ترجمة سورة البقرة

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة البقرة باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

“Alif Lām Mīm” Herufi hizi na nyinginezo, miongoni mwa herufi zilizotajwa mwanzo wa sura, zinaashiria kuwa Qur’ani haigiziki. Washirikina waliwekewa biri walete kitu kama Qur’ani, wakashindwa kushindana nayo, paomoja na kuwa imebuniwa na herufi hizi hizi ambazo Waarabu wanazitumia. Kulemewa kwa Waarabu kuja na Qur’ani kama hii, ingawa walikuwa ni mafasaha wa watu, ni dalili ya kuwa Qur’ani ni wahyi (wahy) utokao kwa Mwenyezi Mungu.
Qurani hii ni kitabu kisicho na shaka kuwa kinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Haifai kwa mtu yoyote kufanya shaka juu yake kwa uwazi wake. Wananufaika kwayo wenye uchajimungu (taqwā), wenye kujikinga kwa elimu yenye manufaa na amali njema, na wao ndio wanaomuogopa Mwenyezi Mungu na kufuata hukumu Zake.
Nao ndio wanao amini ghaibu (ghayb), ambayo haifikiliwi na hisia zao na akili zao pekee, kwa kuwa haijulikani isipokuwa kupitia wahyi wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukie, kama kuamini Malaika, pepo, moto, na mengineyo katika yale yaliyoelezwa na Mtume Wake, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye. Imani (Īmān) ni neno lililokusanya kumkubali Mwenyezi Mungu, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Siku ya Mwisho na Kadari (Qadar), kheri yake na shari yake. Na kutilia nguvu kukubali huko kwa maneno na vitendo, kwa moyo, ulimi na viungo. Na wao, pamoja na kuamini kwao mambo ya ghaibu yasiyoonekana, wanasimamisha Swala kwa kuchunga nyakati zake na kuzitekeleza ipasavyo kulingana na sheria ya Mwenyezi Mungu kwa Nabii wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye yeye. Kadhalika, katika kile tulichowapa wao, miongoni mwa mali, wanatoa sadaka ya mali zao ya wajibu na ya suna.
Na wao ndio ambao wanayaamini yaliyoteremshwa kwako, ewe Mtume, ya Qurani, na yalioteremshwa kwako ya hekima, ambayo ni Sunnah, na Vitabu vyote vilivyoteremshwa kwa Mitume kabla yako, kama Taurati, Injil na vinginevyo, na wanaiamini Nyumba ya Maisha baada ya kufa na yaliyomo ndani ya Nyumba hiyo ya kuhesabiwa na kulipwa. Wanaamini hayo kwa nyoyo zao, imani ya kidhati inayodhihiri kwenye ndimi zao na viungo vyao. Kutajwa Siku ya Mwisho mahususi ni kwa sababu kuiamini ni mojawapo ya vitu vikubwa zaidi vyenye kusukuma na kuhimiza kufanya vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, kujiepusha na vitendo vya haramu na kuifanyia hesabu nafsi.
Wenye sifa hizi wako kwenye nuru inayotoka kwa Mola wao na taufiki inayotoka kwa Muumba Wao na Mwongozi Wao. Wao ndio wenye kufuzu, waliopata matakwa yao na kuokoka na shari ya vitu walivyovikimbia.
Hakika wale walioyakanusha yalioteremshwa kwako kutoka kwa Mola Wako, kwa njia ya kiburi na ujeuri, hakutapatikana kuamini kutoka kwao; ni sawa kwao ukiwa utawatisha na kuwaonya adhabu ya Mwenyezi Mungu au utaacha kufanya hivyo, kwa sababu wao wameamua kukakamia kwenye njia yao ya batili.
Mwenyezi Mungu amewapiga muhuri nyoyo zao, masikizi yao na ameweka finiko juu ya macho yao ya kuonea kwa sababu ya ukafiri na ujeuri walionao, baada ya haki kuwabainikia. Mwenyezi Mungu hakuwaafikia kwenye uongofu. Wao watapata adhabu kali katika Moto wa Jahanamu.
Miongoni mwa watu kuna kundi linalokuwa katika hali ya kutokuwa na uamuzi, linasimama baina ya Waumini na makafiri, nao ni wanafiki wanaosema kwa ndimi zao, “Tumemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho,’ na hali wao, katika undani yao, ni warongo, hawakuamini.
Wanaitakidi, kwa ujinga wao, kuwa wao wanamdanganya Mwenyezi Mungu na Waumini, kwa kudhihirisha kwao Imani na kuficha kwao ukafiri, na wao hawamdanganyi yoyote isipokuwa nafsi zao wenyewe, kwa kuwa madhara ya kudanganya kwao yanawarudia wao. Na kwa kuwa ujinga wao umekolea na nyoyo zao zimeharibika, huwa hawana hisia ya hilo.
Ndani ya nyoyo zao kuna shaka na uharibifu, ndipo wakaomjwa kwa kufanya maasia yenye kuwafanya wastahiki kuadhibiwa, na Mwenyezi Mungu akawazidishia shaka. Watakuwa na adhabu yenye uchungu kwa sababu ya urongo na unafiki wao.
Wanapopewa nasaha wakome kufanya uharibifu katika ardhi kwa kukanusha na kuasi kutoa siri za Waumini na kuwategemea makafiri, huwa wakisema kwa urongo na kubisha, “Sisi ndio watu wakutengeneza.”
Hili wanalolifanya na kudai kuwa ni utengefu ndio uharibifu wenyewe, lakini wao, kwa ujinga wao na ujeuri wao, hawana hisia ya hilo.
Na waambiwapo wanafiki, “Aminini kama walivyoamini masahaba, nako ni kuamini kwa moyo, ulimi na viungo,” huwa wakibisha na kusema, “Basi, tuamini kama vile madhaifu wa akili na maoni walivyoamini, tuwe kama wao katika upumbavu?” Mwenyezi Mungu aliwajibu kwamba udhaifu wa akili na maoni ni wao peke yao. Na wao hawajui kuwa msimamo walionao ndio upotevu na hasara.
Hawa wanafiki wakikutana na waumini huwa wakisema, “Tumeiamini Dini ya Uislamu kama nyinyi,” na wakiondoka kwenda kwa viongozi wao makafiri wasiomjalli Mwenyezi Mungu, huwa wakiwahakikishia kuwa wao wako kwenye mila ya ukafiri, hawajaiacha, na kuwa wao walikuwa wakiwacheza shere waumini.
Mwenyezi Mungu anawacheza shere wao na kuwapa muhula, ili wazidi kupotea, kuwa na shaka na kutokuwa na uamuzi, na Atawalipa kwa kuwacheza shere kwao Waislamu.
Hao ndio wanafiki. Wamejiuza wenyewe katika mapatano ya hasara. Walichukuwa ukafiri na kuacha Imani. Hawakupata faida yoyote, bali walipata hasara ya kukosa uongofu. Huko ndiko kupata hasara kukubwa.
Hali ya wanafiki ambao wameuamini, kidhahiri sio kindani, utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, kisha wakakanusha, wakawa wanaenda huku na kule kwenye giza la upotevu wao bila kujua wanapoenda wala kuwa na matarajio ya kutoka kwenye giza hilo, inafanana na hali ya kikundi cha watu, kwenye usiku wa giza, ambapo mmoja wao aliwasha moto mkubwa ili wapate joto na mwangaza. Moto ulipowaka na kung’arisha pambizo zake, ulizimika na giza likaenea. Wakawa watu hao wako kwenye giza, hawaoni chochote wala hawaongoki kupajua penye njia ya kujua matoko.
Wao ni viziwi, hawaisikii haki kwa kuizingatia, ni mabubu, hawaitamki haki, ni vipofu, hawauoni mwangaza wa uongofu. Kwa hivyo, hawawezi kurudi kwenye Imani ambayo waliiacha na kuchukuwa upotevu badali yake.
Au hali yao inafanana na hali ya kikundi kingine cha wanafiki ambao haki inawadhihirikia wakati mwengine, na huwa na shaka nayo wakati mwengine. Hali yao ni ile ya watu wanaotembea jangwani, wakanyeshewa na mvua nyingi, iliyofuatana na giza lingi lililopandana, mpigo wa radi pamoja na mng’aro wa pepe na vimondo vyenye kuchoma. Hivyo vinawafanya wao, kwa vituko vyake, kuweka vidole vyao kwenye masikio yao, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu Amewazunguka makafiri, hawamponyoki wala hawamshindi.
Hizo pepe, kwa mng’aro wake, zinakaribia kuwatoa macho yao. Pamoja na hivyo, kila pepe ikiwang’arishia njia, wanatembea kwenye mwangaza wake, na ikiondoka, njia huwa na giza ikawabidi wasimame pale waliopo. Lau si Mwenyezi Mungu kuwapa muda, Angewaondolea masikizi yao ya kusikia na macho yao ya kuonea. Na Yeye ni mwenye uweza wa kufanya hilo wakati wowote. Yeye ni Muweza wa kila kitu.
Mwito utokao kwa Mwenyezi Mungu kwa binadamu wote: Muabuduni Mwenyezi Mungu Ambaye Amewalea kwa neema zake, na mumuogope wala msiende kinyume na dini Yake. Kwani yeye ndiye Aliyewaumba kutoka kwenye hali ya kutokuwako, na Akawaumba waliokuwa kabla yenu, ili muwe ni miongoni mwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu ambao Yeye Ameridhika nao na wao wameridhika na Yeye.
Mola wenu ni Yule Aliyewafanyia ardhi iwe ni tandiko, ili maisha yenu yawe mepesi juu yake, na mbingu ziwe zimejengeka madhubuti, na Akateremsha mvua kutoka kwenye mawingu, Akatoa kwa mvua hiyo matunda na mimea aina mbalimbali ili iwe ni riziki kwenu. Basi, msimuwekee Mwenyezi Mungu washirika katika ibada, hali nyinyi mnajua kuwa Mwenyezi Mungu Amepwekeka katika kuumba, kuruzuku na kustahiki kuabudiwa.
Na mkiwa, enyi makafiri, muna shaka juu ya Qurani tuliyomteremshia mja wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani imshukie, na mkadai kuwa haitoki kwa Mwenyezi Mungu, basi leteni sura moja inayofanana na sura ya Qurani, na takeni msaada kutoka kwa yoyote mnayemuweza ili awasaidie, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.
Mkiwa hamuwezi sasa, na hamtaweza wakati unaokuja kabisa, basi uogopeni Moto, kwa kumuamini Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumtii Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.
Waambie, ewe Mtume, watu wa Imani na amali nzuri, habari yenye kuwajaza furaha, kuwa wao huko Akhera watakuwa na Mabustani ya ajabu, ambayo inapita mito chini ya majumba yake makubwa na miti yake yenye vivuli. Kila Anapowaruzuku Mwenyezi Mungu humo aina yoyote ya matunda yenye ladha, watasema, “Mwenyezi Mungu Alituruzuku aina hii ya matunda kipindi cha nyuma.” Watakapoionja wataikuta ni tafauti tamu yake na ladha yake, ingawa inafanana na aina iliyopita kwa rangi, sura na jina. Na katika hayo Mabustani ya Peponi watakuwa na wake waliosafishika na kila aina ya uchafu, wa nje, kama mkojo na damu ya hedhi, na wandani, kama kusema urongo na kuwa na tabia mbaya. Na wao, katika Pepo na starehe zake, watakaa milele, hawafi humo wala hawatoki.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Halionei haya jambo la haki lolote kulitaja, liwe ni kubwa au dogo, hata kama ni kukipigia mfano kitu kidogo sana, kama mbu na nzi na mfano wake, katika vitu Alivyovipigia mfano Mwenyezi Mungu kuonyesha kushindwa kwa kila kitu kinachoabudiwa kisichokuwa Mwenyezi Mungu. Ama waumini, wao wanajua hekima ya Mwenyezi Mungu katika kupigia mfano kitu kikubwa au kidogo miongoni mwa viumbe Vyake. Ama makafiri, wanafanya maskhara na kusema, “Ni nini lengo la Mwenyezi Mungu kupigia mfano vidudu hivi vitwevu?” Mwenyezi Mungu anawajibu kwamba makusudio ni kuwafanyia mtihani na kupambanua Mwenye Imani na kafiri. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu, kwa mifano hii, anawaepusha na haki watu wengi, kwa kuifanyia kwao maskhara, na Anawapa taufiki kwayo wengineo kupata nyongeza ya Imani na uongofu. Na Mwenyezi Mungu Hamdhulumu yeyote, kwani Hawaepushi na haki isipokuwa wenye kutoka nje ya utiifu Kwake.
Wale ambao wanavunja ahadi ya Mwenyezi Mungu Aliyoichukuwa kwao kuwa wampwekeshe Yeye na wamtii, hali ya kuwa Ameiitilia mkazo ahadi hiyo kwa kuleta Mitume na kuteremsha vitabu, na wanaenda kinyume na dini ya Mwenyzi Mungu, kama kukata zao na kueneza uharibifu katika ardhi. Basi wao ndio wenye hasara duniani na Akhera.
Vipi mtaukanusha, enyi washirikina, umoja wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kumshirikisha mwengine katika Ibada, pamoja na kuwa kuna dalili zisizopingika kuhusu hilo katika nafsi zenu? Mlikuwa hamko, hamjaumbwa, Akawafanya muweko kwa kuwaumba, Akapuliza kwenu uhai, kisha Atawafisha baada ya kumalizika muda wenu wa kuishi Aliowaekea, kisha Atawarudisha mkiwa na uhai Siku ya Kufufuliwa, kisha mtarejeshwa Kwake mhesabiwe na mlipwe.
Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Aliyeumba kwa ajili yenu kila kilichoko kwenye ardhi miongoni mwa neema ambazo mnanufaika nazo, kisha Akaelekea na kukusudia kuumba mbingu, Akazifanya mbingu saba. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kitu, na elimu Yake, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, imevizunguka vitu vyote Alivyoviumba.
Kumbuka, ewe Mtume, Aliposema Mola wako kuwaambia Malaika, “Mimi nitawaweka watu kwenye ardhi, ili waiimarishe kwa kupishana: wakiondoka watu watakuja wengine baada yao.” Wakasema, “Ewe Mola wetu! Tufundishe na utuongoze, ni kwa hekima gani kuwaumba hawa, pamoja na kuwa mambo yao yatakuwa ni kuleta uharibifu katika ardhi na kumwaga damu kwa dhulma na uonevu, na hali sisi tuko chini ya amri yako: tunakuepusha na mabaya maepusho yanayonasibiana na Sifa zako njema na utukufu Wako, na tunakusifu kwa kila sifa za ukamilifu na utukufu?” Mwenyezi Mungu Akasema kuwaambia, “Mimi najua msiyoyajua kuhusu uzito wa maslahi katika kuwaumba wao.”
Na ili kubainisha utukufu wa Ādam, Amani imshukiye, Mwenyezi Mungu Alimfundisha majina ya vitu vyote, kisha Akaviorodhesha hivyo vitu kwa Malaika na kuwaambia, “Niambieni majina ya vitu hivi vilivyoko, ikiwa nyinyi ni wakweli kwamba nyinyi mnastahiki zaidi uimarishaji wa ardhi kuliko wao.”
Malaika walisema, “Tunakuepusha na kila sifa pungufu, ewe Mola wetu! Sisi hatuna ujuzi isipokuwa ule uliyotufundisha. Wewe, Peke Yako, Ndiye Mjuzi wa mambo ya viumbe vyako, Ndiye Mwenye Hekima katika uendeshaji Wako.”
Mwenyezi Mungu Alisema, “Ewe Ādam! Waambie majina ya vitu hivi ambayo walishindwa kuyajua.” Ādam alipowaambia hayo majina, Mwenyezi Mungu Alisema kuwaambia Malaika, “Niliwaambia kuwa Mimi ninayajua yaliyofichika kwenu, ya mbinguni na ardhini, na ninayajua mnayoyafanya kwa dhahiri na mnayoyafanya kwa siri.”
Na taja kwa watu, ewe Mtume, takrima ya Mwenyezi Mungu kwa Ādam Aliposema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwaambia Malaika, “Msujudieni Ādam kwa njia ya kumheshimu na kuonyesha fadhila zake.” Wote walitii amri, isipokuwa Iblisi alikataa kusujudu kwa sababu ya kiburi na uhasidi, akawa ni miongoni mwa wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, wenye kuasi amri Yake.
Mwenyezi Mungu Akasema, “Ewe Ādam! Kaa wewe na mkeo Ḥawwā’ kwenye pepo na stareheni kwa matunda yake kwa furaha na ukunjufu popote pale mnapotaka humo, na tahadharini na mti huu, msije mkaingia katika maasia mkawa ni wenye kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu.”
Shetani akawaingiza makosani, kwa kuwashawishi mpaka wakala katika ule mti, ikasababisha kutolewa kwao kwenye Pepo na starehe zake. Na Mwenyezi Mungu Aliwaambia, “Shukeni ardhini, mkiteta nyinyi kwa nyinyi- yaani: Ādam, Ḥawwā’ na Shetani-, na nyinyi katika hiyo ardhi muna utulivu na makao na kunufaika kwa vilivyomo mpaka muda wa maisha yenu ukome.”
Ādam alipokea matamko ya kuomba ili akubaliwe, aliyoletewa na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya ilham (ilham), yaliyokusanya toba na kutaka msamaha, nayo ni neno Lake Aliyetukuka, “Ewe Mola wetu! Tumejidhulumu nafsi zetu. Na Usipotusamehe na Kuturehemu, hakika tutakuwa ni miongoni mwa waliyopata hasara.” (7:23). Mwenyezi Mungu Alikubali toba yake na Akamsamehe. Kwani Yeye, Aliyetukuka, ni Mwingi wa kukubali toba ya Mwenye kutubia miongoni mwa waja Wake na ni Mwenye Kuwarehemu.
Tulisema, “Shukeni kutoka Peponi nyote! Na utawajia, nyinyi na vizazi vyenu vinavyofuatia, ujumbe wenye mambo ya kuwaongoza kwenye haki. Wenye kuufuata huo kwa vitendo, hawatakuwa na hofu kuhusu mustakbala wao wa Akhera, wala hawatakuwa na huzuni juu ya vitu walivyovikosa vya ulimwenguni.
Na wenye kukataa na kukanusha aya zetu zinazosomwa na dalili za Umoja Wetu, basi hao ndio ambao watasalia Motoni, wakiwa humo milele: hawatatoka humo.”
Enyi kizazi cha Ya’qūb, tajeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo nyingi kwenu, nishukuruni na timizeni wasia Wangu kwenu kuwa muviamini Vitabu Vyangu na Mitume Wangu Wote, mfuate Sheria Zangu kivitendo. Mkifanya hivyo, nitawatimizia niliyowaahidi ya kuwarehemu katika ulimwengu na kuwaokoa kesho Akhera. Na Mimi, Peke Yangu, niogopeni na muwe na hadhari na mateso Yangu ikiwa mtavunja ahadi na kunikanusha.
Na iaminini Qur,ani, enyi wana wa Isrāīl, ambayo niliiteremsha kwa Muhammad, aliye Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, ambayo inalingana na yale mnayoyajua yaliyo sahihi katika Taurati. Na msiwe ni kundi la mwanzo la Watu wa Kitabu (ahl al-kitāb) kuikanusha. Na wala msizibadilishe aya zangu kwa thamani chache ya taka za dunia zenye kuondoka. Na Kwangu Mimi, Peke Yangu, fanyeni vitendo vya kunitii na acheni kuniasi.
Wala msichanganye haki niliyowafafanulia, na batili mliyoizusha. Na jihadharini kuificha haki iliyo wazi ya sifa za Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ambazo zimo ndani ya vitabu vyenu. Na nyinyi mnazipata hizo zimeandikwa kwenu, katika vitabu mnavyovijua vilivyoko mikononi mwenu.
Na ingieni kwenye dini ya Uislamu: Msimamishe Swala kwa njia sahihi kama alivyokuja nayo Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mtekeleze Zaka za lazima kwa namna iliyowekwa na Sheria, na mue pamoja na wanaorukuu katika ummah wake, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Ni ubaya ulioje wa hali yenu na hali ya wasomi wenu, mnapoamrisha watu kufanya mambo ya kheri na kuziacha nafsi zenu, hamziamrishi ziingie kwenye hiyo kheri kubwa, nayo ni Uislamu, na hali nyinyi mnaisoma Taurati ambayo ndani yake muna sifa za Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na ulazima wa kumfuata! Kwani hamzitumii akili zenu kisawa?
Jisaidieni, katika mambo yenu, kwa subira za kila aina, na pia kwa Swala ambayo ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.
Wenye kumcha Mwenyezi Mungu na kutaraji Malipo yaliyoko Kwake, wenye kuamini kwa yakini kuwa wao ni wenye kukutana na Mola wao, Aliyetukuka na kushinda, baada ya kufa, na kuwa wao ni wenye kurejea Kwake Siku ya Kiama kwa kuhesabiwa na kulipwa.
Enyi kizazi cha Ya’qūb! Kumbukeni neema zangu nyingi juu yenu, mnishukuru kwa neema hizo na mkumbuke kuwa Mimi nimewatukuza nyinyi juu ya watu wa zama zenu, kwa wingi wa Mitume na Vitabu vilivyoteremshwa kama Taurati na Injili.
Iogopeni Siku ya Kiama, Siku ambayo hakuna mtu wa kumfaa mwengine kitu chochote, wala Mwenyezi Mungu hatakubali maombezi kwa Makafiri na wala hatakubali kutoka kwao kitu chochote cha kuwakomboa, hata kama kilikuwa ni mali yote yaliyoko ardhini, na hakuna yoyote atakayeweza kujitokeza kuwanusuru wao na kuwaokoa na adhabu.
Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipowaokoa nyinyi na mateso ya Fir'awn na wafuasi wake, waliokuwa wakiwaonjesha nyinyi adhabu kali sana, wakiwaua watoto wenu wa kiume kwa wingi na kuwaacha wanawake wenu kwa kutumika na kudhalilishwa. Katika hilo, ni mtihani kwenu kutoka kwa Mola wenu. Na katika kuokolewa kwenu na yeye, ni neema kubwa ambayo inapasa kwenu mumshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika kila zama zenu na vizazi vyenu.
Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipoipambanua bahari kwa ajili yenu na tukafanya ndani yake njia kavu, mkavuka na tukawaokoa na Fir'awn na askari wake na msizame majini. Fir'awn na askari wake walipoingia kwenye njia mlizopitia, tuliwazamisha majini mbele ya macho yenu.
Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipompa Musa agizo la masiku arubaini la kuiteremshiwa Taurati, iwe ni uongofu na nuru kwenu, na punde tu alipoondoka mlichukua fursa ya kuwa yeye hayupo kwa muda mchache, mkamfanya ndama, mliyomtengeneza kwa mikono yenu, kuwa ni mungu wenu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu. Huu ni ukanushaji Mwenyezi Mungu mbaya kabisa. Na nyinyi mlikuwa madhalimu kwa kumfanya ndama ni Mungu.
Kisha tukawasamehe kitendo hiki kibaya, tukakubali toba yenu baada ya kurudi Musa kwa kutarajia kuwa mtamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema Zake na fadhila Zake juu yenu, na hamtaendelea kwenye ukafiri na uasi.
Na Kumbukeni neema Yetu juu yenu, tulipompa Mūsā Kitabu chenye kupambanua baina ya haki na batili- nacho ni Taurati- ili muongoke na mtoke kwenye upotevu.
Na Kumbukeni neema Zetu kwenu, aliposema Mūsā kuwaambia watu wake, “Hakika nyinyi mlijidhulumu nafsi zenu kwa kumfanya ndama ni mungu, basi tubieni kwa Muumba wenu kwa kuuana nyinyi kwa nyinyi. Kufanya hivyo ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu kuliko kukaa milele Motoni.” Na nyinyi mlifuata amri hiyo, ndipo Mwenyezi Mungu Akawafanyia wema kwa kuikubali toba yenu. Hakika Yeye, Aliyetukuka, ni Ndiye Mwingi wa kukubali toba za wenye kutubia miongoni mwa waja wake na ni Ndiye Mwenye kuwarehemu.
Na Kumbukeni pindi mliposema, “Ewe Mūsā! Hatutakuamini kuwa maneno tunayoyasikia kutoka kwako ni maneno ya Mwenyezi Mungu mpaka tumuone Mwenyezi Mungu waziwazi,” ukashuka moto kutoka mbinguni, na nyinyi mnauona kwa macho yenu, ukawaua kwa sababu ya madhambi yenu na ujasiri wenu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Kisha tukawahuisha baada ya kufa kwenu kwa kimondo cha moto, ili muishukuru neema ya Mwenyezi Mungu kwenu. Kifo hiki kilikuwa ni adhabu kwao, kisha aliwafufua wakaendelea kuishi mpaka muda wao kumalizika.
Na Kumbukeni neema Zetu mlipokuwa mnahangaika kwenye ardhi, tukawaletea kiwingu cha kuwafinika ili kiwakinge na joto la jua, tukawateremshia mann, nacho ni ktu kifananacho na gundi chenye ladha ya asali; na tukawateremshia salwa, nayo ni aina ya ndege wafananao na tomboro; na tukawaambia, “Kuleni vitu vizuri tulivyowaruzuku na msiende kinyume na dini ya Mwenyezi Mungu,” lakini hamkufuata amri. Na wao hawakutudhulumu sisi kwa kuzikanusha neema hizi, lakini walikuwa wakijidhulumu nafsi zao, Kwani mwisho mbaya wa dhuluma utawarudia wao.
Na Kumbukeni neema yetu kwenu, tuliposema, “Ingieni mji wa Baitul Maqdis na kuleni vizuri vyake, mahali popote pa mji huo, kwa starehe. Na muwe, katika kuingia kwenu, wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, wadhalilifu Kwake na mseme, ‘Ewe Mola wetu, tuondolee madhambi yetu,’ tutawaitikia, tutawasamehe na kuyafanya yasitirike.” Na wenye Kufanya wema katika amali zao tutawazidishia kheri na thawabu.
Wale wajeuri waliyo wapotevu, katika wana wa Isrāīl, walibadilisha neno la Mwenyezi Mungu na wakaipotoa kauli pamoja na kitendo. Kwani waliingia, na huku wakijikokota kwa matako na wakisema, “habbah fī sha’rah’ (mbegu unyweleni.)”, wakiifanyia maskhara dini ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya kuasi kwao na kutoka kwao kwenye utiifu kwa Mwenyezi Mungu.
Na Kumbukeni neema Yetu kwenu, mlipokuwa na kiu katika kuzunguka kwenu, alipotuomba Musa, kwa unyenyekevu, tuwaletee maji watu wake. Tukasema, “Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako.” Akalipiga, na chemchemi zikabubujika hapo jiweni sehemu kumi na mbili, ikilingana na idadi ya makabila yao, pamoja na kulijulisha kila kabila chemchemi yake ya kutumia, ili wasigombane. Na tukawaambia, “Kuleni na kunyweni riziki ya Mwenyezi Mungu wala msitembee katika ardhi kuleta uharibifu.”
Na Kumbukeni, tulipowateremshia chakula tamu na ndege wa kuvutia, mkawa hamjali, kama ilivyo desturi yenu, ikawapata dhiki na machovu na mkasema, “Ewe Mūsā! Sisi hatutavumilia chakula hicho kwa hicho kisichobadilika siku zote. Basi tuombee Mola wako Atutolee chakula katika mimea ya ardhini kama mboga, matango, mbegu zinazoliwa, adasi na vitunguu.” Musa akawaambia, kwa kuwapinga vikali, “Vipi mnataka hivyi ambavyo ni duni zaidi na mnaacha riziki yenye manufaa ambayo Mwenyezi Mungu amewachagulia? Ondokeni jangwani na mshuke mjini. Huko mtavipata mnavyovitamani sana kwenye mashamba na masoko.” Waliposhuka, iliwabainikia kuwa wao wanatanguliza chaguo lao,kila mahali, juu ya chaguo la Mwenyezi Mungu na wanayafadhilisha matamanio yao juu ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu Alilowachagulia. Kwa hivyo, sifa ya unyonge na umasikini wa moyo iliwaambata, na wakaondoka na kurudi wakiwa wamo kwenye ghadhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuipa mgongo dini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwa wao walikuwa wakikanusha aya za Mwenyezi Mungu na kuua Manabii kwa udhalimu na uadui. Yote hayo ni kwa sababu ya kuasi kwao na kuivuka mipaka ya Mola wao.
Hakika Waumini wa ummah huu waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake na wakatekeleza Sheria Yake, na wale waliokuwa kabla ya kutumilizwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa ummah waliopita katika Mayahudi, Wanaswara na Wasabai (Sābiūn), nao ni watu walioko kwenye tabia za maumbile na hawana dini maalumu wanayoifuata, wote hawa wakimuamini Mwenyezi Mungu, imani ya sawa iliyotakasika, wakaiamini Siku ya kufufuliwa na Malipo na wakafanya amali zenye kumridhi Mwenyezi Mungu, basi thawabu zao zimethibiti kwa Mola wao. Wao hawatakuwa na khofu juu ya mambo yao ya Akhera ambayo wao watayakabili. Na wala wao hawatahuzunika juu ya mambo ya dunia waliyoyakosa. Ama baada ya kutumilizwa Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, kuwa ni mwisho wa Manabii na Mitume, kwa watu wote, Mwenyezi Mungu Hatakubali dini, kwa yoyote, isipokuwa ile aliyokuja nayo ambayo ni Uislamu.
Na kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua kutoka kwenu ahadi ya mkazo ya kumuamini Mwenyezi Mungu na kumpwekesha kwa ibada, na tukaliinua jabali la Tūr juu yenu na tukawaambia, “Chukueni, kwa bidii na jitihadi, Kitabu tulichowapa na mkitunze. Na mkitofanya hivyo, tutaliangusha hili jabali juu yenu liwafinike, na msiisahau Taurati kwa maneno na vitendo, mpate kunicha na kuiogopa adhabu Yangu.”
Kisha mlienda kinyume na mkaasi mara nyingine, baada ya kuchukuwa ahadi ya mkazo na kunyanyuliwa jabali, kama desturi yenu daima. Na lau si wema wa Mwenyezi Mungu na rehema Yake kuikubali toba yenu na kuyasamehe makosa yenu, mungalikuwa ni wenye hasara ya duniani na ya Akhera.
Hakika mlijua, enyi kongamano la Mayahudi na Wanaswara, adhabu iliyowapata mababu zenu waliopita, watu wa kijiji kilichoasi amri ya Mwenyezi Mungu katika yale aliyowachukulia ahadi ya kuitukuza Siku ya Jumamosi. Wakafanya hila ya kuvua samaki siku ya Jumamosi kwa kuweka mitego na kufukua mashimo. Walipofanya hivyo, Mwenyezi Mungu aliwageuza kuwa manyani wenye kudharauliwa.
Tukakifanya kijiji hicho ni mazingatio kwa watu wa vijiji vya karibu ambao itawafikia habari yake na vituko vilivyotokea huko, na ni mazingatio kwa mwenye kufanya madhambi kama hayo baada yake. Na pia tulikifanya ni mawaidha kwa watu wema, wapate kujua kuwa wao wako kwenye haki, ili wasimame imara juu yake.
Na Kumbukeni, enyi wana wa Isrāīl, makosa ya mababu zenu, ushindani wao mwingi na kujadiliana kwao na Mūsā, rehema na amani zimshukie, pindi alipowaambia, “Hakika Mwenyezi Mungu Anawaamuru mchinje ng’ombe.” Wakasema, wakiwa na kiburi, “Unatufanyia mzaha na kutuchezea?” Mūsā akawajibu, “Ninajilinda kwa Mwenyezi Mungu nisiwe ni miongoni mwa wanaofanya stihizai.”
Walisema, “Tuombee Mola wako atufafanulie sifa ya ng’ombe huyu.” Akawajibu, “Mwenyezi Mungu Anawaambia kwamba sifa yake ni asiwe mkubwa wa miaka wala mdogo. Yeye ni wa katikati baina ya uzee na ujana, basi fanyeni haraka kutii amri ya Mola wenu.”
Wakarudi kwenye kujadili kwao wakisema, “Mwambie Mola wako Atufafanulie rangi yake.” Akasema kuwaambia, “Yeye anasema kwamba huyo ni rangi ya manjano iliyoiva sana, anayemtia furaha mwenye kumwangalia.”
Wana wa Isrāīl walimwambia Mūsā, “Tuombee Mola wako Atufafanulie sifa zake nyingine zisizokuwa zilizotangulia. Sababu ng’ombe wenye sifa hizi ni wengi. Kwa hivyo, tumechanganyikiwa hatujui tuchague yupi. Na sisi, Mwenyezi Mungu Anapotaka, tutaongokea kumjua ng’ombe ambaye ilitolewa amri achinjwe.”
Mūsā aliwaambia, “Mwenyezi Mungu Anasema kwamba huyo ni ng’ombe asiyetumiwa kwa kazi ya kulima ardhi ya kilimo, hakutayarishwa kutia maji, hana kasoro yoyote na hana alama yoyote ya rangi isiyokuwa rangi ya ngozi yake.” Wakasema, “Sasa umekuja na ukweli wa sifa ya ng’ombe.” Wakalazimika kumchinja baada ya muda mrefu wa mbinu za kuchelewesha. Na walikuwa karibu kutofanya hilo kwa ushindani wao. Hivi ndivyo walivyojitilia mkazo, ndipo Mwenyezi Mungu Akawafanyia mkazo.
Na Kumbukeni, mlipomuua mtu, mkabishana kuhusu yeye, akawa kila mmoja ajiepushia nafsi yake tuhuma ya kuua na hali Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyafichua yale ambayo mlikuwa mkiyaficha kuhusu kifo cha yule aliyeuawa.
Tukasema, “Mpigeni aliyeuliwa kwa sehemu ya yule ng’ombe aliyechinjwa, Mwenyezi Mungu atamfufua akiwa hai na atawaambia muuaji wake ni nani.” Basi wakampiga kwa ile sehemu ya ng’ombe, Mwenyezi Mungu Akamhuisha na akamtaja muuaji wake. Hivyo ndivyo Anavyohuisha Mwenyezi Mungu wafu Siku ya Kiyama na kuwaonyesha nyinyi, Wana wa Isrāīl, miujiza Yake yenye dalili ya ukamilifu wa uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ili mfikiri kwa akili zenu mpate kujiepusha na vitendo vya kumuasi.
Lakini nyinyi hamkufaidika na hilo. Kwani baada ya miujiza yote hii yenye kupita mipaka ya uwezo wa kiumbe, nyoyo zenu zilikuwa ngumu na shupavu kwa namna ambayo hakuna kheri iliopenyeza ndani, na hazikulainika mbele ya miujiza yenye kushinda niliyowaonesha, mpaka nyoyo zenu zikafikia hadi ya kuwa ni kama jiwe gumu, bali zililishinda jiwe kwa ugumu wake. Kwani miongoni mwa mawe kuna yanayopanuka na kutoboka na maji yakabubujika kwa wingi kutoka humo mpaka yakawa ni mito yenye kupata. Na miongoni mwayo kuna yanayofanya nyufa, yakapasuka na kuchimbuka maji ya chemchemi na mikondo. Na miongoni mwayo kuna yanayoanguka kutoka juu ya milima kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kumuadhimisha. Na Mwenyezi Mungu Hakuwa ni Mwenye kughafilika kwa mnayoyafanya.
Enyi waislamu! Kwani mumesahau vitendo vya Wana wa Isrāīl, ndipo nafsi zenu zikawa na tamaa kuwa Mayahudi wataiamini dini yenu? Wanavyuoni wao walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu ya Taurati, kisha wakiyapotoa kwa kuyageuza na kuyapa maana yasiyo sahihi baada ya kuyafahamu maana yake ya kweli, au kwa kuyageuza matamshi yake, hali wanajua kuwa wao wanayapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kusudi na urongo.
Hawa Mayahudi, wakikutana na Waumina, wanasema kwa ndimi zao, “Tumeamini dini yenu na Mtume wenu aliyebashiriwa katika Taurati.” Na wakiwa faragha, wao kwa wao, hawa wanafiki wa kiyahudi, huwa wakiambiana kwa njia ya kukemeana, “Vipi nyinyi mnawahadithia Waumini yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewabainishia katika Taurati kuhusu Muhammad, mkawapa hoja juu yenu mbele ya Mola wenu Siku ya Kiyama? Kwani hamfahamu mkajihadhari?”
Je, kwani wanafanya uhalifu wote huu na hali wao hawajui kuwa Mwenyezi Mungu Anayajua yote wanayoyaficha na kuyadhihirisha?
Na kati yao kuna watu wasiojua kusoma na kuandika, na wasioijua Taurati na yaliyomo ndani yake ya sifa za Nabii na Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na hawana chochote kuhusu hayo isipokuwa ni maneno ya urongo na dhana mbovu.
Maangamivu na onyo kali kwa wanavyuoni wa shari wa Kiyahudi ambao wanaandika kitabu kwa mikono yao kisha wanaosema, “Hiki kinatoka kwa Mwenyezi Mungu.” Nacho kinaenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu Amemteremshia Nabii wake Mūsā rehema na amani zimshukie, ili wapokee, kwa kitendo hicho, manufaa ya ulimwenguni. Basi wao watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya kuuandika kwao ubatilifu huu kwa mikono yao, na watapata mateso yenye kuangamiza kwa sababu ya mali ya haramu wanayoyachukua kwa shughuli yao hiyo, kama hongo na mfano wake.
Walisema Wana wa Israili, “Moto hautupati huko Akhera isipokuwa kwa siku chache zinazohesabika.” Waambie, ewe Mtume, kwa kuyavunja madai yao, “Kwani nyinyi muna ahadi, kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ya jambo hilo? Mwenyezi Mungu Haendi kinyume ahadi yake. Lakini nyinyi munasema kuhusu Mwenyezi Mungu msiyoyajua kwa kuzua kwenu urongo.”
Hukumu ya Mwenyezi Mungu imethibiti kwamba mwenye kutenda makosa mpaka yakamtia ukafirini na madhambi yake yakamtawala yeye sehemu zake zote, na hali hii haiwi isipokuwa kwa mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wote hao, washirikina na makafiri, ndio wenye kukaa Motoni makao ya milele yasiyokatika.
Na hukumu ya Mwenyezi Mungu iliyothibiti, kwa upande mwengine, ni kwamba wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake imani ya kikweli iliyosafika na Wakafanya vitendo vinavyoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyowapelekea Mitume Wake kwa njia ya Wahyi, hao watakaa Peponi makao ya milele yasiyokatika huko Akhera.
Na Kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua ahadi ya mkazo kwenu kwamba mtamuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake Asiye na mshirika, muwafanyie wema wazazi wawili na watoto waliofiliwa na baba zao nao wako chini ya umri wa kubaleghe na masikini na kwamba muwaambie watu maneno mazuri, pamoja na kusimamisha Swala na kutoa Zaka. Kisha mkageuka na mkavunja ahadi, isipokuwa wachache katika nyinyi waliosimama imara juu yake. Na nyinyi bado mnaendelea kugeuka kwenu.
Na Kumbukeni, enyi Wana wa Isrāīl, tulipochukua kwenu ahadi ya mkazo katika Taurati ya kuharamisha umwagaji damu baina yenu, nyinyi kwa nyinyi, na kutoana majumbani nyinyi kwa nyinyi. Kisha mkakubali hilo na hali nyinyi mnashuhudia kuwa ni kweli.
Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauana, baadhi yenu wanawaua wengine, na baadhi yenu wanawatoa wengine majumbani mwao; na kila kundi kati yenu linajitafutia nguvu kwa maadui dhidi ya ndugu zake kwa njia ya udhalimu na uonevu. Na mkijiwa nao, hao ndugu zenu, ni mateka kwenye mikono ya maadui, mnafanya haraka kuwakomboa kwa kulipa fidia, pamoja na kuwa imeharamishwa kwenu kuwatoa majumbani mwao. Ni ubaya ulioje mnaoufanya wa kuziamini baadhi ya hukumu za Taurati na kuzikanusha nyingine! Basi Malipo ya wanaoyafanaya hayo si mengine ila ni unyonge na fedheha ulimwenguni, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali sana ndani ya Moto. Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika kwa mnayoyafanya.
Hao ndio waliofadhilisha uhai wa ulimwenguni juu ya Akhera, basi hawatapunguziwa adhabu wala wao hawatakuwa na msaidizi wa kuwanusuru na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Hakika tulimpa Mūsā Taurati, na kuwaleta baada yake Mitume wengine miongoni mwa Wana wa Isrāīl. Na tulimpa ' Īsā mwana wa Maryam miujiza iliyo wazi na kumtilia nguvu kwa Jibrili, amani imshukie. Kwani nyinyi mumekuwa kila Mtume anapowajia na Wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, usiolingana na matamanio yenu, mnamfanyia kiburi, wengine mkiwakanusha na wengine mkiwaua?
Wana wa Isrāīl walisema kumwambia Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, “Nyoyo zetu zimezibwa kwa namna ambayo maneno yako hayapenyezi ndani yake.” Mambo si kama walivyodai. Bali nyonyo zao zimelaaniwa, zimepigwa muhuri juu ya hiyo laana. Na wao wamefukuzwa kutoka kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya kukanusha kwao. Wao hawaamini isipokuwa imani chache isiyowafaa.
Na ilipowajia Qur’ani inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, ikisadikisha yale ambayo waliokuwa nayo kwenye Taurati, waliikanusha na kuukataa utume wa Muhammad, rehema na mani zimshukie. Na walikuwa, kabla ya kutumilizwa kwake, wakitumai kusaidiwa na yeye dhidhi ya washirikina wa Kiarabu, na walikuwa wakisema, “Umekaribia wakati wa kutumilizwa Mtume wa zama za mwisho ambaye sisi tutamfuata na tutapigana na nyinyi tukiwa pamoja na yeye.” Alipowajia huyo Mtume, ambaye walizijua sifa zake na ukweli wake, walimkataa na walimkanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu imshukie kila aliyemkanusha Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema na amani zimshukie, na kukanusha Kitabu chake ambacho Mwenyezi Mungu alimletea kwa njia ya Wahyi.
Ni baya chaguo la Wana wa Isrāīl walilojichagulia. Kwani walibadilisha imani kwa ukafiri, (kwa kuacha imani na kuchukua ukafiri) kwa dhulma na uhasidi kwa kuwa Mwenyezi Mungu, kwa fadhila ZAke, Alimteremshia Nabii Wake na Mtume Wake Muhammad, rehema na amani zimshukie. Basi wakarudi na hali ya kuwa Mwenyezi Mungu Ana ghadhabu juu yao kwa kumkanusha kwao Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, baada ya kuwa na ghadhabu juu yao kwa kuipotoa Taurati. Na wenye kukanusha unabii wa Muhammad, rehema na amani zimshukie, wana adhabu yenye kuwabadilisha na kuwafanya wanyonge.
Na baadhi ya Waislamu wanaposema kuwaambia Mayahudi, “Aminini Qur’ani,” wanasema, “Sisi tunaviamini vilivyoteremshwa kwa Mitume wetu.” Na wao wanakanusha vilivyoteremshwa na Mwenyezi Mungu baada yake, pamoja na kuwa ndio haki inayosadikisha vile walivyonavyo. Lau wao walikuwa wanaviamini vitabu vyao kikweli, wangaliiamini Qur’ani iliyozisadikisha. Waambie, ewe Mtume, “Iwapo nyinyi mnayamini yale mliyoteremshiwa na Mwenyezi Mungu kwenu, kwa nini mliwaua Manabii wa Mwenyezi Mungu wakati wa nyuma?”
Hakika Nabii wa Mwenyezi Mungu, Mūsā, aliwajia nyinyi na miujiza iliyo wazi yenye dalili ya ukweli wake, kama mafuriko, nzige, chawa, vyura na mengineyo katika yale aliyoyataja Mwenyezi Mungu katika Qur’ani tukufu. Pamoja na hivyo, mumemchukuwa ndama mkamfanya ni muabudiwa, baada ya Mūsā kuondoka kuenda kukutana na Mola wake. Na nyinyi kwa kufanya hivyo mnavuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Na Kumbukeni, wakati tulipochukua kwenu ahadi yenye mkazo ya kuikubali Taurati aliyokuja nayo Mūsā, mkavunja ahadi, tukaliinua jabali la Tūr juu ya vichwa vyenu na tukasema, “Tuchukueni tulichowapa kwa bidii, na msikie na mtii, au tutaliangusha jabali juu yenu.” Mkasema, “Tumesikia kauli yako na tumeasi amri yako,” kwa kuwa ibada ya ndama imetangamana na nyoyo zenu kwa sababu ya kuendelea kwenu sana kwenye ukafiri. Waambie, ewe Mtume, Ni mbaya iliyoje hiyo njia ya ukafiri na upotevu ambayo imani yenu imewapeleka, iwapo nyinyi mnayasadiki yale yaliyoteremshwa kwenu.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi ambao wanadai kuwa Pepo ni yao peke yao, kwa kudai kuwa wao tu, bila watu wengine, ndio mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuwa wao ni watoto Wake na vipenzi Vyake, “Mambo yakiwa ni hivyo, waapizeni kufa waliyo warongo katika nyinyi au wasiokuwa katika nyinyi, iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu haya.”
Na hawatalifanya hilo kabisa, kwa wanayoyajua ya ukweli wa Nabii Muhammad, rehema na amani zimshukie, na ya urongo na uzushi wao, na kwa ukafiri na uasi walioufanya unaopelekea kukoseshwa Pepo na kuingia Motoni. Na Mwenyezi Mungu Anawajua madhalimu miongoni mwa waja wake na Atawalipa kwa dhulma zao.
Na utajua tena utajua, ewe Mtume, kuwa Mayahudi ni wenye kupenda mno, miongoni mwa watu, maisha marefu, hata yawe ni maisha ya unyonge na udhalilifu namna gani. Kupenda kwao maisha marefu kunazidi vile washirikina wanavyoyapenda. Myahudi anatamani lau ataishi miaka elfu moja. Na umri huo, lau aufikia, hautamwepusha na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hakuna kitu chochote chenye kufichika Kwake katika matendo yao, na Atawalipa, kwa hiyo matendo yao, adhabu wanayostahiki.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi waliposema, “Jibrili ni adui yetu miongoni mwa Malaika.”: “Mwenye kuwa ni adui wa Jibrili, basi ajue kuwa yeye ameiteremsha Qur’ani na kuitia ndani ya moyo wako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ikiwa ni yenye kuvisadikisha vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyoitangulia, yenye kuongoza kwenye njia ya haki na yenye kuwapa wenye kuamini bishara ya kila wema wa dunia na Akhera.”
Mwenye kumfanyia uadui Mwenyezi Mungu, Malaika Wake, Wajumbe Wake ambao ni Malaika au binadamu, hasahasa Malaika wawili: Jibrili na Mikaili, huwa amemfanyia uadui Mwenyezi Mungu. Sababu Mayahudi walidai kwamba Jibrili ni adui wao na Mikaili ni rafiki yao. Mwenyezi Mungu Akawajulisha kwamba mwenye kuwa adui wa mmoja katika wao huwa ni adui wa Mwengine na pia ni adui wa Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu ni adui wa wenye kuyakanusha yale aliyoyateremsha kwa Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukie.
Hakika tulikuteremshia aya zilizo wazi, zinazoonyesha kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kikweli; na hawazikanushi aya hizo isipokuwa wenye kutoka nje ya Dini ya Mwenyezi Mungu.
Ni ubaya ulioje wa hali ya Wana wa Isrāīl katika kuvunja kwao ahadi! Kila wanapotoa ahadi, kinatoka kikundi cha watu katika wao wakaitupa na wakaivunja. Utawaona wanaifunga ahadi leo na kuitangua kesho. Bali wengi wao hawayaamini aliyokuja nayo Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake Muhammad, rehema na amani zimshukiye yeye.
Na alipowajia Muhammad, rehema na amani zimshukie, na Qur’ani inayoafikiana na Taurati waliyonayo, kilitoka kikundi cha watu katika wao wakakitupa kitabu cha Mwenyezi Mungu, na kukiweka nyuma ya migongo yao. Hali yao ni hali ya wajinga wasiojua uhakika wake.
Na Mayahudi walifuata yale ambayo mashetani walikuwa wanawasimulia wachawi katika kipindi cha ufalme wa Sulaimān mwana wa Dāwūd. Na Sulaymān hakukufuru na wala hakujifundisha uchawi. Lakini mashetani ndio walimkanusha Mwenyezi Mungu kwa kuwafundisha watu uchawi, kwa kuwaharibia dini yao. Mayahudi pia waliufuata uchawi ulioshushwa kwa malaika wawili: Hārūt na Mārūt, katika ardhi ya Babil ilyoko Iraq, ukiwa ni mtihani na majaribio kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja Wake. Na hao Malaika wawili hawakuwa wakimfunza yoyote mpaka wamnasihi na kumuonya asijifunze uchawi na kumwambia, “Usikufuru kwa kujifunza uchawi na kuwatii mashetani.” Basi watu walikuwa wakijifunza kutoka kwa Malaika wawili vitu vinavyozusha chuki baina ya mume na mke mpaka wakafarikana. Na wachawi hawana uwezo wa kumdhuru, kwa uchawi wao, yoyote isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na hukumu Yake. Na wachawi hawajifunzi ila shari yenye kuwadhuru na kutowapa nafuu. Mashetani waliupeleka uchawi kwa Mayahudi, ukaenea kwao mpaka wakaufadhilisha juu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na Mayahudi walijua kwamba mwenye kuchagua uchawi na kuacha haki, hatakuwa na fungu lolote la kheri huko Akhera. Ni ubaya ulioje uchawi na ukafiri waliojichagulia nafsi zao kuwa ni badala ya Imani na kumfuata Mtume, lau walikuwa na elimu yenye kuzalisha vitendo vya kufuata mawaidha wapewayo!
Na lau Mayahudi waliamini na kumuogopa Mwenyezi Mungu, wangalikuwa na yakini kuwa thawabu za Mwenyezi Mungu ni bora kwao kuliko uchawi na kuliko yale waliyoyapata kupitia huo uchawi. Lau walikuwa wanajua thawabu na malipo yanayopatikana kwa kuamini na kumcha Mwenyezi Mungu, ujuzi wa kihakika, wangaliamini.
Enyi ambao mliamini, msiseme kumwambia Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, “Rā’nā.” Yaani: tupatie masikizi yako, utufahamu na utufahamishe. Sababu Mayahudi walikuwa wakisema maneno haya kumwambia Nabii, rehema na amani zimshukie, wakipotoa ndimi zao kwa neno hilo, wakikusudia kumtukana na kumnasibisha na kutoelewa. Na semeni badala yake, enyi Waumini, “Undhurnā.” Yaani: tuangalie na utuchunge. Lina maana yale-yale yanayokusudiwa. «Na msikie Kitabu cha Mola wenu mnachosomewa na mkifahamu.» Na wenye kukanusha wana adhabu yenye kuumiza.
Makafiri, miongoni mwa Watu wa Kitabu na washirikina, hawapendi mteremshiwe kheri, hata kama ni ndogo kabisa, itokao kwa Mola wenu, iwe ni Qur’ani au elimu au ushindi au bishara njema. Mwenyezi Mungu Anamhusisha Amtakaye kwa rehema Zake za unabii na utume. Mwenyezi Mungu ni Mwenye vipaji vingi venye kuenea.
Tunaipoibadilisha aya au kuiondoa kutoka nyoyoni na akilini, tunaileta yenye manufaa zaidi kwenu kuliko hiyo au tunaileta iliyo mfano wake katika utekelelezaji na thawabu. Na kila mojawapo ya aya hizo ina hekima yake. Kwani hujui, ewe Nabii, kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza, hakuna kitu kinachomshinda?
Kwani hukujua, ewe Nabii, wewe na ummah wako, kwamba Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Mwenye kumiliki, Ndiye Mwenye kuendesha mambo ya mbinguni na ardhini? Anafanya Analolitaka na Anatoa uamuzi Anaotaka. Anawaamrisha waja Wake na kuwakataza Anavyotaka, na ni juu yao kutii na kukubali. Na wajue wenye kumuasi Yeye kuwa hakuna rafiki mwenye kuwasaidia wala muokozi mwenye kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwapate.
Bali nyinyi mnataka, enyi watu, kumuuliza Mtume wenu Muhammad, rehema na amani zimshukie, awapatie mambo, kwa njia ya ukaidi na ujeuri, kama yalivyotakwa, mfano wa hayo, kutoka kwa Mua. Na jueni kwamba mwenye kuchagua ukafiri na kuacha Imani, ashatoka nje ya njia ya Mwenyezi Mungu iliyolingana sawa na ameingia kwenye ujinga na upotevu.
Wengi wa Watu wa Kitabu watamani kuwarudisha nyinyi, baada ya kuamini kwenu, muwe makafiri kama mlivyokuwa kabla mkiabudu masanamu. Haya ni kwa sababu ya chuki zilizojaa kwenye nafsi zao, baada ya kuwabainikia ukweli wa Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema na amani zimshukiye, katika yale aliyokuja nayo. Basi lipuzeni lolote la ubaya au makosa lililotoka kwao. Na sameheni ujahili wao mpaka Mwenyezi Mungu Alete hukumu Yake ya kupigana na wao (na hili lilikuwa), na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu; hakuna kitu chochote kimshindacho.
Jishughulisheni, enyi Waumini, kutekeleza Swala kwa namna sahihi ipasavyo na kutoa Zaka zilizofaradhiwa. Na mjue kwamaba kila kheri mnayoitangulizia nafsi zenu, mtapata thawabu zake Akhera mbele ya Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye Aliyetukuka ni Mwenye kuyaona matendo yenu na Atawalipa kwayo.
Mayahudi na Wanaswara, kila mmoja katika wao anadai kuwa Pepo itaingiwa na pote lake peke yake, hataingia asiyekuwa katika pote hilo. Hayo ni mawazo yao maovu. Waambie, ewe Mtume, “Leteni dalili yenu juu ya ushahidi wa hilo mnalolidai iwapo nyinyi ni wakweli katika madai yenu.”
Mambo si kama walivyodhania kuwa Pepo ni ya pote fulani tu, si ya pote lingine. Hakika ataingia Peponi mwenye kumtakasa Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiye na mshirika na akawa ni mwenye kumfuata Mtume Muhammad, rehema na amani zimshukie, katika maneno yake yote na vitendo vyake vyote. Basi mwenye kufanya hayo atakuwa na thawabu ya matendo yake mbele ya Mola wake huko Akhera, nayo ni kuingia Peponi, hali ya kuwa wao, hao wenye kuingia Peponi, hawaogopi mambo ya Akhera yanayowakabili mbele yao, wala hawahuzuniki juu ya hadhi za ulimwengu zilizowapita.
Na walisema Mayahudi, “Wanaswara hawako kwenye dini sahihi. Ndivyo hivyo kama walivyosema Wanaswara kuhusu Mayahudi, na hali wote wanasoma Taurati na Injili, ambapo ndani yake kuna ulazima wa kuwaamini Mitume wote. Hivyo ndivyo pia walivyosema wasiojua miongoni mwa washirikina: Waarabu na wengineo. Yaani, walisema kumwambia kila mwenye dini, “Wewe huko kwenye kitu chochote cha maana.” Basi Mwenyezi Mungu Ataamua baina yao Siku ya Kiyama katika yale mambo ya kidini waliotafautiana juu yake, na kumlipa kila mtu kwa matendo yake aliyoyafanya.
Hakuna dhalimu zaidi kuliko wale waliozuia kutajwa Mwenyezi Mungu katika msikiti, kama kusimamisha Swala na kusoma Qur’ani na mengine mfano wa hayo, na wakafanya bidii kuifanya magofu kwa kuivunja au kuifunga au kwa kuwazuia Waumini kuijia. Madhalimu hao haikuwa yapasa kwao kuingia hiyo msikiti isipokuwa wakiwa katika hali ya kuogopa na kutishika wasipate adhabu. Kwa matendo yao hayo, watakuwa na unyonge na fedheha ulimwenguni, na watakuwa na adhabu kali kesho Akhera.
Zote pande mbili, upande wa kuchomoza jua na wa kutwa kwake na vilivyo baina yake, ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mmiliki wa ardhi yote. Basi pande wowote mnaouelekea kwenye Swala zenu kwa kuwa mmeamrishwa na Mwenyezi Mungu, Hakika nyinyi huwa mnaukusudia Uso Wake, hamkutoka kwenye ufalme Wake na utiifu wenu Kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye rehema za kuenea kwa waja Wake, ni Mjuzi wa vitendo vyao, hakuna chochote chenye kufichika Kwake Asikijue.
Na walisema Mayahudi na Wanaswara, “Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto.” Ameepukana Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, na neno hilo la batili! Kwani wote walioko mbinguni na ardhini ni milki Yake na ni watumwa Wake. Wote wanamnyenyekea Yeye na wanapelekewa wakiwa chini ya uendeshaji Wake.
Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Muumba mbingu na ardhi, bila ya kuwa na mfano uliotangulia. Na Anapolikadiri jambo na Akataka liwe, huliambia, “Kuwa,” likawa.
Walisema wajinga miongoni mwa Watu wa Kitabu na wengineo kumwambia Nabii na Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema na amani zimshukie, kwa njia ya inadi, “Si aseme na sisi Mwenyezi Mungu moja kwa moja Atuambie kwamba wewe ni Mtume Wake au itujie miujiza itokayo kwa Mwenyezi Mungu yenye kuonyesha ukweli wako.” Neno kama hili walilisema ummah waliopata kuwaambia Mitume wao, kwa njia ya ukaidi na ujeuri, kwa sababu ya kufanana nyoyo za waliotangulia na waliofuata katika ukafiri na upotevu. Hakika Tumezifafanua aya kwa wale wanaoamini Imani ya kikweli, kwa kumuamini kwao Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuzifuata kwao Sheria Alizowawekea.
Sisi tumekutumiliza, ewe Mtume, kwa Dini ya haki iliyotiliwa nguvu kwa hoja na miujiza. Basi ifikishe kwa watu, pamoja na kuwapa Waumini bishara ya kheri ya dunia na ya Akhera, na kuwatisha wakaidi na adhabu ya Mwenyezi Mungu inayowangojea. Na baada ya kufikisha ujumbe, hutaulizwa juu ya ukafiri wa wenye kukukanusha. Wao wataingia Motoni, Siku ya Kiyama, wala hawatatoka humo.
Na hawataridhika nawe, ewe Mtume, Mayahudi wala Wanaswara isipokuwa ikiwa utaacha Dini yako na ukafuata Dini yao. Waambie, “Dini ya Uislamu ndiyo Dinii sahihi” Na ukifuata matamanio ya hao, baada ya wahyi uliokujia, hutakuwa na rafiki wa kukunufaisha kwa Mwenyezi Mungu wala msaidizi wa kukunusuru. Maneno haya ingawa anaambiwa Mtume, yanalekezwa kwa ummah wote.
Wale Mayahudi na Wanaswara tuliowapa Kitabu, wanakisoma kisomo cha sawasawa, wanakifiuata kipasavyo kufuatwa na wanayaamini yaliyomo ndani yake ya kuwaamini Mitume wa Mwenyezi Mungu, ambao miongoni mwao ni wa mwisho wao, Nabii wetu na Mtume wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,. Na hawayapotoi wala hawayabadilishi yaliyokuja ndani yake. Hawa ndio waliomuamini Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na aliyoteremshiwa. Ama wale waliogeuza sehemu ya Kitabu na wakaficha baadhi yake, hao ndio waliomkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyoteremshiwa. Na wenye kumkanusha, hao watakuwa ni wetu wenye hasara kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Enyi kizazi cha Ya’qūb, tajeni neema zangu kubwa kwenu na mkumbuke kuwa niliwatukuza juu ya watu wa zama zenu kwa wingi wa Manabii wenu na kwa Vitabu walivyoteremshiwa.
Na ogopeni vitisho vya Siku ya Hesabu. Kwani hapo, hakuna nafsi itakayoifaa kitu chochote nafsi nyingine, wala Mwenyezi Mungu Hatakubali fidia, kutoka kwa hiyo nafsi, ya kuiyokoa na adhabu, wala hainufaiki kwa kuombewa na hakuna yoyote wa kuinusuru.
Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Mwenyezi Mungu Alipomfanyia mtihani Ibrāhīm kwa amri Alizomkalifisha nazo, akazitekeleza na kusimama nazo kwa njia nzuri. Mwenyezi Mungu Akamwambia, “Mimi nimekufanya wewe ni kiigizo kwa watu.” Ibrāhīm akasema, “Ewe Mola wajaalie baadhi ya watu wa kizazi chake ni viongozi kwa ukarimu Zako.” Mwenyezi Mungu Akamjibu kwamba madhalimu hawatapata uongozi wa kidini.
Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati tulipoifanya Alkaba ni marejeo ya watu; wanakuja kuikusudia, kisha wanarudi makwao kwa watu wao, kisha wanairudia tena, ni makusanyiko yao katika Hija, Umra, kutufu na kuswali, na pia ni amani kwao: hakuna adui anayewashambulia wakiwa hapo na tukasema, “Pafanyeni hapo Maqām Ibrāhīm ni mahali pa kuswali. Maqām Ibrāhīn ni jiwe ambalo Ibrāhīm alisimama juu yake alipokuwa akijenga Alkaba. Na tulimletea Wahyi Ibrahīm na mtoto wake Ismāīl kwa kuwaambia, «Isafisheni Nyumba Yangu na kila najisi na uchafu kwa ajili ya wenye kuabudu kwa kutufu pambizoni mwa Alkaba au kuketi Itikafu (I’tikāf) Msikitini na kuswali hapo.”
Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Aliposema Ibrāhīm akiwa katika maombi, “Ewe Mola wangu! ijaalie Makkah ni mji wenye amani usiokuwa na kitisho, uwaruzuku watu wake aina ya matunda na uwahusu kwa riziki hii wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho.” Mwenyezi Mungu Alisema, “Na mwenye kukufuru katika wao nitamruzuku ulimwenguni na kumstarehesha starehe chache, kasha nitamlazimisha kwa nguvu kwenda Motoni. Ubaya wa marejeo na makao ni mwisho huu.”
Na Kumbuka, ewe Nabii, wakati Ibrāhīm na Ismāīl walipoinua misingi ya Alkaba, huku wakimuomba Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu, “Ewe Mola wetu! Tutakabalie amali zetu njema na dua zetu! Kwani wewe Ndiye mwenye kusikia maneno ya waja wako, Ndiye mwenye kujua hali zao.
“Ewe Mola wetu, na utujaalie, sisi wawili, ni wenye kusimama imara juu ya Uislamu, ni wenye kukufuata kwa Imani. Utuonyeshe njia za kukuabudu. Utusamehe madhambi yetu. Hakika Wewe Ndiye Mwingi wa kukubali toba za waja wako, Ndiye mkunjufu wa rehema kwao.
“Ewe Mola wetu, mtumilize katika ummah huu mjumbe miongoni mwa watu wa kizazi cha Ismāīl, awasomee aya Zako na awafundishe Kitabu na Sunnah, awasafishe na ushirikina na tabia mbaya. Hakika Wewe Ndiye Mshindi asiyeshindwa na kitu, Ndiye Mwenye hekima Anayeviweka vitu vyote mahali pake.”
Hakuna yoyote anayeipa mgongo Dini ya Ibrahim, nayo ni Uislamu, isipokuwa safihi aliye mjinga. Na hakika tulimchagua Ibrahim duniani kuwa Nabii na Mtume, na kesho Akhera kuwa ni miongoni mwa watu wema ambao wana daraja za juu kabisa.
Na sababu ya kuchaguliwa kwake huku ni kukimbilia kwake kwenye Uislamu bila kusita. Alipoambiwa na Mola wake, “Itakase nafsi yako kwa Mwenyezi Mungu kwa kujisalimisha Kwake.» alikubali Ibrāhīm na kusema, “Nimejisalimisha kwa Mola wa viumbe vyote, kwa kumtakasa, kumpwekesha, kumpenda na kurudi Kwake kwa kutubia.”
Na Ibrāhīm na Ya’qūb waliwahimiza watoto wao kusimama imara juu ya Uislamu wakiwaambia, “Enyi watoto wetu! Mwenyezi Mungu Amewachagulia Dini hii, nayo ni Uislamu, Msiiache muda wa uhai wenu, na msifikiwe na mauti isipokuwa na nyinyi muko kwenye Dini hii.”
Je mlikuwa muko, enyi Mayahudi, pindi kifo kilipomjia Ya’qūb, alipowakusanya watoto wake na kuwauliza, “Mtaabudu nini baada ya kufa kwangu?” Wakasema, “Tutamuabudu Mola wako na Mola wa baba zako: Ibrāhīm, Ismā'īl na Is’ḥāq Ambaye ni Mola Mmoja; na sisi ni wenye kufuata amri Yake na kumdhalilikia.”
Hao ni Ummah waliopita miongoni mwa wale waliowatangulia nyinyi. Wao wana amali zao, na nyinyi muna amali zenu. Wala hamtaulizwa kuhusu amali zao. Na wao hawataulizwa kuhusu amali zenu. Na kila mmoja atalipwa kulingana na aliyoyatenda. Mtu hateswi kwa kosa la yoyote mwengine. Na haimnufaishi mtu ila Imani yake na uchaji Mungu wake.
Na Mayahudi walisema kuwaambia ummah wa Mtume Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukie yeye, “Ingieni kwenye dini ya Kiyahudi mtapata uongofu. Na Wanaswara waliwaambia kama hayo. Waambie, ewe Mtume, “Uongofu ni kuwa sote tufuate Mila ya Ibrāhīm ambaye alijiepusha na kila dini ya ubatilifu na kufuata Dini ya haki, na hakuwa ni miongoni mwa waliomshirikisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.”
Semeni, enyi Waumini, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, “Tumemuamini Mwenyezi Mungu, Aliye Mmoja, Anayeabudiwa kwa haki; na tumeiamini Qur’ani tuliyoteremshiwa ambayo Mwenyezi Mungu alimletea Wahyi Nabii wake na Mtume Wake Muhammad, rehema na amani zimshukie; na tumeziamini Kurasa alizoteremshiwa Ibrāhīm na watoto wake wawili: Ismāīl na Is’ḥāq, na alizoteremshiwa Ya’qūb na Asbāṭ - Manabii wanaotokana na watoto wa Ya’qūb waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya Wana wa Isrāīl-; na tumeiamini Taurati aliyopewa Mūsā na Injil aliyopewa Īsā na Wahyi ulioteremshwa kwa Mitume wote. Hatumbagui yoyote miongoni mwao katika kuamini. Na sisi ni wenye kumdhalilikia Mwenyezi Mungu kwa kumtii na kumuabudu.”
Wakiyaamini Makafiri, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara na wengineo, kama yale milyoyaamini nyinyi katika yale aliyokuja nayo Mtume, basi wameongoka kwenye haki; na wakikataa, basi wao wako kwenye upinzani mkubwa. Mwenyezi Mungu Atakutosheleza, ewe Mtume, shari lao na Atakupa ushindi juu yao. Yeye Ndiye Msikizi wa maneno yenu, Ndiye Mjuzi wa hali zenu.
Jilazimisheni na Dini ya Mwenyezi Mungu ambayo Ameifanya inasibiane na maumbile yenu. Kwani hakuna maumbile mazuri kuliko yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewaumbia watu. Jilazimisheni nayo na mseme, “Sisi ni wenye kuiandama, ni watiifu kwa Mola wetu katika kufuata kwetu mila ya Ibrāhīm.”
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Watu wa Kitabu, “Je mnajadiliana na sisi juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtakasa, hali ya kuwa Yeye ni Mola wa viumbe wote, hahusiki na watu fulani tu bila ya wengine? Sisi tuna amali zetu, na nyinyi muna zenu. Na sisi tunamtakasia Mwenyezi Mungu ibada na utiifu; hatumshirikishi kitu chochote na hatumuabudu yoyote isipokuwa Yeye.”
Au je, Mnasema, kwa njia ya kujadili kuhusu Mwenyezi Mungu kwamba Ibrāhīm na Ismā'īl na Is’ḥāq na Ya’qūb na Asbāṭ - Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya Wana wa Isrāīl wanaotokana na wana wa Ya’qūb - walikuwa katika dini ya Kiyahudi au ya Kinaswara? Huu ni urongo. Kwani hao walitumilizwa na kufa kabla ya Taurati na Injili. Waambie, ewe Mtume, “Kwani ni nyinyi mnaoijua zaidi dini yao au ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka?” Na Mwenyezi Mungu Ameshaeleza katika Qur’ani kwamba wao walikuwa Waislamu wenye msimamo uliolingana sawa. Na hakuna yoyote dhalimu zaidi kuliko nyinyi mnapouficha ushahidi uliothibiti kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kudai kinyume chake kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo. Na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na chochote katika vitendo vyenu. Yeye ni Mwenye kuvidhibiti na ni Mwenye kuwalipa kwavyo.
Hao ni ummah waliopita miongoni mwa wale waliowatangulia nyinyi. Wao wana amali zao, na nyinyi muna amali zenu. Wala nyinyi hamtaulizwa kuhusu amali zao. Na wao hawataulizwa kuhusu amali zenu. Katika aya hii pana kukata njia ya kujifungamanisha na viumbe kwa kujiamabatisha nao, kutoghurika kwa kunasibiana na wao, kwa kuwa linalozingatiwa ni kumuamini Mwenyezi Mungu na kumuabudu Peke Yake na kuwafuata Mitume Wake, na kwamba mwenye kumkanusha Mtume yoyote katika wao, huwa amewakanusha Mitume wote.
Watasema wajinga na madhaifu wa akili, miongoni mwa Mayahudi na mfano wao, wakiwa katika hali ya kufanya maskhara na kupinga, «Ni kitu gani kilichowageuza hawa Waislamu kuacha kibla chao ambacho walikuwa wakisali kukielekea mwanzo wa Uislamu?»(Nacho ni Baitul Maqdis). Waambie, ewe Mtume, «Upande wa Mashariki na wa Magharibi na katikati yake ni milki ya Mwenyezi Mungu. Hapana upande wowote, miongoni mwa pande zote, ulioko nje ya milki Yake. Yeye Anamuongoza Amtakaye, miongoni mwa waja Wake, kumuelekeza njia ya uongofu iliyo sawa.» Katika hayo, pana ujulishaji kwamba mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu, katika kufuata amri Zake, na kwa hivyo, popote tuelekezwapo tutaelekea.
Na kama tulivyowaongoza, enyi Waislamu, kwenye njia sahihi katika Dini, tumewafanya kuwa ni ummah bora ulio muadilifu, ili mue mashahidi juu ya ummah waliopita, kesho Akhera, kwamba Mitume wao waliwafikishia jumbe za Mola wao, na ili Mtume, kesho Akhera, awe vilevile ni shahidi juu yenu, kwamba yeye aliwafikishia ujumbe wa Mola wake. Wala hatukukifanya, ewe Mtume, kile kibla cha Baitul Maqdis ulichokuwa ukikielekea, kisha tukakugeuza tukakuelekeza Alkaba (iliyopo Makkah) isipokuwa ni yapate kuonekana yale tuliyoyajua hapo kale, ujuzi unaofungamana na thawabu na adhabu, ili tumtenganishe yule ambaye atakufuata na kukutii na kuelekea pamoja nawe pale utakapoelekea na yule aliye dhaifu wa imani, awe ni mwenye kubadilika na kuritadi kwa kuacha Dini yake kwa shaka yake na unafiki wake. Hali hii ya kugeuka Muislamu katika Swala yake, kuacha kuelekea Baitul Maqdis na kuelekea Alkaba ni ngumu na nzito, isipokuwa kwa wale walioongozwa na Mwenyezi Mungu na kupewa neema ya Imani na uchajimungu. Na wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupoteza imani yenu Kwake na kumfuata kwenu Mtume Wake kwa kuzibatilisha Swala zenu mlipokuwa mnaelekea kibla cha zamani. Hakika Yeye Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na upungufu wowote na Aliyetukuka, kwa watu ni Mpole na Mwenye huruma.
Hakika Tunauona mzunguko wa uso wako upande wa mbinguni mara baada ya mara, huku ukingojea kuteremka Wahyi juu yako kuhusiana na Kibla. Basi hakika Tutakuepusha na Baitul Maqdis Tukuelekeze kwenye kibla unachokipenda na unachokiridhia, nacho ni upande wa Msikiti wa Ḥarām ulioko Makkah. Basi, elekeza uso wako huko. Na popote mtakapokuwa, enyi Waislamu, na mkataka kuswali, elekeeni upande wa Msikiti wa Haram. Na hakika wale ambao Mwenyezi Mungu amewapa elimu ya Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara wanajua kwamba kugeuzwa kwako kuelekezwa Alkaba ndio haki iliyothibiti katika vitabu vyao. Na wala Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kughafilika juu ya yale wayafanyayo hawa wapinzani wenye shaka, na Atawalipa kwayo.
Na lau utawaletea wale waliopewa Taurati na Injili aina yoyote ya hoja na dalili kwamba kuelekea kwako Alkaba katika swala ndio haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hawangalikifuata kibla chako, kwa inadi na kiburi. Na wala wewe si mwenye kukifuata kibla chao mara nyingine. Wala baadhi yao si wenye kufuata kibla cha baadhi yao. Na lau utafuata matamanio ya nafsi zao kuhusu kibla na mengineyo, baada ya ujuzi uliyoupata kuwa wewe uko kwenye haki na wao wako kwenye batili, wewe wakati huo utakuwa ni miongoni mwa waliozidhulumu nafsi zao. Haya ni maelezo kuambiwa ummah wote, na ni kitisho na kemeo kwa kila afuataye matamanio ya wanaoenda kinyume na Sheria ya Kiislamu.
Wale Tuliowapa Taurati na Injili miongoni mwa wanavyuoni wa Kiyahudi na wajuzi wa Kinaswara wanajua ya kwamba Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, kwa sifa zake zilizotajwa katika vitabu vyao, kama vile wanavyowajuwa wana wao. Na hakika kuna kundi kati yao wanaificha haki na wao wanaujuwa ukweli wake na kuwa sifa zake zimethibiti.
Yale yaliyoteremshwa kwako, ewe Nabii, ndiyo haki kutoka kwa Mola wako. Kwa hivyo, usiwe ni kati ya wale wanaoyatilia shaka. Maneno haya, ingawa anambiwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yanaelekezwa kwa ummah wote.
Kila ummah, miongoni mwa ummah wa kila aina, una kibla chake anachokielekea kila mmoja katika wao kwenye swala yake. Basi kimbilieni, enyi Waumini, hali ya kushindana katika kutenda vitendo vyema ambavyo Ameviwajibisha kwenu Mwenyezi Mungu katika Dini ya Kiislamu. Mwenyezi Mungu Atawakusanya nyote Siku ya Kiyama kutoka popote mtakapokuwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Na mahali popote ulipotoka, ewe Nabii, ukiwa msafiri au ukitaka kuswali, elekeza uso wako upande wa Msikiti wa Haram. Kuelekea kwako huko ndio haki iliyothibiti kutoka kwa Mola wako. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni Mwenye kughafilika juu ya yale mnayoyatenda na Atawalipa kwa hayo.
Na mahali popote utokapo, ewe Nabii, elekea Msikiti wa Haram. Na popote mnapokuwa, enyi Waislamu, katika nchi yoyote miongoni mwa nchi za ardhi, elekezeni nyuso zenu upande wa Msikiti wa Haram, ili watu wapinzani wasiwe na hoja yoyote kwenu kwa njia ya ugomvi na mjadala, baada ya kuelekea huko, isipokuwa wale madhalimu na wenye ukaidi kati yao. Hao watabakia kwenye mjadala wao. Basi, msiwaogope wao, niogopeni Mimi kwa kufuata amri Yangu na kujiepusha na katazo Langu na ili nikamilishe neema Zangu kwenu kuwachagulia sheria zilizokamilika zaidi, na ili mpate kuongoka kufuata haki na usawa.
Kama Tulivyowaneemesha kwa kuelekea Alkaba, Tumewaletea mjumbe anayetokana na nyinyi, anawasomea aya zibainishazo haki kuitenga na batili, kuwasafisha na uchafu wa ushirikina na tabia mbaya, kuwafundisha Kitabu, Sunna na hukumu za Sheria na kuwafundisha habari za Mitume na visa vya ummah waliopita, mambo ambayo mlikuwa hamyajui.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewaamrisha Waumini wamtaje Yeye na Akatoa ahadi kwa hilo malipo bora zaidi, nayo ni kumsifu yule anayemtaja Yeye mbele ya viumbe walioko juu. Pia Amewaamrisha Waumini wamshukuru Yeye Peke Yake kwa maneno na vitendo na wasizikanushe neema Zake juu yao.
Enyi Waumini, takeni msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote, kwa kusubiri juu ya mikasa na misiba, na kuacha maasia na madhambi na kusubiri juu ya kufanya mambo ya utiifu na yale yanayomkurubisha mtu kwa Mola wake, na kwa Swala ambayo kwayo nafsi inapata utulivu na ambayo inakataza machafu na maovu. Hakika Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wenye kusubiri kwa msaada Wake, taufiki Yake na muelekezo Wake. Katika hii Aya kuna kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na Waumini kimahsusi, upamoja unaolazimiana na yaliyotangulia kutajwa. Ama kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na viumbe kijumla kunakolazimiana na elimu Yake na kuwa ujuzi Wake umezunguka kila kitu, basi upamoja huo ni wa viumbe vyote.
Na wala msiseme, enyi Waumini, kuhusu wale wanaouawa hali ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuwa wao wamekufa. Bali wao wako hai, uhai maalumu unaowahusu wao, ndani ya Makaburi yao. Wala hakuna anayejua yako vipi maisha hayo isipokuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, lakini nyinyi hamuyahisi maisha hayo. Katika haya, pana ushahidi kwamba kuna neema za kaburini.
Tutawapa, tena tutawapa, mtihani wa kitu hafifu cha hali ya kuogopa, njaa, upungufu wa mali, iwe ni uzito kuyapata au yaondoke, upungufu wa watu: kwa kufa au kufa-shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kwa upungufu wa matunda ya mitende na mizabibu na nafaka: kwa kupungua mazao yake au kuharibika kwake.Wape, ewe Nabii, habari njema, wale wenye subira juu ya haya na mfano wake, kwa yale yatakayowafurahisha na kuwapendeza ya mwisho mwema duniani na Akhera.
Miongoni mwa sifa za hawa wenye kusubiri ni kwamba wao wanapofikwa na kitu wanachokichukia husema, «Sisi ni waja waliomilikiwa na Mwenyezi Mungu, tunaoendeshwa kwa amri Yake na mapitisho Yake. Anafanya kwetu Alitakalo. Na sisi Kwake, Peke Yake, ni wenye kurudi kwa kufa, kisha kwa kufufuliwa ili kuhesabiwa na kulipwa.
Hao wenye kusubiri wana utajo mwema kutoka kwa Mola wao na rehema kubwa kutoka Kwake, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, na hao ndio walioongoka njia ya uongofu.
Hakika Swafa na Marwa, nayo ni majabali mawili madogo karibu ya Alkaba upande wa Mashariki, ni miongoni mwa alama za dini ya Mwenyezi Mungu zilizo wazi ambazo Mwenyezi Mungu Amezifanya ni sehemu za ibada kwa waja Wake kusai baina yake. Hivyo basi, yoyote mwenye kuikusudia Alkaba kwa kuhiji au kufanya Umra, si dhambi kwake kusai baina ya hayo majabali mawili, bali ni wajibu kwake kufanya hivyo. Na yule mwenye kufanya mambo ya kutii amri, kwa hiyari yake, hali ya kumtakasia Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushukuru, Analipa juu ya kichache kwa kingi, ni Mwenye kuzijua amali za waja Wake: Hazipotezi wala Hampunji yoyote chochote hata kama ni uzito wa chungu mdogo.
Hakika wale ambao wanazificha aya zilizo waziwazi, zijulishazo utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, nao ni wanavyuoni wa Kiyahudi na wajuzi wa Kinaswara na wengineo, miongoni mwa wafichao yalyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, baada ya sisi kuyadhihirisha kwa watu katika Taurati na Injili, hao Mwenyezi Mungu Atawafukuza kutoka kwenye rehema Yake, na viumbe wote watawaapiza laana.
Isipokuwa wale waliorudi hali ya kutubia makosa yao, wakarekebisha waliyoyaharibu na wakayabainisha waliyoyaficha. Hao nitazikubali toba zao na nitawalipa kwa kuwasamehe. Na mimi ni Mwenye kukubali mno toba ya mwenye kutubia kati ya waja Wangu na ni Mwenye huruma kwao kwa kuwapa taufiki ya kutubia na kukubali toba kutoka kwao.
Hakika wale waliokanusha imani na wakaficha haki na wakaendelea hivyo mpaka kufa kwao, juu yao kuna laana ya Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote kwa kuwatoa kwenye rehema Yake.
Watadumu kwenye laana na Moto. Hawatapunguziwa adhabu, wala hawatapumzishwa na kungojewa kwa udhuru wowote watakaoutoa.
Na Mola wenu, enyi watu, ni Mola Mmoja Aliyepwekeka katika dhati Yake, majina Yake, sifa Zake na vitendo Vyake na uja wa viumbe Vyake Kwake. Hapana apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa rehema, Mwenye kusifika kwa sifa ya rehema katika dhati Yake, vitendo Vyake kwa waja Wake wote, na Mwenye kuwarehemu waumini.
Hakika, katika kuumba mbingu kwa kuzifanya ziinuke juu na ziwe kunjufu, na ardhi kwa majabali yake, mabonde yake na bahari zake, na katika kutafautiana usiku na mchana kwa urefu na ufupi, giza na muangaza, na kuandamana kwao kwa kila mmoja kukaa pahali pa mwingine, na katika majahazi yanayopita baharini, yanayobeba vitu vinavyowanufaisha watu, na katika maji ya mvua Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, Akaipa uhai ardhi kwa maji hayo ikawa rangi ya kijani yenye kupendeza baada ya kuwa kavu isiyokuwa na mimea, na vile Alivyoeneza Mwenyezi Mungu humo kila kitambaacho juu ya ardhi hiyo, na katika yale Aliyowaneemesha kwayo ya kuugeuza upepo na kuuelekeza, na katika mawingu yanayopelekwa baina ya mbingu na ardhi, hakika, katika dalili zote hizo zilizopita, pana alama za upweke wa Mwenyezi Mungu na ukubwa wa neema Zake kwa watu wanaoelewa sehemu za hoja na wanaozifahamu dalili za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka juu ya upweke Wake na kustahiki Kwake Peke Yake kuabudiwa.
Pamoja na hizi hoja za kukata, kinatoka kikundi cha watu wakichukua, badala ya Mwenyezi Mungu, masanamu na wategemewa wakiwafanya ni kama Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuwapa mapenzi, heshima na twaa, Mambo yasiyostahiki kufanyiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na Waumini, mapenzi yao kwa Mwenyezi Mungu ni makubwa zaidi kuliko mapenzi ya hawa makafiri kwa Mwenyezi Mungu na kwa waungu wao. Sababu Waumini wamemtakasia Mwenyezi Mungu mapenzi yao yote. Na hao makafiri wamemshirikisha Mwenyezi Mungu katika mapenzi. Na lau wangalijua wale waliojidhulumu nafsi zao kwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu katika maisha ya kidunia, pindi watakapoiona adhabu ya Akhera, kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Peke Yake Mwenye nguvu zote na kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa adhabu, hawangaliwafanya wasiokuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni waungu wakawa wanawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, na kujikurubisha nao Kwake.
Watakapoiyona adhabu ya Akhera, watajitenga wale viongozi waliofuatwa kujiepusha na wale waliowafuata katika ushirikina na zitawakatikia wao aina zote za mawasiliano waliyojifungamanisha nayo duniani: ya ujamaa, ufuasi, dini na mengineyo yasiyokuwa hayo.
Na wale wafuasi watasema, «Twatamani tuwe na marejeo ya duniani, ili tutangaze kujitenga kwetu na hawa viongozi kama walivyotangaza kujitenga kwao na sisi.» Na kama Alivyowaonesha Mwenyezi Mungu ukali wa adhabu Yake, Siku ya Kiyama, Atawaonesha vitendo vyao viovu kuwa ni majuto kwao. Na hawatakuwa ni wenye kutoka Motoni kabisa.
Enyi watu, kuleni katika riziki ya Mwenyezi Mungu, iliyoko kwenye ardhi, ile ambayo Amewahalalishia nyinyi, nayo ni iliyo tohara isiyokuwa najisi, inayonufaisha isiyodhuru wala msifuate njia za Shetani katika kuhalalisha, kuharamisha, uzushi na maasia. Hakika Yeye ni adui yenu mwenye uadui uliyo wazi.
Hakika Shetani anawaamuru mfanye kila sampuli ya dhambi baya linalowatia uovuni, na kila maasia yenye upeo wa uchafu, na mumzulie Mwenyezi Mungu urongo, kama kuharamisha halali na mangineyo, pasi na ujuzi wowote
Na pindi Waumini wasemapo, wakiwanasihi viongozi wa upotofu, «Fuateni Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Qur’ani na uongofu,» wao huendelea kuwa wakakamavu katika kuwaigiza wakale wao washirikina, huku wakisema, «Hatufuati dini yenu, bali tunayafuata yale tuliyowakuta wazazi wetu wakiyafanya.» Wanawafuata baba zao hata kama walikuwa hawaelewi chochote kutoka kwa Mwenyezi Mungu wala hawana muelekeo wowote?
Na sifa za waliokufuru na wale walinganizi wao katika uongofu na imani ni kama sifa ya mchunga anayewapigia kelele wanyama na kuwakaripia, hali wao hawaelewi maana ya maneno yake isipokuwa wanasikia mwito na mlio wa sauti tu. Makafiri hao ni viziwi wameziba masikizi yao wasisikie haki, ni mabubu wamezifunga ndimi zao wasiitamke haki, ni vipofu macho yao hayazioni hoja za haki zilizo wazi. Kwa hivyo, wao hawatumii akili zao kwa mambo yenye kuwafaa.
Enyi Waumini, kuleni katika vyakula mnavyovipenda vilivyo halali ambavyo tumewaruzuku, wala msiwe kama makafiri ambao wanaviharamisha vizuri na kuvihalalisha viovu na mumshukurie Mwenyezi Mungu neema Zake kubwa kwenu kwa nyoyo zenu, ndimi zenu na viungo vyenu, iwapo kwa kweli nyinyi mnafuata amri Yake, ni wenye kusikia na kumtii Yeye, mnamuabudu Yeye Peke Yake Asiyekuwa na mshirika.
Hakika Mwenyezi Mungu Amewaharamishia nyinyi kinachowadhuru, kama mfu ambaye hakuchinjwa kwa njia ya kisheria, na damu inayotiririka, na nyama ya nguruwe, na vichinjwa ambavyo vilikusudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Na katika wema wa Mwenyezi Mungu na usahilishaji Wake kwenu ni kwamba Amewahalalishia nyinyi kuvila vitu hivi vilivyoharamishwa wakati wa dharura. Hivyo basi, yoyote ambaye dharura ilimpelekea kula kitu katika hivyo, pasi na kuwa ni mwenye kudhulumu katika kula kwake kwa kupitisha kipimo cha haja yake, wala kuikiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu katika yale aliyohalalishiwa, basi huyo hana dhambi kwa hilo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao.
Hakika wale wafichao yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika vitabu vyake miongoni mwa sifa za Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na mengineyo ya haki na wakawa na pupa la kuchukua badali ndogo ya pambo la maisha ya duniani kama malipo ya kuficha hayo. Hawa hawakili kile wakilacho kwa kuficha haki isipokuwa moto wa Jahanamu utakaokuwa ukiwaka kwa ukali katika matumbo yao. Wala Mwenyezi Mungu Hatasema nao Siku ya Kiyama kwa hasira Zake na machukivu Yake juu yao, wala Hatawatakasa na uchafu wa madhambi yao na ukafiri wao, na itawapata adhabu iumizayo.
Hao wanaosifika na sifa hizi wamechagua upotevu wakaacha uongofu, na wakachagua adhabu ya Mwenyezi Mungu wakaacha msamaha wake. Ni ujasiri ulioje wao wa kuchagua Moto kwa kufanya vitendo vya watu wa Motoni! Anastaajabu Mwenyezi Mungu kwa kujitokeza kwao kulifanya hilo. Basi oneni ajabu, enyi watu, juu ya ujasiri wao na uvumilivu wao kwenye Moto na kukaa kwao humo. Maneno haya yametumika kwa njia ya kuwatweza na kuwachezea.
Adhabu hiyo ambayo wamestahili iwapate, ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu Ameteremsha Vitabu Vyake, kwa Mitume Wake, vikiwa ni vyenye kukusanya haki iliyo wazi, wakaikanusha haki hiyo. Na kwa hakika, wale waliohitalifiana katika Kitabu, wakaamini baadhi yake na kukanusha baadhi yake, wako katika ugonvi na mfarakano ulio mbali na uongofu na usawa.
Hapana kheri, mbele ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kuelekea kwenye Swala upande wa mashariki na magharibi, iwapo hilo halitokamani na amri ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake. Hakika kheri yote iko katika imani ya aliyemuamini Mwenyezi Mungu na akamkubali kuwa Ndiye muabudiwa, Peke Yake, Hana mshirika Wake, na akaiamini Siku ya kufufuliwa na Malipo, na akawaamini Malaika wote na vitabu vyote vilivyoteremshwa, na Mitume wote bila kubagua, na akatoa mali yake kwa hiyari yake, pamoja na kuwa anayapenda sana, kuwapa jamaa zake na mayatima wenye uhitaji waliofiliwa na wazazi wao hali wao wako chini ya umri wa kubaleghe, na akawapa masikini ambao ufukara umewaelemea, na wasafiri wanaohitaji walio mbali na watu wao na mali yao, na waombaji ambao imekuwa ni dharura kwao kuomba kwa uhitaji wao mkubwa, na akatoa mali yake katika kuwakomboa watumwa na mateka, na akasimamisha Swala na akatoa zaka za faradhi, na wale wenye kutekeleza ahadi, na mwenye kusubiri katika hali ya ufukara wake na ugonjwa wake na katika vita vikali. Hao wenye kusifika kwa sifa hizo, ndio waliokuwa wakweli katika imani zao, na wao ndio waliojikinga mateso ya Mwenyezi Mungu wakajiepusha na vitendo vya kumuasi.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafanya vitendo vinavyoambatana na Sheria ya Mwenyezi Mungu Alioifanya faradhi kwenu kwamba mlipize kisasi kwa muuaji aliyeua kwa kukusudia, kwa sharti ya kufanya usawa na kufananisha malipo: auawe muungwana kwa kumuua mfano wake, na mtumwa kwa mfano wake, na mwanamke kwa mfano wake. Na yule atakayesamehewa na msimamizi wa aliyeuawa kwa kumuondolea kisasi na kutosheka kwa kuchukua dia, nayo ni kiwango cha mali maalumu akitoacho mhalifu kikiwa ni badali ya kusamehewa, ni juu ya pande mbili zijilazimishe tabia njema: yule msimamizi adai diya yake bila kutumia nguvu, na yule muuaji ampatiye haki yake kwa wema bila kuchelewesha wala kupunguza. Msamaha huo, pamoja na kupokea hiyo dia, ni masahilisho ya Mola wenu na ni huruma kwenu kwa ule usahali na kujinufaisha. Hivyo basi,mwenye kumuua muuaji baada ya msamaha na kupokea dia, atapata adhabu kali ya kuuawa kwa njia ya kisasi duniani au kutiwa Motoni Akhera.
Na hakika katika kuwekwa sheria ya kisasi na utekelezaji wake kwa kutarajia kufikia uchaji Mwenyezi Mungu na kumuogopa kwa kumtii daima, kuna maisha ya amani kwenu, enyi wenye akili timamu..
Mwenyezi Mungu Amewafaradhia nyinyi, iwapo mmoja wenu zimedhihiri kwake alama za mauti na vitangulizi vyake, akiwa ameacha mali, atoe wasia wa sehemu ya mali yake iyende kwa wazazi wake wawili na jamaa zake alio karibu naye, pamoja na kuchunga uadilifu, asimuache masikini na akatoa wasia wake kwa tajiri, wala wasia wake usizidi thuluthi ya mali. Hiyo ni haki thabiti ambayo wenye kumcha Mwenyezi Mungu waitenda. Hii ilikuwa kabla ya kuteremka zile aya ambazo Mwenyezi Mungu aliweka fungu la kila mrith.
Yule atakaye kuubadilisha wasia wa maiti baada ya kuusikia kutoka kwake kabla hajafariki, dhambi litakuwa ni la yule aliyebadilisha na kugeuza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuusikia wasia wenu na maneno yenu, ni Mjuzi zaidi wa yale yanayofichwa na nyoyo zenu kuhusu kuelekea upande wa haki na uadilifu au ujeuri na udhalimu, na Atawalipa kwa hilo.
Basi yoyote atakayejua kuwa mwenye kuusia amepinduka, kwa kuiacha haki katika wasia wake kwa njia ya kukosea au kukusudia, akamnasihi mtoaji wasia, wakati wa kutoa wasia, afanye uadilifu, na iwapo hilo halikuwa akaleta upatanishi kati ya pande zinazohusika kwa kugeuza wasia ili ulingane na Sheria, basi atakuwa hana dhambi katika kupatanisha huku. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kuwasamehe waja wake, ni Mwenye huruma kwao.
Enyi ambao mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mukaifuata Sheria Yake kivitendo, Mwenyezi Mungu Amewafaradhia kufunga, kama Alivyowafaradhia uma waliokuweko kabla yenu, ili mupate kumcha Mola wenu na kuweka kinga kati yenu na maasia, kwa kumtii na kumuabudu Peke Yake.
Amewafaradhia Mwenyezi Mungu kufunga siku zinazojulikana idadi yake, nazo ni siku za mwezi wa Ramadhani. Basi yule kati yenu atakuwa mgonjwa, ikawa ni uzito kwake kufunga, au akawa ni msafiri, basi aweza kufungua. Na itamlazimu kufunga idadi ya siku nyengine zinazolingana na idadi ya siku alizokula. Na ni juu ya wale ambao kwao ni vigumu kufunga na ikawa inawaelemea maelemeo yasiyochukulika, kama mzee mkongwe na mngonjwa asiyetarajiwa kupoa, watoe fidiya ya kila siku ambayo watafungua, nayo ni kulisha masikini. Na yule atakayezidisha katika kiwango cha fidiya, kwa hiyari yake, basi hilo ni bora kwake. Na kufunga kwenu ni bora kwenu, pamoja na kuhimili shida, kuliko kutoa fidiya, iwapo mnazijua fadhila kubwa zipatikanazo kwenye kufunga mbele ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Mwezi wa Ramadhani ambao Ameanza Mwenyezi Mungu kuteremsha Qur’ani katika usiku wa cheo na utukufu, laylatul qadr, ilii kuwaongoza watu kwenye haki. Ndani yake Amezifungua wazi dalili za uongofu wa Mwenyezi Mungu na upambanuzi baina ya haki na batili. Kwa hivyo, mtu atakayeufikia mwezi huo, akawa ni mzima na mkazi wa mjini, basi na aufunge mchana wake. Mgojwa na msafiri wanaruhusiwa kufungua, kisha walipe idadi ya siku walizofungua. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anawatakia usahali na wepesi katika Sheria Zake, wala Hawatakii uzito na mashaka, na ili mupate kukamilisha idadi ya kufunga mwezi mzima na mumalize kufunga kwa kwa kumtukuza Mwenyezi Mungu katika Idi ya Mfungo na mpate kumshukuru juu ya zile neema Alizowaneemesha nazo za uongofu, taufiki na usahali.
Na watakapo kukuuliza, ewe Nabii, waja Wangu kuhusu Mimi, waambie, «Mimi Niko karibu na wao, Nasikia maombi ya muombaji yoyote anaponiomba.Basi, ni wanitii Mimi katika Niliowaamrisha nayo na Niliowakaza nayo na waniamini Mimi, wapate kuongokewa kwenye maslahi yao ya dini yao na dunia yao. Katika ayah ii pana utoaji habari kutoka Kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, kuhusu ukaribu Wake kwa waja Wake, ukaribu unaolingana na utukufu Wake.
Amewahalalishia Mwenyezi Mungu masiku ya mwezi wa Ramadhani kuwaingilia wake zenu. Wao ni sitara na hifadhi kwenu, na nyinyi ni sitara na hifadhi kwao. Anajua Mwenyezi Mungu kwamba nyinyi mulikuwa mkizidhiki nafsi zenu kwa kuenda kinyume na yale ambayo Mwenyezi Mungu Aliyaharimisha kwenu ya kuwaingilia wanawake baada ya Isha katika masiku ya kufunga- hilo lilikuwa mwanzo wa Uislamu-, Mwenyezi Mungu Alikubali toba yenu na Akawatolea nafasi kwa hili jambo. Basi sasa waingilieni na mtafute kile Alichowakadiria Mwenyezi Mungu, miongoni mwa watoto, na kuleni na kunyweni mpaka ujitokeze kwenu mwangaza wa asubuhi utengane na weusi wa usiku kwa kujitokeza alfajiri ya kweli. Kisha kamilisheni kufunga kwa kujizuia na venye kutangua mpaka kuingia usiku kwa kutwa jua. Wala musiwaingilie wake zenu, au kufanya kitu cha kusababisha kuwaingilia, iwapo muko kwenye itikafu misikitini, sababu hilo laharibu itikafu- nako ni kukaa msikitini kwa muda maalumu kwa nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka-. Hukumu hizo, ambazo mwenyezi Mungu Amezifanya ni Sheria kwenu, ndiyo mipaka Yake itenganishayo kati ya halali na haramu. Basi msiikaribie, ili msije mkaingia katika haramu. Kwa mfano wa ubainifu huu ulio wazi, Mwenyezi Mungu Anazifafanua aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wamche na kumuogopa.
Na wasile baadhi yenu mali ya wengine kwa njia ya batili, kama kuapa yamini la urongo, kunyang’anya, kuiba, kuhonga, kula riba na mfano wa hayo.Wala msipeleke kwa mahakimu hoja potofu ili mpate kula kwa njia ya utesi mali ya kikundi cha watu wengine kwa njia ya batili, hali ya kuwa nyinyi mnajua uharamu wa hilo juu yenu.
Wanakuuliza watu wako, ewe Nabii, kuhusu miezi michanga na kubadilika hali zake. Waambie, Mwenyezi Mungu Ameifanya miezi kuwa ni alama za watu kujua nyakati za ibada zao zilizowekewa wakati, mfano wa Saumu na Hija, na nyakati za kuamiliana kwao. Kheri haiko katika mambo mliyoyazowea wakati wa ujahilia na mwanzo wa Uislamu ya kuingia majumbani kupitia kwa nyuma, wakati mnapotia nia ya Hija au ya Umra, mkidhani kwamba huko ndiko kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Lakini kheri ni kile kitendo cha mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na akajiepusha na maasia. Na ingieni majumbani kupitia kwenye milango yake wakati mnapohirimia Hija au Umra. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika mambo yenu yote ili mupate kufaulu kuyapata yote mnayoyapenda ya kheri ya dunia na ya Akhera.
Na piganeni, enyi Waumini, ili kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, na wale wanaopigana na nyinyi, wala msifanye yaliyokatazwa ya kukatakata viungo, kufanya hiyana (ya kuchukua kitu katika ngawira kabla ya kugawanywa), kumuua asiyefaa kuuawa miongoni mwa wanawake, watoto, wazee na wanaoingia kwenye hukumu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi wale wanaokiuka mipaka Yake na kuyahalalisha yalioharamishwa na Mewnyezi Mungu na Mtume Wake.
Na waueni wale wanaopigana na nyinyi miongoni mwa Washirikina popote mtakapowakuta, na muwtoe kutoka pahali walipowatoa, napo ni Maka. Na fitina, ambayo ni ukafiri na ushirikina na kuwazuia watu na Uislamu, ni mbaya zaidi kuliko nyinyi kuwaua wao. Wala msiwaanzie vita katika Msikiti wa Haramu, kwa kuheshimu sehemu zake tukufu, mpaka wao wawaanzie vita humo. Na iwapo watawapiga vita katika Msikiti wa Haramu, basi waueni hapo. Mfano wa malipo hayo ya kutisha yatakuwa ndiyo malipo ya Makafiri.
Na iwapo watayaacha yale walionayo ya ukafiri na ya kuwapigeni vita kwenye Msikiti wa Haramu na wakaingia katika Imani, kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma na wao.
Na endeleeni, enyi Waumini, kuwapiga vita washirikina wafanyao uadui mpaka kusiweko tena kuwafitini Waislamu na dini yao wala kumshirikisha Mwenyezi Mungu, na ibakie dini kuwa ni ya Mwenyezi Mungu Peke Yake, hali ya kuwa safi, haabudiwi yoyote pamoja na Yeye. Na iwapo watakomeka na ukafiri na vita, basi komekeni nao.Kwani mateso hayawi ela kwa wale wanaoendelea na ukafiri wao na uadui wao.
Kuwapiga kwenu vita, enyi Waumini, hao washirikina, katika mwezi ambao Mwenyezi Mungu Ameharamisha vita, ni malipo ya wao kuwapiga nyinyi vita mwezi mtukufu.Na yule anayekeuka yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu ya pahali na zama, atapewa mateso yanayofanana na kitendo chake na yanayotokana na jinsi ya kosa alilolifanya. Basi atakayewafanyia uadui kwa vita au chinginecho, wapeni adhabu ifananayo na uovu wao, wala pasiwe na dhiki kwenu kuhusu hilo. kwa sababu wao ndio wenye kuanza uadui. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na msipitishe kipimo cha kufanana kuadhibu. Na juenu kuwa Mwenyezi Mungu Yuko pamoja na wale wamchao na wanaomtii kwa kutekeleza Aliyoyafanya faradhi na kuyaepuka Aliyoyafanya haramu.
Na endeleeni, enyi Waumini, kutoa mali kwa kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kupigana jihadi katika njia yake. Wala msiziingize nafsi zenu kwenye maangamivu kwa kuacha jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuacha kutoa katika njia Yake. Na fanyeni wema katika kutoa na kutii, na mzifanye amali zenu zote ni zenye kutakasika kwa kukusudiwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda watu wenye kutakasa nia na kufanya wema.
Na tekelezeni Hija na Umra ziwe zimekamilika, zimetakasika na kukusudiwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.Na iwapo kitwazuia, kwenda kuzikamilisha baada ya kuzihirimia, kizuizi chochote, kama adui na ugonjwa, lililo wajibu kwenu ni kuchinja kitakacho kuwa chepesi kwenu miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi au kondoo, hali ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ili mpate kutoka katika ihramu zenu kwa kunyoa nywele za kichwa au kuzipunguza.Wala msinyoe vichwa vyenu, mkiwa mumezuiwa, mpaka mwenye kuzuiwa amchinje mnyama wake pale pahali alipozuiwa kisha ajitoe kwenye ihramu yake kama alivyochinja Mtume(S.A.W) hapo Hudaibiya kisha akanyoa kichwa chake. Na asiyekuw yule aliyezuiwa, hatachinja mnyama wake mpaka afike ndani ya eneo la tukufu la Maka, ambapo ndipo pahali pake, sku ya idi ambayo ni siku ya kumi na siku zifuatazo za Tashrīq. Na ambaye kati yenu atakuwa mngonjwa au ana udhia katika kichwa chake akawa anahitajia kunyoa, naye yuko kwenye ihramu, basi atanyoa na ni juu yake atoe fidya: afunge siku tatu au awape sadaka masikini sita, kila mmoja nusu pishi ya chakula, au achinje mbudi au kondoo awape mafukara wa eneo tukufu la Maka. Na pindi mtakapo kuwa kwenye hali ya amani na afya, basi atakaye kujistarehesha kwa kufanya Umra ndani ya Hija, nako ni kuihalalishia mambo alioharamhshiwa kwa sababu ya ihramu baada ya kumaliza Umra yake, inampasa kuchinja kiwezekanacho katika wanyama. Na yule aliyekosa mnyama wa kuchinja, itamlazimu afunge siku tatu ndani ya miezi ya Hija na siku saba mtakapo kumaliza amali za Hija na mkarudi kwenu; hizo ni siku kumi kamili, hapana budi kuzifunga.Mnyama huyo wa kuchinjwa, na yale yaliyopasa juu yake ya kufunga, ni kwa yule ambaye watu wake si wakazi wa ardhi tukufu ya Haram. Na muogopeni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na mujilazimishe kuzitekeleza amri Zake na kujiepusha na Makatazo Yake, na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa mateso kwa yule aendaye kinyume na amri Zake na na kufanya Aliyoyakemea.
Wakati wa Hija ni miezi ijulikanayo, nayo ni Mfungomosi, Mfungopili na siku kumi za Mfungotatu.Basi mwenye kujilazimisha nafsi yake kuhiji ndani ya miezi hiyo, kwa kutia nia ya kuhirimia Hija, ni haramu kwake kuundama na vitangulizi vyake vya kimaneno na kivitendo. Pia ni haramu kwake kutoka kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kutenda maasia, kubishana, katika Hija, kuletako hasira na chuki. Na wema wowote mnaoufanya, Mwenyezi Mungu Anaujua, na Atamlipa kila mtu kwa amali yake. Na jichukulieni akiba ya chakula na kinwaji kwa safari ya Hija, na akiba ya amali njema kwa nyumba ya Akhera. Hakika akiba iliyo bora zaidi ni kumuogopa Mwenyezi Mungu. Basi niogopeni, enyi wenye akili timamu.
Hapana ubaya wowote kwenu kutafuta riziki itokayo kwa Mola wenu, kwa kupata faida ya biashara, ndani ya siku za Hija.Basi mtakapo kuondoka, baada ya kutwa jua, mkirejea kutoka Arafa- napo ni pahali ambapo Mahujaji husimama siku ya tisa ya Mfungotatu-, mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kuleta Tasbihi, Talbiyah(Labbaika Allahumma labbaika..) na dua katika sehemu tukufu ya Al- Mashcar al-Harām: Muzdalifa. Na mumtaje Mwenyezi Mungu kwa njia ya kisawa Aliyowaongoza nayo. Na mlikuwa kabla yauongofu huo mko katika upotevu, hamuijui haki.
Na iwe kuondoka kwenu kutoka kisimamo cha Arafa, ambapo ndipo alipoondoka Ibrahim, amani imshukie, ni katika hali ya kumkhalifu, kwa hilo, yule asiyesimama hapo miongoni mwa watu wa zama za ujinga. Na muombeni Mwenyezi Mungu Awasamehe madhambi yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaghufiria waja wake waombao maghufira, wanaotubia, ni mwenye huruma kwao.
Basi mtakapokamilisha ibada yenu na mkamaliza amali zenu za Hija, mtajeni Mwenyezi Mungu na mumsifu kwa wingi kama vile mnavyotaja fahari za wazee wenu na zaidi ya hivyo. Kwani wamo miongoni mwa watu kikundi ambacho hima yao yote ni dunia. Hapo, wao huomba wakisema, «Ewe Mola wetu, tupe duniani afya, mali na wana.» Hao hawana Akhera hisa wala fungu lolote, kwa kuipuza Akhera na kujishughulisha na dunia tu.
Na miongoni mwa watu kuna kikundi chenye Imani kinachosema katika dua yake, «Mola wetu, tupe duniani afya, mali, elimu inufaishayo, vitendo vyema na mengineyo katika mambo ya dini na dunia. Na katika Akhera, tupe Pepo na utuepushie adhabu ya Moto.» Dua hii ni miongoni mwa dua zilizokusanya. Kwa hivyo, ilikuwa ni dua ambayo Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikuwa akiiyomba mara nyingi zaidi, kama ilivyothibiti kwenye Sahihi Mbili: ya Bukhari na ya Muslim.
Wale wenye kuomba dua hii wana thawabu kubwa kwa sababu ya amali njema walizozichuma. Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuvihesabu vitendo vya waja wake na Mwenye kuwalipa navyo.
Na mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kuleta Tasbihi na Takbiri, katika siku chache, nazo ni siku za tshrīq: siku ya kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu za mwezi wa Mfungotatu.Atakaye kufanya haraka kuondoka Mina kabla ya kutwa jua la siku ya kumi na mbili, baada ya kurusha vjiwe, hana makosa. Na yule atakaye kuchelewa kwa kulala Mina kungojea mpaka arushe vijiwe siku ya kumi na tatu, pia hana makosa, kwa aliyemcha Mwenyezi Mungu katika Hija yake. Na kuchelewa ni bora zaidi, maana huko ni kujiongezea mapato katika ibada na kufuata kitendo cha Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, enyi Waislamu, na mumweke mbele katika amali zenu zote; na mjue kwamba nyinyi kwake Yeye Peke Yake mtakusanywa baada ya kufa kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa.
Na baadhi ya watu miongoni mwa wanafiki yanakuvutia, ewe Mtume, maneno yake yaliyo fasaha ambayo kwayo anataka fungu la hadhi za duniani, si za Akhera, na anaapa huku akimshuhudisha Mwenyezi Mungu yaliyo moyoni mwake ya kuupenda Uislamu, hali ya kuwa yeye ana uadui na utesi mkubwa juu ya Uislamu na Waislamu. Huo ni upeo wa ujasiri juu ya Mwenyezi Mungu.
Na anapoondoka kutoka kwako, ewe Mtume, hufanya bidii na akachangamka katika ardhi ili alete uharibifu humo na kutilifisha mazao ya watu na kuua wanyama wao. Na Mwenyezi Mungu Hapendi uharibifu.
Na anaponasihiwa mnafiki huyo mharibifu na akaambiwa, «Mche Mwenyezi Mungu,ujihadhari na adhabu Yake na ukomeke na kuleta uharibifu katika ardhi,» huwa hakubali nasaha. Bali kile kiburi chake na mori wa kijinga humfanya kutenda maovu zaidi. Basi adhabu yenye kumtosheleza yeye na kumkifu ni Jahanamu. Na hakika uovu wa tandiko ndilo hilo.
Na baadhi ya watu huziuza nafsi zao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu, kwa kupigana jihadi katika njia Yake na kujilazimisha kumtii. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja, Anawarehemu waja wake Waumini rehema kunjufu, katika ulimwengu wao na Akhera yao, na kuwalipa malipo mazuri zaidi.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mola na Muhammad kuwa ndiye Mtume na Uislamu kuwa ndiyo Dini, ingieni katika sheria zote za Uislamu, hali ya kutekeleza hukumu zake zote, wala msiache chochote kati yazo, wala msiandame njia za Shetani katika yale anayowaitia ya maasia.Hakika Shetani kwenu ni adui mwenye uadui uliyo wazi. Basi jihadharini naye.
Na iwapo mtapondoka kwenye njia ya haki, baada ya kujiliwa na hoja wazi-wazi za Qur’ani na Suna, basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, hakuna chochote kilicho nje ya mamlaka Yake, ni Mwingi wa hekima kwenye amri Zake na Makatazo yake, Anaweka kila kitu pahali pake palinganapo nacho.
Hawangojei hawa wakaidi wenye kukanusha, baada ya kusimama dalili wazi, isipokuwa Awajie Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, kwa namna inayolingana na Yeye, Aliyetakasika na kila sifa mbaya, katika vivuli vya Mawingu Siku ya Kiyama ili Aamue baina yao kwa hukumu adilifu, na waje Malaika. Wakati huo, Atahukumu Mwenyezi Mungu, kati yao, hukumu Yake. Na kwake Yeye Peke Yake hurudishwa mambo yote ya viumbe.
Waulize, ewe Mtume, Wana wa Isrāīl wanaokufanyia ukaidi, «Ni aya ngapi zilizo wazi tulizowapa katika vitabu vyao zinazowaongoza wao njia ya haki, wakazikanusha,wakazipa nyongo na wakazipotosha kwa kuzitoa kwenye malengo yake.» Na atakayebadisha neema ya Mwenyezi Mungu, nayo ni dini Yake, na akaikanusha baada ya kuijua na hoja yake kumsimamia, basi Mwenyezi Mungu ni Mkali wa mateso kwake.
Wale walioukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu wamepambiwa maisha ya dunia na vilivyomo humo vya matamanio na vilivyo tamu, na huku wao wanawafanyia shere Waumini. Na hawa wanaomcha Mola wao watakuwa juu ya Makafiri wote Siku ya Kiyama, ambapo Mwenyezi Mungu Atawatia katika Pepo ya daraja za juu na Atawateramsha Makafiri ndani ya mashimo ya Moto ya chini. Mwenyezi Mungu Anamruzuku Amtakaye, katika viumbe vyake, bila ya hesabu.
Watu walikuwa ni kundi moja, wameafikiana katika kumuamini Mwenyezi Mungu, kisha walitafautiana katika dini yao.Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Aliwatuma Manabii, wakiwa ni walinganizi wa dini ya Mwenyezi Mungu, ni wabashiri wa Pepo kwa anayemtii Mwenyezi Mungu na ni waonyi wa Moto kwa anayemkanusha na kumuasi. Na Akateremsha, pamoja nao, vitabu vya mbinguni vilivyokusanya haki, ili wahukumu baina ya watu kwa yaliyomo ndani, katika yale waliyotafautiana juu yake. Na hawakutafautiana juu ya jambo la Mtume na Kitbu alichokuja nacho, kwa uhasidi na udhalimu, isipokuwa ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewapa Taurati na wakayajua yaliyomo ndani miongoni mwa hoja na hukumu. Hapo Mwenyezi Mungu, kwa fadhila zake, aliwaafikia Waumini kuipambanua haki na batili na kuyajua yale waliotafautiana juu yake. Mwenyezi Mungu Anampa taufiki amtakaye, miongoni mwa waja wake, kufuata njia iliyonyooka.
Kwani mlidhani, enyi Waumini, kwamba mtaingia Peponi, na bado haijawapata mitihani kama ile iliyowapata Waumini waliopita kabla yenu: ya ufukara, maradhi, kitisho na babaiko, na wakatikiswa kwa aina nyingi za misukosuko ya kutisha, mpaka akasema Mtume wao na Waumini pamoja naye, kwa njia ya kuharakisha nusura ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, «Ni lini hiyo nusura ya Mwenyezi Mungu?» Jueni kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu iko karibu na Waumini.
Wanakuuliza watu wako, ewe Nabii, «Ni kitu gani wakitoe, katika aina za mali zao, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Na watoe kumpa nani?» Waambie, «Toeni kheri yoyote iliyo tahfifu kwenu katika aina za mali mazuri ya halali, na utoaji wenu uwe ni kwa wazazi wawili, walio karibu katika watu wenu na kizazi chenu, mayatima, mafukara na msafiri mwenye uhitaji aliye mbali na watu wake na mali yake. Na kheri yoyote mtakayoifanya, basi Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni mwenye kuijua.»
Mwenyezi Mungu Amewafaradhia, enyi Waumini, kupigana na Makafiri, hali ya kuwa ni jambo lenye kuchukiwa na nyinyi kimaumbile, kwa uzito wake na hatari zake nyingi. Na huenda mkakichukia kitu nacho, kwa uhakika wake, ni kheri kwenu. Na huenda mkakipenda kitu kwa ajili ya raha na ladha za karibu zilizomo, nacho, kwa uhakika wake, ni shari kwenu. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Analijua lenye kheri kwenu, na nyinyi hamlijui hilo. Kwa hivyo harakisheni kupigana jihadi katika njia Yake.
Wanakuuliza washirikina, ewe Mtume, kuhusu mwezi mtukufu wa Haram, «Inafaa kupigana ndani yake?» Waambie, «Kupigana katika mwezi mtukufu wa Ḥarām ni jambo kubwa kwa Mwenyezi Mungu kuuhalalisha na kumwaga damu ndani yake. Na kuwazuia kwenu watu kuingia katika Uislamu, kwa kuwaadhibu na kuwatisha na kumkanusha kwenu Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na dini Yake, na kuwzuia Waislamu wasiingie kwenye Msikiti wa Haram, na kumtoa Nabii na waliogura naye kutoka huko, ambao wao ndiwo wakazi na wasimamizi wake, hilo ni dhambi kubwa mno na nikosa kubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuliko kupigana katika mwezi mtukufu wa Haram. Na ushirikina mlionao ni jambo kubwa zaidi na baya zaidi kuliko kuua katika mwezi mtukufu wa Haram. Na Makafiri hawa hawatatishika na kukomeka na makosa yao, bali wao ni wenye kuendelea nayo. Wala hawataacha kuwapiga vita mpaka wawatoe kwenye Uislamu kuwatia kwenye ukafiri, iwapo wataweza kulihakikisha hilo. Na mwenye kuwatii wao, kati yenu, enyi Waislamu, akaacha dini yake na akafa katika ukafiri, basi amali zake zitapotea duniani na Akhera na atakuwa ni miongoni mwa watakaodumu kwenye moto wa Jahanamu, hatatoka humo milele.
Hakika wale ambao walimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakazitumia Sheria zake, wale waioyaacha Makaazi yao na wakapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, hao ni wenye kutaraji kupata fadhila za Mwenyezi Mungu na thawabu Zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya waja Wake Waumini, ni Mwenye kuwarehemu rehema kunjufu.
Wanakuuliza Waislamu, ewe Nabii, hukumu ya kutumia khamr kwa kunywa, kuuza na kununua. Khamr ni kila chenye kulewesha kinachofinika akili na kuziba, kiwe ni chenye kunywewa au kuliwa. Na wanakuuliza kuhusu hukumu ya kamari. Kamari ni kupokea au kutoa mali kwa bahati nasibu, nayo ni mashindano ambayo yana kupeana badali kutoka pande mbili za ushindani. Waambie, «Katika hayo pana madhara mengi na uharibifu mwingi katika dini na dunia, na akili na mali. Na yamo, katika mambo mawili hayo, manufaa kwa watu, kwa upande wa kuchuma mali na mengineyo. Na madhambi yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake, kwani huzuia kumtaja Mwenyezi Mungu na kusali, na yote mawili yanaleta uadui na kuchukiana kati ya watu na yanaharibu mali. Huu ulikuwa ni utayarishaji wa kuyaharamisha mambo mawili hayo. Na wanakuuliza kuhusu kiwango ambacho wao wakitoe katika mali yao kwa njia ya sadaka na kujitolea.Waambie, «Toeni kiwango kinachozidi baada ya mahitaji yenu.» Mfano wa haya maelezo yaliyo wazi, Mwenyezi Mungu Anawabainishia aya na hukumu za Sheria, ili mpate kuyafikiria yenye manufaa kwenu
duniani na Akhera. Na wanakuuliza, ewe Mtume, kuhusu mayatima, waingiliane nao vipi katika maisha yao na mali yao. Waambie, «Kuwatengezea kwenu mambo yao ni bora. Basi, wafanyieni daima yanayowafaa wao zaidi.Na iwapo mtatangamana nao katika mambo ya maisha, basi wao ni ndugu zenu katika Dini. Na ni juu ya ndugu kuyalinda maslahi ya ndugu yake.Mwenyezi Mungu Anamjua mpotezaji wa mali ya mayatima na yule mwenye pupa la kuyahifadhi. Na lau Mwenyezi Mungu Angetaka, angewatia dhiki na mashaka kwa kuwaharamishia mtangamano. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika uumbaji Wake, uendeshaji mambo Wake na upitishaji sheria Wake.
Wala msiwaoe, enyi Waislamu, wanawake washirikina wanaoabudu masanamu mpaka waingie katika Uislamu. Na mjue kwamba mwanamke kijakazi, asiyekuwa na mali wala utukufu wa nasaba, anayemuamini Mwenyezi Mungu, ni bora kuliko mwanamke mshirikina, hata kama huyo mshirikina muungwana atawavutia. Wala msiwaoze wanawake wenu waumini, wakiwa ni vijakazi au waungwana, wanaume washirikina mpaka wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Na mjue kwamba mtumwa mwenye Imani, pamoja na ufukara wake, ni bora kuliko mshirikina, hata kama huyo mshirikina atawavutia. Hao wasifikao na ushirikina, wanaume na wanawake, wanamwita kila atangamanaye nao kwenye mambo yapelekayo Motoni. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Anawaita waja Wake kwenye dini Yake ya haki inayowapeleka Peponi na kusamehawa madhambi yao kwa idhini Yake. Na Yeye Anabainisha aya Zake na hukumu Zake kwa watu, ili wapate kukumbuka na wazingatie.
Na wanakuuliza kuhusu hedhi, nayo ni damu inayotiririka kimaumbile kutoka kwenye uzao wa wanawake katika nyakati maalumu.Waambie, ewe Mtume, «Hiyo hedhi ni udhia wenye manyezi unaomdhuru mwenye kuusongelea. Hivyo basi, jiepusheni kuwaingilia wanawake kwenye kipindi cha hedhi mpaka damu ikome. Damu ikomapo, na wakaoga, waingilieni kupitia pale pahali Alipowahalalishia Mwenyezi Mungu, napo ni tupu ya mbele siyo ya nyuma. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waja Wake wenye kutubia na kuomba msamaha kwa wingi na Anawapenda waja Wake wenye kujisafisha ambao hujitenga na maovu na uchafu.
Wake zenu ni pahali pa makulima yenu, mnaweka tone la manii ndani ya uzao wao, wakatoka humo watoto kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, waingilieni pale pahali pake pa kuingiliwa tu, napo ni tupu ya mbele, kwa namna yoyote mtakayo. Na zitangulizieni nafsi zenu amali njema kwa kuzitunga amri za Mwenyezi Mungu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na mjue kwamba mtakutana na Yeye kwa kuhesabiwe Siku ya Kiyama. Na wape bishara njema Waumini, ewe Nabii, kwa yale ambayo yatawafurahisha na kuwapendeza ya malipo mema huko Akhera.
Wala msikifanye, enyi Waislamu, kiapo chenu kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni chenye kuwazuia nyinyi kufanya wema, kuunga kizazi, kumcha Mwenyezi Mungu na kusuluhisha kati ya watu. Nako ni iwapo mtaitwa kufanya lolote katika hayo, mkakataa na kutoa hoja kwamba mliapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hamtalifanya. Bali ni juu ya Mwenye kuapa ageuze kiapo chake, afanye vitendo vya kheri na atoe kafara ya kiapo chake wala asizowee jambo hilo. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu, ni Mwenye kuzijua hali zenu zote.
Mwenyezi Mungu Hatawaadhibu nyinyi kwa sababu ya viyapo vyenu mnavyoviapa bila kukusudia, lakini Atawaadhibu kwa viapo vilivyokusudiwa na nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa yule anayetubia Kwake, ni Mpole kwa mwenye kumuasi kwa kuwa hamharakishii mateso.
Wale wanaoapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba hawatawaingilia wake zao, wana muda wa kusubiriwa wa miezi minne. Iwapo watarudi kabla kumalizika hiyo miezi mine, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasamehe makosa yaliyofanywa na wao ya kiapo kwa sababu ya kurudi kwao, ni Mwenye huruma nao.
Na iwapo wameamua kutaliki, kwa kuendelea kwao na kiapo chao na kuacha kuundama, Basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yao, ni Mjuzi wa Malengo yao, na Atawalipa kwayo.
Na wanawake waliotalikiwa, waingiao hedhini, itawalazimu kungojea bila kuolewa muda wa twahara tatu au hedhi tatu baada ya kutalikiwa. Kukaa kwao kipindi hicho cha eda ni ili wahakikishe kuwa uzao ni safi, hawana mamba. Wala haifai kuolewa na mume mwengine katika kipindi hicho mpaka kiishe. Wala si halali kwao kukificha kile Alichokiumba Mwenyezi Mungu katika zao zao miongoni mwa mimba au hedhi, iwapo hao wanawake walioachwa ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kikweli. Na waume wa wale waliotalikiwa wana haki ya kuwarejea wake zao hao iwapo bado wamo kwenye maeda yao. Na hilo la kuwarejea inapasa liwe ni kwa lengo la kheri na kutengeneza, wala lisiwe ni kwa lengo la kuwadhuru na kuwatesa kwa kulirefusha eda. Na wanawake wana haki kwa waume zao kama waume walivyo na haki kwa wake zao, kwa njia ya wema. Na wanaume kwa wake zao wana cheo cha zaidi kwa kukaa nao kwa uzuri, kutangamana nao kwa wema, kusimamia nyumba na kwamba talaka iko mikononi mwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi, Ana enzi na uwezo wa kutendesha nguvu, ni Mwingi wa hekima, Huweka kila kitu mahali pake panapalingana.
Talaka ambayo mtu anaweza kumrejea mke wake ni mara mbili, moja baada ya nyegine. Basi hukumu ya Mwenyezi Mungu, baada ya kila talaka, ni kumshikilia mwanamke kwa wema na tangamano zuri baada ya kumrejea au kumpa nafasi ya kwenda kwao pamoja na maelewano mema kwa kumtekelezea haki zake, na asimtaje mtalaka wake kwa uovu. Wala si halali kwenu, enyi Waumini, kuwapokonya chochote miongoni mwa vile mlivyowapa, kama mahari na vinginevyo. Isipokuwa wakiogopa waliooana kuwa hawataweza kutekeleza haki za unyumba, hapo mambo yao yatawekwa mbele ya mawalii. Na watakapochelea hao mawalii kuwa wanyumba wao hawataweza kutekeleza haki na mipaka ya Mwenyezi Mungu, hakuna kosa kwa waliooana katika kile atakacho kukitoa mwanamke kumpa mume kama ridhaa ya kupata talaka. Hukumu hizo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu, inayopambanua kati ya halali na haramu, basi msiikeuke. Na wenye kusubutu kuikeuka mipaka ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, hao ndio madhalimi wa nafsi zao kwa kuzihatarisha adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na iwapo mume atamtaliki mkewe talaka ya tatu, basi mke huyo atakuwa si halali tena kwa mume huyo, isipokuwa atakapoolewa na mwanamume mwengine ndoa sahihi na akaingiliwa katika ndoa hiyo, iwapo ndoa hiyo ni ya kutakana, na si kwa nia ya kumhalalisha yule mwanamke kwa mume wake wa kwanza. Na iwapo yule mume mwengine atamuacha mke yule, au akafa na eda lake likaisha, basi hapana dhambi kwa yule mwanamke na mume wake wa kwanza kuoana kwa kifungo cha ndoa kipya na mahari mapya, ikiwa wawili hao waonelea kwamba watazitekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu Alizoziweka kwa waliooana. Hizo ni sheria za Mwenyezi Mungu zilizowekewa mipaka, Anazifunua wazi kwa watu wanaozijua hukumu Zake na mipaka Yake, kwani ni wao wanaonufaika nazo.
Pindi mtakapowataliki wanawake wakakaribia siku za kumaliza eda lao, basi warejeeni hali ya kuwa nia zenu ni kuwatekelezea haki zao kwa njia nzuri, kisheria na kidesturi, au waacheni mpaka eda lao limalizike. Na kueni na hadhari, isije ikawa kuwarejea ni kwa lengo la kuwadhuru kwa kuwafanyia uadui katika haki zao. Na yoyote atakayelifanya hilo, ameshaidhulumu nafsi yake kwa kustahiki mateso. Na wala msizifanye aya za Mwenyezi Mungu na hukumu Zake kuwa ni mchezo na upuzi. Nakumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, kwa kuwafanya Waislamu na kuwafafanulia hukumu Zake. Na yakumbukeni yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, ya Qur’ani na mafundisho ya Mtume Wake. Na mshukuruni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa neema hizi zilzo kubwa. Mwenyezi Mungu Anawakumbusha hayo na Anawatisha msende kinyume nayo. Basi, mcheni Mwenyezi Mungu na mumlindize. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu, hapana kitu chenye kufichika Kwake, na Atamlipa kila mmoja kwa anayostahiki alipwe.
Na mtakapowaacha wake zenu chini ya talaka tatu na eda lao likaisha bila nyinyi kuwarejea, basi msiwadhiki, enyi mawalii, hao walioachwa kwa kuwazuia kurudi kwa waume zao, kwa kufunga ndoa upya, wakiwa wenyewe wametaka hilo na yakapatikana maridhiano kisheria na kidesturi. Hilo aidhiwa kwalo aiyekuwa, miongoni mwenu, ni mkweli kwenye imani yake kwa Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hakika kuacha kuwazuia na kuwawezesha waume kuwaoa waliokuwa wake zao, ni jambo lenye kukuza zaidi na kutakasa zaidi heshima zenu, na ni lenye nafuu kubwa zaidi na thawabu nyingi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu Anayajua yenye maslahi kwenu; na nyinyi hamjui hilo.
Na ni juu ya wanawake waliozaa kuwanyonyesha watoto wao muda wa miaka miwili kamili, kwa yule atakaye kukamilisha unyonyeshaji. Na ni wajibu kwa mababa kuwadhamini wanyonyeshaji, waliopewa talaka, kwa chakula chao na mavazi yao kwa njia ipendekezayo kisheria na kimila. Kwani Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu ela kiasi cha uwezo wake. Na haifai kwa wazazi wawili kumfanya mototo aliyezaliwa kuwa ni njia ya kudhuriana kati yao. Na inamlazimu mrithi, mzazi anapokufa, kile kinachomlazimu mzazi, kabla hajafa, cha matumizi na mavazi. Na wazazi wanapotaka kumuachisha mtoto kunyonya, kabla kukamilisha miaka miwili, basi si makosa kwao iwapo wameridhiana na kushawiriana kwa hilo na kufikia kwenye uamuzi wenye maslahi ya mtoto. Na iwapo wazazi wawili wamekubaliana kumpa mtoto mnyonyeshaji mwengine asiyekuwa mamake ili amnyonyeshe, pia si makosa kwao., iwapo baba atampa mama haki yake, na pia atampa mwenye kunyonyesha haki kwa mujibu wa desturi zinazoeleweka kwa watu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika hali zenu zote. Na mjue kwamba Mwenyezi Mungu kwa mnayoyafanya ni muoni na Atawalipa kwayo.
Na wale wanaofariki kati yenu wakawaacha wake zao baada ya kufa kwao, italazimu wakae eda muda wa miezi minne na siku kumi, wasitoke majumbani mwao, wasijipambe wala wasiolewe. Na pindi muda huo uliotajwa uishapo, si dhambi kwenu, enyi mawalii wa wanawake, kwa yale watakayo kujifanyia nafsi zao, ya kutoka, kujipamba na kuolewa kwa njia iliyowekwa na Sheria. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kutakasika na kila sifa mbaya, ni Mtambuzi wa vitendo vyenu vya wazi na viliyofichika, na Atawalipa kwavyo.
Na wala nyinyi hamna dhambi, enyi wanaume, katika ishara mnazozitoa za kutaka kuwaoa wanawake waliofiliwa na waume zao au wale waliopewa talaka ya mwisho, wakiwa wako katika eda lao. Pia hamna dhambi katika mawazo yanayowapitia ndani ya nafsi zenu ya kutaka kuwaoa wamalizapo eda lao. Mwenyezi Mungu Anajua kwamba nyinyi mtawataja wanawake walio kwenye eda na hamtasubiri kuweza kunyamaza kutowataja, kwa udhaifu wenu. Kwa ajili hiyo, Mwenyezi Mungu amewahalalishia kuwataja kwa ishara au kwa kudhamiria ndani ya nafsi zenu. Na jihadharini kuagana nao kisiri, kwa kuzini, au kukubaliana kuoana wakiwa bado wako kwenye eda, isipokuwa mtakaposema neno lenye maana kwamba mfano wake, mwanamke huyo, waume huwa wanampendelea. Wala msikusudie kufunga ndoa katika kipindi cha eda mpaka muda wake umalizike. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Anayajua yaliyomo katika nafsi zenu, kwa hivyo muogopeni Yeye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa mwenye kutubia dhambi zake, ni Mpole kwa waja Wake, Hana haraka ya kuwatesa.
Hakuna dhambi juu yenu, enyi wanaume, iwapo mtawataliki wanawake baada ya kufunga ndoa nao na kabla ya kuwaingilia au kuwatajia mahari. Hivyo basi, waliwazenikwa kuwapa kitu chenye kuwanufaisha kwa kuwaliwaza na kuwaondolea maudhi ya talaka na kumaliza chuki. Kiliwazo hiki kinalazimu kulingana na hali ya mwanamume aliyetoa talaka: tajiri kulingana na ukunjufu wa hali yake na maskini kulingana na kile alichonacho. Kiliwazo hiko kiwe ni chenye kuambatana na Sheria. Nacho ni haki iliyothibiti juu ya wale wanaowafanyia wema watalaka wao na kujifanyia wema wao wenyewe kwa kumtii Mwenyezi Mungu.
Na iwapo mtawataliki wanawake, baada ya kufunga ndoa nao na kabla hamjawaingilia, na mkawa mumejilazimisha kuwapa kiasi maalumu cha mahari, basi inawapasa muwape nusu ya mahari mliyokubaliana, isipokuwa iwapo watalaka hao watasamehe na kuiacha ile nusu ya mahari iliyopasa wapewe, au iwapo mume atasamehe kwa kumuachia mtalaka mahari yote. Na kusamehe kwenu, enyi wanaume na wanawake, ni jambo lililo karibu zaidi na kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii. Wala msisahau, enyi watu, fadhila na wema kati yenu ambao ni kutoa ambacho si wajibu kwenu kukitoa na kusameheana haki. Hakika Mwenyezi Mungu, kwa mnayoyafanya, ni mwenye ni mwenye kuona. Anawahimiza kufanya kheri na kuwasongeza kufanya wema.
Zihifadhini, enyi Waislamu, Swala tano zilizofaradhiwa kwa kudumu nazo katika kuzitekeleza kwa nyakati zake, masharuti yake, nguzo zake yanayopasa yake. Na muhufadhi swala iliyo katikati ya swala hizo, nayo ni Swala ya Alasir Na simameni katika Swala zenu hali ya kumtii Mwenyezi Mungu, kumnyenyekea na kumdhalilikia.
Na iwapo mtawaogopa maadui maadui wenu, swalini swala ya khofu, mkiwa mwatembea au mumepanda, kwa namna yoyote ile mnayoiweza, hata kama ishara, au hata kama hamkulekea kibla. Na pindi khofu yenu itakapokwisha, swalini swala ya amani na mumtaje Mwenyezi Mungu humo. Wala msiipunguze kwakuitoa kwenye namna yake ya asili. Na mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwafundisha mambo ya ibada na hukumu ambayo hamkuwa na ujuzi nayo.
Na waume wanaofariki na wakaacha wake baada yao, inawalazimu waume hao wawekee wasia hao wake zao kwamba waliwazwe mwaka mzima kuanzia siku ya kufariki, kwa kupewa Makao katika nyumba ya mume, bila ya kutolewa na mawarithi kwa muda wa mwaka. Hilo likiwa ni maliwazo kwa yule mke na ni wema kwa aliyefariki. Na iwapo wanawake hao waliofiliwa watatoka, kwa hiyari yao kabla mwaka kumalizika, basi hamna makosa, nyinyi warithi, katika hilo. Pia, hakuna makosa kwa hao wanawake kwa kitendo chao cha halali walichojifanyia nafsi zao. Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika amri Zake na Makatazo Yake. Aya hii, hukumu zake zimeondolewa kwa neno Lake Mwenyezi Mungu Aliyetukaka, «Na wale wanaofariki kati yenu na wakaacha wake zao, (Basi wake hao) wajizuie nafsi zao miezi mine na siku kumi»(2:234).
Na wanawake waliotalikiwa wanastahiki wapewe kiliwazo cha mavazi na matumizi kwa mujibu wa mpango unaojulikana na kupendekezwa na kisheria. Hiyo ikiwa ni haki juu ya wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu katika amri Zake na Makatazo Yake.
Mfano wa maelezo hayo yaliyo wazi, katika hukumu za watoto na wanawake, Anawabainishia Mwenyezi Mungu mafunzo aya Zake na hukumu Zake kuhusu kila mnachokihitajia katika maisha yenu ya ulimwengu na marejeo yenu ya Akhera, ili mzitie akilini nz mzitumie.
Kwani hujui, ewe Mtume, kisa cha waliokimbia kutoka ardhi yao na nyumba zao, wakiwa ni maelfu mengi, wakiogopa kufa kwa sabababu ya janga la ugonjwa hatari au vita, Mwenyezi Mungu Akawaambia, «Kufeni», wakafa, papo hapo, kwa mara moja, ikiwa ni adhabu kwao kwa kukimbia kadara ya Mwenyezi Mungu, kisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Akawahuisha baada ya muda kupita, ili waukamilishe muda wa uhai wao, na ili wapate kuwaidhika na kutubia? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa kwa watu, kwa neema zake nyingi, lakini watu wengi hawazishukuru fadhila za Mwenyezi Mungu zilio kwao.
Na piganeni nao, enyi Waislamu, hao makafiri ili kuinusuru Dini ya Mwenyezi Mungu, na mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno yenu na ni Mwenye kuzijua nia zenu na vitendo vyenu.
Ni yupi ambaye atatoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, kutoa kuliko kuzuri kwa kutarajia malipo, Mwenyezi Mungu Apate kumuongezea nyongeza nyingi zisizohesabika za thawabu na malipo mema? Hakika Mwenyezi Mungu Anazuia na Anatoa. Kwa hivyo, toeni wala msijali, kwani Yeye Ndiye Mruzuku, Anambana Anayemtaka, miongoni mwa waja Wake, katika riziki na Anaikunjua, hiyo riziki, kwa wengine. Ana hekima kubwa katika hayo. Na Kwake Yeye Peke Yake mtarudi baada ya kufa, na hapo Atawalipa kwa vitendo vyenu.
Kwani hukukijua, ewe Mtume, kisa cha watukufu na mabwana, miongoni mwa Wana wa Isrāīl, baada ya zama za Musa kupita? Walipomtaka Mtume wao amtawalishe kwao mfalme, wapate kukusanyika chini ya uongozi wake na wapate kupigana na maadui zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Nabii wao akawaambia, «Je, mambo ni kama vile ninavyoyatarajia kwamba lau mtafaradhiwa kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa hamtapigana? Kwani mimi nachelea mtaogopa na mtakimbia vitani.» Wakasema wakikanusha matarajio ya Nabii wao, «Ni kizuizi kipi kitakacho kutuzuia tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambapo adui yetu ametutoa kwenye Makao yetu na akatutenganisha na na watoto wetu kwa kutuua na kututeka?» Basi Mwenyezi Mungu Alipowafaradhia kupigana wakiwa na mfalme Aliyewachagulia walikuwa waoga na wakakimbia vitani, isipokuwa wachache kati yao waliojikita imara kwa fadhila za Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Anawajua mno madhalimu, wenye kuzivunja ahadi zao.
Na Mtume wao aliwaambia, «Hakika Mwenyezi Mungu Amewaltea Tālūt kuwa ni mfalme, ikiwa ni kuyaitikia maombi yenu, ili awaongoze katika kupigana na adui yenu kama mlivyoomba.» Wakasema wakuu wa Wana wa Isrāīl, «Vipi Tālūt atakuwa mfalme kwetu, hali yeye hastahiki hilo? Yeye si katika wajukuu wa wafalme, wala hatoki kwenye nyumba ya utume na wala hakupewa ukunjufu wa mali ya kujisaidia nayo katika ufalme wake. Sisi tuna haki zaidi ya huu ufalme kuliko yeye. Kwani sisi ni wajukuu wa wafalme na tunatoka kwenye nyumba ya utume.» Mtume wao akawaambia, «Hakika Mwenyezi Mungu Amewachagulia, na Yeye, Aliyetakasika na kila sifa mbaya, Anayajua zaidi mambo ya waja Wake, na Amemuengezea ukunjufu wa elimu na nguvu ya mwili ya kupigana na adui. Na Mwenyezi Mungu ni Mmiliki wa ufalme. Anampa ufalme wake Anayemtaka katika waja wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa fadhila na utoaji, ni Mjuzi kabisa wa ukweli wa mambo, hapana chenye kufichika Kwake.»
Mtume wao aliwaambia, «Hakika alama ya ufalme wake ni kuwajilieni sanduku ambalo ndani yake muna Taurati,- Sanduku ambalo maadui wao walikuwa wamewanyang’anya-. Ndani yake muna utulivu kutoka kwa Mola wenu unaozithibitisha nyoyo za wenye ikhlasi. Na muna ndani yake mabaki ya vitu vilivyoachwa na jamaa za Musa na jamaa za Hārūn, kama fimbo na vipande vya mbao, yanabebwa na Malaika. Hakika muna katika hayo hoja kubwa kuwa Tālūt amechaguliwa kuwa mfalme wenu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, iwapo mnamuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.»
Alipotoka Twalut na askari wake kwenda kupigana na watu majabari, aliwaambia, «Mwenyezi Mungu Atawapa mtihani wa subira kwa mto uliyo mbele yenu mtakaouvuka, ili abainike mwenye Imani na aliye mnafiki. Yoyote kati yenu atakaye kunywa maji ya mto huo, si katika mimi, wala hafai kuwa na mimi kwenye jihadi. Na yule ambaye hatayaonja maji hayo, yeye ni katika mimi, kwa kutii amri yangu, na anafaa kwa jihadi. Isipokuwa aliyeruhusiwa na akateka mteko mmoja kwa mkono wake, huyo hana lawama. Basi walipofika mtoni, waliyaangukia maji na waliyanywa sana isipokuwa idadi ya watu wachache kati yao, walisubiri juu ya kiu na joto na wakatosheka na mteko wa mkono. Wakati huo wale walioasi amri, walirudi nyuma. Tālūt pamoja na wale Waumini wachache walipouvuka mto - walikuwa watu zaidi ya mia tatu na kumi- kwa ajili ya kupambana na maadui zao na wakaona wingi wa maadui zao na wingi wa silaha walionazo, walisema, «Hatuna uwezo leo wa kupigana na Jālūt na askari wake wenye nguvu. Hapo, wale wliokuwa na yakini ya kukutana na Mola Wao walijibu wakiwakumbusha ndugu zao juu ya Mwenyezi Mungu na uwezo Wake, «Nivikundi vingapi vichache, venye imani na subira, viliyashinda, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, makundi yaliyokuwa na watu wengi makafiri wenye kuasi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Yupo pamoja na wenye subira kwa taufiki Yake na nusra Yake na malipo Yake mema.
Na walipojitokeza kwa Jālūt na askari wake na wakaiona hatari kwa macho yao, walifazaika na kumuelekea kwa Mwenyezi Mungu kwa maombi na kunyenyekea huku wakisema, «EweMola wetu! Tumiminie subira nyingi kwenye nyoyo zetu, Uzithibitishe nyayo zetu ziwe thabiti muda wa kupigana na adui, zisiwe na uoga wa kukimbia vita, na Utunusuru kwa msaada wako juu ya watu makafiri.
Hapo waliwashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Dāwūd, Amani imshukiye, alimuua Jālūt, kiongozi wa majabari. Na Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, baada ya hapo, Akampa Dāwūd ufalme na utume katika Wana wa Isrāīl, na Alimfundisha Aliyoyataka miongoni mwa elimu. Na lau kama si himaya ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwatumia baadhi ya watu- nao ni wale watiifu Kwake na wanaomuamini- kuwazuia wengine- nao ni wanaomuasi Mwenyezi Mungu na kumshirikisha-, basi ardhi ingaliharibika kwa ushindi wa ukafiri na kupata nguvu uharibifu na wenye kufanya maasia. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kwa viumbe wote.
Hizo ni hoja za Mwenyezi Mungu na dalili Zake tunakusimulia wewe, ewe Nabii, kwa kweli, na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume walio wakweli.
Mitume hawa watukufu, Mwenyezi Mungu Amewatukuza baadhi yao juu ya wengine, kulingana na neema za Mwenyezi Mungu juu yao. Miongoni mwao kuna ambao Mwenyezi Mungu Amesema nao, kama Mūsā na Muhammad, rehema na amani ziwashukie. Katika hili pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, kwa namna inayonasibiana na utukufu Wake. Na miongoni mwao kuna ambao Mwenyezi Mungu Aliwainua daraja nyingi za juu, kama Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa kuenea ujumbe wake, kutia kikomo cha unabii kwake, kwa kuwatukuza ummah wake juu ya ummah wengine na yasiyokuwa hayo. Na Mwenyezi Mungu Alimpa 'Īsā mwana wa Maryam, amani imshukie, hoja zilizo wazi, ambazo ni miujiza yenye kushinda, kama kumponya aliyezaliwa kipofu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na kumponya mwenye barasi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kama kuhuisha kwake waliokufa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Alimpa nguvu kwa Jibrili, amani imshukie. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka wasipigane hao waliokuja baada ya hawa Mitume, baada ya kuwafunukia wao hoja zilizo wazi, hawangalipigana. Lakini ilitokea tafauti baina yao: katika wao kuna aliyejikita kwenye Imani yake, na katika wao kuna aliyeshikilia kukanusha. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka, baada ya hizo tafauti zilizotokea zilizopelekea kupigana, hawangalipigana, lakini Mwenyezi Mungu Anampa taufik ya kumtii Yeye na kumuamini Anayemtaka, na Anamuondolea taufiki Yake Anayemtaka akamuasi na kumkanusha, Kwani Yeye Anafanya na kuchagua Analolitaka.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na kumsadiki Mtume Wake na kufanya amali zinazoambatana na uongofu Wake! Toeni Zaka zilizofaradhiwa na mtoe sadaka ya vitu mlivyopewa na Mwenyezi Mungu kabla haijaja Siku ya Kiyama, wakati ambapo hakuna kuuziana ikapatikana faida, wala mali ambayo nyinyi mtajikomboa nayo nafsi zenu kutokana na adhabu ya Mwenyezi Mungu, wala urafiki wa rafiki wenye kuwaokoa, wala muombezi anayemiliki kuwafanya mpunguziwe adhabu. Na makafiri ndio madhalimu na wakeukaji mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu Ndiye Ambaye hakuna yoyote anayestahiki uungu na kuabudiwa isipokua Yeye. Ndiye Aliye hai Ambaye Amekusanya maana yote ya uhai mkamilifu unaolingana na utukufu Wake. Ndiye Msimamizi wa kila kitu. Kusinzia hakumshiki wala kulala. Kila kilichoko kwenye mbingu na kilichoko kwenye ardhi ni milki Yake. Na hatajasiri mtu yoyote kuombea mbele Yake isipokuwa kwa ruhusa Yake. Ujuzi Wake umevizunguka vitu vyote vilivyopita, vilivyoko na vitakavyo kuja. Anajua yaliyo mbele ya viumbe katika mambo ambayo yatakuja na yaliyo nyuma yao katika mambo yaliyopita. Na hakuna yoyote, katika viumbe, mwenye kuchungulia chochote katika elimu Yake isipokuwa kadiri ile ambayo Menyezi Mungu Amemjulisha na kumuonesha. Kursiy Yake imeenea kwenye mbingu na ardhi. Kursiy ni mahali pa nyayo za Mola, uliyo mkubwa utukufu Wake, na hakuna ajuwae namna ilivyo isipokuwa ni Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Wala hakumlemei Mwenyezi Mungu Aliyetakata kuzitunza. (hizo mbingu na ardhi).Yeye Ndiye Aliye juu ya viumbe Vyake vyote, kwa dhati Yake na sifa Zake, Aliyekusanya sifa za utukufu na kiburi. Aya hii ni aya tukufu zaidi katika Qur’ani, na inaitwa Āyah al- Kursīy.
Kwa kuwa Dini hii imekamilika na hoja zake ziko wazi, haihitajii ilazimishwe kwa watu ambao jizya (jizyah) inapokewa kutoka kwao. Kwani dalili ziko wazi ambazo kwa dalili hizo inabainika haki, ikawa kando na batili, na uongofu, ukawa kando na upotevu. Basi mwenye kukanusha vyote vinavyoabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu na akamuamini Mwenyezi Mungu, huwa amethibiti na kulingana kwenye njia bora na ameshikamana na kamba imara ya Dini isiyokatika. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi wa maneno ya waja Wake, ni Mjuzi wa nia zao na vitendo vyao na Atawalipa kwa hayo.
Mwenyezi Mungu Anawasimamia Waumini kwa kuwanusuru, kuwaafikia na kuwahifadhi, Anawatoa kutoka kwenye magiza ya ukafiri kuwapeleka kwenye nuru ya Imani. Na wale waliokufuru, wanusuru wao na wasaidizi wao ni wale wafananishwao na Mwenyezi Mungu na masanamu wanaowaabudu wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Hao wanawatoa wao kutoka kwenye nuru ya Imani kuwapeleka kwenye magiza ya ukafiri. Wao ndio watu wa Motoni wenye kutindikia humo, wenye kusalia humo milele na si wenye kutoka humo.
Je umewahi kuona, ewe Mtume, hali ya kustaajabisha zaidi kuliko ile ya yule aliyemjadili Ibrāhīm, amani imshukie, juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na juu ya uola Wake, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Alimpa ufalme, alipofanya ujeuri na kumuuliza Ibrāhīm, «Ni nani Mola wako?» Alisema, amani imshukie, «Mola wangu ni Ambaye Anavipa viumbe uhai vikahuika na Anaviondolea uhai vikafa. Yeye Ndiye Aliyepwekeka kwa kuhuisha na kufisha.» Akasema, «Mimi nahuisha na kufisha.» Yaani: namuua nimtakaye kumuua, na namuachilia nimtakaye kumuachilia. Ibrāhīm akasema kumwambia, «Mwenyezi Mungu ninayemuabudu Analitoa jua upande wa mashariki. Je unaweza wewe kugeuza mwenendo huu wa kimungu, ulifanye litokeze upande wa magharibi?» Akapigwa na mshangao huyu kafiri na ikakatika hoja yake. Hali yake ni ile ya madhalimu, Mwenyezi Mungu Hawaongozi kwenye haki na usawa.
Au je uliona, ewe Mtume, mfano wa yule aliyepita kwenye kijiji ambacho nyumba zake zilikuwa zimevunjika na kuangukia misingi yake na akasema, «Vipi Mwenyezi Mungu Atakihuisha kijiji hiki baada ya kuwa kimekufa?» Mwenyezi Mungu Akamfisha miaka mia moja kisha Akamrudishia roho yake na Akamwambia, «Ni kwa muda gani ulikuwa umekufa?» Akasema, «Nilikuwa nimekufa kwa muda wa siku moja au sehemu ya siku.» Akampa habari kuwa alikuwa amekufa kwa muda wa miaka mia. Na Akamuamrisha akiangalie chakula chake na kinywaji chake vipi Mwenyezi Mungu Amevihifadhi visiharibike muda huu mrefu. Na Akamuamrisha amtazame punda wake aone vipi Mwenyezi Mungu Alimuhuisha baada ya kuwa mifupa iliyotapakaa. Na Akamwambia, «Na ili tukufanye wewe ni dalili kwa watu.» Yaani: dalili iliyo wazi ya uweza wa Mwenyezi Mungu kufufua baada ya kufa. Na akamuamrisha aitazame mifupa aone vipi Mwenyezi Mungu Anavyoiinua baadhi yake juu ya mingine na kuiunganisha baadhi yake na mingine na kuivisha nyama baada ya kushikana na kisha kuirudishia uhai.Yalipomfunukia hayo waziwazi alikubali ukubwa wa Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na akawa ni dalili kwa watu.
Na Kumbuka, ewe Mtume, maombi ya Ibrahim kwa Mola wake Amuoneshe namna ya Ufufuzi. Mwenyezi Mungu Alimwambia, «Kwani huamini?» Akasema, «La! Nakuamini. Lakini nataka hilo ili nipate yakini zaidi juu ya yakini niliyonayo.» Akasema, «Chukua ndege wanne, uwe nao, uwachinje na uwakatekate kisha weka sehemu ya hao ndege juu ya kila jabali. Kisha waite, watakujia kwa haraka.» Ibrahim, amani imshukie, akawita. Papo hapo kila sehemu ikarudi mahali pake, na papo hapo wakamjia kwa haraka. Na ujue kuwa Mwenyezi Mungu ni Mshindi, hakuna kimshindacho, ni Mwenye hekima katika maneno Yake, vitendo Vyake, sheria Yake na makadirio Yake.
Na miongoni mwa vitu bora zaidi vinavyowanufaisha Waumini ni kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na mfano wa Waumini wenye kutoa mali yao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa mbegu iliyopandwa kwenye ardhi nzuri, muda si muda ikatoa mte wenye sehemu saba. Kila sehemu ikatoa suke moja na kila suke likawa na mbegu mia. Na Mwenyezi Mungu Anamuongezea thawabu anayemtaka, kulingana na kadiri ya Imani aliyonayo yule mtoaji na ikhlasi yake iliyo timamu.Na fadhila za Mwenyezi Mungu zimeenea, na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mjuzi wa yule anayestahiki kuzipata, ni Mwenye kuchungulia nia za waja Wake.
Wale ambao wanatoa mali yao katika jihadi na aina mbali-mbali za kheri, kisha wasifuatishe, yale waliyoyatoa ya kheri, kwa kumsumbulia waliyempa wala kumkera, kwa neno au kitendo, kwa kumhisisha kuwa wamemfadhili, watapata thawabu kubwa mbele ya Mola wao na hawatakuwa na kicho kuhusu mustakbala wao wa Akhera wala hawatahuzunika juu ya kitu chochote kilichowapita wasikipate katika ulimwengu.
Maneno mazuri kujibiwa muombaji na kusamehe utiriri wake katika kuomba, ni bora kuliko sadaka inayofuatiwa na kero na ubaya kutoka kwa mtoaji sadaka. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja ya sadaka za waja, ni Mpole Hana haraka nao ya kuwatesa.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, msiziondoe thawabu za vitu vile mlivyovitoa sadaka kwa usumbulizi na kero. Kwani huyu, mwenye kufanya haya, anafanana na mtu atowaye mali yake ili watu wamuone na wamsifu ilhali yeye hamuamini Mwenyezi Mungu wala hana yakini na Siku ya Akhera. Mfano wa huyo ni mfano wa jiwe laini lenye mchanga juu yake, lililonyeshewa na mvua nyingi, ikaondoa ule mchanga, ikaliacha tupu halina kitu juu yake. Basi hawa wenye kufanya ria ndivo walivyo, amali zao zinapotea mbele ya Mwenyezi Mungu na hawapati chochote cha thawabu kwa utoaji wao. Na Mwenyezi Mungu hawaafikii makafiri kuifikia haki katika vitu wanvyovitoa na mengineyo.
Na mfano wa wale ambao wanatoa mali yao kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu na kwa kuwa na itikadi iliyojikita ya kuwa ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli, ni kama mfano wa bustani kubwa iliyoko kwenye ardhi ya juu iliyo nzuri iliyonyeshewa na mvua nyingi, yakaongezeka kwa wingi matunda yake. Na hata kama haingalinyeshewa na mvua nyingi, rasharasha la mvua lingalitosha kuifanya itoe ongezeko lingi la matunda. Basi hivyo ndivyo ulivyo utoaji wa watu wenye ikhlasi; amali zao zinakubaliwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kuongezwa, ziwe ni chache au ni nyingi. Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuchungulia siri, Ndiye Mwenye kuyaona ya nje na ya ndani, Anampa thawabu kila mtu kulingana na ikhlasi yake.
Je anapendelea mmoja wenu awe na bustani yenye mitende na mizabibu, ambayo inapita chini ya miti yake maji tamu, na ndani yake ana kila aina ya matunda, na amefikia hali ya ukongwe ya kutoweza kupanda mimea kama hii, na ana watoto wadogo wanaohitaji bustani hii, na katika hali hii ukavuma upepo mkali uchomao, ukaja ukaiteketeza? Hivi ndivyo hali ya wasio na ikhlasi kataka utoaji wao; watakuja Siku ya Kiyama na hawana jema lolote lao. Kwa ufafanuzi huu, Mwenyezi Mungu Anawabainishia mambo yanayowafaa nyinyi, ili mtaamali na kumtakasia Mwenyezi Mungu utoaji wenu.
Enyi mlioniamini na mkawafuata Mitume wangu, toeni miongoni mwa halali mliyoichuma na ile tuliyowatolea kutoka kwenye ardhi. Na wala msikusudie kutoa kibaya, katika hiyo halali, kuwapa mafukara, ambacho lau nyinyi mngalipewa, hamngalikipokea isipokuwa mkiwa mtapuuza ubaya na upungufu ulionacho. Ni vipi nyinyi mnaridhika kumpa Mwenyezi Mungu kitu ambacho hamridhiki nacho mkipewa? Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu Aliyewaruzuku Anajitosha kutohitajia sadaka zenu, ni Mstahiki wa kusifiwa na Mhimidiwa kwa kila hali.
Uchoyo huu na kuchagua kibaya kukitoa sadaka yatokana na Shetani ambaye anawaogopesha nyinyi ufukara na kuwahimiza uchoyo, na anawaamrisha nyiyi maasia na kumfanyia kinyume Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kutukuka, Anawaahidi nyinyi, kwa kutoa kwenu, msamaha wa madhambi yenu na riziki kundufu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nyongeza zenye kuenea, ni Mjuzi wa nia na vitendo.
Mwenyezi Mungu Anampa taufiki ya usawa katika kunena na kutenda Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Amemneemesha kwa hilo, Hua Amempa kheri nyingi. Na hatakumbuka hilo na kunufaika nalo isipokuwa wenye akili zenye kung’ara kwa nuru ya Mwenyezi Mungu na uongofu Wake.
Mali yoyote mnayoyatoa na mengineyo, machache au mengi, au sadaka mnayoitoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, au mkajilazimisha nafsi zenu chochote, cha mali au kinginecho, basi Mwenyezi Mungu Anayajua hayo; na Yeye Ndiye Mwenye kuchungulia nia zenu, na Atawalipa kwa hayo. Na yoyote mwenye kuzuia haki ya Mwenyezi Mungu ni dhalimu. Na madhalimu hawana wenye kuwanusuru ambao watawazuia wasipate adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Mkizidhihirisha zile mnazozitoa sadaka kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ni sadaka nzuri mliyoitoa. Na mkizitoa kwa siri mkawapa mafukara, ni bora zaidi kwenu kwa kuwa hivyo ni mbali na ria. Na katika utoaji sadaka pamoja na ikhlasi kuna kusamehewa madhambi yenu. Na Mwenyezi Mungu Anayajua mambo ya ndani; hakuna kinachofichika Kwake katika mambo yenu na Atamlipa kila mtu kwa amali yake.
Si jukumu lako, ewe Mtume, kuwapa makafiri taufiki ya uongofu, lakini Mwenyezi Mungu Anavifungua vifua vya Anaowataka kwa Dini Yake na kuwaafikia kuifuata. Na mali yoyote mnayoyatoa, nafuu yake itawarudia nyinyi wenyewe kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Waumini hawatoi isipokuwa kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mali yoyote mnayoyatoa, kwa kumtakasia Mwenyezi Mungu, mtapewa kikamilifu thawabu zake na hamtapunguziwa chochote katika hizo. Katika hii aya pana kuthibitisha sifa ya Uso kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakata na kila sifa pungufu (wajh Allah) kwa namna inayonasibiana na Yeye.
Wapeni sadaka zenu mafukara Waislamu ambao hawawezi kusafiri kutafuta riziki, kwa kuwa wameshughulika na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, ambao huwadhania wao wasiowajua kuwa hawahitaji sadaka kwa kuwa wamejizuia na kuomba.Utawajua kwa alama zao na athari ya uhitaji walionao. Hawaombi kabisa. Na wakiomba, kwa kukosa budi, hawaombi kwa utiriri. Na mali yoyote mnayoyatoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, hakuna chochote, katika hayo, chenye kufichika kwa Mwenyezi Mungu.Na Mwenyezi Mungu Atalipa kwayo malipo mengi zaidi na makamilifu zaidi Siku ya Kiyama.
Wale ambao wanatoa mali zao kwa kumridhisha Mwenyezi Mungu, mchana na usiku, kwa siri na kwa dhahiri, watapata malipo yao mbele ya Mola wao, na wala hapana khofu juu yao kuhusu mambo watakayoyakabili Akhera wala hawatakuwa na huzuni juu ya vitu vya kidunia vilivyowapita wasivipate. Sheria hiyo ya Ki- Mungu yenye hekima, ndiyo njia ya Uislamu katika utoaji, yenye kuondoa mahitaji ya mafukara kwa heshima na utu, kusafisha mali ya matajiri na kuhakikisha kusaidiana juu ya wema na ucha-Mungu ili kutaka radhi za Mwenyezi Mungu bila maonevu au kulazimisha.
Wale wenye kuamiliana kwa riba- nayo ni nyongeza juu ya rasilmali-, hawainuki kutoka kwenye makaburi yao Siku ya Mwisho isipokuwa ni kama anavyoinuka yule anayepigwa na Shetani akapatwa na wazimu. Hivo ni kwa kuwa wao walisema kwamba biashara ni kama riba, kwa kuwa yote mawili ni halali na yanapelekea mali kuongezeka. Mwenyezi Mungu Akawakanusha na Akabainisha kwamba Yeye Amehalalisha biashara na Ameharamisha riba. Kwa kuwa katika kuuza na kununua kuna nafuu kwa watu binafsi na kwa jamii na katika riba kuna unyonyaji, hasara na maangamivu. Basi mwenye kumfikia yeye makatazo ya Mwenyezi Mungu ya riba akakomeka, achukue iliyopita kabla ya kumfikia yeye uharamu wake, na hana makosa kwa hilo. Na mambo yake ya siku zake za baadae yako kwa Mwenyezi Mungu. Akiwa ataendelea na toba yake, basi Mwenyezi Mungu Hapotezi malipo ya wenye kufanya wema; na akiwa atarudia kwenye riba, basi kitendo chake hiko baada ya kufikiwa na makatazo ya Mwenyezi Mungu, kitamfanya astahili mateso, kwa kuwa hoja imesimama juu yake. Kwa ajili ya hii Alisema Mwenyezi Mungu, «Basi hao ni watu wa Motoni; Wao ndani yake watakaa milele».
Mwenyezi Mungu Anaiyondoa riba yote au Anamnyima mlaji riba baraka ya mali yake asinufaike nayo. Na Anazikuza sadaka na kuzifanya ziwe nyingi na Anawaongezea malipo wenye kutoa sadaka maradufu na Anawabarikia katika mali yao. Na Mwenyezi Mungu Hampendi kila mwenye kushikilia kwenye ukafiri wake, mwenye kujihalalishia ulaji riba, mwenye kukolea nadani ya dhambi na haramu na kumuasi Mwenyezi Mungu.
Hakika wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda matendo mema, wakatekeleza Swala kama Alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatoa Zaka za mali yao, wana thawabu kubwa zinazowahusu wao mbele ya Mola wao na Mruzuku wao. Na hawatapatwa na woga katika Akhera yao, wala masikitiko juu ya mambo mazuri ya kilimwengu waliyoyakosa.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mkamfuata Mtume Wake, muogopeni Mwenyezi Mungu na muache kutaka ziada iliyosalia juu ya rasilmali zenu, ambayo mlistahiki kupata kabla riba haijaharamishwa, iwapo imani yenu ni ya kidhati kimaneno na kivitendo.
Msipokomeka na hilo mlilokatazwa na Mwenyezi Mungu, basi kuweni na yakini ya vita kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na mkirudi kwa Mola wenu na mkaacha kula riba, ni haki yenu mchukue madeni yenu bila ya nyongeza, hamumdhulumu yoyote kwa kuchukua zaidi ya rasilmali zenu wala hamudhulumiwi na yoyote kwa kupunguza kiwango cha pesa mlichokopesha.
Na iwapo mdaiwa hawezi kulipa, mpeni muhula mpaka Mwenyezi Mungu Atakapomfanyia sahali riziki na kuwarudishia mali yenu. Na mkiacha rasilmali yote au baadhi yake mkamuondolea mdaiwa, hilo ni bora zaidi kwenu, mkiwa mnajua fadhila yake ya kuwa hilo ni bora kwenu katika ulimwengu na Akhea.
Na itahadharini, enyi watu, Siku matakaporejeshwa kwa Mwenyezi Mungu, nayo ni Siku ya Kiyama, mtakapo kuorodheshwa kwa Mwenyezi Mungu ili Awahesabu na Amlipe kila mmoja miongoni mwenu kwa alilolitenda la kheri au la shari bila ya kufikiwa na maonevu. Katika aya hii pana ishara kwamba kujiepusha na mapato ya riba yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu, ni kukamilisha Imani na haki za Imani za kutekeleza Swala, kutoa Zaka na kufanya amali njema.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na mkamfuata Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, mkiamiliana kwa mkopo mpaka muda maalumu, usajilini kwa maandishi ili kuhifadhi mali na kuondoa ugomvi. Na asimame kuandika mtu muaminifu mwenye kudhibiti. Na asilikatae hilo yule mtu aliyetunukiwa na Mwenyezi Mungu ujuzi wa uandishi. Na asimame mdaiwa kufanya imla ya deni iliyo juu yake. Na amchunge Mola wake na asipunguze chochote katika deni iliyo juu yake. Iwapo mdaiwa amezuiwa matumizi kwa ubadhirifu wake na utumiaji wake unaopita kiasi, au akawa ni mdogo au ni mwendawazimu, au hawezi kusema kwa ububu au kwa ulemavu wa kutoweza kusema kabisa, basi na asimamie shughuli ya kufanya imla msimamizi wa mdaiwa kwa niaba yake. Na takeni ushahidi wa Waislamu wawili wanaume, waliobaleghe, wenye akili na waadilifu. Iwapo hawatopatikana wanaume wawili, takeni ushahidi wa mwanamume mmoja na wanawake wawili mnaoridhika na ushahidi wao, ili akisahau mmoja wao (hao wanawake wawili) yule mwengine amkumbushe. Na ni juu ya mashahidi kukubali mwito wa mwenye kuwaita kutoa ushahidi. Na ni juu yao kutoa ushahidi wao wakitakiwa kufanya hivyo. Na msichoke kuisajili deni, iwe ni kubwa au ni ndogo, mpaka wakati wake maalumu wa kulipa. Kwani hilo ni la usawa zaidi katika Sheria ya Mwenyezi Mungu na uongofu Wake, na linasaidia sana kabisa katika kusimamisha ushahidi na kuutekeleza, na liko karibu zaidi na kuondoa shaka kuhusu deni yenyewe, kiasi chake na muda wake. Lakini, iwapo ni jambo la kuuza na kununua, kwa kuchukua bidhaa na kutoa thamani yake papo hapo, basi hakuna haja ya kusajili, na inapendekezwa kushuhudisha hilo ili kuepusha ugomvi na utesi. Na katika mambo ya lazima kwa shahidi na mwandishi ni kutekeleza ushahidi kwa njia zake na usajili kama Alvyoamrisha Mwenyezi Mungu. Na hafai kwa mwenye haki na kwa yule ambaye haki iko juu ya shingo yake kuwadhuru waandishi na mashahidi. Pia, haifai kwa waandishi na mashahidi kuwadhuru wanaohitajia uandishi wao na ushahidi wao. Na mkifanya mliyokatazwa, huko ni kutoka nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu; na mwisho mbaya wa kitendo hiko utawafikia. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika maamrisho Yake yote aliyowaamrisha nayo na akawakataza nayo. Na Mwenyezi Mungu Anawajulisha yote yanayotengeneza ulimwengu wenu na Akhera yenu. Na Mwenyezi Mungu kwa kila jambo ni Mjuzi. Hakuna kitu chochote kinachofichika Kwake kuhusu mambo yenu, na Atawalipa kwa hayo.
Na mkiwa muko safarini, na msipate mwenye kuwaandikia, mpatieni yule mwenye haki kitu kiwe ni dhamana ya haki yake hadi mdaiwa atakapolipa deni yake. Na iwapo nyinyi kwa nyinyi mumeaminiana, hapana makosa kuacha kuandika, kushuhudisha na kuweka rahani, na deni itabaki ni amana kwenye shingo ya mdaiwa, ni juu yake kuilipa. Na ni juu yake amchunge Mwenyezi Mungu asimfanyiye hiana mwenzake. Na akikataa mdaiwa deni iliyo juu yake, na ikawa pana mtu aliyekuweko na kushuhudia, huyo itamlazimu kuutoa wazi ushahidi wake. Na mwenye kuuficha ushahudi huu, ni mtu mwenye moyo wa hiana na urongo. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuchungulia siri zote, Ndiye Ambaye ujuzi Wake umezunguka mambo yenu yote, na Atawahesabu kwa hayo.
Ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake, kwa kuvimiliki, kuvipekesha na kuvijua. Hakuna chochote kinachofichika Kwake. Na chochote mnachokidhihirisha, kati ya viliomo ndani ya nafsi zenu au mnachokificha, Mwenyezi Mungu Anakijua, na Atawahesabu nacho. Atamsamehe Anayemtaka na Atampatiliza Anayemtaka. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu. Baadaye Mwenyezi Mungu aliwakirimu Waislamu Akasamehe maneno ya mtu kuiyambia nafsi yake na mawazo ya moyo, yakiwa hayatafuatiwa na maneno au vitendo, kama ilivyothibiti kutoka kwa Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Ameamini na kuyakinisha Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yale aliyoletewa kwa njia ya wahyi kutoka kwa Mola wake. Na ni haki kwake aiyakinishe. Na Waumini pia wameamini na kufanya amali zinazoambatana na Qur’ani Tukufu. Kila mmoja katika wao amemuamini Mwenyezi Mungu kuwa ni Mola na Muabudiwa, Aliyesifika kwa sifa za utukufu na ukamilifu, na kuwa Mwenyezi Mungu Anao Malaika watukufu, na kuwa Yeye Ameteremsha Vitabu na Ametuma Mitume kwa waja Wake. Hatuwaamini, sisi Waumini, baadhi yao na kuwakanusha baadhi yao. Bali tunawaamini wao wote. Na wanasema, Mtume na Waumini, «Tumeusikia, ewe Mola wetu, wahyi uliouleta na tumetii katika yote hayo. Tunatarajia uyasamehe, kwa wema Wako, madhambi yetu. Wewe Ndiye Ambaye Uliyetulea kwa neema Zako Ulizotuneemesha nazo. Kwako, Peke Yako, ndio marejeo yetu na mwisho wetu.»
Dini ya Mwenyezi Mungu ni sahali, haina uzito ndani yake. Mwenyezi Mungu hawatakii waja Wake wasiyoyaweza. Mwenye kufanya uzuri atapata uzuri, na mwenye kufanya ubaya atapata ubaya. Ewe Mola wetu! Usitutese tukisahau chochote miongoni mwa vitu ulivyotufaradhia au tukikosea kwa kufanya kitu chochote ulichotukataza kukifanya. Ewe Mola wetu! Na usitukalifishe kufanya matendo magumu uliyowakalifisha waliokuwa kabla yetu, miongoni mwa waasi, yakiwa ni mateso kwao. Ewe Mola wetu! Na usitubebeshe tusiyoyaweza ya amri ngumu na mikasa. Na uyafute madhambi yetu, uzisitiri aibu zetu na utufanyiwe wema. Wewe Ndiye Mwenye kuyamiliki mambo yetu na kuyaendesha. Tunusuru juu ya wale waliokataa Dini yako na kuukataa umoja wako na wakamkanusha Nabii wako Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Na ujaalie mwisho mwema uwe ni wetu juu yao, ulimenguni na Akhera.
Icon