ﯖ
surah.translation
.
ﰡ
ﭑ
ﰀ
«Hā, Mīm» Yameshatangulia maelezo kuhusu herufi zilizokatwa na kutengwa mwanzo wa sura ya Al-Baqarah.
Hii Qur’ani ni Teremsho linalotoka kwa Mwenyezi Mungu Mwenye kueneza rehema Zake kwa wema na waovu ulimwenguni, Mwenye kuhusisha rehema Zake kwa wema watupu kesho Akhera. Amemteremshia Nabii Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Ni Kitabu kilichobainishwa aya zake ubainifu uliotimia, na yakafafanuliwa maana yake na hukumu zake, ikiwa ni Qur’ani ya Kiarabu iliyofanywa nyepesi kuielewa kwa watu wanaoijua lugha ya Kiarabu.
Hali ya kuwa ni yenye kubashiri malipo ya haraka na ya baadaye kwa anayeiamini na akafanya matendo yanayolingana nayo, na ni yenye kuonya adhabu ya haraka na ya badaye kwa anayeikanusha. Hivyo basi wengi wa watu waliipa mgongo wakawa hawaisikii kusikia kwa kukubali na kuitikia.
Na wanasema hawa wenye kukataa na kumkanusha Nabii Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, «Nyoyo zetu zina vifiniko venye kutuzuilia tusielewe unayotuambia, na masikizi yetu yana uziwi hatusikii, na baina yetu sisi na wewe, ewe Muhammad, pana pazia inayotuzuia kuitika mwito wako. Basi fanya kulingana na dini yako , kama ambavyo sisi tunavyofanya kulingana na dini yetu.»
Waambie, ewe Mtume, «Hakika yangu mimi ni binadamu kama nyinyi, Mwenyezi Mungu Ananiletea wahyi kwamba Mola wenu Anayestahiki kuabudiwa ni Mola Mmoja Asiyekuwa na mshirika. Basi fuateni njia yenye kufikisha Kwake na mtake msamaha Wake.» Maangamivu na mateso yatawapata washirikina walioabudu masanamu, yasiyonufaisha wala kudhuru, badala ya kumuabudu Mwenyezi Mungu.
Wale wasiojisafisha nafsi zao kwa kumpwekesha Mola wao na kumtakasa, na wasiotoa Zaka kuwapa wanaostahiki, basi hao hawamtakasii Muumba wala hawanufaishi viumbe; na wao hawaamini Ufufuzi wala Pepo na Moto.
Hakika ya wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na Kitabu Chake na wakafanya matendo mema, hali ya kumtakasia Mwenyezi Mungu katika matendo hayo, watapata malipo makubwa yasiyokatika wala kuzuiliwa.
Sema, ewe Mtume, uwaambie washirikina kwa kuwakaripia na kulionea ajabu tendo lao, «Je nyinyi mnamkanusha Mwenyezi Mungu Aliyeumba ardhi kwa siku mbili, mnanmfanya kuwa Ana washirika na wanaofanana Naye mkawa mnawaabudu pamoja Naye? Muumbaji Huyo Ndiye Mola wa viumbe wote.
«Na Akajaalia Mwenye kutakasika katika ardhi majabali yaliyojikita juu yake, Akaibarikia kwa kuifanya iwe na kheri nyingi kwa watu wake, Akakadiria humo riziki za chakula kwa watu wake na yale yanayowafaa maishani kwa kipindi cha Siku nne: Siku mbili Aliumba ndani yake ardhi na Siku mbili Aliweka katika ardhi majabali yaliyojikita na Akakadiria katika Siku mbili hizo riziki zake zikiwa sawa kwa wenye kuuliza, yaani kwa mwenye kutaka kuliuliza hilo apate kulijua.
Kisha Akalingana, kutakasika na kutukuka ni Kwake, yaani Akaikusudia mbingu, na ilikuwa moshi hapo kabla, Akasema kuiambia mbingu na ardhi, «Fuateni amri yangu kwa hiari au kwa nguvu!» Nazo zikasema, «Tumekuja tukiwa watiifu kwako. Hatuna matakwa kinyume cha matakwa yako.»
Mwenyezi Mungu Akapitisha kuziumba mbingu saba na kuzisawazisha kwa Siku mbili. Na kwa hilo ukatimia uumbaji wa mbingu na ardhi kwa Siku sita kwa hekima Anayoijua Mwenyezi Mungu, pamoja na uweza Wake, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, wa kuziumba kwa mara moja. Na Akapeleka wahyi katika kila uwingu kwa Analolitaka na kuliamuru. Na tumeupamba uwingu wa karibu kwa nyota zinazong’ara na kwa ajili ya kuuhifadhi na Mashetani wanaosikiliza kwa kuiba. Uumbaji huo mzuri ni makadirio ya Aliye Mshindi katika ufalme Wake, Aliye Mjuzi Ambaye ujuzi Wake umekizunguka kila kitu
Basi wakipuuza wakanushaji hawa baada ya kubainishiwa sifa za Qur’ani zinazotajika vyema, na sifa za Mungu Mkubwa, waambie, «Kwa kweli, ninawaonya nyinyi adhabu yenye kuwamaliza mfano wa adhabu (iliyowashukia watu wa kabila la) 'Ād na Thmud walipomkanusha Mola wao na kuwaasi Mitume wao.»
Walipowajia Mitume hao kina 'Ād na Thamūd, hawa baada ya wengine wakifuatana, wakiwaamrisha kumuabudu Mwenyezi Mungu Peke Yake Asiyekuwa na mshirika, waliwaambia Mitume wao, «Lau Mwenyezi Mungu Angalitaka tumpwekeshe na tusiabudu chochote kisichokuwa Yeye, Angaliteremsha Malaika kutoka mbinguni wakiwa wajumbe wa hilo unalotuitia kwalo, na Hangaliwatuma nyinyi na hali nyinyui ni binadamu kama sisi, basi sisi kwa lile ambalo Mwenyezi Mungu Amewatuma kwetu la kumuamini Mwenyezi Mungu Peke Yake ni wenye kulikanusha.»
Ama hao 'Ād, watu wa Hūd, waliwafanyia waja ujeuri bila haki na wakasema kwa kujiona, «Ni nani mwenye nguvu kali zaidi kushinda sisi?» Kwani hawaoni kuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Aliyewaumba ni Mkali zaidi wa nguvu na kipigo? Na walikuwa ni wenye kuzikanusha hoja zeyu na dalili zetu.
Tukawatumia wao upepo wenye ubaridi mkali, wenye sauti kubwa, katika siku zilizokuwa korofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya unyonge na utwevu katika maisha ya kilimwengu. Na adhabu ya Akhera ina unyonge na utwevu mwingi zaidi, na wao hawatasaidiwa kwa kuzuia adhabu isiwapate.
Na ama hao Thamūd, watu wa Ṣāliḥ, kwa hakika tuliwabainishia njia ya uongofu na usawa, wakafadhilisha upofu juu ya uongofu, kikawaangamiza wao kimondo cha adhabu yenye kutweza kwa sababu ya dhambi waliokuwa wakizitenda kwa kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake.
Na tukawaokoa wale walioamini kutokana na adhabu iliyowapata kina 'Ād na Thamūd. Na hawa waliookoka walikuwa wanamuogopa Mwenyezi Mungu na kumcha.
Na Siku ambayo maadui wa Mwenyezi Mungu watakusanywa wapelekwe kwenye Moto wa Jahanamu, Malaika wa adhabu watawarudisha wa mwanzo wao wawakusanye na wa mwisho wao.
hata watakapoufikia Moto na wakakanusha makosa yao, yatatoa ushahidi dhidi yao masikio yao, macho yao na ngozi zao kwa yale ambayo walikuwa wakiyafanya duniani ya madhambi na makosa.
Na watasema hao watakaokusanywa kupelekwa Motoni miongoni mwa maadui wa Mwenyezi Mungu kuziambia ngozi zao wakizilaumu, «Kwa nini mmetoa ushahidi dhidi yetu?» Na hapo ngozi zao ziwajibu, «Ametutamsha Mwenyezi Mungu Ambaye Amekitamsha kila kitu, na Yeye Ndiye Aliyewaumba nyinyi mara ya kwanza na hamkuwa ni chochote, na kwake Yeye Ndio mwisho wenu baada ya kufa ili mhesabiwe na mlipwe.»
Na hamkuwa mkijificha mlipokuwa mkitenda maasia kwa kuogopa yasije masikio yenu wala macho yenu wala ngozi zenu yakatoa ushahidi dhidi yenu Siku ya Kiyama, lakini mlidhani , kwa kufanya maasia kwenu, kuwa Mwenyezi Mungu hajui mengi kuhusu matendo yenu ambayo kwayo mnamuasi Mwenyezi Mungu.
Hiyo ndiyo dhana yenu mbovu ambayo mliidhania kwa Mola wenu; imewaangamiza na kuwatia Motoni, ndipo mkawa Leo ni miongoni mwa wale waliopata hasara nafsi zao na ya watu wao.
Wakivumilia adhabu, basi Moto ndio makazi yao, na wakiomba kurejea duniani waanze kufanya amali njema huko, hawatajibiwa ombi hilo wala hazitakubaliwa nyudhuru zao.
Na tuliwawekea hawa madhalimu wenye kukanusha marafiki wabaya miongoni mwa Mashetani wa kibinadamu na wa kijini, wakawapambia matendo yao machafu duniani, wakawaita kwenye ladha zake na matamanio yake ya haramu, na wakawapambia wao yaliyo nyuma yao katika mambo ya Akhera wakawasahaulisha wasiikumbuke, na wakawalingania wakatae Marejeo (ya Kiyama). Na kwa hjvyo walistahili kuingia Motoni wawe miongoni mwa wale makafiri wa ummah waliopita wa kijini na wa kibinadamu. Wao walikuwa wamepata hasara ya matendo yao duniani na hasara ya nafsi zao na watu wao Siku ya Kiyama.
Na makafiri walisema wakiambiana wao kwa wao wakiusiana baina yao, «Msiisikilize hii Qur’ani wala msiiandame wala msizifuate amri zake. Na ziinueni juu sauti zenu kwa kelele, kupiga mbinja na kumfanya Muhammad achanganyikiwe anaposoma Qur’ani, huenda mkamshinda akaacha kusoma na kwa hivyo tukapata ushindi juu yake.»
Basi Tutawaonjesha, tena tutawaonjesha, wale waliosema neno hili adhabu kali, duniani na Akhera, na tutawalipa, tena tutawalipa, mabaya zaidi ya makosa waliokuwa wakiyafanya.
Malipo haya ambayo watalipwa waliokufuru ni malipo ya maadui wa Mwenyezi Mungu, nayo ni Moto utakaokuwa ni nyumba yao ya kukaa daima milele, ukiwa ni malipo ya wale waliokuwa wakizikanusha hoja zetu na dalili zetu. Na aya hii inatolea ushahidi ukubwa wa kosa la mwenye kuwapotosha watu na Qur’ani tukufu na kuwazuia wasiizingatie wala wasijiongoze nayo kwa njia yoyote iwayo.
Na watasema wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wao wako Motoni, «Mola wetu! Tuonyeshe mapote mawili yaliyotupoteza miongoni mwa majini na binadamu ili tuyaweke chini ya nyayo zetu yapate kuwa sehemu ya chini kabisa ya Moto.»
Hakika ya wale waliosema, «Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake kisha wakasimama imara kufuata Sheria Yake, Malaika watawateremkia wakati wa kufa waseme kuwaambia, «Msiogopeni kufa na yatakayokuwa baada yake, wala msiwe na masikitiko juu ya yale mtakayoyaacha nyuma yenu katika mambo ya kilimwengu, na furahikeni kwa Pepo ambyo mlikuwa mkiahidiwa.»
Na Malaika watasema kuwaambia wao, «Sisi ndio wasaidizi wenu katika uhai wa ulimwenguni, tunawaelekeza sawa na tunawatunza kwa amri ya Mwenyezi Mungu, na pia tutakuwa na nyinyi huko Akhera. Na mtapata huko Peponi kila kile ambacho nafsi zenu zinakitamani katika vitu mnavyovichagua na ambavyo macho yenu yanatulia kwa kuvipata. Na chochote kile mtakachokitaka kitakuwa mbele yenu,
mkiandaliwa na kuneemeshwa kutoka kwa Mwingi wa kusamehe dhambi zenu, Mwingi wa huruma kwenu.»
Hakuna yoyote aliye na kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kupwekeshwa Mwenyezi Mungu na kuuabudiwa Yeye Peke Yake, na anayesema, «Mimi ni katika Waislamu wanaofuata amri Ya Mwenyezi Mungu na Sheria Yake.» Katika aya hii kuna kusisitiza kulingania kwa Mwenyezi Mungu Aliyetakasika na kueleza utukufu wa wanavyuoni wenye kulingania Kwake kwa ujuzi, kulingana na yale yaliyokuja kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema na amani zimshukie.
Na halilingani jema la waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakasimama imara kwenye Sheria Yake, wakawafanyia wema viumbe Vyake (hilo halilingani) na baya la waliomkanusha Yeye, wakaenda kinyume na amri Yake na wakawafanyia ubaya viumbe Vyake. Msukume, ewe Mtume, kwa msamaha wako, upole wako na hisani yako yule anayekufanyia ubaya, na upambane na ubaya wake kwako kwa kumfanyia wema. Hivyo basi yule aliyekutendea ubaya ambaye baina yako wewe na yeye kuna uadui atakuwa kama kwamba yeye ni mtu aliye jamaa yako wa karibu na mwenye huruma na wewe.
Na hawaafikiwi kwenye mambo haya yanayosifika vyema isipokuwa wale wanaojisubirisha juu ya mambo ambayo nafsi zao zinayachukia na wakajilazimisha kwa yale Anayoyapenda Mwenyezi Mungu. Na haafikiwi hayo isipokuwa mwenye fungu kubwa la hali njema ya duniani na Akhera.
Na Shetani anapotia ndani ya nafsi yako ushawishi wa mawazo ya kukufanya umlipe mbaya kwa ubaya, basi omba himaya ya Mwenyezi Mungu na ushikamane na Yeye. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia sana maombi yako ya kujilinda Kwake, ni Mwenye kuyajua sana mambo ya viumbe Vyake vyote.
Na miongoni mwa hoja za Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake, dalili za upweke Wake na ukamilifu wa uweza Wake, ni kutafautiana mchana na usiku na kufuatana (kila mojawapo kuufuata mwingine) na kutafautiana jua na mwezi na kufuatana, vyote hivyo viko chini ya uendeshaji Wake na utendeshaji nguvu Wake. Msilisujudie jua wala mwezi, kwani hivyo viwili vinaendeshwa na vimeumbwa; na msujudieni Mwenyezi Mungu Aliyeviumba, iwapo nyinyi kwa kweli mnafuata amri Yake, mnasikia na mnamtii Yeye, basi muabuduni Yeye Peke Yake Asiye na mshirika.
Na wakifanya kiburi wshirikina hawa kwa kukataa kumsujudia Mwenyezi Mungu, basi Malaika waliyoko kwa Mola wako hawafanyi kiburi cha kukataa hilo, bali wanamsujudia Yeye na wanamtakasa na kila upungufu, usiku na mchana, na wao hawapumziki na hilo wala hawachoki.
Na miongoni mwa alama za upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake ni kuwa wewe unaiona ardhi ikiwa kavu haina mimea, na tunapoiteremshia mvua, uhai unatambaa ndani yake na inasukikasukika kwa mimea, na ikafura na kunyanyuka. Hakika Yule Anayeihuisha ardhi hii baada ya ukavu wake ni Muweza wa kuwahuisha viumbe baada ya kufa kwao. Hakika Yeye juu ya kila jambo ni Muweza. Na kama usivyoelemewa uweza Wake kuhuisha ardhi baada ya kufa kwake, hivyo hivyo uweza Wake hauelemewi kuwahuisha waliokufa.
Hakika ya wale wanaopotoka na haki wakaikanusha Qur’ani na wakaipotoa, hawafichamani kwetu sisi, bali sisi tunawaona wao. Je, huyu mwenye kuzipotosha aya za Mwenyezi Mungu atakayetiwa Motoni ni bora au ni yule atakayekuja Siku ya Kiyama hali ya kuwa amesalimika na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kustahiki malipo mema Yake kwa kumuamini na kuzisadiki aya Zake? Fanyeni, enyi wapotofu, mnalolitaka, kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anayaona matendo yenu, hakuna kinachofichika Kwake, na Atawalipa kwa hayo. Hapa pana onyo na hadharisho kwao.
Hakika ya wale walioikataa hii Qur’ani na wakaikanusha ilipowajia ni wenye kuangamia na kuadhibiwa. Na hii Qur’ani ni Kitabu kitukufu kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekitukuza na kukitunza na kila ugeuzaji au ubadilishaji.
Ubatilifu haukifikii kutoka upande wowote katika pande Zake, na hakuna kitu chenye kukibatilisha, kwani hiko kimetunzwa kisipunguzwe wala kisizidishwe. Ni teremsho kutoka kwa Mwingi wa hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake, Mwenye kushukuriwa kwa sifa za ukamilifu Alizonazo.
Hawakwambii hao washirikina, ewe Mtume, isipokuwa kile ambacho washakisema kabla yao ummah waliopita kuwaambia Mitume wao. Basi vumilia juu ya kinachokupata katika njia ya ulinganizi kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ni Mwenye msamaha mwingi wa dhambi za wenye kutubia, ni mwenye mateso kwa mwenye kuendelea kumkufuru na kumkanusha.
Na lau tungaliifanya hii Qur’ani tuliyokuteremshia, ewe Mtume, ni kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu, washirikina wangalisema, «Je, si zifafanuliwe aya zake tupate kuzifahamu na kuzijua? Ni vipi hii Qur’ani ni kwa lugha isiyokuwa ya Kiarabu na hali lugha ya huyu aliyeteremshiwa ni ya Kiarabu? Hili haliwi!» Waambie, ewe Mtume, «Hii Qur’ani, kwa wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, ni uongofu kutoka kwenye upotevu na ni ponyesho la yaliyomo vifuani ya shaka na magonjwa. Na wale wasioiamini Qur’ani kuna uziwi ndani ya mashikio yao unaowafanya wasiisikie na wasiizingatie; nayo (hiyo Qur’ani) ni upofu kwao wa nyoyo zao, hawaongoki kwayo.» Basi washirikina hao ni kama yule anayeitwa naye yuko mahali mbali, hamsikii mwenye kulingania wala hamuitiki mwenye kuita.
Hakika tulimpelekea Mūsā Taurati kama tulivyokuletea wewe, ewe Mtume, Qur’ani, wakatafautiana watu wake kuhusu hiyo: katika wao kuna aliyeamini na katika wao kuna aliyekanusha. Na lau si neno (la ahadi) lililotangulia kutoka kwa Mola wako la kuwacheleweshea watu wako adhabu, uamuzi baina yao ungalitolewa wa kuwaangamiza makafiri papo hapo. Na kwa hakika washirikina wana shaka nayo sana Qur’ani.
Mwenye kufanya mema, akamtii mwenyezi Mungu na Mtume Wake, atajipatia mwenyewe thawabu za matendo yake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, atajionea mwenyewe dhambi za matendo yake. Na Mola wako si Mwenye kuwadhulumu waja kwa kuwapunguzia japo thawabu ya jema moja au kuwaongezea japo dhambi la ovu moja.
Kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika, Ndiko kunakorudishwa ujuzi wa kipindi cha kusimama Kiyama, kwani hakuna yoyote anayejua kipindi hiko isipokuwa Yeye. Na hayatoki matunda kwenye vifuko vyake (mitini), na hakuna kiumbe chochote cha kike kinachoshika mimba wala kinachojifungua mimba yake isipokuwa kinajulikana na Mwenyezi Mungu. Hakuna chochote kinachofichamana kwake kuhusu hilo. Na siku ambayo Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Atawaita washirikina Siku ya Kiyama kwa kuwakaripia na kuonyesha urongo wao, Awaambie,»Wako wapi washirika wangu ambao mlikuwa mkiwashirikisha katika ibada yangu?» Hapo waseme, «Tunakujulisha sasa kuwa hatuna yoyote atakayeshuhudia Leo kuwa wewe una mshirika.»
Wakawapotea hao washirikina wale washirika wao ambao walikuwa wakiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, wasiwanufaishe na wakajuwa kwa yakini kuwa hakuna makimbilio yoyote ya kuwaepusha wao na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Binadamu hachoki kumuomba Mola wake Ampatie mema ya duniani, na akipatikana na umasikini na shida, huwa anakata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na anakufa moyo kwa kuwa na dhana mbaya kwa Mola wake.
Na tunapomuonjesha binadamu neema kutoka kwetu baada ya shida na mitihani, hamshukuru Mwenyezi Mungu Aliyetukuka bali anaruka mpaka na kusema, «Haya niliyoyapata yamenijia kwa kuwa mimi ninastahiki kuyapata, na sidhani kuwa Kiyama ni chenye kuja.» Anasema hayo kwa njia ya kukanusha kufufuliwa «Na kwa kukadiria kuwa Kiyama kitakuja na kuwa mimi nitarudi kwa Mola wangu, basi mimi nitapata Pepo Kwake Yeye.» Basi tutawapasha habari wale walioikanusha Siku ya Kiyama kwa yale maovu waliyoyafanya, na tutawaonjesha adhabu kali.
Na tunapomneemesha binadamu kwa afya na riziki au vingineyo, hugeuka na kufanya kiburi kwa kukataa kuifuata haki. Na akipatikana na shida huwa akileta dua ndefu akimuomba Mwenyezi Mungu Amuondolee shida yake; huwa akimjua Mola wake wakati wa shida na hamjui wakati wa neema.
Sema, ewe Mtume, uwaambie hawa wakanushaji, «Hebu nipeni habari, iwapo hii Qur’ani inatoka kwa Mwenyezi Mungu kisha nyinyi mkaikataa na mkaikanusha, basi hakuna mpotevu zaidi kuliko nyinyi, kwa kuwa nyinyi mko kinyume kabisa na haki kwa kuikataa kwenu Qur’ani na kuikanusha.»
Tutawaonyesha, hawa wakanushaji, aya zetu za kuteka miji na kupata nguvu Uislamu katika majimbo mbalimbali na juu ya dini nyingine na maeneo ya mbingu na ardhi, na katika matukio makubwa Anayoyaleta Mwenyezi Mungu humo na ndani ya nafsi zao, na vile vilivyomo humo miongoni mwa alama za kuvutia za utendakazi wa Mwenyezi Mungu na maajabu ya utengenezaji Wake, (tutawaaonyesha hayo yote) mpaka iwafunukie nyinyi, ufunuzi usiyokubali shaka yoyote, kwamba Qur’ani ndiyo haki iliyoletwa kwa njia ya wahyi kutoka kwa Mola wa viumbe wote. Je hauwatoshi wao ushahidi wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuwa ni dalili ya kuwa Qur’ani ni haki na kuwa aliyekuja nayo ni mkweli? Kwani Mwenyezi Mungu Ameishuhudilia kwa kuisadikisha, na Yeye ni shahidi wa kila kitu, na hakuna kitu chochote chenye kutolea ushahidi kuliko ushahidi wa Mwenyezi Mungu, aliyetakasika na kutukuka.
Jueni na mtanabahi kuwa hawa makafiri wako kwenye shaka kubwa kuhusu kufufuliwa baada ya kufa. Jueni na mtanabahi kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Amekizunguka kila kitu kwa ujuzi, uweza na ushindi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake ardhini wala mbinguni.