ﰡ
Enyi watu, muogopeni Mwenyezi Mungu, mjilazimishe na amri Zake na mjiepushe na makatazo Yake. Kwani Yeye Ndiye Aliyewaumba nyinyi kutokana na nafsi moja, nayo ni Ādam, amani imshukiye, na Akaiuumba, kutokana na nafsi hiyo, ya pili yake, nayo ni Ḥawwā. Na Akaeneza, kutokana na nafsi mbili hizo, wanaume wengi na wanawake wengi katika sehemu za ardhi hii. Na mchungeni Mwenyezi mungu Ambaye kupitia Kwake mnaombana nyinyi kwa nyinyi. Na jihadharini msije mkakata vizazi vyenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzichunguza hali zenu zote.
Na wale waliofiliwa na baba zao wakiwa bado hawajabaleghe, na mkawa nyinyi ndio wasimamizi wao, wapeni mali zao wafikapo umri wa kubaleghe, muonapo kutoka kwao kuwa wana uwezo wa kuhifadhi mali zao. Na wala msichukuwe kizuri katika mali zao na mkaweka mahali pake kibaya katika mali zenu. Wala msichanganye mali zao na mali zenu ili mpate kula mali zao kwa hila. Na mwenye kujasiri kulitenda hilo, hakika huyo amefanya dhambi kubwa.
Na iwapo mtachelea kwamba hamtafanya usawa kwa mayatima wa kike ambao wako chini ya usimamizi wenu, kwa kutowapa mahari yao kama wanawake wengine, basi waacheni na oeni waliowapendeza kati ya wanawake wengine, wawili au watatu au wanne. Na iwapo mtaogopa kutofanya uadilifu kati yao, basi toshekeni na mke mmoja, au toshekeni kwa mliowamiliki. Hilo, nililolifanya ni Sheria kwenu kuhusu mayatima wa kike na kuhusu kuoa mke mmoja hadi wane au kuwa na mke mmoja tu au mjakazi aliyemlilikiwa na kutiwa usuriani, liko karibu zaidi na kutofanya ujeuri na kuvuka mipaka.
Na wapeni wanawake, enyi waume, mahari yao, kipewa kinacholazimu na faradhi iliyopasa, kwa roho yenu safi. Na iwapo zitakuwa safi nafsi zao kwenu na kuwatunuku chochote katika mahari, basi kichukueni na mkitumie mnavyotaka, kwani hicho ni halali iliyo nzuri.
Wala msiwape, enyi wasimamizi, wale wafujaji, kati ya wanaume, wanawake na watoto, mali zao ambazo ziko chini ya mikono yenu, kwani wataziweka sehemu isiyokuwa yake. Mali hizi ndizo ambazo juu yake yanasimama maisha ya watu. Wapeni matumizi na mavazi, kwenye mali hizo, na muwaambie maneno mazuri yanayopendeza na muamiliane nao kwa tabia njema.
Wajaribuni mayatima walio chini ya mikono yenu mpate kuujua uwezo wao wa kutumia vizuri mali zao. Mpaka watakapofika miaka ya kubaleghe, mkawajua kuwa ni wema katika dini yao na wana uwezo wa kuhifadhi mali zao, basi wapeni mali zao. Wala msizifuje kwa kuzitumia mahali ambapo si pake kwa kupita mpaka wa matumizi na kukimbilia kuzila kabla hawajazichukua kutoka kwenu. Na mwenye mali katika nyinyi, ajizuie na atosheke na utajiri alionao, na asichukue chochote katika mali ya yatima. Na ambaye ni fukara, basi achukue kadiri ya haja yake wakati wa dharura. Na mtakapojua kuwa wao wana uwezo wa kuzihifadhi mali zao baada ya kubaleghe kwao na mkawapa mali zao, wawekeni mashahidi wakiwa ni dhamana kuwa mali yao yamewafikia kikamilifu, ili wasipate kulikanusha hilo. Na yawatosha nyinyi kwamba Mwenyezi Mungu ni shahidi juu yenu na Atawahesabu kwa mliyoyafanya.
Wanaume, wadogo na wakubwa, wana fungu lililopasishwa na Mwenyezi Mungu katika mali yalioachwa na wazazi wawili au jamaa wa karibu, yawe ni kidogo mali hayo au ni mengi, katika mafungu maalumu yaliyo wazi yaliyofaradhiwa na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, kwa hawa wanaume na pia wanawake.
Watakapohudhuria, kikao chakugawanywa urithi, jamaa wa maiti wa karibu wasiokuwa na haki ya kurithi au waliofiwa na baba zao nao ni wadogo au wasiokuwa na mali, basi wapeni chochote katika mali hayo, kwa njia ya kuwapumbaza, kabla mali hayajagawanywa kwa wenyewe. Na waambieni neno zuri lisilokuwa chafu wala baya.
Na waogope wale ambao lau watakufa na wataacha nyuma yao watoto wadogo madhaifu, wakawachelea dhuluma na kupotea, basi na wamchunge Mwenyezi Mungu juu ya wale mayatima na wengineo walio chini ya mikono yao. Nako ni kuwahifadhia mali yao, kuwalea vizuri na kuwaondolea ya kuwaudhi. Na wawaambie maneno yanayolingana na usawa na wema.
Wale wanaozifuja mali za mayatima wakawa wazichukua pasi na haki, hakika wanakula Moto utakaowaka matumboni mwao Siku ya Kiyama; wataungia Moto ambao watalisikia joto lake.
Mwenyezi Mungu Anawausia na kuwaamrisha, kuhusu wana wenu atakapokufa mmoja wenu na akaacha watoto wa kiume na wa kike, kwamba urithi wote ni wao: mtoto wa kiume atapata mfano wa fungu la watoto wawili wa kike, iwapo itakuwa hakuna mawarithi wengine isipokuwa ni wao tu. Iwapo atawaacha watoto wa kike peke yao, basi watoto wa kike wawili au zaidi watapata theluthi mbili ya alichokiacha.. Na iwapo mrithi ni binti mmoja, basi atapata nusu ya mali, na wazazi wawili wa maiti, kila mmoja atapata sudusi. Hii ni iwapo maiti ana mtoto wa kiume au wa kike, mmoja au zaidi. Iwapo maiti hana mwana, na wakawa mawarithi wake ni wazazi wake wawili, basi mamake atapata theluthi na babake atapata kilichosalia. Na iwapo maiti ana ndugu, wawili au zaidi, wawe ni wanawake au ni wanaume, basi mamake atapata sudusi, baba atapata kilichosalia na ndugu hawatapata kitu. Mgawanyo huu wa mali yalioachwa hufanyika baada ya kutoa wasia aliousia maiti katika kiwango cha theluthi, au baada ya kutoa deni adaiwalo. Baba zenu na watoto wenu ambao wamepangiwa kurithi, hamjui ni yupi katika wao mwenye manufaaa ya ukaribu zaidi na nyinyi katika dunia yenu na Akhera yenu. Kwa hivyo, msimfanye mmoja kati yao ni bora kuliko mwengine. Hili mliousiwa nalo limefaradhiwa kwenu na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa viumbe Wake, ni Mwenye hekima katika Sheria Alizowaekea.
Na nyinyi, enyi wanaume, muna nusu ya kilioachwa na wake zenu baada ya kufa kwao, iwapo hawana watoto wa kiume au wa kike, na ikiwa wana watoto, basi mtapata robo ya walichokiacha ambacho mtakirithi baada ya kutekeleza wasia wao unaofaa au baada ya kulipa deni lao kwa wastahiki. Na wake zenu, enyi waume, watapata robo ya mlichokiacha iwapo hamuna mwana wa kiume au wa kike kutoka kwao, hao wake zenu, au wengineo mliokuwa mumewaoa. Na iwapo mtakuwa na mwana wa kiume au wa kike, basi hao wake zenu watapata thumni ya mlichokiacha. Hiyo robo au thumni itagawanywa kati yao; na iwapo ni mke mmoja, basi hiyo robo au thumni itakuwa ndio fungu lake. Hii ni baada ya kutekeleza kile mlichousia kitekelezwe katika nyasia zifaazo, au kulipa deni lenu. Na iwapo mwanamume au mwanamke atakufa, na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa na ndugu mmoja wa kwa mama, wa kiume au wa kike, basi kila mmoja kati yao wawili atapata sudusi; wakiwa ni zaidi ya mmoja watashirikiana katika theluthi itakayogawanywa baina yao kwa usawa bila kutafautisha baina ya mwanamume na mwanamke. Hili ndilo fungu Alilowaekea Mwenyezi Mungu ndugu wa kwa mama, wa kiume na wa kike, likiwa ni urithi wao, baada ya kutekeleza wasia wa aliyekufa iwapo aliusia chochote ambacho hakina madhara kwa mawarithi au baada ya kulipa madeni yake. Kwa hili Amewausia Mola wenu, wasia wenye manufaa kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno kwa yanayowafaa viumbe Wake, ni Mpole, Hana haraka ya kuwaadhibu.
Hukumu hizo za Kimungu zilizowekwa na Mwenyezi Mungu, kuhusu mayatima, wanawake na mirathi, ni Sheria Zake zioneshazo kuwa zinatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliye Mjuzi, Aliye Mwingi wa hekima. Na yoyote mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake katika hukumu hizi na nyenginezo zilizowekwa na Mwenyezi Mungu kwa waja Wake, Atamuingiza kwenye mabustani ya Peponi, yenye miti mingi na majumba ya fahari mengi, inayopita chini yake mito yenye maji tamu. Watasalia kwenye neema hii, hawatoki humo. Malipo hayo ndio kufuzu kukubwa.
Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake , kwa kuzikanusha hukumu za Mwenyezi Mungu na kuzikiuka Sheria Zake kwa waja Wake, kwa kuzibadilisha au kuacha kuzitumia, huyo Atamuingiza Motoni, adumu humo; na atapata adhabu ya kumtweza na kumfanya mnyonge.
Na wale wanaozini katika wanawake wenu, washuhudisheni kwao, enyi viongozi na makadhi, wanaume wanne waadilifu miongoni mwa Waislamu, Na iwapo watatoa ushahidi juu yao kwa hilo, wazuieni, wanawake hao, majumbani mpaka yamalizike maisha yao kwa kufa au Mwenyezi Mungu awape njia ya kuwaokoa na hilo.
Na wawili wenye kujiingiza kwenye kitendo cha uzinifu basi waudhini kwa kuwapiga, kuwahama na kuwaaibisha. Wakitubia na kitendo walichokifanya na wakajirekebisha kwa kufanya mambo mema, wasameheni na kuacha kuwaudhi. Faida inayotokana na aya hii na ile kabla yake ni kwamba wanaume wakifanya kitendo cha uzinifu wataudhiwa., ama wanawake watafungwa na kuudhiwa. Kifungo, kikomo chake ni kifo. Na udhia, kikomo chake ni toba na kutengea. Hii ilikuwako mwanzo wa Uislamu, kisha ikaondolewa kwa Sheria iliowekwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, nayo ni kupigwa mawe mpaka kufa, kwa yule ambaye ashaoa au ashaolewa, wakiwa wote wawili ni watu huru, waliobaleghe, wenye akili na ambao wameingilia au kuingiliwa katika ndoa sahihi. Ama wasiokuwa hao, adhabu yao ni kupigwa mbati mia na kuhamishwa mwaka mzima. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzikubali toba za waja Wake wanaotubia, ni Mwenye huruma kwao.
Kwa kweli, Mwenyezi Mungu Anaikubali toba itokayo kwa wale wanaofanya maasia na madhambi kwa ujinga wao wa kutojua ubaya wake na kwamba yanasababisha hasira za Mwenyezi Mungu.- Kwa hivyo, kila anayemuasi Mwenyezi Mungu, kwa kukosea au kwa kusudi, yeye ni mjinga kwa kuzingatia maana haya, hata kama anajua kuwa ni haramu.- kisha, hao wanaokubaliwa toba zao, wakarudi kwa Mola wao kwa majuto na kutii kabla ya kukabiliwa na mauti. Basi hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu Anaikubali toba yao. Na Mwenyezi Mungu daima ni Mjuzi kwa viumbe Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo na makadirio Yake.
Kukubaliwa toba si kwa wale wanaoendelea kufanya maasia bila ya kurudi kwa Mola wao mpaka wakafikiwa na shida ya mauti, hapo mmoja wao aseme, «Mimi sasa nimetubia.» Kama ambavyo haikubaliwi toba ya wale wanaokufa na hali wao ni wenye kukanusha, ni wenye kupinga upweke wa Mwenyezi Mungu na ujumbe wa Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Hao wenye kuendeleza maasia hadi kufa kwao, na wakanushaji ambao wanakufa na huku ni makafiri, tumewatayarishia adhabu iumizayo.
Enyi mlioamini, haifai kwenu kuwafanya wake wa baba zenu ni miongoni mwa mali yalioachwa kurithiwa, mkawa mnafanya mtakavyo kwao: kwa kuwaoa, kuwakataza wasiolewe au kuwaoza waume wengine, hali ya kuwa wao hawayataki hayo yote. Na pia haifai kwenu kuwadhuru wake zenu kwa kuwa mnawachukia, ili wapate kusamehe baadhi ya mlivyowapa, mahari au vinginevyo. Isipokuwa wakiwa wamefanya jambo ovu, kama uzinifu, hapo mnayo nafasi ya kuwazuia mpaka mkitwae mlichowapa. Na kule kukaa kwenu na wake zenu yatakikana kuwe ni juu ya misingi ya heshima na mapenzi na kuwatekelezea haki zao. Na iwapo mtawachukia kwa sababu yoyote katika sababu za kidunia, basi kuweni na subira. Kwani huenda mkachukia jambo, miongoni mwa mambo, na ikawa ndani yake muna kheri nyingi.
Na mnapotaka kubadilisha mke mahali pa mke mwengine, na mkawa mumempa yule mnayetaka kumtaliki mali mengi yakiwa ni mahari yake. Si halali kwenu kuchukua chochote katika mali hayo. Je mnayachukua kwa njia ya urongo na uzushi ulio wazi?
Na vipi itakuwa ni halali kwenu kukichukua mlichowapa cha mahari, na kila mmoja kati yenu amejiliwaza na mwenzake kwa kuingiliana na walichukua kutoka kwenu ahadi iliyo nzito ya kuwa mtashikamana nao kwa wema au mtaepukana nao kwa ihsani?
Wala msiwaoe wanawake walioolewa na baba zenu, isipokuwa yaliyopita mliyoyafanya katika zama za jahiliyyah (kabla ya Uislamu). Hayo hamtalipwa kwayo. Hakika ndoa ya watoto kuwaoa waliokuwa wake wa baba zao ni jambo baya lenye upeo wa ubaya, na ni jambo lenye kuchukiza ambalo Mwenyezi Mungu Anamchukia mwenye kulifanya. Na ubaya wa njia na mwenendo ni huo mliokuwa mkiufanya zama za ujinga wenu( kabla ya Uislamu).
Mwenyezi Mungu Amewaharamishia kuwaoa mama zenu, wanaingia kwenye uharamu huu manyanya wa upande wa baba na upande wa mama, na mabinti zenu, wanaingia kwenye uharamu huu mabinti wa watoto wa kiume au wa kike na kwenda chini, na dada zenu kwa baba na mama au kwa baba au kwa mama, na mashangazi zenu, nao ni ndugu wa kike wa baba zenu na babu zenu, na makhalati zenu, nao ni dada za mama zenu na nyanya zenu, na mabinti wa ndugu wa kiume na mabinti wa ndugu wa kike; na waingia humo watoto wao, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu mlionyonya nao; na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ameharamisha kwa ajili ya kunyonya kila aliyeharamishwa kwa ajili ya ukaribu wa nasaba. Pia ni haramu kuwaoa mama za wake zenu, muwe mumewaingilia hao wake zenu au hamukuwaingilia, na mabinti wa wake zenu wa mababa wengine ambao kawaida wanalelewa majumbani mwenu na chini ya uangalizi wenu, wao ni haramu kuwaoa hata kama hawamo majumbani mwenu, lakini kwa sharti ya kuwaingilia mama zao. Na iwapo hamkuwaingilia mama zao , na mkawataliki au wakafa kabla ya kuwaingilia, hapo hapana makosa kuwaoa mabinti wao. Pia amewaharamishia Mwenyezi Mungu kuwaoa waliokuwa wake wa watoto wenu watokao migongoni mwenu, na wale walioshikanishwa na wao ambao ni watoto wenu wa kiume kwa kunyonya. Kuharamishwa huku kunakuwa kwa kufunga ndoa, awe yule mtoto wa kiume amemuingilia mkewe au hakumuingilia. Pia Amewaharamishia kuwakusanya pamoja, kwenye ndoa, dada wawili wa nasaba au wa kunyonya, isipokuwa yale yaliopita mlioyafanya katika zama za kabla ya Uislamu. Kadhalika, haifai kuwakusanya, kindoa, mwanamke na shangazi yake au khalati yake, kama ilvyokuja katika Sunnah. Mwenyezi Mungu daima ni Mwenye kuwasamehe watenda madhambi pindi wanapotubia. Ni Mwenye huruma nao, Hawakalifishi wasiloliweza.
Na ni haramu kwenu kuwaoa wanawake walioolewa, isipokuwa wale mliowateka katika jihadi. Hao ni halali kwenu kuwaoa baada ya kutakasika vizazi vyao kwa kipindi kimoja cha hedhi. Mwenyezi Mungu Amewaandikia uharamu wa kuwaoa hao, na Amewaruhusu kuwaoa wangineo, miongoni mwa wale Aliowahalalishia kuwataka kwa ndoa mkitumia pesa zenu kujihifadhi msitende haramu. Basi wale mliostarehe nao, miongoni mwao, kwa ndoa sahihi, wapeni mahari yao ambayo ni haki yao iliyolazimishwa na Mwenyezi Mungu juu yenu. Na si makosa kwenu, kwa makubaliano yaliyofikiwa baina yenu kwa kuridhiana, kupunguza au kuongeza kiwango cha mahari baada ya kuamuliwa kiwango chake. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika hukumu zake na uendeshaji Wake.
Na asiyeweza kujimudu mahari ya Waumini waungwana, basi ni hiyari yake aoe wengineo miongoni mwa wanawake wenu waumini waliomilikiwa. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Mjuzi wa ukweli wa Imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na wengine katika nyinyi. Basi waoeni kwa ruhusa ya watu wao, na wapeni mahari yao mliokubaliana nayo kwa moyo wenu safi, na wawe ni wenye kujiepusha na haramu, si wenye kudhihirisha zina, wala si wenye kuzini kwa siri kwa kufanya urafiki na wanaume. Wakiolewa na wakafanya kitendo kichafu cha kuzini, adhabu yao ni kadiri ya nusu ya adhabu ya walio huru. Huyo aliyeruhusiwa kuoa wajakazi wenye sifa zilizotajwa, ameruhusiwa iwapo anachelea kuingia kwenye uzinifu na ikawa ni uzito kwake kuvumilia kutoundama. Na kuvumilia kutooa wajakazi pamoja na kujihifadhi ni aula na bora zaidi. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwingi wa msamaha kwenu, ni Mwenye kuwahurumia sana kwa kuwaruhusu muwaoe wao(hao wajakazi) mkishindwa kuwaoa waungwana.
Katika kuwaekea Sheria hizi, Mwenyezi Mungu Anataka kuwafunulia wazi alama za dini Yake iliyolingana na hukumu Zake zenye hekima, kuwaonesha njia za Mitume na watu wema waliokuwa kabla yenu katika halali na haramu na kuwakubalia toba zenu kwa kuwarudisha kwenye kumtii Mwenyezi Mungu. Na Yeye, Aliyetakasika na sifa pungufu, ni Mjuzi wa yale yenye kutengeneza mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowaekea.
Na Mwenyezi Mungu Anataka kuwakubalia toba zenu na kuyasamehe makosa yenu; na wale wanaofuata matamanio yao na starehe zao, wanataka mupotoke muwe kando na Dini kabisa.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa sheria Zake Alizowaekea, Anataka kuwafanyia sahali na kutowafanyia mkazo, kwa kuwa nyinyi mumeumbwa mkiwa madhaifu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo! Si halali kwa baadhi yenu kula mali ya wengine kati yenu pasi na haki, isipokuwa ikiwa itaambatana na Sheria na chumo la halali litokanalo na kuridhiana baina yenu. Na wala msiuane nyinyi kwa nyinyi mkaziangamiza nafsi zenu kwa kufanya maasia yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma sana katika kila Alilowaamrisha kwalo na kuwakataza nalo.
Na Mwenye kutenda Aliyoyakataza Mwenyezi Mungu ya kuchukua mali ya haramu, kama kuiba, kunyang’anya na kudanganya, kwa dhuluma na kukiuka mipaka ya Sheria, Mwenyezi Mungu Atamuingiza kwenye Moto alionje joto lake. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi.
Mkijiepusha, enyi Waumini, na madhambi makubwa, kama kumshrikisha Mwenyezi Mungu, kuwaasi wazazi wawili, kumuua mtu bila ya haki na mengineyo, tutawasamehe madhambi yenu madogo yaliyo chini ya hayo na tutawaingiza mahali pema pa kuingia, napo ni Pepo.
Wala msiyatamani mambo ambayo Mwenyezi Mungu Amewafadhilisha kwayo, baadhi yenu juu ya wengine, ya vipewa na riziki na mengineyo. Kwani Mwenyezi Mungu Amewapa wanaume malipo kulingana na matendo yao na Amewapa wanawake malipo kulingana na matendo yao. Na muombeni Mwenyezi Mungu Aliye Mkarimu na Mpaji Awape nyongeza za ukarimu Wake, badala ya kutamani tu. Hakika Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, na Yeye Anayajua zaidi yanayowafaa waja Wake miongoni mwa kheri Aliyowagawia,
Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea warithi wenye kukirithi kilichoachwa na wazazi wawili na jamaa wa karibu. Na wale mliofungamana nao kwa mayamini yaliyotiliwa mkazo kuwa mtanusuriana na mtawapa kitu katika urithi, basi wapeni walichokadiriwa. Kurithiana kwa mikataba ya kunusuriana kulikuwako mwanzo wa Uislamu , kisha hukumu yake ikaondolewa kwa kuteremka aya za mirathi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuona kila kitu katika vitendo vyenu na Atawalipa kulingana navyo.
Wanaume ni wasimamizi wa kuwaelekeza wanawake na kuwatunza, kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu Amewatunuku nacho cha sifa za usimamizi na kutukuzwa, na mahari na matumizi waliyowapa hao wanawake. Basi wale walio wema katika wao, hao wanawake, kwa kuhifadhiwa na Mwenyezi Mungu na kuafikiwa, wanasimama imara kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu, wanamtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wanatunza kila lisilojulikana na waume zao katika mambo waliyoaminiwa nayo. Na wale katika wao mnaochelea kuwafanyia nyinyi ujeuri kwa kuacha kuwatii, wapeni nasaha kwa maneno mazuri; iwapo maneno mazuri hayakuzaa matunda kwao, wahameni vitandani wala msiwakaribie. Iwapo kuwahama hakukuwafanya waathirike na kubadili mwenendo wao, basi wapigeni kipigo kisicho na madhara. Na wakiwa watawatii, jihadharini kuwafanyia maonevu. Kwani Mwenye zi Mungu Aliye juu, Aliye Mkubwa Ndiye Msaidizi wao, na Yeye ni Mwenye kuwalipiza wale waliowadhulumu na kuwaonea.
Na mkijua, enyi wasimamizi wa mume na mke, kuwa kuna ugomvi baina yao unaopelekea kutengana, wapelekeeni mwamuzi muadilifu wa upande wa mume na mwamuzi muadilifu wa upande wa mke, ili watazame na kutoa uamuzi wenye maslahi ya wao wawili. Na kwa kuwa wale waamuzi wawili wana hamu ya kupatanisha na wanatumia njia nzuri, Mwenyezi Mungu Atawatilia taufiki baina ya mume na mke. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, hakuna chochote kinachofichamana Kwake kuhusu mambo ya waja Wake, ni Mtambuzi wa yaliyomo ndani ya nafsi zao.
Na muabuduni Mwenyezi Mungu na mtiini Yeye Peke Yake, wala msimfanyie mshirika katika ustahiki wa kuwa Ndiye Mola na Ndiye Mwenye kuabudiwa, na wafanyieni wema wazazi wawili na mtekeleze haki zao na haki za jamaa wa karibu, na mayatima na wahitaji, na jirani wa karibu na wa mbali, na rafiki wa safari na wa mjini, na msafiri mwenye uhitaji, na waliomilikiwa na nyinyi, wanaume na wanawake. Hakika Mwenyezi Mungu Hawapendi, katika waja Wake, wenye kiburi na kujigamba kwa watu.
Nao ni wale wanaojizuia kutumia na kutoa kile Alichowaruzuku Mwenyezi Mungu, wakawaamuru wengineo kufanya ubahili, wakazikanusha neema za Mwenyezi Mungu juu yao na wakazificha fadhila Zake na vipewa Vyake. Na tumewaandalia wenye kukanusha adhabu yenye kudhalilisha.
Na pia tumewaandalia adhabu hii wale ambao wanatoa mali yao kwa njia ya ria na kujitangaza na hawamuamini Mwenyezi Mungu, kiitikadi na kivitendo, wala Siku ya Kiyama. Matendo haya mabaya ni miongoni mwa yale yanayolinganiwa na Shetani. Na yoyote yule ambaye Shetani atakuwa ni mwenye kushikamana na yeye, basi mtu mbaya wa kushikamana naye na kufanya naye urafiki ni yeye.
Kwani kuna madhara gani yatakayowafika wao lau walimuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, kiitikadi na kivitendo, na wakayatoa yale Aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa kutaka thawabu na kuwa na ikhlasi. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kuwajua wao na kuyajua wayafanyayo na Atawahesabu kwayo.
Mwenyezi Mungu Hampunguzii yoyote malipo ya matendo yake hata kama ni kadiri ya chungu. Na uwapo huo uzito wa chungu ni jambo jema, basi Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa pungufu, Atamuongezea na kumkuzia mwenye kulifanya, na Atamkirimu kwa nyongeza, kwa kumpa kutoka Kwake thawabu kubwa ambazo ni Pepo.
Vipi itakuwa hali ya watu, Siku ya Kiyama, pindi Mwenyezi Mungu Atakapomleta Mtume wa kila uma, ili atoe ushahidi juu yake kwa yale uliyoyafanya, na atakapo kukuleta wewe, ewe Mtume, utoe ushahidi juu ya uma wako kwamba wewe uliwafikishia ujumbe wa Mola wako?
Siku litakapokuwa hilo, watatamani, wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakampinga Mtume wasimtii, lau Mwenyezi Mungu Angaliwafanya sawasawa, wao na ardhi, wakawa mchanga ili wasifufuliwe. Na wao hawawezi kumficha Mwenyezi Mungu chochote kilichoko ndani ya nafsi zao, kwa kuwa Mwenyezi Mungu Atakuwa Amefunga midomo yao na kutolewa ushahidi juu yao na viungo vyao wenyewe kwa yale waliokuwa wakiyafanya.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Yake kivitendo, msiikaribie Swala wala msisimame kwenda kusali mkiwa katika hali ya ulevi mpaka muyaelewe na muyajue mnayoyasema. -Hii ilikuwa kabla ya kuthibitishwa uharamu wa pombe katika hali zote-.Na wala msikaribie Swala mkiwa na hadathi kubwa, nayo ni janaba. Na pia, mkiwa na janaba, msizikaribe sehemu za Swala, nazo ni misikiti, isipokuwa kwa mpita njia, katika nyinyi, kutoka kwenye mlango hadi mlango mwingine, mpaka mjitwahirishe kwa kuoga. Na mkiwa katika hali ya ugonjwa, mkawa hamuwezi kutumia maji, au hali ya safari, au mmoja wenu akaja kutoka kwenye haja kubwa au ndogo au mkawaingilia wanawake na msipate maji ya kujisafisha, ujieni mchanga uliyo tohara mjipanguse nao nyuso zenu na mikono yenu. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Anayasamehe makosa yenu na Anawasitiria.
Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya Mayahudi waliopewa fungu la elimu kwa Taurati iliyowajia, wanatoa uongofu na kuchukua upotevu badala yake, wanaacha hoja na dalili walizonazo zenye kuonesha ukweli wa ujumbe wa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wanawatakia nyinyi, enyi Waumini, muende kombo na njia iliyolingana ili muwe wapotevu kama wao?
Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa pungufu na kutukuka, Anaujua zaidi kuliko nyinyi, enyi Waumini, uadui wa hawa Mayahudi juu yenu. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa kuwasimamia, na inatosha kuwa Yeye Ndiye Mnusuru wa kuwanusuru juu ya maadui zenu.
Miongoni mwa Mayahudi kuna kundi lililozoea kuyabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu na kuyageuza kinyume cha vile yalivyo kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo na kusema kumwambia Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Tumesikia neno lako na tumeasi amri yako, na sikia kutoka kwetu mwana kutosikia,» na wanasema, «tupe masikizi yako,» yaani, tuelewe na utufahamishe, huku wakizipotoa ndimi zao kwa hilo wakikusudia kumnasibisha na upumbavu, kulingana na lugha yao, na kuitukana dini ya Uislamu. Na lau wao walisema, «Sami'nā wa ata'nā (tumesikia na tumetii),» badala ya kusema «'Aṣaynā» (tumeasi), na walisema «Isma'» (sikia) bila kuongeza «Ghayra musma'» (mwana kutosikia) na walisema, «Unzumā» (tuangalie na utuchunge) badala ya kusema,»Rā'inā», ingalikuwa ni bora kwao mbele ya Mwenyezi Mungu na lingalikuwa ni neno la uadilifu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu Aliwatoa kwenye rehema Yake kwa sababu ya ukafiri wao na kukanusha kwao unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa kuwa hawaamini isipokuwa Imani chache isiyowanufaisha.
Enyi watu wa Kitabu , Aminini na mufuate kivitendo yale tuliyoyateremsha kwenye Qur’ani, yenye kusadikisha Vitabu vilivyoko kwenu, kabla hatujawaadhibu kwa matendo yenu mabaya tukazifuta nyuso na kuzigeuza upande wa migongo au tukawapa laana waharibifu hawa kwa kuwageuza kuwa manyani na nguruwe, kama tulivyowapa laana watu wa Jumamosi ambao walikatazwa kuvua siku hii wasikatazike, Mwenyezi Mungu Akawakasirikia na Akawafukuza kutoka kwenye rehema Yake. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kupita kwa hali yoyote.
Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hamghofirii wala Hamsamehe aliyemshirikisha Yeye na yoyote miongoni mwa viumbe Wake au akamkufuru kwa aina yoyote ya ukafiri mkubwa. Lakini Anayasamehe na kuyafuta madhambi yaliyo chini ya ushirikina kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na yoyote anayemshirikisha Mwenyezi Mungu na mwingine, hakika amefanya dhambi kubwa.
Kwani hukujua, ewe Mtume, hali ya wale wanaojisifu wenyewe na kuyasifu matendo yao kuwa yametakasika na kuwa yako mbali na uovu? Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake Ndiye Ambaye Anamsifu Amtakaye miongoni mwa waja Wake, kwa kuwa Yeye Ndiye Ajuwaye ukweli wa matendo yao. Na wala hawatapunguziwa chochote katika matendo yao, hata kama ni kadiri ya uzi ulio kwenye mwanya wa koko ya tende.
Watazame, ewe Mtume, kwa kuyaonea ajabu mambo yao, vipi wanamzulia Mwenyezi Mungu urongo, na hali Yeye Ndiye Anayetakaswa na kila lisilokuwa laiki na Yeye? Uzushi huu unatosha kuwa ni dhambi kubwa lenye kuonyesha wazi itikadi yao mbovu.
Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale Mayahudi waliopewa sehemu ya elimu, wanakiamini kila kiabudiwacho badala ya Mwenyezi Mungu, miongoni mwa masanamu na mashetani wa kibinadamu na wa kijini, imani inayowapelekea wao kuhukumiana kwa sheria isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu, na wanasema kuwaambia wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, «Hawa makafiri wako kwenye njia iliyo sawa zaidi na yenye uadilifu zaidi kuliko wale walioamini»?
Hao ndio ambao umezidi uharibifu wao na umeenea upotevu wao. Mwenyezi Mungu,Aliyetukuka, Amewatoa kwenye rehema Yake. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Anamfukuza kwenye rehema Yake, hutampatia wa kumnusuru na kumuepushia adhabu mbaya.
Je, kwani wao wana fungu la utawala? Na lau walipewa, hawangalimpa yoyote kitu chochote katika hilo, hata kama ni kadiri ya kitone kilichoko kwenye koko ya tende.
Au je, kwani wao wanamhusudu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye kwa neema za unabii na utume alizopewa na Mwenyezi Mungu na kuwahusudu Masahaba wake kwa neema ya kuongozwa kwenye Imani, kuukubali utume, kumfuata Mtume na kupewa uwezo katika ardhi, wakawa wanatamani neema hizi ziwaondokee? Hakika sisi tuliwapa watu wa kizazi cha Ibrāhīm, amani imshukiye, Vitabu Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwao, wahyi mwingine usiokuwa kitabu chenye kusomwa na tukawapa , pamoja na hayo, utawala wenye kuenea.
Miongoni mwa hawa ambao walipewa fungu la elimu, kuna aliyeamini ujumbe wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na akafuata Sheria aliyokuja nayo kivitendo. Na miongoni mwao kuna aliyekengeuka na asiitike mwito wake na akawakataza watu kumfuata. Wenye kuwatosha nyinyi, enyi wenye kukanusha, ni moto wa Jahanamu ambao utawashwa kwenu.
Hakika wale waliokanusha aya za Mwenyezi Mungu alizoziteremsha, wahyi wa kitabu Chake, dalili na hoja Zake, tutawaingiza kwenye Moto ambao watalionja joto lake; kila zikiungua ngozi zao tunawageuzia ngozi nyengine, ili adhabu yao na uchungu vipate kuendelea. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Mshindi, hakuna chochote chenye kumlemea, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na uamuzi Wake.
Na wale ambao nyoyo zao zilitulia kwa kumuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kuukubali ujumbe wa Mtume Wake, Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na wakasimama imara juu ya utiifu, tutawaingiza kwenye mabustani ya Pepo ambayo, chini ya majumba yake ya fahari na miti yake, inapita mito. Watastarehe humo milele na hawatatoka humo. Watakuwa na wake humo waliotakaswa na Mwenyezi Mungu na kila maudhi. Na tutawatia kwenye vivuli vilivyoshikana vilivyorefuka Peponi.
Mwenyezi Mungu Anawaamrisha nyinyi kutekeleza aina zote za amana mlizoaminiwa nazo kwa wenyewe, msizifanyie dharau. Na Anawaamrisha muhukumu baina ya watu kwa uadilifu na uhaki, mtakapohukumu baina yao.Hilo ni jambo bora zaidi Analowaidhia Mwenyezi Mungu na kuwaongoza mlifanye. Hakika Mweyezi Mungu Aliyetukuka ni Msikizi wa maneno yenu, Anayajua matendo yenu na Anayaona.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, zikubalini amri za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na wala msimuasi, mkubalini Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kwa yale Aliyokuja nayo ya haki na watiini watawala wa mambo yenu isipokuwa katika kumuasi Mwenyezu Mungu. Na mnapotafautiana baina yenu katika kitu chochote, basi irudisheni hukumu yake kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Sunnah ya Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, iwapo nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na Siku ya Mwisho Imani ipasavyo. Kurudisha huko kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunnah ni bora kwenu kuliko kubishana na kusema kwa maoni, na ni mazuri kabisa marejeo yake na mwisho wake.
Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale wanafiki wenye kudai kuwa wameyaamini yale uliyoteremshiwa, nayo ni Qur’ani, na yale waliyoteremshiwa Mitume kabla yako, ilhali wao wanataka kuhukumiwa, katika ugomvi unaotokea baina yao, kwa sheria ya batili, isiyowekwa na Mwenyezi Mungu, na wao waliamrishwa kuikataa batili? Shetani anataka kuwaepusha na njia ya haki na kuwaweka mbali nayo kabisa. Katika aya hii kuna dalili kwamba Imani ya kweli inalazimu kufuata sheria ya Mwenyezi Mungu na kuitumia katika kutoa uamuzi juu ya kila jambo. Kwa hivyo, mwenye kudai kuwa ni Muumini na akachagua uamuzi wa Shetani juu ya uamuzi wa Mwenyezi Mungu, huwa ni Mrongo katika madai yake.
Na hawa wanaponasihiwa na kuambiwa, «Njooni kwenye yale yaliyoateremshwa na Mwenyezi Mungu na kwa Mtume na uongofu wake», utawaona wale wenye kudhihirisha Imani na kuficha ukafiri, wanakugeuka na kukupa mgongo.
Hali ya wanafiki hawa itakuwa namna gani, watakapofikiwa na misiba kwa sababu ya makosa yaliyotendwa na mikono yao kisha wakakujia, ewe Mtume, wakitoa udhuru na kukuhakikishia kwamba wao hawakuwa na malengo yoyote, kwa matendo yao hayo, isipokuwa ni kutenda wema na kuleta upatanishi baina ya wagomvi?
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu Anaujua uhakika unafiki ulio ndani ya nyoyo zao. Basi jiepushe nao, uwaonye ubaya wa mambo waliyonayo na uwaambie maneno yenye kuwaathiri kwa njia ya kuwakemea.
Hatukumtumiliza Mtume yoyote, miongoni mwa Mitume wetu, isipokuwa ni afuatwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na uamuzi Wake. Na lau kwamba hawa waliojidhulumu nafsi zao kwa kutenda mabaya, walikujia, ewe Mtume, katika uhai wako, hali ya kutubia na kumuomba Mwenyezi Mungu Awasamehe madhambi yao, nawe ukawaombea msamaha, wangalimkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, ni Mwingi wa kurehemu.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anaapa kwa nafsi Yake tukufu, kwamba hawa hawataamini kikweli mpaka wakufanye wewe ni hakimu kwenye ugomvi unaotokea baina yao katika uhai wako na watake uamuzi wa Sunnah yako baada ya kufa kwako, kisha wasiingiwe na dhiki katika nafsi zao kwa matokeo ya hukumu yako, na wakwandame, pamoja na hivyo, kwa kukufuata kikamilifu. Kutoa uamuzi kulingana na aliyokuja nayo Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, kutoka kwenye Qur’ani na Sunnah katika kila jambo katika mambo ya kimaisha, pamoja na kuridhika na kusalimu amri, ni miongoni mwa uthabiti Imani
Na lau tuliwalazimisha wanafiki hawa, wenye kuhukumiana kwa taghut (sheria zisizokuwa za Mwenyezi Mungu), wauane wao kwa wao au watoke kwenye majumba yao, hawangalifuata amri hiyo isipokuwa wachache katika wao. Na lau kwamba wao walikubali nasaha walizonasihiwa, hilo lingalikuwa ni lenye kuwanufaisha na ni lenye kutia nguvu zaidi Imani yao,
na tungaliwapa thawabu kubwa kutoka kwetu, duniani na Akhera,
na tungaliwaongoza wao na kuwalekeza njia ya Mwenyezi Mungu iliyo ya sawa.
Na mwenye kukubali amri za Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na uongofu wa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, basi hao ni wale ambao wana utukufu wa mambo na vyeo. Wao watakuwa pamoja na wale waliopewa neema na Mwenyezi Mungu miongoni mwa Mitume na wakweli wa Imani, ambao kuamini kwao yaliyoletwa na Mitume kulikamilika kiitikadi, kimaneno na kivitendo na mashahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu na Waumini wema. Na wazuri wa marafiki wa mtu kuwa nao Peponi ni hao.
Vipewa vingi hivyo vinatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Anazijua hali za waja Wake na Anawajua wenye kustahiki thawabu nyingi kati yao kwa matendo mema waliyoyafanya.
Enyi mlioamini, kuweni na hadhari kwa kujiandaa na adui yenu, tokeni kupambana naye kundi baada ya kundi au mkiwa pamoja.
Hakika miongoni mwenu kuna watu wenye kujichelewesha kutoka kuenda kupambana na maadui kwa kuona uzito kufanya hivyo, na kufanya bidii kuwavunja moyo wengine kwa kusudi. Itokeapo mkapatikana kuuawa na kushindwa, huwa wakisema kwa furaha, «Mwenyezi Mungu Ametulinda kwa kutokuwako na wale waliopatikana na mambo ambayo nafsi zetu zinayachukia.» Na hilo la kutokuwa na nyinyi huwa likiwafurahisha.
Na itokeapo mkapata fadhila za Mola wenu na ngawira, wao wanasema, kwa uhasidi na majuto, kama kwamba hakukuwa na mapenzi ya waziwazi baina yenu, «Laiti mimi nilikuwa pamoja na wao nikafaulu kupata yale waliyoyapata: ya kuokoka, ushindi na ngawira.»
Basi na wapigane jihadi, katika njia ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na kulitukuza neno Lake, wale wanaouza uhai wa dunia kwa Akhera na thawabu zake. Na yoyote mwenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kidhati, akauawa au akashinda, basi tutampa malipo makubwa.
Na ni lipi linalowazuia, enyi Waumini, kupigana jihadi katika njia ya kuitetea dini ya Mwenyezi Mungu na kuwatetea waja Wake wanaodhalilishwa, miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto waliodhulumiwa, na ambao hawana ujanja wala njia ya kufanya isipokuwa ni kumtaka Mola wao Awnusuru wakimuomba kwa kusema, «Mola wetu, tutoe kwenye mji huu (Makkah) ambao watu wake wamejidhulumu nafsi zao kwa kukufuru na wamewadhulumu Waumini kwa kuwakera, na utuletee kutoka Kwako msimamizi wa kusimamia mambo yetu na mtetezi wa kututetea dhidi ya madhalimu»?
Wale walio wakweli katika Imani zao, kiitikadi na kivitendo, wanapigana jihadi katika njia ya kuitetea haki na watu wake, na wale waliokufuru wanapigana katika njia ya uonevu na uharibifu katika ardhi. Basi wapigeni vita watu wa ukafiri na ushirikina wanaomfuata Shetani na kutii amri yake. Hakika mipango ya Shetani anayowapangia wafuasi wake ni dhaifu.
Kwani hukujua, ewe Mtume, mambo ya wale walioambiwa, kabla ya kuruhusiwa kupigana jihadi, «Izuieni mikono yenu kupigana na maadui wenu washirikina. Na jilazimisheni kutekeleza yale mliyofaradhiwa ya Swala na Zaka»? Na Mwenyezi Mungu Alipowafaradhia kupigana, kulitokea kundi la watu katika wao iliobadilika hali yao wakawa wana kicho cha kuwaogopa watu kama vile wanavyomuogopa Mwenyezi Mungu au zaidi na wakawa wanaidhihirisha hofu kubwa iliyowaingia na kusema, «Ewe Mola wetu, kwa nini ulitufaradhia kupigana? Lau wewe ulitupa muhula mpaka muda mchache.» Wakitumai kupata starehe ya maisha ya ulimwengu. Waambie, ewe Mtume, Starehe ya ulimwengu ni chache, na Akhera na yaliyomo ndani ni makubwa zaidi na ni yenye kusalia zaidi kwa mwenye kuwa na uchamungu, akafanya aliyoamrishwa na akajiepusha na aliyokatazwa. Na Mola wako Hatamdhulumu yoyote, hata kama ni kadiri ya uzi unoakuwako kwenye mwanya wa koko ya tende.
Popote mliopo mtafikiwa na kifo, pawe ni mahali popote pale mnapokuwa, muda wenu ukikoma, hata kama mupo ndani ya ngome zilizoimarishwa zilizoko mbali na kiwanja cha mapambano na mapigano. Na wakipatikana na mambo ya kuwafurahisha ya starehe ya maisha haya (ya ulimwenguni), wanayanasibisha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kuwa Ndiye Aliyewapatia, na watokewapo na matukio wanayoyachukia, wanayanasibisha kwa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwa yamesababishwa na yeye kwa ujinga wao na kwa fikira zao kuwa yeye amewaletea nuhusi. Na hawakujua kwamba yote yanatokana na Mwenyezi Mungu Peke Yake, kwa uamuzi Wake na makadirio Yake. Basi kwa nini wao hawakaribii kuelewa maneno yoyote unayowaelezea?
Chochote kinachokupata, ewe binadamu, cha wema na neema, kinatoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Peke Yake, kwa ukarimu na hisani. Na chochote kinachokufika cha tabu na mashaka ni kwa sababu ya vitendo vyako vibaya na makosa na madhambi yaliyotendwa na mikono yako miwili. Na tumekutumiliza, ewe Mtume, kuwa ni Mtume kwa watu wote uwafikishie ujumbe wa Mola wako. Na inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya ukweli wa utume Wako.
Yoyote mwenye kumkubali Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na akafuata uongofu wake kivitendo, basi amemkubali Mwenyezi mungu Aliyetukuka na amefuata amri Yake. Na yoyote aliyekataa kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, basi hatukukutumiliza, ewe Mtume, kwa hawa wenye kukataa uwe ni mtunzi wa kuyadhibiti matendo yao na kuwahesabu kwa hayo. Hesabu yao ni juu yetu.
Na hawa wenye kukataa, wakiwa kwenye baraza ya Mtume, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, wanajidhihirisha kuwa wanamtii Mtume na kuyafuata yale aliyokuja nayo, na wakiwa mbali na yeye na wakaondoka kwenye baraza yake, linatoka kundi katika wao likapanga njama kinyume cha yale waliyoyadhihirisha ya kumtii. Na wao hawakujua kwamba Mwenyezi Mungu Anadhibiti hesabu ya yale wanayoyapanga na kwamba Yeye Atawalipa kwa hayo malipo kamili. Basi wape mgongo na usiwajali, kwani wao hawatakudhuru. Na tegemea kwa Mwenyezi Mungu, kwani yeye Peke Yake Ndiye Mwenye kukutosha kwa usimamizi na utetezi.
Kwani hawa hawaiangalii Qur’ani na haki iliyokuja nayo, kwa kuitaamali na kuizingatia, namna ilivyokuja kwa utaratibu uliopangika unaomfanya mtu awe na yakini kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu Peke Yake? Na lau yalikuwa yatoka kwa asiyekuwa Yeye, wangalipata ndani yake tafauti kubwa.
Na likiwajia, hawa ambao Imani haijakita ndani ya nyoyo zao, jambo ambalo inapasa lifichwe linalofungamana na usalama, ambao heri yake itarudi kwa Uislamu na Waislamu, au hofu, ambayo inatia babaiko ndani ya nyoyo zao, wanalitoa nje na kulitangaza kwa watu. Na lau wao walilipeleka, lile liliowajia, kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na kwa wenye ujuzi na ufahamu, wangaliujua uhakika wake wale wachambuzi kati yao. Na lau si Mwenyezi Mungu kuwafanyia wema na kuwaonea huruma, Mungalimfuata Shetani na mawazo mnayotiwa naye, isipokuwa wachache katika nyinyi.
Basi pigana jihadi, ewe Nabii, katika njia ya Mwenyezi Mungu na kulitukuza neno Lake. Hulazimishwi kitendo cha asiyekuwa wewe wala hutaadhibiwa kwacho. Na wahimize Waumini kupigana jihadi na uwavutie wafanye hivyo, kwani huenda Mwenyezi Mungu Akazuia, kwa ajili yako na wao, mashambulizi ya makafiri na nguvu zao. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ana nguvu nyingi zaidi na Ana adhabu kubwa zaidi kwa makafiri.
Mwenye kumshughulikia mwingine apate mema, atapata fungu la thawabu kwa huko kuingilila kwake kati. Na mwenye kujishughulisha juu ya kumdhuru mwingine, Atapata fungu la mzigo wa dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Shahidi na ni Mtunzi wa kila jambo.
Na Muislamu akiwatolea salamu, muitikieni kwa maneno mazuri zaidi na kwa furaha zaidi, au muitikieni salamu kama vile alivyowatolea. Na kila mmoja ana thawabu zake na malipo yake. Hakika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Mwneye kulipa kwa kila kitu (mnachokifanya).
Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Aliyepwekeka kwa uungu wa viumbe wote, Ndiye Atakayewakusanya nyinyi Siku ya Kiyama isiyokuwa na shaka, kwa kuhesabiwa na kulipwa. Na hakuna yoyote mkweli zaidi wa maneno anayoyatolea habari kuliko Mwenyezi Mungu.
Muna nini nyinyi, enyi Waumini, mumetafautiana makundi mawili kuhusu wanafiki: kundi linasema kwamba wapigwe vita na lingine halisemi hivyo? Na hali Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewatia kwenye ukafiri na upotevu kwa sababu ya vitendo vyao. Kwani mnataka kumpa uongofu yule ambaye Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ameuepusha moyo wake na dini Yake? Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Ameacha kumuafikia kufuata dini Yake na yale Aliyoyaamrisha, basi hana njia ya kufikia kwenye uongofu.
Hawa wanafiki waliwatamania nyinyi Waumini lau mlikanusha uhakika wa lile ambalo nyoyo zenu zimeliamini kama vile wao walivyolikanusha kwa nyoyo zao, ili muwe sawa na wao katika kukanusha. Basi msiwafanye ni wasafiwa wenu mpaka wagure katika njia ya Mwenyezi Mungu kama ushahidi wa ukweli wa Imani yao. Basi wakiyakataa yale waliyolinganiwa kwayo, washikeni popote waliopo na muwaue, wala msimfanye yoyote katika wao kuwa ni msimamizi badala ya Mwenyezi Mungu wala ni mwokozi ambaye mnataka awaokoe.
Lakini wale wanaofungamana na watu ambao baina yenu na wao pana ahadi na mapatano, msipigane nao. Pia msipigane na wale waliowajia na nyonyo zao zina dhiki, hawataki kupigana na nyinyi na pia hawataki kupigana na watu wao, wakawa hawako na nyinyi wala hawako na watu wao, basi msipigane nao. Na lau Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Alitaka, Angaliwapa nguvu juu yenu wakashirikiana na maadui zenu washirikina katika kupigana na nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Aliwaepusha nanyi kwa fadhila Zake na uwezo Wake. Basi wakiwaacha wasipigane na nyinyi na wakawafuata na kujisalimisha kwenu, hamna njia yoyote ya kupigana na wao.
Mtawapata watu wengine miongoni mwa wanafiki wanapenda kuzituliza nafsi zao upande wenu kwa kuwaonyesha kuwa wana Imani na pia wanapenda kujituliza upande wa watu wao walio makafiri kwa kuwaonyesha kuwa wao wako kwenye ukafiri. Kila wakirudishwa kwenye mahali pa ukafiri na makafiri, huingia kwenye hali mbaya zaidi. Basi hawa wasipojiepusha na nyinyi, wakajisalimisha kwenu kikamilifu na wakajizuia wasipigane na nyinyi, washikeni kwa nguvu na muwaue popote waliopo. Wale ndio ambao waliofikia, katika njia hii mbaya sana, kiasi cha kuwapambanua wao na wasiokuwa wao; wao ndio ambao tumewapa nyinyi hoja iliyo wazi ya kuwaua na kuwateka.
Si haki kwa yoyote aliyeamini kumfanyia uadui ndugu yake aliyeamini kwa kumuua bila haki isipokuwa afanye hilo kimakosa kwa kutokusudia. Na yoyote ambaye kosa hilo lilitokea kwake, basi ni juu yake aache huru shingo iliyoamini na atoe dia iliyokadiriwa kiwango chake kuwapa mawalii wa aliyeuawa, isipokuwa iwapo watamuachia kwa njia ya sadaka na watamsamehe. Iwapo muuliwa anamuamini Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na anaiamini haki aliyoteremshiwa Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na akawa ni katika ukoo wa watu makafiri ambao ni maadui wa Waislamu, basi ni juu ya muuaji aache huru shingo iliyoamini. Na iwapo muuliwa ni miongoni mwa watu ambao baina yenu na wao kuna ahadi na mapatano, basi ni juu ya yule aliyemuua, ili Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amkubalie toba yake, aache huru shingo iliyoamini; asipopata uwezo wa kuacha huru shingo iliyoamini, ni juu yake afunge miezi miwili yenye kufuatana. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, ni Mjuzi wa hakika ya mambo ya waja Wake, ni Mwenye hekima katika sheria Zake Alizowawekea.
Na mwenye kumfanyia uadui Muumini akamuua kwa kusudi pasi na haki, mwisho wake atakaoishia ni Jahanamu, hali ya kukaa milele humo, pamoja na kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kufukuzwa kwenye rehema Yake, iwapo Mwenyezi Mungu Atamlipa kwa kosa lake. Na Mwenyezi Mungu Amemuandalia adhabu kali zaidi kwa uhalifu huu mkubwa aliyoufanya. Lakini Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Atawasamehe na kuwafadhili wenye Imani kwa kutowapa malipo ya kukaa milele ndani ya Jahanamu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, mnapotoka kwenye ardhi hali ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuweni na uangalifu wa mnayoyafanya na mnayoyaacha. Na msimkanushie Imani yoyote ambaye imedhihiri kwake chochote katika alama za Uislamu na akawa hakuwapiga vita nyinyi, sababu pana uwezekano ya kuwa yeye ni Muumini anayeificha Imani yake. Msifanye hivyo kwa kutaka starehe za uhai wa kilimwengu kwani kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka pana nyongeza na vipewa vinavyowatosha. Na nyinyi mlikuwa hivyo mwanzo wa Uislamu, mkiificha Imani yenu kwa jamaa zenu washirikina, kisha Mwenyezi Mungu Akawaneemesha na Akawatukuza kwa Imani na kwa nguvu Alizowapa. Basi kuweni kwenye ubainifu na ujuzi katika mambo yenu. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa matendo yenu yote, ni Mwenye kuyaona mambo yenu ya ndani, na Atawalipa kwayo.
Wenye kusalia nyuma wakaacha kuhudhuria jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa wenye nyudhuru kati yao, hawalingani na wenye kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewafadhilisha wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa na Ameitukuza daraja yao Peponi kwa kiwango cha juu. Na Mwenyezi Mungu Amewaahidi wote: wenye kupigana jihadi kwa mali yao na kwa nafsi zao na wenye kukaa, miongoni mwa watu wenye nyudhuru, kwa kutoa kwao na kujitolea katika njia ya haki. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Amewafadhilisha wale wenye kupigana jihadi juu ya wenye kukaa kwa kuwapa thawabu nyingi.
Thawabu nyingi hizi ni daraja za juu, katika mabustani ya Pepo, zitokazo kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, walizopewa waja Wake maalumu wenye kupigana katika njia Yake, na msamaha wa madhambi yao na rehema kunjufu ambayo ndani yake wananeemeshwa. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa anayetubia Kwake na kurejea, ni Mwingi wa rehema kwa wenye kumtii, wenye kupigana jihadi katika njia Yake.
Hakika wale ambao Malaika waliwafisha na wao wako katika hali ya kujidhulumu wenyewe kwa kukaa katika nchi ya ukafiri na kuacha kuhama, Malaika watawaambia kwa njia ya kuwalaumu, «Mlikuwa katika nini kuhusu mambo ya Dini yenu?’ watasema, «Tulikuwa wanyonge nchini kwetu, tumelemewa kuweza kujiepushia dhuluma na maonevu.» Malaika watawaambia kwa njia ya kuwalaumu, «Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa kunjufu mkatoka kwenye ardhi yenu mkaenda ardhi nyingine ambapo mtaaminika na Dini yenu?» Basi hao makao yao ni Moto. Na haya ni makao mabaya ya mtu kuishilia.
Wataepushwa na mwisho huo wakongwe wanaume na wanawake na watoto ambao hawawezi kujiondolea udhalimu na uonevu na hawajui njia yoyote ya kuwaokoa wao na mateso.
Wanyonge hawa ndio wanaotarajiwa kupata msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, kwa kuwa Yeye Anaujua uhakika wa mambo yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Anawasamehe makosa yao na Anawafinikia na kuwasitiria.
Na yoyote mwenye kutoka kwenye ardhi ya ushirikina kwenda kwenye ardhi ya Uislamu kwa ajili ya kukimbia na dini Yake, akitaraji fadhila za Mola wake na akikusudia kuinusuru dini Yake, atapata katika ardhi mahali pa kuelekea ambapo ataneemeka, pawe ni sababu ya yeye kupata nguvu na maadui zake kuwa wanyonge, pamoja na kupata ukunjufu wa riziki na maisha. Na yoyote mwenye kutoka nyumbani kwake kwa lengo la kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye na kulitukuza neno la Mwenyezi Mungu kisha akapatikana na kifo kabla ya kufikia lengo lake, basi malipo ya kitendo chake yameshathibiti kwa Mwenyezi Mungu, kwa fadhila Zake na wema Wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, ni Mwingi wa huruma kwa waja Wake.
Na mnaposafiri, enyi Waumini, kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, hamuna makosa wala dhambi kukupunguza Swala, mkiogopa kufanyiwa uadui na makafiri mkiwa kwenye Swala. Safari nyinygi za Waislamu, katika mwanzo wa Uislamu, zilikuwa za kutisha. Na kupunguza Swala ni ruhusa iliyotolewa kwenye safari, katika hali ya amani au vitisho. Hakika makafiri ni wenye kudhihirisha uadui wao kwenu, basi jihadharini nao.
Na ukiwa, ewe Nabii, kwenye kiwanja cha vita na ukataka kuswalisha, basi kundi moja lisimame nawe ili kuswali, huku wakiwa wameshika silaha zao. Watu wa kundi hili wakiwa kwenye sijda, basi lije kundi lingine liwe nyuma yenu likiwa limeelekea upande wa adui wenu. Watu wa kundi la kwanza watimize rakaa ya pili na kutoa salamu. Kisha watu wa kundi lingine, ambalo bado halijaanza kuswali, waje kukufuata katika rakaa yao ya kwanza, kisha wamalize wenyewe rakaa yao ya pili. Na wajihadhari na adui wao na washike silaha zao. Kwani wenye kukanusha dini ya Mwenyezi Mungu wanatamani mughafilike na silaha zenu na vyombo vyenu wapate kuwashambulia kwa mara moja na kuwaua. Na hamuna makosa, kukiwa na mvua yenye kuwasumbua au mkawa wagonjwa, kuaacha silaha zenu pamoja na kuwa na hadhari. Hakika Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Amewaandalia wenye kuikanusha dini Yake adhabu ya kuwatweza na kuwadhalilisha.
Mtakapomaliza Swala, endeleeni kumtaja Mwenyezi Mungu katika hali zenu zote. Na hali ya kicho iondokapo, itekelezeni Swala kikamilifu, wala msiifanyie dharau, kwani Swala ni faradhi katika nyakati zijulikanazo katika Sheria.
Wala msiwe walegevu katika kuwatafuta maadui wenu na kupigana nao. Mkiwa mnahisi uchungu wa vita na matokeo yake, basi maadui wenu pia wanahisi uchungu wake zaidi, na pamoja na hivyo, hawakomi kupigana nanyi. Basi nyinyi ni aula kwa hilo kuliko wao, kwa kuwa nyinyi mnatarajia thawabu, nusura na kupewa nguvu, na wao hawatarajii hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa hali zenu zote, ni Mwenye hekima katika maamrisho Yake na uendeshaji mambo Wake.
Sisi tumekuteremshia Qur’ani, ewe Muhammad, iliyokusanya haki, ili utoe uamuzi baina ya watu wote kwa wahyi ambao Mwenyezi Mungu Amekuletea na Akakufahamisha. Basi usiwe ni mwenye kuwatetea wale wanaozifanyia hiana nafsi zao, kwa kuificha haki, kwa kuwa wamekudhihirishia maneno yaliyo kinyume na ukweli.
Na utake msamaha kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka katika hali zako zote. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe kwa wanaotarajia nyongeza za mema Yake na vipewa vya msamaha Wake, ni Mwingi wa huruma kwao.
Na usiwatetee wanaozifanyia hiana nafsi zao kwa kumuasi Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, Hampendi yule ambaye hiana yake imekuwa kubwa na dhambi zake zimekuwa nyingi.
Wao wanajificha na watu ili wasipate kuyaona matendo yao mabaya, wala hawajifichi na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka wala hawamuonei haya, ilhali Yeye, Mtukufu wa mambo, Yupo na wao kwa ujuzi Wake, Anawaona wanapopanga, kipindi cha usiku, maneno Asiyoridhika nayo. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ameyazunguka(kwa ujuzi Kwake) maneno yao yote na vitendo vyao vyote, hakuna kitu chochote chenye kufichika Kwake.
Haya nyinyi, enyi Waumini, mnatoa hoja za kuwatetea hawa mahaini wa nafsi zao katika huu uhai wa kilimwengu. Basi, ni nani mwenyemuhoji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuwatetea wao Siku ya kufufuliwa na kuhesabiwa? Au ni nani atakayekuwa wakili wao Siku ya Kiyama?
Na mwenye kufanya tendo baya au akajidhulumu nafsi yake kwa kufanya mambo yaliyo kinyume na hukumu ya Mwenyezi Mungu na sheria Yake, kisha akarudi kwa Mwenyezi Mungu kwa kujuta kwa aliyoyafanya akitaraji Amsamehe na dhambi zake Amsitirie, basi atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha na ni mwingi wa huruma kwake.
Na Mwenye kufanya dhambi kwa kusudi, hakika huwa akijidhuru nafsi yake peke yake. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mjuzi wa uhakika wa mambo ya waja Wake, ni Mwingi wa hekima katika hukumu Zake Azitowazo kwa waja Wake.
Na mwenye kufanya kosa bila kukusudia au akatenda dhambi kwa kusudia kisha akamsingizia, yale aliyoyafanya, mtu asiye na hatia, atakuwa amebeba urongo na dhambi zilizo wazi.
Na lau si Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kukuneemesha, ewe Mtume, kukurehemu kwa neema ya unabii na kukuhifadhi, kwa taufiki Yake, kwa wahyi Aliokuletea, wangaliazimia watu, miongoni mwa wale wanaozifanyia hiana nafsi zao, kukupotosha na njia ya haki. Na wao kwa kufanya hivyo, huwa hawampotoshi yoyote isipokuwa nafsi zao. Na hawawezi kukudhuru kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekuhifadhi, Amekuteremshia Qur’ani na Sunnah yenye kuifafanua, na Amekuongoza ukajua elimu ambayo hukuwa ukiijua hapo nyuma. Na fadhila za Mwenyezi Mungu Alizokuhusisha nazo ni jambo kubwa.
Hakuna manufaa katika mengi ya maneno ya watu ya siri baina yao, isipokuwa yawapo ni mazungumzo yenye kuita kwenye kufanya mema ya utoaji sadaka au maneno mazuri au kuleta upatanishi baina ya watu. Na mwenye kuyafanya mambo hayo, kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, akitarajia thawabu Zake, tutampa thawabu nyingi zilizo kunjufu.
Na mwenye kuenda kinyume na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye baada ya kubainikiwa na haki na akafuata njia isiyokuwa njia ya Waumini na haki ambayo wako nayo, basi tutamuacha na muelekeo wake, hatutamuongoza kwenye heri na tutamtia ndani ya Moto wa Jahanamu, akiteseka kwa joto lake. Ni mabaya yaliyoje marejeo haya kuwa ndio mwisho wa mtu!
Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hasamehe Akishirikishwa na Anasamehe madhambi yaliyo chini ya ushirikina kwa Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na mwenye kumfanyia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliye Mmoja, Aliye Pekee, mshirika yoyote, miongoni mwa waja Wake, atakuwa yuko mbali sana na haki.
Vile wanavyoviabudu washirikina badala ya Mwenyezi Mungu si chochote isipokuwa ni masanamu yasiyonufaisha wala kudhuru, na hawaabudu isipokuwa Shetani aliyemuasi Mwenyezi Mungu aliyefikia kiasi kikubwa cha kuharibika na kuharibu.
Mwenyezi Mungu Alimfukuza kwenye rehema Yake. Na Shetani Akasema, «Nitalichukua fungu maalumu la waja wako niwapoteze kimaneno na kivitendo.
«Na nitawaepusha na haki wenye kunifuata, nitawaahidi kwa urongo mambo wanayoyatamani, nitawaita wayakate na kuyapasua masikio ya wanyama-hoa kwa kuwapambia walifanye jambo hili la ubatili na nitawalingania wageuze umbo la Mwenyezi Mungu Alilowaumbia nalo katika tabia za kimaumbile na hali ya viumbe vile walivyo.» Na mwenye kukubali mwito wa Shetani na kumfanya yeye ndiye muokozi wake badala ya Mwenyezi Mungu, ameangamia maangamivu yaliyo wazi.
Shetani anawaahidi wafuasi wake ahadi za urongo na anawavutia kwa matamanio ya urongo yenye udanganyifu; ahadi zake kwao hazikuwa isipokuwa ni udanganyifu usio na ukweli wala dalili.
Hao marejeo yao ni Jahanamu; na hawatapata mapenyo wala mahali pa kukimbilia ili kuepukana nayo.
Na wale waliokuwa wakweli katika kumuamini kwao Mwenyezi Mungu, Aliyetukua, na wakafuatanisha Imani yao na matendo mema, basi Mwenyezi Mungu Atawaingiza, kwa ukarimu Wake, ndani ya mabustani ya Pepo ambayo chini ya majumba yake ya fahari na miti yake inapita mito, hali ya kukaa milele humo. Hiyo ni ahadi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ambaye Haendi kinyume na ahadi Yake. Na hapana yoyote aliye mkweli zaidi, katika neno lake na ahadi yake, kuliko Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Fadhila hizi kubwa hazipatikani kwa matamanio mnayoyatamani, enyi Waislamu, wala kwa matamanio ya Mayahudi na Wanaswara waliopewa Kitabu. Hakika zinapatikana kwa kumuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kikweli na kuyafanya vizuri matendo ya kumridhisha. Na yoyote mwenye kufanya tendo baya, atalipwa kwalo, na hatompata, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, mtegemewa mwenye kusimamia mambo yake wala msaidizi mwenye kumnusuru na kumuepushia adhabu mbaya.
Na mwenye kufanya matendo mema, awe ni mwanamume au mwanamke, hali ya kuwa anamuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na haki Aliyoiteremsha, basi hao Mwenyezi Mungu Atawaingiza Peponi, nyumba ya starahe ya daima, na hawatopunguziwa chochote katika thawabu za matendo yao, hata kama ni kadiri ya kitone kilichoko kwenye koko ya tende.
Hakuna yoyote aliye mwema wa dini kuliko yule aliyejisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake, kwa moyo wake na viungo vyake vyote, hali ya kuwa ni mwema wa maneno na vitendo, mwenye kufuata amri ya Mola wake, akawa amefuata mila ya Ibrāhīm na Sheria aliyoileta na amejiepusha na itikadi mbaya na sheria zilizo batili. Na Mwenyezi Mungu Alimteua Ibrāhīm, rehema na amani zimshukiye, na Akamfanya ni msafiwa Wake miongoni mwa viumbe Wake. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya al-khullah (ubui) kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, nao ni daraja ya juu kabisa ya mapenzi na uteuzi.
Ni vya Mwenyezi Mungu viumbe vyote vilivyoko ulimwenguni. Hivyo ni milki Yake, Aliyetukuka, Peke Yake. Na Mwenyezi Mungu Amekizunguka kila kitu, hakuna kitu chochote, katika mambo ya waja Wake, chenye kufichika Kwake.
Watu wanakutaka, ewe Nabii, uwaelezee mambo yaliyowatatiza kuyafahamu yanayowahusu wanawake na hukumu zao. Sema, «Mwenyezi Mungu Anawafafanulia kuhusu mambo yao na yale mnayosomewa ndani ya Qur’ani kuhusu mayatima wa kike ambao hamuwapi mafungu yao waliyoandikiwa na Mwenyezi Mungu ya mahari, mirathi na haki nyiginezo, na mkawa mnapenda kuwaoa au hamuna hamu ya kuwaoa. Na pia Mwenyezi Mungu Anawafafanulia kuhusu mambo ya madhaifu miongoni mwa watoto na ulazima wa kuwasimamia mayatima kwa uadilifu na kuacha kuwafanyia maonevu kwa kuwanyima haki zao. Na wema wowote mnaoufanya, Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaujua, hakuna kinachofichika Kwake kuhuso huo na mwengineo.
Na mwanamke akijua kuwa mumewe ana majivuno na madharau na hashughuliki naye, si makosa kwa wao wawili kusikilizana kwa namana ya kuwaridhisha wao wawili kuhusu kugawa siku na matumizi. Kwani masikilizano ni bora zaidi na ni afadhali zaidi. Na nafsi zimeumbwa zikiwa na tabia ya pupa na ubahili, kama kwamba ubahili upo mbele ya hizo nafsi, hauepukani nazo. Na mkiamiliana na wake wenu vizuri na mkamcha Mwenyezi Mungu juu yao, basi Mwenyezi Mungu ni Mjuzi sana wa mnayoyafanya, katika hayo na mengineyo, hakuna kinachofichika Kwake, na Atawalipa kwa hayo.
Na hamtaweza, enyi wanaume, kuhakikisha uadilifu kamili wa mapenzi na muelekeo wa moyo kati ya wanawake, namna mtakavyofanya bidii juu ya hilo. Basi msimpe mgongo, yule msiokuwa na haja naye, kabisa-kabisa mkamuacha akawa ni kama mwanamke ambaye hana mume wala hakutalikiwa, mkaja mkapata madhambi. Na mkizitengeneza amali zenu mkafanya uadilifu katika ugawaji wenu baina ya wake zenu na mkamchunga Mwenyezi Mungu mkamuogopa juu yao, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwingi wa huruma kwao.
Na ukitokea utengano baina ya mwanamume na mkewe, Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika, atamtosheleza kila mmoja kati yao kwa fadhila Zake na ukunjufu wa neema Zake. Kwani Yeye, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu na Aliyetukuka, ni Mkunjufu wa fadhila na neema, ni Mwingi wa hekima katika hukumu Zake Anazozipitisha kwa waja Wake.
Ni milki ya Mwenyezi Mungu vilivyoko kwenye mbingu na vilivyoko kwenye ardhi na vilivyoko baina ya hivyo viwili. Na tuliwausia wale waliopewa Vitabu kabla yenu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, na tukawausia nyinyi pia, enyi ummah wa Muhammad, mumche Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na msimame kutekeleza amri Zake na kuepuka makatazo Yake, na tukawaelezea kwamba nyinyi mkiukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na sheria Zake, basi Mwenyezi Mungu Hawahitajii nyinyi, kwa kuwa vyote vilivyoko kwenye mbingu na vilivyoko kwenye ardhi ni Vyake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha kutowahitjia viumbe Wake, ni Mwingi wa kuhimidiwa katika sifa Zake na vitendo Vyake.
Ni milki ya Mwenyezi Mungu viumbe vilivyoko katika ulimwengu huu. Na inatosha kuwa Yeye, Aliyetakasika na kila sifa pungufu, ni Msimamizi na Mtunzi wa mambo ya viumbe Vyake.
Akitaka Mwenyezi Mungu Atawaangamiza, enyi watu, na awalete watu wengine wasiokuwa nyinyi. Na Mwenyezi Mungu kwa hili ni Muweza.
Mwenye kuwa na hamu miongoni mwenu, enyi watu, ya kupata malipo ya duniani na akaipa mgongo Akhera, basi mbele ya Mwenyezi Mungu kuna malipo ya dunia na Akhera. Basi na atake kutoka kwa Mwenyezi Mungu , Peke Yake, wema wa dunia na Akhera, kwani Yeye Ndiye Anayevimiliki hivyo viwili. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, ni Mwenye kuziona nia zao na vitendo vyao, na Atawalipa kwa hayo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, kuweni ni wasimamizi wa uadilifu, wenye kutekeleza ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hata kama ni kinyume na maslahi ya nafsi zenu au baba zenu au mama zenu au jamaa zenu, namna atakavyokuwa yule mwenye kutolewa ushahidi awe ni tajiri au masikini, kwani Mwenyezi Mungu ni bora kwa wao wawili kuliko nyinyi, na ni Mjuzi zaidi wa mambo ambayo yana maslahi kwao. matamanio na mapendeleo yasiwapelekee nyinyi kuacha uadilifu. Na mkiupotoa ushahidi, kwa ndimi zenu, mkautoa kwa namna isiyokuwa ya kweli, au mkaupuuza kwa kuacha kuutekeleza au kwa kuuficha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa matendo yenu ya ndani na Atawalipa kwayo.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, endeleeni kwenye msimamo mlionao wa kumuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Imani thabiti, kumuamini Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukiye, na kuwatii wao wawili, kuiamini Qur’ani Aliyoiteremsha kwake na kuviamini vitabu vyote Alivyoviteremsha Mwenyezi Mungu kwa Mitume. Na mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Malaika Wake waliotukuzwa, vitabu Vyake Alivyoviteremsha ili kuwaongoza viumbe Wake, Mitume Wake Aliowachagua kufikisha ujumbe Wake na Siku ya Mwisho ambayo watu katika siku hiyo watafufuka baada ya kufa ili waorodheshwe na wahesabiwe, atakuwa ametoka kwenye Dini na atakuwa yuko mbali sana na njia ya haki.
Hakika wale walioingia kwenye Imani, kisha wakarudi kwenye ukafiri, kisha wakarejea kwenye Imani, kisha wakarudi tena kwenye ukafiri, kisha wakavama na kuendelea kwenye ukafiri, Mwenyezi Mungu Hatakuwa ni Mwenye kuwasamehe wala kuwaonesha njia ya uongofu ambayo kwayo wataokoka na mwisho mbaya.
Wape bishara, ewe Mtume, wanafiki - nao ni wale wanaodhihirisha Imani na kuficha ukafiri- kuwa wao watakuwa na adhabu yenye kuumiza.
Ambao wanawategemea makafiri na kuwafanya ni wasaidizi wao, na wanaacha kuwapenda Waumini na kuwategemea, wala hawana haja ya mapenzi yao. Kwani wanatafuta, kwa hilo kuokolewa na kupata hifadhi kwa makafiri? Hili wao hawalimiliki. Kwani uokozi, enzi na nguvu, vyote ni vya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Peke Yake.
Mola wenu Amewateremshia, enyi Waumini, katika Kitabu Chake kwamba mkisikia aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa shere, basi msikae pamoja na wakanushaji hao wanaofanya shere, isipokuwa wakiingia kwenye mazungumzo yasiokuwa mazungumzo ya kukanusha na kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Nyinyi mkikaa nao, na wao wako katika hali hiyo, mtakuwa ni kama wao, kwa kuwa nyinyi mmeridhika na ukafiri wao na uchezaji shere wao. Na mwenye kuridhika na maasia ni kama mwenye kuyafanya. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye Atawakusanya wanafiki na makafiri wote ndani ya Moto wa Jahanamu ambapo humo watakumbana na ukali wa adhabu.
Wanafiki ndio wale wanaongojea yatakayowashukia nyinyi, enyi Waumini, ya misukosuko na vita. Iwapo Mwenyezi Mungu Amewaneemesha kwa fadhila Zake, Akawanusuru juu ya adui yenu na mkapata ngawira, wao wanasema, «Kwani hatukuwa na nyinyi tukiwasaidia?» Na iwapo wakanushaji wa Dini hii wamepata sehemu ya ushindi na ngawira, wao wanasema kuwaambia, «Kwani hatukuwasaidia nyinyi kwa kile tulichowapatia na kuwahami na Waumini?» Basi Mwenyezi Mungu Ataamua baina yao na nyinyi Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu Hatawapa makafiri njia ya kuwashinda waja Wake wema. Basi mwisho mwema ni wa wacha- Mungu, duniani na Akhera.
Hakika mbinu ya wanafiki hawa ni kumhadaa Mwenyezi Mungu kwa Imani wanaojionyesha nayo na ukafiri wanaouficha, kwa kudhani kuwa mbinu yao itafichamana kwa Mwenyezi Mungu, na hali ni kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Anayewahadaa na ni Mwenye kuwalipa malipo yanayofanana na vitendo vyao. Wanafiki hawa wanaposimama kutekeleza Swala, wanasimama kufanya hivyo kwa uvivu, wanakusudia, kwa kuswali kwao, kuonekena na kusikika. Na wao hawamtaji Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, isipokuwa kumtaja kwa uchache.
Hali ya hawa wanafiki ni kutokuwa na msimamo, kuchangayikiwa na kubabaika, hawathibiti kwenye hali moja, hawako pamoja na Waumini wala hawako pamoja na makafiri. Na yoyote ambaye Mwenyezi Mungu Ameupotoa moyo wake usimuamini na usishikamane na uongofu Wake, huyo hutampatia njia ya kufikia uongofu na yakini.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake! Msiwapende na kuwategemea wenye kukanusha Dini ya Mwenyezi Mungu na mkaacha kuwapenda kuwategemea Waumini na kuwapenda. Je, mnataka kwa kuwapenda maadui wenu kumpa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, hoja iliyo wazi kuwa nyinyi si wakweli katika Imani yenu?
Hakika wanafiki watakuwa kwenye mahandaki ya chini kwa chini ya Moto Siku ya Kiyama. Na hutawapatia wao, ewe Mtume, yoyote wa kuwaokoa atakayewakinga wao wasifikie mwisho huu mbaya.
Isipokuwa wale ambao walirejea kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakatubia Kwake, wakazirekebisha hali zao zilizoharibika za ndani na za nje, wakawategemea waja Wake Waumini, wakashikamana na dini ya Mwenyezi Mungu na wakamtakasia Yeye, Aliyetakasika kutokana na kila sifa ya upungufu. Hao ni pamoja na Waumini duniani na Akhera; na Mwenyezi Mungu Atawapa Waumini malipo kubwa.
Mwenyezi Mungu hatawapa adhabu iwapo nyinyi mumefanya amali njema na mumemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake. Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Hana haja na yoyote asiyekuwa Yeye. Yeye Atawaadhibu waja kwa makosa yao. Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarudishia shukrani[1] waja Wake kwa utiifu wao Kwake, ni Mjuzi wa kila kitu.
____________________
[1]Maana ya Shākir ikinasibishwa na Mwenyezi Mungu ni «Analipa thawabu nyingi kwa mema machache». Ang. Tafsiri ya Ibn Kathīr Sura:2, aya:158.
Hapendi Mwenyezi Mungu kwa yoyote adhihirishe neno ovu. Lakini yaruhusiwa kwa aliyedhulumiwa amtaje aliyemdhulumu kwa uovu alionao, ili akibainishe alichodhulumiwa nacho. Na daima Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyasikia mnayoyadhihirisha na ni Mwenye kuyajua mnayoyaficha kati ya hayo.
Amehimiza Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwamba watu wasamehe, na Akaweka msingi wa jambo hilo kwa kuwa Muumini, ima aidhihirishe kheri au aifiche. Na vilevile katika kukosewa, ima adhihirishe kuwa amekosewa katika hali ya kutafuta haki yake kwa aliyemkosea au asamehe na apuuze. Na kusamehe ni bora. Kwani miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu ni kuwasamehe waja Wake pamoja na uwezo Wake juu yao.
Hakika wanaomkanusha Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, kati ya Mayahudi na Wanaswara, na kutaka kutenganisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume Wake, kwa kumuamini kwao Mwenyezi Mungu na kuwakanusha Mitume Wake Aliowatuma kwa viumbe Wake, au wautambue ukweli wa baadhi ya Mitume na kuacha kuwatambua wengine na wadai kwamba baadhi yao wamemzulia Mola wao urongo na wanataka kujifanyia njia ya kuelekea kwenye upotofu waliouanzisha na uzushi waliouzua.
Hao ndio wenye ukafiri wa hakika usiokuwa na shaka. Na tumewaandalia makafiri adhabu itakayowadhili na kuwatweza.
Na wale walioukubali upweke wa Mwenyezi Mungu na wakautambua unabii wa wajumbe Wake wote na wasimbague yoyote kati yao na wakaifuata kivitendo sheria ya Mwenyezi Mungu, hao Atawapa malipo yao na thawabu zao kwa kumuamini kwao Yeye na Mitume Wake. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye huruma kwao.
Wanakutaka Mayahudi, ewe Mtume, uwaonyeshe miujiza mfano wa miujiza ya Mūsā iwe ni ushahidi kwako kuwa ni mkweli, nao ni uwateremshie kurasa zitokazo kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa zimeandikwa, kama vile Mūsā alivyoleta mbao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Usione ajabu, ewe Mtume, kwani wakale wao walimtaka Mūsā, amani imshukie, awaletee makubwa zaidi. Walimtaka Awaonyeshe Mwenyezi Mungu waziwazi, hapo wakateremshiwa moto uliowaua kwa sababu ya kuzidhulumu nafsi zao walipolitaka jambo ambalo si haki yao. Na baada ya Mwenyezi Mungu kuwahuisha, baada ya kufa kwao, na wakaishuhudia miujiza iliyo waziwazi, kutoka kwa Mtume Mūsā, inayopinga katakata ushirikina, waliabuduu kigombe badala ya Mwenyezi Mungu. Kisha tuliwasamehe kosa lao la kuabudu ndama kwa sababu ya kutubia kwao na tukampa Mūsā hoja kubwa zilizotilia nguvu ukweli wa utume wake
Na tukaliinua juu ya vichwa vyao jabali la Tūr walipokataa kujilazimisha na ahadi iliyotiliwa mkazo waliyoitoa ya kuwa watazitumia hukumu za Taurati. Na tukawaamrisha waingie lango la Bait al-Maqdis hali ya kusujudu , nao wakaingia wakijikokota kwa matako yao. Na tukawaamrisha wasifanye uadui kwa kuvua siku ya Jumamosi, wakafanya uadui hivyo hivyo na wakavua. Na tukachukua kutoka kwao ahadi ya mkazo, pia waliivunja hivyo hivyo.
Tukawalaani kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi, kukanusha kwao aya za Mwenyezi Mungu zinazojulisha ukweli wa Mitume Wake, kuua kwao Manabii wa Mwenyezi Mungu kwa maonevu na uadui na kwa kusema kwao, «Nyoyo zetu zimezibwa kwa vifiniko, hatuyafahamu uyasemayo.» Bali Mwenyezi Mungu ameziziba kwa sababu ya ukafiri wao. Kwa hivyo, hawataamini isipokuwa Imani isiyowafaa.
Na vile vile tuliwalaani kwa sababu ya ukafiri wao na kumzulia kwao Maryam urongo kwa yale waliyomsingizia nayo ya uzinifu na hali yeye yupo mabali na hilo.
Na- pia tuliwalaani- kwa sababu ya neno lao, kwa njia ya kukejeli na shere, «Sisi tumemuua Al- Masīh,, ‘Īsā mwana wa Maryam, mjumbe wa Mwenyezi Mungu.» Na wala wao hawakumuua ‘Īsā wala hawakumsulubu, bali walimsulubu mwanamume aliyefanana naye kwa kudhani kwao kuwa yeye ndiye ‘Īsā. Na yoyote aliyedai kwamba walimuua, miongoni mwa Mayahudi na pia wale waliomsalimisha kwao, miongoni mwaWanaswara, wote hao wako kwenye shaka na kuchanganyikiwa; hawana ujuzi wowote isipokua ni kufuata dhana tu, na wala hawana yakini ya kuwa walimuua, bali wana shaka nalo hilo na wanalidhania tu.
Bali Mwenyezi Mungu Alimpaisha ‘Īsā kwa mwili wake na roho yake akiwa hai na Alimuokoa na wale waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika ufalme Wake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake na mapitisho Yake.
Na kwa hakika hatasalia yoyote, kati ya wale waliopewa Kitabu, baada ya kuteremka ‘Īsā zama za mwisho, isipokuwa atamuamini Nabii ‘Īsā kabla ya kufa kwake, amani imshukie, na siku ya Kiyama Nabii ‘Īsā atakuwa ni shahidi kwamba waliomkanusha walikuwa warongo na waliomuamini walikuwa wakweli.
Na kwa sababu ya dhuluma ya Mayahudi kwa madhambi makubwa waliyoyafanya, Mwenyezi Mungu Aliwaharamishia vyakula vizuri vilivyokuwa halali kwao, na pia kwa sababu ya kuzizuia nafsi zao na kuwazuia wengine wao wasiifuate dini ya Mwenyezi Mungu iliyo ya sawa.
Na kwa sababu ya kutumia kwao riba ambayo walikatazwa wasitumie na kujihalalishia kwao mali za watu pasi na haki. Na tumewatayarishia waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake adhabu iumizayo huko Akhera.
Lakini wale waliojikita katika elimu katika hukumu za Mwenyezi Mungu kati ya Mayahudi na wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wanayaamini yale Aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kwako, ewe Mtume, nayo ni Qur’ani, na yale Aliyoyateremsha kwa Mitume kabla yako, kama Taurati na Injili, wanatekeleza Swala kwa nyakati zake, wanatoa Zaka za mali zao na wanamuamini Mwenyezi Mungu, kufufuliwa na malipo. Hao Mwenyezi Mungu Atawapa thawabu kubwa, nayo ni Pepo.
Hakika sisi tumekuletea wahyi, ewe Mtume, ili ufikishe ujumbe kama tulivyomletea wahyi Nūḥ na Manabii wengine baada yake. Na tumewapelekea wahyi Ibrāhīm, Ismā’īl, Isḥāq, Ya‘qūb na Asbāṭ, nao ni Manabii waliokuwa katika makabila kumi na mbili ya wana wa Isrāīl wanaotokana na kizazi cha Ya’qūb, na pia ‘Īsā, Ayyūb, Yūnus, Hārūn na Sulaimān na tukampa Dāwūd Zaburi, nacho ni kitabu na kurasa zilizoandikwa.
Na tumewatumiliza Mitume ambao tumekuelezea habari zao katika Qur’ani, kabla ya aya hii, na Mitume wengine ambao hatukukuelezea hahabari zao kwa hekima tuliyoikusudia.Na Mwenyezi Mungu Alisema na Mūsā waziwazi ili kumtukuza kwa sifa hii. Katika aya hii tukufu kuna uthibitisho wa sifa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ya kusema kama inavyolingana na utukufu Wake, na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Alisema na Nabii Wake Mūsā, amani imshukie, kikweli bila ya mtu wa kati (baina yao).
Nimweatuma wajumbe kwa viumbe wangu wakatoe habari njema ya malipo yangu mema na waonye juu ya adhabu yangu, ili wanadamu wasiwe na hoja watakayoifanya ni kisingizio cha udhuru baada ya kutumiliza Mitume. Na daima Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji mambo Wake.
Iwapo Mayahudi na wengineo watakukanusha, ewe Mtume, hakika Mwenyezi Mungu Anashuhudia kuwa wewe ni Mtume Wake Aliyemteremshia Qur’ani tukufu; Ameiteremsha kwa ujuzi Wake. Na vilevile Malaika wanashuhudia ukweli wa wahyi uliyoletewa. Na ushahidi wa Mwenyezi Mungu Peke Yake unatosha.
Hakika wale walioupinga unabii wako na wakawazuia watu kuufuata Uislamu, wamekuwa mbali kabisa na njia ya haki.
Hakika wale waliomkanusha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakadhulumu kwa kuendelea kwao na ukafiri, Mwenyezi Mungu Hatakuwa ni Mwenye kuwasamehe madhambi yao wala kuwaongoza njia ya kuwaokoa.
Isipokuwa njia ya moto wa Jahanamu, hali ya kuwa wao ni wenye kukaa humo milele. Na hilo kwa Mwenyezi Mungu ni jepesi; hivyo basi, hakuna chenye kumshinda.
Enyi watu, amewajia nyinyi Mjumbe wetu,Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na Uislamu, Dini ya haki, kutoka kwa Mola wenu, basi ikubalini na muifuate, kwani kuiyamini ni bora kwenu. Na iwapo mtaendelea na ukafiri wenu, basi Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Hana haja nanyi, na pia Hana haja ya kuamini kwenu, kwa kuwa Yeye ni Mmiliki wa vilivyo mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mno wa maneno yenu na vitendo vyenu, ni Mwingi wa hekima katika uwekaji Sheria Wake na amri Zake. Na iwapo mbingu na ardhi zimemnenyekea Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika kuwa na kukadiriwa, kama viumbe vyingine vyote vilivyomnyenyekea, basi ni bora kwenu mumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, muiamini Qur’ani Aliyomteramshia na muifuate Dini hiyo kisheria hadi ulimwengu wote uwe ni wenye kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kimpango uliokadiriwa na kisheria. Katika aya hii kuna dalili ya kuwa ujumbe wa Nabii wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, unakusanya ulimwengu wote.
Enyi watu wa Injili! Msiikiuke itikadi ya haki katika dini yenu, na msiseme kuhusu Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Hivyo basi, msimfanye kuwa Ana mke wala msimfanye kuwa ana mwana; hakika Al-Masīḥ ‘Īsā, mwana wa Maryam, ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu Amemtummliza kwa haki na Amemuumba kwa neno ambalo Amemtuma nalo Jibrili alipeleke kwa Maryam, nalo ni neno Lake, «Kuwa!» na ikawa. Nalo ni mvivio kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, aliouvivia Jibrili kwa amri ya Mola Wake. Kwa hivyo , aminini kwamba Mwenyezi Mungu ni Mmoja na mjisalimishe Kwake na muwaamini Mitume Wake katika yale waliowaletea kutoka kwa Mwenyezi Mungu na myafuate kivitendo. Wala msimfanye ‘Īsā na mamake kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Komeni na matamshi hayo! Itakuwa bora kwenu kuliko hayo mliyonayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola Mmoja, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake. Vilivyoko mbinguni na ardhini ni milki Yake. Basi vipi Atakuwa na mke au mtoto kati ya hivyo? Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu Ndiye Msimamizi wa kupanga mambo ya viumbe Wake na kuendesha maisha yao. Hivyo basi, mtegemeeni, Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Mwenye kuwatosha.
Kabisa hatadinda wala hatakataa Al- Masīḥ kuwa ni mja wa Mwenyezi Mungu. Vilevile hawatadinda Malaika waliokaribishwa kukubali kuwa wao ni waja wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na yoyote mwenye kudinda kufuata kikamilifu na kunyenyekea na akafanya kiburi, Basi hao Mwenyezi Mungu Atawafufua Awakusanye Kwake Siku ya Kiyama, Atoe uamuzi baina yao kwa hukumu Yake ya uadilifu na Amlipe kila mmoja kwa kile anachostahili.
Ama wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu, kiitikadi, kimaneno na kivitendo, wakasimama imara kufuata sheria Zake, basi Yeye Atawalipa thawabu za vitendo vyao na Atawaongeza kutokana na fadhila Zake. Na ama waliokataa kumtii Mwenyezi Mungu na wakafanya kiburi kwa kutojidhalilisha Kwake, Atawaadhibu adhabu iumizayo. Hawatampata wa kuwasimamia atakayewaokoa na adhabu Yake, wala wa kuwanusuru ambaye atawanusuru badala ya Mwenyezi Mungu,
Enyi watu, kwa hakika imekuja kwenu ushahidi kutoka kwa Mola wenu, nao ni Mtume wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo miongoni mwa maelezo yaliyo waziwazi na hoja za yakini, kubwa ya hizo ni Qur’ani tukufu, zenye kutolea ushahidi ukweli wa unabii wake na utume wake wa mwisho; na tumewateremshia Qur’ani ikiwa ni uongofu na ni nuru yenye kufafanua mambo waziwazi.
Ama wale waliomuamini Mwenyezi Mungu kiitikadi, kimaneno na kivitendo, na wakashikamana na Nuru ambayo waliteremshiwa, Atawaingiza Peponi ikiwa ni rehema na fadhila kutoka Kwake na Atawaafikia kufuata njia iliolingana sawa, itakayopelekea kwenye mabustani ya Peponi.
Wanakuuliza, ewe Nabii, kuhusu hukumu ya urithi wa kalalah, naye ni aliyekufa akiwa hana mwana wala mzazi. Sema, «Mwenyezi Mungu Anawafafanulia hukumu yake, kwamba yoyote atakayefariki na akawa hana mwana wala mzazi, na akawa ana dada yake wa kwa baba na mama au wa kwa baba tu. Basi dada huyo atapata nusu ya mali yaliyoachwa na aliyefariki. Na iwapo aliyefariki ni huyo dada, na akawa hana mwana wala mzazi, basi kaka yake, wa kwa baba na mama au wa kwa baba, atarithi mali yote. Na iwapo yule aliyefariki, bila ya kuacha mwana wala mzazi, ana dada zake wawili, basi wao watapata theluthi mbili ya mali aliyoyaacha. Na watakapokusanyika pamoja kwenye urithi ndugu wa kiume na wa kike wasiokuwa wa kwa mama basi kila mmoja, katika ndugu wa kiume, atapata mfano wa mafungu mawili ya mwanamke. Mwenyezi Mungu Anawafafanulia namna ya kugawanya urithi na hukumu ya aliyefariki bila ya kuacha mwana wala mzazi, ili msije mkapotea kwenye njia ya haki kuhusu hukumu ya mambo ya uraihi. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzu wa mwisho wa mambo na yaliyo na heri kwa waja Wake.