ﰡ
«Kāf, Hā, Yā, 'Ayn, Ṣād» Yametangulia maelezo kuhusu herufi za mkato kama hizi katika mwanzo wa sura ya Al-Baqarah.
Huu ni utajo wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariyyā. Tutakupasha habari yake , kwani pana mazingatio ndani yake kwa wenye kuzingatia.
Pindi alipomuomba Mola wake kwa siri, ili yawe ni maombi makamilifu zaidi na yenye kutimia katika kumtakasia Mwenyezi Mungu na yawe ni yenye matarajio zaidi ya kujibiwa.
Akasema, «Mola wangu! Mimi nimezeeka na mifupa yangu imedhoofika na nywele nyeupe zimeenea kichwani, na sikuwa huko nyuma nimekataliwa kujibiwa maombi.
«Na mimi ninaogopa kwamba jamaa zangu wa karibu na wenye kusimama na mimi wasije, baada ya kufa kwangu, wakaacha kuisimamia Dini yako vile inavyotakikana isimamiwe na wakaacha kuwalingania waja wako kuwaleta kwako, na mke wangu ni tasa hazai, basi nitunukie kutoka kwako mtoto awe ni mrithi na msaidizi.
«Atakayeurithi unabii wangu na unabii wa kizazi cha Ya’qūb, na umfanye mtoto huyu kuwa ni mwenye kuridhiwa na wewe na waja wako.»
Ewe Zakariyyā! Sisi tunakupa bishara ya kukubaliwa maombi yako. Tumekutunukia mtoto wa kuime, jina lake ni Yaḥyā, hatujampatia jina hili yoyote kabla yake.
Zakariyyā alisema kwa kushangaa, «Mola wangu! Vipi nitakuwa na mtoto wa kiume na hali mke wangu ni tasa hazai, na mimi nimefikia upeo wa ukongwe na ulaini wa mifupa.»
Malaika akasema kumjibu Zakariyyā juu ya kile alichokionea ajabu, «Mambo ni kama unavyosema kuwa mke wako ni tasa na kuwa wewe umefikia upeo wa uzee, lakini Mola wako Amesema, ‘Kumuumba Yah,yā kwa namna hii ni jambo sahali na pesi kwangu.’» Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alimtajia Zakariyyā jambo la ajabu zaidi kuliko lile aliloliuliza akasema, «Na nimekuumba wewe kabla ya Yah,yā na hukuwa ni kitu chenye kutajika wala kilichoko.»
Zakariyyā akasema kutaka kujituliza zaidi, «Mola wangu! Nipe alama ya kwamba kile ambacho Malaika wamenibashiria nacho kishapatikana.» Akasema, «Alama yako ni kutoweza kusema na watu kwa muda wa masiku matatu na michana yake na hali wewe ni mzima mwenye afya.»
Zakariyyā akawajia watu wake kutoka mahali pake pa kuswali, napo ni mahali alipobashiriwa kuwa atapata mtoto, na akawashiria wamtakase Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni kwa kumshukuru Yeye Aliyetukuka.
Alipozaliwa Yah,yā na akafikia umri wa kufahamu maneno, Mwenyezi Mungu Alimuamuru aichukue Taurati kwa bidii na jitihada kwa kusema, «Ewe Yah,yā! lchukue Taurati kwa bidii na jitihada kwa kuyahifadhi matamko yake na kuyafahamu maneno yake na kuitumia, na tulimpa busara na ufahamu mzuri ilhali yeye ni mdogo wa miaka.
Na tulimpa rehema na mapenzi kutoka kwetu na kusafika na madhambi. Na alikuwa ni muogopaji Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na ni mtiifu Kwake, mtekelezaji yale Aliyoyalazimisha na ni mwenye kujiepusha na yale Aliyoyaharamisha.
Na alikuwa mtiifu kwa wazazi wake wawili, na hakuwa ni mwenye kiburi cha kutomtii Mola wake na kutowatii wazazi wake wawili.
Na salamu itokayo kwa Mwenyezi Mungu imshukie Yah,yā na amani iwe na yeye siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa hali ya kuwa hai.
Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Maryam alipojiweka mbali na watu wake, akajifanyia mahali upande wa Mashariki kando na wao.
Akaweka kizuizi chenye kumsitiri na jamaa zake na watu wengine, hapo tukampelekea Malaika Jibrili akajjitokeza kwake katika sura ya binadamu aliyetimia umbo.
Maryam akasema kumwambia, «Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu na wewe usinifanye ubaya, iwapo wewe ni miongoni mwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.»
Malaika akawmambia, «Kwa hakika, mimi ni mjumbe wa Mola wako, Amenituma kwako nikutunuku mtoto wa kiume aliyesafika na madhambi.»
Maryam akamwambia Malaika, «Vipi mimi niwe na mtoto wa kiume, na hakuna binadamu aliyenigusa kwa ndoa ya halali, na mimi sikuwa mzinifu?»
Malaika akasema kumwambia, «Mambo ni hivyo kama unavyoeleza kwamba hakuna binadamu aliyekugusa na hukuwa mzinifu, lakini Mola wako Amesema, ‘Jambo hili kwangu ni pesi, na ili mtoto huyu awe ni alama kwa watu yenye kuonesha uweza wa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, na awe ni rehema itakayotokana na sisi kwake yeye, kwa mamake na kwa watu.’» Na kupatikana kwa Īṣā kinamna hii lilikuwa ni jambo lililokadiriwa katika Ubao uliohifadhiwa, basi hapana budi lifanyike.
Maryam akabeba mimba ya mtoto wa kiume baada ya Jibrili kupuliza kwenye mwanya wa kanzu yake, na pulizo hilo likafika kwenye uzao wake, na kwa sababu hiyo mimba ikaingia, na akaenda nayo mahali mbali na watu.
Na uchungu wa mimba ukamfanya aende kwenye kigogo cha mtende, hapo akasema, «Natamani kama nilikufa kabla ya siku ya leo na nikawa kitu kisichojulikana, kisichotajwa na kisichotambulika ‘ni nani mimi?.’»
Jibrili au 'Īsā akamwita na kumwambia, «usisikitike, kwani Mola wako amekufanyia chini yako mkondo wa maji.
«Na ukitikise kigogo cha mtende, zitakuangukia tende mbivu laini zitokazo mtini.
«Basi zile hizo tende mbivu na unywe maji na ujifurahishe kwa huyo mtoto mwenye kuzaliwa. Na umuonapo yoyote miongoni mwa watu, akakuuliza juu ya jambo lako, mwambie, ‘Mimi nimejilazimisha nafsi yangu kwa Mwenyezi Mungu ninyamaze, sitatasema na mtu leo.’» Kunyamaza kimya kulikuwa ni ibada katika Sheria yao, na haikuwa hivyo katika Sheria ya Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Hapo Maryam aliwajia watu wake, na yeye amembeba mtoto wake, akitokea mahali mbali. Walipomuona namna hiyo, walisema kumwambia, «Ewe Maryam! Umeleta jambo kubwa ulilolizua.
«Ewe dada ya mtu mwema Hārūn! Babako hakuwa ni mtu mbaya anayefanya machafu, na mamako hakuwa ni mwanamke mbaya anayefanya umalaya.»
Maryama akashiria kwa mwanawe Īsā ili wamuulize na waseme naye. Wakasema kwa kumpinga, «Vipi tutasema na ambaye bado yuko mlezini aliye mchanga wa kunyonya?»
Īsā akasema, na yeye yuko katika hali ya uchanga wa kuwa mlezini yuwanyonya, «Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, Ameamua kunipatia Kitabu, nacho ni Injili, na amenifanya Nabii.
«Na Amenifanya niwe na wingi wa wema na manufaa popote nipatikanapo, na ameniusia kutunza Swala na kutoa Zaka muda wa mimi kuwa hai.
«Na Amenifanya mimi niwe mwenye kumtendea wema mamangu, na hakunifanya ni mwenye kujiona wala ni mbaya mwenye kumuasi Mola wangu.
«Na salamu na amani ziko juu yangu mimi siku niliyozaliwa, siku nitakapokufa na siku nitakapofufuliwa nikiwa hai siku ya Ya Kiyama.»
Huyo tuliyokuhadithia, ewe Mtume, sifa zake na habari zake ndiye Īsā mwana wa Maryam pasina shaka, hali ya kuwa yeye ni neno la haki ambalo Mayahudi na Wanaswara walilifanyia shaka.
Haikuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wala hainasibiani na Yeye kujichukulia mtoto miongoni mwa waja wake na viumbe vyake, Ameepukana na kutakasika na hilo; Akiamua jambo lolote, miongoni mwa mambo, na Akalitaka liwe, dogo au kubwa, halimkatalii, kwa hakika Yeye Analiambia, «Kuwa» na likawa kama alivyolitaka liwe.
Na Īsā aliwaambia watu wake, «Na hakika ya Mwenyezi Mungu, Ambaye nawalingania nyinyi Kwake, ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni Yeye Peke Yake Asiye na mshirika, kwani mimi na nyinyi tuko sawa katika uja na kumnyenyekea Yeye. Hii ndio njia isiyo na kombo.
Mapote ya watu wa Kitabu walitafautiana baina yao kuhusu mambo ya Īsā, amani imshukiye, kati yao kuna wanaopita kiasi katika kumtukuza nao ni Wanaswara, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni Mwenyezi Mungu, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu, kati yao kuna waliosema kuwa yeye ni mmoja kati ya waungu watatu, Ametukuka Mwenyezi Mungu na kuwa mbali na hilo wanalolisema, na kati yao kuna waliomwepuka, nao ni Mayahudi, na wakasema kwamba yeye ni mchawi na wakasema kwamba yeye ni mwana wa Yūsuf aliyekuwa seremala. Basi maangamivu ni ya waliokanusha kuwa wataishuhudia siku yenye vituko vikubwa, nayo ni Siku ya Kiyama.
Ni makali yalioje yatakuwa masikizi yao na macho yao Siku ya Kiyama, siku watakayokuja kwa Mwenyezi Mungu , wakati ambapo hilo halitawafaa! Lakini madhalimu leo, katika dunia hii, wametoka nje ya haki waziwazi.
Na uwaonye watu, ewe Mtume, Siku ya Majuto, wakati wa hukumu kutolewa, na mauti yaletwe kama kwamba ni kondoo mzuri, achinjwe hapo na na uamuzi utolewe baina ya viumbe, na hapo watu wa Imani waende Peponi na watu wa ukafiri waende Motoni, na hali wao leo katika dunia hii wameghafilika na yale ambayo walionywa nayo, hivyo basi hawaamini wala hawafanyi matendo mema.
Sisi ndio tutakaoirithi ardhi na walio juu yake kwa kutoeka kwao na kusalia kwetu baada yao, na uamuzi wetu kupitishwa kwao. Na kwetu sisi ndio mwisho wao na kuhesabiwa kwao, na hapo tuwalipe kwa matendo yao.
Na uwatajie, ewe Mtume, watu wako katika hii Qur’ani kisa cha Ibrahīm, amani imshukiye; kwa hakika yeye alikuwa ni mkweli mkubwa na ni miongoni mwa Manabii wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wenye daraja za juu.
Aliposema kumwambia babake, Āzar, «Ewe baba yangu! Ni kwa jambo gani unaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, masanamu wasiosikia, wasioona na wasioweza kuzuia chochote kisikufike?
«Ewe baba yangu! Hakika Mwenyezi Mungu Amenipa ujuzi ambao hakukupa, basi nikubalie na unifuate kwa yale ninayokuitia kwayo, nikuongoze kwenye njia ya sawa ambayo hutapotea ukiifuata.
«Ewe baba yangu! Usimtii Shetani ukawaabudu hawa masanamu, kwani Shetani anaenda kinyume na Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, anakuwa na kiburi kumtii Mwenyezi Mungu.
«Ewe baba yangu! Mimi ninaogopa usije ukafa kwenye ukafiri wako, ikakupata adhabu ya Mwingi wa rehema na ukawa ni rafiki wa Shetani ndani ya Moto.»
Baba yake Ibrāhīm akasema kumwambia mwanawe,»Kwani wewe umegeuka na kukataa kuabudu waungu wangu, ewe Ibrāhīm» Basi usipokomeka kuwatukana, nitakuua kwa kukupiga mawe. Na niondokee, usikutane na mimi wala usiseme na mimi kwa kipindi cha muda mrefu.»
Ibrāhīm alisema kumwambia baba yake, «Amani juu yako kutoka kwangu, halitakufikia kutoka kwangu jambo unalolichukia, na nitakuombea Mwenyezi Mungu uongofu na msamaha. Hakika Mola wangu ni Mwingi wa huruma ni Mpole kwangu kulingana na hali yangu, nikimuomba Ataniitikia.
«Na nitawaepuka nyinyi na waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Na nitamuomba Mola wangu kwa kumtakasia, nikiwa na matumaini kuwa sitapita patupu kwa kumuomba Mola wangu Asinipe ninachomuomba.»
Na alipowaepuka wao na waungu wao wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimruzuku, miongoni mwa watoto tuliomruzuku, Ish,āq na Ya'ūb mwana wa Ish,āq na tukawafanya wawaili hao kuwa Manabii.
Na tukawatunukia wao wote rehema zetu zikiwa ni nyongeza zisizohesabika, na tukawajaalia watajike vizuri na wasifiwe kwa sifa njema zenye kubaki kwa watu.
Na utaje katika Qur’ani, ewe Mtume, kisa cha Mūsā, amani imshukiye. Kwa hakika, yeye alikuwa ni mteule aliyesafishwa, na alikuwa ni Mtume na ni Nabii miongoni mwa Mitume waliokuwa na uthabiti.
Na tulimuita upande wa jabali la Ṭūr Sīnā’ kuliani kwake (Mūsā), na tukamleta karibu na tukamtukuza kwa kusema na yeye. Katika hii pana kuthibitisha sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama inavyonasibiana na utukufu Wake na ukamilifu Wake.
Na tulimtunukia Mūsā, kutokana na rehema zetu, ndugu yake Hārūn akawa Nabii mwenye kumtilia nguvu na kumsaidia.
Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Ismāīl, amani imshukiye. Yeye alikuwa ni mkweli katika ahadi, hakuahidi kitu isipokuwa hukitekeleza, na alikuwa ni Mtume na ni Nabii.
Na alikuwa akiwaamrisha watu wake kusimamisha Swala na kutoa Zaka, na alikuwa kwa Mola wake, Aliyeshinda na kutukuka, ni mwenye kuridhiwa.
Na utaje, ewe Mtume, katika hii Qur’ani habari ya Idris, amani imshukiye. Yeye alikuwa ni mkweli mkubwa katika maneno yake na vitendo vyake, ni Nabii aaliyeletewa wahyi.
Na tukauinua utajo wake kwa viumbe wote na cheo chake kwa wale waliosongezwa karibu. Akawa ni mwenye utajo wa juu na, ni mwenye cheo cha juu.
Hawa niliokusimulia habari zao, ewe Mtume, ni wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaneemesha kwa nyongeza Zake na taufiki Yake, Akawafanya ni Mitume miongoni mwa kizazi cha Ādam, na miongoni mwa kizazi cha wale tuliowabeba pamoja na Nūḥ, katika jahazi, na miongoni mwa kizazi cha Ibrāhīm, na miongoni mwa kizazi cha Ya’qūb, na miongoni mwa wale tuliowaongoza kwenye Imani na tukawateua kwa utume na unabii. Wasomewapo aya za Mwingi wa rehema zinazokusanya upweke Wake na hoja Zake wanajipomosha chini hali ya kumsujudia Mwenyezi Mungu kwa kunyenyekea na kujidhalilisha , na wanalia kwa kumcha Yeye, kutakata ni Kwake na kutukuka ni Kwake.
Wakaja, baada ya hawa walioneemeshwa, wafuasi wabaya, waliacha Swala kabisa au waliitoa nje ya wakati wake au waliacha nguzo zake na mambo yake ya lazima na wakafuata yanayolingana na kunasibiana na matamanio yao. Basi hao watapata shari na upotevu na kupita patupu ndani ya Jahanamu.
Lakini aliyetubia dhambi zake miongoni mwao, akamuamini Mola wake na akafanya mema kusadikisha toba yake, hao Mwenyezi Mungu Atakubali toba yao, na wataingia Peponi pamoja na Waumini, na hawatapunguziwa chochote katika matendo yao mema.
Pepo yenye mabustani ya milele na makazi ya daima, nayo ni ile ambayo Mwingi wa rehema Aliwaahidi waja Wake na kuifanya wasiione, nao wakaiamini bila ya kuwa wameiona. Hakika agizo la Mwenyezi Mungu kwa waja Wake la hii Pepo ni lenye kuja, hapana budi.
Watu wa Peponi hawatasikia maneno ya batili humo, lakini watasikia ‘salamu’ ikiwa ndio maamkizi yao. Na watapata riziki yao humo ya chakula na kinywaji daima, kila wanapotaka, asubuhi na jioni, haina kiasi wala hadi maalumu.
Hiyo ndiyo Pepo inayosifiwa kwa sifa hizo, hiyo ndiyo ambayo tutairithisha na kuitoa kuwapa waja wetu wanaotucha kwa kufuata amri zetu na kujiepusha na makatazo yetu.
Na useme, ewe Jibrili, kumwambia Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Sisi, Malaika, hatuteremki kutoka mbinguni kuja ardhini isipokuwa kwa amri ya Mola wako kwetu, ni Yake yaliyoko mbele yetu yanayotukabili ya mambo ya Akhera na yale yaliyoko nyuma yetu yaliyopita katika ulimwengu na yale yaliyoko baina ya ulimwengu na Akhera. Amri yote ni Yake ya mahali na wakati. Na hakuwa Mola wako ni Mwenye kusahau kitu chochote miongoni mwa vitu.
«Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu na ardhi na vilivyoko baina yake, Ndiye Mmiliki, Muumba na Mwendeshaji wa hivyo vyote, basi muabudu Yeye Peke Yake, ewe Nabii, na uvumilie katika kumtii, wewe na waliokufuata, Hana mfano Wake kitu chochote katika dhati Yake, sifa Zake na vitendo Vyake.»
Na binadamu kafiri anasema, kwa kukanusha kufufuliwa baada ya kufa, «Je mimi nikifa na nikamalizika, kweli nitatolewa kwenye kaburi langu nikiwa hai?»
Vipi binadamu huyu kafiri amejisahau nafsi yake? Kwani hakumbuki kwamba sisi tulimuumba mara ya kwanza na hakuwa ni kitu kilichoko?
Naapa kwa Mola wako, ewe Muhammad, tutawakusanya hawa wenye kukanusha kufufuliwa Siku ya Kiyama pamoja na Mashetani, kisha tutawaleta wote kando ya moto wa Jahanamu wakiwa wamepiga magoti, kwa ukubwa wa misukosuko ambayo wamo ndani yake, hali ya kuwa hawawezi kusimama.
Kisha tutawachukua, katika kila pote, wale wakiukaji amri zaidi na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu zaidi, tuanze kuwaadhibu.
Kisha sisi ni tunawajua zaidi wale wanaostahili kuingia Motoni na kuadhibika kwa joto lake.
Na hakuna katika nyinyi, enyi watu, yoyote isipokuwa ataufikia huo Moto kwa kupita juu Ṣirāṭ (Njia) iliyotandikwa juu ya daraja la moto wa Jahanamu, kila mmoja kulingana na matendo yake. Hilo ni jambo lenye kuwa kwa lazima, Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Amepitisha na Ameamua kwamba halina budi kuwa, hakuna namana ya kuliepuka.
Kisha tutawaokoa wale ambao walimcha Mola wao kwa kumtii na kujiepusha na kumuasi na tuwaache Motoni wale waliojidhulumu nafsi zao katika hali ya kupiga magoti.
Na watu wakisomewa aya zetu zilizoteremshwa zilizo wazi, wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu wanasemakawaambia Waumini, «Ni pote gani kati yetu na nyinyi lenye mashukio bora zaidi na makalio mazuri zaidi?»
Na ni mara nyingi tumewaangamiza ummah kabla ya hawa watu wako, ewe Mtume, waliokuwa na vitu vingi kuliko walivyokuwa navyo watu wako na mandhari ya kupendeza zaidi.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Aliyekuwa amepotea njia ya haki asiyeifuata njia ya uongofu, Mwenyezi Mungu Atampa muhula na Atamnyoshea katika ule upotevu wake, mpaka atakapoyaona kwa yakini yale aliyoyaahidi Mwenyezi Mungu :ima adhabu ya haraka ulimwenguni au kusimama saa ya Kiyama, hapo atajuwa ni nani aliyopo na aliyetulia mahali pabaya na aliye mnyonge wa nguvu na askari.
Na Mwenyezi Mungu Anawaongezea waja Wake, walioongoka katika dini Yake, uongofu juu ya uongofu walionao kwa yale yanayowapitia mara kwa mara ya kuyaamini malazimisho ya Mwenyezi Mungu na kuyafuata kivitendo. Na matendo mema yaliyosalia yana malipo bora kwa Mwenyezi Mungu kesho Akhera, na yana matokeo bora na mwisho mwema.
Je ushajua, ewe Mtume, na ukaona ajabu kuhusu huyu kafiri, Al-'Ās bin Wail na walio mfano wake? Kwani yeye alizikufuru aya za Mwenyezi Mungu, akazikanusha na akasema, «Nitapatiwa-nitapatiwa huko Akhera mali na watoto.»
Je, amechungulia ghaibu akaona kuwa yeye atakuwa na mali na watoto, au ana ahadi juu ya hilo kutoka kwa Mwenyezi Mungu?
Mambo siyo kama vile alivyodai yule kafiri, kwani yeye hana ujuzi wala hakupewa ahadi. Tutatayaandika anayoyasema ya urongo na uzushi juu ya Mwenyezi Mungu, na huko Akhera tutamuongezea aina mbali mbali za mateso, kama alivyojiongezea upotovu na upotevu.
Na tutamrithi mali yake na watoto wake, na atatujia Siku ya Kiyama akiwa peke yake, hana mali wala watoto.
Na washirikina wamewachukua waungu wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ili wawatetee na wajipatie nguvu kwao.
Mambo sivyo kama wanavyodai. Hawa waungu hawatakuwa ni nguvu kwao, lakini waungu hawa watawaruka huko Akhera kuwa waliwaabudu wao na watakuwa ni wenye kusaidia katika kuteta na wao na kuwakanusha , kinyume na vile walivyodhania juu yao.
Je, huoni, ewe Mtume, kwamba sisi tumewasaliti Mashetani juu ya wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, ili wawapoteze na wawaondoe kutoka kwenye utiifu kuwapeleka kwenye uasi?
Basi usiwafanyie haraka, ewe Mtume, kwa kutaka adhabu iwashukie hawa makafiri, kwa kweli sisi tunahesabu umri wao na matendo yao hesabu isiyo na kasoro wala ukawiaji.
Siku ambayo tutawakusanya wachamungu kwa Mola wao Mwenye huruma na wao, wakiwa makundi ya watu wenye kukirimiwa,
na tutawaongoza wenye kumkanusha Mwenyezi Mungu kwa kuwasuta kwa nguvu kuwapeleka Motoni, wakitembea kwa miguu, wakiwa na kiu.
Makafiri hawa hawatakuwa na uwezo wa kumuombea yoyote. Watakaokuwa na uwezo huo ni wale waliochukua ahadi ya hilo mbele ya Mwingi wa rehema, nao ni wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume Wake.
Na hawa makafiri walisema, «Mwenyezi Mungu amejifanyia mtoto.»
Kwa hakika mumeleta, enyi hao wenye kusema, kwa kusema neno hili, jambo kubwa lililo baya.
Zakaribia mbingu kupasuka kwa ubaya mkubwa wa neno hilo, ardhi kuvunjika vipande-vipande ma majabali kuanguka kwa nguvu kwa kukasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu
kwa kumnasibishia mtoto, Mwenyezi Mungu Ametukuka na jambo hilo kutukuka kukubwa sana.
Haifai kwa Mwenyezi Mungu na hainasibiani na Yeye Awe na mtoto, kwani kuwa na mtoto ni dalili ya upungufu na mahitajio, na Mwenyezi Mungu Ndiye Mkwasi Mwenye kuhimidiwa Aliyeepushwa na sifa zote za upungufu.
Hakuna aliye mbinguni, miongoni mwa Malaika, wala aliye ardhini, miongoni mwa binadamu na majini, isipokuwa atamjia Mola wake Siku ya Kiyama akiwa ni mja mdhalilifu mnyenyekevu mwenye kukubali uja wake Kwake.
Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Amewadhibiti viumbe Wake wote na Ameijua idadi yao, hakuna yoyote miongono mawao mwenye kufichika na Yeye.
Na kila mtu, miongoni mwa viumbe, atamjia Mola wake, Siku ya Kiyama, hali ya kuwa hana mali wala watoto pamoja na yeye.
Hakika wale waliomuamini Mwenyezi Mungu, wakawafuata Mitume Wake na wakatenda mema kulingana na sheria Yake, Mwingi wa rehema Atatia katika nyoyo za waja Wake mahaba ya kuwapenda.
Hakika sisi tumeirahisisha hii Qur’ani katika ulimi wako wa Kiarabu, ewe Mtume, ili uwape bishara wachamungu, miongoni mwa wafuasi wako, na uwaonye kwayo wakanushaji wenye utesi sana kwa njia isiyofaa.
Na mara nyingi tumewaangamiza ummah waliotangulia kabla ya watu wako, humuoni yoyote miongoni mwao na husikii sauti yao, basi hivyo ndivyo watakavyokuwa makafiri wa watu wako, tutawaangamiza kama tulivyowaangamiza waliotanguli kabla yao. Katika hii pana onyo na agizo la kuwaangamiza wakanushaji wenye ushindani wa ubatilifu.