ترجمة سورة الكهف

الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
ترجمة معاني سورة الكهف باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس .

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, kwa kuwa Ana sifa ambazo zote ni sifa za ukamilifu na kwa kuwa ana neema zilizo wazi na zilizofichika, za kidini na za kidunia, Ambaye Alifanya wema Akamteremshia mja Wake na Mtume Wake Muhammad, rehema za Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, Qur’ani na Asiifanye iwe na kitu chochote cha kupotoka na haki.
Mwenyezi Mungu Ameifanya kuwa ni Kitabu kilicholingana kisicho na tafauti ndani yake wala mgongano, ili Awaonye makafiri na adhabu kali itokayo Kwake, na Awape bishara njema wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanaofanya matendo mema, kwamba wao watakuwa na malipo mengi, nayo ni Pepo,
watakaa kwenye starehe hiyo, hawataiepuka milele.
Na awaonye kwayo washirikina waliosema, «Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto.»
Hawa washirikina hawana ujuzi wowote wa kile wanchokidai kwamba Mwenyezi Mungu Amejifanyia mtoto, vilevile wale waliopita kabla yao ambao wao wamewaiga, hawakuwa na ujuzi huo. Ni makubwa sana maneno haya mabaya yanayotoka kwenye vinywa vyao. Wao hawasemi isipokuwa urongo.
Huenda wewe, ewe Mtume, ukajiangamiza nafsi yako kwa majonzi na masikitiko baada ya watu wako kukuepuka na kukupa mgongo, iwapo hawataiamini hii Qur’ani na kuifuata kivitendo.
Hakika sisi tumevifanaya vilivyoko juu ya uso wa ardhi viwe ni pambo lake na ni manufaa kwa watu wake, ili tuwatahini ni nani kati yao aliye mzuri zaidi wa vitendo vya utiifu kwetu na ni nani kati yao aliye mbaya zaidi wa kufanya maasia, na tutamlipa kila mtu anachostahiki.
Na sisi, dunia imalizikapo, ni wenye kuvifanya vilivyoko juu ya ardhi, kati ya hilo pambo, viwe mchanga usio na mimea.
Usidhani kwamba kisa cha watu wa pangoni (asḥāb al-kahf) na ubao ulioandikwa majina yao ni jambo geni la ajabu miongoni mwa alama zetu. Kuumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni jambo la ajabu zaidi kuliko hilo.
Kumbuka, ewe Mtume, pindi walipohamia vijana Waumini kwenye pango kwa kuchelea wasiteswe na watu wao na kulazimishwa kuabudu masanamu, na wakasema, «Mola wetu! Tupe rehema kutoka kwako, ambayo kwayo ututhibitishe na utuhifadhi na shari, na utusahilishie njia ya sawa yenye kutupelekea kufanya matendo unayoyapenda, tuwe waongofu na tusiwe wapotevu.»
Hapo tukawalaza usingizi mrefu, na wakasalia kwenye pango miaka mingi.
Kisha tukawaamsha kutoka kwenye usingizi wao ili tuwaonyeshe watu tuliyoyajua hapo kale ipate kupambanuka ni lipi kati ya makundi mawili, yanayobishana juu ya kipindi cha kukaa kwao, limedhibiti zaidi katika kuhesabu: je, walikaa siku moja au mbili au walikaa muda mrefu?.
Sisi tunakuhadithia, ewe Mtume, habari yao kwa ukweli. Watu wa pango ni vijana waliomuamini Mola wao na wakafuata amri Zake, na tukawazidishia uongofu na uimara katika haki.
Na tukazipa nguvu nyoyo zao kwa Imani na tukazikaza nia zao kwa hiyo Imani, waliposimama mbele ya mfalme kafiri, huku naye akiwalaumu kwa kuacha ibada ya masanamu, na wakamwambia, «Mola wetu tunayemuabudu ni Mola wa mbingu na ardhi, hatutaabudu waungu wengine, na tukisema lingine lisilokuwa hili tutakuwa tumesema neno la udhalimu lililo mbali na haki.»
Kisha wakaambiana wao kwa wao, «Watu wetu hawa wamewachukua wasiokuwa Mwenyezi Mungu wakawafanya ni wauungu, basi si watuletee ushahidi waziwazi kuwa hao wafaa kuabudiwa? Hakuna yoyote aliye dhalimu zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo kwa kudai kuwa Ana mshirika katika kuabudiwa.
Na mlipotengana na watu wenu kwa ajili ya dini yenu na mkawaacha waungu wanaowaabudu isipokuwa kumuabudu Mungu Mmoja, basi hamieni kwenye pango iliyoko jabalini mpate kumuabudu Mola wenu Peke Yake, hapo Mwenyezi Mungu Atawakunjulia rehema Yake ambayo kwayo Atawapa sitara ya dunia na Akhera na Atawafanyia njia za maisha ziwe pesi mnufaike nazo katika maisha yenu.
Walipofanya hivyo, Mwenyezi Mungu Aliwatia usingizi wakalala na Akawahifadhi. Na utaliona jua, ewe mwenye kuwatazama wao, linapochomoza upande wa mashariki linapenyeza pale walipo upande wa kulia, na linapozama linawaacha upande wa kushoto, na hali wao wako kwenye sehemu kunjufu ndani ya pango, joto la jua haliwasumbui na hewa haiwakatikii. Hayo tuliyowafanyia vijana hawa ni miongoni mwa dalili za uweza wa wa Mwenyezi Mungu. Basi yoyote yule ambaye Mwenyezi Mungu Atamuafikia kuongoka kwa aya Zake, yeye ndiye mwenye kuongoka, na yoyote ambaye Hatamuafikia hilo, hutapata yoyote wa kumsaidia na kumuongoza kuifikia haki, kwani kuafikiwa na kutoafikiwa viko mikononi mwa Mwenyezi Mungu.
Na utadhani, ewe mwenye kutazama, kwamba watu wa pangoni wako katika hali ya kuangaza, na mambo yalivyo ni kuwa wao wamelala, na sisi tunawaangalia kwa kuwatunza, tunawageuza na wao wamelala, mara nyingine ubavu wa kulia na mara nyingine ubavu wa kushoto, ili ardhi isiwale, na mbwa wao aliyekuwa amefuatana nao ameinyosha miguu yake ya mbele kwenye ukumbi wa pango. Lau uliwashuhudia ungaligeuka kukimbia na unagalijawa na kicho kwa kuwaogopa.
Na kama tulivyowalaza na tukawahifadhi muda huu mrefu, tuliwaamsha kutoka kwenye usingizi wao kama vile walivyokuwa bila kubadilika, ili waulizane wao kwa wao, «Ni muda gani tulikaa tukiwa tumelala hapa?» Baadhi yao wakasema, «Tumekaa siku moja au sehemu ya siku.» Na wengine ambao mambo yaliwachanganyikia walisema, «utegemezeni ujuzi wa hilo kwa Mwenyezi Mungu, kwani Mola wenu ni Mjuzi zaidi wa kipindi mlichokikaa, basi mtumeni mmoja wenu na pesa zenu hizi za fedha aende mjini kwetu aangalie ni mtu gani hapo mjini mwenye chakula kizuri zaidi na cha halali, na awaletee chakula kutoka kwake, na ajifichefiche akiwa na muuzaji katika kununua kwake ili tusigundulike na mambo yetu yakafichuka, na msijulikane kabisa na mtu yoyote.
Kwa hakika watu wenu wakiwagundua mulipo watawapiga mawe wawaue au watawarudisha kwenye dini yao muwe makafiri, na mkifanya hivyo basi hamtafaulu kabisa kupata matakwa yenu ya kuingia Peponi.
Na kama vile tulivyowalaza miaka mingi na tukawaamsha baada yake, tuliwafanya wajulikane na watu wa zama hizo baada ya muuzaji kuzigundua aina ya dirhamu alizozileta yule aliyetumwa na wao, ili watu wapate kujua kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Ufufuzi ni kweli na kwamba Kiyama hakina shaka ni chenye kuja. Kitahamaka hao waliowagundua watu wa Pango wakawa ni wenye kushindana kuhusu jambo la Kiyama: kuna waliolikubali na kuna waliolipinga. Na Mwenyezi Mungu Akajaalia kule kuwagundua watu wa Pango ni hoja kwa Waumini juu ya makafiri. Na baada ya mambo yao kugnuduliwa na wakafa, lilisema kundi moja la wale waliowagundua, «Jengeni kwenye mlango wa pango jengo la kuwasitiri kisha muwawache na mambo yao, Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali yao.» Na wakasema wale wenye kusikizwa maneno yao na wenye uwezo miongoni mwao, «Tutatengeneza mahali pao hapo msikiti wa kufanya ibada.» Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alikataza kuyafanya makaburi ya Manabii na watu wema kuwa misikiti, na alimlaani mwenye kufanya hivyo katika nyasia zake za mwisho kwa umati wake. Pia alikataza kabisa kujenga juu ya makaburi na kuyajengea na kuandika juu yake, kwani yote hayo ni miongoni mwa upitaji kiasi unaopelekea kuwaabudu waliomo ndani.
Watasema baadhi ya Watu wa Kitabu wenye kujishughulisha na mambo yao kwamba wao ni watatu na wa nne wao ni mbwa wao, na kundi lingine litasema kwamba wao ni watano na wa sita wao ni mbwa wao. Maneno ya makundi mawili haya ni maneno ya kudhania bila dalili yoyote. Na kundi la tatu litasema kwamba wao ni saba na wa nane wao ni mbwa wao. Sema, ewe Mtume, «Mola wangu Ndiye Mjuzi kabisa wa idadi yao,» hakuna anayeijua idadi yao isipokuwa ni wachache kati ya viumbe Wake. Basi usibishane na Watu wa Kitabu kuhusu idadi yao isipokuwa ubishi wa juu-juu usiokuwa na undani kwa kuwasimulia yale ambayo Mwenyezi Mungu amekuletea wahyi nayo, na usiulize kuhusu idadi yao na hali zao kwani wao hawalijui hilo.
Na usiseme juu ya kitu chochote unachoazimia kukifanya, «Mimi nitafanya kitu hiko kesho.»
Isipokuwa ufungamanishe neno lako na matakwa ya Mwenyezi Mungu na useme, «Mwenyezi Mungu Atakapo.» Na mkumbuke Mola wako unaposahau kwa kusema, «Mwenyezi Mungu Atakapo.» Na kila unaposahau, mtaje Mwenyezi Mungu, kwani kumtaja Mwenyezi Mungu huondosha kusahau, na useme, «Matarajio ni kwamba Mola wangu Aniongoze njia ya karibu zaidi yenye kufikisha kwenye uongofu na ya sawa.
Na vijana hao walikaa wakiwa wamelala ndani ya pango yao muda wa miaka mia tatu na siku tisa kwa hesabu ya kimwezi.
Na ukiulizwa, ewe Mtume, kuhusu muda wa kukaa kwao kwenye pango, na wewe huna ujuzi wa hilo na hukupata wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, basi usisongee mbele kwa lolote kuhusu jambo hilo, isipokuwa sema,»Mwenyezi Mungu Ndiye Mjuzi zaidi wa muda wa kukaa kwao. Ni wake Yeye ujuzi wa visivyoonekana vya mbinguni na ardhini, ni kuona kulioje Kwake na kusikia kulioje!» Yaani :uonee ajabu ukamilifu wa kuona Kwake na wa kusikia Kwake na wa kukizunguka Kwake kila kitu. Viumbe hawana yoyote mwingine isipokuwa Yeye wa kusimamia mambo yao, na Hana mshirika katika uamuzi Wake, hukumu Yake na sheria Zake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake.
Na usome Qur’ani, ewe Mtume, ambayo Mwenyezi Mungu Amekuletea wahyi nayo, kwani hiyo Qur’ani ni Kitabu ambacho hakuna mwenye kuyageuza maneno yake kwa kuwa ni ya kweli na ya uadilifu, na hutapata isipokuwa kwa Mola wako mahala pa wewe kuhamia wala pa kujilinda.
Na uvumilie nafsi yako, ewe Mtume, pamoja na Masahaba wako miongoni mwa Waumini masikini wanaomuabudu Mola wao Peke Yake na kumuomba Yeye kucha na kutwa, wakiomba kupata radhi Zake, ukae mamoja nao na utangamane nao, na usiuepushe uso wako na wao kuwaangalia wasiokuwa wao miongoni mwa makafiri kwa kutaka kujistarahesha na pambo la uhai wa kilimwengu. Na usimtii yule tulioufanya moyo wake ughafilike kututaja na akafadhilisha kufuata matamanio yake juu ya kumtii Mola Wake na mambo yake yakawa, katika matendo yake yote, yamepotea na kuangamia.
Na usme kuwaambia hawa walioghafilika, «Haya niliyowaletea ndio ukweli utokao kwa Mola wenu. Basi yoyote kati yenu atakye kuamini na akafanya matendo yanayolingana na hiyo Imani, na afanye kwani hilo ni bora kwake, na mwenye kutaka kukanusha na akanushe kwani atakua hakumdhulumu yoyote isipokuwa nafsi yake mwenyewe. Hakika sisi tumewatayarishia makafiri Moto mkali ambao kuta lake limwazunguka. Na makafiri hawa wakitaka msaada Motoni wapatiwe maji kwa vile kiu ilivyo kali, wataletewa maji kama mafuta machafu yaliyo moto sana yanayochoma nyuso zao. Ni kibaya kilioje kinywaji hiki ambacho hakiondoi kiu yao bali kinaizidisha na ni ubaya ulioje wa Moto kuwa ndio mashukio yao na makazi. Katika haya pana onyo na tishio kali kwa yoyote mwenye kuipa mgongo haki na asiuamini utume wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na asifanye vitendo vinavyolingana na Imani hiyo.
Hakika wale waliomuamini Mwenyezi MUngu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema watakuwa na malipo makubwa kabisa. Sisi hatupotezi malipo yao wala hatutawapunguzia kwa matendo mazuri waliyoyafanya.
Hao walioamini watakuwa na mabustani ya Peponi, watakaa humo daima, ambapo mito yenye maji tamu itakuwa ikipita chini ya vyumba vyao na nyumba zao. Watapambwa humo kwa vikuku vya dhahabu, na watavaa nguo za rangi ya kijani zilizofumwa kwa hariri nyembamba na nzito. Watategemea wakiwa humo kwenye vitanda vilivopambwa kwa pazia nzuri. Neema ya malipo ni malipo yao, na Pepo ni nzuri kuwa ni mashukio yao na mahali pao.
Wapigie, ewe Mtume, makafiri wa watu wako mfano wa wanaume wawili miongoni mwa ummah waliopita :mmoja wao ni Muumini na mwingine ni kafiri, na yule kafiri tulimfanya awe na mashamba mawili ya mizabibu tuliyoizungusha na mitende mingi, na tukaotesha kati yake makulima mengi ya sampuli mbalimbali yenye manufaa.
Kila mojawapo ya yale mashamba mawili lilikuwa limetoa matunda yake na halikupunguza kitu katika utoaji wake, na tulipasua mto baina yao ili kuyanosheza kwa usahali na upesi.
Na mwenye hayo mashamba mawili alikuwa na matunda na mali mengine, hapo akasema kumwambia mwenzake akimjadili katika mazungumzo, na huku amejawa na majivuno, «Mimi ni mwingi wa utajiri kuliko wewe na nina wasaidizi wenye nguvu zaidi wenye kunihami.»
Na akaingia shambani kwake , na hali amejidhulumu nafsi yake kwa kukanusha kufufuliwa na kuwa na shaka kwake juu ya kusimama Kiyama, yakampendeza matunda yake na akasema, «Siamini kwamba shamba hili litaangamia muda wa maisha
na siamini kwamaba Kiyama ni chenye kutukia, na kikitukia kwa kukisia tu, kama unavyodai ewe mwenye kuamini, na nikarudishwa kwa Mola wangu, basi huko Kwake nitapata bora zaidi kuliko shamba hili nirudishiwe na nirejeshewe, kwa ajili ya utukufu wangu na cheo changu Kwake.»
Mwenzake Muumini akamwambia, huku akimjadili kwa kumuwaidhia, «Vipi wewe utamkanusha Mwenyezi Mungu Aliyekuumba kwa mchanga kisha kwa tone la manii kisha Akakusawazisha kwa kukufanya binadamu mwenye kimo kilicholingana na umbo?» Katika aya hii pana dalili ya kwamba mwenye uweza wa kuanzisha kuumba viumbe ni muweza wa kuwarudisha.
«Lakini mimi sisemi maneno hayo yako yanayoonyesha ukafiri wako. Kwa kweli, mimi nasema ‘Mwenye kuneemesha na kufanya hisani ni Mwenyezi Mungu Mola wangu Peke Yake, na mimi simshrikishi yeye katika kumuabudu na yoyote asiyekuwa Yeye.
«Kwani si ingalikuwa afadhali, ulipoingia kwenye shamba lako na likakupendeza, kama ulimshukuru Mwenyezi Mungu na ukasema, ‘Haya ni yale Aliyenitakia Mwenyezi Mungu, sina nguvu ya kuyapata isipokuwa ni kwa Mwenyezi Mungu.’ Iwapo waniona mimi kuwa ni mchache wa mali na watoto kuliko wewe,
basi Mwenyezi Mungu huenda Akanipa mimi bora zaidi kuliko shamba lako, na Akakuondolea hiyo neema kwa ukafiri wako, na akailetea shamba yako adhabu kutoka mbinguni ikawa ni ardhi tupu iliyo kavu ambayo nyayo haziwezi kuthibiti juu yake wala hakuna mmea unaoota,
au maji yake ya kuinyosheza yazame ardhini na kukauka usiwezi kuyatoa.»
Yakawa ni kweli yale maneno ya yule Muumini, na shamba likaharibika na vilivyomo ndani vikaangamia, akawa yule kafiri anageuza vitanga vyake vya mikono huku na huku kwa kulilia hasara na majuto kwa gharama aliyoitoa pale, na hali mitiyake imeanguka chini baadhi yake iko juu ya mingine, na akawa yuwasema, «Natamani lau nilizitambua neema za Mwenyezi Mungu na uweza Wake na sikumshirikisha Mwenyezi Mungu na yoyote.» Na haya ni majuto yake wakati ambapo majuto hayamfalii kitu.
Na hakuwa na kundi la watu, kati ya wale ambao alijifahiri nao, wenye kumtetea na adhabu ya Mwenyezi Mungu yenye kumshukia, wala hakuwa ni mwenye kujitetea kwa nafsi yake na nguvu zake.
Katika shida kama hizi mategemeo na usaidizi huwa uko kwa Mwenyezi Mungu wa haki. Yeye ni bora wa kulipa mema na ni bora wa kuwapa mwisho mwema wale waliyoko hifadhini Mwake.
Na wapigie watu, ewe Mtume, hasa wale wenye kujiona kati yao, mfano wa hali ya ulimwengu, ambao wameghurika nao, kwa uzuri wake na upesi wa kuondoka kwake, kwamba ni kama maji aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka juu ambayo kwayo mimea ikatoka kwa idhini Yake na ardhi ikageuka ikawa rangi kijani. Na usipite isipokuwa muda mchache kitahamaka mimea hii ikawa imevunjikavunjika inarushwa na upepo kila upande. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza mkubwa juu ya kila kitu.
Mali na watoto ni uzuri na nguvu za ulimwengu huu wenye kumalizika. Na matendo mema, hasa kuleta tasbihi (kusema Subḥāna-llāh), tahmidi (kusema Alḥmdu li-llāh), takbiri (kusema Allāh Akbar) na tahlili(kusema Lā ilāha illa-llāh) yana malipo mazuri zaidi kuliko mali na wana. Matendo haya mema ndio bora zaidi kwa mtu kutarajia malipo mema kutoka kwa Mola wake na akapata kwayo huko Akhera yale ambayo alikuwa akiyatazamia duniani.
Wakumbushe Siku tutakapoyaondoa majabali kutoka mahali pake, na ukaiona ardhi waziwazi haina vya kuifinika miongoni mwa viumbe vilivyokuwa juu yake, na tukawakusanya wa mwanzo na wa mwisho kwenye kisimamo cha kuhesabiwa, tusimuache yoyote miongoni mwao.
Na hapo watahudhurishwa wote kwa Mola wako wakiwa wamejipanga safu, hakuna yoyote kati yao anayefichwa, na hapo Awaambie «Tumewafufua na mumetujia mkiwa peke yenu, hakuna mali pamoja na nyinyi wala watoto, kama vile tulivyowaumba mara ya kwanza. Bali mlifikiria kwamba hatutawaekea nyinyi wakati wa kuwafufua na kuwalipa kwa matendo yenu.»
Na kitawekwa kitabu cha matendo ya kila mtu kuliani kwake au kushotoni kwake, hapo utawaona waasi wameingiwa na kicho kwa yaliyomo ndani kwa sababu ya mambo ya uhalifu waliyoyafanya, na watasema watakapokiangalia, «Ewe maangamivu yetu! Kina nini kitabu hiki hakikuacha dogo wala kubwa isipokuwa kimelisajili?» Na watayakuta yote waliyoyafanya ulimwenguni yako mbele yao yamesajiliwa. Na Mola wako Hamdhulumu yoyote hata kadiri ya chungu mdogo. Mtiifu hatapunguziwa malipo yake mema, na muasi hataongezewa mateso yake.
Na kumbuka pale tulipowaamrisha Malaika kumsujudia Ādam, kimaamkizi na sio kiibada, na tukamwamrisha Iblisi vile tulivowaamrisha Malaika. Hapo Malaika wote walisujudu, lakini Iblisi aliyekuwa ni miongoni mwa majini, alitoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu na asisujudu kwa kiburi na wivu. Basi mnamfanya yeye, enyi watu, na waliozalikana na yeye kuwa ni wasaidizi wenu, mkawa mnawatii na mnaacha kunitii mimi, na hali yeye ni adui yenu aliye mtesi mno? Ni ubaya ulioje wa madhalimu kumtii Shetani badala ya kumtii Mwingi wa rehema.
Sikumleta Iblisi na kizazi chake, ambao nyinyi mnawatii, katika uumbaji wa mbingu na ardhi, nikataka msaada wao kuziumba, wala sikuwashuhudisha baadhi yao uumbaji wa wengine. Bali mimi nilipwekeka katika kuumba zote hizo bila msaidizi wala mwenye kutilia nguvu, na sikuwa ni mwenye kuwafanya wapotezaji miongoni mwa Mashetani na wengineo kuwa ni wasaidizi, basi vipi nyinyi mnawapatia haki yangu na mnawafanya wao ni wategemewa wenu badala yangu na hali mimi ndiye muumba wa kila kitu.?
Na wakumbushe pindi Atakaposema Mwenyezi Mungu kuwaambia washirikina Siku ya Kiyama, «Waiteni washirika wangu ambao mlikuwa mnadai kwamba wao ni washirika wangu katika ibada, wapate kuwaokoa na mimi leo.» Hapo wakaomba uokozi wao, na wao wasiwaokoe, na tukaweka baina ya wenye kuabudu na waabudiwa kitu cha kuwaangamiza katika moto wa Jahanamu wawe wote ni wenye kuangamia humo.
Na hao wahalifu wakaushuhudia Moto, na wakawa na yakini kwamba wao hapana budi ni wenye kuingia humo na wasipate njia yoyote ya kupitia ili kujiepusha nao.
Kwa hakika tumeeleza na kufafanua katika hii Qur’ani aina nyingi ya mifano ili waaidhike na waamini. Na mwanadamu ni mwingi wa utesi na ubishi miongoni mwa viumbe.
Na hakuna kilichowazuia watu kuamini, alipowajia Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, akiwa na Qur’ani, na kumuomba maghufira Mola wao kwa kutaka Awasamehe, isipokuwa ni kule kushindana kwao na Mtume, kutaka kwao wajiwe na mwendo wa Mwenyezi Mungu wa kuwaangamiza watu waliopita kabla yao au wapatikane na adhabu ya Mwenyezi Mungu waziwazi.
Na hatuwatumilizi Mitume kwa watu isipokuwa wawe ni wenye kuwabashiria Pepo wenye Imani na matendo mema na kuwatisha na Moto wenye kukanusha na kuasi. Na pamoja ya kuwa haki ifunushie wazi, wale waliokanusha wanagombana na mitume wao kiubatili kwa njia ya upotufu, ili wapate kuiondoa, kwa ubatilifu wao, haki aliyokuja nayo Mtume, na wamekifanya kitabu changu, hoja zangu na adhabu ambayo walionywa nayo kuwa ni shere na ni kitu cha kufanyiwa mzaha.
Na hakuna yoyote aliye mwingi wa udhalimu kuliko yule aliyepewa mawaidha ya aya za Mola wake zilizo wazi akazipuuza na akaendelea kwenye ubatilifu wake na akasahau matendo mabaya yaliyotangulizwa na mikono yake miwili asirudi nyuma. Sisi tumeweka vifiniko juu ya nyoyo zao ndipo wasiifahamu Qur’ani na wasiufikie wema uliyomo, na tumefanya ndani ya mashikio yao kitu kinachofanana na uziwi ndipo wasiisikie na wasinufaike nayo, na ukiwaita kwenye Imani hawatakuiitika na hawataongoka kuifuata kabisa.
Na Mola wako Ndiye Mwenye kusamehe dhambi za waja Wake wanapotubia, Ndiye Mwenye kuwarehemu. Lau Awatesa hawa wenye kuzipa mgongo aya Zake kwa madhambi na makosa waliyoyatenda, Angaliwaharakishia adhabu, lakini Yeye, Aliyetukuka, ni Mpole, Haharakishi kutesa. Lakini wana kipindi walichowekewa cha wao kulipwa kwa matendo yao, hawana njia ya kuepukana nacho wala kuhepa.
Vijiji hivyo vilivyo karibu na nyinyi, kama vijiji vya watu wa Nūḥ„ Ṣāliḥ„ Lūṭ, na Shu'ayb, tuliviangamiza watu wake walipodhulumu kwa kukufuru, na tuliwawekea wakati na muda maalumu wa kuwaangamiza; walipoufikia adhabu iliwajia na Mwenyezi Mungu Akawaangamiza kwayo.
Na kumbuka pindi Mūsā alipomwambia mtumishi wake, Yūsha' bin Nūn, «Sitaacha kuendelea kutembea mpaka nifike kwenye makutaniko ya bahari mbili au niende kipindi kirefu mpaka nifike kwa mja mwema nipate kujifunza kwake elimu nisiokuwa nayo.»
Wakajibidiisha kwenda, na walipofika kwenye makutano ya bahari nmbili walikaa penye jiwe la manga, na wakamsahau samaki wao ambaye Mūsā aliamuru achukuliwe kiwe ni chakula chao. Yūsha' alimbeba kikapuni, kitahamaka amekua hai na akawa anajisingirisha kuingia baharini, na akajifanyia njia iliyo wazi.
Walipoondoka pale mahali walipomsahau samaki, na Mūsā akahisi njaa, alimwambia mtumishi wake, «tuletee chakula chetu cha mwanzo wa mchana, hakika tumechoka kwenye safari yetu hii.»
Mtumishi wake akamwambia, «Unakumbuka tuliposhukia kwenye jiwe ambapo tulipumzika? Nilisahau kukwambia habari ya yule samaki, na hakuna aliyenisahaulisha isipokuwa ni Shetani. Na yule samaki, aliyekuwa mekufa, uhai umemrudia, akajirusha baharini na akajitolea njia ya kwendea, na mambo yake ni yenye kustaajabiwa.
Mūsā akasema, «Yaliyotokea ndiyo ambayo tulikuwa tukiyataka, kwani hiyo ni alama yangu ya mahali pa mja mwema.» Hapo wakarudi wakizifuata alama za nyayo zao mpaka wakakoma kwenye jiwe.
Wakamkuta mja mwema miongoni mwa waja wetu ambaye ni al-Khaḍir, amani imshukiye- naye ni Nabii, miongono mwa Manabii wa Mwenyezi Mungu, ambaye Mwenyezi Mungu Amemfisha, tuliyempa rehema kutoka kwetu na tukamfundisha elimu kubwa itokayo kwetu.
Mūsā akamsalimia na akamwambia, «Je, utaniruhusu nikufuate, unifundishe elimu ambayo Mwenyezi Mungu Amekufudisha kadiri ya mimi kujiongoza nayo na kunufaika?
Al-Khiḍir akawmwambia, «Hakika wewe , ewe Mūsā, hutaweza kuvumilia kunifuata na kuwa na mimi.
Na utakuwa na uvumilivu kwa nitakalolifanya miongoni mwa mambo yaliyofichika kwako ambayo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alinifundisha.
Mūsā akamwambia, «Utanikuta, Mwenyezi Mungu Akitaka, ni mwenye kuvumilia kwa nitakayoyaona kwao, na sitaenda kinyume na amri yako yoyote utakayoniamrisha.
Al-Khiḍr akakubali na akamwambia, «Ukifuatana na mimi usiniulize juu ya chochote usichokikubali mpaka nikupe maelezo yake yaliyofichika kwako bila ya wewe kuuliza.»
Wakatoka kwenda kwenye ufuo wa pwani, ikawapita mashua, wakawataka wenyewe wapande na wao. Walipopanda Al-Khiḍr aliukoboa ubao kutoka kwenye mashua na akaitoboa tundu. Mūsā akamwambia,»Umeitoboa mashua ili uwazamishe wenyewe, na hali wao walituchukua bila malipo? Kwa hakika umefanya jambo baya.»
Al-Khiḍr akamwambia, «Nilisema tangu mwanzo, ‘Hakika wewe hutoweza kuvumilia kuandamana na mimi.’»
Mūsā akasema akitoa udhuru, «usinichukulie kwa kusahau sharti yako juu yangu wala usinikalifishe mashaka ya kujifunza kwako, na amiliana na mimi kwa usahali na upole.»
Al-Khiḍr akakubali udhuru wake. Kisha wakatoka mashuani, na walipokuwa wanatembea kwenye ufuo wa pwani, ghafla wakamuona mvulana yuwacheza na wenzake, na Al-Khiḍr akamuua. Mūsā akamlaumu kwa nguvu na akasema, «vipi umeiua nafsi safi isyokuwa na kosa, isiyofikia umri wa kubeba majukumu, na haijaua mtu mpaka istahili kuuawa? Kwa hakika umefanya jambo baya sana.»
Akasema Al-Khiḍr kumwambia Mūsā kwa kumlaumu na kumkumbusha, «Je, sikukwambia kuwa wewe hutoweza kuvumilia pamoja na mimi kwa matendo unayoyaona kutoka kwangu katika yale ambayo hayakuzungukwa na ujuzi wako?»
Mūsā akamwambia, «Nikikuuliza kitu baada ya mara hii, niache na usifuatane na mimi, utakuwa ushapata sababu kuhusu mimi na hutakuwa umefanya kasoro, kwa kuwa ulinambia kwamba mimi sitaweza kuvumilia pamoja na wewe.»
Mūsā akaenda na Al-Khiḍr mpaka wakafika kwa watu wa kijiji, wakataka wapewe chakula kwa njia ya makaribisho. Watu wa kijijini walikataa kuwakaribisha. Kisha wao wawili walipata hapo ukuta ulioinama uliokaribia kuanguka, Al-Khiḍr akaulinganisha mpaka ukawa uko sawa. Mūsā akamwambia, «Lau ungalitaka ungalichukua kwa kazi hii malipo ukayatumia kujipatia chakula chetu kwa kuwa wao hawakutukaribisha.»
Al-Khiḍr akamwambia Mūsā, «Huu ndio wakati wa kupambanukana mimi na wewe. Nitakuelezea habari ya matendo yangu niliyoyafanya ambayo wewe ulinipinga nayo na ambayo hukuweza kuwa na uvumilivu wa kutoyauliza na kutonipinga mimi kuhusu hayo.
«Ama mashua ambayo nilitoboa tundu, ilikuwa ni ya watu masikini wanaofanya kazi baharini wakiwa ndani yake wakijitafutia riziki, nikataka kuitia kombo kwa kuitoboa, kwa kuwa mbele yao kulikuwa na mfalme anayechukuwa kila mashua nzuri kwa kuwanyang’anya wenyewe.
Na ama mvulana niliyemuua alikuwa, katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu, ni kafiri, na babake na mamake walikuwa Waumini, tukaogopa lau huyu mvulana ataendelea kuishi atawatia wazazi wake kwenye ukafiri na udhalimu wenye kupita kiasi kwa kumpenda kwao au kwa kumuhitajia.
«Tukataka Mwenyezi Mungu Ampe badala yake aliyetengenea zaidi kwa wema , dini na utiifu kwa wao wawili.
«Na ama ukuta nilioulinganisha, baada ya kuwa umeinama, mpaka ukawa sawa, ulikuwa ni wa wavulana wawili mayatima hapo kijijini, na chini yake kulikuwa na hazina yao ya dhahabu na fedha, na baba yao alikuwa mtu mwema, Mola wako Akataka wawe wakubwa, wapate nguvu na waitoe hazina yao kwa rehema itokayo kwa Mola wako. Na mimi sikuyafanya yote haya, ewe Mūsā, kwa amri yangu na kivyangu, kwa hakika nimeyafanya kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hayo niliyokueleza sababu zake ndiyo mwisho wa mambo ambayo hukuweza kuyavumilia kwa kuacha kuyauliza na kunipinga kwayo.»
Na hawa washiriikina wa watu wako wanakuuliza, ewe Mtume, kuhusu habari ya Dhulqarnain, mfalme aliye mwema, waambie, «Nitawapa habari kuhusu yeye ya kuwaachia kumbukumbu mupate kuikumbuka na kuizingatia.»
Sisi tulimpa udhibiti katika ardhi na tukampa sababu na njia za kila kitu za kufikia ayatakayo ya kukomboa miji nakuwashinda maadui na yasiyokuwa hayo.
Akazifuata hizo sababu na njia kwa bidii na juhudi.
Mpaka alipofika Dhulqarnain upande wa jua la kuchwa, alilikuta jua kwa vile alivyoliona kama kwamba linakuchwa ndani ya chemchemu ya maji moto yenye udongo mweusi, na akawakuta watu upande huo wa jua la kuchwa. Tulisema, «Ewe Dhulqarnain! Ima uwaadhibu kwa kuwaua au kwa linginelo, iwapo hawatakubali upweke wa Mwenyezi Mungu au uwatendee wema uwafundishe uongofu na uwaonyeshe usawa.»
Dhulqarnain akasema, «Ama yule aliyeidhulumu nafsi yake miongoni mwao na akamkanusha Mola wake, basi tutamuadhibu ulimwenguni kisha atarudi kwa Mola wake Amuadhibu adhabu kubwa katika moto wa Jahanamu.
«Na ama aliyemuamini Mola wake miongoni mwao, akamkubali, akampwekesha na akafanya matendo ya utiifu Kwake, basi atapata Pepo ikiwa ni malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na tutamfanyia wema na tutasema naye kwa upole na tutaamiliana naye kwa usahali.»
Kisha Dhulqarnain akarudi akaelekea upande wa Mashriki akifuata njia na sababu alizompa Mwenyezi Mungu.
Mpaka alipofika upande wa kutoka jua alilikuta hilo jua linawatokea watu wasiokuwa na mjengo ya kuwasitiri wala miti ya kuwapatia kivuli cha kuwakinga na jua.
Hivyo basi ujuzi wetu umeyazunguka mema aliyokuwa nayo na sababu kubwa alizokuwa nazo popote alipoelekea na kuenda.
Kisha akaenda Dhulqarnain akifuata njia na sababu tulizomtunukia.
Mpaka alipofika baina ya majabali mawili yaliyozuia vilivyo nyuma yake, aliwakuta hapo watu wasiokaribia kuelewa maneno ya wasiokuwa wao.
Wakasema, «Ewe Dhulqarnain, kwa hakika, Ya’jūj na Ma’jūj - nao ni binadamu wa mataifa mawili makubwa- wanafanya uharibifu katika ardhi kwa kuangamiza mazao ya ukulima na vizazi, basi je, tukupatie ujira na tukukusanyie mali ili utuwekee kizuizi baina yetu na wao chenye kupambanua baina yetu na wao?»
Dhulqarnain akasema, «Haya Aliyonipa Mwenyezi Mungu ya ufalme na udhibiti wa mambo, ni bora kwangu mimi kuliko mali yenu, basi nisaidieni kwa nguvu zenu niwafanyie kizuizi baina yenu na wao.»
«Nipeni vipande vya chuma» Walipkuja navyo, wakaviweka na wakavipanga karibu baina ya yale majabali mawili, aliwaambia wanaofanya kazi, «Washeni moto.» Na kilpogeuka chuma kuwa moto alisema, «Nipatieni shaba iliyodeuka niimimine juu yake.»
Hawakuweza Ya’jūj na Ma’jūj kupanda juu ya kile kizuizi kwa kuwa kilikuwa kirefu na kinateleza, na hawakuweza kukitoboa kwa chini yake kwa umbali wa upana wake na ugumu wake.
Dhulqarnain akasema, «Hiki nilichokijenga cha kuzuia uharibifu wa Ya’jūj na Ma’jūj ni rehema kwa watu itokayo kwa Mola wangu, na ahadi ya Mwenyezi Mungu itakapokuja ya kutoka Ya’jūj na Ma’jūj, Atakifanya kigongeke- gongeke kivunjike na kiwe sawa na ardhi, na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli.»
Na tutawaacha Ya’jūj na Ma’jūj, siku ya kuwajia ahadi yetu, watangamane wao kwa wao na wachanganyike kwa wingi wao, na Pembe ya Ufufuzi itapulizwa na tutawakusanya viumbe wote ili wahesabiwe na walipwe.
Na tutauhudhurisha moto wa Jahanamu kwa makafiri na tutaudhihirisha kwao waushuhudie, ili tuwaoneshe ubaya wa mwisho wao.
Wale ambao macho yao ulimwenguni yalikuwa yamefinikwa na kutonikumbuka, hayazioni dalili zangu, na walikuwa hawawezi kustahamili kuzisikia hoja zangu zenye kupelekea kuniamini mimi na Mtume wangu.
Je, walidhani walionikanusha kuwa watawafanya waja wangu kuwa ni waungu badala yangu, wawe ni wategemewa wao? Kwa hakika tumewatayarishia wenye kukanusha moto wa Jahanamu uwe ndio mashukio yao.
Waambie watu, ewe Mtume, kwa kuwaonya: Je, tuwapashe habari ya watu wenye vitendo vya hasara zaidi?
Wao ni wale ambao matendo yao yalipotea katika maisha ya ulimwengu- nao ni washirikina wa watu wako na wengineo kati ya wale waliopotea njia ya sawa wasiwe kwenye uongofu wala usawa- na hali wao wanadhania kuwa wanayatengeneza matendo yao.
Hao ndio waliopata hasara zaidi kivitendo, ndio wao waliozikataa aya za Mola wao na wakazikanusha na wakapinga kuwa watakutana na Yeye Siku ya Kiyama, hivyo basi matendo yao yakabatilika kwa sababu ya ukafiri wao na kwa hivyo hatutawajali chochote Siku ya Kiyama.
Malipo hayo waliyoandaliwa kwa kubatilika matendo yao, ni moto wa Jahanamu, kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwenyezi Mungu na kuzifanyia kwao shere na mchezo aya Zake na hoja za Mitume Wake.
Hakika wale walioniamini, wakawakubali Mitume wangu na wakafanya mema watapata Pepo ya juu kabisa, ya kati na kati na yenye mashukio bora kabisa.
Hali ya kukaa milele humo, hawatataka kuepukana nayo kwa kuwa na hamu nayo na kuipenda.
Sema, ewe Mtuume, «Lau maji ya bahari yalikuwa wino wa kalamu za kuandikia maneno ya Mwenyezi Mungu yanayokusanya elimu Yake, hukumu Zake na yale Aliyowatumia wahyi Malaika Wake na Mitume Wake, yangaliisha maji ya bahari kabla maneno ya Mwenyezi Mungu hayajaisha, hata kama tulikuja na bahari nyingine za kuongezea mfano wa bahari hiyo. Katika aya hii pana kuthibitisha kikweli sifa ya kusema kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama kunakonasibiana na utkufu Wake na ukamilifu Wake.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwa kweli, mimi ni binadamu kama nyinyi, ninaletewa wahyi kutoka kwa Mola wangu kwamba mola wenu ni Mola Mmoja. Basi yoyote anayekuwa ni mwenye kuiyogopa adhabu ya Mola wake na ana matumaini kupata malipo yake mazuri Siku ya Kiyama, na atende matendo mema kwa ajili ya Mola wake yenye kuafikiana na sheria Yake, na asimshirikishe yoyote pamoja na Yeye katika ibada.»
Icon