakuta ana chakula kizuri kilichotayarishwa. Akasema, «Ewe Maryam, umepata kutoka wapi chakula hiki kizuri?» Akasema, «Hiyo ni riziki itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu Anamruzuku Anayemtaka miongoni mwa waja Wake bila ya hesabu.»
Alipoona Zakariyyā vile Mwenyezi Mungu Alivyomkirimu Maryam kwa riziki Yake na fadhila Zake, alielekea kwa Mola wake akisema, «Ewe Mola wangu, nipe kutoka Kwako mtoto mwema mwenye kubarikiwa. Wewe ni Msikizi wa maombi ya anayekuomba.»
Hapo Malaika walimuita, naye yuko katika hali ya kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu katika mahali pake pa Swala, huku anamuomba Yeye, wakamuambia. «Mwenyezi Mungu Anakupa habari yenye kukufurahisha, nayo ni kwamba utaruzukiwa mtoto ambaye jina lake ni Yaḥyā, ambaye atalisadikisha neno la Mwenyezi Mungu, naye ni 'Īsā mwana wa Maryam, amani imshukie. Huyo Yaḥyā atakuwa ni bwana wa kaumu yake, atakuwa na cheo na daraja kubwa, atakuwa ni mwenye kujihifadhi: hatendi madhambi wala hafuati matamanio ya kudhuru na atakuwa ni Nabii miongoni mwa watu wema ambao walifikia kilele cha wema.»
Zakariyyā akasema akiwa na furaha na kwa kustaajabu, «Mola wangu! Vipi nitakuwa na mtoto hali ya kuwa uzee umenifikia hadi ya kunifikia na mke wangu ni tasa, hazai.? Akasema, «Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu Anavyofanya Anayoyataka katika mambo ya ajabu yanayokwenda kinyume na mambo ya kawaida.»
Zakariyyā akasema, «Mola wangu, nijaalia alama ambayo itakuwa ni dalili kwangu ya kupata matoto ili nipate kuingiwa na furaha na bashasha.» Akasema, «Alama yako uliyoitaka ni kutoweza kusema na watu kwa siku tatu isipokuwa kwa kuwashiria, pamoja na kuwa wewe uko sawa na mzima. Na katika kipindi hiki, kithirisha kumataja Mola wako na umswaliye katika nyakati za mwisho wa mchana na mwanzo wake.
Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Malaika waliposema, «Ewe Maryam, hakika Mola wako Amekuchagua kwa kumtii na Amekusafisha na tabia duni na Amekuchagua kati ya wanawake wa ulimwengu wote katika zama zako.
«Ewe Maryam, Endelea daima kumtii Mola wako, simama kwa utulivu na unyenyekevu na usujudu na urukuu pamoja na wenye kurukuu kwa kumshukuru Mola wako juu ya neema Alizokutunukia.»
Hizo tulizokusimulia, ewe Mtume, ni miongoni mwa habari za ghaibu alizokujulisha Mwenyezi Mungu kwa njia ya wahyi. Kwani wewe hukuwa pamoja na wao walipotafautiana juu ya nani mwenye haki zaidi na anayefaa kumlea Maryam, ukatokea utesi baina yao, wakapiga kura kwa kuzitupa kalamu zao, ikamwangukia Zakariyyā akapata ushindi wa kumlea.
Kadhalika hukuwako huko, ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu, pindi Malaika waliposema, «Ewe Maryam, Mwenyezi Mungu Anakubashiria mtoto ambaye kupatikana kwake kutatokana na neno la Mwenyezi Mungu, yaani Atamwambia, ‘Kuwa,’ na atakuwa, jina lake ni Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam. Yeye atakuwa na jaha katika ulimwengu na Akhera na atakuwa ni miongoni mwa wenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama.
Na atasema na watu na hali yeye ni mtoto mchanga wa kunyonya kabla hajafikia wakati wa kusema. Na atawaita wao kwa Mwenyezi Mungu, akiwa mkubwa wakati ambapo nguvu zake zitakuwa zimeshikana na ubarobaro wake umekamilika, kwa yale aliyoletewa wahyi na Mwenyezi Mungu. Kusema huku ni kuhusu utume, ulinganizi na uongozi. Na yeye anahesabiwa kuwa ni mmoja wa watu wema na wenye utukufu wa maneno na vitendo.
Maryam alisema kwa kustaajabu, «Vipi mimi nitakuwa na mtoto na sina mume wala si malaya?» Malaika akamuambia, «Tukio hili kwako si jambo lililo mbali kwa Mwenyezi Mungu Muweza Ambaye Anakipatisha chochote anachokitaka kutokana na kisichokuweko. Akitaka kitu chochote kipatikane Anakiambia, «Kuwa,» nacho kikawa.
Na Atamfundisha kuandika, njia ya kuufikia usawa katika kusema na kutenda, Taurati ambayo Mwenyezi Mungu Alimletea Musa, amani imshukie, kwa njia ya wahyi, na Injili ambayo Mwenyezi Mungu Alimteremshia yeye.
Na Atamjaalia awe Mtume kwa Wana wa Isrāīl na atawaambia wao, «Mimi nimewajia na alama kutoka kwa Mola wenu inayoonesha kuwa mimi nimetumilizwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nayo ni kuwa nitawafanyia kwa udongo kitu chenye mfano wa ndege, nitapuliza ndani yake na kitakuwa ndege wa kikweli kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na nitamponya aliyezaliwa kipofu na mwenye barasi na nitamhuisha aliyekufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na nitawaambia chakula mnachokula na mnachoweka akiba majumbani mwenu. Hakika katika mambo makubwa haya, ambayo hayako kwenye uwezo wa wanaadamu, pana dalili kwamba mimi ni Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, iwapo nyinyi ni wenye kuamini hoja za Mwenyezi Mungu na alama Zake, ni wenye kukiri kumpwekesha.
«Na nimewajia nyinyi kuyasadikisha yaliyomo ndani ya Taurati, na ili niawahalalishie, kwa wahyi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu, baadhi ya yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia, yakiwa ni usahilishaji na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na nimewajia na hoja kutoka kwa Mola wenu ya ukweli wa ninayowaambia. Basi Mcheni Mwenyezi Mungu na msiende kinyume na amri Yake na mnitii mimi katika yale ninayowafikishia kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
«Hakika Mwenyezi Mungu Ambaye ninawalingania nyinyi Kwake Ndiye Peke Yake Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni Yeye. Mimi na nyinyi tuko sawa katika uja wetu na unyenyekevu wetu Kwake. Na hii ndio njia ambayo haina mpeteko.»
Alipohisi 'Īsā kutoka kwao ukakamavu juu ya ukafuri, aliita kwa watu wake halisi kwa kusema, «Ni nani atakayekuwa na mimi katika kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu.» Wale wasafiwa wa 'Īsā walisema, «Sisi ni wenye kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na wenye kuilingania, tumemuamini Mwenyezi Mungu na tumekufuata; na ushuhudie, ewe 'Īsā, kuwa sisi tumejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha na kumtii.
«Ewe Mola wetu! Tumeiamini Injili uliyoiteremsha na tumemfuata Mtume Wako 'Īsā, amani imshukie, basi tujaalie ni miongoni mwa waliokutolea ushahidi juu ya umoja Wako na kuwatolea ushahidi Manabii juu ya utume wao.» Nao ni ummah wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambao wanawatolea ushahidi mitume kuwa wao wamewafikishia ummah wao.
Wale waliomkanusha 'Īsā, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, walifanya vitimbi kwa kumpangia wenye kumuua. Mwenyezi Mungu akamtoa anayefanana na 'Īsā kwa mtu ambaye aliwaashiria wauaji kwake, wakamshika wakamuua na wakamsulubu wakidhani kuwa ni 'Īsā, amani imshukie. Na Mwenyezi Mungu ni bora wa wenye kufanya vitimbi. Katika haya pana kuthibitisha sifa ya makr (vitimbi) kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake, kwa kuwa ni vitimbi vya haki na ni katika kukabiliana na vitimbi vya wenye vitimbi.
Na vitimbi vya Mwenyezi Mungu kwao ni pale Aliposema Mwenyezi Mungu kumaambia 'Īsā, «Mimi nitakutwaa kutoka kwenye ardhi bila ya kupatikana na baya lolote, nitakuinua mpaka kwangu kwa mwili wako na roho yako, nitakuokoa na watu waliokukanusha na nitawafanya wale waliokufuata wewe, yaani,waliyo kwenye dini yako, na kufuata yale uliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya dini na bishara ya Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wakamuamini Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kutumilizwa kwake, wakashikamana na Sheria aliyokuja nayo, wawe na ushindi juu ya wale walioukanusha utume wako hadi Siku ya Kiyama; kisha mwisho wenu nyote mtarudi kwangu Siku ya Hesabu, ili nitoe uamuzi juu ya tafauti mliokuwa nazo kuhusu 'Īsā, amani imshukie.
«Ama wale waliomkanusha al- Masīḥ miongoni mwa Mayahudi, au wakamzidishia sifa miongoni mwa Wanaswara, nitawaadhibu adhabu kali katika ulimwengu: kwa kuuawa, kunyang’anywa mali na kuondolewa ufalme, na katika Akhera kwa Moto; na hawatakuwa na msaidizi mwenye kuwanusuru na kuwaepushia adhabu ya Mwenyezi Mungu.»
Na ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wakafanya matendo mema, Mwenyezi Mungu Atawapa thawabu za matendo yao zikiwa kamili zisizopunguzwa. Na Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kujidhulumu kwa ushirikina na ukafiri.
Hayo tuliyokusimulia kuhusu habari ya 'Īsā ni miongoni mwa dalili zilizo wazi za usahihi wa utume wako na usahihi wa Qur’ani yenye hekima inayopambanua baina ya haki na batili; haina shaka wala ubishi.
Hakika mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba 'Īlsa, bila ya baba, ni kama mfano wa Mwenyezi Mungu kumuumba Adam, bila ya baba wala mama. Mwenyezi Mungu Alimuumba kutokana na mchanga wa ardhi kisha Akamwabia, «kuwa kiumbe», akawa. Basi madai ya uungu wa 'Īsā kwa kuwa aliumbwa bila ya baba, ni madai ya urongo. Ādam, amani imshukie, aliumbwa bila ya baba wala mama, na wote wamekubaliana kwamba yeye ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu.
Haki isiyo na shaka kuhusu mambo ya 'Īsā ni ile iliyokujia, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako. Endelea kwenye yakini yako na juu ya msimamo ulionao wa kuacha uzushi. Na usiwe ni miongoni mwa wenye shaka. Katika haya pana kumtia moyo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumtuliza.
Basi yoyote mwenye kujadiliana nawe , ewe Mtume, kuhusu Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam, baada ya ujuzi uliokufikia juu ya ‘Īsā, amani imshukie, waambie, «Njooni tuwahudhurishe watoto wetu wa kiume na watoto wenu wa kiume, wanawake wetu na wanawake wenu na sisi wenyewe na nyinyi wenyewe, kisha tuelekee kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuomba Ayashukishe mateso Yake na laana Yake juu ya warongo katika maneno yao, wenye kukamaa katika upotofu wao.»
Hakika hili nililokuhadithia, ewe Mtume, kuhusu mambo ya ‘Īsā ndio habari ya kweli isiyo na shaka. Na hakuna muabudiwa anayestahiki ibada isipokuwa ni Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na hakika Mwenyezi Mungu Ndiye Mshindi katika ufalme Wake, Ndiye Mwenye hekima katika upelekaji mambo Wake na vitendo Vyake.
Na wakikataa kukuamini na kukufuata, basi wao ndio waharibifu. Na Mwenyezi Mungu Anawajua na Atawalipa kwa hilo.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, «Njooni kwenye neno la uadilifu na haki tushikamane nalo sote. Nalo ni sisi kuielekeza ibada yetu kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na tusimfanye yoyote kuwa ni mshirika pamoja na Yeye, awe ni sanamu au msalaba au Shetani au kinginecho. Na wala wasiwadhalilikie baadhi yetu watu wengine kwa kuwatii badala ya Mwenyezi Mungu.» Basi wakiukataa mwito huu mzuri, waambieni wao, enyi Waumini, «Kuweni ni mashahidi kwetu kuwa sisi tumejisalimisha kwa Mola wetu na tumenyosha shingo zetu Kwake kwa kukubali kuwa ni waja Wake na kwa kumtakasa.» Na mwito huu kwenye neno la sawa, kama unavyoelekezwa kwa Mayahudi na Wanaswara, unaelekezwa pia kwa wenye mwenendo kama wao.
Enyi watu wa vitabu vilivyoteremshwa, miongoni Mwa Mayahudi na Wanaswara, vipi kila mmoja kati yenu anabisha kwamba Ibrāhīm, amani imshukie, alikuwa kwenye mila yake. Ilhali Taurati na Injili hazikuteremshwa ela baada yake? Kwani hamufahamu upotofu wa maneno yenu kwamba Ibrāhīm alikuwa Myahudi au Mnaswara, na hali mnajua kuwa Uyahudi na Unaswara ulizuka baada ya kufa kwake kwa muda?
Ndio nyinyi enyi hawa, mliomjadili Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, juu ya mambo ya dini yenu ambayo muna ujuzi nayo, katika yale yaliyomo ndani ya vitabu vyenu mnayoitakidi usahihi wake. Lakini ni kwa nini nyinyi mnayajadili mambo ya Ibrāhīm ambayo hamuna ujuzi nayo? Na Mwenyezi Mungu Anayajua mambo pamoja na kuwa yamefichika, na nyinyi hamjui.
Ibrāhīm hakuwa ni Myahudi wala Mnaswara, kwa kuwa Uyahudi haukuwa, wala Unaswara, isipokuwa baada yake. Lakini alikuwa mfuasi na mtiifu wa amri ya Mwenyezi Mungu, aliyejisalimisha Kwake, na hakuwa ni miongoni mwa washirikina.
Hakika wenye haki zaidi na Ibrāhīm na wanaohusika naye zaidi ni wale waliomuamini, wakausadiki utume wake na wakaifuata dini yake na huyu Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na waliomuamini yeye.Na Mwenyezi Mungu ni Msaidizi wa wenye kumuamini yeye na kufuata Sheria Yake.
Lilitamani kundi la Mayahudi na Manaswara lau wangaliwapoteza nyinyi, enyi Waislamu, wakawatoa kwenye Uislamu. Wao hawampotezi yoyote isipokuwa nafsi zao na wafuasi wao; na wao hawalielewi hilo wala hawalijui.
Enyi watu wa Taurati na Injili! Vipi nyinyi mnakanusha aya za Mwenyezi Mungu ambazo aliziteremsha kwa Mitume wake katika Vitabu vyenu, na ndani yake muna kuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndiye Mtume anayengojewa na kuwa aliyowajia nayo ndio haki. Na nyinyi mnashuhudia hilo, lakini mnalikanusha.
Enyi watu wa Taurati na Injili! Kwa nini nyinyi mnachanganya haki iliyo ndani ya vitabu vyenu, kwa yale ya ubatilifu mliyoyapotosha na kuya kwa mikono yenu, na kuzificha kwenu sifa za Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ziliomo ndani ya vitabu hivyo viwili na (kuficha kwenu) kwamba Dini yake ndiyo ya haki, na hali nyinyi mnajua hilo?
Na pote la watu wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi lilisema, «Sadikini kilichoteremshwa kwa walioamini mwanzo wa mchana na mkanushe mwisho wake. Huenda wao wakafanya shaka juu ya dini yao na wakaiacha.
«Na msimsadiki kikweli isipokuwa yule aliyefuata dini yenu akawa Myahudi.» Waambie, ewe Mtume, «Uongofu na taufiki ni uongofu wa Mwenyezi- Mungu na taufiki Yake ya kuongoza kwenye Imani sahihi.» Na walisema, «Msiidhihirishe kwa Waislamu elimu mlionayo, wasije wakajifunza kutoka kwenu wakawa sawa na nyinyi katika kuijua na wakawa na ubora juu yenu au wakaichukua kuwa ni hoja kutoka kwa Mola wenu wakawashinda kwayo.» Waambie, ewe Mtume, «Fadhila na vipawa na mambo yote yako mkononi mwa Mwenyezi Mungu na yako chini ya uendeshaji Wake, Anampa Amtakaye miongoni mwa waliomuamini Yeye na Mtume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu na ni Mjuzi: Anawaenea, kwa elimu Yake na upaji Wake, viumbe Vyake vyote vinavyostahiki fadhila Zake na neema Zake.»
Mwenyezi Mungu Anawahusisha Anaowataka katika viumbe Wake kwa kuwapa utume na kuwaongoa kwenye Sheria kamilifu kabisa. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye ihsani na upaji mwingi wenye kuenea.
Na miongoni mwa Watu wa Kitabu, katika Mayahudi, kuna ambaye lau utamuamini kwa mali mengi atakutekelezea bila hiana. Na miongoni mwao kuna ambaye lau utamuamini kwa dinari moja hatakutekelezea, mpaka ufanye juhudi kubwa ya kumfuata. Sababu ya hilo, ni itikadi mbovu inayowafanya wajihalalishie mali ya Waarabu kwa njia ya batili. Na wanasema, «Hatuna dhambi wala kosa kwa kula mali yao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameyahalalisha kwetu.» Huu ni urongo wa kumzulia Mwenyezi Mungu; wanausema kwa ndimi zao na hali wanajua kuwa wao ni warongo.
Mambo si kama vile walivyodai hawa warongo. Mchaji-Mungu kikweli ni yule aliyetekeleza ahadi aliyomuahidi Mwenyezi Mungu ya kutekeleza amana na kumuamini Yeye na Mitume Wake na akajilazimisha kufuata uongofu Wake na Sharia Yake na akamuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa kufuata Aliyoamrisha na kujiepusha na Aliyokataza. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wachamungu wenye kujikinga na ushirikina na maasia.
Hakika wale ambao wanabadilisha ahadi ya Mwenyezi Mungu na wasia Wake Aliowausia katika Vitabu Alivowateremshia Mitume wao, kwa kupokea kitu kitwevu miongoni mwa vyombo vya ulimwengu na taka zake, wao hawana fungu la thawabu katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu Hatasema na wao maneno ya kuwafurahisha; wala hatawaangalia kwa jicho la huruma Siku ya Kiyama na wala Hatawasafisha kutokana na uchafu wa madhambi na ukafiri. Na watakuwa na adhabu yenye kuumiza.
Miongoni mwa Mayahudi kuna watu wanaoyapotoa maneno na kuyaondoa mahali pake. Na wanayabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, ili kuwafanya wasiokuwa wao wadhanie kuwa hayo ni miongoni mwa maneno yaliyoteremshwa katika Taurati, nayo si katika maneno yaliyomo kwenye Taurati kabisa, na wanasema, «Haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, yameletwa kwa Nabii Wake Mūsā kwa njia ya wahyi.» Nayo hayatoki kwa Mwenyezi Mungu. Na wao, kwa ajili ya ulimwengu wao, wanasema urongo kumzulia Mwenyezi Mungu, na hali wanajua kuwa wao ni warongo.
Haitakiwi kwa binadamu yoyote ateremshiwe kitabu na Mwenyezi Mungu chenye kutoa uamuzi kwa viumbe Wake na achaguliwe kuwa ni Nabii, kisha awaambie watu, «Niabuduni mimi badala ya Mwenyezi Mungu.» Lakini atasema, «Kuweni ni watu wa busara, wenye kuelewa na wajuzi wa wahyi wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, mliokuwa mkiwafundisha wengine na mnaousoma kwa kuuhifadhi, kuujua na kuuelewa..»
Na haikuwa kwa yoyote katika wao awaamrishe nyinyi kuwafanya Malaika na Mitume ni wola wasiokuwa Mwenyezi Mungu ambao nyinyi mnawaabudu. Je, inaingia akilini, enyi watu, yeye awaamrishe kumkanusha Mwenyezi Mungu baada ya kufuata kwenu amri yake?
kumbuka, ewe Mtume, pindi Alipochukua Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ahadi ya mkazo kwa Manabii wote kwamba, «Nikiwaletea Kitabu na hekima kisha akaja kwenu mjumbe kutoka kwangu, mwenye kusadikisha vitabu mlivyonavyo, mtamuamini na kumnusuru? Je, mumekiri na kukubali hilo na mumechukua juu yake ahadi yangu ya mkazo?» Wakasema, «Tumekubali hilo.» Akasema, «Kueni mashahidi, baadhi yenu juu ya wengine, na kueni mashahidi kwa hilo juu ya ummah wenu, na mimi ni Mwenye kushuhudia pamoja na nyinyi juu yenu na juu yao. Katika haya pana ahadi nzito Aliyoichukua Mwenyezi Mungu kutoka kwa kila Nabii amuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kuchukua ahadi nzito kutoka kwa ummah wa Manabii wote juu ya hilo.
Basi mwenye kuupa mgongo ulinganizi wa Uislamu baada ya maelezo haya na ahadi hii Aliyoichukuwa Mwenyezi Mungu kutoka kwa Manabii Wake, hao ndio wenye kutoka nje ya dini ya Mwenyezi Mungu na twaa ya Mola wao.
Je, wanataka hawa wenye kutoka nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa Watu wa Kitabu, dini isiyokuwa dini ya Mwenyezi Mungu nayo ni Uislamu ambao Mwenyezi Mungu Alimtumiliza nao Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hali ya kuwa wote walioko mbinguni na ardhini wamejisalimisha na kufuata na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu kwa hiyari, kama walivyo Waumini, na kwa kulazimika wakati wa shida ambapo hilo haliwanufaishi, nao ni makafiri, kama vilivyonyenyekea Kwake viumbe vyote. Na Kwake watarejeshwa Siku ya Marejeo, na alipwe kila mmoja kwa amali yake? Hili ni onyo kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa yoyote, katika viumbe Vyake, atakayerudi Kwake juu ya mila isiyokuwa ya Kiislamu.
Waambie, ewe Mtume, «Tumemuamini Mwenyezi mungu na tumetii. Hatuna Mola isipokuwa Yeye, na hatuna muabudiwa isipokuwa Yeye. Tumeuamini wahyi Aliouteremsha kwetu na ule Aliouteremsha kwa Ibrāhīm aliye rafiki halisi wa Mwenyezi Mungu, na wanawe wawili, Ismā'il na Is’ḥāq, na mwana wa mwanawe,Ya'qūb mwana wa Is’ḥāq, na Asbāṭ: nao ni Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili wanaotokana na watoto wa Ya'qūb, na wahyi uliopewa Mūsā na ‘Īsā wa Taurati na Injili, na wahyi Aliouteremsha Mwenyezi Mungu kwa Manabii Wake. Tunayaamini hayo yote. Wala hatumbagui yoyote katika wao. Na sisi tunamfuata Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa kumtii na kumuabudu, tunakiri Kwake kuwa Yeye Ndiye Mola, Ndiye Mungu na Ndiye wa kuabudiwa
Na Mwenye kutafuta dini isiyokuwa dini ya Kiislamu, ambayo ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha na kumfuata kwa kumtii na kumdhalilikia, na kwa Mtume wake aliye Nabii wa mwisho Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kumuamini na kumfuata na kumpenda kwa dhahiri na kwa siri, basi hiyo haitakubaliwa kwake, na yeye Akhera atakuwa ni miongoni mwa wenye kupata hasara ambao walizifanyia ubahili nafsi zao kwa kuzinyima mambo yenye kuzinufaisha.
Vipi Mwenyezi Mungu Atawaafikia, wamuamini Yeye na wamfuate, watu walioukanusha unabii wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kuuamini na kushuhudia kuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mkweli na yale aliyokuja nayo ni ya kweli na zikawajia wao hoja zinazotoka kwa Mwenyezi Mungu na dalili za usahihi wake? Na Mwenyezi Mungu Hawaafikii kwenye haki na usawa watu madhalimu, nao ni wale waliopotoka kwenye haki wakafuata batili, wakachagua ukafiri badala ya Imani.
Madhalimu hao, malipo yao ni kuwa wao watashukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote. Wao wamefukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu.
Ni wenye kukaa milele Motoni; hawataondolewa adhabu kidogo ili wapumzike wala hawatacheleweshewa kwa udhuru wowote watakaoutoa.
Isipokuwa waliorudi kwa Mola wao kwa kutubia kidhati baada ya ukafiri wao na udhalimu wao na wakayatengeneza, kwa toba yao, waliyoyaharibu. Mwenyezi Mungu Ataikubali hiyo toba, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya waja wake, ni Mwenye huruma kwao.
Hakika wale waliokufuru baada ya kuwa wao wameamini na wakaendelea kwenye ukafiri mpaka kufa, haitakubaliwa toba kutoka kwao mauti yakiwasimamia. Na wao ndio waliopotea njia wakakosa kuifikia.
Hakika wale waliokanusha unabii wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakafa juu ya kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, haitakubaliwa kutoka kwa mmoja wao, Siku ya Kiyama, dhahabu iliyojaa ardhi iwe ni fidia ya nafsi yake kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, lau atajikomboa nayo kikweli. Wao wana adhabu yenye kuumiza; na hawana yoyote wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Hamuwezi kupata Pepo ng’o! mpaka mtoe sadaka katika vile vitu mnavyovipenda. Na chochote mnachokitoa sadaka, kiwe ni kichache au ni kingi, basi Mwenyezi Mungu Anakijua mno na Atamlipa kila mtoaji malipo yanayolingana na kitendo chake.
Vyakula vyote vizuri vilikuwa ni halali kwa wana wa Ya'qūb, amani imshukiye, isipokuwa vile ambavyo Ya’qūb alijiharamishia yeye mwenyewe kwa sababu ya ugonjwa uliompata. Na hayo yalikuwa kabla ya Taurati haijateremshwa. Taurati ilipoteremshwa, Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia Wana wa Isrāīl baadhi ya vyakula vilivyokuwa halali kwao. Na hilo ni kwa sababu ya dhuluma zao na uovu wao. Waambie, ewe Mtume, «Ileteni Taurati na muyasome yaliyomo ndani yake iwapo muna hakika ya madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha humo uharamu wa aliojiharamishia Ya'qūb nafsi yake, ili mpate kuujua ukweli wa yale yaliyokuja katika Qur’ani ya kwamba Mwenyezi Mungu Hakuwaharamishia Wana wa Isrāīl chochote kabla ya kuteremka Taurati, isipokuwa yale ambayo Ya'qūb alijiharamishia nafsi yake.
Basi yule atakayemzulia Mwenyezi Mungu urongo baada ya kuisoma Taurati na ukweli kuwa wazi, basi hao ndio madhalimu wanaomzulia Mwenyezi Mungu ya batili.
Waambie, ewe Mtume, Mwenyezi Mungu Amesema kweli katika Aliyoyatolea habari na yale ya Sheria Aliyoipitisha. Basi iwapo nyinyi ni wakweli katika mahaba yenu na kujinasibisha kwenu na rafiki halisi wa Mwenyezi Mungu, Ibrāhīm, amani imshukiye, fuateni mila yake Aliyoipitisha Mwenyezi Mungu kupitia kwa ulimi wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kwani hiyo ndiyo haki isiyokuwa na shaka. Na wala hakuwa Ibrāhīm, amani imshukie, ni kati ya wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, katika kumpwekesha na kumuabudu, na yoyote.
Hakika nyumba ya mwanzo iliyojengwa kwa ajili ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ni hiyo nyumba ya Mwenyezi Mungu takatifu iliyoko Maka. Na nyumba hiyo imebarikiwa, mema huko huongezwa na rehema huko hushuka. Na katika kuielekea nyumba hiyo kwenye Swala na kuiendea kipindi cha kutekeleza Hija na Umra, pana wema na uongofu kwa watu wote.
Katika Nyumba hii kuna alama waziwazi ya kwamba hiyo ni katika ujenzi wa Ibrāhīm na kwamba Mwenyezi Mungu ameitukuza na kuipa heshima. Kati ya alama hizo ni Maqām ya Ibrāhīm, amani imshukie, nayo ni lile jiwe ambalo alikuwa akisimama juu yake wakati alipokuwa akiziinua nguzo za Alkaba, yeye na mwanawe Ismā'īl. Na yoyote mwenye kuingia Nyumba hii atapata amani ya nafsi yake, hapana yoyote atakayemkusudia kwa uovu. Na Mwenyezi Mungu Amewajibisha kwa mwenye uwezo katika watu, popote atakapokuwa kuiendea nyumba hii ili kutekeleza matendo ya Hija. Na yoyote mwenye kuikanusha faradhi ya Hija, basi huyo amekufuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi naye, Hana haja ya hija yake wala amali yake na wala Hana haja na viumbe vyake vyote.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia waliepewa vitabu kati ya Mayahudi na Wanaswara, «Kwa nini mnazikanusha hoja za Mwenyezi Mungu zinazojulisha kwamba dini ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu na mnayakanusha yaliyomo kwenye vitabu vyenu miongoni mwa dalili na hoja juu ya hilo hali ya kuwa nyinyi mnajua? Na Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya kitendo chenu mnachokifanya.» Katika haya, pana makemeo na ahadi ya adhabu kwao.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, «Mbona mnamzuia kuingia katika Uislamu yule mtu atakaye hivyo na mnamtakia upotofu na kupinduka kwenye lengo na muelekeo wa kisawa, na nyinyi mnajua kwamba niliyokuja nayo ndiyo haki?» Basi, Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika kwa mnayoyatenda, na Atawalipa kwa hayo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazitumia Sheria Zake kwa kuzifuata, iwapo mtalitii kundi la Mayahudi na Wanaswara, miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Taurati na Injili, watawapoteza na watawatia shaka katika dini yenu, ili mupate kurudi nyuma na kuikanusha haki baada ya kuwa mlikuwa waumini wa haki hiyo, basi msiwaamini juu ya dini yenu wala msiwakubalie rai yoyote au shauri.
Na vipi mtamkufuru Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, ilhali mnasomewa aya za Qur’ani, na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anazifikisha aya hizo kwenu? Na yoyote atakayetegemea kwa Mwenyezi Mungu, akashikamana na Qur’ani na mafundisho ya Mtume (Sunnah), basi huyo ameafikiwa kufuata njia iliyo wazi na mpango uliolingana sawa.
Enyi ambao mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake, muogopeni Mwenyezi Mungu kwa namna inavyopasa mumuogope. Nako ni Atiiwe wala Asiasiwe, Ashukuriwe wala asikufuriwe na Akumbukwe wala Asisahauliwe. Na dumuni katika kushikamana na Uislamu wenu mpaka mwisho wa uhai wenu, ili mkutane na Mwenyezi Mungu na nyinyi muko katika hali hiyo.
Shikamaneni nyote na Kitabu cha Mola wenu na uongofu wa Mtume wenu, wala msitende ambayo yatapelekea kutengana kwenu. Na ikumbukeni neema kubwa ambayo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha nayo, pindi mlipokuwa, enyi Waumini, kabla ya Uislamu ni maadui, Mwenyezi Mungu Akazikusanya nyoyo zenu juu ya kumpenda Yeye na kumpenda Mtume Wake, na akatia ndani ya nyoyo zenu mahaba ya kupendana wenyewe kwa wenyewe, hapo mkawa, kwa fadhila Zake, ni ndugu mpedanao. Na mlikuwa kwenye ukingo wa moto wa Jahanamu, Mwenyezi Mungu Akawaongoza kwa Uislamu na Akawaokoa na Moto. Na kama Mwenyezi Mungu Alivyowafunulia wazi alama za imani iliyo sahihi, hivyo hivyo Anawabainishia yote yale ambayo ndani yake muna kutengenea kwenu, mpate kuongoka kweye njia ya uongofu na mpate kuiandama ili msipotee mkaiepuka.
Na kiweko miongoni mwenu, enyi Waumini, kikundi kitakacholingania katika kheri, kiamrishe mema, nayo ni yale yanayojulikana uzuri wake kisheria na kiakili, na kikataze maovu, nayo ni yale yanayojulikana uovu wake kisheria na kiakili. Na hao ndio watakaofaulu kupata Pepo zenye neema.
Na wala msiwe, enyi Waumini, kama waliopewa vitabu, ambao ulizuka uadui kati yao na kuchukiana, wakatengana makundi na vyama mbalimbali na wakatafautiana kwenye misingi ya dini yao baada ya haki kuwa wazi kwao. Na hao wanastahili adhabu kubwa iumizayo.
Siku ya Kiyama zitakuwa nyeupe nyuso za watu wema ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata amri Yake; na zitakuwa nyeusi nyuso za watu waovu kati ya wale waliomkanusha Mtume Wake na wakaasi amri Yake. Basi wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeusi wataambiwa kwa kulaumiwa, «Je, mumekufuru baada ya kuamini kwenu, mkachagua ukafiri mkaacha Imani? Basi ionjeni adhabu kwa sababu ya ukafiri wenu.»
Ama wale ambao nyuso zao zitakuwa nyeupe kwa mn’garo wa neema na kwa yale mema ambayo walipewa bishara nayo, wao watakuwa katika Pepo ya Mwenyezi Mungu na starehe zake. Wao watasalia humo, hawatatoka humo milele.
Hizi ni aya za Mwenyezi Mungu na hoja Zake zenye kung’ara, tunakusomea na kukusimulia, ewe Mtume, kwa ukweli na yakini. Na Mwenyezi Mungu Hakuwa ni mweye kumdhulumu yoyote katika viumbe Wake wala si mwenye kupunguza chochote katika vitendo vyao, kwani Yeye ni Hakimu Mwenye uadilifu Asiyedhulumu.
Na ni Vyake, Yeye Mwenyezi Mungu Peke Yake, vyote vilivyo mbinguni na vilivyo ardhini, ni milki Yake Pekee kwa kuviumba na kuvisimamia. Na marejeo ya viumbe wote ni Kwake Yeye Peke Yake, na Atamlipa kila mmoja kwa kadiri anayostahiki.
Nyinyi, enyi uma wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni bora wa ummah na ni watu wenye manufaa zaidi kwa watu, mnaamrisha mema, nayo ni yale yanayofahamika uzuri wake kisheria na kiakili, na mnakataza maovu , nayo ni yale yanayoeleweka ubaya wake kisheria na kiakili, na mnamuamini Mwenyezi Mungu kikweli-kweli imani inayotiliwa nguvu na vitendo. Na lau kama Mayahudi na Wanaswara waliopewa Vitabu wangalimuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyowajia nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama mlivyoamini nyinyi, lingekuwa hilo ni bora kwao dunianina Akhera. Katiika hao wako Waumini waukubalio ujumbe wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanaoufuata kivitendo ujumbe huo, nao ni wachache. Na wengi wao ni watokaji nje ya dini ya Mwenyezi Mungu na twaa Yake.
Hawatawadhuru nyinyi hawa watu waovu, miongoni mwa watu waliopewa Vitabu, isipokuwa kile kitakachoyaudhi masikizi yenu cha matamshi ya ushirikina na ukafiri na mengineyo. Na wakiwapiga vita, watashindwa na watakimbia hali ya kuwapa mgongo, kisha hawatapata ushindi juu yenu kwa hali yoyote.
Amejaalia Mwenyezi Mungu utwevu na unyonge kuwa ni jambo lenye kuambatana nao Mayahudi na wala haliwaepuki. Kwa hivyo, wao daima ni madhalili wenye kudharauliwa popote waliopo, isipokuwa watakapokuwa na mafungamano na Mwenyezi Mungu na makubaliano na watu ambayo kwayo watajiwekea usalama wa nafsi zao na mali zao. Hayo ndiyo mapatano ya kujidhamini kwao na kujilazimisha kwao kufuata hukumu za Uislamu. Na wamerudi nyuma wakiwa wamepata hasira za Mwenyezi Mungu zilizowastahili. Na wamepigwa na unyonge na umasikini. Kwa hivyo, humuoni Myahudi isipokuwa utamkuta ameshukiwa na hofu na babaiko kwa kuwaogopa Waumini. Hilo ndilo Alilowajaalia Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu, kukeuka kwao mipaka Yake na kuwaua kwao Manabii, kwa udhalimu na uonevu. Na hakuna lolote lililowafanya wao wawe majasiri wa kuyatenda haya isipokuwa ni kule kufanya kwao maasia na kukiuka kwao mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Waliopewa Vitabu hawako sawa: kati yao liko kundi lifuatalo njia iliyolingana sawa juu ya amri ya Mwenyezi Mungu, lenye kumuamini Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ambalo watu wake wanasimama usiku wakizisoma aya za Qur’ani tukufu na wakielekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuomba katika Swala zao.
Wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wanaamrisha mambo ya kheri yote na wanakataza aina zote za shari na wanakimbilia kufanya mema. Hao ni miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu wema.
Na kitendo chochote, kichache au kingi, kati ya vitendo vyema yatakayofanywa na kikundi hiki kilichoamini, hakitapotea mbele ya Mwenyezi Mungu. Bali watashukuriwa na watapewa malipo yake. Mwenyezi Mungu Anawajua zaidi wacha-Mungu ambao wametenda mema na wakajitenga na yaliyoharamishwa kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kutaka thawabu Zake.
Hakikia wale waliozikufuru aya za Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume Wake, mali yao wala watoto wao havitawatetea wao kivyovyote wasipatwe na adhabu ya Mwenyezi Mungu, duniani wala Akhera. Hao ni watu wa Motoni watakaodumu humo pasi na kutoka.
Mfano wa wanachokitoa makafiri, katika mambo ya kheri, katiika maisha haya ya ulimenguni na thawabu wanazozitumaini, ni mfano wa upepo ulio na baridi kali uliovuma juu ya mashamba ya watu waliokuwa wanangojea kwa hamu matokeo mema ya upepo huo. Na kwa sababu ya madhambi yao, upepo huo haukubakisha chochote. Na makafiri hawa, hawatapata thawabu huko Akhera. Na Mwenyezi Mungu hatakuwa Amewadhulumu kwa hilo, lakini ni wao walijidhulumu nafsi zao kwa ukafiri wao na kuasi kwao.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msiwafanye makafiri kuwa ni wategemewa, kinyume cha Waumini, mkawa mnawapa siri zenu. Kwani wao hawakomi kuziharibu hali zenu, na wanayafurahia madhara na maovu yanayowafika. Zimedhihiri chuki nyingi katika maneno yao. Na yanayofichwa na nyoyo zao ya uadui kwenu ni makubwa zaidi na ni mazito. Kwa hakika, tushawaelezea nyinyi alama na hoja za uovu wao ili mpate kuwaidhika na muwe na tahadhari, iwapo mnayatia akilini mawaidha ya Mwenyezi Mungu, amri Zake na makatazo Yake.
Huu ndio ushahidi wa makosa yenu kwa kuwapenda wao. Nyinyi mnawapenda na mnawafanyia wema, na wao hawawapendi. Na wanawabebea nyinyi uadui na chuki, ilhali nyinyi mnaviamini vitabu vyote vlivyoteremshwa, kikiwemo kitabu chao, na wao hawakiamini kitabu chenu. Basi vipi mtawapenda? Na wanapokutana na nyinyi wanasema kinafiki, «Tumeamini na tumesadiki.» Na wanapokuwa faragha, wenyewe kwa wenyewe, yaonekena wana kero na masikitiko. Hapo huwa wakiziuma ncha za vidole vyao, kutokana na hasira kali walionayo juu ya mshikamano wa Waislamu, kuwa neno lao ni moja, kuwa Uislamu umepata nguvu na kuwa wao wamekuwa wanyonge kwa sababu ya kupata nguvu Uislamu. Waambie, ewe Mtume, «Kufeni kwa hasira zenu kali mlizonazo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yanayofichwa ndani ya vifua na Atamlipa kila mmoja kwa aliyoyatanguliza ya kheri au ya shari.»
Na miongoni mwa uadui wa watu hawa ni kwamba nyinyi, enyi Waumini, mpatwapo na jambo jema la ushindi au ngawira, wao hupatwa na butwaa na huzuni; iwapo mtapatwa na maudhi ya kushindwa au upungufu wa mali, watu na matunda, wao hulifurahia hilo. Na mkiwa na subira juu ya yaliyowafika na mkamuogopa Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha na Akawakataza nayo, hautawadhuru udhia wa vitimbi vyao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyazunguka yote wanayoyafanya hao makafiri ya uharibifu na Atawalipa kwayo.
Na kumbuka,ewe Mtume, pindi ulipotoka nyumbani kwako, ukiwa umevaa mavazi ya vita, huku wazipanga safu za Masahaba wako, na unamuweka kila mmoja mahali pake ili kukutana na washirikina katika vita vya Uhud. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzisikia kauli zenu, ni Mwenye kuvijua vitendo vyenu.
Kumbuka, ewe Mtume, yale mambo yaliyowahusu kina Banū Salimah na Banū Ḥārithah wakati walipowaza kurudi nyuma, wao na kiongozi wao, mnafiki Abdullāh bin Ubayy bin Salūl, kwa kuogopa kukutana na adui. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwalinda na Akawahifadhi wakaenda pamoja na wewe wakimtegemea Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na wajitegemeze Waumini.
Hakika Mwenyezi Mungu Aliwanusuru nyinyi, enyi Waumini, katika Badr juu ya maadui zenu washirikina pamoja na uchache wa idadi yenu na vifaa vyenu. Kwa hivyo, muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kutekeleza amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake, ili mpate kumshukuria neema Zake.
Kumbuka, ewe Nabii, yale yaliyowahusu Masahaba wako kwenye vita vya Badr pindi walipoona uzito katika nafsi zao kwa kuwa Makureshi wamepata msaada wa kivita, na Sisi tukakuletea Wahyi uwaambie, «Kwani hauwatoshi msaada wa Mola wenu wa kuwaletea Malaika elfu tatu walioteremshwa kutoka mbinguni mpaka kwenye sehemu ya vita wakawa wanawapa moyo na wanapigana pamoja na nyinyi?»
Ndio, unawatosha nyinyi msaada huu. Na kuna bishara nyingine kwenu, iwapo mtakuwa na subira ya kupambana na maadui zenu na mkamuogopa Mwenyezi Mungu kwa kuyatenda Aliyowamrisha na kuyaepuka Aliyowakataza. Na watakuja makafiri wa Maka kwa haraka kupigana na nyinyi, wakidhani kwamba wao watawamaliza. Mwenyezi Mungu Atawapa nyinyi msaada wa Malaika elfu tano wakiwa wamejitia alama zilizo wazi, wao na farasi wao.
Na Mwenyezi Mungu Hakuuleta msaada huu wa Malaika isipokuwa ni kwa ajili ya kuwapa bishara kwa msaada huo na ili nyoyo zenu zitulie na ziwe nzuri kwa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwenu. Na msaada wa hakika unatoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye kushinda Ambaye Hashindwi, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na matendo Yake.
Na ilikuwa nusura ya Mwenyezi Mungu katika vita vya Badr ni kwa ajili Apate kukiangamiza kikundi cha makafiri kwa kuuawa na yule atakayeokoka na kifo kati yao, basi atarudi akiwa na huzuni, upetwe na dhiki za nafsi yake na unaonekana kwake utwevu na aibu.
Huna, ewe Mtume, katika mambo ya waja chochote kile. Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, Asiyekuwa na mshirika. Na huenda, baadhi ya hawa waliokupiga vita, vifua vyao vikaufungukia Uislamu, wakasilimu na Mwenyezi Mungu Akazikubali toba zao. Na yule atakayesalia katika ukafiri wake, Mwenyezi Mungu Atamuadhibu duniani na Akhera kwa sababu ya udhalimu wake na uadui wake.
Ni vya Mwenyezi Mungu Pekee vilioko mbinguni na vilioko ardhini; Anamsamehe Amtakaye kati ya waja Wake kwa rehema Zake na Anamuadhibu Amtakaye kwa uadilifu Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya waja Wake na ni Mwenye huruma kwao.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, tahadharini na aina zote za riba na msichukue katika mkopo zaidi ya rasilmali zenu, hata kama ni kidogo. Basi itakuwaje iwapo ziada hiyo itaongezeka kila ufikapo muda wa kulipa deni? Na muogopeni Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kufuata Sheria Zake ili mpate kufaulu duniani na Akhera.
Na jiwekeeni kizuizi baina yenu na moto ambao umeandaliwa makafiri.
Na mtiini Mwenyezi Mungu, enyi waumini, katika yale Aliyowaamrisha kwayo ya twaa nay ale Aliyowakataza nayo ya kula riba na mengineyo. Na mtiini Mtume ili mpate kurehemewa na msiiadhibiwe.
Na kimbilieni, kwa kumtii kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ili kupata msamaha mkubwa utokao kwa Mola wenu na mpate Pepo kunjufu, upana wake ni sawa na mbingu na ardhi, Ameiandaa Mweyezi Mungu kwa wachamungu.
Wale ambao wanatoa mali yao katika hali ya wepesi na uzito, na wanaozuia hasira zilizo ndani ya nafsi zao kwa kusubiri, na wanaowasamehe waliowadhulumu wanapokuwa na uwezo. Huu ndio wema ambao Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kuwa nao.
Na wale ambao wakitenda dhambi kubwa au wakizidhulumu nafsi zao kwa kutenda dhambi chini ya hizo, wanaikumbuka ahadi ya Mwenyezi Mungu ya malipo mema kwa wanaomtii na malipo mabaya kwa wanaomuasi na wanaelekea kwa Mola wao hali ya kutubia wakawa wanamuomba Awasamehe madhambi yao na wakawa wana yakini kwamba hapana anayasamehe madhambi isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na wao kwa sababu hiyo hawaendelei kwenye maasia, na wao wanajua kwamba wakitubia Mwenyezi Mungu Atawakubalia toba yao.
Hao waliosifiwa kwa sifa hizo, malipo yao ni kwamba Mwenyezi Mungu Atayasitiri madhambi yao na watapata mabustani ya Peponi ambayo maji tamu yatakuwa yanapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, ilhali ya kukaa humo milele; hawatotoka humo kamwe. Na malipo bora ya wenye kutenda mema ni msamaha na Pepo.
Mwenyezi Mungu Anawazungumzia Waumini walipopatwa na mikasa siku ya vita vya Uhud kwa kuwaliwaza kwamba wamepita kabla yao ummah wengi ambao waumini kati yao walitahiniwa kwa kupigana na makafiri na ukawa ushindi ni wao. Basi, tembeeni katika ardhi mkizingatia yale yaliyowafika wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na na Mtume Wake.
Hii Qur’ani ni ufafanuzi uliyo wazi na ni uongozi kwenye njia ya haki na ni ukumbusho ambao nyoyo za wachamungu zainyenyekea. Nao (hao wachamungu) ni wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu. Wamehusishwa nayo (hiyo Qur’ani kuwa nyoyo zao zinainyenyekea na kuikubali) kwa kuwa wao ndio wanaofaidika nayo, si wengine.
Wala msidhoofike, enyi Waumini, kupigana na maadui wenu, wala msihuzunike kwa yaliyowapata huko Uhud. Na nyinyi ndio washindi na mwisho mwema ni wenu iwapo mtamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mtafuata Sheria Zake.
Iwapo yatawapata, enyi Waumini, majaraha au mauaji kwenye vita vya Uḥud, na mkahuzunika kwa hilo, washirikina pia walipatwa na majaraha na mauaji kama hayo katika vita vya Badr. Hizo ni siku Mwenyezi Mungu huzigeuza kati ya watu: wakati mwengine kushinda na wakati mwengine kushindwa. Kwani katika hayo kuna hekima, mpaka yadhihiri yale Aliyoyajua Mwenyezi Mungu hapo azal (kale isiyokuwa na mwanzo), ili Mwenyezi Mungu Ampambanue aliyekuwa mkweli wa Imani na asiyekuwa mkweli, na ili Awakirimu watu miongoni mwenu kwa kuwafanya wafe mashahidi. Na Mwenyezi Mungu Hawapendi waliozidhulumu nafsi zao na wakakaa kwa kuacha kupigana katika njia Yake.
Na kushindwa huku kuliotokea katika vita vya Uhud kulikuwa ni kuwafanyia mtihani, kuwasafisha Waumini, kuwatakasa na wanafiki na ni maangamivu kwa makafiri.
Enyi Maswahaba wa Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie! Kwani mnadhani kwamba mtaingia Peponi na bado hamjapewa mitihani ya vita na mambo mazito? Haitapatikana kwenu kuingia Peponi tu, hivi hivi, mpaka mjaribiwe na Awajuwe Mwenyezi Mungu, ujuzi ulio wazi kwa viumbe, wale wapiganao jihadi kati yenu katika njia Yake na wenye subira ya kupambana na maadui.
Na kwa hakika mlikuwa, enyi Waumini, kabla ya vita vya Uhud mnatamani kukutana na maadui zenu, ili mpate utukufu wa jihadi na kufa mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu ambao walibahatika nao ndugu zenu kwenye vita vya Badr. Basi hilo ndilo, Iimeshapatikana kwenu, mlilolitamani na mkaliomba. Basi jitokezeni mpigane na msubirishane.
Hakuwa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kiumbe aina nyingine, isipokuwa yeye ni Mtume wa jinsi ya Mitume wengine waliokuweko kabla yake, afikisha ujumbe wa Mola wake. Basi iwapo atakufa, kwa kumalizika muda wake, au atauawa, kama walivyoeneza uvumi maadui, kwani mtarudi nyuma na kuacha dini yenu na kuyaacha aliyowaletea Mtume wenu? Basi yoyote miongoni mwenu atakayerudi nyuma akaiacha dini yake, yeye hatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote, bali ataidhuru nafsi yake madhara makubwa. Ama atakayekuwa na msimamo imara juu ya Imani yake na akamshukuru Mola wake juu ya neema ya Uislamu, hakika Mwenyezi Mungu Atamlipa malipo mazuri kabisa.
Hakuna yoyote atakayekufa isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na makadirio Yake na mpaka aufikishe muda ambao Mwenyezi Mungu Amempangia. Hayo ni maandishi yaliyopangiwa wakati. Na yoyote ambaye kwa vitendo vyake anataka manufaa ya duniani, tutampa tulichomgawia cha riziki, na hatakuwa na fungu lolote kesho Akhera. Na yoyote ambaye anataka kwa vitendo vyake malipo ya Mwenyezi Mungu huko Akhera , tutampa kile alichokitaka na tutampa malipo yake kamili pamoja na fungu lake duniani la riziki alilogawiwa. Kwani huyu kwa utiifu wake na jihadi yake ametushukuru; na wenye kushukuru tutawalipa mema.
Wengi kati ya Mitume waliotangulia, walipigana pamoja nao makundi mengi ya watu waliowafuata. Hawakudhoofika kwa yale yaliyowapata ya majaraha au mauaji, kwani hayo yalikuwa katika njia ya Mola wao. Wala hawakulemewa wala hawakumnyenyekea adui yao, bali walisubiri kwa yaliyowapata. Na Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kusubiri.
Na halikuwa neno la hawa wenye kusubiri isipokuwa ni kusema, «Ewe Mola wetu! Tusamehe madhambi yetu na yaliyotokea kwetu ya kuruka mipaka katika mambo ya dini yetu na uzithibitishe nyayo zetu, tusipate kukimbia tunapopigana na adui yetu na utunusuru na yule anayepinga umoja wako na unabii wa Manabii wako.
Basi Aliwapa Mwenyezi Mungu, wale wenye kusubiri, malipo yao duniani kwa kuwanusuru na maadui zao, kwa kuwafanya wakae kwa utulivu katika ardhi na kwa malipo mema yaliyo makubwa Akhera, nayo ni mabustani ya Peponi yaliyojaa neema. Na Mwenyezi Mungu Anampenda kila mtenda wema katika kumuabudu Mola wake na kuamiliana kwake na viumbe Wake.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo! Iwapo mtawatii walioukanusha uungu wangu na wasiwaamini Mitume wangu, miongoni mwa Mayahudi, Wanaswara, wanafiki na washirikina, katika yale wanayowaamrisha nyinyi nayo na wanayowakataza nyinyi nayo, watawapoteza njia ya haki na mtaritadi muache dini yenu na mrudi na hasara iliyo wazi na maangamivu ya kikweli.
Hakika wao hawatawanusuru nyinyi; bali Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuwanusuru na Ndiye Mnusuru bora Asiyehitajia nusura ya mtu Mwengine.
Tutatia fazaa na hofu kubwa katika nyoyo za waliokufuru, kwa sababu ya kumshirikisha kwao Mwenyezi Mungu na wale wanaodaiwa kuwa ni waungu. Wao hawana dalili au hoja kuwa waungu hao wana haki ya kuabudiwa pamoja na Mwenyezi Mungu. Basi hali yao hapa duniani ni papatiko na babaiko kwa kuwaogopa Waumini. Ama mahali pao watakaposhukia Akhera ni Moto. Na hili ni kwa sababu ya udhalimu wao na uadui wao. Na makao maovu kwao ni makao haya.
Na kwa hakika Aliwahakikishia nyinyi Mwenyezi Mungu yale Aliyowaahidi ya kuwanusuru pindi mlipokuwa mnawaua makafiri katika vita vya uhud kwa idhini Yake Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Mpaka mlipokuwa waoga, mkawa madhaifu wa kupigana na mkatafautiana: je, mtasalia kwenye sehemu zenu za kivita au mtaziacha, ili mkusanye ngawira pamoja na wanaokusanya? Na mkaiasi amri ya Mtume wenu alipowaamrisha msiondoke kwenye sehemu zenu kwa vyovyote vile. Hapo ndipo pigo la kushindwa likawapata baada ya kuwaonesha mnayoyapenda ya ushindi, na ikadhihirika kuwa kati yenu kuna wanaotaka ngawira na kati yenu kuna wanaotaka Akhera na malipo yake. Kisha Mwenyezi Mungu Aliziepusha nyuso zenu na maadui wenu ili awape mtihani. Kwa hakika Aliyajua Mwenyezi Mungu majuto yenu na toba yenu, ndipo Akawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa kwa Waumini.
Kumbukeni, enyi maswahaba wa Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hali zenu zilivyokuwa, mlipokuwa mnalipanda jabali mkiwakimbia maadui zenu, wala hamgeuki kumwangalia yoyote kwa sababu ya yale yaliyowafikia ya babaiko, kuogopa na fazaa. Na huku Mtume wa Mwenyezi Mungu , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, amekita kwenye uwanja wa vita, anawaita nyuma yenu kwa kuwaambia, «Njooni kwangu, enyi waja wa Mwenyezi Mungu,» hali ya kuwa nyinyi hamsikii wala hamuangalii. Hapo yakawa malipo yenu ni kupatwa na machungu, dhiki na kero. Aliyafanya hayo Mwenyezi Mungu ili msihuzunike kwa mliyoyakosa ya ushindi na ngawira wala yaliyowafikia ya kuingiwa na kicho na kushindwa. Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa matendo yenu yote; hakuna chochote katika hayo kinachofichika Kwake.
Kisha ikawa ni katika rehema ya Mwenyezi Mungu kwa waumini waliomtakasia nia kwamba Aliingiza kwenye nyoyo zao , baada ya kero na usumbufu uliowafika, utulivu na Imani thabiti kuhusu ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao. Miongoni mwa alama za utulivu huo ni usingizi uliolifinika kundi katika wao, nalo ni lile la wale waliokuwa na ikhlasi na yakini kwa Mola wao. Na kundi lingine ilikuwa hamu ya watu wake ni kuziokoa nafsi zao; azma yao ilikuwa dhaifu, wakashughulishwa na nafsi zao na wakawa na dhana mbaya kwa Mola wao, kwa Dini Yake na kwa Mtume Wake.Wakadhani kwamba Mwenyezi Mungu Hatalitimiza jambo la Mtume Wake na kwamba Uislamu hautasimama ukaimarika. Kwa hivyo, utawaona ni wenye majuto juu ya kutoka kwao. Na huwa wakiambiana wao kwa wao, «Je tulikuwa na chaguo lolote katika kutoka kwetu kwenda kupigana?» Waambie, ewe Mtume, «Mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Yeye Ndiye Aliyepanga kutoka kwenu na (Ndiye Aliyepanga yale) yaliyowafikia.» Nao wanayaficha katika nafsi zao wasiyoyadhihirisha kwako ya majuto juu ya kutoka kwao kwenda mapiganoni. Huwa wakisema, «Lau kama tungalikuwa na hiyari japo ndogo, hatungeuawa hapa.» Waambie, «Ajali ziko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hata kama mlikuwa majumbani mwenu, na Mwenyezi Mungu Akakadiria mufe, wangalitoka wale ambao Mwenyezi Mungu Amewakadiria mauti, kwenda pale watakapouawa.» Na Hakuyafanya hayo Mwenyezi Mungu isipokuwa ni kuwapa nyinyi mtihani juu ya yaliyomo ndani ya vifua vyenu ya shaka na unafiki na ili Ampambanue mwema na maovu na lipate kudhihirika kwa watu jambo la Muumini na lile la mnafiki, la maneno na vitendo. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa yaliyomo kwenye nyoyo za viumbe Wake. Hakuna chochote, katika mambo yao, kinachofichika Kwake.
Hakika wale waliokimbia kati yenu, enyi Maswahaba wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwenye vita siku waliokutana Waumimini na washirikina katika vita vya Uhud, ni Shetani ndiye aliyewatosa kwenye dhambi hili kutokana na baadhi ya madhambi waliyoyafanya. Kwa kweli Mwenyezi Mungu Amewasamehe na hakuwaadhibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Msamaha kwa wenye madhambi wanaotubia, ni Mpole Asiyekuwa na haraka ya kuwatesa wenye kumuasi.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata Sheria Zake kivitendo, msijifananishe na makafiri ambao hawamuamini Mola wao. Kwani wao huwaambia ndugu zao, miongoni mwa makafiri, wanapotoka kwenda kutafuta maisha yao katika ardhi au wanapokuwa pamoja na wapiganaji, wakafa au wakauawa, «Lau kama hawa hawangetoka wala hawangepigana na wakabakia pamoja na sisi, hawangekufa wala hawangeuawa.» Neno hili linawaongezea machungu, maudhiko na majuto yanayobakia katika nyoyo zao. Ama Waumini, wao wanajua kwamba hili limetokana na kadara ya Mwenyezi Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu Huziongoza nyoyo zao na Huwasahilishia misiba. Na Mwenyezi Mungu Anambakisha hai yule Aliyemkadiria kuishi, hata kama ni msafiri au ni mpiganaji. Na Anamfisha yule ambaye muda wake wa kuishi umekoma, hata kama ni mkazi wa mji. Na Mwenyezi Mungu kwa kila mlifanyalo ni Mwenye kuliona, na Atawalipa kwalo.
Na iwapo mtauawa, enyi Waumini, katika hali ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu au mkafa vitani, Mwenyezi Mungu Atawasamehe madhmbi yenu na Atawarehemu rehema itokayo Kwake. Hapo mtafaulu kwa kuyapata mabustani ya Peponi yenye starehe nyingi. Hayo ni bora kuliko dunia na wanavyovikusanya wapenda dunia.
Na iwapo ajali zenu zitakoma katika haya maisha ya dunia na mkafa juu ya matandiko yenu au mkauawa katika uwanja wa mapigano, ni kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Mtakusanywa; na huko Atawalipa kwa matendo yenu mliyoyatenda.
Na kwa ajili ya rehema za Mwenyezi Mungu kwako na maswhaba wako, ewe Nabii, Mwenyezi Mungu Alikuneemesha ukawa laini kwao. Na lau ungalikuwa na tabia mbaya, mwenye moyo mgumu, maswahaba wako wangalijitenga na kuwa mbali na wewe. Kwa hivyo, usiwe na hasira nao kwa yaliyotokea kwao katika vita vya Uhud. Basi muombe Mwenyezi Mungu, ewe Nabii, Awasamehe na uwashauri katika mambo yanayohitajia ushauri. Na utakapoazimia kufanya jambo kati ya mambo yoyote, baada ya kushauri, litekeleze hali ya kumtegemea Mwenyezi Mungu, Peke Yake. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda wenye kujitegemeza Kwake.
Iwapo Mwenyezi Mungu Atawapa msaada na nusura Yake, hapana yoyota awezaye kuwashinda. Na iwapo Atawaacha kuwasaidia na kuwanusuru, basi ni nani awezaye kuwanusuru nyinyi baada ya Yeye kuacha kuwanusuru? Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, nawajitegemeze Waumini.
Haiwi kwa Mtume kuwafanyia hiana maswahaba wake kwa kutwaa kitu katika ngawira ambayo Mwenyezi Mungu Hakumtengea. Na yoyote mwenye kulifanya hilo, miongoni mwenu, atakuja Siku ya Kiyama akiwa amekibeba kile alichokitwaa, ili afedheheshwe nacho mbele ya kila mtu katika kisimamo kinachojumuisha watu wote. Kisha itapewa kila nafsi malipo kamili ya ilichokichuma pasi na kupunguzwa wala kufanyiwa dhuluma.
Yule ambaye lengo lake ni radhi za Mwenyezi Mungu, halingani na yule ambaye ametopea kwenye maasia na kumkasirisha Mola wake na akastahiki kwa hilo makazi ya Jahanamu ambayo mwisho mbaya wa mtu kuishilia ni hapo.
Watu wa Peponi wenye kufuata yenye kumridhisha Mwenyezi Mungu wanatafautiana daraja. Na watu wa Motoni wanaofuata yenye kumkasirisha Mwenyezi Mungu wanatafautiana katika matobwe. Wao hawalingani. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuziona amali zao, hakifichiki chochote Kwake katika matendo yao.
Hakika Mwenyezi Mungu Amewapa neema Waumini, miongoni mwa Waarabu, Alipomtumiliza Mtume atokaye katika jinsi yao, akawa anawasomea wao aya za Qur’ani, anawatakasa na ushirikina na tabia mbaya na anawafundisha Qur’ani na Suna, pamoja na kwamba kabla ya Mtume huyu walikuwa kwenye upotevu na ujinga ulio wazi.
Kwa nini mlipopatwa na msiba uliowakumba siku ya Uhud, ingawa mumewapata washirikina mara mbili yake siku ya Badr, mlisema kwa kustaajabu, «Mambo haya yatakuwa vipi, na sisi ni Waislamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu yuko na sisi, na hawa ni washirikina?» Sema uwaambie, ewe Nabii, «Haya yaliyowapata yamesababishwa na nyinyi wenyewe kwa kuenda kinyume kwenu na amri ya Mtume wenu na kuelekea kwenu kukusanya ngawira.» Kwa hakika, Mwenyezi Mungu Anafanya Atakalo na Anahukumu Atakavyo. Hakuna mwenye kuitangua hukumu Yake.
Na yale yaliyotokea kwenu ya majaraha au ya mauaji katika vita vya Uhud, siku ulipokutana mkusanyiko wa Waumini na mkusanyiko wa washirikina, na ukawa ushindi, mwanzo wa vita, ni wa Waumini kisha, mara ya pili, ukwa ni wa washirikina, yote hayo yalikuwa kwa uamuzi wa Mwenyezi Mungu na mpango Wake, ili yajitokeze yale Aliyoyajua Mwenyezi Mungu tangu kale, ili Awapambanue Waumini wa kweli miongoni mwenu.
Na ili Awapambanue wanafiki ambao Mwenyezi Mungu Ameyafungua wazi yaliyomo ndani ya nyoyo zao, walipokuwa Waumini wawaambia, «Njooni mpigane pamoja na sisi katika njia ya Mwenyezi Mungu au kuweni ni msaada kwetu kwa kutufanya tuwe wengi.» Wakasema, «Lau kama tunajua kuwa nyinyi mtapigana na yoyote tungalikuwa na nyinyi dhidi yao.» Wao katika ukafiri, siku hii ya leo, wako karibu zaidi kuliko kuwa wao wako karibu na Imani.Kwani wao wanayasema kwa midomo yao yasiokuwa kwenye nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu Anayajua zaidi wanayoyaficha vifuani mwao.
Wanafiki hawa ndio wale walioketi wakawaambia ndugu zao waliopata msiba pamoja na Waislamu kwenye vita vyao na washirikina siku ya Uhud, «Lau kama watu hawa wangalitutii hawangaliuawa.» Sema, ewe Mtume, uwaambie «Zizuieni nafsi zenu na kifo, ikiwa nyinyi ni wa kweli katika madai yenu kwamba wao kama wangaliwatii hawangaliuawa na kwamba mumeokoka na mauti kwa kukaa kwenu kutokwenda vitani.»
Wala usidhani, ewe Mtume, kwamba wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni wafu hawahisi chochote. Bali wao wako hai uhai wa barzakh kwenye ujirani wa Mola wao Ambaye walipigana jihadi kwa ajili Yake na wakafa katika njia Yake, inawapitia riziki yao huko Peponi na wananeemeshwa.
Furaha iliwaenea, wakati Mola wao Alipowaneemesha na kuwapa neema na radhi zenye kuwaliwaza macho yao, zikiwa ni miongoni mwa ukarimu Wake na takrima Yake. Watakuwa wakiwafurahia ndugu zao wenye kupigana jihadi waliowaacha duniani wakiwa hai, wakiwatarajia wafaulu kama walivyofaulu wao. Kwa kuwa wao waelewa kwamba hao ndugu zao, waliowaacha duniani wakiwa hai, watapata heri waliyoipata wao, iwapo watakufa mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu hali ya kumtakasia Yeye, na kwamba hawatakuwa na chochote cha kuogopa kuhusu mambo ya mustakbali wao huku Akhera wanayoyakabili wala hawatakuwa na huzuni juu ya yale yaliyowapita wakayakosa ya hadhi za kilimwengu.
Hakika wao watakuwa wamejawa na furaha kwa neema za Mwenyezi Mungu na vipawa Vyake vingi na hakika Mwenyezi Mungu Hayapotezi malipo ya ya wenye kumuamini, bali Anayakuza na kuyaongeza kwa fadhila Zake.
Wale waliouitikia mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakatoka kuwafuata washirikina mpaka kijiji cha Ḥamrā’ al-Asad baada ya kushindwa katika vita vya Uḥud, pamoja na maumivu na majaraha waliyokuwa nayo, wakafanya upeo wa juhudi zao na wakashikamana na mwongozo wa Mtume wao, basi watenda wema hao na wacha-Mungu hao watapata thawabu kubwa.
Wao ni wale walioambiwa na baadhi ya washirikina , «Abu Sufyani na wenzake wameamua kuwarudia nyinyi ili kuwamaliza, basi jihadharini nao na mjikinge na kukutana nao, kwani hamna nguvu za kupambana nao.» Tahadhari hiyo iliwazidishia yakini na kuikubali kikweli ahadi ya Mwenyezi Mungu kwao na haikuwazuia na uamuzi wao. Hapo walikwenda wakielekea pale Mwenyezi Mungu Alipotaka na wakasema, «Ḥasbunā Allāh wa Ni’ma al Wakīl» Yaani, Mtosheleza wetu ni Mwenyezi Mungu na Yeye Ndiye Wakili mwema Mwenye kutegemezewa mipango ya waja Wake.
Basi wakarudi kutoka Ḥamrā’ al Asad kuja Madina wakiwa wana neema za Mwenyezi Mungu kwa kupata thawabu nyingi na nyongeza za daraja ya juu zitokazo Kwake, huku Imani na yakini zimeongezeka kwao, maadui wa Mwenyezi Mungu wamewadhalilisha, wamefaulu kwa kusalimika na kuuawa na kupigana, na wamefuata mambo ya kumridhisha Mwenyezi Mungu kwa kumtii Yeye na Mtume Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye ihsani na vipawa vingi vyenye kuwaenea wao na wengineo.
Hakika anyewazorotesha nyinyi katika hilo ni Shetani. Amewajia kuwafanya nyinyi muwaogope wasaidizi wake. Basi msiwaogope washirikina, kwani wao ni wanyonge, hakuna mwenye kuwanusuru. Niogopeni mimi kwa kuelekea kwangu kwa utiifu, iwapo nyinyi kweli mnaniamini na mnamfuata Mtume wangu.
Wasikutie huzuni moyoni mwako hawa makafiri, ewe Mtume, kwa kukimbilia kwao kukanusha na kuingia kwenye upotevu. Hakika wao, kwa hilo, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Hakika ni kwamba wao wazidhuru nafsi zao kwa kuzinyima utamu wa Imani na thawabu kubwa. Mwenyezi Mungu Anataka Asiwape malipo mema yoyote huko Akhera, kwa kuwa wao wamejiepusha na ulinganizi wa haki. Na wao watapata adhabu kali.
Hakika wale walioibadili Imani kwa kuandama ukafiri, hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Bali madhara ya kitendo chao yatawarudia wenyewe. Na huko Akhera watapata adhabu iumizayo.
Wala wasidhani wakanushaji kwamba sisi tukiwarefushia umri wao, tukawastarehesha kwa starehe za duniani na tusiwaadhibu kwa ukafiri wao na madhambi yao kwamba watakuwa wamepata heri ya nafsi zao. Hakika tunawacheleweshea adhabu na ajali zao ili wazidishe dhuluma na ukeukaji mipaka. Na watapata adhabu yenye kuwadhalilisha na kuwatweza.
Hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaacha , enyi wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wenye kuzifuata Sheria Yake kivitendo, juu ya hivyo mlivyo ya kuchanganyikana mwenye Imani na mnafiki, mpaka Ampambanue muovu na mwema, ili ajulikune mnafiki na Muumini mkweli. Na haikuwa ni katika hekima ya Mwenyezi Mungu, enyi Waumini, kwamba Atawafunulia ghaibu Anayoijua kuhusu waja Wake, mkamjua Muumini kati yao na mnafiki. Lakini Yeye Anawapambanua kwa misukosuko na mitihani. Isipokuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anamteua Amtakaye katika wajumbe Wake ili kumuonesha ujuzi wa ghaibu kwa wahyi utokao Kwake. Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na iwapo mtaamini, imani ya kweli, na mkamuogopa Mola wenu kwa kumtii, mtapata malipo makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wala wasidhani wale wanaozifanyia ubakhili neema za Mwenyezi Mungu Alizowaneemesha kwa kuwafadhili kwamba ubakhili huo ni bora kwao. Bali hiyo ni shari kwao. Kwani mali hayo waliyoyakusanya yatakuwa ni kitanzi cha moto kitakachowekwa shingoni mwao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Ndiye Mwenye kumiliki ufalme ; na Yeye Ndiye Atakayesalia baada ya kutoweka viumbe Wake wote. Yeye Ndiye Mtambuzi wa matendo yenu yote, na Atamlipa kila mtu kwa kadiri anayostahiki.
Hakika Amelisikia Mwenyezi Mungu neno la Mayahudi ambao walisema, «Mwenyezi Mungu ni muhitji kwetu, Anatutaka tumkopeshe mali, na sisi ni matajiri.» Tutaliandika neno hili walilolisema na tutaandika kwamba wao wako radhi na yale yaliyofanyika ya kwamba mababa zao waliwaua Manabii wa Mwenyezi Mungu kwa dhuluma na uadui. Tutawaadhibu kwa hilo huko Akhera na tutawaambia, nao wamo Motoni waadhibiwa, «Ionjeni adhabu ya Moto unaounguza.»
Adhabu hiyo kali ni kwa sababu ya yale mliyoyatanguliza katika maisha yenu ya duniani kati ya maasia ya kimaneno, ya kivitendo na ya kiitikadi, na kwamba Mwenyezi Mungu si Mwenye kuwadhulumu waja Wake.
Mayahudi hawa walipoitwa kuufuata Uislamu, walisema, «Mwenyezi Mungu Ametuusia katika Taurati kwamba tusimsadiki yoyote atakayetujia na neno la kwamba yeye ni mjumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu mpaka atuletee sadaka, ambayo kwayo atajisogeza karibu na Mwenyezi Mungu, hapo ushuke moto kutoka mbinguni uiteketeze.» Sema uwaambie,ewe Mtume, «Nyinyi ni warongo kwa hayo mnayoyasema. Kwani mababa zenu kabla yangu walijiliwa na Mitume, wakiwa na hoja na dalili za ukweli wao na pia hayo mliyoyasema ya kuleta sadaka ambayo itateketezwa na moto. Basi mbona mababa zenu waliwaua Mitume hao, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu?»
Basi ikiwa Mayahudi hawa na makafiri wengineo watakukanusha, ewe Mtume, hakika wabatilifu wamewakanusha Mitume wengi kabla yako waliowajia kaumu zao kwa miujiza mingi yenye kushinda, hoja zilizo wazi, vitabu vya mbinguni ambavyo ni nuru inayoondosha giza na Kitabu chenye ufafanuzi, kilicho wazi.
Nafsi yoyote, hapana budi, itayaonja mauti. Na kwa hivyo, viumbe wote watarudi kwa Mola wao ili Awahesabu. Na kwa hakika mtalipwa malipo yenu kikamilifu Siku ya Kiyama juu ya vitendo vyenu bila kupunguziwa. Basi yule ambaye Mola wake Atamkirimu, Akamuokoa na Moto na Akamtia Peponi, huyo atakuwa amepata upeo wa ayatakayo. Na hayakuwa maisha ya duniani isipokuwa ni kiliwazo cha kuondoka. Basi msighurike nayo.
Mtapewa mtihani, tena mtapewa mtihani, enyi Waumini, katika mali yenu kwa kutakiwa mtoe matumizi ya wajibu na yanayopendekezwa na kwa mikasa inayoyakumba. Pia mtapewa mtihani katika nafsi zenu kwa kutakiwa mtekeleze ya wajibu ya kumtii Mwenyezi Mungu na kwa misiba inayowafikia ya majaraha au mauaji na kuwakosa vipenzi vyenu. Hilo litaendelea mpaka apambanuke mwenye imani ya kweli na mwenginewe. Na mtasikia, tena mtasikia, kutoka kwa Mayahudi, Wanaswara na washirikina maneno yatakayoudhi masikizi yenu katika matamshi ya ushirikina na kuitukana dini yenu. Na iwapo mtasubiri, enyi Waumini, juu ya hayo yote na mkamcha Mwenyezi Mungu kwa kujilazimisha kumtii Yeye na kujiepusha na kumuasi, hakika hilo ni miongoni mwa mambo ambayo yanakusudiwa kidhati na kushindaniwa.
Na kumbuka, ewe Mtume, pindi Mwenyezi Mungu Alipochukua ahadi ya mkazo juu ya wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, Mayahudi walipewa Taurati na Wanaswara walipewa Injili, ili wavitumie na wawafahamishe watu yaliyomo ndani yake wala wasiyafiche. Lakini wao waliiacha ahadi hiyo na hawakujilazimisha nayo. Na wakachukua thamni duni ikiwa ni badali ya wao kuificha haki na kukipotoa Kitabu. Ni mabaya yalioje manunuzi waliyonunua ya kuipoteza kwao ahadi na kubadilisha kwao Kitabu.
Wala msiwadhanie wale wanaofurahia matendo maovu waliyoyafanya, kama Mayahudi, wanafiki na wengineo, na wakawa wanapenda kuwa watu wawataje vizuri kwa mambo ambayo hawakuyafanya, basi msiwadhanie wao kuwa ni wenye kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu duniani. Na watakuwa na adhabu iumizayo kesho Akhera. Katika haya kuna onyo kali kwa kila mwenye kutenda kitendo kiovu na kukifurahia na kwa kila mwenye kujigamba kwa ambacho hakukifanya ili watu wamsifu na kumshukuru.
Ni wa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, ufalme wa mbinguni na ardhini na vilivyomo humo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Hakika, katika kuziumba mbingu na ardhi, pasi na kuwa na mfano uliotangulia, na katika kufuatana usiku na mchana na kutafautiana kwao, urefu na ufupi, pana dalili na hoja kubwa zinazobainisha upweke wa Mwenyezi Mungu kwa walio na akili timamu.
Ambao wanamtaja Mwenyezi Mungu katika hali zao zote, wakiwa wamesimama, wakiwa wameketi na wakiwa wamelala kwa mbavu zao, huku wana mazingatio juu ya uumbaji wa mbingu na ardhi hali ya kusema, «Ewe Mola wetu, Hukuuleta uumbaji huu kwa upuzi; Wewe Umetakasika na hilo! Basi tuepushie adhabu ya Moto.
«Ewe Mola wetu! Tuokue na Moto, kwani hakika Wewe, ewe Mwenyezi Mungu, yoyote Utakayemuingiza Motoni kwa madhambi yake, ushamfedhehesha na kumtweza. Na watenda madhambi, wanaozidhulumu nafsi zao, hawatakuwa na yoyote wa kuwatetea wasipate adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama.
«Ewe Mola wetu! Sisi Tumemsikia mlinganizi, naye ni Mtume wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, anawaita watu wakuamini Wewe na kukubali Umoja wako na kuzifuata kivitendo Sheria zako, tukauitikia ulinganizi wake na tukauamini utume wake. Basi tusamehe madhambi yetu, uzisitiri aibu zetu na utukutanishe na watu wema.
«Ewe Mola wetu! Tupe yale uliyotuahidi kwenye ndimi za Mitume wako, ya kupata ushindi, umakinifu, taufiki na uongofu. Wala usitufedheheshe, kwa madhambi yetu, Siku ya Kiyama. Hakika wewe ni Mkarimu, Huendi kinyume na ahadi ulizowaahidi waja wako.»
Na Mwenyezi Mungu Akaitikia maombi yao kwamba Yeye Hazipotezi juhudi za yoyote aliyetenda amali njema, awe ni mwanamume au ni mwanamke. Kwani wao, katika undugu wa kidini, kukubaliwa amali zao na kulipwa kwazo, ni sawa. Kwa hivyo, wale waliohama kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, wakatolewa kwenye majumba yao, wakaudhiwa katika kumtii Mola wao na kumuabudu kwao Yeye Peke Yake, wakapigana na wakauawa katikia njia ya Mwenyezi Mungu kwa kulikuza neno Lake, hao Mwenyezi Mungu Atawapa sitara kwa maasia waliyoyafanya kama Alivyowasitiri nayo duniani na Hatawahesabu kwayo. Na atawaingiza, tena Atawaingiza, kwenye mabustani ya Peponi ambayo inapita mito chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Hayo yakiwa ni malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo mazuri.
Usihadaike, ewe Mtume, kwa yale waliyonayo wenye kumkufuru Mwenyezi Mungu, ya ukunjufu wa riziki, hali nzuri ya maisha na kuhama kwao kutoka mahali kwenda pengine kwa ajili ya biashara na kutaka faida na mali. Kwa muda mchache, yote hayo yatawaondokea na watakuwa ni wenye kufungika na kuwekwa dhamana kwa vitendo vyao viovu.
Hiyo ni starahe ndogo yenye kuondoka.Kisha marejeo yao Siku ya Kiyama ni Motoni. Na huo Moto ni tandiko ovu mno.
Lakini wale waliomuogopa Mola wao , wakazifuata amri Zake na wakajiepusha na makatazo Yake, Mwenyezi Mungu Amewaandalia mabustani ya Pepo ambayo mito inapita chini ya majumba yake ya fahari na miti yake. Mabustani hayo yatakuwa ni makazi yao ya kudumu; hawatatoka humo. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa zaidi na bora zaidi kwa watiifu kuliko yale ya starehe za ulimwengu ambazo hao waliokufuru wanatanga huku na kule kwa kuzitafuta.
Baadhi ya waliopewa vitabu wanamuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola Mmoja na Mungu Mwenye kuabudiwa, wanaiamini Qur’ani mliyoteremshiwa nyinyi na Taurati na Injili walizoteremshiwa wao, hali ya kumdhalilikia Mwenyezi Mungu na kumnyenyekea. Hawazibadilishi aya za Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo ya takataka za duniani wala hawayafichi Aliyoyataremsha Mwenyezi Mungu na wala hawayapotoshi kama wanavyofanya wengineo miongoni mwa waliopewa Vitabu. Hao watapata thawabu kubwa mbele ya Mola wao Siku ya kukutana Naye, na watapewa malipo yao kamili, bila ya kupunguzwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu. Hakumshindi Yeye kuyadhibiti matendo yao na kuwahesabu wao kwayo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, kuweni na subira juu ya kumtii Mola wenu na juu yaliyowashukia ya madhara na shida, na washindeni maadui zenu katika kusubiri wasipate kuwa wasubirifu zaidi kuliko nyinyi, na simameni wima katika kumpiga vita adui yangu na adui yenu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, katika hali zenu zote, ili mfaulu kupata radhi Zake ulimwenguni na Akhera.