ﮙ
ترجمة معاني سورة الرعد
باللغة السواحلية من كتاب الترجمة السواحلية - عبد الله محمد وناصر خميس
.
ﰡ
Alif, Lām, Mīm. Maelezo kuhusu herufi ziliokatwa na kutengwa yametangulia mwanzo wa sura ya Al-Baqarah. Hizi ni aya za Qur’ani zenye cheo kitukufu. Na Qur’ani hii uliyoteremshiwa, ewe Mtume, ndiyo haki, na sivyo kama vile wanavyosema washirikina kwamba wewe mwenyewe ndio uliyoileta. Pamoja na hili, wengi wa watu hawaiamini wala hawaifuati kivitendo.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Ndiye Aliyeziinua mbingu saba kwa uweza Wake bila ya nguzo, kama vile ambavyo mnaziona, kisha akalingana - yaani akawa juu - ya Arshi kulingana kunakonasibiana na utukufu Wake na ukubwa Wake, na Akalidhalilisha jua na mwezi kwa manufaa ya waja, kila moja wapo ya viwili hivyo kinazunguka kwenye anga lake mpaka Siku ya Kiyama. Anapekesha, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, mambo ya ulimwenguni na Akhera, Anawafafanulia dalili zenye kuonyesha uweza Wake na kwamba yeye hakuna mungu isipokuwa Yeye, ili muwe na Imani ya kikweli kwa Mwenyezi Mungu na mjiyakinishe kurudi Kwake, mpate kuamini ahadi Yake ya thawabu na adhabu na mumtakasiye ibada Peke Yake.
Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Ambaye Aliifanya ardhi iwe kunjufu iliyonyoshwa, Akaitayarisha kwa maisha yenu, Akayaweka humo majabali yenye kuithibitisha na mito ya nyinyi kunywa na kunufaika, Akaweka humo aina mbili za kila matunda, katika hayo kukawa kuna meupe na meusi, tamu na kali, na Akaufanya usiku ufinike mchana kwa giza lake. Hakika katika hayo yote pana mazingatio kwa wenye kuyafikiri wakawaidhika.
Na kwenye ardhi kuna sehemu zinaopakana, kati ya hizo kuna zilizo nzuri zenye kuota mimea inayowafaa watu na kati ya hizo kuna kavu zenye chumvi zisizootesha chochote. Na katika ardhi nzuri kuna mashamba ya zabibu, na Amejaalia humo aina tafauti za makulima na mitende iliyokusanyika mahali pamoja na isiyokusanyika hapo, vyote hivyo viko katika mchanga mmoja na vinakunywa maji mamoja, isipokuwa vinatafautiana katika matunda, ukubwa, utamu na mengineyo: hili ni tamu na hili ni kali, na mengine ni bora kuliko mengine katika kula. Katika hilo kuna dalili kwa mwenye moyo unaoyaelewa maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo Yake.
Ukiona ajabu , ewe Mtume, ya makafiri kutoamini baada ya dalili hizi, basi ajabu kubwa zaidi ni kusema kwao, «Je, tukifa na tukawa mchanga tutafufuliwa upya?» Hao ndio wenye kumkanusha Mola wao Aliyewafanya waweko kutoka kwenye hali ya kutokuwako. Na hao kutakuwa na minyororo kwenye shingo zao Siku ya Kiyama. Na hao wataingia Motoni na hawatatoka kabisa.
Na wale wakanushaji wanakuharakisha uwaletee adhabu ambayo mimi sikuwaharakishia kabla ya kuamini Imani ambayo kwayo kunatarajiwa usalama na matendo mema. Na yashapita mateso ya wakanushaji kabla yao, kwa nini wao hawawi ni wenye kuwaidhika na wao? Hakika Mola wako ni Mwenye msamaha wa dhambi za watu waliotubia dhambi zao juu ya udhalimu wao, Atawafungulia mlango wa msamaha na Atawaita waingie, na huku wao wanazidhulumu nafsi zao kwa kumuasi Mola wao. Hakika Mola Wako ni Mkali wa mateso juu ya walioendelea kwenye ukafiri, upotevu na kumuasi Mwenyezi Mungu.
Na makafiri wa Makkah wanasema, «Basi si ajiwe na miujiza inayoonekana kama fimbo ya Mūsā na ngamia wa Ṣāliḥ.» Na hilo haliko kwenye mkono wako, ewe Mtume; hukuwa wewe isipokuwa ni mwenye kuwafikishia na ni mwenye kuwatisha adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na kila ummah una mjumbe wa kuwaongoza kwenye njia ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Mwenyezi Mungu Aliyetukuka Anakijua alichokibeba kila mwanamke ndani ya tumbo lake: ni cha kiume au ni cha kike, ni chema au ni kibaya. Na anakijua kile ambacho zao zinakipunguza kikazaliwa kimekufa au kabla ya kutimia myezi tisa au kikapita muda huo. Na kila kitu, chenye kuzidi au kupungua, kimekadiriwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kipimo kisichopitisha kiasi.
Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyofichika na macho na yanayoonekana, Aliye Mkubwa wa dhati, majina na sifa , Aliye juu ya viumbe Vyake vyote kwa dhati Yake, uweza Wake na kutendesha nguvu Kwake.
Analingana, katika ujuzi Wake Aliyetukuka, yule anayesirisha maneno, katika nyinyi, na anayedhihirisha. Na analingana Kwake yule anayefanya matendo yake kwa siri ndani ya giza la usiku na yule mwenye kuyafanya waziwazi kwenye mwangaza wa mchana.
Na Mwenyezi Mungu Anayetukuka Ana Malaika wanaompitia binadamu, kundi baada ya kundi, mbele yake na nyuma yake, wanamhifadhi kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuyadhibiti yanayofanywa na yeye, mema au maovu. Hakika Mwenyezi Mungu , Aliyetakata na kutukuka, Hageuzi neema aliyowaneemesha watu mpaka wakiwa wao watayageuza yale waliyoamrishwa na Mola wao na wakamuasi. Na Mwenyezi Mungu Akiwatakia watu mitihani basi hakuna namna ya kuyakimbia, na hawana wao asiyekuwa Mwenyezi Mungu msimamizi yoyote wa kuyasimamia mambo yao, akawaletea yanayopendwa na akawakinga na yanayochukiwa.
Yeye Ndiye Ambaye anawaonesha umeme, nao ni mwangaza unaong’aa kutoka ndani ya mawingu, mkawa mnaogopa msishukiwe na vimondo venye kuchoma kutokana na umeme huo, na pia mkawa mnatazamia mvua inyeshe. Na kwa uweza Wake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, anayleta mawingu yanayobebeshwa maji mengi kwa ajili ya manufaa yenu.
Na radi linamtakasia Mwenyezi Mungu sifa Zake njema, matakaso yanayoonyesha dalili kwamba linamnyenyekea Mola Wake. Na Malaika wanamwepusha Mola wao na kila la upungufu kwa kumuogopa kwao Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu Anatuma vimondo vyenye kuangamiza, Akawaangamiza kwavyo anaowataka kati ya viumbe vyake. Na makafiri wanabisha juu ya upweke wa Mwenyezi Mungu na uweza Wake kufufufua, na hali Yeye Ana uweza mwingi na nguvu na ujabari wa kuwatesa waliomuasi.
Ni wa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kutukuka, Peke Yake, ulinganizi wa tawhīd «Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu.» Haabudiwi wala haombwi isipokuwa Yeye. Na waungu ambao wao wanawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawaitiki maombi ya mwenye kuwaomba. Na hali yao pamoja na hao waungu ni kama hali ya mwenye kiu anayenyosha vitanga vyake viwili vya mkono kwenye maji kutoka mbali ili yafike kwenye kinywa chake, yakawa hayafiki. Na maombi ya makafiri kwa hao waungu hayakuwa isipokuwa yako mbali na usawa, kwa kuwa wao wanamshirikisha wengine pamoja na Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu Peke Yake wanamsujudia, wakinyenyekea na kufuata, walioko mbinguni na ardhini wote, Waumini wanamsujudia na kumnyenyekea kwa ridhaa na hiari, na makafiri wanamnyenyekea kwa nguvu, kwa kuwa wao wanafanya kiburi kumuabudu na hali yao na maumbile yao yanawakanusha juu ya hilo. Na vivuli vya viumbe vinafuata utukufu wa Mwenyezi Mungu, vinatembea kulingana na matakwa Yake mwanzo wa mchana na mwisho wake.
Waambie washirikina, ewe Mtume, «Ni nani muumba mbingu na ardhi na mwenye kuziendesha?» Sema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Muuumba Mwenye kuziendesha. Na nyinyi mnalikubali hilo.» Kisha waambie ukiwalazimisha hoja, «Je, mnawafanya wasiokuwa Yeye ni waabudiwa wenu, na hali ya kuwa wao hawawezi kuzinufaisha nafsi zao au kuzidhuru, wacha kule kuwanufaisha nyinyi au kuwadhuru, na mkaacha kumuabudu mwenye kuwamiliki wao?» Waambie, «Kwani analingana kwenu nyinyi kafiri, ambaye ni kama kipofu, na Muumini, ambaye ni kama anayeona? Au kwani unalingana kwenu nyinyi ukafiri, ambao ni kama giza, na Imani, ambayo ni kama mwangaza? Au ni kwamba wale wasimamizi wao wanaowafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu wanaumba kama Anavyoumba, vikawatatiza viumbe vya washirika na viumbe vya Mwenyezi Mungu, ndipo wakaitakidi kwamba wao wanastahiki kuabudiwa?» Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ni Muumba kila kilichoko ambacho hakikuwako; Yeye Ndiye Anayestahiki kuabudiwa Peke Yake na Yeye Ndiye Aliye mmoja Mwenye kutendesha nguvu Anayestahiki uungu na ibada, na sio masanamu na mizimu isiyodhuru wala kunufaisha.»
Kisha Mwenyezi Mungu Akapiga mfano wa ukweli na urongo kuwa ni kama maji Aliyoyateremsha kutoka juu, yakapita kwenye mabonde ya ardhi kwa kadiri ya udogo wake na ukubwa wake, mikondo ya maji ikabeba povu likiwa juu yake lisilo na faida. Na akapiga mfano mwingine wa madini ambayo watu huyachoma moto ili kuyayeyusha kutaka kutengeneza pambo, kama vile dhahabu na fedha, au kutaka manufaa ya kujinufaisha, kama vile shaba, ukatoka uchafu wake usio na faida kama ule uliokuwa pamoja na maji. Kwa mfano huu, Mwenyezi Mungu Apigia mfano ukweli na urongo. Urongo ni kama povu la maji, linapotea au linatupwa kwa kuwa halina faida, na ukweli ni kama maji safi na madini yaliyotakasika, yanasalia kwenye ardhi kwa kunufaika nayo. Kama Alivyowafafanulia nyinyi mifano hii, hivyo ndivyo Anavyoipiga kwa watu upate kufunuka wazi ukweli ujitenge na urongo, na uongofu ujitenge na upotevu.
Pepo ni ya wenye kuamini ambao wanamtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na Moto ni wa wale ambao hawakumtii na wakamkanusha. Na lau walikuwa wanamiliki kila kilichoko ardhini na zaidi ya kama hiko pamoja nacho, wangalikitoa kwa kujikomboa nafsi zao na adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, na hakingalikubaliwa kutoka kwao. Wao watafanyiwa hesabu kwa kila tendo baya walilolitenda. Na makazi yao ya kukaa ni Jahanamu, itakuwa ni tandiko kwao. Na tandiko baya mno ni hilo walilojitayarishia nafsi zao.
Je, yule anayejua kwamba kile ulichokuja nacho, ewe Mtume, ndicho ukweli unaotoka kwa Mwenyezi Mungu na akauamini ni kama kipofu asiyeuona ukweli ambaye hakuamini? Hakika wanaowaidhika ni wenye akili timamu
ambao wanatekeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu Ambayo Aliwaamrisha kwayo na wasiitangue ahadi ya mkazo ambayo walimuahidi nayo Mwenyezi Mungu.
Nao ndio ambao wanawaunga wale ambao Mwenyezi Mungu Amewaamrisha wawaunge kama jamaa wa karibu na wahitaji, wanamtunza Mola wao na wanaogopa Asiwahesabu kwa madhambi yao yote na Asiwasamehe chochote katika hayo.
Nao ndio ambao walivumilia udhia na kusimama juu ya utiifu na kujiepusha na uasi kwa kutafuta radhi za Mola wao, walitekeleza Swala kwa namna iliyotimia zaidi, walitekeleza Zaka za lazima za mali yao na matumizi yanayopendekezwa kwa siri na kwa dhahiri na wakawa wanaondoa baya kwa zuri lenye kulifuta. Hao wanaosifika kwa sifa hizi watakuwa na mwisho wenye kusifiwa huko Akhera.
Mwisho wao ni mabustani ya Pepo ya 'Adn, watakaa humo, hawataondoka kutoka humo, na pamoja nao watakuwamo waliokuwa wema miongoni mwa mababa, wake na watoto waume kwa wake, na huku malaika waingia kwao kutoka kila mlango wakipongeza na kuingia Peponi.
Malaika watawaambia, «Amani iwashukie, yakiwa ni maamkizi yenu peke yenu, na msalimike na kila baya kwa uvumilivu wenu katika kumtii Mwenyezi Mungu. Neema ya nyumba ya mwisho ni Pepo.»
Ama waovu, wamesifiwa kwa sifa kinyume na zile za Waumini. Wao ni wale ambao hawatekelezi ahadi za Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, kwa ibada baada ya kujitukulia ahadi ya mkazo. Na wao ni wale wanaokata kile ambacho Mwenyezi Mungu amewaamrisha kukiunga kama vile kukata zao na mengineyo na wanafanya uharibifu katika ardhi kwa kufanya maasia. Hao waliosifiwa kwa sifa hizi mbaya watakalolipata ni kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu na watakuwa na mambo ambayo ni mabaya kwao ya adhabu kali katika Nyumba ya Akhera.
Mwenyezi Mungu Peke Yake Anamkunjulia riziki Anayemtaka miongoni mwa waja Wake na Anambania Anayemtaka kati yao. Na makafiri waliufurahia ukunjufu duniani. Na dunia hii haikuwa ikilinganishwa na Akhera isipokuwa ni kitu kidogo cha kustarehe nacho, na kwa haraka sana kinaondoka.
Na makafiri wanasema kwa kushindana, «Si ateremshiwe Muhammad miujiza inayoonekena kama miujiza ya Mūsā na 'Īsā. Waambie kwamba Mwenyezi Mungu Anampoteza Anayemtaka miongoni mwa washindani wasiotaka uongofu na haimfai miujiza na Anawaongoza kwenye dini Yake ya haki anayerejea Kwake na kutaka radhi Zake.
Na Anawaongoza wale ambao nyoyo zao zimetulia kwa kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kumtaja zikapata utulivu. Jua utanabahi kwamba kumtii Mwenyezi Mungu, kumtaja na malipo mema kutoka Kwake yanafanya nyoyo zitulie na zipumbae.
Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafanya matendo mema watakuwa na furaha, kipumbazi cha jicho, hali nzuri na marejeo mema kwenye Pepo ya Mwenyezi Mungu na radhi Zake.
Kama tulivyowatuma Mitume kabla yako, tulikutuma, ewe Mtume, katika ummah waliopita kabla yao ummah wa Mitume, ili uwasomee ummah huu Qur’ani iliyoteremshwa kwako, na hali ya watu wako ni kuukanusha upweke wa Mwingi wa rehema. Waambie, ewe Mtume, «Mwingi wa rehema Ambaye hamkumpwekesha na mkamfanya ni Mola mmoja Ndiye Mola wangu, Peke Yake; hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Kwake Yeye nimetegemea na nina imani, na Kwake Yeye ndio marejeo yangu na makimbilio yangu.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawarudi makafiri ambao walitaka kwamba Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ateremshiwe miujiza yenye kuonekana, kwakuwaambia, «Lau kulikuwa na Qur’ani itakayosomwa ikafanya majabali yaondoke mahali pake au ardhi ipasuke itoe mito au wafu wafufuke na waseme, kama walivyotaka kwako, hii Qur’ani ingalikuwa ndiyo yenye kusifika na hayo na si kitu kingine, na pia hawangaliamini.. Bali ni ya Mwenyezi Mungu amri juu ya miujiza na mengineyo. Kwani hawakujua Waumini kwamba lau Mwenyezi Mungu Anataka, watu wote wa ardhini wangaliamini bila ya miujiza? Na hawataacha makafiri kuendelea kuteremkiwa na mkasa kwa sababu ya ukafiri wao, kama kuuawa na kutekwa katika vita vya Waislamu, au kuteremkiwa na mkasa huo karibu na nyumba zao, mpaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ije ya kuwapa ushindi juu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake.
Na iwapo wameufanyia shere ulinganizi wako, ewe Mtume, basi kuna ummah kabla yako waliwafanyia shere Mitume wao. Basi usiwe na masikitiko, niliwapa muhula wale waliokufuru kisha nikawapatiliza kwa mateso yangu; na yalikuwa ni mateso makali.
Je, Yule Anayesimamia kila nafsi Akiyadhibiti yale inayoyafanya, ni mwenye haki zaidi ya kuabudiwa au ni hivi viumbe visivyojiweza? Na wao, kwa ujinga wao walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika miongoni mwa viumbe Wake wakawa wanawaabudu. Waambie, ewe Mtume, «Tajeni majina yao na sifa zao.» Na hawatapata kwenye sifa zao chochote cha kuwafanya wao wastahiki kuabudiwa. Au nyinyi mnampasha habari Mwenyezi Mungu kuwa Ana washirika katika ardhi Yake ambao Hawajui? Au mnawaita ni washirika kimaneno tu bila ya kuwa na hakika? Bali Shetani aliwapambia makafiri neno lao la ubatilifu na akawazuia njia ya Mwenyezi Mungu. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu Hakumwafikia kuongoka basi hakuna yoyote mwenye kumuongoza na kumwafikia kwenye haki na uongofu.
Makafiri hawa wenye kuzuia njia ya Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu ngumu katika maisha ya ulimwenguni kwa kuuawa, kutekwa na kuhiziwa. Na kwa hakika, adhabu yao huko Akhera ni nzito zaidi na ni kali zaidi, na hawatakuwa na kizuizi chenye kuwazuia wasipate adhabu ya Mwenyezi mungu.
Sifa ya Pepo ambayo Mwenyezi Mungu Amewaahidi nayo wale wanaomuogopa na kwamba mito inapita chini ya miti yake na majumba yake ya fahari, Matunda yake hayamaliziki na kivuli chake hakiondoki. Malipo mema hayo ya Pepo ndio mwisho wa waliomuogopa Mwenyezi Mungu wakajiepusha na mambo ya kumuasi na wakatekeleza faradhi Zake. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
Na wale ambao tuliwapa Kitabu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, yoyote kati yao mwenye kukuamini, kama 'Abdullāh bin Salām na Najashi, wanaifurahia Qur’ani uliyoteremshiwa kwa kuwa inaenda sambamba na kile walichonacho. Na miongoni mwa wale wanaojiweka pamoja kukupinga, kama Sayyid na 'Aqib: maaskofu wawili wa Najran , na Ka'b bin al-Ashraf, wanaokanusha baadhi ya yale uliyoteremshiwa. Waambie, «Mwenyezi Mungu Ameniamrisha nimuabudu Yeye Peke Yake na nisimshirikishe chochote. Nawaita watu wamuabudu, na Kwake Peke Yake ndio marejeo yangu na marudio.
Na kama tulivyowateremshia Mitume Vitabu kwa lugha zao, tulikuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani kwa lugha ya Kiarabu, ili uitumie katika kuhukumu. Na lau ulifuata mapendeleo ya washirikina katika kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, baada ya haki iliyokujia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hutakuwa na msaidizi yoyote mwenye kukuhami na kuzuia adhabu ya Mwenyezi Mungu isikufikie.
Na kumbuka waliposema, «Una nini, ewe Mtume, unaoa wanawake?» Hakika tulituma kabla yako Mitume kati ya wanadamu na kuwafanya wawe na wake na watoto. Na pia utaje waliposema, «Lau alikuwa ni Mtume angalituletea miujiza tuliyoitaka.» Haiko kwenye uwezo wa Mtume yoyote, kuleta miujiza ambayo watu wake waliitaka isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila jambo alilolihukumu Mwenyezi Mungu lina maandishi na wakati, Mwenyezi Mungu Ameliandika hapo Kwake, halitangulii wala halichelewi.
Mwenyezi Mungu Anakifuta Akitakacho miongoni mwa hukumu na mengineyo, na Anakiacha kisalie Akitakacho miongoni mwa hizo kwa hekima fulani Anayoijua. Na Kwake kuna asili ya Kitabu, nacho ni Al-Lawh„ Al-Mah,fūd,: Ubao uliohifadhiwa ambao yamethibitishwa ndani yake kimaandishi hali za viumbe mpaka Siku ya Kiyama.
Na tukikuonesha , ewe Mtume, baadhi ya mateso tuliyowaahidi maadui zako ya kuhizika na kuungulika ulimwenguni, basi hayo ni yale tuliyowaharakishia. Na tukikufisha kabla hujaona hayo, basi wajibu wako haukuwa isipokuwa ni kutekeleza ulinganizi, na hesabu na malipo ni juu yetu.
Kwani hawaoni hawa makafiri kwamba sisi tunaijia ardhi na kuipunguza pambizoni mwake kwa kuwapa Waislamu ushindi wa kuiteka miji ya makafiri na kuishikanisha na miji ya Kiislamu? Na Mwenyezi Mungu Anaamua, hakuna Mwenye kuurudi uamuzi Wake na hukumu Yake. Na Yeye ni Mpesi wa kuhesabu, basi wasifanye haraka ya kutaka kuletewa adhabu, kwani kila lenye kuja liko karibu.
Hakika wale waliokuwa kabla yao waliwapangia njama Mitume wao, kama vile hawa walivyokufanyia. Basi vitimbi vyote vina Mwenyezi Mungu, Anatangua vitimbi vyao na kuwarudishia wenyewe wapite patupu na wajute. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu Kwake, Anakijua kile ambacho kila mtu anakichuma, chema au kibaya, na atalipwa kwa hicho. Na watajuwa makafiri, watakapofika kwa Mola wao, ni nanani atakuwa na mwisho mwema baada ya dunia hii. Huo ni wa wafuasi wa Mitume. Katika haya kuna onyo na tishio kwa makafiri.
Na wenye kumkanusha Nabii wa Mwenyezi Mungu wanasema, «Ewe Muhammad, hukutumilizwa na Mwenyezi Mungu.» Waambie, «Inatosha kuwa Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya ukweli wangu na urongo wenu, na unatosha ushahidi wa wenye ujuzi wa Kitabu miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara kati ya wale waliouamini utume wangu na kwamba yale niliokuja nayo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na akaufuata ukweli na akatoa ushahidi huo waziwazi na asiufiche.