surah.translation .

Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, timizeni ahadi za Mwenyezi Mungu zilizotiliwa mkazo za kuamini Sheria za Dini na kuzifuata, na tekelezeni ahadi mlizopeana nyinyi kwa nyinyi miongoni mwa amana mlizowekeana, biashara na mengineyo kati ya yale yasiyoenda kinyume na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na mafundisho ya Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Na hakika Mwenyezi Mungu Amewahalalishia wanyama wa mifugo, nao ni ngamia, ng’ombe na mbuzi na kondoo, isipokuwa yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaelezea ya kuwaharamishia mfu, damu na mengineyo; na ya kuwaharamishia kuwinda mkiwa kwenye hali ya ihramu (kwa ibada ya Hija au Umra). Kwa hakika Mwenyezi Mungu Anahukumu Anachokitaka kulingana na hekima Yake na uadilifu Wake.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuta sheria Zake kivitendo, msivuke mipaka ya Mwenyezi Mungu na alama Alizoziwekea hiyo mipaka yake. Na msihalalishe vita katika miezi mitukufu, nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu- na hilo lilikuwa katika mwanzo wa Uislamu-. Na msivunje heshima ya wanyama waliokusudiwa kuchinjwa katika ibada ya Hija, wala msivunje heshima ya vitu walivyovishwa navyo. Kwani walikuwa wakiwavalisha kwenye shingo zao miseja ya sufi au ya nyoya, ikiwa ni kitambulisho kwamba mnyama huyo ni wa kuchinjwa katika ibada ya Hija na kwamba mwenye mnyama anaenda Hija. Wala msihalalishe kuwapiga vita wenye kuikusudia Nyumba tukufu, ambao wanazitafuta fadhila za Mwenyezi Mungu zinazowatengezea maisha yao na kumridhisha Mola wao. Na pindi mnapomaliza ibada yenu ya Hija, mnahalalishiwa kuwinda. Na isiwapelekee nyinyi kuwachukia baadhi ya watu kwa kuwa waliwazuia nyinyi kufika Msikiti mtukufu, kama ilivyotokea katika mwaka wa Hudaibiyah, kuacha kuwafanyia uadilifu. Na saidianeni kati yenu, enyi Waumini, kufanya wema na kumcha Mwenyezi Mungu wala msisaidiane kwenye mambo ya madhambi, maasia na kuivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na jihadharini kuenda kinyume na amri ya Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Mkali wa kutesa.
Mwenyezi Mungu Amewaharamishia mfu, naye ni mnyama aliyekufa mwenyewe bila ya kuchinjwa. Na pia Amewaharamishia nyinyi damu inayotiririka inayomwagwa, nyama ya nguruwe, mnyama ambaye wakati wa kuchinjwa ametajiwa jina lisilokuwa la Mwenyezi Mungu, mnyama aliyenyongwa kwa kuzibwa pumzi zake mpaka akafa, mnyama aliyekufa kwa kupigwa gongo au jiwe, mnyama aliyeanguka kutoka mahali pa juu au aliyeanguka kisimani akafa na mnyama aliyekufa kwa kupigwa pembe na mwenzake. Na pia Amewaharamishia mnyama aliyeliwa na mnyama mwingine kama simba, chuimarara, mbwamwitu na mfano wake. Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na sifa za upungufu, Amewatoa, miongoni mwa wale Aliowaharamisha, kuanzia wale walionyongeka na waliofuatia, wale mliowahi kuwachinja kabla hawajafa, hao ni halali kwenu. Na Amewaharamishia nyinyi wanyama waliochinjiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu miongoni mwa vitu vilivyosimamishwa viabudiwe, viwe ni mawe au vinginevyo. Na Amewaharamishia kutaka kujua mambo, mliyoandikiwa na msiyoandikiwa, kwa viapo; navyo ni vipande ambavyo walikuwa wakitaka uamuzi kwavyo wakitaka kufanya jambo kabla hawajalifanya. Hayo mliyotajiwa katika aya hii kati ya yaliyoharamishwa, yakifanywa, huwa ni kutoka kwenye amri ya Mwenyezi Mungu na twaa Yake na kwenda kwenye maasia. Sasa imekatika tamaa ya makafiri kwamba nyinyi mtaiacha Dini yenu muende kwenye ushirikina baada ya mimi kuwapa ushindi juu yao. Basi msiwaogope wao na mniogope mimi. Leo nimeshawakamilishia dini yenu, Dini ya Uislamu, kwa kuuhakikisha ushindi na kuikamilisha Sheria, nimewatimizia neema zangu kwenu kwa kuwatoa kwenye giza la ujinga na kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani na nimewaridhia kwamba Uislamu ndio Dini, basi shikamaneni nayo wala msiiache. Na yule aliyepatikana na dharura ya njaa ikambidi ale mfu, na akawa hakukusudia kutenda kosa, basi inafaa kwake kumla. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kumsamehe na ni Mwenye huruma naye.
Wanakuuliza Maswahaba wako, ewe Nabii, «Ni kipi walichohalalishiwa kukila?» Waambie, «Mumehalalishiwa kula vilivyo vizuri na viwindwa vya wanyama mliowafundisha kati ya wanyama wanaowinda kwa kutumia makucha na meno yao, miongoni mwa mbwa, chui na kozi na kama hao kati ya wale wanaofundishwa. Mnawafundisha kuwatafutia viwindwa kwa yale Mwenyezi Mungu Aliyowafundisha. Basi kuleni wanyama waliowashikia na mlitaje jina la Mwenyezi Mungu wakati mnapowatuma kuwawindia. Na muogopeni Mwenyezi Mungu katika yale Aliyowaamrisha na yale Aliyowakataza.» Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
Na miongoni mwa ukamilifu wa neema ya Mwenyezi Mungu kwenu leo hii, enyi Waumini, ni kwamba Amewahalalishia vilivyo halali vizuri. Na vichinjwa vya Mayahudi na Wanaswara, iwapo watawachinja wanyama wao kuambatana na sheria yao, ni halali kwenu ; na vichinjwa vyenu ni halali kwao. Na Amewahalalishia nyinyi, enyi Waumini, kuwaoa wanawake wanaojihifadhi, nao ni wale walio huru kati ya wanawake Waumini wanaojizuia na uzinifu. Vilevile ni halali kuwaoa wanawake walio huru wanaojiepusha na uzinifu, miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara, iwapo mtawapa mahari yao na mkawa mumejihifadhi kwa kutofanya uzinifu na kuweka mahawara na mkawa mumejiaminisha kuwa hamutaathirika na dini yao. Na mwenye kuzikataa sheria za fmani, basi vitendo vyake vimishaharibika, na yeye, Siku ya Kiyama, atakuwa ni miongoni mwa wenye kupata hasara.
Enyi mlioamini! Mkitaka kuinuka ili kuswali, hali ya kuwa hamuna udhu, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visukusuku (Kisukusuku ni kiungo kilichoko kati ya mkono na nyoka-mkono). Na pakeni maji kwenye vichwa vyenu na muoshe miguu yenu pamoja na macho mawili ya miguu ( nayo ni mifupa miwili iliyojitokeza katika makutano ya muundi na nyayo). Na mtakapopatikana na tukiyo la hadathi kubwa ya kuondoa utohara, basi jitahirisheni kwa kuoga kabla ya kuswali. Na mkiwa ni wagonjwa au muko safarini katika hali ya afya, au iwapo mmoja wenu amemaliza haja yake, au amemuingilia mke wake, na mkawa hamkupata maji, basi ipigeni ardhi kwa mikono yenu na mupukuse nyuso zenu na mikono yenu kwayo. Mwenyezi Mungu Hataki kuwadhiki katika jambo la kujitoharisha, ndipo Akawatolea nafasi na kuwahurumia kwa kuwaruhusu kutayamamu (kutumia mchanga) badala ya kutumia maji katika kujitoharisha. Ruhusa ya kutayamamu ilikuwa ni katika kuzikamilisha neema ambazo zinapelekea kumshukuru Mneemeshaji kwa kumtii katika yale Aliyoyamrisha na kuyakataza.
Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu katika sheria Yake Aliyowaekea na kumbukeni ahadi Yake Yeye Aliyetukuka, Aliyoichukua kwenu ya kumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwasikiliza na kuwatii. Na mcheni Mwenyezi Mungu katika Aliyowaamrisha na Aliyowakataza. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyaficha katika nafsi zenu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, kuweni wasimamizi wa haki kwa ajili ya kuzitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, muwe mashahidi kwa uadilifu. Wala kusiwapelekee nyinyi kuwachukia watu kuacha kufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu baina ya maadui na vipenzi kwa daraja moja sawasawa. Kufanya uadilifu huko kuko karibu zaidi na kumuogopa Mwenyezi Mungu. Na jihadharini na kufanya udhalimu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mtambuzi wa mnayoyafanya na Atawalipa kwa hayo.
Mwenyezi Mungu Amewapa ahadi, wale ambao wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakatenda mema, kwamba Atawasamehe madhambi yao na Atawalipa Pepo kwa hilo. Na Mwenyezi Mungu Haendi kinyume na ahadi Yake.
Na wale waliokanusha upweke wa Mwenyezi Mungu unaoijulisha haki iliyo waziwazi na wakazikanusha dalili zake walizokuja nazo Mitume, hao ndio watu wa Motoni watakaosalia humo.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na mkazifuata sheria Zake kivitendo, yakumbukeni yale Aliyowaneemesha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa neema ya usalama, kutia uoga kwenye nyoyo za maadui zenu waliotaka kuwavamia, Mwenyezi Mungu Akawaepusha na nyinyi na Akaweka kizuizi kati yao na yale waliyoyataka kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, muwe na hadhari naye. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, katika mambo yenu ya kidini na ya kidunia na muwe na hakika ya kupata msaada Wake na uokozi Wake.
Na kwa hakika Mwenyezi Mungu Alichukua kwa Wana wa Isrāīl ahadi ya mkazo kwamba wamtakasiye ibada Yeye Peke Yeke. Na Mwenyezi Mungu Alimuamrisha Mūsā awawekee wao viongozi kumi na mbili kulingana na idadi ya koo zao, wachukue kwao ahadi ya mkazo ya kumsikiliza na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kukifuata Kitabu Chake. Na Mwenyezi Mungu Aliwaambia Wana wa Isrāīl, «Mimi niko pamoja nanyi kwa hifadhi yangu na nusura yangu. Iwapo mtasimamisha Swala na mtawapa Zaka za faradhi wanaostahiki kupewa na mtawaamini Mitume wangu katika yale wanayoyatolea habari, mtawanusuru na mtatoa katika njia yangu, hakika nitawafutia makosa yenu na nitawaingiza ndani ya mabustani ya Peponi ambayo mito inapita chini ya majumba yake ya fahari.Basi mwenye kuikana ahadi hii, kati yenu, hakika amejiepusha na njia ya haki na kuifuata njia ya upotevu.»
Kwa sababu ya hawa Mayahudi kuvunja ahadi zao zilizotiliwa mkazo, tuliwafukuza kutoka kwenye rehama yetu na tukazijaalia nyoyo zao kuwa ngumu, hazilainiki kwa Imani, wanayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu ambayo Alimteremshia Mūsā, nayo ni Taurati, na wakaacha kuitumia sehemu ya yale waliyokumbushwa nayo. Na utaendelea , ewe Mtume, kupata kutoka kwa Mayahudi uhaini na uvunjaji ahadi, kwani wao wako kwenye njia ya mababu zao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi samehe kwa mabaya wanayokutendea na usiwe na chuki juu yao. Hakika Mwenyezi Mungu Anampenda anayefanya uzuri wa kusamehe na kutokuwa na chuki kwa aliyemfanyia ubaya. (Hivi ndivyo vile watu wapotovu wanapata njia ya kufikia malengo yao mabaya kwa kuyapotoa maneno ya Mwenyezi Mungu na kuyapa maana ambayo siyo yake. Wakishindwa kupotoa na kugeuza maana, wanayaacha yale yasioafikiana na matamanio yao katika sheria ya Mwenyezi Mungu ambayo hawatathibiti juu yake isipokuwa wachache waliyohifadhiwa na Mwenyezi Mungu kati yao).
Na tulichukua ahadi ya mkazo kwa wale waliodai kuwa wao ni wafuasi wa Al-Masīḥ ‘Īsā mwana wa Maryam, na hali wao sio hivyo, kama ile tulioichukua kwa Wana wa Isrāīl, kwamba watamfuata Mtume wao, watamnusuru na watamsaidia, lakini walibadilisha Dini yao na wakaacha kutumia sehemu ya yale waliyokumbushwa nayo, kama walivyofanya Mayahudi. Kwa hivyo tulitia uadui na chuki kati yao mpaka Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu Atawapa habari, Siku ya Hesabu, ya yale ambayo wao walikuwa wakiyafanya, na Atawatesa kwa matendo yao.
Enyi watu mliopewa Kitabu , miongoni mwa Mayahudi na Wanaswara! Amewajia nyinyi mjumbe wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kuwafafanulia mengi ambayo mlikuwa mkiyaficha kwa watu katika yale yaliyomo ndani ya Taurati na Injili, na kuacha kuyafafanua yale ambayo busara haitaki yafafanuliwe. Hakika umewajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwngaza na Kitabu chenye ufafanuzi, nacho ni Qur’ani tukufu.
Kwa kitabu hiki chenye ufafanuzi, Mwenyezi Mungu Anawaongoza wenye kufuata yenye kumridhi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, njia za amani na usalama, Anawatoa kutoka kwenye giza la ukafiri kuwapeleka kwenye mwangaza wa Imani na Anawaafikia wao kufuata dini Yake iliyolingana sawa.
Kwa hakika wamekufuru Wanaswara wanaosema kwamba Mwenyezi Mungu ni Al-Masīh mwana wa Maryam. Sema, ewe Mtume, kuwaambia Wanaswara hawa wajinga, «Lau Al-Masīh angalikuwa Mungu, kama wanavyodai, angaliweza kuuzuia uamuzi wa Mwenyezi Mungu ukimjia wa kumwangamiza yeye na mama yake na watu wote wa ardhini. Na mama yake ‘Īsā alikufa, hakuweza kumkinga na kifo. Vilevile hawezi kujitetea nafsi yake. Kwani wote wawili ni waja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu, hawawezi kujiepusha na maangamivu. Hii ni dalili kuwa yeye ni mwanadamu kama wanadamu wengine. Na vitu vyote vilivyoko mbinguni na ardhini ni milki ya Mwenyezi Mungu, Anaumba na kupatisha anachotaka na yeye ni muweza wa kila kitu. Hakika ya tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) inawajibisha kupwekeka Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa sifa za uola na uungu; hakuna yoyote anayeshirikiana naye, katika viumbe Wake, kwa hilo. Na mara nyingi sana watu huingia kwenye ushirikina na upotevu kwa kuwatukuza Mitume na watu wema kupita kiasi, kama walivyopita kiasi Wanaswara katika kumtukuza Al-Masīh. Ulimwengu wote ni wa Mwenyezi Mungu, na viumbe viko kwenye mkono Wake Peke Yake. Na miujiza na alama kubwa zinazodhihiri, marejeo yake ni Mwenyezi Mungu.Anaumba, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, na Anafanya Anachotaka.
Mayahudi na Wanaswara walidai kuwa wao ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema kuwaambia, ewe Mtume, «Basi ni kwa nini Atawaadhibu kwa madhambi yenu.» Lau mlikuwa ni vipenzi Vyake hangaliwaadhibu. Kwani Mwenyezi Mungu Hampendi isipokuwa Anayemtii. Na waambie wao, «Bali nyinyi ni viumbe kama walivyo binadamu wengine, mkifanya wema mtalipwa mema kwa wema wenu, na mkifanya ubaya mtalipwa shari kwa ubaya wenu.» Mwenyezi Mungu Atamsamehe Anayemtaka, na Atamuadhibu Anayemtaka. Yeye Ndiye Anayeumiliki ufalme, Anaupeleka Anavyotaka na Kwake ndio marudio. Na hapo Atatoa uamuzi kwa waja Wake na Atamlipa kila mmoja anachostahiki.
Enyi Mayahudi na Wanaswara, amewajia mjumbe wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, ili kuwafunulia haki na uongofu baada ya kipindi kirefu cha wakati baina ya kumtuma yeye na kumtuma ‘Īsā mwana wa Maryam, ili msije mkasema, «Hakutujia mjumbe, mwenye kutoa bishara wala mwenye kuonya.» Hakika ashawajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu mjumbe anayempa bishara njema mwenye kumuamini na anayemuonya mwenye kumuasi. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu, wa kumtesa mwenye kuasi na kumpa thawabu mwenye kutii.
Na kumbuka, ewe Mtume, pindi aliposema Mūsā, amani imshukie, kuwaambia watu wake, «Enyi Wana wa Isrāīl, Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, pindi Alipochagua Manabii kati yenu, Akawafanya wafalme, mnayatawala mambo yenu baada ya kuwa mumetawaliwa na Fir‘aun na watu wake. Na hakika Aliwatunuku nyinyi aina mbalimbali za neema ambazo Hakumtunuku nazo yoyote miongoni mwa walimwengu wa zama zenu.
«Enyi watu wangu, Ingieni kwenye ardhi takatifu, yaani iliyotakaswa, nayo ni Bait al-Maqdis na sehemu zilizo kando-kando yake, ambayo Mwenyezi Mungu Ametoa ahadi muingie na mkapigane na makafiri waliyo humo wala msirudi nyuma mkaacha kupigana na hao majabari, kwani mkifanya hivyo mtaikosa heri ya duniani na heri ya Akhera.»
Walisema, «Ewe Mūsā, hakika huko kuna watu wakali wenye nguvu ambao hatuna uwezo wa kupigana nao. Na sisi hatutaweza kuingia huko na wao wako. Watakapotoka huko, sisi tutaingia.»
Walisema watu wawili kati ya wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ambao Mwenyezi Mungu Aliwapa neema kwa kumtii kwao Yeye na kumtii Mtume Wake, kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Ingieni kwa majabari hao kupitia lango la mji wao, ikiwa ni mojawapo ya njia za kutafuta sababu za ushindi. Mtakapoingia langoni, mtawashinda. Na kwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, jitegemezeni, iwapo nyinyi mnamuamini Mtume Wake katika yale Aliyowaletea, mnaiandama sheria Yake kivitendo.»
Watu wa Mūsā walisema kumwambia, «Hatutaungia mji huo kabisa, iwapo hao majabari wamo humo. Hivyo basi, nenda wewe na Mola wako mkapigane. Ama sisi, tunakaa hapa- hapa na hatutapigana na wao.» Hii inaonesha kushikilia kwao kuenda kinyume na Mūsā, amani imshukie.
Mūsā alielekea kwa Mola wake akiomba, «Mimi sina uwezo isipokuwa wa nafsi yangu na ndugu yangu, basi hukumu kati yetu na watu wenye kuasi.»
Mwenyezi Mungu Alisema kumwambia Nabii Wake Mūsā, amani imshukie, «Hakika hiyo ardhi takatifu ni haramu kwa hawa Mayahudi kuiingia kwa muda wa miaka arubaini, watakuwa wakitanga katika ardhi wakiwa kwenye hali ya mshangao. Basi usiwasikitikie, ewe Mūsā, watu waliotoka kwenye utiifu wangu.»
Wasimulie, ewe Mtume, Wana wa Isrāīl habari ya wana wawili wa Ādam, Qābīl na Hābīl, nayo ni habari ya kweli, alipotoa kila mmoja wao sadaka, nayo ni ile inayotolewa ili kujisogeza karibu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Hapo Mwenyezi Mungu Aliikubali sadaka ya Hābīl kwa kuwa alikuwa mcha-Mungu, na Hakuikubali sadaka ya Qābīl, kwa kuwa hakuwa mcha-Mungu. Qābīl alimhusudu ndugu yake na akasema, «Nitakuua.» Hābīl akajibu, «Kwa hakika Mwenyezi Mungu Huikubali sadaka itokayo kwa wale wenye kumuogopa.»
Hābīl akasema, akimpa mawaidha ndugu yake, «Iwapo utaunyosha mkono wako kwangu ili uniue, hutapata kutoka kwangu mfano wa kitendo chako. Mimi namuogopa Mwenyezi Mungu mola wa viumbe wote.
«Mimi nataka urudi ukiwa umebeba dhambi la kuniua mimi na dhambi lililokuwa juu yako kabala ya hilo, upate kuwa ni miongoni mwa watu wa Motoni na watakaosalia humo. Na hayo ndiyo malipo ya wanaofanya uadui.»
Basi ilimpambia Qābīl nafsi yake amuue ndugu yake, akamuua na akawa ni kati ya waliopata hasara, ambao waliuza Akhera yao kwa dunia yao.
Qābīl alipomuua ndugu yake, hakujua aufanye nini mwili wake. Hapo Mwenyezi Mungu Alimtuma kunguru, akawa anafukuwa shimo katika ardhi ili amzike humo kunguru aliyekufa, ili amjulishe Qābīl namna ya kuuzika mwili wa ndugu yake. Qābīl alistaajabu na akasema, «Kwani nimeshindwa kufanya vile kunguru huyu alivyofanya nikapata kuificha aibu ya ndugu yangu?» Hapo Qābīl alimzika ndugu yake. Na baada ya hasara aliyorudi nayo, Mwenyezi Mungu alimpa mateso ya majuto.
Kwa sababu ya uhalifu huu wa mauaji, tuliwaekea sheria Wana wa Isrāīl kwamba yoyote mwenye kumuua mtu pasi na sababu ya kulipiza kisasi au ya uharibifu katika ardhi, kwa aina yoyote kati ya aina za uharibifu zinazopelekea mauaji, kama ushirikina na uharamia, atakuwa ni kama kwamba amewaua watu wote kwa jinsi atakavyostahili mateso makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba yule atakayejizuia asiue mtu ambaye Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, ni kama kwamba amewahuisha watu wote. Hivyo basi, kulinda heshima ya binadamu mmoja ni kulinda heshima ya binadamu wote. Hakika Mitume wetu waliwajia Wana wa Isrāīl kwa hoja na dalili juu ya usawa wa yale waliyowalingania kwayo ya kumuamini Mola wao na kuyatekeleza yale yaliyofanywa wajibu kwao na Mola wao. Kisha, wengi kati yao, baada ya kujiwa na Mitume ni wenye kupita mipaka ya Mwenyezi Mungu kwa kuyafanya yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu na kuyaacha maamrisho yake.
Hakika malipo ya wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na wanaojitokeza wazi kumfanyia uadui na kuzifanyia uadui hukumu zake na hukumu za Mtume Wake na kufanya uharibifu katika ardhi kwa kuwaua watu na kupora mali, ni wauawe au wasulubiwe pamoja na kuuawa (Kusululubiwa ni kufungwa mhalifu juu ya bao) au ukatwe mkono wa kulia wa mpiga vita na mguu wake wa kushoto. Iwapo hatatubu ﴿kwa kuendelea na uharamia wake﴾, ukatwe mkono wake wa kushoto na mguu wa kulia, au wahamishwe wapelekwe mji usiokuwa wao, wafungwe kwenye jela ya mji huo mpaka iyonekane toba yao. Na haya ndiyo malipo Aliyoyaandika Mwenyezi Mungu kwa wenye kupiga vita; nayo ni unyonge wa duniani. Na huko Akhera itawapata adhabu kali iwapo hawatatubia.
Lakini atakayekuja kati ya wale wanaopiga vita kabla hamjawatia mkononi na akaja akiwa mtiifu mwenye majuto, atafutiwa yale yaliyokuwa ni haki ya Mwenyezi Mungu. Na jueni, enyi Waumini, kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha kwa waja Wake, ni Mwenye kuwarehemu.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata Sheria Yake kivitendo, muogopeni Mwenyezi Mungu na mjisogeze karibu Kwake kwa kumtii na kufanya yanayomridhisha, na mpigane jihadi katika njia Yake ili mpate kufaulu kwa kuingia mabustani ya Pepo Yake.
Hakika wale walioukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu na sheria Yake, lau walikuwa wao wamemiliki vyote vilivyoko ardhini na wakavimiliki vyingine mfano wake, na wakataka kuzikomboa nafsi zao, Siku ya Kiyama, na adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa hivyo walivyovimiliki, Mwenyezi Mungu Hangalikubali hilo. Na itawapata wao adhabu yenye kuumiza.
Makafiri hawa watataka watoke Motoni kwa ajili ya visanga vyake wanavyovipata, lakini hawatakuwa na njia yoyote ya kufanya hivyo. Na watakuwa na adhabu ya kudumu.
Na mwizi wa kiume na mwizi wa kike, wakateni, enyi watawala, mikono yao kuambatana na Sheria. Hayo yakiwa ni malipo yao kwa kuchukua kwao mali ya watu pasi na haki, na ni mateso ambayo kwayo Mwenyezi Mungu Anawazuia wengineo kufanya mfano wa kitendo chao. Na Mwenyezi Mungu ni Mshindi katika mamlaka Yake, ni Mwenye hekima katika amri Zake na makatazo Yake.
Basi yule atakayetubia baada ya wizi wake na akawa mwema katika vitendo vyake vyote, kwa hakika Mwenyezi Mungu Ataikubali toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwasamehe waja Wake, ni Mwenye huruma kwao.
Kwani hujui, ewe Mtume, kwamba Mwenyezi Mungu ni Muumba wa ulimwengu, ni Mwenye kuuendesha na Mwenye kuumiliki na kwamba Yeye, Aliyetukuka, Ndiye Mfanya wa Alitakalo, Anamuadhibu Amtakaye na Anamsamehe Amtakaye; na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza.
Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wale ambao wanakimbilia kuukanusha unabii wako miongoni mwa wanafiki ambao wameonyesha Uislamu na huku nyoyo zao ni tupu, kwani mimi ni Mwenye kukuokoa na wao. Na lisikuhuzunishe lile la kukimbilia kwa Mayahudi kuukanusha unabii wako, kwani wao ni watu wanaosikiliza urongo, wanayakubali yanayozuliwa na wanavyuoni wao na wanawasikiliza watu wengine wasiohudhuria kwenye baraza yako; na wengine hawa wanayageuza maneno ya Mwenyezi Mungu baada ya kuyaelewa na wanasema, «Yakiwajia kutoka kwa Muhammad yanayolingana na yale tuliyoyageuza na tukayapotosha katika hukumu za Taurati, basi yatumieni. Na yakiwajia kutoka kwake yanayokwenda kinyume na hayo, basi jihadharini kuyakubali na kuyatumia.» Na ambaye Mwenyezi Mungu Ataka apotee, basi hutaweza, ewe Mtume, kulizuia hilo lisiwe kwake na wala huwezi kumuongoza.. Na hakika hawa wanafiki na Mayahudi, Mwenyezi Mungu Hakutaka kuzitakasa nyoyo zao na uchafu wa ukafiri, wana udhalilifu na fedheha hapa duniani, na watapata, huko Akhera, adhabu kubwa.
Mayahudi hawa wanakusanya kati ya usikilizaji urongo na ulaji haramu. Basi watakapokujia wakishtakiana kwako, basi hukumu kati yao au waache. Na usipohukumu kati yao, hawataweza kukudhuru kwa chochote. Na iwapo utahukumu, basi hukumu kati yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu Anawapenda waadilifu.
Kitendo cha Mayahudi hawa ni cha kushangaza. Wao wanashitakiana kwako, ewe Mtume, na wao hawakuamini wewe wala Kitabu chako, pamoja na kuwa ile Taurati wanayoiamini wanayo, na humo muna hukumu ya Mwenyezi Mungu; kisha wanaondoka baada ya kutoa hukumu yako, iwapo haikuwaridhisha, wakakusanya kati ya kuzikataa sheria zao na kuipa mgongo hukumu yako. Na hawakuwa hao, wanaosifika na sifa hizo, ni wenye kumuamini Mwenyezi Mungu, kukuamini wewe na kuikubali hukumu uliyoitoa.
Hakika tumeiteremsha Taurati. Ndani yake muna uongozi wa kumuepusha mtu na upotevu na ufafanuzi wa hukumu ambazo Mitume wamezitumia katika kuhukumu. Mitume ambao waliiandama na kuikubali hukumu ya Mwenyezi Mungu kati ya Mayahudi na wasitoke nje ya hukumu Yake wala wasiipotoshe. Pia walihukumu, kutumia sheria hiyo, wafanyi ibada wa Kiyahudi na wasomi wao ambao wanawalea watu kwa sheria za Mwenyezi Mungu. Hilo ni kwamba Manabii wao waliwaamini kwa kuwapa majukumu ya kuifikisha Taurati, kukielewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kukitumia. Na wacha-Mungu na wanavyuoni walikuwa ni mashahidi ya kwamba Manabii wao walihukumu kati ya Mayahudi kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anasema kuwaambia wasomi wa Kiyahudi na wanavyuoni wao, «Msiwaogope watu katika kupitisha hukumu yangu, kwani wao hawawezi kuwanufaisha nyinyi wala kuwadhuru. Lakini niogopeni, kwani mimi Ndiye Mwenye kunufaisha, Mwenye kudhuru. Wala msichukue, kwa kuacha kuhukumu kwa sheria nilizoziteremsha, badali twevu.» Kwani kuhukumu kwa ambayo hayakuteremshwa na Mwenyezi Mungu ni katika vitendo vya makafiri. Na wenye kubadilisha hukumu ya Mwenyezi Mungu Aliyoiteremsha kwenye Kitabu Chake, wakaificha, wakaikana na wakahukumu kwa isiyokuwa hiyo wakiitakidi uhalali wake na kufaa kwake, basi hao ndio makafiri.
Na tulilifanya ni lazima kwao katika Taurati kwamba mtu huuawa akiua mtu, hutolewa jicho akitoa jicho la mtu, hukatwa pua akikata pua ya mtu, hukatwa sikio akikata sikio la mtu, na hung’olewa jino aking’oa jino la mtu na kwamba hulipizwa kisasi kwa kutia mtu majaraha. Mwenye kusamehe haki yake ya kulipiza kisasi kwa aliyemfanyia uadui, basi huko ni kujifutia na kujiondolea sehemu ya madhambi ya yule aliyefanyiwa uadui. Na yule asiyehukumu kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, katika kisasi na megineyo, basi hao ni wakiukaji wa mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Na tukawafuatishia, Manabii wa Wana wa Isrāīl, ‘Īsā mwana wa Maryam akiwa ni mwenye kuyaamini yaliyomo ndani ya Taurati na kuzitumia hukumu zilizomo kati ya zile ambazo hazikufutwa na Kitabu chake na tukamteremshia Injili ikiwa ni yenye kuongoza kwenye haki na yenye kuyaeleza yale ambayo watu hawakuyajua katika hukumu za Mwenyezi Mungu na ni yenye kutoa ushahidi juu ya ukweli wa Taurati kwa hukumu zake ilizokusanya Na tumeifanya ni bainifu kwa wale wanaomuogopa Mola wao, ni yenye kuwakemea wasiyafanye yaliyoharamishwa.
Basi na wahukumu watu wa Injili, ambao alitumwa kwao Īsā, kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu ndani yake. Na wale ambao hawakuhukumu kwa yaliyoteremshwa na Mwenyezi Mungu, Basi hao ndio wenye kutoka kwenye amri Yake, wenye kumuasi.
Na tumekuteremshia wewe, ewe Mtume, Qur’ani. Na yote yaliyomo ndani yake ni haki, yanatoa ushahidi juu ya ukweli wa Vitabu kabla yake na kwamba -vitabu hivyo- vinatoka kwa Mwenyezi Mungu, hali ya kuuthibitisha usahihi uliomo, kuufafanua upotovu uliomo na kuzifuta baadhi ya sheria zake. Kwa hivyo, wahukumu kati ya wale Mayahudi wanaoshitakiana kwako kwa sheria zile ulizoteremshiwa katika hii Qur’ani, wala usiiepuke haki, ambayo Mweyezi Mungu Amekuamrisha uitumie, ukafuata matakwa yao na yale waliyoyazoea. Kwani kila kundi la watu tumewawekea sheria na njia iliyo wazi ya wao kuifuata. N a lau Mwenyezi Mungu Angalitaka, Angalizifanya sheria zenu kuwa ni moja, lakini Yeye, Aliyetukuka, Alizifanya zitafautiane ili awape mtihani, ili mtiifu na mwenye kuasi wajulikane waziwazi. Basi yakimbilieni yale yaliyo bora kwenu katika Makao Mawili yenu(duniani na Akhera), kwa kuyafuata yaliyomo kwenye Qur’ani kivitendo. Kwani mwisho wenu ni kurudi kwa Mwenyezi Mungu; huko Atawapa habari ya yale mliyokuwa mkitafautiana juu yake, na hapo Atamlipa kila mmoja kwa amali yake.
Hukumu, ewe Mtume , kati ya Mayahudi kwa Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu katika Qur’ani, wala usiyafuate matakwa ya wale wanaoshitakiana kwako. Na jihadhari nao wasikuzuie na baadhi ya Aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu ukaacha kuyatumia. Na iwapo wataikataa hukumu unayoitoa, basi jua kwamba Mwenyezi Mungu Anataka kuwaepusha na njia ya uongofu kwa sababu ya madhambi waliyotangulia kuyafanya. Na kwa hakika, wengi wa watu wako nje ya utiifu wa Mola wao.
Je, wanataka Mayahudi hawa uhukumu kati yao kwa yale ya upotevu na ujinga waliyoyazoea washirikina wanaoabudu masanamu? Hayo hayawi wala hayafai kabisa. Na ni nani aliye muadilifu zaidi kuliko Mwenyezi Mungu katika hukumu Yake kwa aliyeziifahamu sheria za Mwenyezi Mungu, akamuamini na akawa na yakini kwamba hukumu ya Mwenyezi Mungu ndiyo ya haki?
Enyi mlioamini, msiwafanye Mayahudi na Wanaswara ni washirika na wasaidizi wenu juu ya watu wa Imani. Hii ni kwa kuwa wao hawawapendi Waumini. Mayahudi wanasaidiana wao kwa wao, na hivyo hivyo ndivyo walivyo Wanaswara. Na makundi yote mawili yanakutana kwenye kuwafanyia nyinyi uadui. Na nyinyi, enyi Waumini, mnafaa zaidi kusaidiana nyinyi kwa nyinyi. Na yoyote mwenye kuwategemea wao katika nyinyi, basi yeye atakuwa ni miongoni mwao, na hukumu yake ni yao. Mwenyezi Mungu Hatawaafikia madhalimu wanaowategemea makafiri.
Mwenyezi Mungu Anasimulia habari ya kikundi cha wanafiki kwamba wao walikuwa wakikimbilia kupendana na Mayahudi kwa kuwa ndani ya nyoyo zao mulikuwa na shaka na unafiki, na walikuwa wakisema, «Sisi tunapendana nao kwa kuogopa wasije wakawashinda Waislamu wakatudhuru sisi pamoja na wao.» Mwenyezi Mungu, uliotukuka utajo Wake, Anasema: Huenda Mwenyezi Mungu Akauleta ushindi- yaani ushindi wa kuukomboa mji wa Makkah-, Akamnusuru Nabii Wake na Akaupa nguvu Uislamu na Waislamu juu ya makafiri au Akatayarisha mambo ambayo yataifanya iyondoke nguvu ya Mayahudi na Wanaswara, na hapo waje wawanyenyekee Waislamu. Wakati huo watajuta wanafiki kwa yale waliyoyaficha kwenye nafsi zao ya kuwategemea Mayahudi na Wanaswara.
Wakati huo watasema baadhi ya Waumini kuwaambia wengine, wakionea ajabu hali ya wanafiki, pindi mambo yao yatakapofichuka, «Je, hawa ndio wale ambao waliapa viapo vizito kwamba wao wako nasi?» Zimebatilika amali za wanafiki walizozifanya ulimwenguni, hawana malipo mema ya amali hizo, kwa kuwa wao walizifanya bila ya Imani. Hapo basi, wamepata hasara ya ulimwenguni na Akhera.
Enyi mliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkazifuata sheria zake kivitendo, Yoyote kati yenu atakayerudi nyuma akaiacha Dini yake, na akachukua badala yake dini ya Kiyahudi au ya Kinaswara au dini nyengineyo, basi hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote; na Atawaleta watu bora kuliko wao: Anaowapenda na wanaompenda, wenye huruma kwa Waumini, wakali kwa makafiri, wanapigana jihadi na maadui wa Mwenyezi Mungu na hawamuogopi, kwa kumridhisha Mwenyezi Mungu, yoyote. Kuneemeshwa huko ni miongoni mwa nyongeza za Mwenyezi Mungu anazompa Amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa fadhila, ni Mjuzi wa anayestahiki fadhila Zake katika waja Wake.
Hakika msaidizi wenu , enyi Waumini, ni Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na Waumini wanaojilazimisha na Swala za faradhi na wanatekeleza Zaka kwa hiari yao na hali wao ni wanyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu.
Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu na akafuata muongozo wa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na akawa na muelekeo wa Waumini, basi yeye ni katika kundi la Mwenyezi Mungu, na kundi la Mwenyezi Mungu ndilo la washindi wenye kunusurika.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiwafanye wale wanaoifanyia shere na kuichezea Dini yenu, miongoni mwa waliopewa Vitabu na makafiri, kuwa ni wasimamizi wa mambo yenu. Na muogopeni Mwenyezi Mungu mkiwa nyinyi mnamuamini Yeye na mnaziamini sheria Zake.
Na anapoadhini mwadhini wenu, enyi Waumini, kuita watu kwenye Swala, Mayahudi, Wanaswara na washirikina wanafanya shere na kuukejeli mwito wenu wa hiyo Swala. Hii ni kwa sababu ya ujinga wao wa kutomjua Mola wao na kwa kuwa wao hawajui uhakika wa ibada.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hao wanaofanya shere kati ya hao waliiopewa Kitabu, «Mnalolikuta kuwa ni jambo la kutukanika au ni la aibu, hilo kwetu ni zuri kusifika nalo. Na hilo ni lile la kumuamini kwetu Mwenyezi Mungu na vitabu Vyake vilivyoteremshwa kwetu na waliokuwa kabla yetu na kuamini kwetu kwamba wengi wenu muko nje ya njia ilyo nyofu.»
Sema, ewe Nabii, kuwaambia Waumini, «Je, niwajulishe yule ambaye atalipwa, Siku ya Kiyama, malipo makali zaidi kuliko hawa wenye kutoka nje ya utiifu?» Hao ni waliowatangulia wao ambao Mwenyezi Mungu Aliwafukuza kwenye rehema Yake, Aliwakasirikia na akawageuza maumbile yao Akawafanya manyani na ngurue kwa kuasi kwao, kuzua kwao urongo na kuwa na kiburi, kama ambavyo walikuwa kati yao wenye kuabudu Tāghūt (kila kinachoabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu nacho kimeridhika). Hao, ni pabaya mno mahali pao huko Akhera; na harakati zao ulimwenguni zilikosa mwelekeo wa njia ya sawa.
Na wakiwajia nyinyi, enyi Waumini, wanafiki wa Kiyahudi husema, «Tumeamini,» na hali wao wako ukafirini na wanaendelea nao :hakika wameingia kwenu wakiwa na ukafiri wanaouitakidi ndani ya nyoyo zao, kisha wametoka wakiwa bado wanaushikilia ukafiri huo. Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa siri zao hata wakionyesha kinyume cha hivyo.
Na utawaona, ewe Mtume, wengi miongoni mwa Mayahudi wanayakimbilia maasia ya kusema urongo, uzushi, kuzifanyia uadui hukumu za Mwenyezi Mungu na kula mali ya watu kinyume na haki. Ni maovu mno matendo yao na uadui wao.
Mbona viongozi wao na wasomi wao hawawakatazi hawa ambao wanayakimbilia madhambi na kufanya uadui, kusema urongo, uzushi na kula mali za watu kinyume na haki? Ni kiovu mno walichokifanya, walipoacha kukataza munkar (mabaya).
Mwenyezi Mungu Anamjulisha Mtume Wake sehemu ya makosa ya Mayahudi, kitu walichokuwa wakikizungumza kwa siri baina yao, kuwa wao walisema, «Mkono wa Mwenyezi Mungu umefungwa kutotenda mema, Ametufanyia ubahili riziki kwa kutubania na kutotupanulia.» Walisema hilo wakati walipopatwa na ukame na ukosefu wa mvua. Mikono yao ndiyo iliyofungwa, kwa maana: mikono yao imezuiliwa kutenda mema, na Mwenyezi Mungu Amewafukuza kutoka kwenye rehema Yake kwa sababu ya neno lao. Mambo sivyo kama wanavyomzulia Mola wao, bali mikono Yake miwili imekunjuliwa, haikuzuiliwa wala hakuna pingamizi ya kumzuia kutoa. Kwani Yeye ni Mpaji, ni Karimu, Anatoa kulingana na hekima na yale yenye maslahi kwa waja. Kwenye aya hii kuna thibitisho la sifa ya Mikono miwili kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetakasita na kila sifa ya upungufu na kutukuka, kama inavyolingana na Yeye, pasi na kufananisha wala kueleza namna ilivyo. Lakini wao watazidi ukiukaji mipaka na ukafiri kwa sababu ya chuki yao na uhasidi wao kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekuchagua wewe kwa utume. Mwenyezi Mungu Anayatolea habari makundi ya Mayahudi kwamba wao wataendelea, mpaka Siku ya Kiyama, kufanyiana uadui wao kwa wao na kuchukiana wao kwa wao. Kila wanapopanga njama ya kuwafanyia vitimbi Waislamu, kwa kuzusha fitina na kuuwasha moto wa vita, Mwenyezi Mungu Anavikomesha vitimbi vyao na kuutenganisha mkusanyiko wao. Na Mayahudi hawataacha kuendelea kumuasi Mwenyezi Mungu kwa kufanya yanayoleta uharibifu na misukosuko katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hawapendi waharibifu.
Lau kama Mayahudi na Wanaswara wangalimuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, wakazifuata amri Zake na kuyaepuka makatazo Yake, tungaliwafutia madhambi yao na tungaliwatia kwenye mabustani ya Pepo ya starehe katika Nyumba ya Akhera.
Na lau kama wao wangaliyatekeleza yaliyomo ndani ya Taurati na Injili na yale uliyoteremshiwa wewe, ewe Mtume, nayo ni Qur’ani, wangalipata riziki kutoka kila njia: tukawateremshia mvua na kuwaoteshea matunda. Na haya ni malipo ya duniani. Na kwa hakika, miongoni mwa watu waliepewa Kitabu, lipo kundi la wastani lililojikita kwenye haki. Na wengi kati yao , vitendo vyao ni viovu na wamepotea njia ya sawa.
Ewe Mtume, fikisha wahyi wa Mwenyezi Mungu uliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako. Na iwapo utapunguza bidii katika kuufikisha, ukaficha chochote katika wahyi huo, basi utakuwa hukuufikisha ujumbe wa Mola wako. Na kwa hakika, Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, alifikisha ujumbe wa Mola wake kikamilifu. Basi yoyote atakayedai kuwa yeye alificha chochote, katika yale aliyoteremshiwa, atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake urongo mkubwa. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwenye kukulinda na kukuokoa na maadui zako. Si juu yako lolote isipokuwa ni kufikisha. Kwa hakika Mwenyezi Mungu hamuelekezi kwenye uongofu aliyepotea njia ya haki na akayapinga uliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Mayahudi na Wanaswara, «Nyinyi hamuna fungu lolote la dini, madhali hamkuyafuata kivitendo yaliyomo ndani ya Taurati na Injili na Qur’ani aliyokuja nayo Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.» Na hakika wengi wa wale waliopewa Kitabu, haiwaongezei kuteremshiwa wewe Qur’ani isipokuwa ni ujabari na kukanusha. Kwa hivyo, wao wanakuhusudu kwa kuwa Mwenyezi Mungu Amekutuma kwa ujumbe huu wa mwisho, ambao Ameeleza humo aibu zao. Basi usiwe na huzuni, ewe Mtume, juu ya kule kukukanusha kwao.
Hakika wale walioamini (nao ni Waislamu), Mayahudi na al- Ṣābiūn (Masabai, nao ni watu waliosalia kwenye umbile lao na hawana dini fulani waifuatayo), Wanaswara (nao ni wafuasi wa al-Masīḥ), waliomuamini Mwenyezi Mungu miongono mwao Imani kamilifu, nayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kumuamini Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, wakaiyamini Siku ya Mwisho na wakatenda matendo mema, basi hao hawatakuwa na hofu yoyote juu ya janga la Siku ya Kiyama wala wao hawatakuwa na huzuni juu ya yale waliyoyaacha nyuma yao duniani.
Kwa hakika tulichukuwa ahadi ya mkazo kwa Wana wa Isrāīl katika Taurati kuwa watasikia na watatii na tukawapelekea kwa ahadi hiyo Mitume wetu. Lakini walivunja ile ahadi iliyochukuliwa kwao, wakafuata matamanio yao na wakawa kila akiwajia Mtume, miongoni mwa hao Mitume, kwa yale ambayo nafsi zao haziyataki, wanamfanyia uadui: wakawakanusha baadhi yao na wakawaua wengine.
Na walidhania waasi hawa kwamba Mwenyezi Mungu Hatawatia mkononi kwa kuwaadhibu kwa sababu ya kuasi kwao na kutakabari kwao, ndipo wakaendelea katika matamanio yao na wakawa vipofu wa kutouona uongofu na wakawa viziwi wa kutoisikia na kutonufaika na haki. Hapo Mwenyezi Mungu Aliwateremshia adhabu Yake, wakatubia na Mwenyezi Mungu Akawakubalia toba zao. Kisha wengi wao walikuwa vipofu na viziwi baada ya kubainikiwa na haki. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona matendo yao, mazuri na mabaya, na Atawalipa kwa matendo yao hayo.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anaapa kwamba wale ambao walisema, «Mwenyezi Mungu Ndiye al-Masīh, mwana wa Maryam,» wameshakufuru kwa maneno yao haya. Na Alitoa habari Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwamba al- Masīh, alisema kuwaambia Wana wa Isrāīl, «Muabuduni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, kwani mimi na nyinyi katika uja tuko sawa.» Kwa hakika, yoyote atakayemuabudu mwengine, pamoja na Mwenyezi Mungu, Aliye Pweke, basi Mwenyezi Mungu Ataifanya Pepo kuwa ni haramu kwake na Ataufanya Moto kuwa ndio makao yake na hatakuwa na msaidizi wa kumuokoa nao Moto huo.
Hakika wamekufuru Wanaswara waliosema, «Mwenyezi Mungu ni mkusanyiko wa vitu vitatu: Baba, Mwana na Roho mtakatifu.» Kwani Wanaswara hawa hawakujua kwamba watu hawana isipokuwa muabudiwa Mmoja, Hakuzaa wala Hakuzaliwa? Na iwapo wenye kusema maneno haya hawatakoma na uzushi wao na urongo wao, hakika itawapata wao adhabu iliyo kali iumizayo kwa sababu ya kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu.
Mbona Wanaswara hawa hawarudi kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakatubia kwa waliyoyasema na wakamuomba msamaha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Kwani Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, ni Mwenye kuyasamehe madhambi ya wenye kutubia, ni Mwenye huruma kwao.
Hakuwa al-Masih, mwana Maryam isipokuwa ni Mtume kama wale Mitume waliomtangulia; na mamake aliamini Imani ya dhati, kiilimu na kivitendo. Na wote wawili wanahitajia chakula kama walivyo binadamu wengineo. Na anayehitaji chakula ili aishi, hawi ni mungu. Basi izingatie, ewe Mtume, hali ya hawa makafiri.Tumekufafanulia alama zinazoonyesha upweke wetu na ubatilifu wa yale wanayoyadai kuhusu Mitume wa Mwenyezi Mungu. Kisha wao, pamoja na hilo, wanapotea njia ya haki ambayo sisi tunawaongoza waifuate. Kisha hebu angalia, vipi wanaepushwa na haki baada ya ufafanuzi huu?
Sema, ewe Mtume, kuwaambia makafiri hawa, «Vipi mtamshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyeweza kuwadhuru chochote wala kuwaletea manufaa yoyote?» Mwenyezi Mungu Ndiye Mwenye kuyasikia maneno ya waja Wake, Ndiye Mwenye kuzijua hali zao.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia Wanaswara, «Msiikiuke haki katika yale mnayoyaamini kuhusu mambo ya al-Masih. Wala msifuate matamanio yenu kama Mayahudi walivyofuata matamanio yao katika mambo ya dini, wakaingia kwenye upotevu, wakawafanya watu wengi wamkanushe Mwenyezi Mungu na wakatoka kwenye njia nyofu, wakaifuata njia ya upotovu na upotevu.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anatoa habari kwamba Amewafukuza kutoka kwenye rehema Yake makafiri miongoni mwa Wana wa Isrāīl, kama ilivyoandikwa kwenye kitabu ambacho Mwenyezi Mungu Alikiteremsha kwa Dāwūd, amani imshukie, nacho ni Zaburi, na kwenye kitabu Alichokiteremsha kwa Īsā, amani imshukie, nacho ni Injili, kwa sababu ya kuasi kwao na kuyafanyia uadui kwao mambo Aliyoyatukuza Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Walikuwa, Mayahudi hawa, wakiyafanya maasia waziwazi, wakiridhika nayo na hawakuwa wakikatazana wao kwa wao maovu yoyote waliyoyafanya. Na hili ni katika vitendo vyao viovu. Na kwa hilo walistahiki kufukuzwa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Utawaona, ewe Mtume, wengi wa hawa Mayahudi wanawafanya washirikina kuwa ni wategemewa wao. Ni baya mno hilo walilolifanya la mshikamano huo uliokuwa ni sababu ya kukasirikiwa kwao na Mwenyezi Mungu na kukaa kwao milele kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama.
Na lau hawa Mayahudi ambao wanasaidiana na washirikina walikuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakayakubali yale yaliyoteremshwa kwake, nayo ni Qur’ani tukufu, hawangaliwafanya makafiri kuwa ni marafiki na waokozi. Lakini wengi katika wao wako nje ya twaa ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake.
Utakuta tena utakuta, ewe Mtume, kwamba watu wenye uadui mno kwa wale waliokukubali wakakuamini na wakakufuata ni Mayahudi, kwa sababu ya ukaidi wao, ukanushaji wao na kuichukia kwao haki, na wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu kingine, kama wanaoabudu masanamu na wengineo. Na utakuta tena utakuta kwamba walio karibu mno kimapenzi na Waislamu ni wale waliosema, «Sisi ni Wanaswara.» Hilo ni kwamba miongoni mwao kuna wasomi wanaoijua dini yao, wacha-Mungu, wanaofanya jitihadi ya ibada kwenye mindule, na kwamba wao ni wanyenyekevu, hawafanyi kiburi cha kutiubali haki. Hao ndio wale walioukubali ujumbe wa Mtume Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakauamini.
Na miongoni mwa yale yanayoonyesha mapenzi yao kwa Waislamu ni kuwa kundi katika wao (nao ni tume ya watu wa Habashah walipoisikia Qur’ani) yalibubujika machozi macho yao wakawa na yakini kuwa hiyo ni haki iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakamuamini Mwenyezi Mungu, wakamfuata Mtume Wake na wakanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu wakimuomba awatukuze kwa heshima ya kushirikiana na umati wa Muhammad, amani imshukie, katika kuwatolea ushahidi umma wengine Siku ya Kiyama.
Na walisema, «Kwani tuna lawama gani sisi kwa kumuamini kwetu Mwenyezi Mungu, kuikubali haki ambayo alikuja nayo kwetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kumfuata kwetu yeye, na hali tunatumai kuwa Mola wetu Atatutia kwenye Pepo Yake, Siku ya Kiyama, pamoja na walio watiifu Kwake?»
Mwenyezi Mungu Akawalipa, kwa waliyoyasema ya kujienzi kwa kuuamini kwao Uislamu na kutaka kwao kuwa pamoja na watu wema, mabustani ya Pepo ambayo, chini ya miti yake inapita mito, hali ya kukaa humo, hawatatolewa humo wala hawatahamishwa. Hayo ndiyo malipo ya wema wao wa maneno na vitendo.
Na wale ambao waliukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, wakaukataa unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakazikanusha aya Zake zilizoteremshwa kwa Mitume Wake, hao ndio watu wa Motoni wenye kukaa daima humo.
Enyi ambao mliamini, msiharamishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu, miongoni mwa vyakula na vinywaji na kuoa wanawake, mkayatia mkazo mambo ambayo Mwenyezi Mungu Ameyatolea nafasi kwenu, na msipite mipaka ya vitu alivyoviharamisha Mwenyezi Mungu. Kwani Mwenyezi Mungu Hawapendi wenye kupita mipaka.
Na mstarehe, enyi Waumini, kwa halali nzuri Aliyowapa Mwenyezi Mungu na kuwatunukia. Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri Zake na kujiepusha na makatazo Yake. Kwani kumuamini kwenu Mwenyezi Mungu kunawalazimisha nyinyi kumcha Yeye na kumtunza[2].
____________________
[2]Neno la kiarabu hapa ni murāqabah lenye maana ya kuangalia kwa makini, kutunza, kuchunga, kulinda n.k. Makusudio hapa ni kuwa na yakini kuwa Mwenyezi Mungu Akuona, akusikia na azijua harakati zako zote, yakini ambayo inamfanya mtu amuogope Mwenyezi Mungu.Kwa maelezo zaidi, ang. 'Uthaimīn,M.S. Sharh Riy,ād al-Sālihīn, Vol. I, P.324
Mwenyezi Mungu Hatawapa mateso, enyi Waislamu, kwa mayamini mliyoapa bila ya kukusudia, mfano wa vile baadhi yenu wanavyosema, «Sivyo, naapa kwa Mwenyezi Mungu», «Kwa Nini? Naapa kwa Mwenyezi Mungu.» Lakini Yeye Atawapa mateso, kwa sababu ya mayamini mliyoyakusudia ndani ya nyonyo zenu. Basi mkiwa hamtekelezi yamini, dhambi lake litafutwa na Mwenyezi Mungu, kwa kafara mtakayotoa mliyowekewa na Mwenyezi Mungu ya kuwalisha masikini kumi, kila masikini mmoja apewe nusu ya pishi [kadiri ya kilo mbili na nusu] ya chakula cha kati na kati kinachotumiwa na watu wa mji aliyoko, au kuwavisha kwa kumpa kila maskini mavazi yanayomtosha kulingana na desturi, au kuacha huru mmilikiwa kumtoa kwenye utumwa. Basi mwenye kuapa ambaye hakutekeleza yamini lake ana hiari afanye mojawapo ya mambo matatu. Asipopata chochote kati ya hayo, ni juu yake afunge siku tatu. Kufanya hayo ndio kafara ya kutoyatekeleza mayamini yenu. Na yachungeni mayamini yenu, enyi Waumini, kwa kujiepusha na kuapa au kutekeleza kiapo mnapoapa au kutoa kafara msipotekeleza kiapo. Na kama alivyowaelezea Mwenyezi Mungu hukumu ya mayamini na namna ya kujivua nayo, ndivyo Anavyowaelezea hukumu za dini Yake, ili mumshukuru Yeye kwa kuwaongoza nyinyi kwenye njia iliyolingana sawa.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo! Hakika pombe: nayo ni kila kinacholewesha kinachofinika akili, al-maysir, nayo ni kamari ambayo inakusanya aina za kuwekeana dau na mfano wake, kama zile za kuekeana badali kutoka pande mbili za wacheza kamari na kuzuia kumtaja Mwenyezi Mungu, al-ansab: mawe ambayo washirikina walikuwa wakichinja mbele yake kwa njia ya kuyatukuza na yale yanayosimamishwa ili kujisongeza karibu yake kwa ibada na al-azlam: vipande vinavyotumiwa na makafiri kutafuta uamuzi kabla ya kufanya au kuacha kufanya jambo. Hayo yote ni dhambi inayopambiwa na Shetani. Basi jiepusheni na madhambi haya, huenda nyinyi mkafuzu kwa kupata Pepo.
Hakika Shetani anataka, kwa kuwapambia madhambi, kuweka baina yenu chenye kuleta uadui na chuki, kwa sababu ya kunywa pombe na kucheza kamari, na kuwaepusha na kumtaja Mwenyezi Mungu na kuswali, kwa kutokuwa na akilil katika unywaji pombe na kujishughulisha na pumbao la uchezaji kamari. Basi komekeni na hayo.
Na Fuateni amri, enyi Waislamu, ya kumtii Mwenyezi Mungu na kumtii Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, katika kila mnalolifanya na mnaloliacha. Na mcheni Mwenyezi Mungu na mumtunze katika hayo. Na mkikataa kufuata amri na mkayafanya mliyokatazwa, basi jueni kuwa jukumu la mjumbe wetu Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni ufikishaji ulio wazi.
Waumini waliokunywa pombe kabla haijaharamishwa hawana dhambi kwa kufanya hilo, iwapo wataiacha, wakajikinga na mambo yanayomkasirisha Mwenyezi Mungu na wakatanguliza matendo mema yanayoonyesha kuwa wao wanamuamini Yeye na wana hamu Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, Awe radhi nao, kisha wakazidi kumtunza Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, na kumuamini mpaka wakawa, kwa ile yakini yao, wanamuabudu kama kwamba wao wanamuona. Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawapenda wale ambao wamefikia kiwango cha ihsani (iḥsān) mpaka wakawa kuiamini kwao ghaibu (al-ghayb) ni kama vile wanavyoyaamini wanayoyaona.[3]
____________________
[3]Rudia 2:3 kwa ufafanuzi wa al-ghyb.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, Mwenyezi Mungu Atawapa mtihani wa baadhi ya viwindwa vya barani, watakaokuja karibu na nyinyi kwa namna isiyo ya kawaida muweze kuwashika wadogo wao bila kutumia silaha na kuwashika wakubwa wao kwa kutumia silaha, ili Mwenyezi Mungu Awajue, ujuzi uliyofunuka wazi kwa viumbe, wale wanaomuogopa Mola wao kwa ghaibu kwa kuwa wana yakini kuwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuhusu wao umekamilika, na kwa hivyo waache kuwinda wakiwa katika hali ya ihram (ihramu: kuingia kwenye ibada ya Hija au Umra). Basi yoyote mwenye kuvuka mpaka wake, baada ya maelezo haya, akafanya ujasiri wa kuwinda, na hali yeye yuko kwenye ihramu, anastahili adhabu kali.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Zake kivitendo, msiue viwindwa wa barani na nyinyi muko kwenye ihramu ya Hija au Umra au mkawa muko ndani ya Haram. Na yoyote mwenye kuua kiwindwa yoyote kati ya viwindwa wa barani kwa kusudi, basi malipo yake ni achinje, miongoni mwa wanyama- howa: ngamia au ng’ombe au mbuzi na kondoo, anayefanana na kiwindwa huyo, baada ya waadilifu wawili kumfanyia makadirio, na amgawe kwa masikini wa eneo la Ḥarām au anunue chakula kwa thamani ya mfano wake na awagawie masikini wa eneo la Haram, kila masikini nusu pishi au afunge, badala yake, siku moja kwa kila nusu pishi ya chakula hicho. Mwenyezi Mungu Ameyapasisha malipo haya , ili mkosa apate matokeo ya kitendo chake. Na wale ambao ilitukia kwao kufanya lolote kama hilo kabla ya kuharamishwa, basi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ashawasamehe. Na yoyote mwenye kurudia uhalifu huo kwa kusudi, baada ya kuharamishwa, huyo amejihatarisha kupata mateso ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu katika mamlaka Yake, na miongoni mwa enzi Yake ni kuwa Yeye atamtesa anayemuasi Akitaka, hakuna chenye kumzuia kufanya hivyo.
Mwenyezi Mungu Amewahalalishia, enyi Waislamu, mtapokuwa kwenye hali ya ihramu, viwindwa wa baharini, nao niwale wavuliwao baharini wakiwa hai, na chakula chake, nacho ni kiumbe kilichokufa kitokacho humo, kwa ajili mnufaike mkiwa ni wakazi au ni wasafiri. Na Ameharamishia viwindwa wa barani muko kwenye ihramu ya Hija au ya Umra. Na muogopeni Mwenyezi Mungu na mtekeleze amri Zake zote na mjiepushe na makatazo Yake yote, mpaka mfuzu kwa thawabu Zake kubwa na msalimike na ukali wa mateso Yake mnapofufuliwa ili mhesabiwe na mlipwe.
Mwenyezi Mungu Amewafadhili waja Wake kwa kuijaalia Alkaba, Nyumba takatifu, ni utengenefu wa Dini yao na amani ya uhai wao. Hivyo ni kwa kuwa wamemuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakasimamisha faradhi Zake. Na Ameharamisha uadui na kupigana katika miezi mitakatifu (nayo ni Mfungopili, Mfungotatu, Mfungone na Rajabu) ili mtu yoyote asimfanyie mwingine uadui katika miezi hiyo. Na Ameharamisha, Aliyetukuka, kuwavamia wanyama- howa wanaotolewa kuwa ni tunu kwa Haram. Kadhalika, Ameharamisha kuvivunjia heshima qalaid, navyo ni vitu vilivyovishwa shingoni mwa hao wanyama kuonyesha kuwa wanakusudiwa kuchinjwa kwa ibada. Hivyo basi, ni mupate kujua kuwa Mwenyezi Mungu Anayajua yote yaliyo mbinguni na ardhini, miongoni mwayo ni sheria Alizoziweka kuwahami viumbe Wake wasidhuriane wao kwa wao. Na pia mupate kujua kwamba Mwenyezi Mungu kwa kila kitu ni Mjuzi, hakuna chochote chenye kufichika Kwake.
Jueni, enyi watu, kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni Mkali wa mateso kwa anyemuasi na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa Kusamehe, ni Mwingi wa rehema kwa anayetubia na kurejea.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anawaelezea kwamba shughuli ya Mtume Wake , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, ni kuongoza kwa kuelekeza na kufikisha na kwamba uongofu wa taufiki uko mkononi mwa Mwenyezi Mungu, Peke Yake, na kwamba mambo yaliyomo ndani ya nafsi za watu, katika yale wanayoyafanya kwa siri na wanayoyatangaza, ya uongofu na upotevu, Mwenyezi Mungu Anayajua..
Sema, ewe Mtume, «Hakilingani kiovu na chema cha kila kitu»: Kafiri halingani na Muumini, mwenye kuasi halingani na mtiifu, mjinga halingani na mjuzi, na mwenye kufanya uzushi halingani na mwenye kufuata njia, na mali ya haramu hayalingani na ya halali, ingawa unakuvutia wewe, ewe binadamu, wingi wa viovu na idadi kubwa ya watu wake. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili bora, kwa kujiepusha na machafu na kufanya mazuri, mpate kufuzu kwa kulifikia lengo kubwa, nalo ni radhi ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kufaulu kupata Pepo.
Enye ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, msiulize mambo ya Dini ambayo hamkuamrishwa chochote kuhusu hayo, kama kuuliza kuhusu mambo ambayo hayajatukia au yale ambayo yatapelekea mikazo ya Sheria ambayo lau mlikalifishwa nayo yangalikuwa ni magumu kwenu, na lau mliyauliza wakati wa uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, wakati Qur’ani inateremka, mungalielezewa, na pengine mkakalifishwa nayo na mkalemewa nayo. Hayo Mwenyezi Mungu Ameyaacha ili kuwapumzisha waja Wake nayo. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehefu sana kwa waja wake wanapotubia, ni Mpole sana kwao, Hawaadhibu wakirudi Kwake.
Mfano wa maswali hayo, waliwahi waliokuwa kabla yenu kuwauliza Mitume wao. Walipoamrishwa yale waliokuwa wakiyauliza waliyakanusha na wasiyatekeleze. Basi, tahadharini msiwe kama wao.
Mwenyezi Mungu Hakuwawekea washirikina yale waliyoyazua ya kuacha kunufaika na baadhi ya wanyama wa mifugo na kuwafanya ni wa masanamu. Nao ni baḥīrah: anayekatwa sikio lake akiwa amezaa idadi fulani ya watoto, sāibah: anayeachiwa masanamu, waṣīlah: ambaye amezaa watoto wa kike mfululizo na hāmī: ngamia dume iwapo, kutokana na yeye, wamazaliwa idadi fulani ya ngamia. Lakini makafiri waliyanasibisha hayo kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kumzulia urongo. Na wengi wa makafiri hawapambanui baina ya haki na batili.
Na hawa makafiri, wanaoharamisha yaliyohalalishwa na Mwenyezi Mungu, wanapoambiwa, «Njooni kwenye hukumu zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu na uwamuzi wa Mtume Wake, ili halali na haramu ziwafunukie, wao huwa wakisema, «Yanatutosha yale tuliyoyarithi kwa baba zetu ya maneno na vitendo.» Je wanayasema hayo ingawa baba zao walikuwa hawajui chochote: yaani, hawaielewi haki, hawaitambui wala hawaongoki kuifikia? Basi vipi watawafuata na hali ni hii? Kwa kweli, hakuna mwenye kuwafuata isipokua mjinga zaidi kuliko wao na mpotevu zaidi wa njia.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, jilazimisheni nafsi zenu kujishughulisha kumtii Mwenyezi Mungu na kujiepusha na kumuasi na endeleeni daima kufanya hivyo, hata kama watu hawatakubaliana na nyinyi. Mkifanya hivyo, hautawadhuru nyinyi upotevu wa mwenye kupotea madhali nyinyi mnajilazimisha na njia ya usawa, mnaamrisha mema na mnakataza maovu. Kwa Mwenyezi Mungu ndiko marejeo yenu nyote kesho Akhera, huko atawapa habari ya matendo yenu na atawapa malipo yake.
Enyi ambao mlimuamini Mwenyezi Mungu, Mtume Wake na mkafuata sheria Yake kivitendo, mmoja wenu akiwa karibu na kufa, basi ni juu yake awashuhudishe wasia wake waaminifu wawili miongoni mwa Waislamu, au wawili wengine miongoni mwa wasiokuwa Waislamu ikibidi hivyo, na kusiwe na Waislamu. Hao mtawashuhudisha iwapo muko safarini kwenye ardhi na mkafikiwa na kifo. Na iwapo mtautilia shaka ushahidi wao, wasimamisheni baada ya Swala, yaani, swala ya Waislamu, hasa Swala ya Alasiri, waape kwa Mwenyezi Mungu kiapo cha dhati kwamba wao hawachukui kwa ushahidi wao thamani ya kilimwengu kama badala, wala hawamfanyii mapendeleo jamaa yao na wala hawafichi kwa kiapo chao ushahidi wa Mwenyezi Mungu uliyoko kwao na kwamba wao wakilifanya hilo, basi wao watakuwa ni miongoni mwa waliofanya hatia.
Wakigundua wanaohusika na maiti kuwa wale mashahidi wawili wamefanya makosa ya hiana katika ushahidi au wasia, basi na wasimame mahali pao pa ushahidi watu wawili wenye ujamaa na aliyekufa waape kwa Mwenyezi Mungu: Ushahidi wetu wa kweli unastahiki zaidi kukubaliwa kuliko ushahidi wao wa urongo. Na sisi hatukukiuka haki katika kutoa ushahidi wetu. Na tukifanya dhuluma na kutoa ushahidi usio wa haki, basi sisi tutakuwa ni miongoni mwa madhalimu wenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.
Hukumu hiyo ya kuapa baada ya Swala na kutokubali ushahidi wa hao wawili, baada ya kuutilia shaka, ndiyo inayouleta karibu zaidi uwezekano wa wao kutoa ushahidi kama ulivyo kwa kuogopa adhabu ya Akhera au kwa kuchelea yamini lao la urongo lisikataliwe na wale wenye haki baada ya kuapa kwao na asije akafedheheka yule mrongo ambaye yamini lake lilikakataliwa hapa ulimwenguni baada ya kufunuka uhaini wake. Na muogopeni Mwenyezi Mungu, enyi watu, na mumtunze msije mukaapa kiapo cha urongo na msije mkanyakuwa kwa mayamini yenu mali ya haramu. Na msikie mnayowaidhiwa nayo. Na Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu wenye nyendo mbaya waliotoka nje ya utiifu Wake.
Na ikumbukeni, enyi watu, Siku ya Kiyama, siku Mwenyezi Mungu atakapo kuwakusanya Mitume, amani iwashukie, na awaulize kuhusu majibu ya watu wao waliyoyapata, pindi walipowalingania kwenye tawhīd (kumpwekesha Mwenyezi Mungu). Na wao watajibu, «Hatuna ujuzi, sababu hatuyajui yaliyomo ndani ya nyoyo za watu wala yale waliyoyazua baada yetu. Hakika yako wewe ni Mjuzi wa kila kitu kilichofichika na kilicho wazi.
Atakaposema Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Kumbuka neema yangu kwako, nilipokuumba bila ya baba, na kwa mamako, nilipomteua juu ya wanawake wa ulimwengu na nikamuepusha na hatia aliyobandikwa nayo.» Miongoni mwa neema hizi kwa ‘Īsā ni kwamba Mwenyezi Mungu Alimpa nguvu na Akamsaidia kwa Jibrili, amani imshukie, akasema na watu na yeye ni mchanga wa kunyonya kabla ya wakati wa kusema na akawaita wao kuja kwa Mwenyezi Mungu na yeye ni mkubwa, nguvu zake zimeshikana, na ubarobaro wake umekamilika, kwa wahyi wa tawhīd ambao Mwenyezi Mungu Alimletea. Na miongoni mwa hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Alimfundisha kuandika na (kusoma) maandishi bila ya mwalimu, Alimpa nguvu ya kufahamu na kuelewa, Alimfundisha Taurati Aliyomteremshia Mūsā, amani imshukie, Injili Aliyomteremshia yeye ili kuwaongoza watu. Na miongoni mwa neema hizi ni kwamba yeye anasinyanga kwa udongo kama umbo la ndege na kisha anapuliza kwenye umbo hilo na likawa ni ndege kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamponyesha aliyezaliwa kipofu akawa anaona na anamponyesha mwenye mbalanga ikarudi ngozi yake kuwa na uzima kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na miongoni mwazo ni kwamba yeye anamuomba Mwenyezi Mungu Awahui wafu, na wakainuka kutoka kwenye makaburi yao wakiwa hai. Yote hayo ni kwa matakwa Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka, na idhini Yake. Nayo ni miujiza yenye kushinda, inautilia nguvu unabii wa ‘Īsā, amani imshukie. Kisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Anamkumbusha neema Yake kwake alipowazuia Wana wa Isrāīl walipotaka kumuua na akawajia wao na miujiza iliyo wazi yenye kuonyesha dalili za unabii wake. Hapo walisema waliokufuru kati yao, «Hakika haya aliyokuja nayo ‘Īsā, miongoni mwa dalili zilizo wazi, ni uchawi uliofichuka.
Na ukumbuke, ewe ‘Īsā, nilipotia ilhamu na msukumo katika nyoyo za watu, miongoni mwa wale waliosafiwa nawe, kuwafanya wauamini upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na unabii wako, wakasema, «Tumeamini, ewe Mola wetu. Na ushuhudie kuwa sisi ni wenye kukunyenyekea na ni wenye kufuata kwa utiifu amri Yako.
Na ukumbuke waliposema Ḥawāriyyūn (wasafiwa wa Nabii ‘Īsā kati ya wafuasi wake), «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Je, Anaweza Mola wako, ukimuomba, kututeremshia meza ya chakula kutoka mbinguni?» Jawabu yake ilikuwa ni kuwataka wao wajikinge na adhabu ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakiwa ni wenye kuamini Imani ya kikweli.
Ḥawāriyyūn wakasema, «Tunataka kula kutoka kwenye meza hiyo, nyoyo zetu zipate kutulia kwa kuishuhudia, tupate kujua kwa yakini ukweli wako kuhusu unabii wako na tupate kuwa ni wenye kuishuhudia miujiza hii kwamba Mwenyezi Mungu Ameiteremsha iwe ni hoja kwetu juu ya upweke Wake na uwezo Wake kufanya Alitakalo na pia iwe ni hoja kwako juu ya ukweli kuhusu unabii wako.»
‘Īsā mwana wa Maryam Aliyakubali matakwa ya Ḥawāriyyūn akamuomba Mola wake , Aliyetukuka na kuwa juu, kwa kusema, «Mola wetu! Tuteremshie meza ya chakula kutoka mbinguni, tupate kuifanya siku hiyo ya kuteremka kwake ni sikukuu kwetu, sisi tutaitukuza na pia watakaokuja baada yetu, na hiyo meza itakuwa ni alama na ni hoja kutoka kwako , ewe Mwenyezi Mungu, juu ya upweke wako na juu ya ukweli wa unabii wangu, na ututunuku miongoni mwa vipewa vyako vyingi, na wewe ndiye bora wa wenye kuruzuku.»
Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, Akasema, «Mimi ni Mwenye kuwateremshia Meza ya chakula. Basi yoyote mwenye kuukanusha upweke wangu, miongoni mwenu, na unabii wa ‘Īsā, amani imshukie, baada ya kuteremka meza, nitamuadhibu adhabu kali ambayo sitamuadhibu nayo yoyote miongoni mwa viumbe.» Meza iliteremka kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu.
Na kumbuka pindi atakaposema Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Siku ya Kiyama, «Ewe ‘Īsā mwana wa Maryam! Kwani wewe uliwaambia watu, ‘nifanyeni mimi na mamangu kuwa ni waabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu’?» ‘Īsā akajibu, kwa kumtakasa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kumuepusha na sifa za upungufu, «Haipasii kwangu kuwaambia watu yasiyokuwa haki. Nikiwa nimesema hili, basi ushalijua. Kwani hakuna chochote kinachofichika kwako. Wewe unayajua yaliyomo ndani ya nafsi yangu, na mimi siyajui yaliyomo ndani ya nafsi yako. Hakika yako wewe Ndiye Mjuzi wa kila kitu, kilichofichamana au kuwa wazi.»
‘Īsā, amani imshukie, atasema, «Ewe Mola wangu! Sikuwaambia wao isipokuwa yale uliyonitumia wahyi nayo na ukaniamrisha kuyafikisha, ya kukupwekesha wewe tu na kukuabudu. Na mimi nilikuwa nikishuhudia vitendo vyao na maneno yao nilipokuwa nikiishi na wao. Na uliponikamilishia muda wangu wa kuishi kwenye ardhi, ukanipaza mbinguni nikiwa hai, ulikuwa wewe ndiye Mwenye kuzichungulia siri zao, na wewe ni Mwenye kushuhudia kila kitu, hakifichiki kwako chochote cheneye kufichika ardhini au mbinguni.
Hakika yako wewe , ewe Mwenyezi Mungu, ukiwa utawaadhibu, basi wao ni waja wako, na wewe ndiye Mjuzi wa hali zao, unawafanya unavyotaka kwa uadilifu wako. Na ukiwa utawasamehe, kwa rehema yako, wale waliofuata njia za kuwafanya wasamehewe, basi wewe ndiye Mshindi Asiyeshindwa, Mwenye hekima katika uendeshaji mambo Wake na amri Zake. Aya hii inamsifu Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa hekima Yake, uadilifu Wake na ukaimilifu wa ujuzi Wake.
Mwenyezi Mungu Atamwambia ‘Īsā Siku ya Kiyama, «Hii ndiyo Siku ya Malipo ambayo kutawafaa wale waliompwekesha Mwenyezi Mungu kule kumpwekesha kwao Mola wao na kufuata kwao sheria Yake, ukweli wao wa nia zao, maneno yao na matendo yao. Watakuwa na mabustani ya Pepo, inayopita mito chini ya majumba yake ya fahari, hali ya kukaa humo milele. Mwenyzi Mungu Ameridhika nao ndipo Akayakubali mema yao, na wao wameridhika na Yeye kwa malipo mazuri mengi aliyowapa. Malipo hayo na kuwa Yeye Ameridhika na wao ndiko kufuzu kukubwa.
Ni wa Mwenyezi Mungu Peke Yake ufalme wa mbinguni na ardhini na vilivyomo ndani yake, na Yeye, Aliyetakata na kila sifa mbaya, kwa kila kitu ni muweza; hakuna kitu kinachomshinda.