ترجمة سورة الفاتحة

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الفاتحة باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .
Naanza kusoma Qur’an kwa jina la Mwenyezi Mungu nikiomba msaada Wake. «Allah» ni jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa baraka Mwenye kutukuka, Anayestahiki kuabudiwa na sio mwingine. Nalo ni jina mahsusi zaidi miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na haitwi kwa jina hili yoyote isipokuwa Yeye Aliyetakasika na sifa za upungufu. «Al-Raḥmān» Mwenye rehema nyingi Ambaye rehema Zake zimewanea viumbe vyote. «Al-Raḥīm» mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya, kati ya majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, yanakusanya uthibitishaji wa sifa ya urehemefu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kama inavyonasibiana na haiba Yake.
Kila jinsi ya sifa njema ni ya Mwenyezi Mungu, Mwenye sifa ambazo zote ni za ukamilifu, Mwenye neema za nje na za ndani, za kidini na za kidunia. Na ndani yake kuna amri ya Mwenyezi Mungu kwa waja Wake wamsifu Yeye kwa kuwa Yeye Ndiye Mstahiki wa kusifiwa Peke Yake.
Mwingi wa rehema Ambaye rehema Zake zimewaenea viumbe vyote, Mwenye kuwarehemu Waumini. Na majina mawili haya ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Na Yeye, kutakasika ni Kwake, Peke Yake Ndiye Mwenye mamlaka ya Siku ya Kiyama, nayo ni Siku ya Malipo kwa matendo yaliyofanywa na waja. Muislamu anapoisoma aya hii katika kila rakaa, inamkumbusha siku ya Akhera na inamhimiza ajitayarishe kufanya matendo mema na kujiepusha na maasia na mabaya.
Sisi tunakuabudu wewe peke yako, na tunataka msaada kwako peke yako katika mambo yetu yote. Mambo yote yako mkononi mwako, hakuna asiyekuwa wewe anayemiliki chochote katika hayo hata kadiri ya uzito wa chungu mdogo. Katika aya hii kuna dalili ya kuwa mja haifai aelekeze kitu chochote miongoni mwa aina za ibada, kama kuomba, kutaka kunusuriwa, kuchinja na kutufu, isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Pia ndani yake kuna ponya ya nyoyo kutokana na ugonjwa wa kufungamana na asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na kutokana na ugonjwa wa ria, kujiona na kiburi.
Tuonyeshe, tuongoze na tupe taufiki ya kuelekea njia iliyonyoka na ututhibitishe juu yake mpaka tukutane na wewe, nayo ni Uislamu ambao ndio njia iliyo wazi yenye kufikisha kwenye radhi za Mwenyezi Mungu na kwenye Pepo yake, njia tuliyoonyeshwa na aliye mwisho wa Mitume wa Mwenyezi Mungu na Manabii Wake, Muhammad, reheme ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwani hakuna kufaulu kwa mja isipokuwa kwa kusimama imara juu yake.
Njia ya wale uliowaneemesha miongoni mwa Manabii, wakweli wa imani, mashahidi na wema. Wao ndio watu wa uongofu na kusimama imara. Na usitufanye kuwa miongoni mwa wale waliofuata njia ya waliokasirikiwa, wale walioijua haki na wasiifuate kivitendo, nao ni Mayahudi na wale waliofanana na wao; wala usitufanye ni miongoni mwa wapotevu, nao ni wale ambao hawakuongoka kwa ujinga waliokuwa nao, wakapotea njia, nao ni Wanaswara na waliofuata mwenendo wao. Katika dua hii kuna ponya ya moyo wa Muislamu ya ugonjwa wa ukanushaji, ujinga na upotevu, na ni dalili kwamba neema kubwa zaidi kuliko zote ni neema ya Uislamu. Basi mwenye kuwa mjuzi zaidi wa haki na akawa mfuataji zaidi wa hiyo haki, basi huwa ni aula zaidi wa njia iliyonyoka. Na hapana shaka kwamba Maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ndio watu aula zaidi wa hilo baada ya Manabii, amani iwashukie. Basi aya hii yaonyesha utukufu wao na ukubwa wa daraja yao, Mwenyezi Mungu Awe radhi nao. Ni sunna kwa msomaji aseme katika Swala baada ya kusoma Fatiha «Āmīn», na maana yake ni: Ewe Mola! Takabali. Nayo si aya katika sura ya Fatiha kwa maafikiano ya wanavyuoni. Na kwa hivyo wamekubaliana kwa umoja wao kutoiandika kwenye Misahafu.
Icon