ﮒ
surah.translation
.
ﰡ
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, Mwenye sifa ambazo zote ni sifa za ukamilifu, Mwenye neema za nje na za ndani, za kidini na za kidunia, Ambaye Aliumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, Aliumba giza na mwangaza kwa kupishana usiku na mchana. Katika hili pana ishara ya utukufu wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kuwa Yeye Peke Yake Anastahiki kuabudiwa. Haifai kwa yoyote kumshirikisha mwengine na Yeye. Na pamoja na uwazi huu, makafiri wanamsawazisha mwingine na Mwenyezi Mungu na wanamshirikisha na Yeye.
Yeye Ndiye Ambaye Alimuumba baba yenu Ādam kutokana na udongo na nyinyi mnatokana na kizazi chake, kisha Akaandika muda wa kusalia kwenu katika uhai huu wa kilimwengu, na Akaandika muda mwingine maalumu hakuna aujuwao isipokuwa Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, nayo ni Siku ya Kiyama. Kisha nyinyi baada ya haya mnashuku juu ya uwezo wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wa kufufua baada ya kufa.
Na Mwenyezi Mungu, Aliyetakata na kila sifa ya upungufu, Ndiye Mola Mwenye kuabudiwa kwa haki mbinguni na ardhini. Na miongoni mwa dalili za uungu wake ni kwamba Yeye Anayajua yote mnayoyaficha, enyi watu, na mnayoyadhihirisha na Anayajua matendo yenu yote, mazuri na mabaya. Na kwa ajili hii, Yeye Peke Yake, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye Mola Anayestahiki kuabudiwa.
Makafiri hawa Ambao wanamshirikisha mwingine na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wamejiwa na hoja zilizo wazi na dalili dhahiri juu upweke wa Mwenyezi Mungu, Aiyetukuka na kuwa juu, na ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, juu ya utume wake na yale aliyokuja nayo. Lakini punde tu yalipowajia waliyaepuka na kukataa kuyakubali na wasiyaamini.
Makafiri hawa waliikataa haki ambayo alikuja nayo Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na wakawafanyia shere walinganizi wake kwa sababu ya ujinga walionao kuhusu Mwenyezi Mungu na kughurika kwao na muhula Aliowapa. Basi watakuja kuyaona yale waliyoyafanyia shere kuwa ni haki na ni kweli. Na Mwenyezi Mungu Atawabainishia wakanushaji urongo wao na uzushi wao na awalipe kwa hayo.
Kwani hawayajui, hawa wanaoukanusha upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kustahiki Kwake, Peke Yake, kuabudiwa na wanaomkanusha Mtume Wake Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,, yale yaliyowashukia watu waliokanusha kabla yao ya maangamivu na uharibifu? Hao tuliwapa utulivu kwenye ardhi kwa namna ambayo hatukuwapa nyinyi, enyi makafiri, utulivu kama huo na tuliwaneemesha kwa kuwateremshia mivua na kupita mito chini ya makao yao kwa njia ya kuwanyoshea na kuwapa muhula, wakazikanusha neema za Mwenyezi Mungu na wakawakanusha Mitume. Hapo tuliwaangamiza kwa sababu ya madhambi yao na tukawaumba baada yao watu wengine walioshika nafasi zao katika kuiamirisha ardhi.
Na lau tulikuteremshia kitabu kutoka mbinguni, katika kurasa, wakazigusa washirikina hawa kwa mikono yao, wanagalisema, «Uliokuja nao ni uchawi ulio wazi uliobainika».
Na walisema washirikina hawa, «Si Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amteremshie Muhammad Malaika kutoka mbinguni ili amsadiki kwa yale aliyokuja nayo Ya utume.» Na lau tulimteremsha Malaika kutoka mbinguni kwa kujibu ombi lao, uamuzi wa kuwaangamiza ungalipitishwa, na wasingepewa muhula wa kutubia, kwani imetangulia kwenye ujuzi wa Mwenyezi Mungu kuwa wao hawataamini.
Na lau kama tulimfanya mtume aliyeteremshwa kwao ni Malaika, kwani hawakukinai na Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, tungalimfanya Malaika huyo kwenye sura za mwanadamu, ili waweze kumsikia na kusema naye. Kwani haimkiniki kwao kumuona Malaika katika sura zake za kimalaika. Na lau Malaika aliwajia kwa sura za mtu, jambo hilo lingaliwafanya wachanganyikiwe kama lilivyowafanya wachanganyikiwe jambo la Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Na kwa kuwa kutaka kwao kuteremshwa Malaika kulikuwa ni kwa njia ya kumfanyia shere Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, Mwenyeyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwaelezea kwamba kuwafanyia shere Mitume, amani iwashukie, si jambo jipya; kwani jambo hilo lilitukia kwa makafiri waliopita kuwafanyia Mitume wao, wakazungukwa na adhabu ambayo walikuwa wakiifanyia shere na wakipinga kuja kwake.
Sema kuwaambia, ewe Mtume, «Endeni katika ardhi kisha muangalie: namna gani Mwenyezi Mungu aliwaletea maangamivu na hizaya mwishoni? Basi tahadharini yasiwafikie mfano wa maanguko yao, na ogopeni yasije yakawashukia nyinyi kama yale yaliyowashukia wao.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Ni ya nani mamlaka ya mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake?» Sema, «Ni ya Mwenyezi Mungu. Na kama mnavyolikubali hilo na kulijua, basi muabuduni Yeye Peke Yake. Mwenyezi Mungu Amechukua ahadi juu ya nafsi Yake kurehemu, Hatawaangusiliza waja Wake kwa kuwatesa. Kwa hakika Atawakusanya nyinyi kwenye Siku ya Kiyama ambayo haina shaka ili mhesabiwe na mlipwe. Wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu wamejiangamiza nafsi zao; wao hawampwekeshi Mwenyezi Mungu wala hawaiamini ahadi Yake ya Pepo na Moto na hawaukubali unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.
Ni wa Mwenyezi Mungu umiliki wa kila kitu, kilicho mbinguni na ardhini, kilichotulia na kinachotembea, kilichofichika na kilicho wazi. Vyote ni watumwa Wake na viumbe Vyake na viko chini ya utendeshaji nguvu Wake, uendeshaji Wake na upangaji Wake. Yeye Ndiye Msikizi wa maneno ya waja Wake, Ndiye Mjuzi wa siri zao na matendo yao.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na asiyekuwa Yeye, «Je, nimchukue asiyekuwa Mwenyezi Mungu kuwa ni msaidizi na ni mwokozi, na hali Yeye ni Muumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake, na Yeye Ndiye Mwenye kuwaruzuku viumbe Wake na hakuna mwenye kumruzuku Yeye?» Sema,ewe Mtume, «Mimi nimeamrishwa niwe ni wa mwanzo aliyemnyenyekea Yeye na kumwandama katiika umma huu. Na nimekatazwa kuwa ni miongoni mwa wanaomshirikisha Yeye na asiyekuwa Yeye.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asiyekuwa Yeye, «Mimi naogopa nikimuasi Mola wangu, nikaenda kinyume na maamrisho Yake, na nikamshirikisha Yeye na asiyekuwa Yeye, kuteremkiwa na adhabu kubwa Siku ya Kiyama.
Yule ambaye Mwenyezi Mungu Amemuepushia adhabu kali hiyo, basi Amemrehemu. Kuepushwa huko ndiko kufaulu kuliko wazi kwa kuokolewa na adhabu kubwa.
Na Akikupatia Mwenyezi Mungu jambo la kukudhuru, kama ufukara na ugonjwa, hakuna mwenye kuliondoa hilo isipokuwa Yeye; na Akikupatia zuri, kama utajiri na afya, hakuna mwenye kuondoa wema wake na hakuna mwenye kuzuia mapitisho Yake, kwani Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, ni muweza wa kila kitu.
Mwenyezi Mungu, Aliyetakasika na kila sifa ya upungufu, Ndiye Mwenye kutendesha nguvu, Aliye juu ya waja Wake. Shingo zimemdhalilikia na majabari wamenyongeka Kwake. Yeye Ndiye Mwenye hekima Anayeweka vitu mahali pake kulingana na hekima Yake. Ndiye Mtambuzi Ambaye hakuna kitu chenye kufichika Kwake. Na mwenye kusifika na sifa hizi inapasa asishirikishwe. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya ujuu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kuwa Yuko juu ya ya viumbe vyake vyote; ujuu wa aina zote unaonasibiana na utukufu Wake, kutakasika na kila sifa ya upungufu ni Kwake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Ni kitu gani chenye ushahidi zaidi katika kuthibitisha ukweli wangu katika haya ninayowaambia kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu?» Sema, «Mwenyezi Mungu ni shahidi baina yangu mimi na nyinyi.» Yaani: yeye Ndiye Mjuzi wa niliyokuja nayo kwenu na yale mtakayonambia. «Na Mwenyezi Mungu Ameniletea mimi Qur’ani hii kwa njia ya wahyi ili ni waonye nayo adhabu ya Mwenyezi Mungu isiwashukie, na niwaonye nayo ummah wengine ambao itawafikia.» Nyinyi mnakubali kwamba, pamoja na Mwenyezi Mungu, pana waabudiwa wengine mnaowashirikisha Naye. Waambie, ewe Mtume, «Mimi sitoi ushahidi juu ya lile mlilolikubali. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola mmoja Asiye na mshirika. Na mimi nimejiepusha na kila mshirika mnayemuabudu pamoja na Yeye.
Wale tuliowapa Taurati na Injili wanamjua Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, kwa sifa Zake zilizoandikwa kwao kama wanavyowajua watoto wao. Na kama ilivyo wao hawachanganyikiwi kuwajua watoto wao walio mbele yao kuwapambanua na wengine, vilevile Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hachanganyiki na mwingine, kwa sababu ya uwazi wa sifa zake zilizo ndani ya vitabu vyao. Lakini wao walifuata matamanio yao, walipomkanusha Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na yale aliyokuja nayo, ndipo wakapata hasara nafsi zao.
Hakuna yoyote mwenye udhalimu mbaya zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, urongo na akadai kwamba Yeye Ana washirika katika ibada, au akadai kwamba Yeye Ana mtoto au mke, au akazikanusha hoja Zake na dalili ambazo kwazo Aliwapa nguvu Mitume Wake, amani iwashukie. Hakika ya mambo ni kwamba madhalimu waliomzulia Mwenyezi Mungu urongo hawafaulu na hawapati matakwa yao ulimwenguni wala Akhera.
Na wajihadhari washirikina hawa wenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Siku ambayo tutawafufua kisha tutasema kuwaambia, «Wako wapi waungu wenu ambao mlikuwa mkidai kuwa wao ni washirika na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ili wawaombee nyinyi?»
Kisha hayakuwa majibu yao, walipojaribiwa na kupewa mtihani kwa kuulizwa kuhusu washirika wao, isipokuwa walijitoa na wao na wakaapa kwamba wao hawakuwa ni wenye kumshirikisha yoyote na Mwenyezi Mungu.
Fikiri, ewe Mtume, vipi washirikina hawa wanasema urongo juu ya nafsi zao, na wao kesho Akhera watajiepusha na ushirikina! Yatawaondokea wao na kuwapotea yale waliokuwa wakiyadhania ya kuwa waungu wao watawaombea.
Kati ya washirikina hawa kuna wanaokusikiliza usomapo Qur’ani, ewe Mtume, na isifike kwenye nyoyo zao. Kwa kuwa wao, kwa sababu ya kufuata matamanio yao, tumeweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasipate kuifahamu Qur’ani. Na tumejaalia kwenye masikio yao uzito na uziwi, hayasikii wala hayafahamu chochote. Na wanapoziona dalili nyingi zenye kuonyesha ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, hawaziamini. Na hata wakikujia , ewe Mtume, baada ya kuzishuhudia dalili zenye kuonesha ukweli wako, huwa wakisema wenye kuzikanusha aya za Mwenyezi Mungu, «Haya tunayoyasikia si chochote isipokuwa ni ngano zinazohadithiwa na watu wa kale zisizo na ukweli.»
Na washirikina hawa wanawakataza watu kumfuata Mtume Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kumsikiliza, na wao wenyewe wanajiepusha naye. Na wao hawamuangamizi yoyote, kwa kuzuia kwao njia ya Mwenyezi Mungu isifuatwe, isipokuwa nafsi zao wenyewe, na wao hawatambui kuwa wajishughulisha na mambo ya kuzitia kwenye maangamivu.
Na lau utawaona, ewe Mtume, washirikina hawa Siku ya Kiyama, utaona jambo kubwa, nalo ni wakati wao watakapofungwa juu ya Moto, na watakaposhuhudia yaliyomo humo miongoni mwa minyororo na pingu, na kujionea kwa macho yao mambo makubwa hayo na vituko hivyo. Hapo watasema, «Twatamani turudishwe kwenye maisha ya kilimwengu, tupate kuziamini aya za Mwenyezi Mungu na tuzitumie na tuwe ni miongoni mwa Waumini.»
Mambo si kama hivyo! Bali Siku ya Kiyama yatawadhihirikia wao yale waliokuwa wakiyafanya kwa nafsi zao, ya kuamini ukweli wa yale ambayo Mitume walikuja nayo ulimwenguni, ingawa walikuwa wakiwadhihirishia wafuasi wao kinyume chake. Na lau ilikadiriwa warudishwe ulimwenguni na waongezewe muda, wangalirudi kwenye upinzani kwa kukufuru na kukanusha. Na kwa kweli wao ni warongo katika neno lao, «Lau tutarudishwa ulimwenguni hatungalizikanusha aya za Mola wetu na tungalikuwa Waumini.»
Na hawa washirikina wanaokanusha kufufuliwa wanasema, «Hakuna maisha isipokuwa maisha haya tuliyonayo, na sisi si wenye kufufuliwa baada yakufa kwetu.»
Na lau utawaona, ewe Mtume, wenye kukanusha kufufuliwa watakapofungwa mbele ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ili uamuzi wa Mwenyezi Mungu upite kuhusu wao Siku ya Kiyama, ungaliona hali mbaya sana, pindi Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, Atakaposema, «Je, ufufuzi huu, mliokuwa mkiukanusha ulimwenguni, si kweli?» Watasema, «Kwani? Tunaapa kwa Mola wetu kuwa huu ni kweli.» Hapo Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema, «Basi onjeni adhabu kwa mlivyokuwa mkikufuru,» yaani, adhabu ambayo mlikuwa mkiikanusha ulimwenguni kwa sababu ya kumkataa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Mtume Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Hakika wamepata hasara wale waliokanusha kufufuliwa baada ya kufa. Mpaka Kiyama kitakaposimama na wakashutushwa kwa mwisho mbaya, watazipigia nafsi zao kelele za majuto juu ya kile walichokipoteza katika maisha yao ya ulimwenguni, hali ya kwamba wanabeba madhambi yao juu ya migongo yao. Ni mibaya iliyoje mizigo hiyo mizito iliyo miovu ambayo wataibeba!
Maisha ya kilimwengu hayakuwa, katika wingi wa hali zake, isipokuwa ni udanganyifu na ubatilifu. Na matendo mema, kwa kutengeneza nyumba ya Akhera, ndiyo bora kwa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, wakajikinga na adhabu Yake kwa kumtii na kujiepusha na mambo ya kumuasi. Kwani hamuelewi, enyi washirikina mlioghurika na pambo la uhai wa kilimwengu, mukayatanguliza yanayosalia mbele ya yanayomalizika?
Hakika sisi tunajua kwamba msimamo wa kaumu zako wa kukukanusha waziwazi unakutia huzuni moyoni mwako. Basi subiri na ujitulize. Kwani wao hawakukanushi wewe kutoka ndani ya roho zao; wao waamini ukweli wako, lakini wao kwa udhalimu na uadui walionao, wanazikataa hoja zilizo wazi zinazoonyesha ukweli wako, ndipo wakakufanya mrongo kwa yale uliyokuja nayo.
Hakika makafiri waliwakanusha Mitume kabla yako Aliyowatuma Mwenyezi Mungu, Aliyotukuka, kwa umma wao. Wao waliudhiwa katika kufuata njia Yake na wakasubiri juu ya hilo na wakaendelea katika ulinganizi wao na bidii yao mpaka ikawajia nusura ya Mwenyezi Mungu. Na hakuna mwenye kuyageuza maneno ya Mwenyezi Mungu, nayo ni yale Aliyoyateremsha kwa Nabii Wake Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, yenye ahadi Yake kwamba Atampa ushindi juu ya wanaomfanyia uadui. Na hakika imekujia wewe, ewe Mtume, habari ya Mitume waliokuwa kabla yako na nusura ya Mwenyezi Mungu iliyohakikishika kwao na mateso ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu Zake zilizowafikia wenye kuwakanausha. Basi wewe una kiolezo chema na mfano wa kuiga kutoka kwa Mitume waliotangulia. Katika hili pana kumliwaza Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie,.
Na iwapo umekuwa ni mzito kwako, ewe Muhammad, upinzani wa hawa washirikina na kujiepusha kwao kukubali ulinganizi wako, basi ukiweza kujifanyia mapito ndani ya ardhi, au ngazi ya kupandia mbinguni ili uwaletee alama na dalili ya usahihi wa maneno yako, zisizokuwa hizi tulizokuletea, fanya hivyo. Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka kuwakusanya kwenye uongofu ambao nyinyi munao na kuwaongoza kwenye Imani, Angalifanya hivyo. Lakini Hakulitaka hilo, kwa hekima Anayoijua Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake. Basi, usiwe kabisa ni miongoni mwa wale wajinga ambao huzuni zao zilizidi na wakawa na majonzi mpaka hayo yakawapelekea kwenye babaiko kubwa.
Hakika wale wanaokukubali wewe, ewe Mtume, kwa yale unayoyalingania ya uongofu ni wale ambao wanayasikia maneno kwa kuyakubali. Ama makafiri, wao wamo kwenye hesabu ya wafu. Kwani uhai wa kikweli unakuwa kwa Uislamu. Na wafu, Mwenyezi Mungu Atawatoa kutoka kwenye makaburi yao wakiwa hai. Kisha watarudi Kwake Siku ya Kiyama ili watimiziwe hesabu yao na malipo yao.
Na washirikina walisema, kwa ujeuri na kiburi, «Kwa nini Mwenyezi Mungu Hateremshi alama iyoneshayo ukweli wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, miongoni mwa alama za kimiujiza.» Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwateremshia miujiza, lakini wengi wao hawajui kwamba kuteremsha miujiza kunakuwa kulingana na hekima Yake, Aliyetukuka.»
Hakuna katika ardhi mnyama yoyote anayetembea chini au ndege anayepaa juu kwa mbawa zake isipokuwa ni aina ya makundi yaliyoumbwa kama nyinyi. Hatukuacha katika Allawh, Almaḥfūd (Ubao Uliohifadhiwa) chochote isiopokuwa tumekithibitisha. Kisha wao, Siku ya Kiyama, watafufuliwa wapelekwe kwa Mola wao, na hapo Mwenyezi Mungu Atamhesabu kila mtu kwa alilolitenda.
Na wale waliozikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni viziwi hawasikii yanayowafaa, ni mabubu hawaitamki haki. Wao wametunduwaa kwenye giza, hawakufuata njia iliyolingana sawa. Yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumpoteza Anampoteza na yule Anayetaka kumuongoza Anamfanya awe kwenye njia iliyolingana sawa.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina, «Nipeni habari, ikiwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu ulimwenguni, au ikawajia saa ya nyinyi kufufuliwa, je, mutamuomba hapo asiyekuwa Mwenyezi Mungu awaondolee shida iliyowakumba, iwapo nyinyi ni wakweli kwamba waungu wenu mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wanawanufaisha au kuwadhuru?»
Bali hapo mtamuomba Mola wenu Aliyewaumba, si mwingine, na mtamtaka Awaokoe na Awaondolee shida kubwa zilizowashukia Akitaka, kwani Yeye Ndiye Muweza wa kila kitu; na wakati huo mtaacha masanamu wenu na wategemewa wenu.
Hakika tuliwatuma, ewe Mtume, Wajumbe kuwaendea makundi ya watu kabla yako kuwalingania kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakawakanusha na tukawapa mtihani katika mali yao, kwa ufukara mwingi na dhiki za maisha, na tukawapa mitihani katika miili yao, kwa magonjwa na kuumwa, ili wajidhalilishe kwa Mola wao na wanyenyekee Kwake Peke Yake kwa ibada.
Basi si ilipowajia, umma hawa wenye kukanusha, mitihani yetu wajidhalilishe kwetu. Lakini wao nyoyo zao zilisusuwaa na Shetani aliwapambia yale ambayo waliokuwa wakiyafanya ya maasia na wakiyaleta ya ushirikina.
Basi walipoacha kufuata amri za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuzipa mgongo, tuliwafungulia milango ya kila kitu miongoni mwa riziki, ndipo tukawabadilishia shida kwa kuwapa raha ya maisha, na tukawabadilishia magonjwa kwa kuwapa uzima wa miili, kwa kuwavuta kidogo kidogo. Hata watakapofanya kiburi na wakajiona kwa mema na neema tulizowapa, tutawashushia adhabu ya ghafla, wakitahamaki watajikuta wamekata tamaa wamekatika na kila zuri.
Watu hawa walimalizwa na kuangamizwa walipomkanusha Mwenyezi Mungu na kumkanusha Mtume Wake; hakuna yoyote aliyesalia kati yao. Shukrani na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Muumba na Mwenye kumiliki kila kitu, kwa kuwapa ushindi mawalii Wake na kuwaangamiza maadui Zake.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Nambieni ikiwa Mwenyezi Mungu Ameyaondoa masikizi yenu Akawafanya viziwi, Akayaondoa macho yenu Akawafanya vipofu na Akapiga mhuri juu ya nyoyo zenu mkawa hamufahamu neno, basi ni mola gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, awezaye kuwarudishia nyinyi vitu hivyo?» Angalia, ewe Mtume, ni namna gani sisi tunawatolea hoja aina mbalimbali, kisha wao baada yake wanakataa kukumbuka na kuzingatia?
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Nambieni iwapo mateso ya Mwenyezi Mungu yamewashukia ghafla na hali kwamba nyinyi hamuna hisia nayo, au yakawa waziwazi yanaonekana na nyinyi mnayaangalia: Je, kwani kuna wanaoteswa isipokuwa wale watu madhalimu ambao wamekiuka mpaka kwa kuipeleka ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi mungu, Aliyetukuka, na kwa kukanusha kwao Mitume Yake?»
Na hatuwatumi wajumbe wetu isipokuwa wenye kuwapa bishara njema wenye kututii kuwa watakuwa na starehe ya daima, na kuwapa onyo wenye kuasi kuwa watakuwa na adhabu kali. Basi mwenye kuamini, akawasadiki mitume na akafanya mema, hao hawataogopa wakati wa kukutana na Mola wao wala hawatakuwa na masikitiko juu ya chochote walichokikosa miongoni mwa hadhi za kilimwengu.
Na wale waliozikanusha aya zetu za Qur’ani na miujiza, hao itawapata adhabu Siku ya Kiyama kwa sababu ya ukafiri wao na kutoka kwao kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hawa, «Mimi sidai kuwa ninamiliki hazina za mbingu na ardhi nikawa ninazitumia nitakavyo; na sidai kuwa mimi najua al-ghayb (yasiyoonekana); na sidai kuwa mimi ni Malaika. Mimi ni Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, nafuata yale nliyoteremshiwa kwa njia ya wahyi na nawafikishia watu wahyi Wake.» Waambie, ewe Mtume, washirikina hawa. «Je, kafiri aliye kipofu wa kutoziona aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, asiziamini yuko sawa na Muumini anayeziona aya za Mwenyezi Mungu na akaziamini? Kwani nyinyi hamuzifikirii aya za Mwanye ili muione haki na muiamini?»
Na watishe, ewe Mtume, kwa hii Qur’ani wale ambao wanajua kuwa wao watafufuliwa wapelekwe kwa Mola wao. Wao wanaiyamini ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwalipa mema wenye kufanya wema na kuwalipa maovu wenye kufanya uovu. Wao hawana, isipokuwa Mwenyezi Mungu, mtegemewa mwenye kuwanusuru wala muombezi mwenye kuwaombea mbele Yake Aliyetukuka Akawaokoa na adhabu Yake. Kwani huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kwa kuyafanya maamrisho na kuyaepuka makatazo.
Na usiwatenge, ewe Nabii, kukaa na wewe Waislamu wanyonge wanaomuabudu Mola wao mwanzo wa mchana na mwisho wake, hali wakitaka, kwa matendo yao mema, radhi za Mwenyezi Mungu. Kitu chochote kuhusu hesabu ya maskini hawa hakiko juu yako; hesabu yao iko juu ya Mwenyezi Mungu. Na si juu yao chochote kuhusu hesabu yako. Basi ukiwatenga , utakuwa ni miongoni mwa wenye kuivuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, wenye kuweka vitu mahali pasipokuwa pake.
Na hivyo basi Mwenyezi Mungu Amewapa mtihani waja Wake kwa kutafautiana mafungu yao ya riziki na umbo, Akawafanya baadhi yao matajiri na wengine maskini, baadhi yao wenye nguvu na wengine madhaifu Na Akawafanya baadhi yao ni wahitaji wa wengine ili kuwajaribu kwa hilo, wapate makafiri matajiri kusema, «Ni madhaifu hawa, miongoni mwetu, Mwenyezi Mungu Amewapa neema ya Uislamu?» Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, si Mjuzi zaidi wa wanaoshukuru neema Yake Akawaafikia kwenye uongofu wa dini Yake?
Na wakikujia, ewe Nabii, wale wanaoamini aya za Mwenyezi Mungu zenye kushuhudia ukweli wako juu ya Qur’ani na mengineyo, kutaka fatuwa kuhusu toba ya madhambi yao yaliyotangulia, basi wakirimu kwa kuwarudishia salamu na uwape bishara ya rehema ya Mwenyezi Mungu iliyo kunjufu. Kwani Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ametoa ahadi Yake Mwenyewe kuwarehemu waja Wake kwa kuwafanyia wema kwamba mwenye kufanya dhambi kwa kutojua mwisho wake mbaya na kuwa linapelekea kukasirikiwa na Mwenyezi Mungu-Basi kila mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu kwa kukosea au kwa kusudi huwa ni mjinga kwa mtizamo huu, ingawa ajua kuwa ni haramu- kisha baada yake akatubia na akaendelea kufanya matendo mema, basi Mwenyezi Mungu Atamsamehe dhambi lake, kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe kwa waja Wake wenye kutubia, ni Mwingi wa rehema kwao.
Na mfano wa ufafanuzi huu tuliokufafanulia, tunakufafanulia, ewe Mtume, hoja zilizo wazi kwa kila mtu, ili ifunuke njia ya watu wa haki wanayoikanusha watu wa batili, na ifunuke njia ya watu wa batili wenye kuwaendea kinyume Mitume.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Amenikataza niabudu masanamu ambao mnaowaabudu badala Yake.» Na uwaambie, «Sitafuata matamanio yenu. Nitakuwa nimepotea njia ya sawa nikifuata matamanio yenu na sitakuwa ni miongoni mwa walioongoka.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mimi niko kwenye hoja iliyo wazi ya sheria ya Mwenyezi Mungu Aliyoniletea kwa njia ya wahyi. Nayo ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu Peke Yake kwa ibada. Na hili mlilikanusha. Na haliko kwenye uwezo wangu jambo la kuwateremshia adhabu mnayoitaka kwa haraka. Na uamuzi wa kuchelewesha hilo uko tu kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Yeye Anahadithia ukweli na Yeye Ndiye bora wa kupambanua baina ya haki na batili kwa uamuzi Wake na hukumu Yake.»
Sema, ewe Mtume, «Lau mimi nina mamlaka ya kuwateremshia adhabu ambayo mnaitaka kwa haraka, ningaliiteremsha kwenu, na uamuzi, baina yangu mimi na nyinyi, ungalitoka. Lakini hilo liko kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na Yeye Anawajua zaidi madhalimu ambao wamepita mipaka yao wakawashirikisha wengine pamoja na Yeye.
Na kwa Mwenyezi Mungu , Aliyetukuka na kuwa juu, kuna mafātih( al-ghayb, yaani: hazina za mambo ya ghaibu yaliyofichika, hakuna azijuwazo ila Yeye. Miongoni mwazo ni ujuzi wa Kiyama, kuteremka mvua, viliyomo ndani ya zao, matendo ya siku zinazokuja na mahala mtu atakapokufa. Na Anajua kila kilichoko barani na baharini. Na hakuna jani, linaloanguka kutoka kwenye mmea wowote, isipokuwa Yuwalijua. Na kila chembe iliyofichika ardhini na kila kibichi na kikavu, kimethibitishwa kwenye kitabu kilicho wazi kisicho na utatizi nacho ni Al-Lawh(Al-Maḥfūẓ ( Ubao Uliohifadhiwa)
Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Anayezichukua roho zenu usiku kwa namna inayofanana na vile roho hizo zinachukuliwa kipindi cha kifo, na Anayajua matendo mnayoyafanya mchana, kisha Anazirudisha roho zenu kwenye miili yenu kwa kuamka kutoka usingizini kipindi cha mchana kwa namna inayofanana na kuhuisha baada kufa, ili umalizike muda maalumu uliowekwa wa maisha yenu ulimwenguni. Kisha marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, baada ya kufufuliwa kwenu kutoka kwenye makaburi yenu mkiwa hai. Kisha Atawaelezea yale mliokuwa mkiyafanya kipindi cha maisha yenu ya ulimengu. Kisha Atawalipa kwa hayo.
Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Al-Qāhir (Mtendesha nguvu), Aliye juu ya waja Wake, ujuu wa kila namana usio na mipaka unaonasibiana na utkufu Wake, kutakata na kila sifa mbaya ni Kwake na kutukuka ni Kwake. Kila kitu kinaunyenyekea utukufu Wake na ukubwa Wake. Yeye Anawatuma kwa waja Wake Malaika kuyadhibiti matendo yao na kuyahesabu. Mpaka kifo kinapomshukia mmoja wao, Malaika wa mauti na wasaidizi wake wanaichukua roho yake, na wao hawaachi kutekeleza walichoamrishwa kukifanya.
Kisha hawa waliokufa watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Mola wao wa kweli. Jua utanabahi kwamba hukumu na uamuzi baina ya waja Wake, Siku ya Kiyama, ni Vyake Yeye tu. Na Yeye Ndiye Mwpesi wa wenye kuhesabu.
Waambie, ewe Mtume, hawa washirikina, «Ni nani mwenye kuwaokoa na vitisho vya magiza ya bara na bahari? Kwani si Mwenyezi Mungu mnayemuomba kwenye matatizo mkionesha unyonge wenu kwa dhahiri na kwa siri? Huwa mkisema, ‘Hakika Mola wetu Akituokoa na vitisho hivi, tutakuwa ni wenye kushukuru kwa kumuabudu, Aliyeshinda na kutukuka, Peke Yake, Asiye na mshirika.»
Waambie, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Ndiye Mwenye kuwaokoa na vitisho hivyi na kila tatizo, kisha nyinyi baada ya hapo mnawashirikisha wengine pamoja Naye katika ibada.»
Sema, ewe Mtume, «Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Ndiye Muweza, Peke Yake, kuwatumia adhabu kutoka juu yenu, kama kupigwa majiwe au mvua ya mafuriko na mfano wake, au kutoka chini ya miguu yenu, kama mitetemeko ya ardhi na kuzama ndani ardhi, au Awavurugie mambo yenu muwe makundi yanayozozana, mnauana nyinyi kwa nyinyi,» Angalia, ewe Mtume, vipi tunazifanya aina mbalimbali hoja zetu zilizo wazi kwa hawa washirikina ili waelewe na wazingatie!
Na waliikanusha hii Qur’ani makafiri kati ya watu wako, ewe Mtume; nayo ni kitabu chenye ukweli katika kila kilichokuja nacho, Waambie, «Mimi si mlinzi wala mtunzi juuu yenu. Mimi ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu, nawafikishia nyinyi yale niliotumwa nayo kwenu,.
Kila habari ina kituo cha kutulia na kikomo cha kukomea, hapo haki na batili zitafunuka. Na mtajua, enyi makafiri, mwisho wa jambo lenu, itakaposhuka adhabu ya Mwenyezi Mungu kwenu.
Na uwaonapo, ewe Mtume, washirikina wanaoleta maneno juu ya aya za Qur’ani, kwa urongo na kwa kufanya shere, jiepushe na wao mpaka waingie kwenye maneno mengine. Na iwapo Shetani amekusahaulisha jambo hili, basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu wenye uadui walioleta maneno ya urongo juu ya aya za Mwenyezi Mungu,
Na wale Waumini wanaomuogopa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, wakatii amri Zake na wakaepuka makatazo Yake, hawana jaukumu lolote juu ya hesabu ya Mwenyezi Mungu kwa wale wenye kuvama kwenye maneno yasiyofaa, wenye kuzifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu. Lakini ni juu yao wawaidhie waache kulete maneno hayo ya batili, kwani huenda wao wakamcha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka.
Na waache, ewe Mtume, hawa washirikina ambao wameifanya dini ya Uislamu ni mchezo na pumbao, wazifanyia shere aya za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na yamewaghuri wao maisha ya kilimwengu pamoja na pambo lake. Na wakumbushe, kwa Qur’ani, hawa washirikina na wengineo, ili nafsi isifungike kwa madhambi yake na kumkanusha kwake Mola wake. Haina, isipokuwa Mwenyezi Mungu, mlinzi mwenye kuinusuru akaiokoa na adhabu Yake, wala muombezi mwenye kuiyombea mbele Yake. Na ikitoa ili kujikomboa kiwango kiwacho cha fidia haitakubaliwa kwake. Hao ndio ambao wamefungika na dhambi zao. Watakuwa na kinywaji moto sana na adhabu yenye kuumiza Motoni, kwa sababu ya kumkanusha kwao Mwnyezi Mungu, Aliyetukuka, Mtume Wake, Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na dini ya Uislamu.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Je, tuabudu, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, masanamu yasionufaisha wala kudhuru? Je, turudi ukafirini baada ya Mwenyezi Mungu kutuongoza kwenye Uislamu, tukafanana, katika kurudi kwetu ukafirini, na aliyeharibika akili yake kwa kusawazwa na mashetani akapotea njia ardhini na hali yeye ana marafiki wenye akili, wenye Imani, wamwita kwenye njia ya sawa ambayo wao wako akawa anakataa?» Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Uongofu wa Mwenyezi Mungu Aliyenituma mimi ndio uongofu wa haki. Na sote tumeamrishwa tujisalimishe kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Bwana wa vuimbe vyote, kwa kumuabudu, Peke Yake, Asiye na mshirika, kwani Yeye Ndiye Mola na Mmiliki wa kila kitu.»
Na hivyohivyo tumeamrishwa tusimamishe Swala kikamilifu, tumuogope Yeye kwa kufanya maamrisho Yake na kuepuka makatazo Yake. Na Yeye, Aliyetukuka na kuwa juu, Ndiye Ambaye Kwake Yeye watakusanywa viumbe wote Siku ya Kiyama.
Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa pungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi kwa haki. Na taja,ewe Mtume, Atakaposema Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama, «Kuwa» na ikawa kulingana na amri Yake, kama kupepesa macho au muda mfupi zaidi. Neno lake Ndio haki iliokamilika. Na ni Wake ufalme, Peke Yake, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Siku Malaika atakapovuvia Parapanda, mvuvio wa pili ambao, kwa huo, roho zitarudi kwenye miili. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni kwake, Ndiye Anayeyajua yaliyofichika na hisi zenu, enyi watu, mnayoyaona kwa macho yenu. Yeye Ndiye Mwenye hekima, Anayeweka mambo mahali pake, Mtambuzi wa mambo ya viumbe Vyake. Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Anayehusika na mambo haya na mengineyo, mwanzo na mwisho, kuanzisha kuumba na ukomo wake. Na Yeye, Peke Yake, Ndiye Ambaye inapasa kwa waja kufuata sheria Yake, kujisalimisha kwa hukumu Yake na kuwa nahamu ya kupata radhi Zake na msamaha Wake.
Na kumbuka, ewe Mtume, mahujiano ya Ibrāhīm, amani imshukiye, na baba yake Āzar. Ibrāhīm alipomwambia, «Je, unawafanya masanamu ni waungu, unawaabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka? Mimi nakuona wewe na watu wako muko kwenye upotevu uliyo wazi, muko kando na njia ya haki.
Na kama tulivyomuongoza Ibrāhīm, amani imshukiye, kwenye haki katika jambo la ibada, tunamuonesha ufalme mkubwa unaokusanya mbingu na ardhi na uwezo wenye kushinda, ili awe miongoni mwa wenye kuvama katika Imani.
Giza la usiku lilipomuingilia Ibrāhīm, amani imshukiye, na kumfinika, alijadiliana na watu wake ili kuwathibitishia kuwa dini yao ni ya urongo. Na wao walikuwa wakiabudu nyota. Ibrāhīm, amani imshukiye, aliona nyota, akasema, akiwavuta watu wake, ili awathibitishie tawhīd (upweke wa Mwenyezi Mungu) kihoja, «Hii ni mola wangu.» Nyota ilipozama alisema, «Mimi siwapendi waungu wanaozama.»
Ibrāhīm alipouona mwezi umechomoza alisema kuwaambia watu wake kwa njia ya kumvuta mtesi, «Huu ni mola wangu.» Ulipozama, alisema, akiwa ahitajia uongofu wa Mola wake, «Asiponiongoza Mola wangu kwenye usawa juu ya kumpwekesha Yeye nitakuwa ni miongoni mwa watu waliopotea njia ya sawa kwa kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
Alipoliona jua limechomoza, alisema kuwaambia watu wake, «Hili ni mola wangu, hili ni kubwa kuliko nyota na mwezi.» Lilipozama, alisema kuwaambia watu wake, «Mimi nimejiepusha na ushirikina mulionao wa kuabudu mizimu, nyota na masanamu mnayoabudu badala ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.
«Mimi nimeelekea kwa uso wangu, katika ibada, kwa Mwenyezi Mungu, Aliyeshinda na kutukuka, Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi, nikiwa kando na ushirikina na nikielekea kwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Na mimi sikuwa ni miongoni mwa wenye kuwashirikisha wengine pamoja na Mwenyezi Mungu.»
Watu wake walimjadili kuhusu kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, akasema «Mwanijadili juu ya kumpwekesha kwangu Mwenyezi Mungu kwa ibada, na hali Yeye Ameniongoza nikaujua upweke Wake? Na iwapo nyinyi mnanitisha na waungu wenu wasije wakanidhuru, basi mimi siwaogopi na hawatanidhuru isipokuwa Mola wangu Atake jambo. Mola wangu Ameenea kila kitu kwa ujuzi. Basi hamkumbuki mkajua kuwa Yeye, Peke Yake, Ndiye Mstahiki wa kuabudiwa?
«Na ni vipi nitaogopa masanamu yenu na hali nyinyi hamumuogopi Mola wangu Aliyewaumba na Akayaumba masanamu yenu ambayo mnamshirikisha nayo Mwenyezi Mungu katika ibada, bila ya kuwa na hoja yoyote juu ya hilo? Basi ni lipi kati ya makundi mawili, kundi la washirikina na kundi la wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, lenye haki zaidi ya utulivu na usalama na kuaminika na adhabu ya Mwenyezi Mungu? Iwapo mnajua ukweli wa ninayoyasema, niambieni.»
Wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na wakafuata sheria Yake kivitendo, na wasichanganye imani yao na ushirikina, wao ndio wenye utulivu na usalama na wao ndio walioongozwa kwenye njia ya haki.
Hoja hiyo ambayo Ibrāhīm, amani imshukiye, aliwahoji nayo watu wake ndiyo hoja yetu tuliyomuongoza nayo mpaka hoja yao ikakatika. Tunamtukuza daraja tunayemtaka, miongoni mwa waja wetu, ulimwenguni na Akhera, Hakika Mola wako ni Mwenye hekima katika kuendesha mambo ya waja Wake, ni Mjuzi kuhusu wao.
Na tulimneemesha Ibrāhīm, amani imshukiye, kwa kumruzuku Is’ḥāq kuwa mtoto wake na Ya‘qūb kuwa mjukuu. Na wote wawili tuliwaongoza kwenye njia ya uongofu. Pia tulimuongoza Nūḥ kwenye haki, kabla ya Ibrāhīm na Isḥāq na Ya’qūb. Na pia tuliwaongoza kwenye haki, kati ya kizazi cha Nūḥ, Dāwūd, Sulaimān, Ayyūb, Yūsuf, Mūsā na Hārūn, amani iwashukie. Na kama tulivyowajazi Manabii hawa kwa wema wao, ndivyo tunavyomjazi kila mwema.
Na vilivile tulimuongoza Zakariyyā, Yaḥyā, ‘Īsā na Ilyās. Na Manabii wote hawa, amani iwashukie, ni miongoni mwa watu wema.
Na tulimuongoza, vilevile, Ismā‘īl, Ilyasa‘ na Lūṭ,. Na Mitume wote hawa tuliwatukuza juu ya watu wa zama zao.
Na pia tuliwaongoza kwenye haki tuliowataka kuwaongoza kati ya wazazi wa hawa, watoto wao na ndugu zao. Na tuliwateua wao wafuate Dini yetu na wafikishe ujumbe wetu kwa wale tuliowatuma kwao. Na tuliwaonesha njia sahihi, isiyopotoka, nayo ni ile ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na kumwepusha na mambo ya kumshirkisha..
Uongofu huo ni taufiki ya Mwenyezi Mungu ambayo kwayo Anamuongoza Anayemtaka miongoni mwa waja Wake. Na lau hawa Manabii walimshirikisha Mwenyezi Mungu, kwa kuchukulia na kukadiria, amali zao zingalipomoka. Kwani Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hakubali amali yoyote pamoja na ushirikina.
Manabii hao tuliowaneemesha kwa uongofu na unabii, ndio wale tuliowapa Kitabu, kama vile kurasa za Ibrāhīm, Taurati ya Muūsā, Zaburi ya Dāwūd na Injili ya Īsā. Na tuliwapa ufahamu wa Vitabu hivi na tukawateua kufikisha wahyi wetu. Na iwapo makafiri wa watu wako, ewe Mtume, watazikanusha aya za hii Qur’ani, basi tumewategemezea watu wengine jambo hilo, - yaani: Muhājirūn (masahaba waliohamia Madina pamoja na Mtume) na Ans,ār (masahaba wenyeji wa Madina) na wafuasi wao mpaka Siku ya Kiyama- ambao hawatakuwa ni wenye kuzikanusha. Bali watakuwa ni wenye kuziamini, ni wenye kuzitumia.
Manabii hao waliotajwa ndio ambao Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewaongoza kwenye dini Yake ya haki. Basi fuata uongofu wao, ewe Muhammad, na andama njia yao. Waambie washirikina, «Mimi sitaki kutoka kwenu, kwa kufikisha Uislamu, badala ya ulimwengu. Malipo yangu yako kwa Mwenyezi Mungu. Na Uislamu ni kuita watu wote kwenye njia iliyolingana sawa na ni ukumbusho kwenu na kwa kila aliyekuwa kama nyinyi, kati ya wale wanaoendelea kwenye batili; huenda nyinyi mkawaidhika nao mkanufaika.
Na hawa washirikina hawakumtukuza Mwenyezi Mungu ipasavyo kumtukuza, kwani walikanusha kwamba Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amemteremshia yoyote miongoni mwa binadamu, chochote katika wahyi wake. Waambie, ewe Mtume, «Iwapo mambo ni kama mnavyodai, ni nani aliyeteremsha kitabu alichokuja nacho Mūsā kwa watu wake, kikiwa ni mwangaza kwa watu na mwongozo kwao?» Kisha maneno yakaelekea kwa Mayahudi kwa kuwakemea kwa kusema «Mnakigawanya kitabu hiki kwenye kurasa mbalimbali, nyingine mnazionesha na nyingi katika hizo mnazificha.- Kati ya hizo walizozificha ni maelezo ya sifa za Muhammad , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na unabii wake.- Pia Mwenyezi Mungu Aliwafundisha, nyinyi Waarabu, Qur’ani ambayo Aliiteremsha kwenu, ndani yake mna habari ya walio kabla yenu na walio baada yenu na yatakayokuwa baada ya kufa kwenu, habari ambazo hamkuwa mkizijuwa, nyinyi wala wazazi wenu.» Sema, «Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeiteremsha.» Kisha waache hawa wavame na kucheza katika mazungumzo yao ya ubatili.
Na hii Qur’ani ni Kitabu tulichokuteremshia, chenye manufaa makubwa, kinatoa ushahidi juu ya ukweli wa vitabu vilivyoteremshwa vilivyokuja kabla yake na juu ya kwamba vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Tumekiteremsha ili uwatishie nayo, watu wa Makkah na walioko pambizoni mwake kwenye majimbo yote ya ardhi, adhabu ya Mwenyezi Mungu na mateso Yake. Na wenye kuamini uhai wa Akhera, wanaamini kwamba Qur’ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu na wanajilazimisha kusimamisha Swala kwa nyakati zake.
Ni nani mbaya zaidi wa udhalimu kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, neno la urongo, akadai kwamba Yeye Hakumtuma mjumbe yoyote miongoni mwa wanadamu, au akafanya madai ya urongo kwamba Mwenyezi Mungu Amemletea wahyi na hali hakumletea wahyi wowote, au akadai kwamba yeye ni muweza wa kuteremsha mfano wa Qur’ani Aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu? Na lau wawaona hawa wenye kupita mpaka, nao wako kwenye vitisho vya kufa, ungaliona jambo la kufazaisha, huku Malaika wakizitwaa roho zao, wameikunjua mikono yao kwa adhabu, wanawaambia, «Zitoeni nafsi zenu. Leo mtadhalilishwa upeo wa kudhalilishwa, kama mlivyokuwa mkisema urongo juu ya Mwenyezi Mungu na mkiona kiburi kufuata aya Zake na kuandama Mitume Wake.»
Hakika mumetujia ili muhesabiwe na mulipwe mkiwa peke yenu, kama tulivyowafanya mpatikane ulimwenguni mara ya kwanza mkiwa miguu mitupu, hamuna nguo, mumeviacha nyuma yenu vitu ambavyo tuliwamakinisha navyo miongoni mwa mali ya ulimwenguni mliokuwa mkijigamba nayo. Na hatuwaoni masanamu wako na nyinyi Akhera ambao mlikuwa mkiitakidi kuwa watawaombea na mkidai kuwa ni washirika pamoja na Mwenyezi Mungu katika ibada. Mashikamano yaliyokuwa kati yenu ulimenguni yameondoka, na yamewaondokea yale mliokuwa mkiyadai kwamba waungu wenu ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, na imefunuka wazi kwamba nyinyi ndio mliopata hasara ya nafsi zenu, watu wenu na mali yenu.
Hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Anapasua mbegu ukatoka mmea, na Anapasua koko ukatoka mti. Anatoa chenye uhai kutokana na kilichokufa, kama vile binadamu na mnyama kutokana na tone la manii ya binadamu na mnyama. Na Anatoa kilichokufa kutokana na chenye uhai, kama tone la manii linalotokana na binadamu na mnyama. Huyo Ndiye Mwenyezi Mungu. Yaani Mwenye kufanya hili ni Mwenyezi Mungu, Peke Yake, Asiye na mshirika, Anayestahiki kuabudiwa. Basi vipi nyinyi mtaepushwa na haki mpelekwe kwenye batili mkamuabudu pamoja na Yeye mwingine asiyekuwa Yeye?
Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Ambaye Alipasua mwangaza wa asubuhi kutoka kwenye giza la usiku, na Akaufanya usiku ni wakati wa utulivu, anatulia humo anayechoka mchana na kupata fungu lake la mapumziko, na Akalifanya jua na mwezi zinatembea katika njia zake kwa hesabu ya sawsawa iliyokadiriwa, haibadiliki wala haigongani. Hayo ndiyo makadirio ya Al- ’Azīz, Mwenye kushinda, ambaye ufalme Wake umeshinda, Al- ’Alīm, Aliye Mjuzi wa maslahi ya viumbe Wake na kuendesha mambo yao. Al- ’Azīz na Al- ’Alīm ni miongoni mwa majina ya Mwenyezi Mungu mazuri yanayoonesha ukamilifu wa ushindi na ujuzi.
Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyewawekea, enyi watu, nyota ni alama ya nyinyi kujua njia kipindi cha usiku mnapopotea kwa sababu ya giza lingi, barani na baharini. Tumezifafanua hoja zilizo wazi, ili wazizingatie miongoni mwenu wenye elimu ya kumjua Mwenyezi Mungu na sheria Yake.
Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyeanza kuwaumba, enyi watu, kutokana na Ādam, amani imshukiye, Alipomuumba kwa udongo, kisha mkawa nyinyi ni kizazi chenye kuendelea kutokana na yeye, Akawafanyia kituo cha nyinyi kutulia, nacho ni zao za wanawake; na Akawafanyia hazina ya nyinyi kuhifadhiwa , nayo ni migongo ya wanaume. Tumeshawabainishia hoja na kuwapambanulia dalili na kuzithibitisha kwa watu wenye kufahamu vituo vya hoja na sehemu za mazingatio.
Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za pungufu ni Kwake, Nadiye Aliyetaramsha mvua kutoka kwenye mawingu, Akatoa kwayo mimea ya kila kitu, Akatoa, kutokana na mimea, nafaka na miti mibichi, kisha akatoa kwenye mimea ya nafaka mbegu zilizoshikana, kama masuke ya mahindi, ngano na mpunga. Na Akatoa kutoka kwenye kizao cha mtende, nacho ni kile ambacho karara la tende linachomoza hapo, mitungo ambayo kuitunda ni karibu. Na Akatoa, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, mashamba ya mizabibu. Na Akatoa mizaituni na mikomamanga ambayo majani yake yanafanana na matunda yake yanatafautiana kimaumbile, uatamu na kitabia. Angalieni, enyi watu, matunda ya mimea hii inapotoa mazao na kuiva kwake na kustawi kwake yanapostawi. Hakika katika hayo, enyi watu, kuna dalili ya ukamilifu wa uwezo wa muumba vitu hivi, hekima Yake na rehema Yake kwa watu wenye kumuamini Yeye, Aliyetukuka, na kuzifuata sheria Yake kivitendo.
Na hawa washirikina wamefanya majini ni washirika wa Mwenyezi Mungu katika ibada, kwa kuitakidi kwao kuwa wao wanalete manufaa au madhara, na hali Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Amewaumba wao na wanavyoviabudu kutoka kwenye ‘adam ( hali ya kutokuwako). Basi ni Yeye Aliyepwkeka kwa kuumba, Peke Yake, na inapasa Apwekeke kwa kuabudiwa Peke Yake, Asiye na mshirika. Na, kwa kweli, hawa washirikina walisema urongo kumzulia Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, walipomnasibishia Yeye watoto wa kiume na wakike, kwa kutojua kwao sifa Zake za ukamilifu zinazompasa. Ameepuka na kuwa juu ya yale, ambayo walimnasibisha nayo washirikina, ya urongo na uzushi.
Na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Aliyezipatisha mbingu na ardhi na vilivyomo humo, kwa namna isiyokuwa na mfano uliotangulia. Vipi Awe na mtoto, na hakuwa na mke? Ametukuka Mwenyezi Mungu kutukuka kukubwa na yale wanayoyasema washirikina, Na Yeye Ndiye Aliyeumba kila kitu kutokana na hali ya kutokuwako na hakuna chochote chenye kufichika Kwake katika mambo ya viumbe.
Huyo, enyi washirikina, Ndiye Mola wenu, Aliyeshinda na kutukuka; hapana Mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye; Mwenye kuumba kila kitu. Basi mwandameni na mumnyenyekee kwa kumtii na kumuabudu. Na Yeye, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mtegemewa na ni Mtunzi, Anayaendesha mambo ya viumbe vyake.
Macho hayamuoni Mwenyezi Mungu ulimwenguni. Ama kwenye nyumba ya Akhera, Waumini watamuona Mola wao bila kumuenea. Na Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, anayafikia macho na kuyazunguka, na kuyajua vile yalivyo. Na Yeye ni Al-Latīf (Mpole) kwa mawalii Wake, Anayejua mambo yenye upeo wa udogo, Al-Khabīr (Mtambuzi) Anayejua mambo ya ndani.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mumejiwa na hoja zilizo wazi kutoka kwa Mola wenu, mnaonea nazo uongofu na upotevu, miongoni mwa zile zilizokusanywa na Qur’ani na akaja nazo Mtume, rehema na amani zimshukiye. Basi mwenye kufunukiwa na hoja hizi na akayaamini yale yanayolekezwa nazo, faida yake itamfikia mwenyewe. Na yule ambaye hakuuona uongofu baada ya hoja kumfunukia , basi amejikosea mwenyewe. Na mimi si mtunzi wa kudhibiti matendo yenu. Mimi ni mfikishaji tu. Na Mwenyezi Mungu Anamuongoza Anayemtaka na Anampoteza Anayemtaka kulingana na ujuzi Wake na hekima Yake.»
Na kama tulivyowafafanulia washirikina, katika hii Qur’ani, hoja zilizo wazi juu ya jambo la kumpwekesha Mwenyezi Mungu, utume na marejeo ya Kiyama, tunawafafanulia hoja katika kila wasichokijua. Na hapo wanasema urongo, «Umejifunza kutoka kwa watu wa Kitabu!» Na ili tufafanue haki, kwa kuzileta aya, kwa watu wanaoijua na kuikubali na kuifuata, nao ni waliomuamini Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, na kile alichoteremshiwa.
Fuata, ewe Mtume, wahyi tuliokuteremshia, wenye maamrisho na makatazo ambayo, kubwa lake ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kutakata na sifa za upungufu ni Kwake, na kuita watu huko. Na usijali ushindani wa washirikina na madai yao ya urongo.
Na lau Mwenyezi Mungu Alitaka wasishirikishe hawa washirikina hawangalishirikisha, lakini Yeye, Aliyetukuka, ni Mjuzi wa yatakayokuwa ya ubaya wa uchaguzi wao na kufuata kwao matamanio yaliyopotoka. Na hatukukufanya wewe ni mchunguzi wa kuwatunzia matendo yao wala hukuwa ni msimamizi wao wa kuwapangia maslahi yao.
Na msiyatukane, enyi Waislamu, masanamu ambyo washirikina wanayaabudu, kwa ajili ya kuziba kipengele, ili hilo lisije likawafanya wao wamtukane Mwenyezi Mungu kwa ujinga na kwa uadui, bila ya kuwa na ujuzi. Na kama tulivyowapambia hawa matendo yao mabaya, yakiwa ni mateso kwao kwa uchaguzi wao mbaya, ndivyo tulivyowapambia kila umma matendo yao. Kisha marejeo yao wote ni kwa Mola wao; hapo Mwenyezi Mungu Awaambie matendo yao waliokuwa wakiyatenda ulimwenguni kisha Awalipe kwayo.
Na waliapa washirikina hawa viyapo vya mkazo, «Lau Atatujia Muhammad kwa alama yenye miujiza, tutayaamini yale aliyoyaleta.» Sema, ewe Mtume, «Kuja kwa miujiza yenye kushinda kunatokana na Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Yeye Ndiye Mwenye uwezo wa kuileta Akitaka.» Na nilipi liwajulishalo nyinyi, enyi Waumini: huenda miujiza hii ikija hawataiamini hawa washirikina?.»
Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao, tuweke kizuizi baina yake na kunufaika na alama za Mwenyezi mungu, wasiziamini kama walivyokuwa hawakuziamini aya za Qur’ani zilipoteremka kwa mara ya kwanza, na tutawaacha wao wameduwaa katika kumuasi kwao Mwenyezi Mungu, hawaongoki kwenye haki na usawa.
Na lau kama sisi tungaliyaitikia maombi ya washirikina hawa na kuwateremshia Malaika kutoka mbinguni na tukawafufulia wafu wakazungumza nao na tukawakusanyia kila kitu walichokitaka wakakiona ana kwa ana, hawangaliyakubali yale uliyowaitia, ewe Mtume, na hawangaliyatumia, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Alimtakia uongofu. Lakini wengi wa hawa makafiri hawaijui haki ambayo umekuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na kama tulivyokujaribu wewe, ewe Mtume, kwa maadui zako miongoni mwa washirikina, tuliwajaribu Manabii wote, amani iwashukie, kwa maadui miongoni mwa waasi wa watu wao na maadui miongoni mwa waasi wa majini, wanapelekeana wenyewe kwa wenyewe maneno waliyoyapamba kwa uharibifu, ili adanganyike mwenye kuyasikia na apate kupotea njia ya Mwenyezi Mungu. Na lau Mola wako, Aliyetukuka na kuwa juu, Alitaka, angaliweka kizuizi kati yao na ule uadui, lakini huo ni mtihani kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Basi waache na kile wanachokibuni cha urongo na uzushi.
Na ili zielekee huko nyoyo za makafiri ambao hawaamini maisha ya Akhera wala hawayafanyii matendo ya kuwafaa, na ili nafsi zao zipate kuyapenda, na ili wapate kuyafanya maovu ambayo wao ni wenye kuyafanya. Katika haya, pana onyo kubwa kwao.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Kwani kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, Aliye Mola wangu na Mola wenu, natafuta uamuzi kati yangu na nyinyi, na hali Yeye, kutakasika na sifa pungufu ni Kwake, Amewateremshia Qur’ani ambayo ndani yake pana ufafanuzi wa uamuzi wa yale ambayo mlikuwa mkiteta juu yake kuhusu mambo yangu na mambo yenu?» Na Wana wa Isrāīl waliopewa na Mwenyezi Mungu Taurati na Injili wana ujuzi wa yakini kwamba hii Qur’ani imeteremshwa kwako, ewe Mtume, kutoka kwa Mola wako kwa haki. Basi usiwe, tena usiwe, ni miongoni mwa wenye shaka juu ya chochote ambacho tumekuletea wahyi.
Na limekamilika neno la Mola wako, nalo ni Qur’ani, likiwa lina ukweli wa habari na maneno, lenye uadilifu wa hukumu. Hakuna anayeweza kuyabadilisha maneno yake yaliyokamilika. Na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka, Ndiye Mwenye kuyasikia wanayoyasema waja Wake, Ndiye mwenye kuyajua mambo yao yaliyo waziwazi na yaliyojificha
Na lau itakadiriwa, ewe Mtume, kwamba wewe uliwasikiliza wengi kati ya watu wanaokaa ardhini, kwa kweli wanagalikupoteza ukawa kando na dini ya Mwenyezi Mungu. Kwani wao hawaendi isipokuwa kwenye yale wanayoyaona kuwa ni haki kwa kuwaiga wakale wao. Na hawakuwa wao isipokuwa tu wanadhania na wanasema urongo.
Na kwa hakika, Mola wako Ndiye Anayewajua zaidi wenye kupotea njia ya uongofu; na Yeye Anawajuwa zaidi, kuliko nyinyi, wale walio kwenye njia ya uongofu na usawa; hafichiki Kwake yoyote katika wao.
Basi kuleni, kati ya wanyama waliochinjwa, wale ambao jina la Mwenyezi Mungu lilitajwa wakati wa kuchinjwa, iwapo nyinyi mnaziamini hoja za Mwenyezi Mungu, aliyetukuka, zilizo wazi.
Na kitu gani kinachowazuia, enyi Waislamu, kumla mnyama ambaye jina la Mwenyezi Mungu lilitajwa wakati wa kuchinjwa, ambapo Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Amewaelezea nyinyi yote aliyoyaharamisha kwenu? Lakini yale ya haramu ambayo dharura imepelekea yatumiwe, kwa sababu ya njaa, kama mfu, basi mumehalalishiwa. Na wengi, kati ya wapotofu, wanawapoteza wafuasi wao na kuwaepusha na njia ya Mwenyezi Mungu katika kuhalalisha haramu na kuharamisha halali kwa matakwa yao kwa ujinga walionao. Kwa hakika, Mola wako, ewe Mtume, Ndiye Amjuwaye zaidi yule aliyekiuka mipaka Yake katika hayo; na Yeye Ndiye Atakayesimamia hesabu yake na malipo yake.
Na acheni, enyi watu, maasia yote, yaliyo waziwazi na yaliyo ya siri. Hakika wale wanaofanya maasia, Mola wao Atawatesa kwa sababu ya yale maovu ambyo walikuwa wakiyafanya.
Na wala msile, enyi Waislamu, katika vichinjwa, yule ambaye halikutajwa jina la Mwenyezi Mungu wakati wa kuchinjwa, kama mfu na aliochinjiwa masanamu na majini na wasiokuwa hao. Na kwa hakika kuwala wanyama hao ni kutoka kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka. Na majini waasi wanawatia marafiki zao, miongoni mwa mashetani wa kibinadamu, ushawiwishi wa kuwatatiza kuhusu uharamu wa kula mfu; wanawaamrisha wawaambie Waislamu wanapobishana nao, «Hakika nyinyi, kwa kutokula kwenu mfu, huwa hamli anachokiua Mwenyezi Mungu, ambapo mnakula mnachokichinja.» Na iwapo mtawasikiliza, enyi Waislamu, katika kuhalalisha mfu, basi nyinyi mtakuwa sawa na wao katika ushirikina.
Je, yule ambaye amekufa katika upotofu, ameangamia na ameshangaa, tukaufufua moyo wake kwa Imani, tukamuongoza kwenye Imani na tukamuafikia kuwafuata Mitume Wake, akawa anaishi kwenye miangaza ya uongofu, atakuwa ni kama mfano wa yule aliye ndani ya ujinga, matamanio ya moyo na namna mbalimbali za upotevu, asiyeongokewa kwenye sehemu yoyote ya kupenya na hana wa kumuokoa na yale ambayo yumo ndani yake? Hao wawili hawalingani. Na kama nilivyomuachilia kafiri huyu anayebishana na nyinyi, enyi Waumini, nikampambia vitendo vyake viovu akaviona ni vyema, vilevile nimewapambia wenye kukanusha vitendo vyao viovu ili wapaswe, kwa hilo, kupata adhabu.
Na mfano huu uliopatikana kwa viongozi wa makafiri huko Maka wa kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, tumeweka katika kila mji watu waovu wanaongozwa na wakubwa wao, ili wapate kufanya vitimbi humo kwa kuzuia dini ya Mwenyezi Mungu; na wao hawazifanyii vitimbi isipokuwa nafsi zao, na wala hawalihisi hilo.
Na pindi inapowajia washirikina hawa, miongoni mwa watu wa Maka, hoja iliyo waziwazi juu ya unabii wa Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, wanasema baadhi ya wakubwa wao, «Kamwe hatutaukubali unabii wake mpaka Mwenyezi Mungu Atupe unabii na miujiza mfano wa Aliyowapa wajumbe wake waliotangulia» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Aliwajibu kwa neno lake,: “Mwenyezi Mungu Anajua zaidi wapi Auweke ujumbe Wake.» Kwa maana kuwa Anawajua wale wanaofaa kubeba ujumbe Wake na kuufikisha kwa Watu. Utawapata unyonge wakiukaji mipaka hawa, na watakuwa na adhabu iumizayo ndani ya Moto wa Jahanamu kwa sababu ya vitimbi vyao kwa Uislamu na watu wake.
Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu Anataka kumuafukia aikubali haki, Anakikunjua kifua chake kukubali Imani na upweke wa Mwenyezi Mungu; na yule ambaye Anataka kumpoteza , Anakifanya kifua chake kiwe katika hali ya dhiki kubwa na kukunjika katika kuukubali uongofu, kama hali ya anayepaa kwenye tabaka za anga za juu, hapo akapatwa na uzito mkubwa wa kuvuta pumzi. Na kama anavyovifanya Mwenyezi Mungu vifua vya makafiri vibanike sana na kukunjika, hivyo basi ndivyo Atakavyowapatia adhabu wale wasiomuamini.
Na haya tuliliyokubainishia, ewe Mtume, ndio njia inayofikisha kwenye radhi za Mola Wako na Pepo Yake. Tumezifunua wazi hoja kwa yule anayekumbuka miongoni mwa wenye akili zilizokomaa.
Wale wanaokumbuka watapata mbele ya Mola wao, Aliyetukuka na kuwa juu, Siku ya Kiyama Nyumba ya Salama na Amani, isiyo na makero, nayo ni Pepo. Na yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, ni Mwenye kuwanusuru na kuwalinda; hayo yakiwa ni malipo kwao kwa matendo yao mema.
Na kumbuka, ewe Mtume, ile Siku Atakayowakusanya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, makafiri na wategemewa wao, miongoni mwa mashetani wa kijini, na kuwaambia, «Enyi mkusanyiko wa majini, hakika mumewapoteza binadamu wengi.» Na watasema wategemewa wao miongoni mwa makafiri wa kibinadamu, «EweMola wetu, kila mmoja katika sisi amenufaika na mwengine, na tumefikia kikomo ambacho umekiweka kwetu kwa kumalizika uhai wetu wa duniani.» Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Atasema Awaambie, «Moto ndio mashukio yenu, mtakaa milele, isipokuwa yule ambaye Mwenyezi Mungu Ametaka asikaye milele,» miongoni mwa walioasi wenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake na utengenezaji Wake, ni Mjuzi mno wa mambo yote ya waja Wake.
Na kama tulivyowapa uwezo mashetani wa kijini juu ya makafiri wa kibinadamu wakawa ni wategemewa wao, hivyohivyo tunawapa uwezo madhalimu wa kibinadamu juu ya wenyewe kwa wenyewe duniani kwa sababu ya maasia wayafanyayo.
Enyi majini na binadamu mlio washirikina, kwani hawakuwajia Mitume miongoni mwenu- Maandiko yanaonesha kuwa Mitume wanatoka kwa wanadamu tu.[4]- wanaowapa habari za alama zangu zilizo wazi, zinazokusanya maamrisho na makatazo, zinazofafanua kheri na shari na wanaowaonya kukumbana na adhabu yangu Siku ya Kiyama? Watasema washirikina hawa, maijini na binadamu, «Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu kwamba Mitume wako wametufikishia aya zako na wametuonya makutano ya Siku yetu hii, na sisi tukawakanusha.» Na hawa washirikina, liliwadanganya wao pambo la maisha ya dunia. Na walizishuhudilia nafsi zao kwamba wao walikuwa wakiukataa upweke wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na wakiwafanya warongo Mitume Wake, amani iwashukie.
____________________
[4]Hii ndio kauli yenye nguvu ya maimamu wa nyuma na waliokuja baada yao. Na hii 1 aya si dalili wazi ya kuwa kuna Mitume wa kijini. Angalia Tafsiri ya lbn Kathīr katika kusherehi aya hii.
____________________
[4]Hii ndio kauli yenye nguvu ya maimamu wa nyuma na waliokuja baada yao. Na hii 1 aya si dalili wazi ya kuwa kuna Mitume wa kijini. Angalia Tafsiri ya lbn Kathīr katika kusherehi aya hii.
Ili asiadhibiwe yoyote kwa kujidhulumu nafsi yake kwa kufanya maovu na hali ulinganizi wa Uislamu haujamfikia, sisi tulituma Mitume na tukateremsha Vitabu kwa kuwaondolea majini na binadamu hoja watakayoichukua kama kisingizio. Hivyo ndivyo tulivyowaondolea hoja umma waliyopita, hatukumuadhibu yoyote isipokuwa baada ya kuwapelekea Mitume.
Na kila mwenye kufanya vitendo vya kumtii Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, vya kumuasi ana daraja kutokana na vitendo vyake, Mwenyezi Mungu Atamfikishia viwango hivyo na Atamlipa kwavyo. Na Mola wako, ewe Mtume, Hakuwa ni Mwenye kughafilika na wanayoyafanya waja Wake.
Na Mola wako, ewe Mtume, Aliyewaamrisha watu kumuabudu, Ndiye Mkwasi Peke Yake, na viumbe wote wanamhitajia Yeye. Na Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Mwenye rehema kunjufu. Na lau Alitaka Angaliwaangamiza na Akawaleta watu wengine wasiokuwa nyinyi watakaokuwa badala yenu baada ya kumalizika kwenu na watende matendo ya kumtii Yeye, Aliyetukuka, kama Alivyowaleta nyinyi kutokamana na kizazi cha watu wengine waliokuwako kabla yenu.
Hakika yale mateso ambayo Anawaahidi nayo Mola wenu, enyi washirikina, kwa ukafiri wenu, ni yenye kuwapata. Na hamutamlemea Mola wenu kwa kumkimbia. Kwani Yeye ana uwezo wa kuwarudisha, hata kama mtakuwa mumegeuka mumekuwa mchanga na mifupa.
Sema, ewe Mtume, «Enyi watu wangu, fanyeni kwa njia yenu, na mimi nitafanya kwa njia yangu ambayo Mola wangu, Aliyetukuka na kuwa juu, Aliniwekea. Mtakuja kujua, pindi mateso yatakapowashukia, ni nani atakayekuwa na mwisho mwema?» Hakika hatafaulu kupata radhi za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na Pepo yule aliyekiuka mpaka Wake na akadhulumu, na akamshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye.
Na wale wenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kuwa juu, waliziweka kando sehemu ya vitu Alivyoviumba miongoni mwa mazao, matunda na wanyama howa wakawapatia wageni na maskini; na wakaziweka kando sehemu nyingine za vitu hivi kwa washirika wao, miongoni mwa masanamu na mizimu. Basi zile zilizotengewa washirika wao zafikishwa kwao peke yao, na hazifiki kwa Mwenyezi Mungu; na zile zilizotengewa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, zinafika kwa washirika wao. Ni mbaya ulioje uaumuzi wa hao watu na kigawanyo chao.
Na kama ambavyo mashetani waliwapambia washirikina wamtengee Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika mazao na wanyama howa, fungu maalumu na fungu kwa washirika wao, vilevile mashetani wamewapambia wengi kati ya washirikina kuwaua watoto wao kwa kuchelea ufukara, ili wawaingize wazazi hawa kwenye maangamivu kwa kuziua nafsi ambazo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuliwa isipokuwa kwa haki, na ili wawavurugie dini yao iwachanganyikie wapate kupotea na waangamie. Na lau Angalitaka Mwenyezi Mungu wasiifanye hilo hawangalilifanya, lakini Yeye Amelikadiria liwe kwa kujua Kwake uovu wa hali yao na marejeo yao. Basi waache, ewe Mtume, na mambo yao, katika yale ya urongo wanayoyazua , na Mwenyezi Mungu Atahukumu baina yako na wao.
Na walisema washirikina kwamba ngamia hawa na makulima haya ni vitu haramu; haifai kuvila kwa mtu yoyote isipokuwa yule wanayemruhusu, kulingana na madai yao, miongoni mwa wasimamizi wa mizimu na wengineo. Na hawa ni ngamia ambao ilipewa heshima migongo yao, haifai kupandwa wala kubebeshwa vitu juu yake kwa namana yoyote. Na hawa ni ngamia ambao hawawatajii jina la Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, katika jambo lolote linalowahusu wao.Waliyafanya hayo kwa urongo utokao kwao, kumzulia Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu Atawalipa kwa urongo waliokuwa wakimzulia Yeye, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake.
Na walisema washirikina, «Watoto waliyomo ndani ya wanyama howa, wakizaliwa wakiwa hai, ni halali tu kwa wanaume kati yetu na ni haramu kwa wanawake miongoni mwetu.» Na wakizaliwa nao wamekufa wanashirikiana katika kuwatumia. Mwenyezi Mungu Atawatesa kwa kujiwekea sheria za kuhalalisha na kuharamisha ambazo Mwenyezi Mungu hakuziruhusu. Hakika Yeye Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni Mwingi wa hekima katika uendeshaji Wake mambo ya viumbe Wake, Mjuzi sana kuhusu wao.
Hakika wamepata hasara na wameangamia wale ambao, kwa udhaifu wa akili zao na kwa ujinga wao, waliwaua watoto wao na wakaziharamisha, kwa kumzulia Mwenyezi Mungu urongo, zile Alizowaruzuku. Wako mabali na haki na hawakuwa ni miongoni mwa watu wa uongofu na muelekeo wa sawa. Kuhalalisha na kuharamisha ni miongoni mwa mambo mahususi ya uungu katika uwekaji sheria. Halali ni Aliyoihalalisha Mwenyezi Mungu, na haramu ni Aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu. Na haipasii kwa yoyote kati ya viumbe wake, awe mmoja au kundi, kuwaekea sheria waja Wake ambayo Mwenyezi Mungu Hakuidhinisha.
Na Mwenyezi Mungu, kutkata na sifa za upungufu ni Kwake na kutukuka ni Kwake, Ndiye Aliyewaanzishia mashamba: miongoni mwa mimea yake kuna ile iliyoinuliwa juu ya ardhi na kuegemezewa vitu vyingine, kama mizabibu, na miongoni mwayo kuna isiyoinuliwa, bali inasimama yenyewe kwenye vigogo vyake, kama mitende na miti mingine ya mazao. Mimea yote hiyo ikiwa ina tamu tafauti. Mizabibu na mikomamanga, maumbile yake yanafanana na matunda yake yanatafautiana tamu yake. Kuleni, enyi watu, matunda yake na mtoe Zaka zake zilizolazimishwa kwenu siku mnapoyavuna na kuyatungua, na msiikiuke mipaka ya usawa katika kutoa mali na kula chakula na mengineyo. Hakika Yeye, Mwenyezi Mungu, Hawapendi wenye kukiuka mipaka Yake kwa kutumia mali katika njia zisokuwa zake.
Na Ameleta katika wanyama wale ambao wametayarishwa kwa kubebeshwa kwa kuwa ni wakubwa na ni warefu, kama ngamia. Na miongoni mwao kuna waliotayarishwa si kwa kubebeshwa kwa kuwa ni wadogo na wafupi, kama ng’ombe, mbuzi na kondoo. Kuleni wale Aliyowahalalishia nyinyi Mwenyezi Mungu miongoni mwa hawa wanyama, wala msiwaharamishe wale Aliyowahalalisha miongoni mwao kwa kufuata njia za Shetani kama walivyofanya washirikina. Hakika Shetani, kwenu nyinyi, ni adui mwenye uadui wa wazi.
Wanyama hawa ambao Mwenyezi Mungu Amewaruzuku waja Wake, miongoni mwa ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo, ni aina nane: nne kati ya hizo ni mbuzi na kondoo, nao ni kondoo: waume na wake, na mbuzi: wume na wake. Sema, ewe Mtume, uwaambie hao washirikina, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha madume wawili wa mbuzi na kondoo?» Wakisema, «Ndio», watakuwa wamesema urongo kuhusu hilo. Sababu wao hawalifanyi kila dume la kondoo na mbuzi kuwa ni haramu. Na waambie, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha majike wawili wa mbuzi na kondoo?» wakisema, «Ndio», watakuwa pia wamesema urongo. Sababu wao hawamuharamishi kila mwanambuzi na mwanakondoo mke. Na sema uwaambie, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha watoto walio matumboni mwa majike wawili wa mbuzi na kondoo walio na mimba?» Wakisema, «Ndio.» Watakuwa wamesema urongo pia. Kwani hawaiharamishi kila mimba ya namna hiyo. Nambieni kwa misingi ya elimu inayoonesha usahihi wa msimamo wenu, mkiwa ni wakweli katika hayo mnayoyanasibisha kwa Mola wenu.
Na aina nne nyingine ni aina mbili za ngamia, waume na wake, na aina mbili za ng’ombe, waume na wake. Sema, ewe Mtume, kuwaambia washirikina hao, «Kwani Mwenyezi Mungu Amewaharamisha madume wawili au majike wawili? Au Ameharamisha vilivyomo ndani ya matumbo ya majike wawili, wawe madume au majike? Au mlikuwa, enyi washirikina, mupo pindi Mwanyezi Mungu Alipowapa wasia wa uharamu huu wa wanyama howa? Hakuna dhalimu mbaya zaidi kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu urongo, ili awapotoshe watu, kwa ujinga wake, na njia ya uongofu. Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Hamuelekezi kwenye muelekeo wa sawa yule aliyekiuka mpaka wake, akamzulia urongo Mola wake na akawapoteza watu.
Sema, ewe Mtume, mimi sipati, kati ya yale aliyoniletea wahyi Mwenyezi Mungu, kitu kilicho haramu kwa mwenye kukila, kati ya vile mnavyovitaja kwamba vimeharamishwa miongoni mwa wanyama howa, isipokuwa awe amekufa bila kuchinjwa, au ni damu itiririkayo, au iwe ni nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni najisi, au akawa ni mnyama ambaye kuchinjwa kwake kumetoka nje ya utiifu wa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kama akiwa mnyama aliyechinjwa ametajiwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu, wakati wa kuchinjwa. Basi mwenye kulazimika kula chochote kati ya hizo zilizoharamishwa kwa dharura ya njaa kali, pasi na kutaka kujifurahisha wala kukiuka mpaka wa dharura, hakika Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, ni mwenye kumsamehe, ni mwenye huruma naye. Na hakika imethibiti, baadaye, kwa mafundisho ya Mtume kuwa ni haramu kula kila mnyama mwitu anayewinda kwa kutumia meno, kila ndege anayewinda kwa kutumia kucha, punda na mbwa.
Na watajie washirikina hawa, ewe Mtume, wanyama na ndege tuliowaharamishia Mayahudi: nao ni kila ambaye hana pasuko vidoleni mwake, kama ngamia na mbuni, na mafuta ya ng’ombe, mbuzi na kondoo isipokuwa yale mafuta yaliyoshikana na migongo ya wanyama hao na tumbo zao, au yaliyoshikana na mfupa wa mkia na mbavu na mfano wake. Uharamishaji huu uliotajwa juu ya Mayahudi ni adhabu kutoka kwetu kwa sababu ya matendo yao maovu. Na sisi ni wakweli kwa yale tuliyoyaeleza kuhusu wao.
Na wakikufanya mrongo, ewe Mtume, wanaokwenda kinyume na wewe miongoni mwa washirikina, Mayahudi na wengineo, waambie, «Mola wenu, Aliyetukuka na kuwa juu, ni Mwenye rehema kunjufu. Na wala haiyepushwi adhabu Yake kwa watu walitenda maovu wakapata madhambi na wakajitokeza wazi na ubaya. Katika haya pana onyo kwao, kwa kwenda kwao kinyume na Mtume , rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie.
Watasema wale walioshirikisha, «Lau Mwenyezi Mungu Alitaka tusishirikishe, sisi na baba zetu, na tusihararamishe kitu chochote kinyume na matakwa Yake, hatungalifanya hilo.» Hapo Mwenyezi Mungu Aliwarudi kwa kuwaeleza kwamba utata huu ulivumishwa na makafiri kabla yao, wakautumia kuukanusha ulinganizi wa Mitume wao na wakaendelea kufanya hivyo mpaka ikawateremkia adhabu ya Mwenyezi Mungu. Waambie, ewe Mtume, «Je, mnayo elimu sahihi mtuoneshe, juu ya wanyama howa na makulima mliyoharamisha na juu ya madai yenu kwamba Mwenyezi Mungu Aliwatakia ukafiri, Akauridhia kwenu na Akaupendelea kwenu? Hamuna mnachofuata, katika mambo ya dini, isipokuwa dhana tu; na hamukuwa nyinyi isipokuwa mnasema urongo.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia wao, «Mwenyezi Mungu, Alietukuka na kuwa juu, Ndiye Mwenye hoja ya mkato, yenye kuzikata dhana zenu. Na lau Alitaka Angaliwaongoza nyote kwenye muelekeo wa sawa.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Waleteni mashahidi wenu ambao watatoa ushahidi kwamba Mwenyezi Mungu Ndiye Aliyeharamisha vile mlivyoviharamisha vya makulima na wanyama howa.» Wakitoa ushahidi huo, kwa urongo na uzushi, usiwaamini wala usikubaliane na wale waliojitolea uamuzi wenyewe kulingana na mapendeleo ya nafsi zao, wakazikanusha aya za Mwenyezi Mungu katika yale waliyoyashikilia ya kukiharamisha Alichokihalalisha Mwenyezi Mungu na kukihalalisha Alichokiharamisha Mwenyezi Mungu. Wala usiwafuate wale ambao hawayaamini maisha ya Akhera wala wasiotenda vitendo vya kuwafaa huko na wale ambao Mola wao wanamshirikisha wakawa wanamuabudu mwingine pamoja na Yeye.
Waambie, ewe Mtume, «Njooni niwasomee Yale Aliyoyaharamishia Mwenyezi Mungu: Msishirikishe pamoja na Mwenyezi Mungu kitu chochote, miongoni mwa viumbe Vyake katika kumuabudu Yeye; bali zielekezeni aina zote za ibada Kwake Yeye Peke Yake, kama kucha, kutaraji, kuomba na megineyo. Muwafanyie wema wazazi wawili kwa kuwasaidia, kuwaombea Mungu na mengineyo ya wema kama hayo Msiwaue watoto wenu kwa sababu ya ufukara uliowshukia, kwani Mwenyezi Mungu Anawaruzuku nyinyi na wao. Wala msiyasongelee madhambi makubwa yaliyo wazi na yaliyofichika. Na msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu Ameharamisha kuuawa, isipokuwa kwa njia ya haki, nayo ni kuchukuliwa kisasi kwa aliyeua, au kwa uzinifu baada ya kuoa au kuolewa, au kuacha Uislamu. Hayo yaliyotajwa ni miongoni mwa yale ambayo Mwenyezi Mungu Amewkataza nayo na Akawapa maagizo muyaepuke na ni miongoni mwa yale Aliyowaamrisha nyinyi kwayo. Amweausia nayo Mola wenu ili mupate kuyaitia akilini maamrisho Yake na Makatazo Yake.
«Wala msiyasogelee, enyi wasimamizi, mali ya yatima isipokuwa kwa namana ya kuyatengeneza na kuyafanya yenye faida, mpaka atakapofikia myaka ya kubaleghe na awe mwangalifu. Na pindi afikiapo umri huo, mpeni mali yake. Na tekelezeni vipimo na mizani kwa usawa kwa namna ambayo utekelezaji utakuwa umefanyika kwa ukamilifu. Na mtakapojibidiisha uwezo wenu, hapana ubaya kwenu katika yale ambayo huenda yakawa na upungufu upande wenu. Kwani hatumlazimishi mtu isipokuwa uwezo wake. Na msemapo, basi jitahidini katika maneno yenu kuchunga usawa pasi na kupotoka kwenye haki kwenye utoaji habari au ushahidi au hukumu au kwenye uombezi, hata kama yule ambaye neno hilo linamuhusu yeye ana ujamaa na nyinyi, msilemee upande wake bila ya haki. Na tekelezeni yale aliyowaagiza mufanye ya kujilazimisha na sheria Yake. Hukumu hizo mlizosomewa, Mola wenu Amewausia mzifuate kwa matarajio kwmba mkumbuke mwisho wa mambo yenu.
«Na miongoni mwa mambo aliyowausia Mwenyezi Mungu ni kwamba huu Uislamu ndio njia ya Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, iliyolingana sawa. Basi ifuateni wala msifuate njia za upotevu zikawatawanya na kuwaepusha na njia ya Mwenyezi Mungu iliyolingana sawa. Muelekeo huo upande wa njia nyofu, ndio Aliowausia nao Mwenyzi Mungu ili mjikinge na adhabu Yake kwa kuyatekeleza maamrisho Yake na kijitenga na makatazo Yake.»
Kisha sema, ewe Mtume, uwaambie hawa washirikina, «Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, Ndiye Aliyempa Mūsā Taurati, kwa kuzitimiza neema Zake kwa watu wa mila yake wanaofanya wema, na kwa kufafanua kila kitu katika mambo ya dini yao, na kuwapa uongofu na muelekeo wa njia iliyolingana sawa, na kuwarehemu, kwa matumaini kuwa watakubali kwamba kuna kufufuliwa baada ya kufa na kuna hesabu na malipo, na hilo liwafanya watende mema.
Na hii Qur’ani ni kitabu tulichokiteremsha kwa Nabii wetu Muhammad, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie. Kheri yeke ni nyingi. Basi kifuateni kwa yale anayowaamrisha na kuwakataza. Na muogopeni Mwenyezi Mungu msije mkaenda kinyume na amri Yake yoyote, kwa matumaini kuwa mtarehemewa na mtaokolewa na adhabu Yake na mpate malipo Yake mema.
Na tumeiteremsha hii Qur’ani, ili msije mkasema, enyi makafiri wa Kiaarabu, «Hakika Kitabu kutoka mbinguni waliteremshiwa Mayahudi na Wanaswara; na sisi tuna mambo ya kutushughulisha kutowahi kuvisoma vitabu vyao; na sisi hatuna ujuzi navyo wala maarifa.»
Na ili msije mkasema, enyi washirikina, «Lau kama sisi tuliteremshiwa kitabu kutoka mbinguni, kama walivyoteremshiwa Mayahudi na Wanaswara, tungalikuwa na muelekeo madhubuti sana kwenye njia ya haki kuliko wao.» Hakika kimewajia Kitabu kwa lugha ya Kiarabu chenye ufafanuzi. Na hiyo ni hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu, ni muongozo wa njia ya haki na ni rehema kwa umma huu. Na hapana yoyote mbaya wa dhuluma na uadui kuliko yule aliyezikanusha hoja za Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, na akazipa mgongo. Basi hawa wenye kupa mgongo tutawatesa mateso makubwa kwenye Moto wa Jahanamu, kwa sababu ya kuzipa mgongo kwao aya zetu na kuzuia kwao njia zetu.
Kwani wanangojea, hawa wenye kukataa na wakazuia watu wasiifuate njia ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa awajie wao Malaika wa mauti na wasaidizi wake kuzichukua roho zao au aje Mola wako, ewe Mtume, kutoa uamuzi kati ya waja wake Siku ya Kiyama, au zije baadhi ya alama za Kiyama na vitambulisho vyake vinavyoashiria kuja kwake, navyo ni kuchomoza jua kutoka upande wake wa Magharibi? Basi litakapokuwa hilo hakuna nafsi yoyote itakayofaidika na Imani yake, iwapo haikuwa imeamini kabla ya hapo, wala hayatakubaliwa matendo mema mapya ya hiyo nafsi, ikiwa ilikuwa imeamini, iwapo haikuwa imeyatenda kabla ya hapo. Waambie, ewe Mtume, «Ngojeeni kuja kwake, ili mpate kumjua aliye kwenye usawa na aliye kwenye makosa, na mtenda maovu na mtenda mema. Sisi tunalingojea hilo.»
Hakika wale walioigawanya dini yao, baada ya kuwa mkusanyiko mmoja juu ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na kufuata sheria Yake kivitendo, wakawa ni makundi na mapote, wewe, ewe Mtume, uko mbali na wao. Hukumu yao iko kwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka, kisha Yeye Atawapa habari za matendo yao, Amlipe aliyetubia miongoni mwao na akafanya wema, kwa wema wake na Amtese mtenda maovu kwa uovu wake.
Mwenye kukutana na Mola wake, Siku ya Kiyama, akiwa na jema moja miongoni mwa matendo mazuri, atapata mema mfano wake mara kumi. Na mwenye kukutana na Mola wake akiwa ana ovu moja, hatateswa isipokuwa kadiri ya mfano wa ovu hilo, na wao hawatadhulumiwa hata kiasi cha uzito wa chungu mdogo.
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Mimi Ameniongoza Mola wangu kwenye njia iliyolingana sawa yenye kufikisha kwenye Pepo Yake, nayo ni Dini ya Uislamu yenye kusimamia mambo ya dunia na ya Akhera; nayo ni Dini ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Dini ya Ibrāhīm, amani imshukiye. Na Ibrāhīm, amani imshukiye, hakuwa ni miongoni mwa wenye kumshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu asiyekuwa Yeye.»
Sema, ewe Mtume, kuwaambia hawa washirikina, «Hakika Swala yangu na nusuk yangu, yaani kuchinja kwangu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Peke Yake; si kwa ajili ya masanamu wala wafu wala majini wala wasiokuwa hao kati ya wale, wasiokuwa Mwenyezi Mungu, mnaowachinja na kutaja majina yasiyokua jina Lake, kama mnavyofanya.. Pia uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe wote.
«Asiye na mshirika katika uungu Wake wala katika uola Wake wala katika majina Yake na sifa Zake. Kumpwekesha huko Mwenyezi Mungu kulikosafishika ndiko Alikoniamrisha mimi Mola wangu, Aliyetukuka na kuwa juu. Na mimi ni wa kwanza kumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu katika umma huu.»
Sema, ewe Mtume, «Kwani natafuta mola mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ni Muumba wa kila kitu, ni Mwenye kukimiliki na kukiendesha?» Na hafanyi Mwanadamu yoyote tendo baya isipokuwa dhambi zake zitamshukia mwenyewe, wala haitabeba, nafsi yenye dhambi, dhambi za nafsi nynigine. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Siku ya Kiyama, awape habari ya yale mliokuwa mkitafautiana juu yake katika mambo ya dini.»
Na Mwenyezi Mungu, kutakasika na sifa za upungufu ni Kwake, Ndiye Aliyewafanya nyinyi mushike nafasi za waliowatangulia katika ardhi baada ya Mwenyezi Mungu kuwaondoa na kuwaweka nyinyi badala yao, mupate kuiamirisha baada yao kwa kumtii Mola wenu. Na amewainua daraja baadhi yenu, katika mapato na nguvu, juu ya wengine ili kuwapa mtihani katika alichowapa miongoni mwa neema Zake, apate kuwa wazi kwa watu mwenye kushukuru na asiyeshukuru. Hakika Mola wako ni Mwepesi wa adhabu kwa aliyemkanusha na kumuasi. Na Yeye ni Mwingi wa msamaha kwa aliyemuamini na akafaya matendo mema na akatubia na dhambi yenye kuangamiza, ni Mwenye huruma Kwake. Al-Ghafūr (Mwingi wa kusamehe)na Al-Raḥīm (Mwenye kurehemu) ni majina mawili matukufu katika majina ya Mwenyezi Mungu.